Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 22. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 22.

‘Ingekuwa ni amri yangu, kwa hakika usingepita unakopita sasahivi. Lakini nimeshindwa kukulinda Jelini. Pole na samahani. Ila jua nakupenda na nakutakia mema. Naamini utapata ulichokuwa ukikitafuta na mimi kushindwa vibaya sana kukupa. Unastahili mazuri Jelini, kwa kuwa moyo wako pia ni mwema kwa kila mtu. Utafanikiwa tu. Na nakutakia kila la kheri.’ Akamtumia huo ujumbe na kuongeza mwingine.

‘Utakapofika mahakamani, usiogope. Naamini kila kitu kitaenda sawa. Narudia tena kuomba msamaha kwako Jelini. Nisamehe kukupitisha hapo. Nia ilikuwa njema. Sikutaka TUACHANE tu bila maelezo. Unastahili kila jema, lakini walio kinyume yangu wameishia kukuumiza wewe, wasijue wananiumiza mimi zaidi. Moyo wangu umpweke, nikijua nakukosa Jelini. Lakini kwa upande mwingine, nafurahia unaishia pazuri. Kila la kheri.’ Akatuma.

Baada ya muda mfupi akashangaa Jelini amemjibu. Hakuamini. ‘Colins, kwa hakika. Kutoka ndani ya moyo wangu, nimekusamehe na samahani kukutupia lawama wewe moja kwa moja. Najua na mimi kuna sehemu nilikosea kwa kuzembea. Nawajibika kukuomba msamaha. Sitilii mashaka juu ya mapenzi yako kwangu, Colins. Japo nahisi ungeongeza juhudi kidogo tusingekuwa hapa tulipo. Ila naomba kukushauri kitu.’ Akaendelea kusoma kwa shauku.

‘Inaweza ikawa ndio ujumbe wangu wa mwisho kwako, lakini amini nataka usiishi mpweke. Hustahili adhabu ya Love.’

‘Usikubali akakuacha mpweke. Utakuwa umempa nguvu kubwa sana ambayo hastahili. Unastahili kupendwa na kuwa na furaha. Pale tulipopita mimi na wewe iwe shule yetu.’

‘Popote utakapoamua kufungua moyo wako, usirudie makosa tuliyofanya nyuma. Nakuhakikishia Mungu hajaishiwa na anakuwazia mema Colins. Usifunge moyo wako. Utakuwa sawa. Unaweza usiamini, lakini bado upo moyoni mwangu, na nakuombea mema na mazuri. Nataka uwe na furaha Colins. Hata kama hujisikii kuchukua hatua, tafadhali fanya kwa ajili yangu. Daima nitakupenda Colins.’

~~~~~~~~~~~~~~~

Colins alimaliza kusoma akajikuta machozi yamefika kidevuni. Akajifuta kwa haraka sana huku akiangalia kulia na kushoto kama kuna aliyemuona.

Jelini amezungumza naye! Amemjibu! ‘Daima nitakupenda Colins!’ Alijawa furaha! Akabaki akirudia ujumbe wa Jelini asijue muda unazidi kwenda. Ofisini hajaingia! Yupo ndani ya gari na mrembo Kamila amelala. Akatulia hapo mpaka Kamila aliposhituka kutoka usingizini.

“Colins! Mbona mpaka pamepambazuka kabisa!?” “Nilitaka ulale kidogo. Nilijua hukulala vizuri usiku.” “Sasa si tutakuwa tumechelewa kazini?” “Usijali. Nilitaka ulale vizuri ili uweze kufikiria vizuri unapozungumza na Luca. Sasa unataka kwenda jikoni au kwa leo utulie uendelee kesho? Maana tutatoka kama  kwenye mida ya saa 6.” Akaangalia saa. “Acha niende hata kwa muda mfupi tu.” Ndipo wakatoka garini sasa.

Mfupa Uliomshinda Fisi.

Akiwa ofisini akaona simu ya Noah inaingia. Akapokea akiwa na mshangao. Kwanza bado ilikuwa asubuhi, na si kawaida yake kumtafuta mida hiyo. Kwanza mida hiyo kwa Noah ni kama usiku wa manane, anakua amelala kabisa. Akapokea lakini hakumsikia akizungumza. Akaita mara kadhaa mpaka akamfanya Ezra aache shuguli zake amtizame.

“Naona imejipiga. Wakati anataka kukata akasikia sauti ya Hope kama anafoka! Akaongeza sauti na kuweka kwenye spika. Wote wakabaki kusikiliza. Wakaangaliana kama kuulizana ni wapi! Na nani! Na kwa nini mida hiyo! Ikawavuta masikio zaidi ndipo wakapata majibu yote.

Alikuwa akimpandishia Emelda kwa jazba haswa. Mwishoe wakamsikia Emelda akimwambia, “Unachofanya hapo ni kunipotezea muda, Hope.” “Sio wifi tena!? Mnafiki mkubwa wewe! Mchawi na mwanga wa mchana kweupe wewe.” Alishituka Junior! Akatamani iwe ndoto.

“Nakusaidia tu Hope, unajiumiza wewe mwenyewe. Hayo matusi unayarudiarudia tu. Na kukusaidia zaidi, huna tusi jipya ukanitusi ambalo sijawahi kutusiwa. Nimekua nikizungukwa na watu wa aina yako kuanzia nina akili zile za kuelewa za kitoto mpaka sasa. Huna jipya, ila unajiumiza tu wewe mwenyewe na kunipotezea muda wangu ambao sina. Naomba nipishe nimalizie shuguli zangu, nitoke hapa nikamuone mama yangu hospitalini.” Akasikika Emelda kwa sauti ya kutulia tu.

 “Esther yupo sahihi. Ndio amekuja kukuongezea uchawi! Amekutana na nguvu za Mungu yamemrudi, mnajidai mgonjwa!” Hapohapo Junior akachukua funguo za gari akatoka akikimbia.

Na Ezra naye akampigia Junior, kisha akamwambia asikate. Akampigia na Hope. Ikaita mpaka ikakatika. Akampigia tena na tena ndipo akapokea.

“Hicho unachokifanya hapo kwa Emelda ni fujo, na mimi binafsi sitakuruhusu.” “Ana…” “Hapana Hope. Junior si mtoto mdogo kiumri wala kiroho. Ana nguvu za Mungu zinazomlinda, wala malango ya kuzimu hayatamshinda, labda uniambie leo kama unaamini kama uchawi una nguvu kuliko Mungu.” Akataka kujibu.

“Sina muda wa kubishana na wewe, ila nakuja pointi ya pili. Kwa kuwa Junior sio mtoto mdogo kwamba amerubuniwa na Emelda, ni chaguzi yake mwenyewe, na mimi ni shahidi wa hili, basi, mtafute yeye Junior ndio umpe hayo matusi. Ila iwe mara yako ya kwanza na ya mwisho kumtusi Emelda. Umesikia Hope?” Ezra akaendelea.

“Hicho kikundi chako na Esther mkakifanyie nyumbani kwa Esther, lakini sio hapo alipo Emelda, tena kwa kipindi hiki kigumu kwake. Anamuuguza mama yake, na bado anamajukumu ya napo nyumbani akiwa mama mchungaji hayupo, halafu bado anamdogo wake wa kumsimamia.”

“Sasa basi, baada ya dakika 5 kama bado utakuwepo hapo, mimi mwenyewe nitakuletea polisi na kukushitaki kumvamia Emelda. Haya, ondoka na usiongeze neno jingine kwa sababu ukikiuka tu, shitaka lako linakufuata. Siku njema.” Kimya. Simu ikakatwa.

Hapohapo Ezra akampigia Noah. “Naomba weka kwenye spika na Hope asikie.” “Tayari.” Noah akajibu. “Sasa nichukulie video ya Hope akiwa hapo na kila neno atakalozungumza. Kisha nitumie sasahivi. Nitaanzia kwa mwajiri wake, anayempa ruhusa ya kuzunguka kwenye majumba ya watu asubuhi asubuhi akitukana badala ya kuwa kazini akifanya kazi, kisha polisi.”

“Mbona tayari! Nilikuwa namrikodi kuanzia aliponiamsha kwa kelele zake. Hapa namtumia mchungaji wake, Esther shoga yake ili asije ruka maneno yote aliyosema ameambiwa na Esther, kisha kwa yule mwanamme wake, ajue anajiingiza kwa mwanamke wa namna gani.” “Uchonga…” “Yaani hata hapa unaponijibu, jua na kurikodi.”

“Umepatwa nini wewe Hope!? Umechanganyikiwa wewe?” Wakamsikia Junior upande wa pili. “Kama kuna nguvu za giza je?” “Sasa wewe shida yako nini? Ninayelogwa si mimi ambaye ulisema hunitaki mimi na misingi yangu ya maisha? Kinacho kuuma wewe ni nini? Wewe si umesema unaye mwanamme wako na mpo serious? Sasa kwa nini wewe na Esther hamuangalii ya kwenu mnahangaika na yangu?” “Esther…” Kabla hajaendelea akamuwahi.

“Mimi sijali Esther amekwambia nini. Ila kama unadhani Ezra anakutania, basi nikukute hapo. Na iwe mwisho kuzungumza na Emelda hivyo. Usirudie kumtukana wala kumpandishia sauti. Huyo si mchumba tu. Mke wangu na mama wa watoto wangu. Hakuna mtakalosema nikaacha kumuoa Emelda. Sijaribishi kwake. Nimemaliza. Hilo mfikishie Esther na uongeze kuwa sina shida ya kulogwa na Emelda. Mimi mwenyewe napenda na nataka aniloge zaidi. Kama nyinyi wawili mna tatizo naye, nifuateni mimi. Lakini yeye mwiko. Umesikia Hope?”

“Kwanza toka hapo. Huyo Emelda ana mambo mengi ya msingi, unampotezea tu muda. Anategemewa kuongoza hiyo nyumba mpaka mama arudi na bado ana mgonjwa hospitalini. Noah?” Akamuita mdogo wake.

“Nipo bro.” “Hawa wananichezea kupita kiasi na wamevuka mpaka. Leo ndio mwisho kuzungumza hivyo na Emelda, siwapi nafasi ya pili. Na Hope utakuwa fundisho kwa wote. Piga simu getini wamshikilie mpaka nitakapo kuja na polisi. Nakaribi…” Kabla hajamaliza, Hope akakimbia kama mwizi. Wakamsikia Noah akicheka kishabiki haswa. “Nakurikodi Hope. Video yako utaipata. Na kama umeni block utaikuta kwa mashoga zako, mchungaji wako, wazee wako wa kanisa na kwa yule mwanamme wako.” Wakamsikia akiongea akicheka kwa kumdhihaki Hope.

Kila Msingi, Hujengwa kwa garama.

Kwenye mida ya saa 6 mchana Colins akaacha shuguli zake zote, wakawa wanatoka hapo kuelekea kwa huyo mwanasheria akimsindikiza huyo Kamila kupata ukweli juu ya Mike. Alikuwa ametulia garini. Baada ya kuendesha kidogo akamuita Colins taratibu. “Colins!” Akamwangalia. “Asante kuwa na mimi mpaka sasa. Wewe ni wa kuaminika. Unasimamia ahadi zako hata kama nakugarimu muda wako muhimu.” “Usijali. Naamini kila kitu kitakwenda sawa.” Akatulia.

Walifika ofisini kwa huyo mwanasheria wakashangaa kukuta wazazi wake wanasubiria nje. “Si mmesema hamtakuwepo?” “Tumeona tuwepo na sisi ili Kamila binti yangu asijisikie mpweke.” “Kweli mama?” “Umeshakuwa mmoja wa familia Kamila mwanangu. Umetupa nafasi ya heshima kuwepo nyumbani kwetu, umeshakuwa binti yetu. Tutasimama na wewe katika kila hatua ya maisha yako. Usiogope.” Colins hakuamini.

 Mama yake alionekana kama aliyepata mapumziko haswa. “Na kazini?!” Akauliza akimtizama baba yake. “Mimi nikitoka hapa nitakwenda. Kuna wagonjwa lazima nikawaone. Ila mama yako atapumzima leo. Sasa hivi usiwe na wasiwasi mpaka hili likae sawa. Acha tuongeze uzito hata kwa hao kina Luca wajue kuanzia sasa, Kamila hayupo peke yake. Ana wazazi wanao msimamia. Hawaruhusiwi kumchezea tena.” “Asante baba!” Colins akashukuru asiamini. Wakawa wamejirudi wakati muafaka akiwa kweli anawahitaji.

“Baba yako aliona ukitokea tu wewe, Luca anaweza asione uzito. Akahisi ni kijana tu ambaye unataka kujinufaisha na Kamila. Asione uzito.” Akachomekea makusudi kama kumsogeza baba yake karibu naye akimpa sifa na yeye asamehewe. “Sikuwa nimefikiria hilo! Nafikiri yupo sahihi. Itaongeza uzito. Asanteni.” Wakakaribishwa ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda mfupi Luca na dada yake wakawasili na wao. Wakasalimiana na utambulisho. “Hawa wapo hapa kama wazazi wa Kamila.” Wakashangaa sana. “Huyu mtoto si alisema ni yatima huyu!?” Dada mtu akauliza kwa mshangao. “Ni yatima ndiyo, lakini hawa ndio wazazi wake kwa sasa. Ndio wanao ishi naye kwa sasa, na ndio wanao mtunza. Wanadhamana naye. Kwa chochote tutakachozungumza hapa, wanaruhusiwa na Kamila kuwepo na kusikiliza.” “Hata kuhoji maswali.” Akaongeza Kamila mwenyewe.

 Wakamwangalia. “Namaanisha na wao kama walezi wangu wanaruhusiwa kuuliza maswali.” Wakakubaliana. “Haya, Kamila karibu.” “Mike yuko wapi? Nataka kujua walipomficha. Hilo tu, mimi sina shida ya pesa ila Mike.” “Acha niwaambie ukweli. Hilo tu ndio pona ya huyu msichana. Lasivyo, nilitaka kumfungulia mashitaka ya kumuua Mike.” “Mimi!?” Kamila akashangaa sana.

“Naombeni tu mnisikilize. Eti Mike awepo nyumbani kwangu mpaka usiku. Akiwa mzima kabisa. Na alikuwa naye huyu. Halafu eti baada ya masaa machache alfajiri yake nipigiwe simu eti Mike amefariki! Tena inashukiwa kama amenyweshwa sumu! Hata kama ni nyinyi jamani, mngefikiria nini, kama si mtu wa mwisho kuwa naye ndiye aliyempa hiyo sumu!?” “Mimi nataka kujua Mike alipo. Na msinidanganye. Wamesema mimi ni kama mkewe.” Wote mpaka upande wa kina Colins na huyo mwanasheria wakashangaa kwamba hasikii au!

“Mike amezikwa makaburi ya Kinondoni.” “Mnadanganya. Mimi nilikuwa naye hospitalini. Tena nikamuaga kabisa kuwa nitarudi. Akaitika kabisa.” Akawasimulia ilivyokuwa. “Eti narudi, wananiambia Mike hayupo! Awe ameenda wapi kama si wamemchukua hawa?”

“Mimi nilipigiwa simu kuwa Mike amefariki na ndani ameanza kuharibika. Ikabidi kwenda kushuhudia nikiwa siamini. Walichoniambia ni alikuja na msichana pale, akamuacha. Hakika roho yangu ikaniuma sana. Nikajua huyu alimtelekeza kwa sababu zake mwenyewe. Hayo mengine sikuyajua mimi!” Luca naye akaongeza.

“Inavyoonekana kwa taarifa za hospitali, Kamila aliporudi hospitalini siku ile akapewa taarifa za kifo cha Mike, alishituka sana na kupoteza fahamu kwa karibia siku tatu.” “Hayo ndio nayasikia leo! Ila yeye aliporudi nyumbani akaanza fujo kwelikweli kama mwehu, anamtafuta Mike. Ndio angalau akaniaminisha sio yeye aliyemuua Mike.”

“Na ilinibidi kumzika kwa haraka. Muulize dada hapa. Mike alishaanza kunuka mapema sana, mpaka tukashangaaa ni nini alinyweshwa! Maana ni kama aliharibika kila kitu ndani! Hatukuwa na sababu ya kumchelewesha ila kumzika.”

“Muongo Luca. Anadanganya kwa sababu hampendi Mike.” “Wala sitadanganya. Mike aligeuka mpinzani na kuamsha hasira ndani yangu. Hata nyinyi wenyewe fikirieni jamani! Mimi ndio mtoto wa kiume mkubwa kwa mzee wangu. Eti leo mtu baki ndio apewe mali za familia ndio aongoze! Hata kama ni nyinyi mngefurahia kweli?” Wote kimya.

“Lazima kama mwanadamu nichukie. Lakini si kwa kumficha! Muda wote huo! Miaka miwili! Namficha mtu kama Mike, ili iweje? Kama wewe huamini twende ukaone kaburi lake.” “Nitajuaje kama aliyepo humo ni yeye hamdanganyi? Nyinyi mna roho mbaya sana.” “Basi tutakuonyesha picha zake za siku ya mazishi yake, uangalie.” Akanyamaza, wakamuona anaanza kutetemeka. Amebadilika amekua mwekundu mpaka masikio.

“Kamila, una swali jingine au ombi jingine?” “Naomba uthibitisho kama kweli Mike amefariki. Nafsi yangu inakataa jamani! Mike alikuwa mzima kabisa. Sijapitia naye popote tokea tunatoka nyumbani kwa Luca au kwamba tulikula kwengine! Kwanza ilishakuwa usiku mwingi. Eti tunafika nyumbani ndio anaanza kulalamika tumbo, wakati alikuwa mzima kabisa! Moyo wangu hauamini.” “Dada, mtolee picha na pia tutakupeleka kwenye kaburi lake.”

“Kingine, naomba waambie wanipe pete yangu ya uchumba alinivalisha Mike na gari alinipa mimi zawadi. Ni haki yangu, Luca akanipokonya. Ni hivyo tu ndio nataka.” “Mimi sijui ni nini kimetokea jamani! Ile pete ilipotea kwenye mazingira ya ajabu, sijui ilikuwaje! Mara nilikuwa nayo, mara ikapotea.”

“Haya, ile gari yenyewe nusura imuue Robi, mwanangu wa kwanza. Alipata ajali mbaya sana. Gari imeharibika, haijasalia hata kioo! Imefanya kukusanywa na kutupwa. Kwa hiyo hapa nilipo sina hiyo pete wala gari. Ushahidi huu hapa.” Akatoa simu yake na kuanza kuwaonyesha picha za ajali aliyonusurika kijana wake. Wote wakashangaa.

Kamila akazidi kulia. “Na ningesema nimlipe, lakini hizo mali zimekuwa kama na mkosi! Muulize dada. Kila siku ni hasara, mpaka biashara nakaribia kufunga. Naendesha kwa mkopo. Sina kitu. Hata kama atadai mali, hakuna. Labda ile nyumba.” “Mimi sina shida na ile nyumba.” Kamila akajibu akilia na kushangaza wote. Hataki nyumba!

Ila mama Colins akaingilia. “Nyinyi mlimfukuza yatima, tena kama mke wa kaka yenu. Halafu ni kama mlimdhulumu Mike maisha yake, Mungu naye akatoa mkono wake kwenu ndio maana na mali na zenyewe zinaondoka.” “Kwa hakika mimi sijamuua Mike. Na Mungu ni shahidi. Tulikuwa hatuelewani, lakini si kwa kumuua.”

“Ila mimi inanishangaza jamani! Japokuwa sikuwa karibu na Mike, na mimi kwa sababu kama za Luca tu, lakini  kwa jinsi alivyokuwa Mike, nani atakuwa amemuua!? Yule kiumbe mbali yetu sisi kumchukia sababu ya kuwa kiongozi wetu kwa mali za baba yetu, jamani Mike alikuwa mwema. Hata Luca katika hilo atasema.” Dada mtu akaongeza kama akiwaza.

“Wala sitabisha. Mike alikuwa mtu mzuri. Anaweza akafanya jambo mpaka ukashangaa. Sidhani kama alikuwa na maadui yule. Kwa hakika sijui nini kilimpata Mike! Pengine iwe sumu alipewa muda mrefu ikaendelea kumuharibu taratibu mpaka usiku. Ila kusema kuna mtu anaweza kuweka uadui naye! Si rahisi. Kwanza mwenyewe utashindwa kwa ile haiba yake Mike. Kuna jinsi Mungu alimuumba, ngumu kuweka uadui naye.” “MmmH!” Dada mtu akaguna kwa kushangazwa kabisa. Wote wakabaki kimya kwa muda wakiwaza.

Mwishoe Colins akavunja ukimya. “Tafadhali naomba tuone picha za Mike. Uthibitisho kwa Kamila.” Ndipo wote wakaonyeshwa picha za siku ya mazishi ya Mike. Kuanzia yupo kwenye jeneza mpaka anazikwa. Kamila alilia, alilia sana. Ikawa ndio kama ukweli ukamuingia, kuwa Mike hayupo duniani. Akalia sana.

Safari ya makaburi ya Kinondoni ikaanza ili waonyeshwe mahali walipoweka mwili wa Mike. Wakafika ila Kamila akilia vilevile. Wakaonyeshwa kaburi lake. Lenye jina lake kamili. Kamila akazidi kulia akilishika na kurudia kusoma. “Jamani Mike!” Akaendelea kuomboleza kwa uchungu akiwa amepiga magoti hapo kaburini. Wote kimya, hamalizi! Muda unazidi kwenda.

Luca akaaga kuwa inabidi arudi kazini. Akaondoka na dada yake. Kamila bado analia. Alikuwa hawezi hata kusimama kwa kulia. Mwanasheria naye kazi yake ikawa imeisha. Akaondoka. Kamila bado analia ameshikilia kaburi anamuita Mike kama amsikie.

Mwishoe Colins akambeba na kumuweka kwenye gari ya wazazi wake. Akawaomba warudi naye nyumbani. “Mimi nilazima nirudi kazini. Ila nitawahi kutoka. Nakuomba mama, ukae naye mpaka nitakaporudi.” Mama yake akakubali maana mzee alikuwa na yeye anakwenda kazini. Wakarudi nyumbani, Colins kazini.

~~~~~~~~~~~~~~~  

Mama Colins akaanza kazi ya kumbembeleza huyo Kamila masaa kwa masaa mpaka akalala hapo kwenye chumba alichopewa kwenye hiyo nyumba yao. Akamuacha alale akatoka taratibu. Mumewe alishaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~  

Safari ya Mike hapa duniani imeisha, Jelini haonyeshi kurudi nyuma. Ezra ni mume kwa hakika. Maisha lazima yaendelee.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment