Kwenye majira ya saa moja na nusu wakaanza kusikia magari
yanaingia ndani. Colins akatoka kwenda kuwapokea akiwa na wazazi wake. Alipoona
aina ya hayo magari hapo nje, Colins mwenyewe akanywea. Kamila akashuka kwenye
gari ya nguvu na kumuacha akijiuliza sasa hiyo gari aliyoagiza ndio itakuaje!
Mill mwenyewe na Jerry ni neema tupu. “Sasa
huyu jamaa kama hapa ndio kaishiwa, akiwa nazo ndio inakuaje?” Akajiuliza
Colins wakiwa wanawasogelea. Huyo Mill alijawa heshima kama apige goti, mpaka
akawafanya wenyeji watulie. Maana alijawa mafanikio yanayoimba utajiri
waziwazi.
Baada ya salamu akamvuta Kamila na kumkumbatia mbele yao.
Harufu aliyoipata kutoka kwa Mill ni kama ile perfume aliyomkatalia
Kamila. Safi, kisha tulivu. “Kwa niaba ya ndugu yangu Mike, naomba niwashukuru
wazazi wangu na Colins.” Akaanza Mill akiwa amemkumbatia Kamila.
“Kamila amenieleza kwa kifupi, hakika nyinyi watu Mungu awabariki.”
“Usijali mwanangu Mill. Mjisikie nyumbani kabisa. Karibuni ndani.” Wakakaribia,
akiwa bado amemshika Kamila kama mtoto.
Wakakaa kochi moja, na kumvuta karibu. Akapandisha miguu
juu ya kochi, akajikunja vizuri, kisha akarudia kumkumbatia tena kwa mkono
mmoja ubavuni kwake. Vinywaji vikaletwa. “Na chakula kipo tayari kabisa.”
“Tunashukuru mama. Asante sanaaa. Tena sanaa.” Kisha akaendelea. “Kabla na sisi
hatujaleta zawadi zetu, acha nijitambulishe kwa kifupi tu. Sisi wanne, na Mike
ni marafiki tokea shule ya sekondari. Tulimuacha Kamila shuleni, sisi tulipohitimu
kidato cha sita.”
“Mimi na Mike ni kama tulibahatika kupita kwenye familia
tu za watu kama hivi mlivyompokea Kamila. Ila si kama hivyo Colins
kulelewa na wazazi wote moja kwa moja. Mwenzetu Jerry yeye alibahatika wazazi
waliomjali na kumlea vizuri. Tumekuwa tukipambana na maisha, tokea wadogo mpaka
sasa. Utajiri wetu mkubwa ni watu, ila Mike alizidi.” “Aisee yule
jamaa! Kila mtu alikuwa akimuuliza ni wakati gani anakua anakasirika!”
Kidogo wakacheka.
“Ndugu zangu, mimi nina uhakika kwa asilimia zote,
hamjawahi kukutana na mtu mwema kama Mike. Yule jamaa sijui Mungu
alimuumbaje jamani!” “Mimi mwenyewe bado sijakutana naye aisee! Unaweza
mkanyaga Mike, akaishia kukufanya wewe ujisikie vizuri. Pale shule ya
sekondari alipogombania ukiranja, wote tukataka awe Kaka Mkuu.”
Wakacheka.
“Unakumbuka Kamila?” “Nakumbuka. Alikuwa anaongea na
mwalimu mkuu kama rafiki yake mpaka nilikuwa namshangaa!” Zikapambwa
sifa za Mike hapo.
“Na akili ya kufikiria pia hapo nilimnyanyulia
kofia. Biashara niliyokuwa nimeanzisha kule nilikokuwa, sijui kama Kamila
alijua hili! Nilikwama parefu, mpaka nikataka kushindwa kufanya. Na kule
kwa wakati ule nilikuwa sikopesheki. Alinipa ile pesa kama ilivyo,
hakutaka hata niandikishane naye! Ila kila nilipotaka kumlipa, aliniambia hivi,
tena kwa kusisitiza!” Akafikiria kidogo kama anayejaribu kukumbuka.
“Yaani yule mtu ni kama alijua kesho yake na Kamila!
Mpaka siku ya mwisho naachana naye, mimi naingia jela nikiwa nina pesa, sina
uhakika kama nikitoka nitakua nayo au hata kama nitakuja kutoka!” Wakamuona yeye na Kamila machozi yanazidi kutoka. Yeye
akajifuta, Kamila akajificha hapo upande wa ubavu akiendelea kulia.
“Kila nilipokuwa nikimsisitiza achukue pesa yake
alikuwa akisema, ‘Usiwe na wasiwasi, utakuja kujua tu siku nitakapo hitaji
unilipe.’ Yaani hivyo tu.” Akajifuta machozi.
“Poleni sana. Poleni.” “Aisee baba! Sisi tumefiwa jamani! Tunamsiba ambao sijui
kama utakuja kuisha!” “Mungu atawafanyia wepesi.” “Mtuombee
mama. Pengo la Mike hata mimi siwezi kuziba. Muulize Jerry.” “Halizibiki aisee! Mimi ndio naona alinibeba!
Mwingine angeishiwa mbeleko.” Wakacheka wakilia.
“Ila sitatulia,
mpaka nijue kwa hakika ni nini kilimdhuru Mike.” Kamila akajitoa kabisa na kumwangalia. “Kabisa Kamila.
Mike hastahili kutendwa ubaya na yeyote kwa sababu hajawahi mtenda mtu ubaya.
Hata kama itanigarimu pesa yote, nitamsaka aliyemtenda ubaya, na nitahakikisha analipa
bila kukosa.” “Asante Mill. Nilikuwa nikumia, sijui chakufanya.” “Tutampata tu aliyetuondolea Mike hapa duani.
Wala usijali. Nafungua kesi upya kabisa. Naanza upelelezi kana
kwamba ndio imetokea jana. Mbona nitampata tu!” Wakatulia kama wakiwaza.
“Poleni sana. Na naona taarifa zake zimetunzwa vizuri
sana pale hospitalini. Mkihitaji nitawapa.” Colins naye akaongeza. “Tunashukuru
kaka. Huo utakuwa msaada mkubwa sana nitakao hitaji kwa haraka. Najua sasahivi
ni wakati wakulipa madeni yake yote. Ikiwemo na Kamila. Mike alimpenda
sana Kamila. Sana, kupita nitakavyoweza eleza, mkaelewa!” “Sana,
kama mwehu!” Wote wakacheka, Kamila akajificha akicheka japo alikuwa akilia
taratibu hapo ubavuni kwa Mill huku akimbembeleza.
“Wewe ushawahi muona Kaka Mkuu anafagia uwanja wa
mwanamke!” Jerry akawafanya wazidi kucheka. “Au kumwagilia maua, halafu kama
Kamila hasubirii pembeni, basi anamwambia akaoge, ajiandae na mstarini, yeye
anafanya kazi zake.” Mill akaongeza, wakazidi kucheka.
“Yaani vikao vingine mnamfuata Kaka Mkuu akiwa anafagia
uwanja!” “Haiwezekani!” “Muulizeni Kamila huyo. Mpaka ikabidi Kamila apewe light
duty ili Kiranja Mkuu apunguziwe majukumu, aweze kuongoza mambo.”
Wakazidi kucheka. Stori zao hao wawili zikaendelea, Kamila akicheka kwa aibu.
Mwishoe Mill akaendelea. “Najua Kamila amepewa kazi
kwenye hospitali yenu. Nakushukuru sana Colins. Asante.” Akashukuru mpaka
akampa mkono. “Sijui Kamila amekwambia nini! Ila kazi yenyewe ni upishi
tu! Anapika chakula cha wagonjwa!” “Hata Mike angekua hapa, angekwambia hili.
Sisi watatu, hatukujaliwa maisha ya kuchagua. Kwetu sisi tulishaambiana,
kazi ni kazi. Unafikiri ni kwa nini nilifanikiwa kwenye ile biashara?” Wote
wakabaki wakimwangalia.
“Nilianza kama mwajiriwa. Natumika kwenye Homes za
watu kulea wagonjwa na wazee. Nawaogesha na kuwasafisha kabisa. Ndio Mike
akaniambia kile ninacho kifanya naweza kukikuza. Mwanzoni nilisita. Nikiwa
sina uhakika kama nitaweza. Akaanza kutembea na mimi hatua kwa hatua. Tukahangaika
mpaka na mimi nikafungua ya kwangu.”
“Anachokifanya
Kamila sasahivi, mbali ya kwamba ni kitu anachokipenda sana. Maana
Kamila anajua kupika bwana! Akikupikia huyu hata maharage tu, mtagombania
sufuria. Alikuwa akija kwangu kule ugaibuni, hakuna kula hoteli labda
tusafiri wote kwa mapumziko.”
“Basi itabidi na hapa tumuachie jiko.” “Kama mpaka
sasahivi hujamuachia jiko mama, umejipunja.” Wote wakacheka. “Lakini
mbali ya kuwa umempa kitu anachokipenda, pia amekuwa akifanya kitu kikubwa
zaidi yake. Umemtoa kwenye kujifikiria mwenyewe, angalau akasaidia
wenye shida, kitu ambacho hata Mike angekushukuru. Asingetoka
alipokuwepo bila kupata kitu kizito cha kumfanya afikirie. Ile kuingia
asubuhi mpaka jioni, anasaidia kuwafanya wagonjwa wale vizuri, mbali na pesa,
kwake imekua therapy ya buree. Asante sana Colins.” Angalau akajisikia
vizuri.
“Asanteni wazazi wangu kwa kumpokea Kamila, mtu wa
muhimu sana kwangu na Mike. Asanteni sana.” “Karibu sana Mill na Jerry.
Mjisikie nyumbani.” “Sasa hilo ni kosa mama yangu. Muulize Kamila. Sisi
hatuambiwi hivyo! Kesho utashangaa nakuletea wajukuu.” Wote wakacheka.
“Hao ndio tunawataka. Walete kabisa waje washinde hapa. Wajue
wapo bibi na babu.” “Kumbe ndio maana Kamila amegoma kuondoka!” Mill
akawashangaza kidogo, ila yeye akamchungulia pale alipokuwa amemuegemea.
“Kweli nyinyi ni watu wazuri. Na namuelewa Kamila.
Nilidhani anaishi na watu wabaya. Nikamwambia shemeji yangu huyu, nyumba ipo, aje
tujibane wote. Akaniambia yeye amepata familia ya baba na mama wanao mpenda.
Mmempokea na mnamjali. Anaomba abakie hapa.” “Kabisa. Na si kwake
tu, hata wewe, Mill mwanangu. Pafanye kabisa hapa ni nyumbani. Leta
wajukuu. Watambulishe hapa. Msikae peke yenu.” Akasimama na kuwapa mkono
wote akishukuru.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ila katika yote, Colins akasikia akimtambua Kamila kama shemeji.
Angalau mapigo ya moyo yakaanza kwenda kwa utaratibu wake. Amani ikaanza kurudi
na tumaini pia.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kama ndio hivyo basi sisi tukaribie mezani.” Wakacheka
na kusimama kuhamia mezani. Mama Colins alishaishi nchi za wenye nazo, anajua
kujiandaa kwelikweli, meza ilikaa vizuri. Napo hapo wakashukuru
vyakutosha. Kabla hajaanza kula, simu ya Jerry ikaanza kuita bila kukoma.
“Wewe nenda Jerry. Mimi nakushukuru sana hata kuzunguka
na mimi leo. Tujipange tena.” Wakamsikia Mill akimwambia. “Nashukuru kunielewa
Mill. Na samahani.” “Bila shaka. Mwambie Sadra nitakuja kumuona.” “Bora
hivyo, pengine atatulia.” Wakacheka, Mill na Kamila wakasimama kumsindikiza
wengine wasielewe ila Colins akawa kama ameelewa kutokana na alivyosimuliwa na
Kamila juu ya wivu wa kupitiliza wa mkewe Jerry.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakarudi na kuendelea kula. Wakati wanakula mama Colins
akaanza. “Nimesikia wajukuu, mke ulimuacha hukohuko Marekani?” Colins
akamwangalia mama yake kwa kushituka. “Mama!” “Hakuna shida. Si ndio
nimekaribishwa kwenye familia? Hayo ndio maswali ya msingi ili kufahamiana.”
“Bora umwambie.” Wakacheka.
“Huyo mkwe wa huko ndiye aliyenichelewesha mama yangu. Ameniadhibu
adhabu ninayostahili kabisa.” Akawasimulia mwanzo mpaka mwisho wao.
“Pole sana Mill! Sasa hapo unastahili vipi?” Ikabidi mzee aulize.
“Hivi unavyomuona au kumsikia Kamila na Mike, na
mimi nilipata msichana baba yangu. Japo sisi hatukuanza kama wao wakiwa
wadogo sana. Ila ni msichana wa hapahapa nyumbani. Mtulivu kama hivi
Kamila. Hana makuu! Alijitunza mpaka nilipomchumbia mimi. Kwa
hakika nilijua ndio wa mpaka kifo. Mimi na Mike na kina Jerry tulilipa mahari
kabisa, kipindi bado nipo huko.” Akaendelea.
“Baba alipofariki, wakati huo sikuwa bado raia wa huko,
maisha yakazidi kusumbua, nikashindwa kufanya mengi, ikanibidi nioe mwanamke wa
kule ili kupata uraia kabisa, kusaidia urahisi wa maisha. Hapo nikafanikiwa,
huku nyumbani mchumba ananisubiri, hajui kama nimeoa kule. Ila
nia ilikuwa nimdanganye wa kule, nikiweka sawa mambo yangu, nimuache,
nirudi huku nyumbani nije kumuoa Pam wangu.” Wakamuona anatingisha kichwa
kabisa kwa masikitiko.
“Mungu akaiona hila yangu, bwana. Akanibananisha,
kutoka ikaanza kuwa ngumu. Ni kama naye yule alijua nilikuwa nikimtumia akaniwahi
bila ya mimi nikiwa najua. Kila nililokuwa nikipanga juu yangu na yeye, ili kuhitimisha
ikawa anakuwa hatua moja mbele yangu, sifanikiwi. Mafanikio niliyokuwa
nimeyapata akakusudia asijitoe kwa haraka. Akakusudia mali yangu iwe yake.”
“Akanitafuta kwenye mengi, akanikosa. Sijakaa sawa baraka
za uraia wa Marekani na mafanikio ya biashara, vikaanza kuleta na watoto,
aliokuwa kinidanganya anatumia uzazi wa mpango, kumbe
muongo. Maana mimi nilikusudia kabisa nisizae nae hata mtoto mmoja. Ila akawa
ananitega ashike mimba, mimi sina taarifa. Nia ni kunibana akijua
wazi itakua ngumu kumuacha akiwa na watoto wangu tayari. Na hakukosea. Nikashindwa
kumuachia watoto wangu ambao wazi yeye mwenyewe hakuwa tayari nao, au hakuwa akiwataka.
Ila akawageuza ikawa ndio nguzo yake tu kujipatia pesa yangu.”
“Matatizo ya
ndoa yakaendelea mpaka ndio akanifunga jela kwa shutuma mbaya. Hivi isingekuwa
akili ya Mike, bado ningebakia jela mpaka kifo. Nilipotoka na kupata watoto
wangu, sikutaka kurudi nyuma. Nikaamua kurudi hapa nchini na wanangu.” “Pole
sana.” “Ndio nilikuwa nikizungumza na Kamila na Jerry, juu ya Pam.” Hapo Colins
akajiweka sawa.
“Jerry ameniambia Pam yupo na mpaka mara ya mwisho
amekutana naye bado hakuwa ameolewa. Na kama kawaida ya Kamila, shemeji
yangu, amenishawishi kurudi kuomba msamaha.” “Hawa walikuwa wanapendana
sana. Hata Mike alikuwa akisema Mill hatakuja pata mwanamke kama Pam. Ni mzuri,
halafu mtulivu sana.” Hapo moyo wa Colins akapoa kabisa. Alijua Mill
amekuja kupindua majeshi kumbe anamuheshimu kama shemeji tu! Hapo
akaanza kuchangamka na kuanza kutoa na ushauri.
“Kuna nafasi za pili za upendeleo huwa Mungu
anatoa. Usipokuwa mwangalifu, ukazubaa, ukiendelea kushikilia ya nyuma, unaweza kupoteza hizo bahati na unaweza isije
rudia tena, ukaishia pabaya. Mimi
nipo kama Kamila. Kama kweli mlipendana,
atakuelewa na kukupokea tu. Japo inaweza isiwe rahisi.” “Na watoto wawili?!”
“Na wewe mwenyewe ukiwemo.” Colins akamjibu kwa uhakika.
“Kuna package huwa Mungu anatoa kama zawadi kwa mtu, huwezi kutenganisha.
Ukitenganisha tu, unaharibu ladha nzima. Mimi najua ninachozungumzia, nilipita
hapo unapohofia kumpitisha Pam. Wala kwangu sikuona ni tatizo ila double
blessing.” Colins akaendelea.
“Unajuaje kama Pam ana uwezo wa kuzaa?” Akamuuliza Mill.
“Lakini kweli!” “Unaweza kuta ukawa umemletea faraja ya maisha. Mapenzi
ya kweli na watoto.” “Kumbe bora
nimezungumza! Aisee asanteni sana. Nafikiri nitamtafuta.”
“Sasa sio unakwenda kujaribu
mara moja! Ukang’ang’anie mpaka usamehewe, kwa sababu ulichofanya
ni usaliti, na Mike nilimwambia. Haitakuwa rahisi, maana ukumbuke ni
kama na Mike naye alikuwa akimkwepa sababu hakutaka awe katikati
yenu. Alikuwa anasema hatakuwa na majibu mazuri ya kumpa Pam. Na hakuwa
tayari yeye ndio amuumize Pam kwa ukweli halisi ulivyo juu ya
hatima yenu, na hakuwa tayari kumdanganya. Mike alikuwa akisema Pam ni
msichana mwema, hakustahili ulikompitisha.” Wakamuona Mill ametulia mawazo
mbali.
“Kama alivyokwambia Colins, haitakuwa rahisi,
lakini kama kweli hutaki kurudia kosa kwenye ndoa, ukifanikiwa kumpata Pam, utasahau
yote. Na najua unajua hata Mike angekuwepo, angekwambia hivihivi.” Mill akabaki
ameinama akifikiria.
“Daah! Halafu katika hangaika yote hiyo, hata pesa
yenyewe niliyohangaikia mpaka kumtoa Pam wangu kafara, ilikuwa sio tamu!
Chungu kuliko shubiri! Ikakosa ladha na maana nzima! Fujo, amani hamna
na mpo na kila kitu!” Wakamsikia akiwaza kwa sauti.
“Kwanza kabla sijamtaka anirudie, nafikiri ninawajibika
kumtafuta, nimueleze ukweli na kumuomba msamaha. Nimemdhalilisha vibaya
sana kwenye jamii. Nilimchumbia hadharani, nikitangaza nitamuoa niondoke naye
nchini, kisha nikaja kupotea kabisa na kukata mawasiliano yote! Hakika
nilimtenda vibaya yule msichana.” Akasikika kujutia.
“Nafikiri hilo ndilo la msingi Mill. Ulifanya kosa
kubwa sana. Lakini kukiri kosa, kunaweza kusaidia kumfanya hata
kukusikiliza.” Mzee akaongeza.
“Nafikiri upo sahihi mzee wangu. Nianzie hapo. Na
sitakata tamaa. Yeye alinisubiri, na mimi nitamsubiri mpaka aje arudi kujenga
tena imani na mimi. Sitaki kuanza na mtu mgeni. Umri umeshakwenda.” Wakacheka
kidogo. {Simulizi ya Mill&Pam itaendelea kwenye, Love at first sight.}
“Bado unadai kabisa Mill.” “Utaacha kunisifia basi! Hata nikizeeka
utasema mimi kijana.” Wakataniana kidogo, akaendelea akiguna. “Jamani, msiombe
kuishi na mwanamke asiyekupenda, mkorofi, halafu anajua kuongea.
Colins!” Wakaanza kucheka jinsi alivyomuita Colins.
“Kaka, utajuta kuzaliwa. Nahisi nililala vizuri
waliponifunga jela, kuliko nilivyokuwa na yule mwanamke aisee.” “Pole Mill
mwanangu.” “Acha mama! Sasa amemuharibu mtoto wangu yule wa kiume, anajua jinsi
ya kuzungumza ni kuzungumza kwa jeuri au kukataa kila kitu. Yaani
hapa nipo kwenye kumfudisha kuwa kama mtoto wa kawaida.” “Pole sana. Naamini
atabadilika tu. Jipe muda.”
“Nashukuru mama yangu. Na nafikiri pia akizungukwa na
mazingira tulivu kama hivi, pengine itamsaidia. Atajua sio watu wote wapo kama
ile familia yetu.” “Kwani ndio ilikuwa mbaya hivyo!?” “Acha Colins! Acha kaka.
Kamila anajua ninachozungumzia aisee, maana mara nyingi tulikuwa tukizungumza
kupitia Mike.”
“Yaani wewe na mkeo?!” “Kumbe! Yaani tunaishi nyumba
moja, lakini hatuwezi kuzungumza. Mtu wa katikati yetu alikuwa Mike.
Yaani tunampigia simu Mike huku, ili asaidie mawasiliano, jambo
lifanyike kule. Mbishi. Jambo zuri la maendeleo hata kwa watoto, mtavutana
mpaka utashangaa.” “Mike alikuwa anasema, alishajua udhaifu wako ni kwa
watoto ndio alikuwa akiutumia.” “Basi aliniweza aisee!”
“Pole.” “Nashukuru, ila madhara aliyoacha kwangu
na watoto, wala hutayatafuta. Ukikaa na wanangu hata kwa muda mfupi tu, utajua
ni watoto waliotoka kwenye makuzi ya ajabu. Tuyaache hayo.” Akaona
aishie hapo maana walimuona ameshabadilika kabisa.
“Jambo la mwisho wazazi wangu ili niwaache
mkapumzike. Kwa heshima kabisa,
naomba niweke mazingira ya Kamila kuacha
kazi pale.” Wakatulia wakisikiliza japo walitegemea.
“Kama nilivyowaambia, mimi na Mike tumepambana sana
jamani. Sana. Hapo aliporudi Kamila, Mike alishamtoa huko. Lengo
ilikuwa tufungue sehemu, huyu, aiendeshe mwenyewe. Anakipaji
kikubwa sana. Mgahawa atakao uendesha huyu, wenye vyakula vya mataifa
mbalimbali, utakao wasaidia wageni na wazawa ndio ilikuwa ndoto
zangu na Mike.”
“Kumpa sehemu inayofanana na kicho Mungu
alichokiweka ndani yake. Sio kwamba nadharau anachofanya sasa, ila nina deni
kwa Mike, kuendeleza alipoachia. Tafadhalini sana.” “Sidhani kama kuna
tatizo. Ni yeye tu mwenyewe.” Akajibu Colins.
“Nimezungumza na Kamila, ameniambia kwa siku mbili, leo
na kesho jumamosi, kuna upungufu wa wapishi wawili pale kazini. Hawezi kuomba
hata off, lazima asaidie. Na mimi
naungana naye. Hawezi anza jambo akaliacha
katikati. Lazima atatoa notice.
Angalau ya majuma mawili ili kiongozi wake azibe pengo. Ila baada ya hapo,
naomba tuanze kujipanga jinsi ya
kuanzisha cha kwake.”
“Unaonekana una akili sana Mill.” Mzee akasifia. “Mzee
wangu, wala si mimi. Ni Mike. Nimetoka jela nimevurugikiwa kabisa. Hapa natembea na ramani yake yeye Mike. Kila siku nikiamka najiuliza tulipanga nini na Mike! Na nikikutana na jambo linanitatiza
huwa najiuliza, katika hili kama ni Mike angefanyaje! Ndio ninavyoishi kwa
sasa. Hatua moja moja, huku nikiamini nitakuja tulia, niweze kufikiria na
kujipanga tena upya.”
“Ila kwa sasa kulikuwa na ramani tulishaweka na
Mike, ndio naifuata. Na mbali ya
kuwa nitatafuta aliyemtenda ubaya. Hakika nitamtafuta kwa udi na
uvumba. Lakini pia nina mpango wa kumfanyia memorial
service. Kamila ameniambia ameridhika kuwa ni kweli amefariki.
Hakuna aliyemzika kati yetu. Nataka kukusanya watu wetu waliotufahamu mimi na
Mike. Tufanye tafrija ya kukumbuka maisha yake, ndipo nikajengee sasa kaburi lake.” Kamila akaanza kulia kwa uchungu sana.
“Mill,
namkumbuka Mike. Namkumbuka sana. Mungu amenipokonya Mike jamani! Hakika mimi
nimefiwa!” Wawili hao wakaanza kulia tena, hapohapo,
taratibu mpaka huruma. Kuona mwanaume analia kama hivyo Mill! Ikawa simanzi ya
namna yake. Wakawatuliza, Mill akaondoka kuwahi watoto kwa ahadi ya kuwaleta
hapo siku ya jumapili, Kamila akiwa off.
Ukweli Mchungu.
Wakiwa wanasaidiana kutoa vyombo na kusafisha ili
kurudishia hivyo vyombo vizuri sehemu yake, mama Colins akaanza, walikuwa peke
yao hapo jikoni. Colins aliingia chumbani kwake kuoga, mzee naye hivyohivyo,
msichana wa kazi alishakula, akajiwahi chumbani kwake mapema sana wala hakutaka
kukaa nao hapo mezani na wageni.
Akaanza taratibu. “Colins ameniambia hutahama naye.” “Nimeona nimueche awe huru, mama yangu. Nafikiri hofu ilinifanya nisimuelewe. Lakini tokea tumekutana, Colins amekua akisisitiza mambo kadhaa. Mpaka jana nilipotoka hapa kumpelekea ile snack na
juisi amerudia tena.” “Nini?!”
“Ameniambia hana nafasi ya mtu yeyote nafsini
kwake isipokuwa Jelini.” Mama Colins alishituka, hakutegemea. “Amerudia hilo kwa kurudia rudia. Na kusema mimi
ni mzuri, ila nafaa kwa mwanaume yeyote yule
lakini si yeye.” “Haiwezekani Kamila!” “Mwanao ni muwazi mama! Muwazi
sana. Ni uchague tu kutokukubaliana naye. Na amesema nisikate tamaa, Mungu atanipa
nafasi ya pili, na mtu mwingine, ila si yeye maana yeye
alishapewa ya pili kwa Jelini.” Mama Colins nusura aangushe bakuli.
“Kama ungekuwa ukizungumza naye, angethibitisha haya.
Sijaongeza mama yangu labda niwe nimepunguza. Maana ameniambia kifasaha
wala si kwa kukosea! Yaani nimepata
nafasi ya kutafakari mazungumzo yetu, mpaka nimejichukia mama yangu.
Sijui nilipatwa nini! Sijui nimekua mjinga vipi kung’ang’ania kitu
ambacho si changu na wala hakitakuja kuwa changu na hapakuwa na usiri.
Colins amekua muwazi kwangu kabisa.
Sasa ni kwa nini nihame naye wakati ameshanifikisha hapa?” Kimya.
“Mimi mwenzio nakupenda mama. Wewe mpole, mtulivu na unaupendo.
Hapa kwako ni kama mazingira tuliyokuwa tukiishi na Mike. Vile
ulivyosikia wakimsema Mike, ndio yupo hivyo mpaka chumbani tukiwa wawili. Sauti
ya juu utakayoweza isikia kwetu na Mike, kama si vicheko basi tv maana
nahisi yule alikuwa na uziwi.” Kidogo
wakacheka.
“Muulize Mill. Hawezi sikiliza radio wala tv kwa sauti ya
chini. Ila si kugomba, wala si kelele. Mtulivu kama hivyo wewe.
Hana ubaya na mtu yeyote. Mpaka watu waliokuwa wakitufanyia kazi pale
nyumbani walikuwa wakimpenda.
Anaweza amua kwenda nje kuzungumza nao tu, kama rafiki na pengine kusaidiana
nao kazi. Anachokula ndani, kama kuna mtu amekuja kufanya kazi, hata kama
nikibarua wa masaa machache, ilimradi huo mlo umemkuta pale kwetu, yaani
anapakua yeye mwenyewe na kumpelekea huyo mtu alipo. Alikuwa mtu wa hivyo.
Akanilemaza kwa upendo, amani, utulivu pamoja na furaha muda wote. Basi ndio
ilivyokuwa nyumbani kwetu, kama hapa kwako.” Akajua na gomba ya mwanae
imemuogopesha.
“Halafu hapa nina
uhakika sitafukuzwa. Msichana wako ameniambia Connie, huyo mwanao
daktari yupo kama wewe.” Wakacheka. “Amesema ongea yake yenyewe ni shida!
Ndio maana na yeye amekaa sana hapa. Hamna tatizo na mtu. Sasa kwa nini
niondoke hapa? Colins akija kuoa huko? Naanza upya? Hapana mama. Acha nipumzike.
Hata Mill nimemkatalia. Nimemwambia hapa nimefika. Siondoki labda na mimi nije pata mwanaume wakueleweka.”
Mama Colins akashindwa chakujibu, akabaki akipangusa vyombo akirudisha
kabatini.
Kamila akaaga baada ya kumaliza, akarudi chumbani kwake
ili ajipumzishe. Mama Colins akabaki ameduaa jikoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment