“Asante kujali Colins.” Akacheka taratibu akimtizama
lakini wazi alionekana ametingwa. “Ningeelewa kama ungehitaji muda wa peke
yako.” “Hapana, ahadi ni deni. Nisingeweza kukuacha tu hivihivi.” Hiyo
haikusikika vizuri kwa Kamila. “Kwamba yupo hapa kama kutimiza wajibu, si
kupenda kwake!” Kidogo ikamsumbua. Ila akajikaza kama kawaida yake, Kamila
hataki makuu.
“Pole. Sikujua kama ndio ilikuwa mbaya hivyo!” “Ilikuwa
mbaya zaidi hata ulivyosikia. Ilikuwa mbaya sana. Na nilipokuja kurudiwa
na akili ndio nikajikuta nimepoteza kila kitu pamoja na Jelini. Nilijawa
na hasira, uchungu na majuto kwa muda wote huo mpaka wewe
ulipokuja kwenye maisha yangu.” “Kweli Colins!?” Kwa jinsi anavyomchukulia,
ikamuwia ngumu kuamini.
“Oooh yeah! Nilikuwa na hali mbaya sana. Muda mfupi
uliopita nilitaka kujifungia na kuzidi kukasirika, nikakumbuka wewe upo
na unanisubiria. Ikabidi nitoke. Lakini kama si hivyo, hayo ndio yalikuwa
maisha yangu. Nakaa tu chumbani nikizidi kuumia. Kwahiyo nazidi kuamini Mungu amekuleta
kwenye maisha yetu ili kunisaidia mimi.” Kamila akafikiria, hajui
afurahie au la!
“Mwenzio kuna mtu aliniambia hivi. Sihitaji kupata majibu
yote kwa wakati mmoja. Hatua ndogondogo kama mtoto mdogo.” Colins akacheka
akijua anamzungumzia yeye. “Nimefuata ushauri wako. Sasa hivi mwenzio naishi
kwenye familia ya baba na mama. Na wananikarimu. Lakini wakati ule napita
pale pagumu na wewe unanishauri hivyo, nilikuwa sioni mwanga.
Lakini ona nilipo na wanao nizunguka.” Colins akatulia akimwangalia kwa
kutulia.
“Kwa hiyo na wewe
jipe muda Colins. Mungu atakurejeshea vile vizuri ulivyopoteza, kama Ayubu.”
Colins akacheka. “Kumbe unajua bibilia!” “Sio kwamba ni mkristo mzuri sana,
lakini tulikuwa tukienda kanisani na Mike, halafu wakati mwingine tunaomba
pamoja. Halafu usisahau mimi mwenzio mtoto wa masista.” Colins akazidi kucheka
akimtizama.
“Kwa hiyo usiogope, na usisahau hata siku moja kuwa
Kamila yupo. Najua mimi si Jelini, na sitaweza kuwa yeye
kama ulivyoniambia juu ya Mike. Lakini ujue mimi nipo Colins. Na sina
nipokwenda.” “Asante Kamila.” Wakaangalina na kucheka taratibu Kamila akainama
kama kwa aibu.
“Acha niweke movie
tuangalie wakati ukitafuta usingizi.” Akaweka na kurudi kukaa. “Jilaze hapo
kwenye mto, niku masaji miguu.”
Colins hakutegemea, akabaki kama amepatwa na ububu. “Nina uhakika utapenda, itakufanya
utulie kabisa. Lala, nipe miguu.” Akasisitiza na kumfanya ajilaze chali.
Akatoka kwenda kufuata lotion yake, Colins akimsindikiza
kwa macho akiwa na nguo yake ya kulalia ila ya heshima tu. Wakati anageuka, na
yeye akarudisha macho kwenye luninga kwa haraka.
Akakaa kitandani kabisa. Akamnyanyua miguu taratibu
akimtizama. Akaiweka mapajani kwake. Akampapasa kwanza taratibu. Juu
mpaka chini. Mikono laini na moto ya Kamila ikamsisimua kiajabu sana.
Akajikaza. Akaanza kumvuta vidole vya miguu taratibu.
Akafanya hivyo kwa vyote, tena utaalamu wa namna yake, ulioamsha raha kwa Colins. Ndipo akampaka sasa hiyo
lotion yake maana hakuwa na mfuta ya masaji. Alimpaka bila papara, taratibu,
kisha akaanza kumchua. Juu mpaka kwenye nyayo na katikati ya vidole. Kwa hakika
akaanza kumchanganga Colins.
Hisia zilizokuwa zimekufa kwa muda mrefu akashangaa zinaanza kufufuka. Ikawa Kamila naye kama
anayemfanyia makusudi vile!
Aliendelea na wakati mwingine alitumia kucha, gafla mzee akasimama!
Colins alishituka na kuvuta mto, akajiwekea juu kama kujiziba. Kamila
akajifanya kama hajaona. Akaendelea na yake, akiwa ameinamisha kichwa, macho
kwenye anachokifanya, akiendelea.
“Asante.” Akamsikia akishukuru. Akamwangalia. “Inanifanya
nitulie!” “Ndio vizuri. Lala.” “Na wewe?” “Mimi bora nijue upo pembeni yangu,
nitalala tu.” “Unauhakika? Maana kwa hivyo unavyonifanyia, ni kama
unanibembeleza!” “Natamani na mimi niwe faraja yako Colins!” Hapo anaongea
vidole vyake vinavuta vinyweleo vya miguu taratibu.
“Umeyabadili maisha yangu Kamila. Amini umekua msaada
kwangu zaidi nitakavyoweza kukiri kwako.” Maneno yake na moyo wake vilimfanya Kamila
kutosadiki kwa asilimia kubwa sana. Akanyamaza na kuendelea na hiyo
masaji.
Akamuona anaanza
kulegea ile ya kunogewa kabisa. Akajua amemwamsha kupitiliza.
Alichoshangaa na kumuumiza ni vile alivyoweza kujitoa pale. “Nashukuru,
lakini naomba nitumie choo, tuje tulale. Na wewe upumzike.” Hakutegemea! Akatoa
miguu yake taratibu, suruali ikiwa imemtuna haswa kwamba yupo juu, lakini
akatoka na kwenda kutumia choo, hapohapo chumbani. Akamsikia amefungulia maji
ya kwenye sinki kama anayeosha uso. Kimya kwa muda.
Kamila akajirudisha kulala kwa unyonge. Hakutegemea
katika hali ile na bado akamuacha!
Alitegemea mengi hapo, hata kama si mapenzi basi hata kiss za
nguvu! Yeye mwenyewe alishaanza kuloa.
Kitendo cha kujitoa hapo mikononi mwake na mautundu yote aliyokuwa
akimfanyia, ikamuumiza na hapo ndipo alipojihakikishia kwa hakika.
“Huyu hakuna kitu jitakuja
kumfanyia akanifurahia kama Jelini.”
Akajinung’unisha. Akavuta shuka na kujifunika mpaka shingoni, akiwa ameficha
kabisa nguo nzuri ya kulalia aliyokuwa amevaa. Kisha akajivuta pembeni.
Baada ya muda akamuona anatoka. Yupo vilevile, jamaa kagoma kushuka. Akarudi kujilaza hapo
pembeni yake. “Pumzima.” Akatingisha kichwa kukubali. Akamuona jinsi alivyo
nyongea.
Akajisogeza karibu yake akamgeukia na kumvuta mkono. Wote
wakalala ubavu ila wamegeukiana. Aliutoa huo mkono ndani ya shuka. Akaushika
vizuri. “Nashukuru kwa masaji. Nimeifurahia sana. Lakini Itabidi
nitafute siku maalumu, na sehemu nzuri utakayonifanyia. Lakini si
hapa kwa wazazi na si
leo.” Kamila akamwangalia akitilisha huruma.
“Unanielewa lakini?” “Ndiyo.” Akamtizama kwa muda kama
kutaka uhakika. Wakiwa wanaangaliana kwa karibu kabisa. “Nimekuelewa Colins.” Akarudia
kama kumuaminisha ila akajua hajaridhika.
“Wewe ni msichana mzuri sana, na ni mwema wa namna
yako, Kamila. Sitaki kukuchanganya na mambo yanayoendelea sasahivi. Haustahili
kuchanganywa na chochote, zaidi hizi fujo zinazoendelea kwenye maisha
yangu. Si sawa kwako. Tafadhali naomba unielewe, japo najihisi nakaribia ukingoni.
Patatulia tu. Sawa?” Akatingisha kichwa kukubali.
Akambusu ule mkono aliokuwa ameushikilia. Akamsikia
akivuta pumzi kwa nguvu. Akajua na yeye hali ilishakiwa ya tofauti,
anajaribu kutulia. Akamuhurumia, asijue chakufanya.
Ila hata hilo busu akalithamini japo ni la mkono tu.
Akamsikia akishukuru. “Asante.” “Wewe ndio nikushukuru. Nitakuja kukwambia ni
kwa nini nakushukuru na utaelewa tu.
Ila hiki ulichonifanyia hapa, nilikata tamaa. Umenirudishia tumaini. Asante.” “Karibu.”
Kisha akajigeuza kumpa mgongo, akalala. Akiwa amekubali matokeo.
ASUBUHI.
Asubuhi ikamkuta hapo kitandani kwa Kamila. Safari hii hakukurupuka
vibaya. Akatulia hapo kitandani akitafakari ya jana. Akamtizama Kamila
alivyolala pale. Taa ilikuwa ikiwaka. Safari hii amemgeukia. Akamtizama kwa
kutulia akiyatafakari maisha.
“Unaweza kuta katika yote, Kamila ndio mke Mungu
aliyenitayarishia tokea mwanzo!”
Akawaza ila safari hii kwa hofu kidogo. Akamtizama vile alivyolala vizuri
na kuvutia. Kamila ni mzuri, ila hisia zipo kwa Jelini!
“Kama kweli ni wangu kwa nini bado najihisi hivi kwa
Jelini!” Akawaza akijua historia imeshajirudia.
Alichokifanya kwa Jelini, ndio amekifanya kwa Kamila. Ila hajui chakufanya. Colins
si mchanganyaji. Akianzisha jambo na mahusiano, husimamia mpaka
mwisho, ila huwa ina mcost/mgarimu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini alimkuta kwenye mahusiano magumu na Love,
na yeye Kamila amemkuta kwenye mahusiano mazito, yaliyojaa penzi lililo katiliwa, la Jelini. Wote wanapendana,
ila mazingira yamewakatalia kuwa pamoja. Colins hawezi kujisaidia,
alichojisikia kwa Jelini, hajawahi kujisikia kabla. Jelini alikuja kama
kumtoa kwenye jua kali na kumuweka kivulini. Kabla hajatulia
kwenye hilo huba, wakamrudisha tena kwenye fukuto. Bado moyo unatamani
alicho onjeshwa na Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu huku
akimtizama Kamila. Akajikuta amepotelea mawazoni akimtizama. Bila kutarajia
akajikuta na kumbusu kwenye shavu la juu, maana alilala ubavu. Akajishangaa,
ila kama akafurahia! Akamtizama na tabasamu, kisha akatoka kitandani.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anatoka chumbani kwa Kamila, akasikia shuguli
jikoni, akajua na mama yake atakuwepo. Akamfuata. “Bado Kamila anaogopa tu?”
Akacheka sana akijua anamkejeli. “Wala sitakujibu mama. Umeamka salama?”
“Tumalize kwanza yako.” “Hapana mama. Wewe ni mchokozi tu.” “Mimi tena! Sio
kwamba najali? Nataka kujua hali zenu!” “Huna lolote.” “Au na leo umepitiwa
tena na usingizi?” “Mimi naona wewe unaendelea vizuri.” Akaondoka hapo mama
yake akicheka.
“Mchana nakuja tule wote chakula cha mchana.” Akamsikia
akiongea huku anapotelea koridoni. “We Colins! Si unakikao na kina Simba wewe?
Tafadhali naomba malizana nao, kutulie.
Mimi sitaki kuja kudaiwa usiku usiku.” Akarudi.
“Nitamalizana nao mama, usiwe na wasiwasi. Nimejiandaa.
Sawa?” “Sitaki maneno maneno ya yule mama mpaka kazini, akilalamika tunawadhulumu
haki zao.” “Kila kitu kitakuwa sawa.
Naomba muda nirekebishe. Na hatuwezi kuepuka kulalamika kwao. Hawa watu walizoea kuchota pesa pale hospitalini
bila ya nyinyi kujua wala kufuatilia. Wakajinufaisha watakavyo. Sasa, sasahivi
nimewadhibiti kwa pesa waliyozoea kuchota kiurahisi, nilazima
watalalamika tu. Ila nakuahidi patatulia.” Akamuona amenyamaza.
“Kwa hiyo nije tule wote?” Akamuuliza kwa kumbembeleza. “Nishakuwa
na mipango na mama yako.” Akasikia sauti ya baba yake. “Hiyo mipango yako ...”
“Ya chakula cha mchana, Colins. Naomba usiingilie.” Colins akacheka kwa kusikitika.
“Mbona kama nahisi umedandia mipango yangu?” “Muulize mama yako kama jana usiku sijamwambia kama leo
nakwenda kula naye. Labda akatae sababu anakupendelea wewe.” “Wewe bwana
hutabiriki! Utanifanya nikose ofa ya Colins, halafu uje uniambie umepata
mgonjwa wa dharula.” “Mama Colins!” “Si ubishe sasa? Maana na juzi ilikuwa
hivyohivyo.” “Leo nimekuapia, lazima.
Sasa wewe usikate tamaa. Na umeona jana nimekutoa kabisa na simu nikazima. Siku
nzima mpaka asubuhi mimi na wewe tu. Na wewe bisha.” Kamila akasikia
wakimgombania huyo mama.
“Wewe kuwa na msimamo. Acha kuyumbishwa na Colins.” “Au
tumuulize mwenyewe anataka kwenda na nani!” “Acha ukorofi Colins! Mimi nilishamuwahi.” “Sasa wewe si umtoe dinner?”
“Muulize kama sina miahadi naye na ya dinner huyo.” “Baba! Kwamba
unamtoa lunch na dinner!?” “Si upo naye hapo, muulize abishe.”
“Sasa kwa nini!?” “Hee! Wewe vipi Colins? Mke wangu, pesa ninayo.
Kwa nini kunipangia?” Colins akachoka kabisa.
“Sawa baba. Basi kesho.” “Sasa hapo inategemea na
kitakachozaliwa leo.” “Kwamba na kesho tena unataka kumtoa mchana na
usiku?!” “Wewe una wasiwasi gani?” “Basi mimi kule nakufukuza kazi.”
“Aliyekwambia sitakuja kwenye kliniki zangu ni nani? Wewe tulia. Pengine kesho
utapata kimoja wapo. Au unasemaje mke wangu.” “Mmmh!” Wakamsikia anaguna.
“Mama mwenyewe hana imani na wewe!” “Hiyo imani
itarudi tu. Wewe nipe siku ya leo nitengeneze.” “Basi bwana baba. Ila ikitokea
unapatwa na zile dharula zako, naomba mimi ndio niwe wa kwanza
kujulishwa, niende nikale naye.” “Sasa hiyo ndio akili.” Mzee akasikika
kufurahia hilo.
“Nilijua tu. Hana uhakika huyo! Ikifika mchana lazima
nitamsikia yule msaidizi wake akinipigia simu, amepatwa dharula yupo theater.
Kuna mgonjwa mahututi anatakiwa upasuaji wa haraka. Hapo kuja kumsikia tena
mwenyewe ni jioni!” Mama Colins akasikika.
“Wewe kuwa na imani bwana! Hiyo ni inategemea.
Kwanza haitegemei.” “Si tupo hapa. Tutaona.” “Wewe usijali bwana.
Mchana, utaniona.” Mama Colins akanyamaza, Colins akakubali kushindwa. Ila nia
yao ni kumfurahisha tu huyo mama. Alishanyongea kwa muda mrefu.
Njia Ya Muongo, Huwa Fupi.
Alipofika tu chumbani kwake kitu cha kwanza akafungua laptop
yake kuona kama rafiki yake alimjibu. Akakuta alimjibu na ametengeneza ile video.
Haraka sana akaifungua. Akaitizama na kushangazwa mno. Ilionekana kama
mchana! Mpaka kitu kilichotumbuzwa ndani ya glasi ya juisi ya embe aliyopewa
Jelini kikaonekana bila shida.
Alifurahi Colins akashindwa kujizuia. Akaanza kupiga
kelele akishangilia. “Yes! Yesss!” “Ni nini!?” Mama yake akamfuata.
“Mungu anawalipa watesi wangu. Na safari hii hakuna wa kukimbia hukumu.”
Mzee naye akasogea mlangoni.
Akawasimulia jinsi alivyomuita Jelini kwa mazungumzo,
lakini Love na Kemi wakamuwekea sumu. Hao wazazi walishituka!
Hawakuwa na taarifa. “Haiwezekani Colins!” “Yaani kesi ilishindikana sababu ya
ushahidi tu. Halafu wakili wao akawafundisha na kumuwahi mwenye hoteli eti wao
ndio walipwe! Badala yake yaani wao ndio wakaishia kuwa wahanga na washindi.
Sasa kuna mtu amenisaidia kunitolea giza, angalia walichofanya.” Wote wawili
wakasogea kwenye laptop yake. Wakaangalia mwanzo mpaka mwisho.
Mama Colins akajikuta machozi yakimtoka, mzee amehamaki,
macho mekundi. “Sikujua kama huyu binti wa Simba ndio mbaya wa kiasi
hiki!” “Ila atalipa. Hakika atalipa. Kila siku atakayoishi hapa
duniani, atajuta kuingilia mapenzi yangu na Jelini. Ni heri angefanya
chochote lakini si kunitenga na Jelini. Hakika atalipa.” Kamila na yeye
akasikia vile anavyoapa kwa uchungu.
“Sasa si unakwenda kuwapa pesa ya kumtolea dhamana?
Atalipa vipi?” “Baba!” Colins akaita na kucheka kwa masikitiko. “Yaani hii siku
ya LEO na JANA, nilishaziona kabla
yake. Nishaziishi na nishajua chakufanya. Nikikwambia nimejipanga, jua nimejipanga.”
“Nikikwambia nitakutafutia pesa mpaka zikukinahi! Jua
utapata pesa. Nimejipanga.” “Unataka nifanye nini ili unisamehe Colins?
Nimekosa, na pesa sio nia yangu.” “Ilikuwa nia yako baba. Ndio maana ulinitoa
kwenye ndoto zangu, mipango yangu, na kunifikisha hapa nilipo sasa. Nalipa
garama ya maamuzi yako.” “Najua umenikasirikia hutaki kunisikia. Lakini
mimi kama baba, nilikuwa nikikuwazia mema Colins! Nikikuwazia wewe mpaka watoto
wa watoto wako. Mimi ninayo pesa Colins! Huna utakachoongeza sasahivi kwenye
maisha yangu kikabadilisha hivi nilivyo.”
“Baba mwenye nia njema, anaangalia maisha ya kijana wake
kwenye kila pande. Sio pesa tu na elimu. Ulinitoa kwenye maisha
yangu, kazi yangu nzuri iliyonipa heshima na kuonyesha kipaji changu
kilichotambulika kwenye ile kampuni nzima! Ukaniweka kwenye ndoto zako
wewe na Simba.”
“Ukanitoa kwenye mapenzi ya kweli na kuniweka kwa
mwanamke muovu, akaishia kunitesa kwenye jumba la thamani, na kuniwekea mapepo.
Yote hayo umeyafanya kinyume na matakwa yangu, tena nikikusihi uniachie
maisha yangu na nikakupa ukweli halisi, halafu unasema ulikuwa ukiniwazia
mema!?” Wakaanza wawili hao asubuhi asubuhi hata saa 12 ilikuwa haijafika.
“Ningejua vipi kama Love ni msichana mbaya wa
namna hii wakati alikuwa akinifuata mpaka kazini akilia anakupenda?” “Ungeniamini
MIMI kuliko yeye. Hapo ndio
ningejua unanipenda na kuniwazia mema. Uliamua kuchukua upande wake,
ukamwamini kuliko mimi! Tena mama akiwa anajua undani wetu.
Sikuacha kumshirikisha mama jinsi tulivyokuwa na Love. Lakini wote
mlinigeuka.” Colins akawa ameshakasirika. Ananguruma nyumba nzima na hasira ya
zamani ikawa imesharudi.
“Nimekosa Colins. Nimekosa. Sasahivi nimejifunza, nitaheshimu…”
“Itasaidia nini sasahivi, baba?! Itasaidia nini wakati Jelini anaolewa
na mwanaume mwingine?” Akazidi kukasirika.
“Hivyo Kamila anavyompenda Mike na kumlilia, ndivyo Jelini alivyo kuwa kwangu. Na mimi nilibahatika
kupendwa kama hivyo Mike alivyopendwa na Kamila, lakini mimi mmenikatili.
Mike ameondoka hapa duniani akiwa ameshiba mapenzi ya kweli, lakini
mimi nitakufa nikiwa nadandia mapenzi ya watu wengine!” Kamila
aliposikia hivyo, akaishiwa nguvu kabisa na tumaini dogo lililokuwa limebakia
moyoni likafa kabisa.
“Mmeniweka mahali pabaya. Mmeua ndoto na mipango
yangu. Mama niliyemuamini na maisha yangu ya sirini kabisa, ulinisaliti.
Mkiwa mnajua ukweli. Nawalilia kuwaaminisha, lakini mkaenda kunikabidhisha kwa shetani
huyu ili anitese?”
“Colins, nimekosa. Nimekosa. Ila naomba ukumbuke jambo la
mwisho. Yote nimefanya kwa sababu nakupenda, na nakuwazia
mema. Najua sasahivi huwezi amini, na haitaleta maana tena, lakini usisahau
hilo. Habari za Jelini kwangu zililetwa na uthibitisho kabisa. Muulize
mama yako. Zilikuwa na uthibitisho ambao na mimi ilibidi kufuatilia,
nikagundua kwa asilimia 90 niliyoambiwa ni kweli. Muulize mama yako, kama
sikuelekezwa mpaka baa alizokuwa akishinda Jelini na mimi kwenda kuuliza na
kuambiwa ni kweli hapo ndipo maskani yake usiku kuchwa.”
“Huyo alikuwa Jelini wa zamani. Na alikuwa bora
Jelini aliyekuwa akishinda baa, alijawa upendo. Mwaminifu.
Si malaya kama Love ambaye anashinda kanisani huku analala na
wanaume hovyo na kuwaleta mpaka ndani ya chumba chetu. Roho yake mbaya. Anajali
maslahi yake tu.” “Ningejuaje yote hayo?” “Kwa kunisikiliza mimi kwa
sababu mimi ndiye niliyekuwa kwenye maisha ya hao wanawake wote wawili.”
“Nikawafahamu kwenye ngazi ya mahusiano ya kimapenzi
lakini si wewe uliwafahamu kwenye ngazi ya ubaba mkwe, wanajionyesha
kwako kwa kadiri wanavyojua wewe ungetaka kuona.”
“Umenikosea baba. Umeniachia donda la
maisha. Nitakufa nikiwa sijaonja mapenzi ya kweli. Nitakufa nikiwa sijui
kuishi na mwanamke atakayenipenda kwa dhati mimi kama Colins, na mimi nikaacha
historia ya kwanza na nzuri kwa mwanamke. Hakuna mwanamke atakuwa na kumbukumbu
zangu nzuri mimi nikiwa wa kwanza kwake, nitaishia kufananishwa kiwango
changu na wanaume wengine waliopita kwenye maisha yao. Na hapo naweza kupungua
sana, nisifikie kiwango, akaishia kuishi na mimi kwa kunivumilia akikumbuka
mapenzi ya kwanza na mimi nikiwa ni matokeo ya kukosa kwake!”
“Jelini anakupenda Colins. Alikiri.” “Unazungumza nini
baba yangu? Jelini anaolewa na mwanaume mwingine akijua sijawahi mpenda
yeye kama Love. Na hiyo ni wewe umesaidia kuiweka akilini mwake.
Anachojua ananipenda sana ila mimi sijawahi kumpenda.”
“Si mara moja nimemuacha Jelini akiwa amejiandaa kabisa,
ananisubiria, lakini wewe ukalazimishia niende kwa Love. Si usiku mmoja
amelala akilia kwa ajili yangu. Siku mmekuja kwangu na kina Love kuniwekea
mapepo, na kunipoteza ufahamu wangu kabisa, ndio siku nilikuwa nakwenda
kumuweka sawa, nijirudi, nimuombe nimuoe.”
“Na yote hayo mabaya niliyokuwa nikimfanyia, lakini
Jelini alimtuma James kuniambia, yupo tayari kuwa na mimi mpaka nijifunze
kumpenda, akidhania simpendi. Aliandaa siku hiyo, akanipikia kabisa,
akinisubiria. Na mimi nilishajipanga na kumuomba James aniandalie vikao vya
harusi kwamba namuoa Jelini bila nyinyi, nikijua mkija mfahamu Jelini, mtampenda
tu. Lakini mkanivamia, mkaniweka mateka, na ndio mkagongelea msumari
wa mwisho kwenye kufunga mahusiano yangu na Jelini.”
“Jelini anakumbukumbu za Colins aliyempenda,
lakini sijawahi mpenda! Na japokuwa alikuwa akiona picha zangu na Love
alizokuwa akizisambaza, mimi sina ufahamu, lakini alikuwa akinisubiria
muda wote mpaka akakata tamaa kabisa akiamini kweli sijawahi mpenda,
anasubiria penzi ambalo si lake!”
“Mmenifungia humu ndani, mmeshindwa kumtaarifu, mnakuja
kumtaarifu mwishoni kabisa! Lakini pia, kwa vile anavyonipenda yule msichana,
nikiwa nipo kama kinyago, sitizamiki, nina madonda mwili mzima,
ile kuniona tu, akasahau kabisa kama tayari alishatoa ndiyo yake kwa
Ezra. Akasahau kila kitu akawa kama ameokota lulu! Kwa mabaya yote hayo,
alikuwa tayari kuniuguza kwa mapenzi yote, yeye mwenyewe mpaka
alipokuja kukumbushwa yupo Ezra.”
“Niambie baba. Nakuja kupata wapi mwanamke wa kunipenda
kwa namna hiyo kama sio nakuja kuishia kwa mwanamke aliyejawa mapenzi ya
mwanaume mwingine mimi nikiwa nalinganishwa kuona kama nafikia hicho
kiwango? Yaani mimi nitaishia kuwa kwenye mahusiano ya kujithibitisha
mpaka kifo changu!” Pakazuka ukimya hapo, wote wakajisahau kama ni waajiriwa.
Mwishoe mzee akamalizia akiwa kama yupo mawazoni. “Ni
kweli nimekukatili Colins. Nimekukatili vibaya sana.” Akamalizia hivyo
na kuondoka. Mkewe naye akafuata nyuma. Wakamuacha hapo chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ø
Giza limeshajitenga na nuru. Kukiwa na tumaini la kutoka rumande kwa
dhamana, uovu wake na Kemi aliyeponea chupuchupu kuwa naye lupango, wawekwa bayana.
Love yu mgonjwa wazazi wanahangaika
kumtoa akatibiwe. Akiwa na kesi ya wizi, shitaka
la kusudio la kutaka kuua, linamuwinda.
Colins ameapa kumlipiza kisasi mpaka ajute. Ameshamuweka Chris mtetezi wao upande wake, tayari kulipiza kisasi cha maumivu.
Ø
Akiwa anapambana na yote, huku kwa Kamila ni kama anakosa. Amefika mwisho, na yeye akiwa
na uhakika Colins hatakuja kumpenda kama Jelini. Na huku nako atakuja kumbuka
shuka kumekuchwa!?
Itakuaje?
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment