![]() |
Mwishoe akamtumia ujumbe. ‘Bakisha nafasi ya dessert
tuje tule wote.’ Akaona simu ya Kamila inaingia. Akajua
amesoma ujumbe. “Nimechelewa sana?” “Hapana. Kuna dessert nzuri sana,
inayoendana na mapishi yako, nilikununulia, pengine utaipenda. Sikutaka ushibe
ukashindwa kula tukiwa wote usiku wa leo.” Akajua
ilikuwa ni njia tu ya kumwambia arudi nyumbani, ila akafurahia. Kwamba usiku
huo atakuwa na Colins! Akajawa furaha. “Asante kunifikiria. Nakuja.
Sipo mbali na nyumbani.” “Basi nitakuwa nikikusubiria.” “Sawa.” Kabla hajakata simu, akaongeza.
“Umekua na
wakati mzuri lakini?” “Inatosha kwa leo.” “Mbona kama nakusikia hujafurahia?”
“Watoto wamekua, halafu wamebadilika, sio kama mara ya mwisho nilivyowaacha.”
“Wamebadilika kwa uzuri au ubaya?” Akaendelea
kudodosa kumuonyesha anajali.
“Nafikiri kule
kufungwa kwa Mill, na kuwaacha watoto na mkewe pamoja na huyo mwanaume,
kuliharibu sana. Sura ni Mill, ila tabia! Mmmh! Mpaka namuhurumia Mill. Ila
mwenyewe anaonekana ana imani! Anaamini watabadilika.” “Na mimi naamini hivyo. Poleni.” Akamsikia
akicheka taratibu, na kuongeza.
“Nahisi
kama Mike angekuwepo, angemsaidia zaidi kuliko mimi nisiyejua chakufanya! Mike
ana namna yake na watu. Mimi najiona sio msaada kabisa! Najiona kama sitaweza
kumsaidia kwa chochote.” “Wakati mwingine watu hawategemei msaada mkubwa sana
kama ambavyo ungeweza kufikiria. Ile tu kumuonyesha upo, na unajali, inaweza
kuwa msaada tosha.”
“Usiwakatie
tamaa watoto, na mtie moyo Mill. Ni watoto, wapo kwenye kukua, wamepitishwa
kwenye magumu, naamini watakuja kuwa sawa tu. Na wewe usijidharau na
kujikatia tamaa. Mungu anajua wewe ni mtu sahihi kwao kwa wakati huu.”
“Nashukuru
kunitia moyo. Na kweli Mill anahitaji mtu. Amerudi amejikuta yupo peke yake!
Marafiki wamesambaa na maisha yamebadilika. Amekwama peke yake na watoto.” “Inamaana
hiyo ni nafasi nzuri kwake. Atapata muda wa kutosha na watoto wake. Sio jambo
baya. Wakati mwingine kuna mambo Mungu anaruhusu kwa mtu kwa kusudi.
Inawezekana alihitaji huu muda wa peke yake ili atulize akili kwa wanae.”
“Pengine kweli! Bora kumbe nimezungumza na wewe! Sasa naona na mimi
niliongezeka kwenye tatizo.” Akamsikia akicheka.
“Kwa nini
tena?” “Mwenzio nilikuwa sijui chakufanya. Kila wakati nalia. Namwambia bora
Mike angekuwepo. Basi nikawa namtia na yeye simanzi. Mwishoe nikamwambia
bora niondoke tu. Nikaondoka kwenda madukani ili tu kutuliza mawazo. Nimefika.
Nakuja ndani.” “Nije kukupokea?” Mpaka
Kamila akashangaa.
“Hamna
haja. Sina mizigo mingi, nimenunua vitu vichache tu. Nakushukuru.” Wakaagana ila na maswali. Colins wa jana siye huyu! Huyu
amebadilika kweli! Anajali kupita kiasi na ameanza na mabusu
ya shavuni! Kumsubiria, na kutaka kumpokea kabisa! Kamila akabaki
akijiuliza ila kwa furaha.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akamkuta akimsubiria nje ya mlango. Akaanza kucheka.
“Kama umenimiss vile!” Akamuanza akicheka. “Sana. Nimekuzoea Kamila.
Najua unaweza usielewe kwa sababu pengine kwa nje sijakuonyesha, lakini
uwepo wako kwangu ni faraja. Natamani kuwa na wewe wakati wote.” Kamila
asiye na makuu akafurahi huyo!
Akabaki akicheka. “Umekula vizuri?” “Mimi nipo sawa. Na
wewe?” “Na mimi nimekula. Ila nimenunua desert nzuri, tuje tule wote.”
“Basi acha nikaoge, nije tule. Au umechoka, unataka kuwahi kulala?” “Hapana.
Kesho nitakua off, siwahi kulala.”
Kisha akaongeza sauti akiangalia ndani kusudi. “Tunajiandaa
kucheza karata. Nataka kumfunga mzee kabla hajalala.” “Acha kumdanganya
Kamila.” Sauti ya baba yake ikasikika ndani.
Wote wakacheka. “Huwa anabishaga hivyohivyo, ila
anaishia kwenda kulala mnyonge!” “Wewe usiongee sana. Acha muda ujibu.”
Kamila akaingia akicheka. “Pole baba yangu. Kumbe ndio hali inakuaga mbaya
hivyo?” “Anakudanganya tu. Huwa tunawafunga sana hao wawili. Ni vile Connie hayupo.
Lakini humu ndani ushindi uliozoeleka, miaka yote, ni mimi na Connie.
Yeye na mama yake ni udhulumishi kila wakati.” “Baba!” “Sasa unachobisha
ni nini wakati tutacheza hapa na yeye atapata majibu yake! Wala hakuna
sababu yakubishana.” Kamila akazidi kucheka.
“Sasa na Connie anakuja. Leo anakuja kulala nyumbani.
Ndio tuone, uache visingizio. Maana huwa haishiwi sababu huyo baba yako.”
Wakasikia sauti ya mama yao jikoni. Kamila akazidi kucheka, ila Colins ikamuingia
mpaka nafsini mwake.
Inamaana kweli
dada yake alikuwa akiogopa kurudi nyumbani sababu yake! Kidogo
akanyongea akiamini maneno ya mama yake kuwa ndiye aliyekuwa akipoteza amani
ya pale kwao. Ule msamaha na kuzungumza naye, umesaidia!
“Sasa sio aje amechoka, tukafungwa mkase…”
“Umesikia Kamila? Ushajua ambao wanafungwa humu ndani. Visingizio ndio
kama hivyo!” Kamila akazidi kucheka. “Hawa wawili wanachagua zile siku
wanazojua mimi na Connie tumechoka, ndio wanataka kucheza ili kusudi
tu, watupate akili ikiwa haiwezi kufikiria, wajichukulie ushindi.”
“Kamila ameshapata jibu baba. Wala usiendelee kujitetea.”
Wakazidi kubishana wakicheka. “Basi nakuja sasahivi. Acha nikaoge nije
nishuhudie.” Ni kweli Colins alikuwa ameshika amani ya humo ndani.
Nyumba ilikuwa imechangamka na kumejaa amani kama zamani, wala Kamila hajawahi
ona kabla.
Colins Kabadilishia Gia Kubwa Angani.
Anaingia chumbani kwake akiwa amejawa furaha na hamasa
kuwa Colins amejirudi, kumbe ni zaidi ya hivyo! Akakuta kitandani kwake kuna
maua rose, mekundu tupu. Pembeni ya hayo maua kuliwekwa kadi
kubwa hasw a ndani ya bahasha nzuri nayo ya rangi nyekundu. Kisha kukawa kama
kumemwagwa na chocalate pembeni yake. Kamila nusura arukeruke akijua
vinatoka tu kwa Colins.
Akatupa kipochi na mizigo yote sakafuni na kuvamia maua.
Akayanusa na kujitupa kitandani akiwa ameyakumbatia. Akayaacha kifuani na
kufungua kadi imeandikwa hivi, ‘I’m Thankful for you.’ Moyo ukazidi kujawa furaha. Kufungua ndani ilikuwa
imeandikwa kwa mkono. Akaanza kusoma.
‘Kamila,
sikujua kama kuja kwako kwenye maisha yangu ni upendo wa Mungu kupita kiasi
kwangu. Katika mapungufu yangu yote, natambua umuhimu ‘wako’ kwenye maisha yangu.’ Kisha akaendelea.
‘Unaweza
usielewe Kamila, lakini umeyabadilisha maisha yangu kwa haraka
sana. Sikuwa hivi! Nikidhani nakusaidia wewe, nimekuja kugundua kumbe
nilikuwa nikijisaidia mimi mwenyewe.’
‘Naweza
nikawa sijakuonyesha vya kutosha, uthamani wako kwangu, lakini uwepo wako
kwangu, nimegundua imekua faraja niliyokuwa nikiitafuta muda wote,
maishani mwangu. Kuna jinsi ulinishika, uliamsha hisia ambazo ziliuwawa
muda mrefu sana, kwenye maisha yangu mpaka nilijikatia tamaa.
Sikujua kama zingeweza kuja kurudi mpaka WEWE uliponishika.’ Bwana Kamila
alifurahia.
Akajua ni ile masaji
tu. Akidhania siku ile alijidhalilisha, kumbe amefanya jambo kubwa
la kuja kutunzwa moyoni kwa Colins! “Inamaana katika hili nimempita hata Jelini!”
Kamila asiye na makuu, akaanza majigambo nafsini kwake akiridhishwa na sifa
hiyo.
‘Wanasema better late than
never. Najua nimechelewa. Pengine nimekuumiza kwa maneno na vitendo,
naomba unisamehe. Lakini mimi mwenyewe sita jisamehe endapo nitashindwa
kuomba nafasi kwako.’
‘Nina uwezo
wa kwenda kuishi kwangu, lakini moyo wangu umeshindwa kukuacha Kamila.
Najihisi wewe ni nafasi ya pekee Mungu amenitumia, sitaki
kuipoteza. Umejawa upendo. Hujui kutunza vitu vibaya moyoni. Unajali kupita
kiasi! Halafu ni mkarimu.’ Hapo akagutuka. Ametoka kufanya manunuzi, hajamnunulia kitu!
“Mkarimu!” Akajisuta.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ila alihofia asije
rudia kosa. Kumnunulia zawadi kwa nia njema, halafu kuja kumuumiza.
Akatulia akiangalia zawadi alizomjazia yeye pale kitandani, akatamani na yeye
angemnunulia hata pipi tu, kama alivyomfanyia yeye na kumpelekea kabisa!
Akapotelea mawazoni akijilaumu kushindwa kufanya hivyo akiwa madukani, kisha
akumbuka kurudi kusoma.
~~~~~~~~~~~~~~~
‘Naahidi kubadilika
ili nisikuumize zaidi. Naweza kuwa nimekuchanganya kutokana na nilivyokuwa
nimekwambia juu yangu, na wewe. Lakini huu ndio ukweli ambao pengine nilitaka
kuupuuza. Nimegundua nitajipunja mimi mwenyewe endapo nitakukosa
wewe, Kamila. Kama sijachelewa, tafadhali naomba nifikirie mimi.
Usimpe mtu mwingine nafasi ya Mike moyoni mwako ila mimi.
Nakuahidi kuitendea haki, sitakuumiza.’ Ilimgusa Kamila mpaka akajishika
moyoni.
‘Kama
nilivyokwambia, sitakaa niwe Mike, sitaweza vaa viatu vyake, sitaweza
ziba pengo lake, lakini naahidi ukiwa na mimi kama Colins, na wewe hivyohivyo
ulivyo. Nikijua na kuelewa wewe sio Jelini, na sitaki uwe Jelini.
Nakutaka wewe kama Kamila. Hivyohivyo ulivyo umbwa na Mungu nikiamini ni kwa
ajili ya mapungufu yangu. Naamini tukipeana nafasi tutakuwa na wakati
mzuri sana hapa dunaini. Nakuhitaji Kamila.’
Kamila hakuamini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudia tena na tena. Na kuhakikisha kweli inatoka kwa
Colins. Alijawa furaha! Akamsamehe dhambi zote. Yaani akawa hakumbuki
tena hata ya Jelini. Akawa anajiona tu yeye atakavyoanza kupata kiss
kutoka kwenye midomo hiyo miekundu kama pinki ya Colins! Atakavyoshikwa
naye! Hiyo sauti yake nzito ya kiume atakavyokuwa akiisikia masikioni
kwake, akiwa amemkumbatia akimbembeleza! Raha kama zote!
~~~~~~~~~~~~~~~
Akabaki amekaa kitandani anagaragara na maua, anarudia kusoma huku anakula chokleti, kumbe
huko mwenzie mapigo ya moyo yanakwenda kasi akijua Kamila amesoma, na yeye anamlaumu
kama Jelini, hamtaki. Tumbo likaanza kumnguruma Colins, kadiri
alivyokumbuka maneno aliyokuwa akimwambia Kamila.
“Aisee nimekurupuka vibaya sana! Bora ningefikiria
kwanza.” Colins akazidi kuwaza. “Au pengine
ningeanza kwa kujirudi taratibu. Ningejipa muda. Yaani kama hivi nilivyofanya
leo, ningefanya hata kwa siku 7 mfululizo, ndio nimwambie!” Akaendelea
kujivunja moyo.
“Sijui nilikuwa nikifikiria nini! Ndio nitakuwa
nimemfukuzia mbali kabisa! Na alivyo mzuri hivi Kamila! Mwanaume yeyote ambaye
angepewa nafasi kama yangu, anayejielewa, angempokea kwa haraka sana, tena kwa
mikono yote miwili! Nimejichanganya na kujichelewesha kwa ujinga wangu mimi
mwenyewe! Daah! Nimemkosa na Kamila naye hivihivi!” Akazidi kujiumiza, akijua yeye mwenyewe amerudisha historia
kama ya kwa Jelini. Na Kamila naye atabaki akimlaumu hampendi,
anayependwa ni Jelini. Kumbe mwenzie huko ndani, amejawa furaha, hana
hata wazo la Jelini!
Mama ni Mama.
Mpaka Connie anafika hapo, Kamila hajatoka chumbani
kwake. Wakasalimiana, ila akagundua hayupo sawa na wakati waliagana vizuri tu! Sasa
hao watuhumiwa wawili, madaktari wa Muhimbili, wakamgeukia mkombozi
wao. Mama yake. Alipoona Connie na baba yake wanamwangalia, akaelewa.
Akamtoa hapo. “Coly, njoo nisaidie kitu hapo jikoni.”
Akanyanyuka kwa haraka tu, bila ya kufikiria wala asijue alikuwa amekaa
wapi, kumbe ilikuwa sebuleni, katikati ya wote, yeye kimawazo hakuwepo
hapo.
“Ni nini tena Colins?!” Mama yake akamuuliza mara
walipofika jikoni nakujikuta wapo peke yao. “Hamna shida. Nahisi najipanikisha
tu.” “Kwa nini?” “Mbona Kamila hatoki chumbani?” Mama yake akawa hajaelewa.
Akamuelezea mama yake kwa kifupi na kuongeza.
“Nimerudia kosa nililofanya kwa Jelini, mama.
Halafu nimeharakisha kumwambia kama namuhitaji. Ataona nina mdanganya!
Au sijielewi! Sijui ninachotaka!” Akajikuta anajisalimisha kwa
mama yake.
“Inawezekana mwenzio hafikirii hayo kabisa! Unajipanikisha
tu bila sababu. Nimemsoma Kamila, kwa haraka anaonekana ana moyo mzuri.”
“Sasa unajuje kama hata katika hili atalibeba vizuri?” “Sasa kabla
hujanikatisha na mimi tamaa, na kunitia wasiwasi wako, nenda ukamgongee ujue
kinachoendelea, kuliko hicho unachokifanya sasahivi hapa.”
“Nisije..” “Colins! Niangalie mimi.” “Nakuangalia mama!”
“Hapana. Nataka utulize mawazo hapa kwangu, uniangalie na kunisikiliza
ninachokwambia. Wewe umepaniki, na kusahau huyu msichana alikuwa akikuomba
nafasi hii muda mrefu sana ila wewae ndio hakuwa tayari.” “Sasa
si ndio ninachokwambia sasa! Pengine atakuwa amechoka, hataki tena!”
“Mapenzi ya kweli huwa hayafi kwa haraka
kiasi hicho. Na katika hili ndio utagundua kama umepeta wako wa ukweli au
la. Hii ndio nafasi ya kweli na ya pekee itakayokusaidia kujua kama kweli
alikupenda au alibabaishwa na huo uzuri wako tu.” Colins akaanza
kucheka.
“Muone! Nenda.” Akambusu mama yake na kumkumbatia kwa
muda mrefu. “Ujue nilikumiss sana?” Kisha akaongeza. “Wewe ndio msiri
wangu, nashangaa kwa nini unakubali kuyumbishwa!” “Unapoteza muda, nenda Coly.
Na usiende kinyonge, utaanza kwa kumboa. Jibebe kijasiri kama
ambaye unajielewa na unamaanisha ulichomwandikia.” Akatoka hapo jikoni jasiri
kama sio yeye!
~~~~~~~~~~~~~~~
“Na mimi nilikumiss
Connie. Nisubiri tutapata muda mzuri. Tuwafunge madaktari wa Muhimbili, ndio
mkalale.” Akatupia neno akipita hapo akielekea chumbani kwa Kamila, angalau wakaanza
kucheka tena. “Hizo ni dua za kuku.” “Sawa baba.” Akapotelea koridoni
akifuata chumba cha Kamila.
Msamaha ni kwa ajili yetu.
Hufungua milango mingi na migumu ambayo
haifunguki kwa chochote isipokuwa
kuachilia uchungu
moyoni na KUSAMEHE.
Usipitwe na usiku wa Kamila & Colins.
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment