Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 37. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 37.

Kamila mwenyewe alikuwa akisikiliza. Kwani wawili hao wakianza, ni nyumba nzima mtasikia. Alifurahi! Alifurahi sana. Hakuwahi kupata ulinzi wa kibaba wa namna hiyo kabla. Ikawa kwa mara ya kwanza, anaonja kupiganiwa. Akabaki ametulia chumbani kwake. Ila akaanza kurudishia vitu vyake sehemu yake, akijua safari ya Kigamboni ndio imeishia hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Wewe Connie nenda kapumzike. Mimi nampa muda atulie, nimpigie.” “Acha nimpigie mimi.” Hawakutegemea! “Nilimuacha kipindi cha Jelini. Safari hii nataka kuwa naye.” Wazazi hao kimya. Akampigia.

Ikaita, baada ya muda akapokea. “Ninaye sonara mzuri sana. Tukimfuata kesho, anaweza tengeneza pete nzuri na kwa haraka. Tutaandaa mazingira mazuri ya ku propose. Kisha tuulize taratibu za mahari. Na kwa sababu umerudi kanisani.” “Connie!” Ikabidi aanze kucheka.

“Ulipotea kanisani Coly! Ila sasa, sababu umerudi, itakua rahisi kuandikisha ndoa. Njoo nyumbani tujipange vizuri. Usikasirike. Njoo.” Sauti ya Connie mwenyewe ni ya utulivu, ukiwa mbali kidogo humsikii. Kidogo akaanza kutulia. “Unakuja?” “Nageuza. Nakuja. Ila mwambie baba asiniongeleshe tena usiku huu. Aniache kabisa.” Akakata.

 “Anarudi. Ila amesema usimuongeleshe kabisa.” Mama mtu akahema kwa nguvu akitingisha kichwa kwa masikitiko. Mzee akazidi kucheka.

“Anataka kutumia dhambi zangu kunifunga macho na mdomo nisifanye majukumu yangu ya ubaba! Hata kidogo.” “Ushafikisha ujumbe wako, sasa naomba umuache. Tafadhali Henry.” “Sawa. Kwani mimi nina neno? Yeye ndiye mwenye neno.”

“Ila katika yote, hili nakushukuru baba Colins. Nilijisahau. Nikataka kurudia kosa. Si sawa kwa Kamila na kwetu pia. Huyu binti ametuheshimu sana. Kumtoa hapa kimyakimya si sawa. Na ni dhambi.” “Sasa ukikaa na yule mwanao, kichwa ngumu, usisahau kumwambia hayo!” “Hicho kichwa sijui karithi wapi?!” Akamkejeli kwa swali wakijua wazi ni kopi yake, Connie akaanza kucheka

“Sawa. Mimi kwani nakataa! Lakini yeye…” “Huyo anakuja. Naomba unyamaze Henry.” “Sasa mimi nimefanyaje!?”“Nyamaza.” Akacheka akitingisha kichwa. Mlango mkubwa ukafunguliwa, wote kimya wakijua ni yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Nilitaka kwenda kulala. Niliposikia maandalizi ya harusi, nikaona nisubiri nisipitwe. Na mimi nataka kushiriki.” Wote wakashangaa. “Nilikwambia nini Connie!?” Mzee hana mbavu. “Mimi na mama tumetoka kumuonya sasahivi hapa! Akaahidi atatulia.” “Wewe kaa chini tuanze mipango ya harusi. Huu mchezo hautaki hasira.” Akamtizama baba yake ila akakaa.

Wakamuona ametulia kama anayetaka kusema kitu kinamuia ngumu kukitoa mdomoni. “Umekubali wazo langu?” Connie akamuuliza kwa kujali. Tuzungumze kesho, sitaki mwenyewe asikie.” Hapo akapunguza sauti. Wakaelewa.

Akamgeukia baba yake. “Japokuwa unaniudhi SANA, ila katika hili naona upo sahihi.” Mzee alishangilia huyo nakufanya wacheke. “Mpaka nimejuta!” “Wewe mbishi sana bwana! Na jeuri. Kwa kukubali hivyo! Nahisi naota!” “Nakushukuru kwa kumpokea Kamila kwa kiasi hicho. Nina uhakika umemtoa hofu kubwa sana aliyokuwa nayo. Alikuwa anahofu akijua kwa sababu Mike ameondoka, hatapata mtetezi tena. Nina uhakika kwa hili atatulia japo kwangu umenikatili.” “Wewe tulia, nikuozeshe kwa heshima. Acha wizi.” Angalau pakatulia hapo. Ila wakabadili kabisa mazungumzo, kwamba mipango iendelee Kamila akiwa hayupo.

~~~~~~~~~~~~~~~

Hawakukaa sana hapo, wakatawanyika kwenda kulala, kesho yake siku ya kazi, wote waajiriwa. Ikabidi Colins kwenda chumbani kwa Kamila. Akagonga, akamfungulia kama aliyekuwa akimsubiria.

“Pole.” “Unanicheka Kamila!?” Kamila akazidi kucheka. “Hakika siamini!” “Mimi mwenyewe siamini. Ila nimefurahi Colins! Nimefurahi sana. Nilikuwa nikiwaza hapa, kwamba kama ningekuwa na wazazi wangu kama hivi tokea zamani, inamaana nisingeishi hata vile na Mike!” Colins akakaa na kuinama.

Akaenda kukaa pembeni yake. Akamuwekea mkono mgongoni akimpapasa na kucha. “Pole.” Akamwangalia. “Najua ni kwa kiasi gani ulikuwa ukitamani twende tukaishi wote kule. Pole.” “Wala sirudi kule.” “Colins!” “Hakika sirudi. Ile nyumba vile ilivyo ilikuwa imebeba historia mbaya, yaani wewe ndio umeirudishia uhai. Siwezi rudi kule bila wewe. Tutaishi tu hapahapa.”

~~~~~~~~~~~~~~~

Wawili hao maisha yakarudi kwa wazazi. Tena safari hii ikawa kila mtu analala chumbani kwake. Ilibidi Kamila aweze tu, maana alijua mzee anaangalia. Na Colins naye kikamuingia kichwani na moyoni. Akawa muaminifu kusubiri kama baba yake alivyomwambia alifanya. Kutomgusa mama yake mpaka ndoa. Japokuwa alikuwa akimtamani sana Kamila, na mchezo aliokwisha fanya naye wa nguvu, lakini akawa mwaminifu kwa baba yake. Akamuacha kabisa, penzi la wizi wakaacha kabisa.

Love Come To Those Who Believes It.

Ilikuwa imebaki juma moja harusi ya mapacha hao waliokuwa wakimuoa Jelini na Emelda, ifungwe. Mama mchungaji aliomba watakao weza kufunga, wafanye hivyo kwani alitaka siku hiyo iwe siku maalumu ya kuombea shuguli nzima ya harusi kabla Emelda na Jelini hawajapotea kwenye macho ya wengi mpaka kuja kujitokeza tena siku ya kitchen party kwa watakao hudhuria, kisha harusi. Walipanga kuanzia juma hilo, wapumzike kabisa, wasitoke hata nje, wawaze ndoa tu.

Akaomba ndugu wa karibu na hao maharusi wajumuike nao. Kina Ezra wenyewe pamoja na wachumba zao walifunga, wakiwa wamehamasika haswa. Kwani walishaweka mipango mizito, siku ya harusi yao nzima. Jinsi itakavyokuwa. Jinsi watakavyoingia na kucheza ukumbini. Jelini mpenda mziki, akawa ameshatafuta nyimbo nzuri zitakazoendana na kucheza kwao. Wakatafuta mwalimu maalumu akawa akiwafanyia mazoezi jinsi wao wanne watakavyocheza siku hiyo ya harusi yao.

 Ulishachaguliwa na kulipiwa ukumbi wa maana na vyakula vya nguvu wakijua aina ya wageni wao. Upande wa wakina Junior na Ezra ni wafanyakazi wa BOT. Kwanza michango yao wenyewe ilikuwa ya neema. Kwahiyo lazima kuwalisha kutokana na hadhi yao na pesa yao. Maandalizi yalikuwa mazito, na ungejua wanao oa ni wenye nazo.

Kisha mchungaji ndio alikuwa anaozesha vijana wake! Kwanza wanajitoa sana kanisani. Kanisa la wenye nazo. Kila mmoja akasukumwa kutoa kwa mapana na urefu, ilimradi tu harusi hiyo iwe gumzo na kumfurahisha mchungaji wao.

Na wenyewe hao wawili, waliandaa fungate la nguvu. Kwanza kutaka kujipongeza kwa kuweza kusubiri mpaka ndoa, na pili walipata wanawake wa ndoto zao. Walijawa furaha na hekaheka hao, akili ilikuwa siku hiyo ya jumamosi. Kwenye shuguli nzima, na nyuma ya pazia.

Hati zao wote wanne za kusafiria zilishakuwa tayari na visa zao zilishagongwa kabisa, zinawasubiria wao tu. Harusi ifungwe, waende fungate.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ndio mama mchungaji akaona jinsi maandalizi yalivyo mazito, akataka na mkono wa Mungu juu ya yote. Kulikuwa na mwitikio mkubwa sana, kila kitu kilikuwa kikienda shwari, lakini akataka lazima wapate siku moja tulivu. Kila kitu kisimame, watulie kwenye uso wa Mungu, waombe aende nao katika juma hilo. Maana hata kitchen Party yenyewe ya Jelini na Emelda, kina Junior wenyewe waliweka pesa. Iliandaliwa kama harusi ya mamilioni!

~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa hiyo hata mchungaji na mkewe pia walifunga pamoja na hao maharusi. Ikawa ibada ni nyumbani kwa mchungaji. Wanakutana hapo kuomba kwa pamoja kisha kula na kunywa.

Aliandaa vizuri sana ikawa kama tena ni tafrija ya namna yake. Alifanya kabisa catering. Watu maalumu walimpikia kila kitu, yeye akiwa kwenye maombi tu siku nzima. Jioni wakiwa kwenye ibada ya kusifu, kuabudu na maombi haohao watu aliowalipa kumpikia walifika hapo wakaandaa meza, kama karamu ya mwisho! Vyakula vingi, vizuri na vya kuvutia.

Mama Jema, dada wa mama Jema, Mode hakukosa. Ni Jelini tena! Shoga yake anaolewa! Mama mdogo Modesta hakukosa. Tena wakamuonya asifike kwa mchungaji akiwa amelewa. Cheko limemjaa, furaha zote kuwa Jelini kapata wa kumtuliza ndani. Mama yao, yaani bibi wa Jelini na Jema, alikuwa akifika siku ya jumapili kutokea Kilimanjaro.

Jema na familia yake pia walikuwepo. Jelini na mwanae pamoja na familia ya mchungaji mpaka wengine waliokuwa wametoka kijijini  upande wa mchungaji na mkewe waliokuwa wamekuja kuhudhuria hiyo harusi wote walikuwa sehemu moja wakizungumza pamoja huku wakiendelea kula baada ya ibada nzuri sana jioni hiyo. Vilijaa vicheko hapo, furaha na amani, ungejua walifanikiwa kuvuta uwepo wa Mungu katikati yao.

Moyo Wa Mtu Msitu.

Simu ya James ikaita. Mkewe akamtizama. Akaingalia akamuona anacheka. Akapokea. “Leo umenikumbuka?” “Wewe ndio umenitupa.” “Mzima lakini?” “Nipo kaka. Namshukuru Mungu anasaidia. Nilitaka kukukaribisha uhudhurie jambo tulilokuwa tumeanza mimi na wewe, lakini sikufanikiwa kwa upande wa shemeji yako, ila Mungu amenikumbuka.” James hakutegemea.

“Acha masihara Colins!” Alipomtaja jina kwa kuhamaki, akafanya wote wamuangalie baada ya kujua ni Colins. Jelini moyo ukapasuka paa! Kusikia Colins! “Ni msichana wa wapi?! Lakini acha nikupe kwanza hongera aisee! Siamini!” Kijiko alichokuwa ameshika Jelini akila, kikadondoka. Ezra akamwangalia. “Samahanini jamani.” James akajua amesumbua. Akasimama na kutoka simu sikioni.

Jelini akajishitukia. Akakuta Junior na Ezra wote wanamwangalia. Akaokota kijiko chake na kuondoka hapo katikati ya watu akijua ashamwaga mchele kwenye kuku wengi. Ya ndani yote ameyatoa nje. Akaelekea jikoni kama anayeenda kusafisha hicho kijiko.

Huku Kwa James na Colins.

James alitoka nje  barazani ili asisumbue. “Aisee siamini!” “Hata mimi siamini aisee! Nahisi Mungu alinihurumia tu. Aisee James, Mungu anajua kufuta machozi.” “Usiniambie!” “Nimepata msichana huyo! Nahisi ndio maana nilikuwa nikisumbua wasichana wengine. Huyu ndiye Mungu alimuumba kwa ajili yangu mimi!” James akacheka sana.

“Hakika tena. Ananijulia kupita nitakavyokwambia ukaelewa. Na alinikuta na hali mbaya! Mpweke! Hasira za kumpoteza Jelini! Hasira kwa wazazi! Nilikuwa silali aisee! Lakini amenifanya nimetulia kabisa. Nimejikuta nampenda, na kwa hakika namuhitaji. Malalamishi yote uliyokuwa ukiyasikia juu yangu, na dhambi zangu zote, bwana huyu msichana amebeba! Amebeba na ananifanya niishi kama nisiye na hatia yeyote hapa duniani. Hana lawama kwangu hata kidogo! Acha nioe kaka, na mimi nitulie.”

“Daah! Hatimaye!” “Kabisa. Umri umekwenda. Nimepata anayenipenda na kunienzi.” Akatengeneza huo usemi. “Ananipenda na mimi nampenda kwakweli. Halafu mzuri. Mzuri sana.” James akazidi kucheka kwa furaha.

“Aisee hongera sana Colins!” “Nashukuru kaka. Nilikaribia kukata tamaa. Lakini Mungu amenihurumia. Siku ya jumamosi, tumemuandalia kitu kizuri sana, ili nimchumbie. Ukiweza, karibu. Ukishindwa, nitaelewa.” “Siwezi kukosa aisee! Lazima nije nishuhudie. Maana mwanzoni nilikuwa niwe mwenyekiti kabisa wa harusi yako na Jelini!” Wakacheka.

“Kweli maisha ni kitendawili!” “Na kwa hakika mipango ya Mungu si kama yetu James! Hata mimi sikujua kama naweza pata mwanamke mwingine mbali na Jelini, na nafsi yangu ikafurahi hivi. Aisee nimepata msichana James!” “Acha masihara!” “Acha kaka! Imekua mwisho wa mahangaiko yangu kwa upande wa mapenzi. Huyu sisubiri. Nakimbiza kanisani haraka sana.” James akazidi kucheka mpaka ndani wakawa wanamsikia sasa.

“Hutaki tena kuporwa!” “Aisee huyu hapana. Huyu nitapambana naye mpaka mwisho. Na nashukuru wazazi wamesimama na sisi. Mzee amefurahi huyo! Kama sio yeye aliyekuwa akinichagulia wanawake.” “Atakuwa amejifunza.” “Na Kamila wangu anapendeka bwana. Hana makuu!” “Hongera sana Colins.” Bado James alikuwa haamini.

“Karibu na wewe ushuhudie kile Mungu amenitendea mimi na familia yangu. Maana wazazi ni kama wamepata binti mwingine.” “Lazima nitakuja. Nipe muda na sehemu.” Wakazungumza kidogo, wakaagana. Wawili hao walishapoteza mtiririko wa mazungumzo kwa  muda mrefu.

Alirudi ndani, amejawa tabasamu usoni bado anaangalia simu kama ambaye bado haamini! Jema akamtizama. Ila akawa muungwana, akanyamaza kama asianzishe jambo sehemu isiyo yake.

Huku Kwa Jelini.

Ezra alipoona harudi, akamfuata huko jikoni. Akamkuta anaosha vyombo kwenye sinki. “Humalizii chakula chako?” “Najihisi kushiba.” Akaendelea kuosha vyombo. “Naomba uache hivyo vyombo, tutoke kidogo.” Wasiwasi ukamuingia Jelini. Akabaki akimwangalia kwa wasiwasi.

“Kausha mikono, tutoke.” “Nichukue pochi kabisa?” “Hapana. Tunaenda kuzungumza baraza la nyuma kabisa. Tutarudi.” Akajikausha na kumfuata nyuma. Kimyakimya mpaka ndani ya baraza. Na lenyewe liliezekwa na kuzungushiwa uzio wa nyavu tu. Kusiingie mbu. Kulikuwa na viti. Akakaa, ikabidi na Jelini akae.

“Kuna kitu nataka kukusaidia.” Jelini akamwangalia. “Hujachelewa.” Jelini akakunja uso kama ambaye hajaelewa. Ezra akaendelea kwa kujiamini.

“Kwangu ndoa ni agano la mpaka kifo. Natamani kuingia na mtu ambaye amenichagua mimi kama Ezra, na kunipenda. Sio kwa sababu mama yake anataka awe na mimi. Au amejikuta ni kama amejifunga, hana njia ya kutoka tena. Sijui kama unanielewa?” Jelini akabaki ameganda. Hawezi hata kupepesa nyusi.

“Na wewe hivyohivyo. Usikubali kuolewa na mtu eti kwa sababu amekutambulisha kila mahali mpaka kanisani na kwa wazazi. Unaogopa kumuumiza au kumuingiza aibu. Ni afadhali aibu, kuliko fedheha. Unanielewa Jelini?” Akazungumza naye kifasaha haswa kama anayetoa shule nzito, anataka aeleweke. Kimya. Jelini hakujibu.

Akageuka kabisa vizuri akimwangalia na kumuuliza kwa msisitizo, kama asiyetaka kubabaishwa. “Umenielewa Jelini?” Asijue ashamkera mchumba, hasira zimepanda, anajaribu kuzuia. Ila akaishia kujibu. “Sawa.” Ikawa tena kama ambaye hakutegemea aina hiyo ya jibu.

Yaani katika yote hayo, Jelini akajibu hivyo tu, na hakuongeza  kingine na yeye safari hii akaonekana na sura ya kujiamini, sio yakubembeleza tena kama alivyomzoea akimbembeleza na kumuomba asimpokonye pete. Safari hii akakutana na Jelini mwingine kabisa, sio wakubembeleza mpaka akamtia wasiwasi.

Kabla hajaongeza neno, Junior na Emelda wakawa wanawatafuta kwa kuwaita. Ikabidi watoke hapo. Mazungumzo yakaishia hapo ila kwa hakika Ezra alitishika mpaka akajuta kutingisha kiberiti.

~~~~~~~~~~~~~~~

Sasa wakati Ezra anatangulia kutoka, yeye akabakia nyuma kidogo na kumpigia simu mama yake hapohapo. Akaanza kuzungumza kama mama yake ndio amempigia. “Vipi mama?” Akasikiliza kidogo na kuendelea. “Sasa hivi!?” Mama yake akawa hajaelewa huko sebuleni. Ila yeye akaendelea. “Lakini ni jambo la kumshukuru Mungu. Japo muda umeenda. Tusiiachie hiyo tenda, twende tu tukamalizane nao. Anza kuaga, na mimi naaga huku. Nakuja tuondoke sasahivi.” Mama Jema akajua tayari. Kuna ambalo halijakaa sawa huko.

Hakutaka mengi, kweli akatengeneza uongo wake pale kwa mchungaji na mkewe. Kuwa wamepata wateja wanaotaka kukutana nao muda huo, lazima waondoke. Na dada zake nao wakaona waondoke. Wakata maji. Shuguli isiyo na pombe, si yakukaa muda mrefu. Ilikuwa kesho yake ndio wanakutana kwa mama Jema. Dada hao walipanga wakanywe huko, na nyama choma mpaka kukuchwe. Na jumapili mama yao akija pia warudi hapo kwa mama Jema kuendelea kulewa. Sasa walioona mama Jema na Jelini wanaondoka, na wenyewe haraka sana, wakaaga.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati wakiendelea kuaga huko sebuleni, huku kwa Jelini naye alikuwa akizungumza na mama yake, Ezra alikuwa akimsikiliza, na kumalizia walipowafikia Junior na Emelda.

Ila Junior akamuhisi hayupo sawa. “Kwema?” “Kwema. Ila inabidi niondoke na mama sasahivi. Tumepata tenda na wanataka kutuona sisi wenyewe tuwape uhakika, sio wafanyakazi waliowakuta pale. Usiku mwema. Acha mimi niwahi na mama.” Akaondoka bila hata ya kusubiri yeyote ajibu kati yao, na wala hakumtizama Ezra. Wakabaki wakimwangalia mpaka akapotea mbele ya macho yao.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ndugu wa mama Jema, wanawake wa kichaga waliofanikiwa biashara hapo jijini. Kila mmoja ana usafiri wake wa nguvu. Wakaingia kwenye magari yao, wakatawanyika. Mama Jema, Jeremy na huyo Jelini nao wakaingia kwenye gari yao, walitokea pamoja.

“Haya, safari hii ni ya wapi?” Ikabidi mama Jema amuulize maana alishamuona amekasirika haswa. “Tunarudi nyumbani.” Akajibu kwa jazba. “Kwema?” Mama Jema akajaribu tena. Jelini akaanza kama aliyepata jukwaa.

“Mimi sio wakubabaishwa. Sio kila wakati mimi ndio natakiwa kumuonyesha mtu kama nampenda na kumuhitaji, halafu yeye kila wakati ananionyesha hataki kubabaishwa. Kwa kipi mno?” Akaendelea.

“Yaani kila wakati mtu anakuwa anakuonyesha kama yeye hana shida sana, wewe ndio uwe unaonekana unashida! Hapana kwakweli. Kwanza yeye nimemvumilia sana na kuyabadili maisha yangu yote kwa ajili yake. Mimi sikuwa naenda kanisani na sikuwa na tatizo.” “Halafu ushazoea mwenyewe ndio wakubembelezwa.” Mama mtu akachomekea. Maana alijua udhaifu wake.

“Ewaah! Mimi nababaikiwa bwana! Nabembelezwa na wanaume wazima na akili zao. Na mimi ndio nataka hivyo. Siwezi nikawa mimi ndio nambembeleza. Kama mtu hawezi basi. Sio lazima yeye ndio akanioa.” Hapo mama Jema akashituka.

“Jelini?!” “Hapana mama! Kila mtu anaudhaifu wake. Kubembelezwa ndio udhaifu wangu, na kuna wanao ujulia huo udhaifu wangu. Kama yeye hawezi basi. Inamaana sio andiko langu. Hawezi akawa ananiringia mapema hii, hata hajaniweka ndani! Akiniweka ndani je? Hapana kwakweli.”

“Hata kama na wewe utanisema. Niseme tu. Mimi sijali. Siwezi ingia kwenye ndoa ya namna hiyo. Kama hana shida na mimi, BASI. Nitaenda kwa wanao nihitaji kwa kunibembeleza.” Mama Jema kimya.

“Hee! Kwa nini haswa!? Kama anaona mimi sifai, akatafute mwingine. Asinibabaishe.” “Jelini umekasirika, mama yangu mzazi. Tulia mama.” “Nimekasirika haswa mama. Yeye sio mwanaume pekee hapa duniani. Akinishindwa yeye, nitapata wa kwangu. Na mimi nasema kama yeye. Nataka kuolewa na mtu anayenipenda. Asinichezee akili yangu.”

“Si ameniambia sijachelewa yeye. Basi TUTAONA. Hanijui vizuri. Acha nimkutanishe na Jelini anayeliza wanaume hapa mjini. Yeye nimemkubali kirahisi ndio anataka kubweteka! Sasa sio kwangu. Wanawake wamejaa kibao. Akatafute wakumringia. Mimi ndio naringia watu. Eti hujachelewa! Kweli?” “Naomba tuanze taratibu Jelini. Tafadhali mama. Harusi imekaribia. Bibi yako anaingia hapa kesho kutwa, kesho mama zako kama unavyowajua, wanataka wakeshe pale.”

Sijali tena mama. Siwezi kuwafurahisha watu kwa siku chache, halafu eti mimi ndio nikasononeke kwenye ndoa ya mpaka kifo! Hapana kwakweli. Waje wakeshe, wanywe mpaka wachoke, lakini si kwa mimi kulipa garama. Kwanza yeye mwenyewe amesema ni bora aibu kuliko fedheha. Ezra mwenyewe pia hana shida na hii ndoa. Tena kwa kunihakikishia yeye mwenyewe usiku huu. Sasa mimi nahangaika kwa kipi!” “Kwani imekuaje!?” Akamsimulia mama yake mwanzo mpaka mwisho.

“Na hii sio mara ya kwanza mama. Ezra anamtindo wa kunionyesha hataki kubabaishwa. Sasa tutamuona. Yeye si anasema bora aibu kuliko fedheha? Sasa tutamuona.” “Au hujamuelewa vizuri?!”

“Mama, amefanya kunigeukia kabisa kuniuliza eti kama nimemuelewa alichoniambia kuwa ‘SIJACHELEWA’. Nisiolewe na mwanaume eti kwa sababu mama yangu anataka. Kweli mama.” “Haiwezekani!” “Mungu ni shahidi. Sasa ni maneno gani hayo yakumwambia mtu kama si udhalilishaji huo? Eti yeye anafikiria mimi Jelini, naolewa sababu wewe unataka! Kweli!?” Akafyoza kabisa.

“Huko si ni kunidharau kwa hali ya juu, na kuniona mimi sina akili, nina akili ya kushikiwa? Au kwa sababu anajua sijasoma ndio maana ananifikiria hivyo!?” “Jelini, unakwenda mbali mama!” “Hakika amenifikisha mbali. Na huo ujinga mimi sifanyi. Ebo!”

“Yaani mimi nimeishi na watu wanao aminika hapa duniani, wanaakili zao, wanafanya mambo makubwa ya kushangaza watu, lakini bado wana amini akili zangu, na…” “Wana kubembeleza?” Mama yake akamalizia akimwangalia vile alivyowakwa hasira.

“Haswa! Tena si kunibembeleza tu, wananitetemekea kabisa. Aache kunifanyia michezo ya kitoto. Na ndio atajua hakuna ubora kwenye chochote. Si aibu, wala si fedheha. Vyote havina ubora.” Wakawa wamefika kwao, Jelini anawaka kwelikweli wapo kwenye gari hataki kushuka, anaongea hamalizi.

Mwishoe mama mtu akaona ahitimishe yeye. “Naomba tushuke, huyu mtoto akalale Jelini. Hayo mengine tutayajua baadaye, kama ndoa ipo au haipo. Tutajua baadaye.” “Kabisa. Na mimi mtu asinibabaishe. Kwani lazima kuolewa? Mbona watu wengi tu wanaishi vizuri tu na hawajaolewa! Asitake kunichanganya mimi. Eti ‘sijachelewa’. Basi nitamuhakikishia kama kweli na mimi sijachelewa.” Mama Jema hakuongeza neno akijua ndio habari imeshapinduka. Akajichukulia mjukuu wake na kuingia ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mapenzi&Pesa!

Zikiwa zimebakia siku chache wafunge ndoa, bado Ezra anatishwa na penzi la Jelini kwa Colins. Ametibuwa mambo BILA kutarajia.

Siku waliyokuwa wamefunga na kuombea harusi yao, ndio KUMETIBUKA vibaya sana.

{Jamani! Shetani naye hujihudhurisha pamoja na wana wa Mungu wanapokwenda mbele za Mungu. Hanaga mipaka. Ayubu 2:1-2}

Jelini ametoa mengi ya moyoni na Ezra naye ameonyesha hataki kubabaishwa. Kwa maneno yake mwenyewe, amesema Jelini HAJACHELEWA.

Moyo wa mtu msitu!

Tusisahau, bado Colins hajaoa, na Jelini ndio huyo bado mapigo ya moyo yanakwenda kasi amsikia!

Ni Nini Kitaendelea Tena!

USIPITWE…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment