“Mbona huniangalii? Nimekuudhi nini tena!?” Colins
akasogea kabisa. “Hamna kitu.” “Mama!” “Uliponiambia unahisi umechelewa,
ulimaanisha nini?” Colins akabaki akimwangalia. “Coly?” “Haina maana tena mama!
Wewe acha tu kama ilivyo.”
“Labda nikuulize, unategemea Jelini aje aachane na
mchumba wake akurudie wewe?” Colins akaanza kubadilika sura. Nakushindwa
kujibu. “Kabla hujapandisha hasira, naomba utulie na kutafakari. Makosa yalishatendeka. Mimi na baba
yako tulishakosea. Maisha ya Jelini yanaendelea kama kawaida. Utabaki na kushikilia ya zamani mpaka lini?” “Hayo
yote yanatoka wapi?!” Colins akashangaa sana.
“Huwezi
kutengeneza nyuma Colins, ila kuanzia pale uliporudiwa na akili zako. Kwa jinsi
ulivyoweza kutengeneza kwingine kote, ukijisahau wewe mwenyewe, jua na yako unaweza tengeneza na ukaishia kuwa
na furaha. Mungu si mwanadamu hata
aseme uongo. Mungu ni mwingi wa upendo. Hajaishiwa upendo hata mara
moja na hataanzia kwako. Sasa toka
huko unakojificha, na kushikilia kisicho chako, tengeneza yako.” Kabla
hajajibu mama yake akaongeza.
“Kuna mambo magumu
huwa yanampata mtu, kwa haraka yanakuwa hayana
majibu, lakini si kwa Mungu. Wakati
mwingine ni yeye mwenyewe anatunza waovu
kwa siku ya maangamizi. Soma.{Mithali 16:4} Huwezi jua alitutumia sisi kukuumiza ili aje akupe kitu kizuri zaidi.” “Zaidi ya Jelini!?” “Wewe ulishamuoa Jelini, ukaishi naye kama mke nyumba moja? Ukajua anavyokua akiwa mjamzito na
amezaa, kisha mkapita naye kwenye
maisha yote, shida na raha! Ugonjwa na uzima. Kisha ukamjua kwa undani wote mpaka
sasahivi ubaki unashikilia hutaki kuachia kama hivyo Kamila alivyoishi
na Mike?” Kimya akiwa amemfanya afikirie.
“Wewe mwenyewe umesema ulishindwa kutengeneza kumbukumbu nzuri kwake. Sasa kinacho kushinda kuanza upya ni nini kama si
kutaka kuendelea kujiharibia zaidi?”
Kimya. “Eti Coly?” “Nyinyi ndio mmeniharibia mama!” “Kwa hiyo? Unataka kukaa
hapo mpaka lini? Utatulaumu mpaka lini? Utajiadhibu mpaka lini? Maana
unachokifanya hapo ni kuendeleza pale sisi tulipoharibu. Tena wewe ndio
unafanya vibaya zaidi.” “Kivipi?” Mama yake akabaki akimwangalia.
“Mama?” “Hivi unanisikia kweli ninachokwambia Coly au
umeamua kuendelea kubeba hasira tu? Mpaka lini!? Au unachotaka ni
nini kitokee ili uweze kusamehe na uendelee?” “Siwezi kusahau?” “Umeshanisikia
mimi nikikwambia sahau?!” Akamuuliza kwa ukali kidogo ila kwa sauti cha
chini kama akinong’ona. Colins hakutegemea. Akabaki kimya maana ni kama
alimvamia.
“Eti Coly? Umesikia hawa wawili jinsi wanavyoimba sifa
za Mike. Na vile alivyompenda Kamila. Na Kamila kumsubiria kwa muda wote
huo mpaka kujiridhisha kweli amefariki. Lakini mbona mwenzio Kamila amekubali
kuendelea, wewe umegomea hapohapo?” Akabaki kimya.
“Jambo hili utabeba
mpaka lini baba mzazi wewe? Eti Coly? Utanichukia mimi mpaka lini?
Wengine watapita na kubadilika majina kwako, lakini mimi ni mama yako tu. Niwe
hai au nimekufa, nitabaki mama daima. Huwezi badilisha. Na baba yako
hivyohivyo. Mwenyewe ulisema hukujaliwa wazazi wazuri. Kwa hiyo?!”
“Nilihitaji muda.” Akajirudi taratibu. “Basi ujue unakaribia
kuchelewa. Huko unakojificha, unapoteza muda. Ukija kutoka huko, utajikuta
unakosa bara na pwani, wakati wenzio maisha yanaendelea, wewe unajiumiza tu. Mimi nakwambia ukweli.
Hata ukinichukia zaidi, huo ni ukweli. Unajichelewesha na unajinyima raha
na faraja wewe mwenyewe. “
“Jelini anaolewa, kwake hurudi tena. Kubali huo
ukweli na utoke hapo.” Akampita na kuondoka zake, akamuacha amesimama hapo
jikoni.
Sharp Corner.
Akasimama hapo akijua mama yake yupo sahihi. Ikawa kama
kengele masikioni kwake. Lakini anafanyaje? Aliyebaki karibu yake ni Kamila na kwake
nako ameshaharibu. Ni kweli Jelini hatakaa akamrudia tena.
Anafanyaje? Akaona kilichobaki kwenye hiyo safari aliyokuwa akiendesha
kwa mwendo kasi karibu aingize gari korongoni au tayari amefika ukingoni,
basi ni kukata kona kali/sharp corner.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akajikuta
anakwenda mpaka chumbani kwa Kamila, akagonga. Baada ya muda mfupi
akamfungulia. “Nimekuamsha?” “Hapana. Bado sikuwa nimelala. Vipi?” Akamuona
anasita ila anatilisha huruma.
“Nikikukaribisha ndani itakua vibaya?” Colins
hakutegemea, maana alibakia mlangoni akijua na hiyo siku atarudishiwa
mlangoni. “Nitashukuru Kamila.” Ikawa kama anaibembelezea hiyo nafasi ya
kukaribishwa ndani. Akampisha mlangoni. Akaenda kukaa mwanzoni mwa kitanda
akainama kama anayetafuta jinsi ya kujieleza. Kamila akaenda kukaa mbali kabisa
ila hapohapo kitandani na kunyamaza.
“Nakujali Kamila.” Akavunja ukimya. Kamila akamwangalia.
“Nakujali na sitaki kukuumiza.”
Kamila akamwangalia kwa muda na kuinama. “Nia yangu haikuwa mbaya kwako. Nataka
kukuona na furaha.” “Hujaniumiza Colins. Kwa vyovyote utakavyoniona, jua ni maumivu ambayo tayari ninayo, wala wewe
huusiki na kuwepo kwake.” “Una uhakika?” “Kabisa Colins! Ungekuwa mwanaume tapeli, ungenitumia vibaya kwa sababu
nilikuwa kwenye kipindi kibaya. Lakini binafsi nimekuheshimu. Nimeona
umenithamini na kuniambia ukweli japo nilianza kuonyesha nia mbaya.”
“Naomba usiseme hivyo.” “Ni kweli, wala si uongo. Amini nimejichukia Colins. Sijui nilipatwa na
nini! Nahisi ni hofu ya kubaki peke
yangu, na wewe ukawa umenielewa, nikapitiliza.
Lakini mimi sio msichana wa namna hiyo.” “Sikuelewi vibaya hata kidogo, ila
najilaumu.” Kamila akakunja uso akimwangalia.
“Kila Mungu anaponitumia bahati, inanikuta nipo katikati ya mambo mengi, akili haijatulia.
Najikuta nikiharibu na kuumiza nilioletewa
kwangu kwa upendo.” Kamila akamwangalia kama akijaribu kumuelewa akashindwa,
akaangalia pembeni akifikiria.
“Nilimuumiza sana Jelini. Sana. Tokea mwanzo mpaka sasa haamini
kama kweli nampenda. Ila ni kwa kuwa alinikuta katikati ya mahusiano ya utata, sikutaka kumchanganya kama hivi wewe.
Nimefanikiwa kujitoa huko, kwa shida. Mpaka nakaribia kumalizana huko
nilikokuwa, nimejikuta nimempoteza
Jelini na hajui kama nilimpenda kwa dhati! Sasa najihisi narudia kosa.” Kamila akamwangalia na kunyamaza.
“Na sijui kwa nini nazungumza yote haya! Samahani. Nahisi
nimekuja tu bila kufikiria.”
“Usijali. Tafadhali kuwa na amani. Naamini utakuwa sawa tu. Binafsi naona watu
wa aina yako ni wachache sana. Umeongezeka kwa Mike na Mill. Hao ndio
wanaume niliozungukwa nao, naweza wafananisha na wewe. Usijilaumu, ni tabia
nzuri.” Colins hakutegemea.
“Kweli Kamila!?” “Kabisa Colins. Sio kitu kibaya. Binafsi
nimekuweka kwenye kundi la hao wachache niliofanikiwa kuwa nao karibu huku
wanawake wakiwatolea mate, lakini wakabaki na msimamo. Ngumu
kumzungumzia Jerry kwakuwa mwanamke wake anamchunga sana, lakini hao
wawili ni kama wewe. Wana msimamo na
mambo yao. Hawana tamaa. Wakiwa kwenye mahusiano, wanasimamia hayo
mahusiano.”
“Hata Mill kuoa huko, si kwa kupenda au tamaa!
Ilimlazimu lakini ni kosa anajutia mpaka leo, kama ulivyomsikia mwenyewe.
Alimpenda sana Pam. Anahisi anapata mikosi sababu ya kumuumiza Pam.
Ameshindwa kujisamehe kabisa japo alichofanya ni jambo la kawaida kwa wanaume
wengine.”
“Kwa hiyo usijiumize Colins. Ni tabia nzuri.
Mwanamke atakayefanikiwa kuishia na wewe, atafurahia hili na atakua
amebahatika sana. Wewe ni muaminifu kwenye mahusiano. Si mkimbiaji hata
maji yakizidi shingoni. Kwa hiyo kamwe usijitilie mashaka. Naamini ni muda tu,
Colins. Utakuja kupumzika siku moja na utasahau yote haya.”
“Daah! Sijui ni lini aisee! Mpaka nakata tamaa! Naona naharibu
kila mahali na sijui au sina uwezo wa kutengeneza.” “Ni muda tu. Na ninakuhakikishia utasahau. Mimi
nazungumzia kwa kuwa nilipita hapo na najua pumziko unalopata unapopata mtu
sahihi na yeye akakupenda. Utafurahia na kusahau yote.”
“Fanya kama ulivyoniambia mimi. Weka sawa mambo yako na
Jelini. Ukijiridhisha, usiogope kufungua moyo kama ulivyoniambia mimi. Celine
aliimba huu wimbo. Mike aliupenda sana. Alisema hivi, ‘Love come to those
who believe it.’ Ukiamini, hutaishia
pabaya.” Colins hakutegemea.
“Kumbe ni afadhali nimekuja kuzungumza na wewe!” Kamila
akacheka na kunyamaza. “Nimefurahi umeweza kunielewa. Nahisi ni kilema
kinachowaumiza wengi.” “Ni maumivu
ya muda tu, tena si mabaya. Lakini
mtu yeyote akitulia na kukutafakari,
hicho unachosema ni kilema, utatamani wanadamu wote wawe nacho.” Angalau Colins akacheka.
“Kweli Colins. Una msimamo
mzuri. Nenda kapumzike.” “Na wewe unalala?” “Bado. Nimemuona Mill, siamini!
Hapa nilikuwa nikichat naye, tena
baada ya kuzungumza naye kwenye simu bila kumaliza. Tunakuaga na stori tokea
sekondari na mpaka hivi sasa. Ana haiba ya kujali kama Mike, kumpata
hivi, ile hofu yote niliyokwambia
ninayo, imeisha.” “Nimekuona!” Akacheka
wazi akionekana na tumaini jipya.
“Nilikuwa naogopa sana. Mike alikuwa mzuri sana wa
mipango.” “Hata Mill amemsifia.” “Sasa bora mwenzangu yeye anaikumbuka, na
kuitendea kazi. Lakini mimi nilijawa hofu, nikawa sikumbuki kila kitu.” “Sasa hivi umekumbuka?” Akaanza kucheka
akitingisha kichwa akikubali kwa furaha. “Kichwa kingine kimerudi! Sina hofu tena. Na safari hii naandika
kabisa. Sitaki kujikuta naanza kila wakati.”
“Utanikimbia kila mahali Kamila! Nyumbani, kwenye gari na
kazini! Unaniacha mpweke! Nahisi nishakupoteza
na wewe!” “Huwezi poteza kitu ambacho hujawahi kuwa nacho Colins.”
Colins akashituka kidogo ila akajikaza na kuuliza.
“Kivipi tena?” “Kwenye gari tulikuwa wote,
lakini ulikuwa hata hujui kama nipo! Ulikuwa ukimzungumzia Jelini tu
na kupotelea mawazoni hata hujui kama na mimi nipo.” Hapo ndio
akawa kama anamfungua macho, asiamini.
“Kweli Kamila?!” “Kabisa. Na kazini kwenyewe
ilikuwa ni mpaka nikutafute mimi. Nikinyamaza na wewe hutajali mpaka…” Akasita ila akabadili
na kuendelea. “Na hapa nyumbani nilibaki kuwa kama mzigo kwako. Nakuomba
vitu vilivyokuwa vikikunyima raha! Hunihitaji Colins. Huwezi kuwa mpweke
na wala hutanipoteza kwa sababu hujawahi kuwa na mimi. Utakua tu
sawa, usiwe na wasiwasi wakupoteza ambacho haukuwa nacho.” Hakutegemea.
Akamwangalia na kuinama. Akajua huo ndio ukweli.
Kwengine kule ni jumla yake. “Daah!” Akamsikia akisikitika. “Utakuwa sawa
Colins.” “Na sisi?!” Akamuuliza swali ambalo akashindwa kujibu. “Eti Kamila? Na
sisi, baada ya yote hayo, tutakuja kuwa sawa tena!?” Jinsi alivyomuuliza
kwa kumbembeleza, hiyo ikamuingia mpaka rohoni. Akamuona kama anayetaka kutokwa
na machozi.
Ila akajibu kwa kujihami asijekuwa amemuelewa vibaya. “Naamini
tutakuwa sawa Colins. Sasahivi nimekuelewa.” Akamwangalia kwa muda mpaka Kamila
akainama. “Nikuombe kitu?” Kamila akamwangalia na kumuuliza, “Nini?” “Naomba usinikatie
tamaa. Naomba nipe muda. Usinifungie milango yote. Naomba nitakapoweka
mambo yangu sawa, nisiwe nimekupoteza na wewe. Tafadhali Kamila.”
“Mimi nipo Colins. Unakumbuka nilikwambia hivyo?” “Naona
mambo yanabadilika kwa haraka
haraka! Mpaka naingiwa hofu nahisi
kukupoteza tayari.” Akazidi kumlainisha nafsi. “Mimi nipo Colins. Sina ninapokwenda ila tu narudia ndoto zangu.
Hichi ulichonipa ni cha thamani sana. Sina nitakapokwenda nikakipata. Nahisi
nyinyi wote, mpaka Connie, mtaondoka hapa, mimi mtaniacha.” Colins akacheka akimwangalia.
“Huondoki?” “Niende wapi tena!? Mwenzio nilikuwa nalala
kwenye gari na pesa ipo benki. Ilimradi tu niwe na wale watu pale japo walikuwa
wakininyanyasa. Mwenzio napenda undugu. Na hivi Mill naye amekaribishwa
na wanae!” “Kumbe nyinyi mnachukulia kwa ukubwa huo!” “Hatutanii sisi.
Hapa Mill ashajiandaa jumapili kuleta wanae hapa, waanzie kanisani na wazazi.
Anataka wanae wabadilike, wawe kwenye familia kama hii pengine itawasaidia.
Kwa hiyo hapa sisi tupo sana, mpaka mtatuchoka.” “Wazazi wangu hawana neno.
Ndio vizuri tutakuwa wengi.” Angalau akawa ameupata moyo wa Kamila.
Alijaliwa moyo mwepesi. Huhitaji mambo mengi kuupata moyo
wake. Anaridhika na vitu vidogovidogo! Mpaka Colins anatoka hapo, amefarijika
na Kamila anacheka.
Jumamosi.
Asubuhi akiwa anavaa akasikia hodi. Akatupia jicho kwenye
saa ya ukutani. Bado ilikuwa mapema. Akajiuliza ni nani mida hiyo anayemgongea,
haikuwa kawaida! Akajifunika kwa haraka na kufungua.
“Colins! Mbona mapema? Kwema!?” “Nimekuja kukuaga, nisiondoke kimyakimya.
Nakwenda kazini.” Kamila akacheka kwa kujisuta akikumbuka lalamika yake
ya jana usiku.
“Mbona mapema!” “Usingizi nao ulikata mapema, nimeona
niende tu nikaanze siku, ili na mimi leo niwahi kutoka, nipumzike. Wewe si upo
sawa swala la usafiri?” “Kabisa. Na mimi nitatoka muda si mrefu ili niwahi foleni.”
“Basi nitakuona kazini. Kuwa mwangalifu barabarani.” “Na wewe.” Akashangaa
anamsogelea na kumpa busu la shavuni. Hakutegemea, ila alifurahia sana.
Akacheka na kujishika shavuni. “Asante.” Akamshukuru, Colins akacheka na
kuondoka akamuacha ameduaa, mkono shavuni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye majira ya saa nne hivi akiwa katikati ya
maandalizi ya chakula cha mchana, akasikia watu wakisalimia kuanzia mlangoni
kisha mzee Yusuf. “Leo umetutembelea bosi wangu! Au ukaguzi?” “Hii ofisi yako
wewe mwenyewe ukiwepo, sina shida
nayo. Naona mnapamudu. Napita tu
kumuona Kamila.” “Sasa hapo tena ndio ujue umeharibu
siku yangu nzima!” Kamila akaanza kucheka. Ukaanza utani.
Kina Dula ushabiki!
Kamila hana mbavu. “Mzee Yusufu, nimesema napita tu kumuona! Simchukui! Wewe unashinda naye hapa siku nzima! Mimi
namuona tu, na zawadi kidogo, basi.” “Zawadi tena!?” “Ni pipi tu mzee wangu!
Usiingiwe hofu na wala siwezi
kukushinda wewe unayemlisha siku nzima!” “Ulikumbuke hilo Kamila! Mimi nakulisha hapa siku nzima! Sasa sio urubuniwe na pipi tu.” Cheko mtoto wa
kike, angalau hapo akapachangamsha, Kamila akamfuata.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakatoka. “Wenzio wanakuogopa!” “Kweli!? Kwa nini!? Mbona
wamenichangamkia tu!” “Wanasema wewe hupendi ujinga kama yule meneja mwingine aliyekuwa hapa. Alilala na kila
mwanamke hapa. Kuanzia wafagizi mpaka manesi! Wewe hutaki mazoea ila kazi.” Colins akacheka tu bila ya
kuongeza.
“Nimekuletea pipi na kukuomba tule wote chakula cha
mchana.” “Asante kwa pipi, lakini
hapa nishamrubuni Mill, anakuja kwenye mida ya mchana tule naye, jioni nitawahi kutoka kidogo, nikaone watoto.” Colins
akawa amekwama.
“Ila nakushukuru. Nimefurahi.” Colins akabaki akimwangalia.
“Nikuletee chakula ofisini au utatoka?” “Kama nitatoka nitakutaarifu.
Asante.” Akacheka kwa kuridhika akimwangalia asiamini hayo mabadiliko! Colins
anajirudi kwa vitendo wala si maneno!
“Kwa hiyo unahama lini?” Akamuuliza taratibu wakiwa
wamekaa tu hapo nje ya jiko. “Sijui Kamila! Sitaki tena kuwa peke yangu.”
Akaongea kwa upole. “Sitaki tena kuwa mpweke. Najua unaweza usiamini sababu
nimekuumiza, lakini kuja kwako umeyabadili maisha yangu. Umenitoa pabaya
nilipokuwa nimekwama, sitaki kurudi huko tena. Kwa hiyo sidhani kama
nitahamia Kigamboni. Sitaki kuwa peke yangu.” Kamila akasikiliza,
akashindwa chakujibu, akainama akifikiria. Wakatulia kidogo, akaona aage.
“Acha nikuache ukafanye kazi.” “Nimefurahia kuja kuniona
Colins. Asante kwa kuja na asante kwa zawadi.” Hivyo alivyoshukuru, akajikuta
anampa kiss nyingine ya shavuni. Akasimama. “Nitawahi kurudi nyumbani.
Nitakuwa nikikusubiria, ukirudi tuwe wote.” Kamila akabaki ameduaa,
mkono shavuni alikoachiwa kiss. Colins akacheka na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akili ikawa ipo kwa Kamila. Kama ambaye ameshachelewa
anakimbizana na muda. Kazi zikawa zinaanza kuwa nzito. Wasiwasi
kwa Kamila. Mill asije badili mawazo akaamua kubaki naye. Watesi wake,
zaidi Love ni kama anakaribia kuwafikisha ukingoni, wapo magotini. Ya
Jelini nayo ni kama yanakaribia ukingoni
pia, ila si mwisho kabisa. Hataki kuishia njiani kabla hajaona mwisho wake.
Na hataki kuwa na Kamila huku anahangaika na Jelini
pamoja na kuhitimisha ramsi na Love. “Utakuwa usaliti kwa Kamila. Hata mimi
nisingependa awe na mimi huku akimuhangaikia mwanamme mwingine.” Akazidi kujichanganya
mawazoni, akili ikizunguka. Kengele za kuchelewa zikizidi kulia. Na maneno ya
mama yake yakizidi kumsumbua akilini. “Nisije kosa kweli bara na pwani!”
Akazidi kuwaza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kipi anaachia kipi anashikilia?!
INAENDELEA.
![]() |
0 Comments:
Post a Comment