Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 27. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 27.

Hapohapo akampigia simu mwenye hoteli. Akapokea. “Najua umekata tamaa juu ya shitaka lako la yule binti aliyepewa sumu kwenye hoteli yako.” Akashituka huyo mmiliki. Akauliza. “Wewe ni nani?” “Nilikusaidia kuiwahi ile video. Nilikuwa na yule binti aliyenyweshwa sumu hotelini kwako.” Ndipo akamkumbuka.

“Wamenifungia sehemu kubwa sana inayoniingizia pesa, aisee! Nipo hatarini kufungwa na hoteli yangu pia kufungwa. Na bado natakiwa kuwalipa fidia! Wameibua pressure ambayo nilijua imepona! Sasahivi naishi kwa madawa. Sijui kama nitapona!” “Sasa huu sio wakati wa kukata tamaa.” Colins akaendelea.

“Mwambie wakili wako, anitafute mida jioni. Nina ushahidi mpya wakumsaidia kushinda kesi. Na hili usizungumze na mwingine yeyote, ili kuwashitukiza washitaki wako. Lazima kujipanga upya. Ila nakuhakikishia safari hii utashinda kama ukifuata ushauri wangu.” Akaibua tumaini jipya. Colins akamuweka sawa na kukata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~

Safari ya kwenda kazini kwa wote ikaanza. Kimya njiani kila mmoja akiwaza lake. Kamila ndio hakuthubutu kuanzisha mazungumzo yeyote yale. Alishamsikia akiunguruma asubuhi hiyo kwa wazazi wake, kama simba, akajiweka pembeni. Ila mazungumzo kati yake na wazazi wake yakaendelea kujirudia kichwani mwake.

Vile alivyoendelea kumlilia Jelini. “Hatakuja kuwa na nafasi ya msichana mwingine moyoni mwake. Hapa nitajichelewesha na kuendelea kujiumiza. Bora nijiachie.” Kamila akaendelea kuwaza.

Akakumbuka sifa za Jelini alizoambiwa na mama Colins, alichoona ni cha tofauti na yeye ni ile hali ya kusema anajituma sana kwenye biashara zake na amefanikiwa. “Labda ndio maana anashindwa hata kunifikiria! Ananiona nitakuwa tegemezi daima. Sifananii na Jelini mchapakazi na mwenye maendeleo.” Akaendelea kuwaza.

 “Lazima kubadilika. Hapa sina changu.” Akaazimia moyoni akiendelea kujipanga na kutafakari juu ya kuchukua hatua. Yeye Colins alikuwa mbali kimawazo. Kimya. Kama ambaye yupo peke yake garini. Akamuona ni kama anamipango mingi mawazoni, akaona bora hivyo. Pakatulia.

Wakati wa Kujenga.

Kwenye majira ya saa nne, akaingia baba yake ofisini kwake. “Kwema?” “Nataka kuwepo hapa kukuongezea nguvu, ukiwa unamalizana na kina Simba kwenye ile nyumba ya Kigambini. Najua wamejipanga. Sitaki liaharibike jambo, tumalizane nao kwa haraka.” “Nashukuru.” “Mambo yanaendaje lakini?” “Mwanzo ulikuwa mgumu. Uzembe mwingi. Lakini naona sasahivi tunakwenda sawa. Kila shift nimepata watu. Naona sio mbaya.” Baba yake akatulia kidogo.

Akamuona kama kuna kitu anataka kuuliza ila anasita. “Ni nini?” “Nataka kukuuliza kitu, lakini sitaki kukutibua.” Colins akamwangalia akaona anyamaze. Kisha akafikiria tena akaona amuulize tu, akakuta ametulia tu akimwangalia.

“Ulitaka kuniuliza nini?” “Kwa yote uliyofanya hapa, na kwa kiasi hiki! Kweli hufurahii hata kidogo?” “Hizi ni ndoto zako baba.” “Sawa. Lakini hata katika hili, kweli hujivuni hata kidogo!?” “Kidogo.” Baba yake akacheka.

“Hukunitendea haki baba.” “Nia yangu ilikuwa nzuri Colins.” Akanyamaza. “Ila nikwambie kweli tu. Japokuwa imeua mahusiano yetu, mimi na wewe, lakini kibinafsi najivunia sana.” Colins akamtizama! Ila akaona amuache tu.

 Ila mzee akashindwa kujizuia tena. Akaendelea kwa tahadhari. “Umepita matarajio yangu.” “Naona hata ya Simba.” Wakacheka. “Naona yeye na familia yake ndio zaidi. Hawakukutegemea kabisa! Wapo kwenye mshituko ambao nadhani hautakuja kuisha. Utabaki kuwa usiku wa giza nene.” Angalau wakazidi kucheka.

Mara sekretari akapiga kumwambia ana wageni. “Waruhusu waingie.” Mzee akajiweka sawa. Wakaingia. Chris, mama Simba na mumewe. Wakasalimiana, lakini wazi ni ile ya salamu ya bora yaishe. Chris alikuwa kwenye heshima zake zote kama anayeomba jambo lisiharibike hapo. Na yeye Colins akajifanya kama hamjui! Kumbe alishampa vitisho vyakutosha, hapo ameadabika.

 Wakamkabidhi kabrasha. Colins akafungua na kuanza kusoma. Kila kurasa aliomaliza alimkabidhi baba yake na yeye asome. Wakaridhia mpaka kiwango cha pesa. Akajua Chris aliwaweka sawa. Hapohapo bila ya kuchelewa akawaandikia hundi ya pesa yao tasilimu. Tena kutoka kwenye akaunti yake binafsi wala si ya kampuni. Akawakabidhi wasiamini kwamba Colins ndio anakiwango hicho chote cha pesa!

“Tumemalizana ramsi kwenye nyumba ya Kigamboni. Mwambieni Love, haruhusiwi kuonekana kule. Mizigo yake yote nitamtuma dereva ailete nyumbani kwenu. Muwe na siku njema.” Wakamtizama kama wammeze, ila walikuwa na mengi. Wakatoka hapo kwa haraka, ili kutoa hiyo pesa benki ya kuweka dhamana, wakamtoe Love huko lupango, wamkimbize hospitalini.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakamuacha hapo na baba yake. “Hongera kwa kununua nyumba.” Colins akacheka na kunyamaza. “Nina ushauri.” Colins akamwangalia. “Naruhusiwa?” “Lini hilo limekuzuia?” Mzee akacheka na kutingisha kichwa. “Ni nini?” “Kwa sasa, wakati ukisubiria nyumba yako, nashauri kabla nyumba ya Kigamboni hujaifanya ya biashara, ukaishi huko ili uwe na uhuru.” Hilo likawa si jambo baya. Lakini akamuona anafikiria.

“Vipi?” “Naona si wazo baya. Ila namfikiria Kamila!” “Kwa nini usimpe nafasi? Yule binti anakupenda, Colins.” Colins akashangaa sana. “Umejuaje?!” “Amemwambia mama yako.” Colins akanyamaza. “Mpe nafasi. Anaonekana ni binti mzuri. Kuwa naye karibu bila kuanzisha mahusiano ya kimapenzi kwanza, ili kumchunguza na kumfahamu kwa karibu.”

“Huwezi jua pengine kuna kitu kizuri kinaweza zaliwa. Mungu hawezi kukuacha moja kwa moja, na Jelini hawezi kuwa mtu wa mwisho kukupenda. Na kabla sijakupandisha hasira, ukanikatalia, naomba ufikirie. Ni hilo tu.” Mzee akaondoka.

Wakati Wakuvuna Kwa Kila Aliyepanda Lake.

Hawakupishana sana na wakili wa yule mwenye hoteli na Peter mwenyewe. Kweli alionekana mgonjwa. “Nashukuru kutusaidia.” “Acha kwanza muone ushahidi wenyewe.” Akawawekea ile video na kuamsha tumaini kubwa kwao. Akazungumza naye jinsi ya kujipanga kutetea ile kesi. Akampa madhaifu yake kama alivyoambiwa na Chris.

“Tafadhali jipange na kuwa na hoja za msingi. Wakili unayeshindana naye anajulikana ni mzuri, na mwenzio anajua kujipanga. Ukijiweka sawa, kwa hakika kwa huu ushahidi utashinda tu.” Kisha akaongeza.

“Na sasa pasipoe. Kwa haraka sana wahi mahakamani sema unaushahidi mpya, unaomba waitishe tena kesi. Najua wewe unajua zaidi.” Akamtia morali haswa, lakini lengo ni Love asikae sana uraiani. Yaani awe anatolewa kwa kumkamilishia lengo lake yeye Colins.

Kutoa familia ya Simba kwenye ile nyumba ya Kigamboni, ibakie kuwa yao kina Komba, kisha arudi jela sasa kwa shitaka la jaribio la kutaka kuua. Ambako huko atakuwa na shoga yake Kemi, mpaka kifo. Wakili akatoka hapo kama akimbie.

Kakumbuka Shuka Pashakuchwa.

Ilipofika mida ya usiku, akapata ujumbe kwa Kamila. ‘Mimi nipo tayari, utakapokuwa tayari unijulishe tafadhali, ili nisogee garini.’ Akaona ampigie. “Leo umekua kimya!” “Kuna muda nilikuletea chakula nikaambiwa umetoka kwa chakula cha mchana.” “Oooh yeah! Baba alishindwa kwenda kula na mama, ndio akaniambia niende, ili tusimuache peke yake. Nahisi nimekuwa na mambo mengi kwa karibukaribu nikasahau kukutaarifu.” “Ingekuwa mimi ni Jelini, wala asingesahau kuniaga. Sina maana kwake kabisa!” Kamila akawaza na kunyamaza.

“Kamila?” “Nipo, nakusubiria huku jikoni.” “Kwa nini usije huku?” “Huku pia nipo tu sawa. Hamna shida.” “Basi niseme naomba uje kuna kitu nataka kukwambia.” “Sawa. Nakuja.” Wakaagana ila akamuhisi amekua mzito, sio kawaida yake.

Moyo Uliokata Tamaa.

Baada ya muda akamuona amesimama mlangoni. “Karibu.” Akaingia na kukaa kama aliyepo mbele ya hakimu. “Una ratiba yeyote ile baada ya hapa?” Akatingisha kichwa kukataa. “Basi naomba nisindikize Kigamboni. Kuna kitu nataka kukuonyesha kisha tuzungumze.” Akakubali akiwa amepoa haswa.

Safari ya Kigamboni ikaanza akiwa ametulia haswa. “Upo sawa?” “Ndiyo.” Akajibu hivyo tu na kutulia. Akaona amuache. Safari ikaendelea mpaka kwenye hilo Jumba lililokuwa likimtoa roho Love.

“Ni pazuri!” Akasifia Kamila akiangaza macho lakini si kwa kushangazwa kama aliyezoea aina hiyo ya mazingira. Colins hakushangaa sana kutokana na sifa alizosikia za Mike. Akahisi alikuwa akiishi kwenye aina hizo za mazingira.

Alishaandaa mafundi kuanzia asubuhi alipoinunua hiyo nyumba kubadili vitasa vya nyumba nzima. Hapo anafika mafundi wanamsubiria malipo na funguo mpya.

Akamalizana nao ndipo akaingia sasa ndani. Akamzungusha Kamila kila mahali, akifuata tu kwa nyuma akiwa anamuonyesha mazingira yote. Kisha wakarudi sebuleni. “Naomba tukae kidogo.” Akakaa.

“Sasa kwa sababu hapa pamekuwa kwangu rasmi. Sio pote, inamaana na familia. Na kwa sababu nyumba yangu bado anatumia yule mpangaji kama nilivyokwambia mwanzoni, hata baba ameshauri nihamie tu hapa kwa uhuru.” “Hongera Colins.” Colins akacheka akimwangalia.

“Namaanisha. Hapa ni pazuri na kweli utapata uhuru.” “Sawa. Lakini nakukaribisha na wewe. Tunaweza hamia wote.” Akabaki akimtizama kwa muda kisha akamuona amekunja uso na kuinama. Colins hakutegemea.

“Eti Kamila?!” “Unahamia lini?” “Mapema iwezekanavyo.” Akamjibu huku akijaribu kumsoma. “Mimi naona nitabaki tu pale nyumbani.” Colins alishituka, hakutegemea! Kabla hajafikisha taarifa moyoni, Kamila akaongeza.

“Ila naomba msaada wako.” Colins akabaki akimtizama, ashabadilika rangi. “Kuna sehemu mbili tatu najua wanauza magari. Naomba ukipata nafasi unisindikize nikanunue gari ili na mimi  nipate usafiri wa kunisaidia hapa mjini. Nikipata kama ile gari aliyokuwa amenipa Mike, ningependelea ile zaidi. Vinginevyo nitanunua yeyote tu kwa sasa wakati nikiagizia ile, ikija naweza fanyia hii ya sasa biashara au nikaiuza.” Colins akapoa! Hakutegemea kama atakataa kuhamia naye hapo. Maana tokea mwanzo ombi lake ilikuwa akihama, basi ahame naye.

Kulikoni! Likabakia swali kwa Colins akiwa amenyongea na hisia za kukataliwa zimemjaa. Akatulia kwa muda, akajikaza. “Sawa. Sioni kama kuna tatizo.” Kamila akanyamaza ila na yeye kwa kuumia. Hata hakumbembeleza! Akazidi kuamini yupo sahihi kwenye maamuzi yake. Si kwamba Colins anamuhitaji, ni kumsaidia tu.

Wakajikuta wote wametulia hapo sebuleni, kwenye madhari nzuri ya kuvutia, ila mawazo hayopo hapo. Mwishoe Colins akasimama. “Naomba nisubirie kidogo, tutaondoka muda si mrefu.” Akaondoka hapo akiwa mwekundu haswa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akakusanya vitu vya Love na kuviweka chumba kimoja. Akagundua Love alimkusanyia yeye vitu vyake vyote na kwenda kuvitupa chumba kingine. Wala hakuwa amempangia. Akaangalia na kuumia sana. Akiwa anaangalia chumba alichokuwa akitumia Love ambacho ndio Master bedroom, akagundua baadhi ya nguo ngeni kwake, za kiume! Akazidi kuumia. Akajua ni kweli Festo alikuwa akija kulala hapo.

Swali lakumuumiza likabaki je, alikuwa akiishi naye hata yeye alipokuwa hapo au la! Hakuwa akikumbuka. Akazidi kukasirika kadiri alipogundua upo hata mswaki na viatu kabisa! Kama ambaye alikuwa akiishi hapo! Akatoka kwa hasira, akarudishia mlango na kuamua kutoka kabisa hapo.

Akamuita mlinzi. “Kesho watakuja watu wakusafisha hapa na maagizo ya kukusanya kila kitu kwenye kile chumba. Waweke kwenye maboksi na kuacha hapo nje. Dereva atakuja kuchukua.” Hilo likakaa sawa. Akamwambia Kamila waondoke.

~~~~~~~~~~~~~~~

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment