Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 23. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 23.

Mbio za Sakafuni, zimeishia Ukingoni. Huku kwa Colins wakati anaingia getini walinzi wakamsimamisha, akashangaa kumuona Chris pale. Amepoa kuliko maelezo. “Tafadhali naomba tuzungumze.” “Unataka nini Chris?” “Tunaweza pata faragha?” “Ni muda wa kazi sasahivi.” “Nafahamu. Isingekuwa muhimu, nisingekuja mida hii.” Colins akafikiria, akawaambia wamruhusu aingie.

Walipofika sehemu ya kuegesha magari, akamuwahi. “Huruhusiwi kuingia ofisini kwangu hata na walet. Nikimaanisha acha simu yako, saa ya mkononi na vingine vyote kwenye gari yako, ndipo uingie. Kama hutaki, basi.” Chris hakuamini ila kutii.

Akasimama wima akimtizama mpaka akatoa kila kitu mifukoni na kuweka kwenye gari yake. Alipohakikisha mifuko yake ni mitupu ndipo wakaongozana mpaka ofisini kwake.

“Nikusaidie nini Chris?” Maana alikaa kwa kunyongea kama mgonjwa. “Nimeamua kuacha kuwawakilisha kina Kemi na Love.” Colins akabaki akimtizama. “Nimeona nijitoe.” Kimya. “Ndio hilo tu. Nilitaka kukutaarifu.” “Unanitaarifu mimi kama nani na ili iweje?!” Colins akamshangaa kabisa.

“Sitaki kujiingiza kwenye vita isiyo yangu.” “Hilo umeligundua lini?!” “Nimeona heri nijitoe.” “Unanipotezea muda wangu Chris. Maana hichi unachokifanya hapa ni fujo na si sehemu yake.” “Nataka tuwe ukurasa mmoja mimi na wewe.” Alimuudhi Colins, mpaka akabadilika rangi.

“Unataka kuwa ukurasa mmoja na mimi wakati unalipwa kuniangamiza mimi na watu wengine wasio na hatia!?” Akamuuliza kwa ukali kabisa. “Hivi unajua mwanamke uliyemuweka kizimbani leo, na kumuhoji, pengine kama mhalifu, ndiye aliyekuwa mwanamke wangu? Ilikuwa nimuoe mimi, halafu hao unao watetea wakanitenda? Walinigeuza kichaa kabisa natembea barabarani kama tahira!”

“Wamemnywesha sumu mwanamke wangu. Ndio walikuwa wakigongelea msumari wa mwisho kabisa wa kunitenga na mwanamke wangu. Leo unawatetea kwa kuwafundisha kumdhulumu mtu asiye na hatia! Alianza biashara yake pengine akiwa hana kitu! Amefika alipofika, unamdhulumu bila hatia huku ukitupia mbali tuhuma za kunyweshwa sumu mpenzi wangu! Halafu eti unakuja kwangu unaniambia unataka kuwa ukurasa mmoja! Halafu eti njia yenyewe unayotumia ni kujitoa kwenye ulichoanzisha na kukichochea!?”

“Inawezekana nimetumia neno lisilo sahihi. Lakini nia ni kurekebisha. Mimi sikuyajua hayo yote.” “Hukuja hapa nikakwambia unao watetea wanakutoa muhanga? Ukatoka hapa ukinitusi?” “Kwanza kesi ya leo nimeomba iairishwe mpaka tujipange mimi na wewe.” “Acha kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Ondoka Chris. Toka ofisini kwangu.”

“Nisikilize Colins. Niliahirisha kesi na pia nimejitoa kuwa wakili wao. Sasa kwa nini tusijipange upya?” “Unajipanga vipi na mimi wakati umeanzisha jambo halafu umejitoa!? Yaani unaharibu halafu unakimbia!? Wewe ni mtu wa namna gani Chris!? Utakuwa ukikimbia uharibifu wako mpaka lini?” Hapo akamjumuisha mpaka Zulfa.

“Nimekubali kosa. Ndio maana nipo hapa. Niambie basi vile unataka nirekebishe, nitafanya.” “Unauhakika?” “Ndio maana nipo hapa. Sina sababu ya kukufuata kama si kutaka kutengeneza.” “Anza kwa kurudi kuomba kuwa wakili wao.” “Haiwezekani Colins! Nimetoka kuwaambia sitaweza kuwawakilisha tena.” “Nguvu ileile uliyoitumia mwanzoni kuwaweka upande wako, ndio uitumie tena kurudi. Unanielewa Chris?” Akabaki ameduwaa.

“Chris?” Akamuita kwa ukali. “Acha mimi nisiwawakilishe. Halafu niwe na wewe nikusaidie mbinu zaku…” “Toka ofisini kwangu. Unanipotezea muda. Sina shida na msaada wako. Toka.” “Sawa. Sawa Colins. Tufanye nimefanikiwa kurudi kuwawakilisha. Ndio inakuaje?” “Simamia haki! Swali gani hilo?!” Akawa hajaelewa.

“Unanielewa? Anza kusimama kama mwanaume, wajibika. Acha kukimbia. Tengeneza uharibifu wako. Kila uliyemdhulumu, mpe haki yake. Sitaki unitetee. Sitaki upendeleo. Simamia haki kisheria. Simama ukiwa unasikiliza na kutetea haki, hilo tu. Acha uonevu kwa watu wasio stahili. Rudi kazini.” “Lakini kuna mambo ambayo yameshatokea, siwezi kurekebisha moja kwa moja.” “Kwa hiyo unataka mimi niache kazi zangu, nikufundishe jinsi ya kurekebisha uozo wako?” Kimya.

“Tafadhali nipishe nifanye kazi. Na sitaki umtese Jelini mahakamani kwa maswali yatakayo muumiza. Kwanza mpaka sasa unamtesa kwa kuendelea kumkutanisha na maadui zake wanao mchukia bila sababu! Unamfedhehesha na kumpotezea muda. Acha kucheza na haki za watu, Chris.” Akazidi kupandisha hasira.

“Yaani unatetea watu waliokuwa wamekusudia kumuua! Wauwaji wale ndio unawapongeza kwa kuwahonga mamilioni ya pesa za mtu anayejinyima kufanya biashara yake! Unawalipa kwa kufanikiwa kumnywesha sumu mpenzi wangu! Hakika toka Chris. Toka.” Akasimama kabisa na kumfungulia mlango.

“Basi nipe muda wa kutengeneza. Naomba tusiende mbali. Mimi mwenyewe nitatengeneza kila mahali. Kote. Makosa haya na ya nyuma pia.” Akamuelewa kuwa anamaanisha hata kwa Zulfa. “Nipe muda. Na pia muandae basi hata wakili wa upande wenu! Yule jamaa hajui kazi. Hakuna mtu atanielewa mahakamani, nikishindwa na mtu kama yule. Hana uzoefu. Angalau kuonekane hata kama ipo kesi nzito inayoendelea na ndio kushinda kwenu.”

“Ninachoomba kama kweli narudi mimi kuwawakilisha, basi kuwepo na mazingira mazuri ya kesi. Angalau kuonekane kuna kesi kwelikweli. Ajiandae. Ni hilo tu. Mengine nitajua mimi.” Akabaki amemshikilia mlango. Akatoka. Lakini akawa amemuelewa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alipotoka na kujiridhisha yupo mwenyewe, akamtafuta rafiki yake aliyekuwa amesoma naye zamani, ila yeye alikuwa mmarekani, anafanya kazi kama alizokuwa akifanya zamani na kina James, ila nchini marekani.

Akamtumia ile video, na kumuomba kama anaweza kuisafisha ili ionekane vizuri zaidi. Akamjibu kwa kumuuliza swali. ‘Ina uharaka wa kiasi gani?’ ‘Yesterday, na ni muhimu sana.’ ‘Nipe muda.’ ‘Nashukuru.’ Colins akamjibu akijua ataifanyia kazi tu. Ndipo akarudisha akili kazini.

Huku Nyumbani kwa kina Colins

Wakati yupo jikoni, akimsaidia msichana wake wa kazi kuweka sawa mlo wa jioni, maana siku hiyo hakwenda kazini, Kamila akaamka na kumfuata. “Vipi mama?” “Naendelea vizuri.” “Kaa hapo nikupe kitu kidogo ule.” Akakaa na kunyamaza. “Pole mama. Pole sana. Utakuwa sawa, usiogope.” “Nashukuru kunisaidia kujua ukweli. Angalau sasahivi nitajua moja. Kuliko vile nilivyokuwa nikihangaika kumtafuta nikijua wamemficha.” “Utakua sawa. Pole.” Akampa chakula maana hakuwa amekula.

“Sijisikii kula kabisa. Colins amerudi?” “Bado.” Akanyamaza. “Jitahidi ule kidogo. Itakusaidia.” Akamuwekea chakula, akaendelea na shuguli zake, akimuacha ale, hapohapo jikoni si mbali na yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Nikuulize swali mama?” “Karibu.” Akamuona amesita. “Ni nini?” “Jelini ni mzuri sana?” Akashituka sana, hakutegemea hilo swali zaidi kwa wakati huo! Ila akajikaza. “Kwa uzuri, kwa kweli ni mzuri sana. Halafu nadhifu mno. Ukimuona kwa haraka unaweza kumdhania sivyo. Lakini alijaliwa wema wa namna ya kipekee. Anaupendo ule wa kujali usio wa kujifanya.” Sifa zikaendelea.

“Anaakili ya biashara. Maana kwa sasa anafanya vizuri sana kwenye biashara zake. Anajituma haswa si mvivu au si legelege kama ambavyo ungedhania ukimuona. Halafu alimpenda sana Colins. Sana. Na Colins alimpenda.” “Sasa kwa nini Colins hakumuoa?” Akaguna na kurudi kukaa mbele yake.

“Acha nikwambie ukweli Kamila binti yangu. Sisi, nikimaanisha mimi na baba yake ndio tulichangia. Na tulifanya kosa, lakini out of love. Tukijua tunamuokoa Colins asijiingize kwa msichana mbaya, kumbe ndio tulikuwa tukimtoa kwenye mapenzi ya kweli na kumpeleka pabaya.” Akamueleza kwa kifupi juu ya Love na vile ilivyokuwa.

“Sisi bila ya kujua. Tukajikuta tunajiingiza kwenye kumsaidia Kemi kulipiza kisasi kwa Jelini na kumuumiza sana Colins. Yote tuliyoletewa kwa uongo juu ya Jelini kumbe ni kinyume kabisa. Tukamtenga Colins na upendo wa kweli, tukamuweka kwenye mikono miovu. Kwa hakika aliteswa. Hivyo unavyomuona yupo kwenye kupona.”

“Na hivi kukusaidia wewe, ndio imekuwa kinyume. Imekua msaada kwake yeye mwenyewe. Isingekuwa kutoa msaada kwako, alikuwa na hali mbaya sana. Ametoa mawazo kwake, sasahivi anakuangalia wewe, ndio angalau unaweza kumuona hata ametulia.”

“Lakini kwangu naona ni kama...” Akasita. “Nini?” “Anamsimamo Colins! Anamsimamo sana. Na sidhani kama atakuja mpenda mtu mwingine kama Jelini. Akianza kumzungumzia Jelini, anakuwa wa tofauti, na maumivu makali, kwamba anaolewa na mtu mwingine! Sidhani kama atakuja kumpenda mtu tena.” Mama Colins akamuona vile anavyoongea kwa kulalamika na wivu, akajua tayari amempenda Colins.

Ila hakutegemea! Alitegemea majonzi zaidi juu ya Mike. “Ila nashukuru hata kwa hivi mnavyonisaidia. Hata hivyo na mimi sijasoma. Nipo kama huyo Jelini tu. Mike hakuwa hata na shida na mimi kuishia hivi nilivyo. Na pia sikuwahi kujua kama unaweza kukataliwa ukweni sababu ya kutosoma!” Hilo likamshitusha kidogo mama Colins.

“Nisikilize Kamila. Kwa upande wetu, nakiri tulikosea sana. Nyumba haijengwi na usomi. Kama ni hivyo, Love na Colins wangekuwa na familia nzuri sana. Lakini imeshindikana. Bora Jelini ambaye hajasoma mara elfu kwa vile alivyomjali Colins, kuliko huyo Love msomi.”

“Jelini ambaye hakuwa na shule ila mapenzi ya kweli kwa Colins, ilichukua masaa machache sana kumrudisha Colins kwenye uzima, wakati Love na shule yake alimchanganya mpaka akawa akitembe hajitambui mitaani. Kwa hiyo na sisi tumejifunza mama. Shule siyo inayojenga familia ila mapenzi ya kweli.” Akatulia na kufikiria kidogo.

“Ila kwa jinsi nilivyomsoma Colins, sijui mama! Hawezi kuja kupenda tena.” Akajirudia kama ambaye ndio kitu kinamsumbua huko moyoni. “Anahitaji muda tu na mtu sahihi ambaye hatamkatia tamaa. Ambaye yupo tayari kumsubiri na kumuonyesha mapenzi ya kweli. Hakuna mtu anakataa kupendwa. Ila kwa Colins yupo makini sana kwa sababu wengi wanavutiwa na vile alivyo.” “Ila kweli ni mzuri!” Akaropoka na kumfanya mama Colins kucheka.

Kamila akaona aibu. “Sasa hilo ndilo linamfanya achukue muda. Mpaka ahakikishe mtu anampenda Colins wa ndani kabla wa huyu wa nje. Na usifikiri hata kwa Jelini ilikuwa rahisi.” “Kweli?!” “Atakuja kukwambia mwenyewe. Ni mpaka alipojiridhisha Jelini anampenda zaidi ya muonekano ndipo akamfungulia milango yote. Kwa hiyo na wewe mpe muda.” Kamila akaona aibu.

“Mimi nilikuwa sisemei mimi!” Mama Colins akacheka na kusimama. “Mimi nilikuwa naulizia tu kwa watu wengine. Kama ikitokea msichana anampenda halafu yeye hataki hata kuwa naye karibu! Anakuwa anaweka msimamo. Hataki mambo fulani fulani. Anasema labda sio sawa, japo jambo lenyewe sio lakumvunjia heshima. Anakua...” Akajishitukia na kunyamaza. Mama Colins akacheka.

“Wewe umekuja wakati muafaka kwenye maisha yake na yetu. Wote tupo kwenye kujenga si kubomoa. Ndio maana umeona leo, hata baba yake ambaye yupo busy sana, ameacha shuguli zake zote ilimradi tu kuwa naye kwenye jambo kama hili. Ambalo ni lako, lakini akitaka kumuongezea nguvu na heshima. Sasahivi baba yake hazembei tena. Yupo kwenye kumuunga mkono. Ikitokea anafungua tu moyo, jua na sisi tupo nyuma yake.” Akanyamaza.

“Umeelewa?” “Nitakuwa mvumilivu. Si mtaniruhusu kuendelea kuishi hapa au unafikiri ni nunue tu nyumba nihamie kwangu? Maana sasahivi nishajua moja, bora maisha yaendelee.” “Kwamba unayo pesa ya kununulia nyumba!?” “Ninayo mama yangu. Ni hofu tu yakuanza peke yangu.” “Basi tulia hapa kwa muda. Nina binti yangu na yeye anasomea mambo ya udaktari anataka kuwa kama baba yake . Huwa anakuja hapa. Hana neno. Utakuja kukutana naye. Utamfurahia tu. Hapa hakuna atakayekubugudhi mpaka utakapoamua kuondoka mwenyewe. Lasivyo sisi tutakuozesha sisi wenyewe.” Kamila akafurahi sana.

“Basi mimi nabaki hapahapa mpaka nipate mchumba. Nisipopata, nabaki hivihivi. Mimi siwezi kuishi mwenyewe. Naogopa.” “Basi tulia hapa.” Akaanza kula huku wakizungumza machache. Mpaka walipomsikia Colins.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akaenda mpaka jikoni na maua. Kamila akadhania ni yake. Akashangaa anamkabidhi mama yake. “Hakuna kufa.” Akamnong’oneza na kumbusu kichwani. Kisha akamwambia kwa sauti. “Nashukuru kukaa na Kamila.” “Kamila binti yangu. Wala usijali. Pole na kazi.” “Asante.” Akaenda kukaa alipokaa Kamila.

“Vipi?” “Nipo sawa. Asante kunisindikiza. Angalau nimejua moja.” “Umeridhika?” “Nimeamini Colins. Nimemuona Mike kwenye jeneza nimeamini ndiye aliyekuwepo pale kaburini. Sina jinsi ila kukubali ukweli na kuendelea mbele.” “Utakuwa sawa Kamila. Usiogope. Nimezungumza na wazazi, wanakukaribisha hapa. Ishi hapa kama nyumbani. Utakuwa sawa. Sisemi kama tutaziba pengo la Mike, lakini huu unaweza kuwa mwanzo mwingine na ukaupenda tu.” “Nashukuru. Na mama naye ameniambia hivyohivyo. Naona nitatulia hapa.” Mama yake kimya tu akiendelea na yake.

“Nimeleta movie, tutaangalia usiku wakati wa kulala. Tutakuwa wote. Leo sitakuacha peke yako. Tutakaa mpaka ukipitiwa usingizi, ndio nitaondoka.” “Nashukuru.” Akasimama na kumfuata mama yake.

“Umepima pressure?” “Ipo sawa.” “Kweli au unanipa tu moyo?” “Baba yako alinipima kabla hatujatoka hotelini. Ipo sawa.” “Kama hivyo sawa. Umependa maua?” Akamsikia akimuuliza mama yake kwa kumbembeleza.

“Hayo maua yana ujumbe wake. Unachoshindwa kusema ni nini unahangaika tu.” Ikamfanya na Kamila naye kuyaangalia vizuri hayo maua na kujaribu kuelewa. Yalijaa rangi ya dhambarau na nyekundu kidogo tu. “Ni baba huyo, si mimi.” Akamsikia Colins akijitetea.

“Sawa.” Mama yake akajibu kwa kifupi tu na kumuona anatafuta chupa nzuri maalumu ya hayo maua. Akaijaza maji. Akaanza kuyakata vizuri na kuyapanga humo, Colins akimwangalia kama aseme kitu anashindwa. “Ni mazuri, asante.” Akasimama hapo kidogo na kuondoka.

Baada ya muda mfupi akarudi tena na chokleti. “Na hizi nilikuletea nimesahau kwenye mfuko.” Mama yake akajua anahangaika tu. Anasumbuliwa na dhamira ila ubishi, anashindwa kuomba msamaha.

Akapokea akicheka. “Sasa unacheka nini?” “Nimefurahi! Wewe vipi Coly?!” “Sawa. Umependa sasa?” Akawa anahangaika tu hapo. “Hata sijala!?” “Lakini si unazijua?” “Haya, nitapenda. Asante.” Akacheka na kutoka kama aliyejisuta.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mama yake akamgeukia Kamila. “Ametoka kazini. Umejua siku yake imekuaje?” Kamila akaelewa. Akasimama kwa haraka. “Njoo kwanza.” Akamfuata. “Wewe unajua anachokifanya pale?” “Waliniambia ni kama bosi.” “Si kama bosi. Ile hospitali nzima, ni yeye anayeiongoza. Anamajukumu mazito sana.” “Kumbe!?” “Kabisa. Hakuna kinachofanyika pale bila yeye. Yupo busy mno. Na bila wewe, ujue sasahivi asinge bkuwepo hapa. Hii si mida yake. Inamaana amewahi hapa kwa ajili yako. Sasa tumia hii nafasi vizuri.” “Asante mama. Ila namuogopa! Anamsimamo huyo!”

“Sasa hiyo ndio nguvu yako. Baba yake yupo hivyohivyo. Inamaana ndiyo yake kwako, itabakia kwako tu. Sasahivi yupo kwenye ndiyo aliyoitoa kwa Jelini. Ndiyo inayo mfunga. Sasa hapo ni mpaka ahakikishe huko alikotoa hiyo ndiyo yake, milango yote imefungwa. Hakuna nafasi yake tena. Halafu apate ambaye yupo tayari kumsubiria na kusimama naye kipindi hiki ambacho ni kigumu kwake. Sio jambo la siku moja. Na si kazi rahisi au maneno tu. Taratibu.”

“Nitasubiri mama. Naona yeye ananielewa.” “Anza taratibu. Sasahivi mpelekee hii juisi na snack. Anapenda kula. Hapo utampata. Akishakupokea hivyo, muulize siku yake ilikuaje. Hakikisha yeye ndio anazungumza. Mpe muda na endelea kumdodosa katika hilo. Hapo ndio atajua unamaanisha swali lako, kwamba kweli unataka kujua siku yake imeendaje. Maana lasivyo atakujibu tu nzuri, wakati kuna mengi yanayoendelea, hana wakumwambia.”

“Ukifanikiwa kumpa sikio lako, akajua unamjali yeye kama yeye, jua ndio unamsogeza karibu yako. Si vinginevyo. Hajajaliwa tamaa za wanawake kirahisi. Usimuone hivyo. Kwa hiyo muonekano tu, au uzuri tu wa mwanamke, havimchanganyi.” Akazungumza naye kwa sauti ya chini sana akimnong’oneza. Akamuona ameelewa. “Haya mfuate.” “Chumbani kwake!?” “Popote alipo, akakupokea na kukukaribisha, ndio hapohapo. Nenda.” Akamkabidhi vitu, akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kila jambo na wakati wake.

Je, huu ni wakati mwafaka kwa Colins anayehangaikia kulipiza kisasi na kumtoa Jelini kwenye kesi anayojilaumu yeye amemsababishia! Kwamba amepewa sumu na Love aliyekuwa mpenzi wake yeye, japo na Kemi bado yupo! Mama Colins anamuunganisha Kamila, ni wakati muafaka?

Chris amejirudi. Japokuwa anawatetea kina Kemi&Love lakini anafuata muongozo wa Colins, atachezaje hizo karata mpaka kumridhisha Colins asimuharibie kwa mkewe na jamii?

            INAENDELEA. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment