Njiani nako kimya. Hasira za usaliti wa Love zilikuwa
zimeshampanda Colins, hawezi kuzungumza. Na Kamila naye akabakia tu kimya,
safari ya kurudi kwao ikaendelea.
Wakati wanakaribia nyumbani Colins akavunja ukimya.
“Ulitaka kwenda kununua hilo gari saa ngapi?” “Utakapokuwa wewe na nafasi,
ukiniambia, nitazungumza na mzee Yusuf ili nitoke. Na pia kama ukizidiwa
na majukumu, tafadhali usiwe na wasiwasi. Bado napakumbuka, naweza nikachukua taksii
inipeleke. Nitakapo kwama nitakuomba ushauri. Si ni sawa?” Colins akamtizama
kama anayejaribu kusoma kitu.
“Kwani mzee Yusuf amekupa siku za off lini?” “Nilimwambia nataka kuwa nikienda tu
kazini bila off, mpaka nitakapojiweka sawa. Lakini nafikiri kwa sasa
nipo tayari.” “Unamaanisha nini?” Akatulia kidogo.
“Eti Kamila?” “Najiona kama naweza timiza ndoto
zangu! Niendelee pale aliponiacha Mike, sio kukwama tena au kurudi tena nyuma
kama kwenye ajira, ambako Mike alinitoa ili nianzishe kitu changu.
Acha nifuate ushauri wako. Niishi kama mtu niliyewahi pendwa, na
ninayejua maisha ni nini. Siwezi kuwa tegemezi hivi daima.
Nimejitafakari nikagundua Mike aliniachia ramani nzuri tu ya maisha.
Nikitulia, nisijichanganye tena, naweza kuifuata na nikafanikiwa tu.”
“Umehisi unajichanganya?” “Kabisa. Najiona nataka vitu vikubwa
ambavyo havijawahi kuwa vyangu, na havitakaa kuwa vyangu.
Najiweka njia panda bila sababu! Si sawa kwangu. Naona ni bora nishike vyangu
na kuviendeleza, na mimi niwe na kitu kinachoeleweka sio kudandia vya watu.
Sina sababu yakufanya hivyo kwakweli.” Colins akapata ujumbe wake vizuri.
Alimringia Kamila! Ikawa akimsukuma mpaka
amefanikiwa kumfikisha mwisho. Sasahivi Kamila hataki tena.
Akaanza kuona anakosa bara na pwani. Akatulia akili ikizunguka. Hajui
chakusema, hajui jinsi ya kujirudi. Na pia hakujua kama ni wakati
muafaka wa kujirudi! Wakatulia mpaka nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakawakuta wazazi sebuleni. Wakaenda kusalimia. Ila
wakagundua wana ukimya usio wa kawaida yao. “Vipi Kamila mwanangu.” “Leo mzee
Yusuf ameniachia kupika mboga zote. Amependa huyo, amesema anaongeza mahari.”
Wote wakacheka. “Kwa hiyo hapa nilipo nimeaga umasikini?” “Kabisa baba yangu.
Wewe subiria mahari kubwa, tena sana.” “Sawa mama.” “Chakula kipo
mezani.” Akaongeza mama Colins.
“Mimi nimekula mama yangu. Hapa nimechoka, leo tulikuwa
na mapishi mengi. Wagonjwa wa kisukari waliongezeka, wengine wa pressure.
Tukawa tunamapishi mengi, siku nzima. Kama hakuna chakusaidia jikoni,
naomba niwahi kulala. Maana na kesho ametuambia mapishi ya kuanzia asubuhi
itakuwa hivyohivyo.”
“Wewe nenda tu kapumzike. Huko jikoni kupo sawa.” “Basi
usiku mwema wazazi wangu. Colins, kesho. Uwe na usiku mwema.” Akabaki
akimwangalia, Kamila akamtizama, akaangalia chini na kuondoka. Wazazi wakawaona
wakajua kuna jambo.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Vipi nyumba?” Mama yake akauliza kama kumrudisha pale
maana macho yalibakia kule alipopotelea Kamila. “Kila kitu kipo sawa.
Wameshabadilisha vitasa. Hivi kesho natuma dereva akatoe pale vitu vya Love na
Festo.” Wakashituka sana.
“Kwamba Festo alihamia pale!?” “Acha tu. Love ananiuma
kama kidonda! Sasa sijui walikuwa wakiishi pale na mimi nikiwepo pale
nahangaika mtaani!” “Najua ni ngumu Colins, na mimi ni mtu wa mwisho
kutaka kunisikia kukupa ushauri. Lakini jitahidi huko usirudi tena.
Ukirudisha tu mawazo yako huko, utakwama na hutakaa ukatoka.”
Akanyamaza.
Wakashangaa safari hii hajibu akabaki ameinama kama
anayewaza kitu. “Vipi kazini?” Mama yake akamjaribu tena. “Kila kitu kinaenda
sawa. Acha nikale na mimi nilale.” Akasimama.
“Colins?” Mama yake akamuwahi. “Najua mwanzo ni mgumu.
Lakini jitahidi kutafuta siku hata moja ya mapumziko. Itakusaidia kufikiria
mambo mengine.” Akabaki amesimama akifikiria.
“Au bado unaona unahitajika sana?” Akaongeza swali kwa
upendo maana Colins aliyekuwa naye kwa chakula cha mchana siye huyu. “Hakuna
siku pale hapahitaji mtu wakusimamia. Walizoeshwa vibaya.” “Basi ongeza
msaidizi ambaye mtakuwa mkipishana siku. Unahitaji kupumzika.” Baba yake naye akaongeza
kwa kujihami. “Nafikiri nitafanya hivyo.” Akaelekea mezani kula. Lakini
wakashangaa amepoa sana. Si kwa ukali, ila kama ametingwa na jambo. Wakaona
wamuache tu.
Njia Panda.
Baada ya hapo akarudi chumbani kuoga akijiuliza kama ndio
aende kwa Kamila au la! Alimuahidi kuwa atakuwa akimsubiria mpaka alale. Lakini
Kamila ni kama amembadilikia fulani hivi! Akavaa na kuona amfuate tu chumbani
kwake. Akagonga kidogo na kufungua kama kawaida yake lakini akashangaa chumba kimefungwa
na funguo kwa ndani. Akajua ndio hakaribishwi tena.
Mara mlango ukafunguliwa akiwa anaonekana ametoka
kitandani. “Ahadi ya kukusubiria mpaka ulele, bado ipo palepale.”
Akacheka kinyonge akiwa amesimama mlangoni, asimpishe aingie. Akaangalia chini
kama anayefikiria kitu, kisha akamjibu. “Nashukuru Colins. Lakini
nafikiri nitakua sawa tu. Asante. Nenda na wewe ukapumzike.” Akabaki akimwangalia
asiamini.
Akacheka kidogo ya kujibaraguza kisha akaongeza kiutani
kama kumtoa njiani. “Usije nisahau asubuhi.” “Unajua siwezi, Kamila.” Akacheka
kama kumridhisha lakini wazi alionekana amebadilika. “Basi acha na mimi
nijaribu kulala, ili niamke na nguvu. Usiku mwema.” “Asante na wewe.” Akarudi
ndani na kufunga mlango akiwa amemuacha amesimama palepale. Akapigwa na butwaa
akishindwa hata kusogea, mwishoe akaondoka kurudi chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa bado yupo kwenye sintofahamu, amepigwa na bumbuwazi,
hajui awaze nini, ujumbe ukaingia kwenye simu ya Mike. Akaiwahi kwa haraka sana
kujua safari hii Kamila anamwambia nini. Na pia ilikuwa njia rahisi sana kujua
kinachoendelea moyoni kwa Kamila kupitia mawasiliano yake na Mike.
‘Mike
mpenzi, umeondoka na wapangaji wetu wote na kuniachia majengo ambayo ni mazuri
kwa nje, lakini ndani ni matupu. Umeondoka na Utulivu, Furaha, Amani na Upendo pia! Bora
ungeniachia hao waliokuwa wapangaji wetu, isingekuwa ngumu kuanza.
Lakini nakuahidi mwanzo mpya. Najua itakua ngumu, lakini sitaacha kujaribu
mpaka nifikie ulipotaka nifike nikiwa na wote hao wanne wakiwa wamerudi
tena kwenye maisha yangu, tuje kukutana tena kwenye maisha ya milele.’ Akaendelea kusoma.
‘Ulinipa
vitu vilivyoonekana ni rahisi sana kutoa, kumbe sivyo ilivyo! Wengi wanafikiri kumiliki
majengo mazuri na ya thamani ni kila kitu, lakini wanashindwa kumiliki wapangaji
tulio miliki mimi na wewe! Daima utabaki wa pekee Mike. Milele nitakukumbuka.’ Ikawa kama kibao usoni kwa Colins. Akajua ile gomba ya
asubuhi akiwa amemuahidi hatarudia tena, imemtisha Kamila, asijue na mengine
mengi yanachangia.
Asuhubi.
Aliamka kwa kuchelewa sababu ya kulala kwa kuchelewa
akiwaza bila kupata majibu. Akajitayarisha kwa haraka. Maana alamu ilimuamsha,
akaizima na kurudi kulala. Akatoka kwa haraka, akamkuta Kamila anamsubiria upande wa kulia chakula, wazazi
walishaondoka.
“Samahani sana. Nimekuchelewesha.” Akanyanyua uso
akamtizama kama ambaye alikuwa akichat kwenye simu yake kitu kisicho cha
kawaida kwa Kamila. Alimfahamu kama yuko peke yake. “Hamna shida. Mimi nipo
tayari.” Akasimama kabisa na pochi yake, kisha akarudisha macho kwenye simu.
Akamuona anaandika kwa kifupi, na kuweka simu kwenye pochi.
“Umependeza Kamila!” Akacheka kidogo na kushukuru.
“Asante na wewe umependeza kama kawaida yako.” Colins akamtizama na tabasamu, wakatoka
hapo. Njiani akasikia simu yake kama imeingia ujumbe. Akamuona anatoa,
anaendelea kuchat kwa muda mrefu tu kama ambaye hayupo hapo kwenye gari au
kama hajali uwepo wa Colins . Akaanza kusumbuka rohoni kana kwamba si
kawaida yao kuwa kimya garini, wakati hata jana yake waliendesha kimyakimya na
yeye akiwaza yake.
Wakati mwingine alimuona anasoma kisha kufikiria kidogo,
anajibu halafu kusubiria majibu kwa muda kidogo. Akaendelea hivyo mpaka
wanafika kazini bado anachat. Kuuliza, hawezi. Akashuka na
kumtakia siku njema kama anayeitupa tu. Hajamwangalia wala nini, ila
kuzungumza huku akichukua kipochi chake na kushuka garini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Siku ilikuwa nzito kwa Colins, hajui chakufanya. Hofu ya
kupotelewa na Kamila ilikuwa bayana lakini akawa hajui chakufanya wala
kujirudi. Akatamani kama angeendelea vilevile akiwa chini yake mpaka
atakapokuwa tayari naye, lakini Kamila ameonyesha hatafanya hivyo tena.
Alishamwambia hana sababu ya kufanya hivyo tena, anaendelea na yake.
Kazi zikaendelea mpaka kwenye majira ya saa tano na nusu
hivi akamtumia ujumbe. ‘Naona naweza pata nafasi baada ya nusu saa hivi, tunaweza kutoka
kwenye saa sita.’ Akabaki akisubiria majibu, kimya.
Akasubiri baada ya hiyo nusu saa akampigia. Wakati
inakaribia kukatika akapokea. “Pole, simu ilikuwa kwenye pochi na mimi napika.”
“Hamna shida. Uliona ujumbe wangu?” “Wala sikuwa na simu. Samahani. Acha
niangalie.” “Hamna haja, tunaweza kuzungumza tu. Nimepata nafasi, tunaweza
kutoka sasahivi tukaangalie magari.” “Nilishakwenda kwenye majira ya saa tatu hivi,
palikuwa hakuna mambo mengi, ndio mzee Yusufu akaniruhusu muda huo ili nirudi
mapema tusaidiane kwenye chakula cha mchana.”
Colins akapoa ila akajikaza.
“Umefanikiwa?”
“Kwa asilimia fulani.” “Unamaanisha nini? Hukupata gari unayopenda?” “Hapana. Mill
amenishauri kuliko kununua gari ambalo nitakuja uza, tena pengine kwa hasara,
wakati nikisubiria gari ninayotaka, ni bora aniazime yake nitumie mpaka yangu
itakapokuja. Kwa hiyo amenisaidia kuagiza, akiwa ananipa yake nitumie.
Nitakueleza vizuri baadaye. Ni sawa nikikuaga kwa sasa? Kuna kitu kipo jikoni
napika.” “Hamna shida. Baadaye.” “Asante.” Simu
ikakatwa.
“Mill tena ni nani
huyo!?”
Colins akabaki amekodoa macho
akijiuliza mwenyewe. “Daah!” Akabaki hajui tena chakufanya. Akili ilishavurugika
hata kazi tena zikawa haziendi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa hakika kichwa kilishindwa kufanya kazi kabisa. Akaona
bora atoke hapo. Akamwangalia mama yake alipo. Akashangaa kuwaona wapo pamoja
na baba yake kwenye mgahawa. Akajua wamekutana kwa chakula cha mchana.
Akajikuta anachukua funguo za gari na kutoka kuwafuata.
Hawakutegemea kumuona Colins. “Umejuaje tulipo!?” “App
ya 360.” Akajibu akikaa ila wakamuona hayupo sawa. “Au nitawaingilia?”
“Nimetaka kumtoa tu mama yako kwenye yale mazingira ya kazini kwa muda mfupi,
wala hakuna cha peke yetu. Agiza chakula.” Walimjua Colins kwa chakula.
Akaagiza kinywaji na chakula wao wakiendelea kula
taratibu. “Vipi kazini mama?” “Naendelea hivyohivyo.” “Si uje ufanye kazi pale.
Nitakupa uongozi wa manesi wote pale. Na nitakulipa vizuri.” Baba yake
akamwangalia kama aliye hamaki kwa hilo. Ila mkewe kimya. “Na sio kwamba nakupa
kazi kwa kukuonea huruma, ni kwa sababu nataka ujuzi wako na kuwa na mtu
wangu wa karibu pale. Wana uzembe mwingi inabidi kuwafuatilia kila wakati.”
“Siwezi kuacha kazi kule kabla sijastaafu.
Nitapoteza mafao yangu. Nitakua sawa.” “Chukua likizo bila malipo huku
ukisogeza siku mpaka ustaafu.” Wakamuona amenyamaza. “Na hutakuwa ukikimbia
mama Coly.” Mumewe akawa kama amemsoma mkewe. “Nataka Connie akimaliza shule
yake kabisa, akiwa daktari kamili, akiwa anapita round na mimi
niwepo. Ndio ndoto zangu, jamani! Mwanangu amejitahidi na kujinyima kweli.
Nataka kujivunia kiziwanda wangu akiwa anapita pale, na mimi nipo.
Kuondoka sasahivi nitakuwa nakimbia na kumpa yule mama nguvu.
Hivyo hapana.” Wakawa wamemuelewa.
“Nimekuelewa mama.” Akakubali akionekana ana mawazo.
Akapotelea mawazoni. Mama yake akajihisi amefanya upendeleo. “Ila naweza
nikachukua likizo hata ya miezi 6, nije kukusaidia kupaweka pale sawa,
kisha nirudi kazini kwangu, ili Connie na yeye anikute.” Akamwangalia kama
aliyemtoa mawazoni.
“Unataka kufanya kwa kuwa unapenda au kwa kunihurumia?
Maana mimi nitakua sawa tu. Nataka wewe uwe na mazingira mazuri nyumbani na
kazini.” “Ni kwa kutaka kwangu mwenyewe.” Colins akabaki akimwangalia. “Nini
sasa?” “Si umetoka kunikatalia wewe, ukitaka kumuunga mkono Connie na si
mimi?” Akaanza kucheka. “Umejishitukia na kuhukumiwa?” Akamuuliza na kufanya
wote wacheke.
“Samahani Coly, mwanangu.” “Usijali.” Kisha akatulia.
Wakaangaliana hao wazazi wawili. Kinywaji chake kikaletwa. “Nikija utanilipa
kiasi gani?” “Kikubwa mpaka utakataa kurudi Muhimbili.” Wakacheka sana.
“Muulize baba jinsi nilivyobadilisha malipo ya wafanyakazi. Madaktari pale
walikuwa wakizembea kuja sababu ya pesa ndogo, lakini sasahivi wanapigania shift
za pale.” “Ni kweli.” Mzee akaafiki.
“Hongera Coly. Umefika mbali kwa muda mfupi!” “Lakini
havina raha! Havina raha kabisa. Kila nikikamilisha jambo vizuri,
nategemea kujisikia hali fulani, lakini sipati. Nazidi kujisikia…”
Akasita. Kama anayefikiria. “Mpaka sioni maana ya maisha!” Akajikuta
akizungumza cha moyoni mbele ya wazazi wake. Kimya kwa muda wote wakijua maisha
yamekosa maana sababu ya kumpoteza Jelini.
“Labda ukihamia kwako, ukawa na uhuru wako. Na Kamila
anaweza saidia kukuchangamsha. Anaonekana ni biti mzuri, Coly. Mpe nafasi.” “Amekataa kuhama na mimi. Ameamua kubaki
na nyinyi pale.” Wote wakashangaa.
“Kamila!?” “Si ndiye tunayemzungumzia au?” “Nahisi kuna
kitu hakijakaa sawa Coly. Kamila niliyezungumza naye mimi jana, alikuwa yupo
tayari kukusubiria kabisa!” Colins
akamtizama na kukunja uso. “Kamila anaonekana anakupenda, ila anajua bado moyo
wako upo kwa Jelini.” Hapo akanyamaza. Chakula chake kikaletwa, akaanza kula.
“Jelini anaolewa Coly. Usije kosa bara na pwani.”
Mama yake akaongea kwa tahadhari. “Nahisi nimeshachelewa.” Akajibu tu
hivyo na kuendelea kula akionekana amebadilika kabisa. Wakaona wamuache. Akala
kwa haraka, akaondoka na kuwaacha hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati yupo na sitaki nataka, dunia bado
inaendelea kuzunguka. Haimsubiri yeye. Kamila
ameshapata ujumbe wake, ameamua kuendelea na yake. Mill tena ni nani!? Swali lilobakia kichwani kwa Colins, kazi haziendi tena.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment