Wakajikuta wametulia hapo mezani, kila mtu anawaza lake,
Colins kapotelea mawazoni, na yeye akabaki akimwangalia huku akiwaza. Chakula
kikaletwa. Kama kawaida ya Colins, linapofika swala la mlo, hana kujivunga. Akala chakula chake mpaka
akamaliza.
“Unauhakika hutaki hata kubeba kitu? Usije umwa na njaa
usiku. Maana najua pale nyumbani hakuta pikwa. Wazazi hawatakuwepo.”
“Wamesafiri!?” “Baba amemtoa mkewe kwa usiku mmoja tu. Kesho wote wanatakiwa
kazini. Itabidi warudi.” Kamila akanyamaza, Colins akalipia na kumwambia
waondoke bila ya kurudia kumuulizia chakula, akijua amekataa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa njiani akawaza kwa sauti. “Nimemiss Mike!” Colins
akamsikia. “Pole. Ila angalau ukweli wa kesho utasaidia kukutoa njia panda.” “Kwa
ukweli wowote ule mbali ya kuwa nampata tena Mike, kwa hakika maisha
yangu hayatakuja kuwa kama zamani.” “Nakuelewa kabisa. Kunaweza kukawa na mwanzo
mpya, ambao huwezi jua Kamila. Unaweza usiwe mbaya sana.” “Sijui! Sidhani
kama nitakuja pata mtu akanipenda na
kunijali kama Mike.” Colins akatulia
akitafakari. Kimya kwa muda hapo garini.
“Mimi naamini hivi.” Akavunja ukimya. “Ukiwa tayari
kupokea huo upendo na kujaliwa, naamini hivi, ukifungua
moyo, na ukampa mtu nafasi, kama uliyompa Mike. Kukufahamu vizuri na kukuelewa.
Na wewe ukaruhusu moyo wako kumpenda, anaweza asiwe Mike, ila ukashangaa
vile Mungu alivyo wa ajabu, kwa kukutumia upendo mwingine wa tofauti.”
“Wewe upo tayari?” “Kwa sasa, tena kwa mara ya pili, bado.
Sidhani.” “Unamaanisha nini kwa mara ya pili?” “Jelini ndio alikuwa upendo
wangu niliokuwa nimetumiwa na Mungu nikiwa nimekata tamaa. Lakini mimi nilichezea
bahati yangu ndio maana naona nisubiri kwanza nisije harakisha
nikaharibu tena.”
“Wanasema third
time is a charm. Ndio maana naona niongeze umakini nisikimbilie. Nisije
haribu. Kwa hiyo kwa kujibu swali lako, kwa sasa hapana. Ndio maana nakwambia usiogope.
Utakuwa sawa. Kwa kuwa nina uhakika. Mungu hakutengeneza Mike mmoja tu. Anao
kina Mike wengi tu. Ni wewe tu kufungua moyo na kutoa muda. Utakuja zisimulia
kumbukumbu za Mike si kwa kuumia, ila kwa furaha ukisaidia wengine kuwa,
Mungu hajaishiwa kina Mike, endapo hatarudi. Na kama yupo dunia hii, nakuahidi
kukusaidia mpaka umpate Mike wako.” Kidogo akacheka.
“Umefurahi sasa?” “Kidogo. Umenifariji. Asante.” “Na ili
ulale vizuri, kwa kuwa hujala, tukifika nyumbani nakutengenezea mayai mawili
tu. Ukila hayo nitakuwa na amani utalala kama jana. Nataka uamke kama leo.”
Hapo akaupata moyo wa Kamila. Dhambi zote akasamehewa. Akasahau hata ya
asubuhi. Angalau akaanza kuzungumza. Stori zikaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Ahadi ya mayai bado ipo?” Akauliza wakiwa wanaingia.
Nyumba ilikuwa kimya. Kuashiria hata msichana wa kazi ameshalala. “Kabisa. Au
unataka chakula kabisa?” “Hata nikitaka chakula tutapata wapi sasahivi?”
“Nakupikia kwa haraka.” “Kwamba wewe unajua kupika!?” “Sana tu. Mbona
umeshangaa!” “Sijategemea! Huonyeshi kabisa!” Colins akacheka tu. “Mike alikuwa
hajui kupika hata chai! Ukimnyima chakula ndio basi.” Hapo hakuchangia.
Akanyamaza.
“Ila mayai yatatosha. Naenda kuoga kabisa.” “Kama ni
hivyo acha na mimi nikaoge. Sitachelewa. Utanikuta jikoni.” Wakaachana kila mtu
akaenda chumbani kwake.
Baada ya muda akamfuata jikoni. “Vinanukia! Ni yai tu
hilo?” “Nimeona nifanye omlet ili ushibe vizuri. Kaa.” Akakaa akicheka.
“Nini sasa?” “Ujue weweni bosi wangu, mkubwa sana! Halafu nakutumikisha!”
“Tukiwa kazini. Sio hapa. Na hunitumikishi.” Akamuandalia na glass ya maziwa. Akamuwekea
mbele yake. Akala kama aliyekuwa na njaa. Colins macho kwenye simu yake.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Jana nililala vizuri kwa kuwa nilijua tupo wote.” Colins
akatoa macho kwenye simu na kumuangalia kama aliyekuwa amezama kwenye simu.
Akamuona analamba midomo yake taratibu na kuingiwa na aibu za kike. Ila
alishajua kuna namna akiwa ametulia akimwangalia msichana, wengi hubabaika.
Kule kulamba midomo yake alijua ni sababu ya midomo yake.
Alichukua midomo yenye rangi ya pinki kama nyekundu kutoka kwa mama yao.
Alivutia na kubabaisha wengi. Sasa alipomgeukia Kamila, mwili mzima wa Kamila
gafla ukapigwa kama shoti ndogo ya umeme, akasisimkwa
mpaka akalamba midomo yake.
“Samahani.
Umesema?” Akamuuliza na ile sauti
yake ya kiume iliyotulia ila kwa sura ya makini kidogo iliyombadili mawazo
mrembo. “Asante kwa chakula.” Akabadilisha. Colins akajua ila akaona amuache
tu. Tokea mwanzoni alimsikia vizuri tu, ila alitaka uhakika na alichozungumza.
Na pia hakutaka wajenge mazoea ya
kulala pamoja.
“Umeshiba lakini?” “Ndiyo. Nashukuru.” Akajibu kwa
kunyongea kidogo. Colins akamtizama na kurudisha macho kwenye simu. Akamsikia akiondoka
na vyombo mpaka kwenye sinki akaanza kuviosha.
Akajiiba kumwangalia. Ukweli Kamila alikuwa akivutia. Lakini alikuwa bado ana mambo mengi yanayoendelea kwenye maisha
yake. Colins hakutaka kuanzisha jambo lolote lile hata dogo kwa namna gani
linalo muhusu yeye binafsi au kujiingiza kwa namna yeyote ile itakayo mchanganya
zaidi yeye Kamila au hata yeye mwenyewe. Akabaki akimwangalia kwa nyuma mpaka
alipomaliza ndipo akarudisha macho kwenye simu.
Akahisi anamsogelea kwa hofu. Akamuacha tu mpaka akafika
pale na kurudi kukaa ila safari hii akasogeza kiti karibu. Colins akamwangalia.
“Upo sawa?” Akatingisha kichwa kukubali.
“Twende ukalale.”
“Na leo utanisubiria nilale au hutaki
kujenga mazoea?” Ikawa kama amesoma mawazo yake. “Jana nilipitiwa na
usingizi kitandani kwako. Unajua?” “Ndio maana nililala vizuri. Kila nilipokuwa
nikigeuka nikikuhisi, nikawa narudi kulala bila shida. Nilijua.” Colins akatoa
tabasamu akimwangalia. Eti akaona aibu.
“Kwa nini vibaya?” “Wewe unaonaje? “Mwenzio napenda.” Colins akaanza kucheka.
Hakutegemea. “Usinicheke bwana. Nakua siogopi. Au wewe unaona ni vibaya?”
Akarudia swali. Akamuona anafikiria kidogo kama anayetafuta jinsi ya kuongea.
“Vibaya, hapana. Sidhani kama vibaya ni neno
sahihi. Lakini sioni kama n i sawa.” Akaumia sana moyoni. Kamila alijijua ni mzuri
na hajawahi kuwa na mwanaume karibu yake, asivutiwe naye. Leo anampa
Colins bahati japo ya kuwa naye kitanda kimoja anakataa! Ikamuuma
sana na kushindwa hata kumtizama. Akaangalia chini kwenye mikono yake. Akabaki
akiweka vidole kwa kila mtindo.
“Sidhani kama ni sawa tukiendelea kulala wote Kamila. Sio mazoea mazuri. Ila nakuahidi kubaki na wewe mpaka utakapo lala. Na u a. “Acha mimi nikalale.” Akasimama kabisa na kuanza kutoka hapo jikoni. “Kamila?” Akamuwahi kabla hajatoka. Akageuka na uso ulioumia haswa. “Usiku mwema Colins. Kesho.” “Na wewe. Ila usisite kunipigia ukiogopa. Nitakuwa chumbani nikifanya kazi kidogo.” “Naona nijizoeshe tu mpaka niweze. Siwezi kuwa tegemezi daima. Usiku mwema.” Akaondoka.
Akatamani amfuate ila akaona asimamie maneno yake. “Mwisho wa yote ni nini kama si
kuchanganyana tu?” Akawaza Colins. “Yupo
mwanzoni sana mwa maumivu yake. Hajapitia hata hatua ya kwanza ya tukio lake la
mapenzi. Hajaamini kama kweli Mike amepotea. Bado kabisa.
Nikianzisha jambo hapa, akimaliza kuomboleza na kichwa kikakaa sawa, mimi
nikiwa nilishaanzisha jambo, akagundua alikosea? Hapana. Acha tuache tu
hivihivi.” Akaafikiana na mawazo yake. Akazima taa pale jikoni na kurudi
chumbani kwake na yeye.
Dhambi Haiozi.
Kesho yake ilikuwa siku ya kusikilizwa tena kesi ya yule mmiliki wa ile hoteli na
kina Kemi, kwa swala la ile sumu
aliyowekewa Jelini. Na Jelini alitakiwa mahakamani. Akafikiria jinsi ya
kusaidia. Akajua njia sahihi ni kumpunguza
makali Chris.
Safari hii akamtumia kwenye simu yake kabisa. Ule ujumbe
wa Zulfa wa kumshutumu kuwa alimlazimisha kutoa mimba, halafu akamuacha.
Akamtumia na picha alizozikuta kwenye kumbukumbu za zamani za Zulfa walizopiga
pamoja kwa kificho. Kisha akamtumia ujumbe, ‘fikiria tu jinsi magazeti
yatakavyopendeza kwa taarifa hizi.’
Akatuma usiku huo akijua wazi kama hayupo nyumbani kwa mkewe, basi yupo ofisini
akijiandaa na kesi ya kesho yake. Akajua atamchanganya tu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akacheka na kuangalia simu yake kuona kama Kamila
alimtafuta. Akaona hakuna jumbe wala missed call. Akajua amelala kumbe
mwenzie analia. Aliingia chumbani kwake na kujifunika mto usoni, kilio kikaanza. Alilia kwa uchungu sana
akikumbuka enzi zake na Mike, akiwa malikia katika ufamle wake, huku watu
wakimfuatilia kwa sifa kemkem huko mitandaoni. Leo hana thamani tena! Kilio kikazidi.
Yeye Colins alipomaliza yake mtandaoni, akajiweka
kitandani, hapohapo akapitiwa na usingizi kama mtoto asijue alipo mpaka alamu
ya asubuhi ilipomrudisha kwenye ulimwengu wa wenye mengi.
Asubuhi.
Akakimbilia kuoga.
Wakati akivaa akagundua ile simu yenye namba ya Mike ina ujumbe. Akajua Kamila
amemuandikia Mike. Akapata hamu ya kujua alichoandika akiwa na uhakika ni
ujumbe wa usiku uliopita. Akakaa na kuanza kusoma.
‘Mike! Niitikie
mpenzi wangu. Hakuna mtu mwingine ananiona vile jicho lako linaniona. Nimebakia
kichekesho na mtu wa kudharauliwa na watu. Uzuri uliosema ninao, kumbe ni jicho
lako tu. Lakini sivyo nilivyo kwa wengine. Natamani kurudi kuwa na wewe
uliyenijaza bila kuacha nikiwa nimepungukiwa. Moyo wangu unalia kwa uchungu na
upweke. Usiku umegeuka kuwa tishio sio kama ilivyokuwa ulipokuwa na mimi. Usiku
ulikuwa ni muda wetu. Ulimwengu mzima hunyamaza, nakubakia sisi tu. Naogopa
Mike. Nisaidie mpenzi. Rudi kwangu.’
Alishituka sana baada ya kusoma, akajua inamaana usiku
hakulala vizuri. Akajisikia majuto kumkatalia kulala naye. Lakini akabaki
akifikiria. Kwahakika akajihisi hayupo tayari kulala naye tu. “Nitafanya hivyo
mpaka lini! Mwisho wake ni nini! Halafu ndio tunakuwa tukifanya nini hicho!?”
Akajiuliza na kukosa jibu. Akaona amalize kujiandaa atoke akaangalie anaendeleaje.
~~~~~~~~~~~~~~~
Chakushangaza akamkuta alishaamka, akamuandalia kifungua
kinywa kizuri, yupo tayari anamsubiria mezani, ila amejiinamia. Alipomsogelea
akasimama kama aliyemfumania. Akagundua alikuwa ameinamia simu yake. Alijawa
wasiwasi na hofu. Uso ukawa kama alivyomkuta siku za mwanzoni.
“Ulilala salama?” “Leo nitajua ukweli juu ya Mike.
Naamini Luca hatanidanganya.” “Nafikiri watamuwekea mazingira ya kutodanganya
na pia tutahakikisha anatoa uthibitisho.” “Hapo sawa. Maana wasije danganya,
kumbe Mike yupo sehemu.” “Ulipata muda wa kulala hata kidogo?” “Ndiyo.” Lakini
alionyesha wazi hakulala muda wa kutosha.
“Nimekuandalia kitu cha kula ili twende kazini ukiwa
umeshiba.” “Kaa tule wote.” “Naona nitatulia nikishazungumza na Luca
nikajiridhisha hanidanganyi. Natamani jibu la kuwa Mike yupo sehemu! Mike ananielewa, Colins. Ananijali hata vile
ninavyojisikia. Vile vitu vyangu vyakijinga
kwa wengine, kwake ni muhimu, hapuuzi na hanichoki. Nitapata wapi mtu kama huyo
hapa duniani? Siwezi ishi bila
Mike.” Ile hofu ya mwanzoni ikajirudia kabisa. Akawa
kama amechanganyikiwa.
“Naogopa
Colins! Naogopa sana. Bora unisaidie
nimpate Mike.” “Naomba tulia Kamila. Na naomba usilie.
Tutakwenda kuzungumza na Luca kisha tutachukua hatua kuanzia hapo. Usiogope.
Sawa?” Akatingisha kichwa akijifuta machozi.
“Umependeza sana. Itabidi mzee Yusuf akuone kabla
hujabadili.” Kidogo akacheka akiendelea kujifuta machozi. “Mwenzio
nimevaa vizuri nikijiandaa pengine leo nitakutana
na Mike!” “Basi ua ndege wawili kwa jiwe moja.”
“Nikamringishie mzee Yusuf kwanza?” “Kabisa.” Akacheka taratibu. “Utakuwa sawa
Kamila. Usiogope.” Akatulia tu hakujibu. Ila akagundua si mtu mgumu kuishi
naye. Anaridhishwa na vitu vidogovidogo.
Akala kwa haraka
wakatoka hapo angalau akiwa ametulia. Haikuchukua muda akapitiwa na usingizi.
Akajua ni kweli hakuwa amelala, anausingizi. Akapunguza sauti ya radio ili
alale.
Alifika mpaka sehemu ya kuegesha magari hapo hospitalini,
hakuzima gari ili A/C iendelee na alale kidogo. Akabaki akifikiria mpaka
akarudi kwa Jelini na siku ya kesi yake siku hiyo. Jinsi ya kumsaidia pekee ili
asiulizwe maswali ya kumuumiza zaidi yeye akiwa muhanga ikabaki ni kumchanganya zaidi Chris.
Bado ilikuwa mapema tu. Akavuta mkoba wake wenye ile
laptop yake. Akamuandikia ujumbe Chris. ‘Wakati ukiendelea kuharibu
vizazi vya mabinti za watu, ukimwaga
damu zisizo na hatia, huku ukigaramia pesa nyingi kwa mkeo azae, na kuhakikisha unamficha asijue kinachoendelea, jua vilio vya
watoto unao waua nje, vinakufuata mpaka kwenye kitanda chako cha ndoa,
na huyo mtoto mmoja Mungu aliyekupa ni kusudi kukukumbusha watoto unao waua huko nje.’ Akamtumia na jumbe alizokuwa akitumiwa na Zulfa alipotoa
mimba na baada ya kumfungia simu zake.
‘Mkeo na Magazeti
yanayopenda kukusifia kila unaposhinda kesi ukiwadhulumu wasio na hatia,
watapenda sana kuona haya.’ Akaongeza na huo ujumbe.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akabaki akitafakari mawili matatu. Akiwa hana uhakika wa
kujibiwa, lakini akaonelea kumtumia ujumbe na Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ø
Anataka kumwambia nini Jelini?
Ø
Je, Chris amepata ujumbe? Atafanya nini?
Ø
Ukweli juu ya Mike unamkabili Kamila ambaye anaamini kurudi kwake,
au kukutana naye siku hiyo. Ni nini kitaendelea?
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment