Baada ya muda akaja Kamila liyependeza kama wa asubuhi.
Ametulia kweli. “Karibu.” Akaenda kukaa mbele yake. “Asubuhi ilibidi kumtafuta
Jerry. Mmoja wa rafiki wa Mike. Na yeye mfanyabiashara. Anaagiza vitu nje ya nchi,
na anakampuni ya kuingiza na kutoa vitu bandarini. Kwa ufupi anafahamiana na
watu wengi. Na ni kaka mzuri tu, huwa wakati wote anautayari wakutusaidia mimi na Mike.”
“Nikamueleza uhitaji wangu wa gari, tukiwa tumepotezana
tokea kuondoka kwa Mike. Ndipo akaniambia na Mill amerudi nchini. Kama ni sawa
nimpe mawasiliano yangu.” “Mill ni nani?” “Walikuwa marafiki watatu tokea form
five wamekuja pale shuleni. Walikuwa wakisoma pamoja na walikuwa karibu
sana wakati huo mimi nipo na Mike. Walipomaliza tu baba yake Mill, akiwa mtoto
wa nje ya ndoa, akampeleka nje kusoma. Lakini kabla hajamaliza chuo huko mzee
wake akafariki. Ada ikasumbua, ikabidi kuoa
mwanamke wa huko, ili kumsaidia kumpa uraia.”
“Akamaliza chuo Mungu akasaidia maisha yake huko yakawa safi sana. Ndiye tuliyekuwa tukienda
kwake kipindi cha mapumziko yetu na Mike. Urafiki kati yao ikawa kama undugu
ila Jerry yeye mambo yalibadilika alipompata huyu mwanamke.”
“Aisee mwanamke anawivu huyo, na anajua kumbana Jerry hujawahi
ona. Hicho ndio kitu kilichoanza kututenga naye. Ikawa ni ngumu tena kukutana
naye. Safari za pamoja zikafa kabisa, huyo mwanamke hataki. Hata alipoondoka
Mike, ikawa ngumu kwa Jerry kuwa karibu na mimi sababu ya huyo mwanamke.
Alikuwa akifanya fujo anahisi Jerry atanichukua, ndio tukaona bora
kuleta amani, tuache hata kuwasiliana maana alikuwa akifuatilia kila mawasiliano
yetu. Tukapotezana na Jerry mpaka leo asubuhi.” Kamila akaendelea Colins
akimsikiliza kwa makini.
“Sasa huku kwa Mill, mwanamke alikuja kumgeuka vibaya
sana. Akaanzisha mahusiano na mwanaume mwingine. Mill alipojua akataka kumuacha
abaki na watoto. Alipoona ataachika bila kugawana mali, sababu
kweli kosa ni lake, alijua kwa vyovyote vile, Mill akipeleka ushahidi wa usaliti
wake mahakamani, ataachika bila pesa ya Mill, ambayo ni ngingi. Maana ni kweli
Mill alifanikiwa sana huko.”
“Akaanza kudanganya kuwa Mill anampiga. Siku moja
akajikata kisha akapiga simu 911 kuwa Mill, amempiga mpaka kumuumiza.”
“Haiwezekani! Na kama ni Marekani hilo ni kosa la jinahi. Mbaya sana.”
“Hukohuko. Aisee ilikuwa mbaya! Mbaya sana. Walimfunga bila kufikiria mara
mbili.”
“Mike alihangaika kumtoa jela huku akitumia pesa nyingi
kweli kumlipa mwanasheria kumtoa jela, lakini wapi! Yaani mpaka Mike ameondoka
akawa hajafanikiwa kumtoa, maana mwanamke alikuwa anatoa ushahidi wa
uongo ili tu Mill abakie jela, yeye achukue mali zote.”
“Tulirudi tena huko, Mike alienda mpaka kwake kuzungumza
na yule mama ili tu afute kesi, Mill atoke. Akakataa akijua Mill akitoka
atarudi pale nyumbani kwao na yeye alishamuhamishia mwanamme wake pale,
sisi hatujui. Siku za mwisho za Mike ndio akaja kusikia fununu kuwa anaishi na
huyo mwanaume wake pale, hataki Mill atoke jela. Na mbaya zaidi ni kama watoto wanateseka,
yule mwanaume hataki wale watoto wa Mike.”
“Ndio tukarudi tena kule, Mike akaenda kuzungumza na Mill
kuwa akubali kupoteza kila kitu, amuachie kwa maandishi yeye atoke jela, aje
aanze huku upya. Ikawa ngumu kwa Mill kukubali, zaidi watoto. Mama hataki
na watoto akijua Mill akichukua watoto, itabidi achukue mali, ila hakuwa
muwazi, akabaki anasema hataki na watoto.” “Wana watoto wangapi?” “Wawili.
Wakike na wakiume. Bwana watoto wazuri hao! Halafu wote wamefanana na Mill.”
Inamaana Mill ni mzuri. Wivu tayari.
“Anayemsimamia kesi Mill na Mike wakaanza kubembeleza
pande zote ilimradi kufikia muafaka. Mill yupo jela, mkewe huku anatapanya na huyo
mwanaume. Hatunzi watoto.” “Kwani Mill alikuwa akifanya nini huko?” “Alifungua
biashara ya nusing home and care. Bwana Mill alifanikiwa kwa hali
ya juu sana. Sana.”
“Ulikuwa ukifika kwake hutosheki kwa macho. Halafu
alijenga nyumba ramani alichukua kama ya Mike. Wakawa na nyumba zinazofanana,
ila yeye akabahatika uwanja mkubwa sana, mbele na nyuma. Akatafuta architectural
wa hukohuko. Aisee aliipangilia ile nyumba ndani na nje kwa uthamani mkubwa
sana. Sana. Halafu akabahatika thamani za ukweli sio huku unanunua kitu
leo, kesho kimeharibika. Kwa ufupi Mill alifanikiwa.”
“Basi. Kwa kuwa aliyekuwa na akili ya biashara alikuwa
Mill, mkewe matumizi makubwa, haingizi, akaanza kuishiwa. Biashara
ikaanza kumuwia ngumu. Mike aliposikia kutoka kwa yule wakili kuwa ameanza
kuuza magari ya Mill, ndio akapata akili ya kurudi tena kwa Mill. Akazungumza
naye sana. Akubali kupoteza kila amwambie yule mama amuachie watoto. Sasa
safari ya mwisho kabisa tuliyoenda na Mike, sijui alizungumza naye nini. Mimi
nilikuwa siendi huko jela. Mike alikuwa ananiacha hotelini, ila Mike alisema
Mill alikubali kumsainishia kila kitu kuwa ni chake. Ampe mali zote na
yeye ampe watoto kisheria.”
“Tuliondoka kule yule mwanasheria wa Mill alikuwa ndio
yupo kwenye mchakato, Mike akisimamia. Ndio tumerudi huku hata hatukukaa sana,
ndio Mike akaondoka. Sikujua kinachoendelea tena, kwa sababu kwanza
nilipotezana na Jerry, pili nahisi nilikuwa nimechanganyikiwa, sikujua tena
jinsi ya kumfikia yule wakili Mike alimtafutia Mill, na Mill mwenyewe ambaye
ndiye aliyekuwa kama Mike wa pili, hakuwa ametoka jela.”
“Sasa leo asubuhi wakati nimemtafuta Jerry, akaniambia
Mill amefanikiwa kurudi nchini, majuzi tu, na watoto wake. Ananitafuta karibu
kuchanganyikiwa. Luca amemwambia hajui jinsi ya kunipata. Kwa hiyo ile kumtafuta
asubuhi ndio ikawa msaada kwake.”
“Anavyojitetea kwa Mill eti sio kwamba alinitelekeza
ila eti mwanamke wake alifuta namba zangu zote na kuni block ili
nisiwasiliane naye. Ni mambo mengi juu ya Jerry na mwanamke wake. Mill na Mike
walishawaelewa hao wawili, lakini ni kama Jerry mwenyewe anamuendekeza yule
mwanamke sababu ya pesa.”
“Jerry hakutoka kwenye maisha kama ya Mill na Mike. Wao
kwao walikuwa mambo safi sana. Hajui shida na kujituma.
Alishazoea pesa nyingi tokea mtoto. Sasa ashakuwa mtu mzima, maisha ya vingi
bado anapenda, na hawezi tena kupokea kutoka kwa wazazi, ndio mkewe
anamfanya aishi kitajiri. Hawezi kumkorofisha japo anampelekesha kupita
kiasi, wakati mwingine mpaka kero kuwa nao.”
“Ila kufupisha habari, nimefurahi sana kichwa cha pili
cha Mike, kimerudi. Tumezungumza naye mida fulani hivi!” Akamuona anacheka kwa
unyonge ila tumaini. “Amenitia sana moyo. Sana. Naona amenirudisha
kwenye mstari wenyewe, na ameahidi hata kama tumeishiwa, maana anasema
amerudi hana kitu kabisa, lakini ameahidi tutarudi kusimama kwenye ramani
yetu ya kwanza, tuliyokuwa tumeweka na Mike.”
“Alitaka aje mchana, ila nimemwambia nina kazi nyingi,
nisingeweza toka. Swali, unafikiri ni sawa akija nyumbani? Anatamani kuona
ninapoishi na kushukuru wazazi kunipokea. Au itakuwa jioni, leo
nikakutane naye sehemu nyingine, nimkaribishe nyumbani wakati mwingine?” Kabla
hajajibu akaongeza.
“Na baada ya muda mfupi.” Akaangalia saa. “Tumekubaliana
tukutane mahali na Jerry.” “Sioni kama kuna tatizo. Utahitaji usafiri?”
“Alishamtuma dereva aniletee gari. Hapa ninalo gari kabisa.” Colins akabaki
ameshangaa.
“Nilikwambia ile asubuhi. Alisema nitumie gari yake
wakati tunaagiza gari kama ile aliyonipa Mike. Mida ya mchana ndio ikaletwa.”
“Nilifikiri umesema ameishiwa kabisa.” Kamila akacheka. “Wewe ishiwa ya
Mike na Mill hutaiweza. Mill akikwambia ameishiwa kabisa, usidhani ndio
hana pesa. Walijijenga sana na Mike. Sana.”
“Hapa nyumbani kwenyewe alijenga nyumba nzuri sana,
na Mike alihakikisha anamkumbusha kuwekeza huku pia. Anayo pesa huku na miradi,
japo si kama kule. Ndio maana Mike alikuwa akimwambia aachie
kule, arudi nyumbani na watoto.” Akafikiria kidogo na kuangalia saa.
~~~~~~~~~~~~~~
Kamila wa safari hii hata usoni alibadilika. Sura ya
tumaini ilirudi kama ile ya mtandaoni kabisa. Jasiri, mzuri na utulivu
sio paniki na mbembelezaji. Colins akajua ameshakosa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Mimi naona niwaandae wazazi kwanza ndipo waje
wakutane na Mill, isiwe kama nawavamia tu na watu baki. Leo acha kwanza
tukutane sisi tu. Na sitachelewa kurudi nyumbani, ili nisiwavuruge
wazazi.” “Sidhani kama wanashida. Nafikiri watafurahi kukutana na watu wa
upande wa Mike pia. Familia itaongezeka.” Akafikiria kidogo kama akasita.
“Mmmh! Sioni kama ni sawa. Ila acha nikazungumze na Mill,
nione atashaurije na yeye. Isiwe tunavamia tu bila taarifa.” Akafikiria kidogo.
Kisha akaongeza. “Acha nikuache nisikupotezee muda zaidi.” “Uwe na wakati
mzuri.” Akasimama.
Kabla hajaondoka akaongeza. “Nakushukuru sana Colins.
Sana. Asante kwa kunisaidia. Najua umenivumilia kwa mengi. Nimekugarimu muda
ambao kama ulivyosema, huna nafasi ya mtu mwingine isipokuwa
Jelini.” Colins alishituka sana moyoni. Hakutegemea angeileta kwa namna hiyo na
mazingira hayo.
“Lakini ulijitoa kwangu. Nilikuwa kwenye kipindi
kigumu, nilihitaji mtu wa namna yako wakunivusha pale.” “Mtu wa namna yangu!
Unamaanisha nini?” “Umenifanya nijifikirie na kujirudi kwa haraka sana. Mill na
Mike wananidekeza kwa kunipa kila ninachotaka. Wewe umenisukumia
kwenye kujitegemea, maisha ambayo sijawahi ishi, na najua ningekuwa na
Mill, asingeweza kunifikisha hapa kwa haraka hivi.”
“Jana, nikiwa najua nimempoteza Mike na Mill, sina mtu.”
“Mimi nilikuwepo Kamila!” “Najua upo, lakini hukuacha
kunisisitiza moyo wako ulipo, na mimi nastahili mtu mwingine si wewe.”
Colins akabaki amepigwa butwaa.
“Nafikiri nilishindwa au nafikiri hofu ilikataa kukuelewa
tokea mwanzo. Lakini kwangu hukuwa mnafiki Colins. Uliniwekea mazingira ya wazi
na ukawa kwangu mkweli kabisa. Jana kwa mara ya kwanza ndio ukweli ukawa umeniingia
kwa wazi kabisa.”
“Ikanifanya nikumbuke nilikotoka na ninakotakiwa
kusimama.” Akarudi kukaa. “Mimi, Mike na Mill ni kama yatima fulani hivi.
Tulishajiambia sisi na yeyote atakayeongezeka kwetu tutamfanya ndugu.
Chuki, hasira na kuzira ni mwiko kwetu kama tukitaka watoto wetu waje
kuwa na familia. Tukaishi kwa kukumbatiana sana, na kumbeba kila
aliyetosogelea. Ndio maana japokuwa Jerry anatofauti zake, bado Mike na Mill
waliendelea kuwa naye.”
“Nakushukuru kwa kuwa japokuwa leo Mill amerudi, lakini
angalau umenifanya nisimame sehemu fulani. Angalau Mill amenikuta nimesimama
nikiwa nimejiwekea mikakati tayari. Najua angenikuta kama wewe ulivyonikuta,
ningemchanganya zaidi. Nimezungumza naye kwenye simu, ile tu kunisikia,
ameniambia amefurahi. Alijua ningekuwa nimejawa hofu, nimechanganyikiwa. Lakini
wewe umeiweka hiyo hali. Isingekuwa hivyo, ningetoka kwenye kumtegemea
Mike, na kuhamia kwako. Nikawa mzigo zaidi.”
“Nisingejali Kamila! Ila sikutaka kukuingiza kwenye
kipindi hiki ninachopita.” “Mimi nilikuwa tayari kukusubiri Colins. Na
nilikwambia kwa wazi kabisa, ila hukuacha kwa kurudia kuniambia huna
nafasi yangu isipokuwa Jelini. Nikakung’ang’ania japo hukuchoka
kujirudia kwangu kwa kila namna, mpaka jana ndio kama nimefunguliwa macho.
Nimeumia Colins! Nimeumia sana na kujilaumu kutaka kujiingiza katikati yako na
mipango yako na Jelini huku wewe ukiniweka wazi unampenda Jelini na hutakaa
ukampenda mtu mwingine.”
“Nimejilaumu kwa sababu mimi si mjinga. Najua, nakuelewa
maana ya mapenzi na mahusiano. Nimejidharau kukung’ang’ania, kwa kujidhalilisha
kwa kaisi hicho.” “Tafadhali usiseme hivyo Kamila. Umenielewa vibaya na hivyo
sivyo nilivyotaka unielewe.” “Hapana Colins. Ulichotaka nikuelewe, nina uhakika
nimekuelewa na wala sikulaumu. Nina uhakika, hata jana usiku nilikuwa
nikilifikiria hili. Hata mimi, kama Mike wangu angekuwa hai kama
hivyo Jelini, nahisi ningefanya kama wewe au zaidi yako.” Colins
akapoa kama maji.
“Najua kupendwa na kujaliwa, Colins. Najua jinsi
mwanaume anavyokuwa anapokuhitaji. Nimeishi hayo maisha ndio maana
nakwambia nimekuelewa vizuri, japo kwa kujichelewesha.”
“Sitaki kuendelea kuwa mzigo kwako. Umenisaidia
vyakutosha. Umenipa familia, sina jinsi ya kukulipa ila kukupa nafasi na mpenzi
wako. Si sawa kuendelea kukufuata nyuma kila unapokwenda na kuishi.
Nimeona si sawa kwako, mwishoe nitakufanya ushindwe kusaidia wengine. Acha na
mimi niwe na shukurani, nipishe na wengine nao wanao hitaji msaada .” Colins alipoa, akawa kama amemwagiwa
maji.
“Nikikuona kabla ya kulala, sawa. Vinginevyo usiku mwema
Colins. Acha niwawahi kina Mill, na niwalete kwa wazazi pia wawasalimie kabla
hawajalala.” “Sawa.” Akatoka na kumuacha Colins ameganda kama barafu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akafikiria hili na lile akaamua kumpigia simu mama yake.
Akamueleza kwa kifupi juu ya ujio wa Mill na huyo Jerry kurudi kwenye maisha ya
Kamila. “Sasa kwa nini wasije nyumbani kwa chakula kuliko wakutanie
barabarani?” “Unafikiri nimshauri hivyo?” “Kabisa. Hapa ni kwa kina Kamila.
Nimemwambia nitamuozesha mimi mwenyewe. Sasa kwa nini akutane na watu
barabarani?” “Basi acha nimwambie. Asante mama.” “Mbona sasa kama umepoa?” Akanyamaza.
“Colins?” “Wewe
hata nikikwambia mambo yangu haisaidii. Unakuja kunigeuka. Unanisaliti. Acha
nimtafute Kamila.” Mama yake akaumia sana. “Nilikosa
Colins.” Akanyamaza. “Basi jua ninakuombea na
nitazidi kukuombea. Mungu atarudisha furaha yako.” “Sijui mama! Nahisi
nimeshachelewa na naendelea kurudia makosa kwa kila mtu. Achana na mambo yangu.
Acha nimpigie Kamila. Halafu nitakurudia ili uniambie nikuletee nini kukusaidia
chakula, ili msilemewe na mapishi.” “Hapo sawa.”
Akakata.
~~~~~~~~~~~~~~~
Majuto, ni Mjukuu!
Mapenzi & Pesa.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment