“Siamini Kamila!” “Wewe
bakia kulekule juu, usianze tamaa. Mwenzio kule nimepata mchumba, mzee
Yusufu ameniambia kwa mara ya kwanza, anamuolea mkewe, mke wa pili.”
“Wewe huyo?” “Wewe usinione hivi.” Colins kwa mara ya kwanza baada ya muda
mrefu wa machungu akasikika akicheka.
“Kwa hiyo usiniambie kupendeza huku ni kwa
mzee Yusufu!?” “Hataniona. Naenda kubadili kwanza, ndio niende, ili anione namaanisha
kazi. Wameniambia ndio kiongozi wao pale, hataki mchezo. Mkali sana. Ila
mwenzio mimi nimependwa. Dula kaniambia.” Colins hana mbavu.
“Ila ujue mzee Yusufu
mkristo!” “Dula kwa wivu wake na yeye alisema hivyohivyo, ila mzee Yusufu
ameniambia nisiwe na wasiwasi, mimi anaenda kuniolea bomani.” Colins
alicheka kwa sauti, asiamini kama Kamila ndio yupo hivyo! “Kamila!” “Mwenzio
nilikuwa na usingizi tu. Jana nimelala vizuri. Sijaogopa wala kushituka mpaka
alamu.” Wakawasikia wakitoka wanaongea.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakataniana kidogo tu
wakiwa njiani, akamuona Colins amepotelea mawazoni kabisa. Akajua ni Jelini
ndiye anayewazwa. Akataka kuhakikisha maana alisikia kidogo mazungumzo kati yake na mama yake. “Pole Colins.”
Bila kufikiria kama aliyekuwa akiwaza naye akajikuta akisema, “Aisee maisha
hayatabiriki! Ukiambiwa Jelini anaolewa na mwanaume mwingine na si mimi!
Nahisi kama ndoto!” Akajua ni kweli.
“Usingekubali. Ningekuwa
mimi kwa Mike, ningempigania.” “Mimi si kama Mike, Kamila. Mike alifanikiwa
kuweka kumbukumbu nzuri kwako ndio maana unasema hivyo. Kwangu imekua
kinyume. Jelini alinipenda sana. Alinipenda vile nilivyo. Lakini tokea
mwanzo wetu, namaanisha siku ya kwanza, nimekua nikimuumiza.
Sikumbuki kuacha kumbukumbu kwake ya kumfanya aniimbe kama hivyo wewe
kwa Mike.” Kamila akainama.
“Yeye alikuwa na sababu
zote za kuniacha toka siku ya kwanza, lakini mapenzi ndio yalimfanya
abaki akinivumilia na kunisubiria akiamini ipo siku nitatulia naye. Lakini nimechelewa.
Na aliyeniwahi amefanikiwa kuweka msingi mzuri, halafu kikubwa zaidi,
amefanikiwa kupata ahadi ya Jelini ambayo ni kila kitu. Jelini hajipingi
kwenye ahadi zake.” Akaamsha maswali kwa Kamila.
“Unamaanisha nini kuwa yeye
aliweka msingi mzuri na sio wewe?” “Jelini ni mzuri sana. Sana.” Wivu
tayari kwa Kamila. “Ukimuona kwa haraka unaweza fikiria hongo yake ni nyumba na
magari, kwa jinsi alivyojaliwa thamani ya muonekano. Mzuri na anajipenda
sana. Lakini pia alijaliwa moyo wa tofauti. Ana upendo usio na unafiki.
Yeye hongo anayotaka ni kupendwa tu. Na kilio chake tokea namkuta,
anataka mtu wa peke yake, kitu kinachosikika rahisi lakini nilishindwa
kumpa.” Akamshangaza kidogo.
“Kwamba ulikuwa na wanawake
wengi?!” “Jelini mmoja, ni kama wanawake 10 kwa mpigo, ila aliyebeba zile tabia
zao bora tupu.” Mpaka Kamila akashangazwa. “Ukiwa na Jelini, huwezi hata
fikiria mwanamke mwingine. Kwanza kuna jinsi anakuwa mikononi!” Akamuona
anavuta hisia nzito, wazi zilijaa penzi. Akamuona amepotelea kabisa
mawazoni. Kimya na uso wa huzuni ukawa bayana. Hakuzungumza tena alichotaka
kuzungumzia juu ya huyo Jelini. Akawa amekwama kwenye hizo fikra za mapenzi.
Kamila naye akaamua amuache mpaka wanafika kazini na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye mida ya saa nne
asubuhi baba yake akampigia. Akaiangalia kwa muda mrefu karibu inakatika ndipo
akapokea bila hata kuitika. “Kama
nitakuwa nimekosea tena, basi unisamehe. Lakini nia ni kusaidia.” “Umefanya
nini tena baba jamani!” “Sio kitu kibaya, ni juu ya Kamila.” Nusura asimame kwa mshituko.
“Umefanya nini tena!?” “Niliona niwasaidie tu
zaidi yeye kumtoa kwenye sintofahamu. Tokea uliponiambia juu yake na alipokwama
juu ya mumewe.” “Hakuwa mumewe. Maana nashangaa kwa muda wote huo ameishi na
msichana kama Kamila asimuoe! Sidhani kama ni sawa. Hastahili kuitwa mume.
Muite tu Mike.” Akajikuta anapandwa jazba kwa jambo ambalo
halikuwa la msingi na wala hakuwahi kuliwaza. Akashangaa hapo analipuka. Wivu
tayari. Wakati na yeye aliishi na Love bila ndoa.
Mzee akashangaa kidogo. “Ila kisheria anatambulika
kama mkewe kihalali! Hawa watu wameishi zaidi ya miaka miwili! Lakini hilo silo
lililonifanya nikupigie.” Mzee akawahi kabla hajaharibu.
“Japo hilo
limesaidia kwenye hili ninalotaka kukwambia. Kama sio muda mzuri, tunaweza
zungumza hata wakati mwingine.” Colins akajaribu kujirudi
maana na yeye alijishitukia.
“Imekuaje?”
“Nilimtafuta mwanasheria na kuomba amsaidie kisheria kupata taarifa kamili juu
ya Mike. Nilimueleza hali ya Kamila na ndugu za Mike. Nikamwambia yeye hataki
mali, ila tu ukweli. Ndio akasema atafuatilia kwa hao ndugu akiwatisha kuwa
Kamila ana haki zote kama mkewe, anaweza kuwafilisi endapo akiamua,
lakini yeye hana shida hiyo, anataka ukweli tu juu ya Mike.” Colins kimya akisikiliza.
“Ametoka
kunipigia simu kuwa ameweza kumpata na kuzungumza na Lucas, kama kiongozi wa
familia, yupo tayari kwa mazungumzo na kujibu maswali yote ya Kamila.” Colins hakutegemea.
“Asante
sana baba. Utakuwa umemsaidia sana kuendelea na maisha yake. Asante.”
“Karibu. Na naona ameshafuatilia huko Wizara ya Vizazi na Vifo. Amehakiki kuwa
kweli Mike amefariki kwa kuwa cheti chake na kifo kilishatoka na kilishapelekwa
mahakamani. Kwa hiyo taarifa za hapo hospitalini ni sahihi. Mike alifariki muda,
na siku hiyo uliyoona hapo hospitalini. Kwa kufupisha habari ili nisikuchukulie
muda wako zaidi, taarifa zahapo hospitalini juu ya Mike zipo sahihi.”
“Nakushukuru
sana baba. Hili ni jambo kubwa sana kwa Kamila. Ni sawa leo jioni tukutane nao?”
“Nitamtaarifu kisha atakupigia. Kila la kheri.” “Nilifikiri utakuwepo!?” “Baada
ya muda mrefu sana, mke wangu ana raha. Siwezi subiri, nishatafuta
sehemu, nampeleka hata kwa usiku mmoja tu. Kwa hiyo leo usiku hatutakuwepo nyumbani.”
“Naomba
umwangalie tafadhali.” “Wala usizungumze kama unanionya mimi! Wewe
ndiye unayempa pressure mama yako wala si mimi. Wewe ukitulia,
ujue ndio pona yake. Ukiendelea hivyo kwa hakika utamuua.” “Ila na wewe
pia unahusika baba. Usitupe lawama kwangu. Wewe ndiye uliyeanza,
ukamuingiza kwenye mambo ya Jelini. Wewe ndiye uliyemsababishia maradhi.
Sio mimi.” “Tangia unazaliwa mpaka sasa na ukubwa wako huo, ushawahi sikia mimi
nikimfoka mama yako hata mara moja?”
Kimya.
“Wewe ndiye
uliyekuwa ukimfoka na kumsukumizia mbali wakati unajua wewe na
Connie ndio kila kitu kwa mama yenu! Aliacha maisha yake yasimame, akabaki
kuwalea nyinyi kitu ambacho mama Simba anamsimanga nacho mpaka leo! Halafu unasahau
hilo, unamfukuza kwenye maisha yako! Unamsimanga kwa makosa yangu
na kusahau garama yote anayolipa kwetu sisi wote watatu! Hutaki akuuguze!
Hutaki akusogelee! Mkali kwake! Unaleta mtu baki akuhudumie na ungali unajua jinsi
anavyokuthamini! Wewe ulitegemea nini?”
“Wewe ndiye
uliyenisababishia baba. Wewe ndio chanzo cha yote.” Akaendelea kujitetea
ila si kwa jeuri kama mwanzo. “Kwa hiyo ukaona adhabu
yangu ili iniume vizuri, ni uniadhibie mke wangu? Mwanadamu asiye
na hatia ila upendo tu.”
Kimya. Safari hii baba yake na yeye akamkatia simu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hiyo siku ikavurugika kabisa kwa Colins. Hukumu huku
akijitetea nafsini mwake. Akajitetea kwa hili na lile, ukabakia ukweli juu ya
mama yake. Kamila anakuja kumletea chakula cha mchana, akamkuta tofauti. Akajua
ni sababu ya Jelini tu, kumbe mwenzie ana vita kali inaendelea nafsini kwake.
Hakumuongelesha sana zaidi ya kushukuru kwa chakula na
kutaka kujua anavyoendelea huko. Tena kama bosi kwa mfanyakazi tu. Akaona
amuache, aondoke zake. “Anaonekana anampenda sana Jelini. Ngumu kwake hata
kuwa rafiki wa kawaida na mtu mwingine.” Akaanza kujilalamisha akiondoka. “Lakini
kwani mimi nilimwambia nina nia naye mbaya! Si ni urafiki tu wa kawaida!” Akaendelea
kujilalamisha nafsini kwake na yeye.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika mida ya jioni ndio akili ikamkumbuka Kamila. Akaweza
kurudisha simu ya huyo mwanasheria. Wakazungumza ndipo akampigia na Kamila. “Umeshinda
salama?” “Ndiyo.” “Mbona kama umepoa? Mzima?” “Mimi nipo sawa tu. Tunamalizia
kuweka sawa hapa jikoni.” “Mbona kama huna raha na wakati asubuhi uliamka vizuri. Ni nini kimekuudhi tena na kukuchukulia
furaha yote!?” Asijue alishampoteza tokea kwenye gari
wanaelekea hapo.
“Nipo tu
sawa, Colins. Vipi wewe? Nilikuja ulionekana busy!” “Sio sana. Mambo mengi
yanaendelea.” “Pole.” “Mimi nipo sawa kabisa, ila nina habari njema. Ukimaliza
njoo.” “Sawa.” Baada
ya kama lisaa na nusu akawasili.
~~~~~~~~~~~~~~~
Colins akamwangalia akiacha kila kitu. “Asubuhi ulivutia
zaidi sababu ulikuwa na furaha. Sasahivi umenyongea! Ni nini?” “Hamna kitu.
Niambie habari njema.” “Kama kungekuwa na kitu, ungeniambia?” “Chakuzungumzika
ndiyo.” “Ni vitu gani havizungumziki?” Akanyamaza akiangalia chini.
Colins akatoka kabisa mezani, akavuta kiti akakaa karibu
ila mbele yake. “Niangalie Kamila.” Akamwangalia. “Ni nini?” “Nafikiri mimekua
na siku ndefu tu. Nipo sawa.” “Bado unafurahia kule jikoni?” “Ni watu wazuri.
Nafurahia. Umeniambia kuna habari njema. Ni nini!?” Akamsimulia alichofanya
baba yake, na mazungumzo aliyotoka kuyafanya na huyo mwanasheria, Kamila
asiamini. Ila hakumwambia juu ya cheti cha kifo. Akaona akajulie hukohuko.
“Kwa hiyo unanafasi ya kukaa na Luca. Ukamuuliza maswali
yote unayotaka mpaka ukaridhika. Na anawajibika kisheria kukujibu.” “Naomba
twende leo.” Akaangalia muda. “Nahisi tumechelewa, lakini acha nimpigie tena
simu tuone. Maana nilipozungumza naye aliniambia ukiwa tayari umtafute.
Anaonekana na mtu mzuri.” “Nitashukuru Colins. Acha nijue ukweli juu ya Mike,
pengine itanisaidia kutulia kimawazo na kujipanga upya.”
~~~~~~~~~~~~~~~
Akampigia na yeye akapokea bila ya kuchelewa. Akamwambia
kama wanaweza kukutana mida hiyo. “Nashauri tuandae mazingira
ya kiofisi. Nimpigie simu Lucas, tupange tukutane ofisini kwangu. Au unaonaje?
Ili tusipeleke mambo kiholelaholea, ikakosa uzito.” “Naona wazo sio baya. Kwenye mida
ya mchana ni sawa?” Wakapanga na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudisha majibu kwa Kamila. Akaridhia. Wakaondoka hapo
ofisini. Kamila akiwa ametulia. Akaona amuache tu, akijua ni mambo ya Mike,
kumbe na yeye anachangia na kumuacha ndio anazidi kumuumiza Kamila
aliyezoea kufuatilizwa na Mike. Kimya safari ya kurudi nyumbani.
“Njaa unaniuma Kamila. Naomba tupitie sehemu tule ndio
turudi nyumbani.” “Hutaki kwenda kula nyumbani? Leo jioni sikupenda
kilichokuwepo pale ndio maana sikukuletea. Ila naweza kwenda kupika nyumbani.”
“Kwanza huwajibiki na kula yangu kabisa. Tafadhali usijiongezee hiyo
kazi.” “Mimi napenda. Sioni kama ni kazi.” “Kama hivyo sawa. Ila sitaki ujione unawajibika
na kula yangu. Ukiweza sawa, ukishindwa pia ni sawa. Unanielewa? Sitaki
niwe moja ya jukumu lako.” “Sawa. Lakini naweza kwenda kukupikia nyumbani.” “Nashukuru,
lakini nahitaji kula sasahivi, sitaki kusubiria zaidi.” Wakatafuta mahali
kwenye vyakula vizuri, wakakaa hapo.
Wakati mtu wa vinywaji amekuja anataka kuwahudumia
vinywaji, akatoa na oda ya chakula. “Aisee siwezi subiri.” Kamila yeye akataka
soda tu, akasema ameshiba. Colins akajua ameshakula jikoni. Akamuacha. Kumbe
Kamila anazidi kuumia kwamba kwa nini hajajali kutokula kwake, Colins
hana habari.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wamekutana watu wawili wenye historia mbili tofauti. Kamila
aliyekuwa malkia kwenye ufalme wa Mike, kabla hajalia shida, Mike amefanya. Na
Colins ambaye bado ana mengi anayofikiria kichwani. Visasi na mapenzi. Akili haijatulia kufikiria
vizuri. Kila siku anaiendesha kwa kadiri inavyomjia zaidi kwa mrembo Kamila,
lakini moyo upo kwa Jelini, akisubiria pengine atabadili mawazo
au muujiza utatokea, Jelini amrudie yeye. Hivyohivyo Kamila akitumaini
pengine Mike atakuwa sehemu atakuja kurudi.
Ila je asiponirudia!? Likabaki swali la kila mmoja
wao hapo.
Ndio wamebaki mguu mmoja ndani mwingine nje kwa walichonacho na
wanachojisikia.
Si kuharibu kabisa chochote walichonacho lakini pia tahadhari wasije
jifunga halafu wenza wakarudi wakawakuta kwenye mahusiano mengine.
Full kujiwinda, ila hisia ndio mchanganyiko.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment