“Na wala hatutakosana sababu ya Kamila.” “Una uhakika
Colins?” “Mimi si mbambaishaji Mill. Sijui kuwa na mwanamke mmoja na
kutongaza mwingine. Sijawahi fanya hivyo na sitaanzia kwa Kamila.
Na wala sitakuficha, mimi sina historia nzuri kama yako na Mike. Sijawahi
kuwa kwenye mahusiano kama hivyo nyinyi. Kote nilikopita ni majanga.”
“Na huyo mwanamke niliyesikia unaye?” Akamuelezea kwa
kifupi juu ya Jelini. “Kwa hiyo Jelini ni mapenzi niliyokuwa nikiyatizamia
kwa hamu sana. Nikiwa na uhakika wa pumziko, ndio maana nilikuwa
nikihangaika kupigania penzi lake, nikiwa na uhakika ananipenda, nitatulia.
Lakini nimekuja rudiwa na akili zangu, nakujikuta nimechelewa na
nikamuingiza na yeye matatizoni. Hivi ndio kama kesi yake inakamilika.”
Akaendelea akiwa ametulia tu.
“Kama ulivyosema, Kamila ni binti mzuri. Naomba
niongeze na ni mwema mno. Sikutaka kumchanganya kwenye mambo yangu. Kwanza
nimemkuta akiwa na hali mbaya sana.” “Ameniambia.” “Basi kwa kuwa na mimi
nilikuwa natafuta kupendwa kama hivyo nyinyi, nilitaka kuchaguliwa
mimi kama mimi, sio mtu anichague sababu nilimsaidia. Sijui kama
unanielewa?” “Kwa hilo nimekuheshimu.”
“Basi, ndio maana nilimuweka Kamila karibu, na kuwa muwazi
kwake. Lakini Mill, katika magumu yangu yote hapa duniani, nina uhakika nikiwa
na Kamila, ni Mungu kunifuta machozi. Yaani kabla wewe mwenyewe
hujaingiwa na wasiwasi juu ya jinsi ya mapenzi yangu kwa Kamila, jua mimi
namuhitaji yeye kuliko utakavyodhania. Wewe nisindikize tu nikatafute
pete, nimvalishe. Mengine yaendelee.” Mill akacheka sana.
“Kwamba unaomba baraka zangu na ushenga
pia?!” “Wala sitakudanganya. Na mimi nimepoteza marafiki wote.
Nimerudiwa na akili na kujikuta ni kama nimetua katika ulimwengu mwingine
kabisa! Isingekuwa Kamila, maisha yangu ilikuwa nyumbani, kulala kwa
masaa machache, narudi kujifungia kazini. Sikuwa na kingine nafanya.”
“Basi naona upo kama mimi. Nimetoka jela, nimejikuta peke
yangu! Sina Mike, sina yeyote labda huyo Kamila. Jerry kumpata ni shida
sana. Sababu ya mambo ya kifamilia. Tuyaache hayo. Ninachotaka kukwambia,
ukifanikiwa kumuweka Kamila ndani, ujue umeyapatia maisha. Yule msichana
ametulia na hana makuu.” “Nimemgundua aisee! Tofauti na
anavyoonekana kabisa!” Colins naye akaafiki.
“Basi hata Mike alikuwa akisema, yaani yeye mwenyewe ndio
alikuwa akimfanyia makuu lakini si Kamila. Halafu amepoa haswa!”
“Pia ni mzuri sana.” Mill akacheka.
“Wala si uongo. Kamila mzuri bwana! Mimi nimekutana naye
hata nywele hajachana, lakini bado alikuwa anavutia! Ila
kilichonivutia zaidi kwake ni ile level ya commitment yake!
Hakika sijawahi ona! Yaani anamtafuta Mike aliyepotezana naye kwa
miaka miwili na hakati tamaa! Hakika ilinigusa na kuona kweli
mimi sikuwahi kupendwa.” “Acha masihara!” Ikabidi amsimulie jinsi
alivyokutana na Kamila, jinsi alivyomuuguza, kuokolewa kwenye hatari ya kutaka
kujiua.
“Bado akawa haamini kama Mike hayupo hapa duniani. Juhudi
za kumsaka Luca zikafanyika kuthibitisha. Ndipo akaonyweshwa picha za Mike
kwenye jeneza na kufikishwa makaburini ndipo akaamini.”
“Daah! Hakika ulimsaidia. Nakushukuru Colins. Asante
sana. Mimi aliniambia ulimsaidia matibabu!” “Acha kaka. Kuna wanaume wanapendwa
kaka.” “Ni kubahatika. Mimi nilipiga teke bahati yangu kwa Pam!
Aisee roho inaniuma Colins! Inaniuma sana.”
“Kama hujachelewa, naamini unanafasi ya kutengeneza.”
“Sijui aisee! Nilimuacha vibaya sana. Sana. Halafu usifikiri Pam
mwenyewe choka mbaya!” “Usiniambie!” “Ni vile alikuwa amebeba historia mbaya
kutoka kwa mama yake. Nikamkuta anakwepa wanaume kama ukoma, hakutaka
kurudia kosa la mama yake, akawa anajitunza sana. Lakini ilikuwa shuguli!
Shuguli haswa.”
“Walio nazo na wasio nazo wote
tulikuwa tukimpigania Pam. Mzuri! Halafu amepoa haswa. Udhaifu wangu
wote kwa wanamke, basi Mungu akamuumba nao Pam.” Colins alicheka. Akacheka
sana.
“Acha kaka! Nilikuwa kama nimepagawa na Pam. Kaumbwa
na mambo yangu yote! Nilikuwa nikiwa naye, sitaki kutoka ndani, sitaki
muingiliano, hata Mike simtaki. Na Mike alikuwa akijua. Nikiwa na Pam,
alikuwa anasema sina masikio.” “Acha masihara!”
“Acha kaka. Ushawahi kukaa na mwanamke kitandani. Sio kwa
kufanya mapenzi tu. Ila kuwa naye tu. Mna romance zaidi ya masaa 4, hammalizi
na hamtosheki!” “Nimekwambia mimi sikubahatika Mill!” “Basi na mimi sijabahatika
tena! Ilikuwa mwanzo na mwisho wangu.” Akavuta kumbukumbua!
Akatoa mlio wa masikitiko kama aliyekumbuka mbali sana.
“Aisee Pam ni watofauti bwana! Hachoshi! Kuna kipindi nilitakiwa
kuondoka hapa nchini, nilishindwa aisee!” “Acha masihara!” “Acha kaka!
Na nilipoona Mike ananisumbua. Maana alinipa nyumba ya nje, pale alipokuwa
akiishi na Kamila. Ikawa kila nikirudi nchini, nafikia hapo. Pakawa kama kwangu
kabisa. Nikirudi nchini najifungia humo na Pam.”
“Sasa safari hiyo alipoona siondoki, na kule
nahitajika, akaanza kunizonga. Hodi kwangu haziishi, ananikumbusha
kurudia majukumu ugaibuni, niondoke nchini. Nikaona isiwe shida, usiku
wamelala, nikatoroka mjini na Pam wangu. Nikaenda kujifungia naye Bagamoyo.”
Colins alicheka. Akacheka sana.
“Bwana Mike alinitafuta! Siku ya tatu usiku, tumelala,
nashitukia amenisimamia mlangoni.” “Hotelini?!” “Kumbe! Bagamoyo. Hakuniongelesha,
akaomba kuongea na Pam. Akamueleza umuhimu wa mimi kurudi chuo. Na kwamba mzee
ashalipa ada, halafu mgonjwa. Haijulikani kesho yake. Na mimi namtegemea yeye
peke yake. Kwamba nikipoteza shule na mzee akafariki, basi ndio ajue maisha
yangu yameharibika kabisa. Akazungumza sana na Pam, naona akamuweka sawa
Pam, ndio nikaweza kuondoka nchini.”
“Lakini kaka!” “Eeeh!?” Akaitika Colins akicheka sana.
“Acha ndugu yangu! Pam habari nyingine kabisa! Unaona hiyo rangi ya
Kamila?” “Ndiyo.” “Basi iwe mara mbili yake, halafu aive zaidi. Usiku mkiwa
chumbani, huhitaji, taa. Na ukiwasha taa tu, jua umejiloga mwenyewe! Unaweza
kesha naye.” Colins alikuwa akicheka. Mbavu hana, anamwangalia, hammalizi Mill.
“Nakwambia hivi, udhaifu wangu wote, mambo
yangu yote, Mungu akamuumba nao yeye, kama kunikomoa vile!” Colins
alicheka mpaka kupiga makofi. “Acha kaka! Nilimpenda yule msichana,
mpaka kurukwa akili. Nilikuwa kama mwehu kwake! Nina uhakika,
hakutegemea kile kilichotokea kati yetu. Nina UHAKIKA, mpaka leo anahisi ni
ndoto, sio kweli. Asiee tulipendana mno.”
“Wasiwasi wangu ni kwa vile alivyo Pam, sidhani kama
mpaka leo atakua hajapata mtu! Sidhani aisee.” Akaongea kwa masikitiko kama
aliyekumbushwa mbaliii. “Stori nzima ya Pam&Mill itarushwa kwenye Simulizi ya Love at
First Sight.”
Akafikiria kidogo, na kurudisha akili pale. “Ila tuyaache
hayo. Akikukubali Kamila, nakupongeza. Utatulia. Kama ulivyosema.
Tuanzie kwenye pete kwanza.” Wawili hao urafiki ukaanzia siku hiyohiyo,
hukohuko ufukweni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mara ya mwisho anaondoka kwenye hoteli hiyo, alikuwa
ameumizwa vibaya sana. Love na Kemi walikuwa wamegongelea msumari wa mwisho
kwenye penzi lake na Jelini. Lakini siku hiyo, hoteli
hiyohiyo akapata tumaini jipya. Akaanzisha urafiki na Mill, na baraka
ya kumpata Kamila.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya watoto kula na kucheza vyakutosha, Mill akaaga
kwa ajili ya maandalizi ya shule kesho yake, wakabakia hao wanafamilia. Bado
akamuona Kamila hana raha. Kama kuna jambo linamsumbua! Akamuomba wakatembee
naye ufukweni kama alivyokuwa na Mill. Wakatoka na kuwaacha wazazi na Connie.
“Mbona kama huna
raha? Tafadhali niambie ni nini kimekuudhi.” “Hamna kitu kimeniudhi Colins!”
“Basi niseme ni nini kimekunyima raha?” “Nahisi ni mambo na mipango mingi
inaendelea kichwani mwangu, ndio maana unaona nimetulia.” Akaendelea.
“Sikumbuki kufanya maamuzi mimi mwenyewe isipokuwa
kumfuata Mike katika kila jambo. Sasa, sasahivi nakuwa kama naanza upya! Kazi
niliyokuwa nikifanya ambayo ni ya watu inamaana inafika mwisho, natakiwa
kufikiria mwenyewe ili kufanya biashara yangu vizuri. Kuna hofu
inayoendelea. Kuna kujitilia mashaka.”
“Ni kitu unachotaka na unajiona upo tayari?” “Nikwambie
ukweli?” “Ndivyo ninavyotaka.” “Sipo tayari kabisa. Naona kama naharakishwa!
Halafu haya yalikuwa mawazo ya Mike, si yangu. Na nilikubali kwa sababu nilijua
atakuwepo mwenyewe, nakusimamia hiyo resort.” “Sio mgahawa tena!?”
Ikabidi aulize.
“Mambo ya Mike na Mill sio kama wanavyotamka. Hawajui
jambo dogo. Akikwambia Mill kama ni mgahawa wa kutoa vyakula vya mataifa
mbalimbali, usifikiri ni jiko moja na ukumbi mdogo wa kuweka watu wale! Hapana.”
“Walishanunua uwanja. Nikikwambia uwanja, jua ni maheka
mengi sio kiwanja kidogo. Wakanunua kwa majina yetu wote watatu kusudi watu wa
pembeni wasije ingilia. Kwamba hata ndugu wa Mike wangetaka kuchukua,
wangeshindwa kwa sababu ni mali ya watu watatu, halafu nina uhakika hakuna
anayejua kama upo huo uwanja mbali yetu. Nitakuja kukupeleka ukaone. Wamejengea
uzio kabisa, wakilinda watu wasije chukua maana ni nje ya mji kidogo.”
“Walitaka kujenga nini?” “Resort itakayokuwa na
sehemu ya kulala kabisa. Kuwe na vitu mbali mbali. Na siku maalumu za mpaka
bendi ziwe zikipigwa live. Kuwepo vitu vya asili kwa watalii kama ngoma
za kabila tofauti tofauti zitakazopigwa siku za weekend. Kuwepo na
sehemu maalumu pia kutakapokuwa na michezo ya kisasa ya watoto itakayovutia
wazazi. Wazazi wakija ndio na kula na mambo mengine.”
“Umepata angalau picha ya ninachokwambia?” “Aisee ni
mawazo mazuri sana. Halafu yanasikika ni makubwa! Ingekuwa ikivutia.
Kama vile Disney Land?” “Ewaaa! Walikuwa wanapicha hiyohiyo ila iwe nchini
Tanzania. Sasa naona yote hayo bila Mike, nipo peke yangu! Naingiwa hofu.”
“Na mimi nipo Kamila!”
“Kwa sasa upo. Tena upo na majukumu mazito
ya hospitali. Lakini na kingine ambacho umeshindwa kunijibu Colins. Je,
ikitokea Jelini anarudi kwenye maisha yako?” Akajua hicho ndicho kinachomnyima
raha.
“Kwa nini unawasiwasi na Jelini ambaye anakaribia
kuolewa, Kamila?” Hata yeye alijua anakwepa kujibu swali. “Jelini ana maisha
yake. Haya ndio maisha yetu!” “Kwa sasa ukiwa umekata tamaa kuwa anaolewa.
Watu wanabadilika siku ya harusi, tena kanisani. Iweje agundue mapenzi
yapo kwako na hawezi ishi bila wewe, akakurudia tukiwa
tumeweka mipango mimi na wewe?”
“Huyo si Jelini. Na haitakaa itokee. Namfahamu
Jelini. Na namfahamu mwanaume aliye naye sasahivi. Anampa Jelini kile
alichokuwa akikitafuta wakati wote, na mimi kushindwa kumpa. Hana sababu
yakurudi kwangu. Tafadhali usifikirie huko.” Kamila akanyamaza akijua wazi
anakwepa kujibu upande wake.
“Niangalie Kamila.” Akamwangalia. “Unakumbuka ahadi ya kutokukuacha
peke yako zaidi ukiwa unanihitaji?” “Nakumbuka Colins.” “Basi haitabadilika.
Tafadhali kuwa na imani na mimi. Na usifanye kitu ambacho hutaki. Najua
unapenda kupika. Unaweza anza kidogo. Hata catering. Kwenye sherehe.
Ukiona upo sawa, unajiongeza. Hivyohivyo. Taratibu. Sawa?”
“Naona kama nitamkatisha tamaa Mill! Ataona mimi ni mvivu.”
“Hapana. Nimezungumza naye, anaonekana ni muelewa. Sidhani kama anataka kukulazimisha
ufanye jambo. Ninachomuona ni kutaka kumuenzi Mike kwa kuendeleza
alipoachia. Anajihisi ana deni. Lakini sidhani kama atafanya yote hayo kwa
garama ya kukuumiza wewe. Anakupenda na anakujali sana. Usiogope, kuwa muwazi
kwake.”
“Jiwekee malengo madogo madogo na muda wako wewe.
Ndio ufanye. Tena kama unapenda. Sio watu wote wamezaliwa ni wafanyabiashara
Kamila. Si kweli.” “Hutanidharau? Maana nimesikia Jelini anafanya
biashara na amefanikiwa sana.” Colins akashangaa sana.
“Kamila! Hayo mawazo unayatoa wapi!? Wewe si
Jelini! Na sitakaa nikataka uwe Jelini. Unasifa nzuri sana ambazo
wala hazilinganishwi na Jelini. Nyinyi ni watu wawili tofauti! Tafadhali usijifananishe
naye. Na nakuahidi sitakufananisha naye nikitamani uwe yeye.”
“Kweli Colins!?” “Sasa itakuwa na faida gani kuwa na wewe!?
Si nitaishia kujitesa mwenyewe! Nakutaka wewe kama wewe, na hivyo
Mungu alivyokuumba. Usijibadilishe ukawa Jelini. Kwa vyovyote ulivyosikia juu
yake, jua ni yeye. Ila mimi nipo na wewe kama Kamila.” Akaridhika japo
bado hakuwa amejibu kama endapo atarudi, itakuaje.
“Kwa hiyo si tunarudi wote Kigamboni?” Hapo akamuona anasita. Akaingiwa wasiwasi
kidogo. “Kwamba
Kamila amebadili mawazo hataki tena kuishi na mimi!?” Akawaza Colins
akimtizama kwa makini na kutaka kujua wasiwasi unatoka wapi?!
“Nitamuagaje baba? Maana pale mlipotuacha, ukiwa na Mill.
Amenitambulisha ramsi kwa Connie, na kumwambia mimi ni binti yake, Mungu amempa.
Ametutaka mimi na Connie tuishi kama ndugu wa damu kabisa. Tusijione tofauti.
Na amesema ndivyo na yeye atakavyotuchukulia. Hatabagua. Na mimi nimuone
kama baba kabisa na mama niwe huru naye kama mama yangu. Sasa leo waone
naondoka tena nyumbani!” Hilo akalifurahia Colins kuona Kamila amepokelewa kama
mmoja wa familia. Asijue madhara yake mbeleni.
“Mimi nitazungumza nao. Wewe usijali. Turudi nyumbani.
Fungasha vitu vyako vyote. Chukua vya muhimu. Vingine atafuata dereva kesho.”
“Naogopa Colins! Naogopa sana.” “Unaogopa nini?!” “Tukishindwa? Halafu mimi
ndio nakua nimeshapoteza familia! Maana pale nyumbani kutabakia nyumbani
kwenu tu, hata kama leo nimekaribishwa rasmi!”
“Cha kwanza, nakuhakikishia Kamila, mimi sikutumii
tu kwa muda. Kwamba nakutaka sasahivi huku nikiangalia nje. Hapana. Na nakuhakikishia
tena, hutashindwa kuishi na mimi. Hali uliyonikuta nayo, wewe, umeimaliza.
Najisikia amani. Sitakubadilikia. Na cha mwisho, nakuhakikishia pia,
mama atabaki kuwa mama yako, na baba hivyohivyo. Hutawapoteza.
Kile chumba umepewa, ni chako. Na kukuhakikishia hivyo. Unaweza bakisha
vitu vyako baadhi pale ili kujipa amani.” “Kama ni hivyo sawa.” Wakakubaliana.
Shilingi Yapinduka.
Wakarudi mezani walipokuwa wamewaacha wazazi na Connie,
hawakukaa sana wakarudi pamoja nyumbani. Wakati Kamila yupo chumbani akikusanya
mizigo yake tayari kuhamia Kigamboni kwenda kuishi na Colins unyumba, yeye
Colins akaomba kuzungumza na familia yake zaidi wazazi, ila Connie naye akawepo.
“Nampenda Kamila. Nataka kumuoa.” Wakabaki kimya
wakimtizama. “Na baba, sio kwamba nakuomba ruhusa. Nakutaarifu.
Na safari hii sitaki…” “Colins! Unapandisha hasira wakati hujanipa muda
wa kunisikiliza.” “Katika hili SITAKI kukusikiliza.” Wakaanza kubishana, bila
kujua wanabishana wapo upande mmoja.
Connie akataka kuingilia kuwasaidia, mama yake akamzuia.
“Wewe wala usijichoshe. Waache wabishane mpaka wachoke. Ila mjue nawahesabia
dakika. Mimi nikichoka kuwasikiliza, naondoka.” “Ni baba huyo!” “Sasa
mimi nimefanyaje?!” “Unataka nikuandikie ulichofanya au?” Wakaanza tena.
“Hivi nyinyi mnajua mnabishania kitu kimoja?!” Connie akawauliza
asiamini. “Ndio hichohicho. Maana baba..” Wakaendelea, hawamalizi. “Hivi ujue
Henry wewe ni baba, acha utoto?” “Ni Colins, sio mimi!” “Sasa
wewe nyamaza mimi nimuulize Colins.” “Sawa. Lakini…” “Hapana baba Coly.
Nyamaza.” Akanyamaza lakini kama ambaye hajaridhika.
“Haya, Colins. Wewe unabishana nini hapa?” “Si baba huyo!”
“Amefanyaje?” “Anapenda kuniingilia kwenye mambo yangu, ana…” “Katika hili,
amekuingilia kivipi?” “Afadhali. Maana..” “Nyamaza Henry.” Mkewe akamkatisha.
“Eti Colins?” “Si katika maswala yangu ya mke!” “Ndio
nakuuliza, katika hili, amekuingilia vipi?” Akatulia akijaribu kufikiria
tokea mwanzo wa hayo mazungumzo, wakamuona anaanza kutulia. “Umeona umekamatwa!
Tena umekamatwa vibaya sana. Sasa na mimi aniombe msamaha.” “Haiwezekani
baba!” “Basi mjibu mama yako, halafu ndio tujue kama na mimi sistahili
kuombwa msamaha!” Wakaanza tena.
Connie akabaki kimya akiwatizama, hawamalizi. “We
Colins? Niangalie mimi na unijibu swali langu, acha kupotea kwa maneno mengi.
Katika hili amekupinga kivipi?” “Anapenda kuniwekea vikwazo kwenye mambo
yangu.” “Nakuuliza katika hili, umemsikiliza, umesikia amesemaje?” Hajui
alikimbilia kujihami bila kusikiliza. Kimya.
“Basi mwambie aniombe msamaha. Si sawa kwangu.”
“Kweli baba wewe!?” “Hakika tena. Mama Colins! Zungumza na mwanao. Ameniweka
kwenye kundi baya, wakati mimi nipo upande mwema. Nia yangu ni
kukusaidia na safari hii nataka kukutendea haki. Na nataka kusimama na
wewe mpaka uoe. Sitaki uishi maisha ya unyumba kama ulivyoishi na Love.”
Hapo akamshitua Colins, hakutegemea.
“Hai..” “Subiri kwanza nimalize. Kama kweli unampenda
Kamila binti yangu. Chumbia. Akikubali, toa mahari. Oa
ndio uhame naye hapa. Lakini si kienyeji.” “Haiwezekani. Nishahama naye.
Nitamchumbia, halafu…” “Hutahama naye hapa. Hapo HAPANA Colins.” Mzee
akabadili gia. Akavaa ya ubaba.
“Huyu binti amenipa heshima kama baba. Ni yatima.
Ambacho sitataka mwanaume amfanyie Connie, ndivyo hivyohivyo kwake. Hutamtumia
ndio ukamuoa. Anabaki hapa mpaka siku unamuoa. Ukikabidhiwa pale
kanisani, ndio wako.”
“Haiwezekani baba!” “Hakika anza kuamini. Inawezekana.
Na ndivyo itakavyokuwa. Kamila HATAONDOKA
hapa mpaka kwa utaratibu unao eleweka. Huwezi kunywa
maziwa, hujanunua ng’ombe. Usitake kunichanganya. Kama alivyomkatalia Mill,
kuwa hapa ni nyumbani, basi na kwako ni hivyohivyo.” Colins hakuwa akiamini.
“Mbona kama unanipinga kila wakati ninapotaka…”
“Acha kunichanganya na habari za Jelini. Kule nilifanya kosa. Nimekiri kwako,
nimekuomba msamaha. Kunisamehe hiyo ni sehemu yako. Mimi naendelea kama
baba. Siwezi kukuacha ukaishi maisha ya kihuni tu, eti kwa sababu
naogopa tutagombana! Hapana. Nichukie utakavyo, lakini hutaishi maisha
ya kihuni, na sitamtoa Kamila hapa kwenda popote bila utaratibu
maalumu.”
“Mbona niliishi na Love, Marekani na hapa na
hukuwa na shida?!” “Nani amekwambia sikuwa na shida? Muulize mama yako
kama hilo jambo halikuwa likinikera kupita nitakavyokwambia, ukaelewa.
Nilishazungumza na wote hawa watatu. Simba na mkewe pamoja na mama yako.”
“Tokea mpo Marekani na mama zenu, wao wanajiandaa kurudi
huku na Connie pamoja na Loreta. Nilipouliza utaratibu unakuaje nyinyi
mnapoachwa kule, niliposikia, mama yako ni shahidi. Nilipinga kabisa.
Nikawaambia kabisa, ni bora nijinyime, nikulipie apartment yako,
kuliko uishi na Love nyumba moja nikihofia msije anza ishi unyumba
wakati hamjaoana. Muulize mama yako majibu aliyonipa mama Simba.” Kabla
hajamuuliza, akaendelea.
“Na hapa hivyohivyo. Japokuwa sikumtaka Jelini, lakini
nilimwambia kabisa Simba na mkewe, tena na Love mwenyewe akiwepo. Mama yako huyu
hapa shahidi yangu katika hili. Nikawaambia hivi, kama kweli mnamtaka
huyu Colins, basi wasihame kimya kimya. Hili jambo lipate baraka
za Mungu. Love akanieleza mambo mengi akisaidiwa na mama yake. Mama yako
huyu hapa, muulize.”
“Sasa mbona lakini uliwakubalia wao na tukaishi?
Hivi ni kwa nini mimi unakua mgumu sana kuafikiana na mambo yangu!?” “Yaliyo
sawa hata machoni mwa Mungu, na ambayo na mimi naweza fanya, nitasimama
na wewe mpaka mwisho wake, kwa garama yeyote ile. Lakini siwezi ukawa unalala
kwako kwa amani, halafu eti mimi nabakia nikikesha natubia dhambi
zako. Hapana.”
“Wewe baba…” “Acha kunipotezea muda wangu, na maneno
mengi na kupoteza amani ya humu ndani kwangu, Colins. Kamila hataondoka
humu ndani, mpaka kwa utaratibu maalumu. Hiyo ndio kauli ya mwisho.
Hakuna wakumtumia tena huyu binti bila kibali maalumu. Sitajirudia
tena kwako Colins. Na hiyo ndio kauli yangu ya mwisho kwako.”
“Ila kuishi na Love aliyekuwa akinitesa ni sawa!” “Sasa iliwafikisha
wapi? Jiangalie ulipoishia na yeye alipoishia baada ya yote hayo,
bila baraka za Mungu. Wewe unataka kujifunza lini Colins!? Unataka kuteswa
na shetani mpaka lini ndio ukimbilie chini ya rehema za Mungu? Unafikiri ni
wewe peke yako ndio uliyeanza kupenda wasichana wazuri, wengine
hatukubahatika?”
“Muulize mama yako kama mimi nilimfanyia mambo ya vichochoroni.
Au muulize mama yake. Nilimuheshimu mpaka nilipomuoa. Leo unataka
ufanye ujanja ujanja kwa binti wa watu! Hapana Colins! Kama wewe mnywaji
wa maziwa kweli, nunua ng’ombe na mimi nitakusaidia.” Akasimama kwa
hasira.
“Na nakuonya usibamize mlango wowote unapotoka
hapa. Mke wangu ana pressure.” Colins alikaribia kupasuka. “Unanielewa
Colins?” “Hakika sitakujibu baba. Nina hasira ya kupitiliza.” “Basi
usiende kumalizia hizo hasira zako kwenye milango yangu. Taratibu.” Akaondoka
kabisa hapo ndani. Mama yake na Connie kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~
Haya tena, kwa mara nyingine tena, Colins anapambana na baba yake
kwenye maswala ya mwanamke. Safari hii itakuaje?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment