“Lakini pia nilikununulia
kofia zinazofanana na hizo zako. Mike hakuwa mpenzi wa kofia kama wewe, labda
bichi au sehemu ya jua kali.” Colins hakutegemea. Maana aliongea kwa upendo na
unyenyekevu. “Sidanganyi Colins. Nilinunua kutokana na nilivyokuona wewe. Sema
sasahivi nimeshachanganyikiwa sijui
zilipo.” Alikuwa akitetemeka, mpaka Colins ikabidi ajirudi.
“Pengine ipo ndani ya hiyo
mifuko uliyoshika.” Ndiyo na yeye akawa kama amegutuka. Akajiangalia, akagundua
amejikumbatia na mifuko. Akatoa kwa haraka kwa bahati mbaya ile chupa ya perfume akaigonga ukutani kwa nguvu upande
wa pili, mpaka inatua sakafuni, harufu ya manukato yakaanza kuenea hapo
taratibu. Kwamba imevunjika.
Hakujali, akaangalia mfuko
mwingine, akakutana na hizo kofia. Akatoa kwa haraka akiwa amepaniki. “Hizi
hapa mbili. Angalia. Zinafanana na hiyo uliyovaa. Sema moja ni nyeusi, nyingine
nyekundu. Maana nimeona unavaa nyeupe. Na nimenunua hizi sio kwa kutaka
kukubadilisha. Ila nimesema kama utataka kuvaa rangi nyingine. Ila ikileta sura
mbaya, basi. Nitampa mtu mwingine au
hata kuzitupa.” Akawa anamuonyeshea ila kama anayeogopa kumpa.
Colins mwenyewe akapoa. Akajua amemmalizia yeye hasira za wote. “Usikasirike Colins. Nimekosea.
Usinichukie, sijakusudia kukuku…” Akamsogelea na kumshika kabisa mkono ambao
viganja vilikuwa ndani ya mfuko wa suruali, ila akamshika kiwiko kwa juu.
“Samahani. Mimi nimekosa.
Usiniache hapa. Naogopa sana.” Akaingiwa na huruma. Kamila ni mnyenyekevu
ambaye hajawahi ona! Alitegemea angesusa, na kuamua kubaki. Kwanza pesa
anayo, shida yake ni watu tu.
“Nisamehe.” Akarudia kwa
upendo na kumtia hukumu. Akajisikia vibaya! Akaona ameua mbu kwa bunduki. “Basi
yameisha. Na mimi unisamehe Kamila. Inawezekana nimezungumza kwa ukali. Lakini nimemaanisha kila nilichokwambia. Watu wamenichezea
sana, na wamenirudisha nyuma! Isingekuwa kuzembea kwangu, mimi ndio ningekuwa nikimuoa Jelini sasa hivi. Lakini
niliruhusu kila mtu kuingilia maisha
yangu nikifumbia macho mambo niliyojua wazi yananitenga na Jelini.”
“Nipo hapa mpweke si kwa bahati mbaya, ni kwa
kuzembea kwangu. Siwezi kuruhusu
tena. Mwishoe nitakua mtu wa kuanza
kila wakati, nibaki kichekesho daima. Hapana
Kamila.” “Sitarudia tena. Nimekosa, nisamehe.” “Basi twende
nyumbani. Watakuwa wakitusubiria. Huwa wanawahi kulala sababu ya kazi siku
inayofuata.” Ukweli hiyo harufu ilienea vizuri sana hapo chumbani, mpaka Colins
mwenyewe aliipenda.
Nzuri, imepoa. Akajua ni ya
pesa nyingi. Akainyamazia tu. Wakati anamsaidia kuweka vitu vyake kwenye gari
yake, akamuona akiokota vipande vyake vya chupa ili atupe. Akafanikiwa kusoma
jina lake. “Angalia usijikate.” Akawa kama amemgutusha mawazoni. Akasimama,
maana alikuwa amepiga magoti akikusanya hivyo vipande. Hakujibu ila akarudi kuendelea
kukusanya taratibu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Njiani alipoa Kamila,
ungemuhurumia. Kimya amejikunyata kitini, kama anayeogopa kuzungumza chochote
asije haribu. Colins naye akamuacha tu.
Nyumbani kwa kina Colins.
Walifika kwao ni kama
walikuwa wakisubiriwa wao. “Vipi pressure?” Likawa swali la kwanza kwa
mama yake, hata kabla ya salamu. “Naendelea vizuri. Mpishe basi mgeni hapo
mlangoni Coly, vipi bwana!?” Maana alikuwa amesimama mlangoni, Kamila nyuma
yake kama anayemkinga. “Na msije sahamu maagizo yangu.” “Pisha Coly!” Mama yake
akawa kama anachungulia kwa nyuma, mzee yeye ndio hakutaka hata kutoka kwenye
kochi.
Akapisha, wakamuona Kamila
amesimama hapo na baadhi ya mizingo yake. “Shikamoo mama Colins.” Akasalimia
kwa heshima. Mama Colins akacheka.
“Nimejua kama wewe ni mama yake. Maana
mmefanana sana. Amechukua uzuri wako. Colins ni mzuri kama wewe mama.”
Mpaka Colins akageuka vizuri. Mama Colins hana mbavu. “Sasa kwa yale mashariti
yako, sijui hapa nafanyaje!” Akawa anamkejeli Colins aliyesema wasimuongeleshe
Kamila.
“Bwana mama! Hapo muitikie.”
“Aaaha! Sawa. Marahaba Kamila mwanangu. Mimi ndiye mama yake.” Kamila akawa
hajaelewa. Ila akamuongezea swali. “Umekula mama?” “Tulikula kabla hatujatoka kazini
kwa Colins. Asante kunikaribisha nyumbani kwako. Pazuri, halafu patulivu.” “Karibu
sana. Ujisikie kama upo nyumbani kabisa. Twende nikuonyeshe chumba chako.” Mzee
hakutaka hata kuingilia. Matunda yalipelekwa kwa mama tu, kuashiria wao bado wanabifu.
Akajituliza kochini kimya.
Colins akaanza kushusha
mizigo yake na kumpelekea chumbani kwake. “Chumba kikubwa halafu kisafi! Asante
sana.” Akaendelea kushukuru, Colins na baba yake wakisikiliza.
“Ila mimi usiku huwa
naogopa sana.” Colins akasikia akimwambia mama yake, akiwa anaingiza mizigo.
Ikabidi asimame kwanza nje ya mlango akisikiliza.
“Huwa
silali gizani. Naogopa. Hata Mike hakuwa akizima taa usiku.” “Basi na
hapa pia usiwe ukizima.”
“Ndugu zake Mike walikuwa
wanalalamika wanasema namaliza umeme.” “Hapa hakuna shida ya umeme. Wewe washa
taa hata masaa 24. Umesikia Kamila mwanangu?” “Hapo sawa. Asante.” “Na
nitakuonyesha chumba cha Colins kilipo, na changu. Usiku ukitaka kitu chochote
au ukiingiwa na hofu. Unaweza kunigongea mimi au Colins. Tutakaa wote mpaka
upate usingizi. Usikae ukiogopa peke yako.” “Sitakuwa nikiwasumbua sana?” “Hata
kidogo. Nataka ujisikie upo nyumbani kabisa. Na kuwa huru na tutaomba pamoja
kabla ya kulala. Usiogope.” “Wewe ni mama mzuri! Mpole. Halafu
unaonekana una upendo.” Mama Colins akacheka kumtuliza.
“Una kila kitu au kuna kitu
unataka?” “Naona nimenunua kila kitu. Asante.” Ndio Colins akaingia akiwa na
mizigo ya mwisho. “Makabati yote hayo yapo wazi. Kesho ukisha pumzika, utapata
muda wa kuweka vitu vyako vizuri. Acha niwapishe.” “Hutaniombea tena?” Akamuwahi
kabla hajatoka. Akamwangalia mwanae kama anayeomba ruhusa.
“Labda ukiniombea
nitalala vizuri. Sijaomba muda mrefu! Ila mimi na Mike tulikuwa tukienda
kanisani.” Alipomuona Colins ameridhia, akarudi. “Basi tuombe ulinzi wa kimungu
na amani ipitayo amani yote ikufunike.” Haraka sana akakaa, na kufunga macho
akionyesha utayari wa maombi. Colins mwenyewe akashangaa. Ikabidi na yeye akae
akipandisha mabega juu kama anayemwambia mama yake na yeye haelewi. Ila mama
Colins akafurahia ule utayari wa maombi.
Colins mwenyewe ndio akawa
kama amekumbushwa yupo Mungu. Alibeba hasira, hakuwa akikumbuka maswala
ya Mungu kabisa. Akatulia. Mama yake akaomba vizuri tu, mpaka akamaliza.
“Asante. Nimefurahi.”
“Karibu Kamila binti yangu. Uwe na usiku mwema. Ukitaka kitu, Colins
atakuzungusha humu ndani ili upafahamu vizuri. Usikwame popote. Ila asubuhi
yupo mrembo mwingine humu, ameshalala. Utamuona. Sisi huwa tunawahi kuondoka
sababu ya kazi.” “Na mimi nitaondoka na Colins. Naenda naye kazini. Napenda
kupika.” “Colins alituambia. Hongera mama.” Akacheka. “Asante. Usiku mwema.”
Akatoka mama Colins na kuwaacha hapo hao wawili.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Upo sawa?” Maana alimuona
ametulia tu hapo kitandani baada ya mama yake kutoka. “Mama yako anaonekana
mpole. Halafu hapa pametulia. Usije nisahau asubuhi.” “Siwezi. Lazima
tutaondoka wote. Usiwe na wasiwasi.” “Sawa.” Colins akamuacha akitaka kwenda
kuoga.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa ndio amepitiwa na
usingizi ujumbe ukaingia kwenye simu yake na kumfanya aamke. Kusoma, unatoka
kwa Kamila. ‘Unisamehe nimekuumiza Colins. Lakini haikuwa nia yangu. Nilitaka
kuweka furaha kama niliyoiona kwa Mike siku niliyompa ile perfume.
Ilikuwa chaguo langu mimi, wala si Mike. Niliipenda sana, ndio nikamnunulia
zawadi kama hivyo nilivyofanya kwako. Tena akiwa na yake. Yeye aliipenda sana,
akaamua kuendelea kutumia. Furaha niliyoiona kwake, nilitaka kuiona na kwako pia,
kwa upendo ulionionyesha.’
‘Moyo wangu unaniuma kuona imekua vinginevyo,
nimekuumiza. Samahani Colins. Sitaki kukubadilisha au kukuchanganya. Sitaki
uchanganyikiwe. Nakutegemea wewe Colins. Ukichanganyikiwa tu, ujue na mimi
nitachanganyikiwa. Sitaki uwe mtu mwingine ila wewe. Maana ungekuwa mwingine, usingeweza
nisaidia. Wewe kama Colins ndio msaada wangu na sivinginevyo. Nisamehe.’ Colins akazidi kuhukumiwa.
Akaona amjibu. ‘Naomba nije kukuona,
kama si usumbufu.’ ‘Bado nipo macho. Hunisumbui.’ Akamjibu kwa haraka. Colins akaamka na kutoka
kitandani kumfuata.
Akamkuta amejilaza kinyonge. Akatoa chandarua, akakaa akimwangalia vile
alivyojilaza pale. Ungependa kumwangalia.
“Nilikwambia yamekwisha
Kamila!” “Lakini nimekuumiza Colins! Nimeingia kwenye kundi la watu walio kuumiza.
Sikudharau. Sikuoni na mapungufu yeyote. Nilitaka ufurahi.” “Sasahivi
nimeelewa. Ila acha nikwambie ukweli.”
“Umenikuta wakati mbaya
sana. Tena sasahivi nina nafuu. Moyo wangu umejeruhiwa vibaya sana. Natembea na
madonda ambayo yanatonesheka kirahisi sana. Nasikitika na wewe umepita kipindi
hiki. Lakini Colins wa zamani, hakuwa mkali kama uliyemuona hotelini leo.
Nimekumalizia tu hasira, lakini kwa jinsi unavyonieleza sasahivi, nia yako ni
nzuri kabisa, hukuwa na kosa. Umenielewa?”
Akatingisha kichwa kukubali.
“Umeniamini?” “Najua mimi sio Jelini, na hutaniona kama yeye. Lakini
na mimi nakuheshimu Colins.” “Sasahivi nimeelewa Kamila.” “Kwa hiyo unaniweka
kundi gani? La wale waliokuumiza?” Akajua anataka kuwa kundi moja na Jelini. Akasita.
Akatulia kwa muda akitafakari. Akamwangalia akakuta anasubiria jibu ambalo
hakuwa tayari kumpa.
“Tafadhali, nipe muda
Kamila. Ila jua nimekuelewa na nahitaji kukuelewa zaidi.” “Ila ujue mimi
sitakudharau wala sitataka ubadilike. Kwanza upo vizuri Colins. Hakuna
chakukubadilisha.” “Nashukuru. Naomba ulale.” “Hujanichukia?” “Hapana.
Imenifanya nikufahamu zaidi. Wewe ni mnyenyekevu sana. Ngumu kukuchukia.
Na kwa kuwa nimekuelewa, naahidi ile hali ya pale hotelini haitarudia tena.
Naomba ulale. Na nitakusubiria.” Akafurahi huyo!
Akajisogeza karibu kabisa
akicheka nakumfanya Colins naye acheke akimwangalia anavyojipanga vizuri.
“Nilitaka kukwambia usogee ili nirudishie chandarua ulale vizuri!” “Hapa hamna
mbu. Usirudishe. Hivi nikiwa karibu ndio nitalala kwa haraka.” Colins akacheka
akimtizama. Vile alivyomzuri, halafu na unyenyekevu, akamfanya Colins azidi
kuvutiwa naye.
Akatoa kabisa chandarua
Colins akimtizama kisha akajilaza karibu yake kabisa akivuta mto. “Nikuwekee
kitu chochote kwenye tv au nyimbo?” Akakubali. Akaunganisha hapo, nyimbo
zilizokuwa zikumliwaza Jelini, zikaanza kusikika hapo. Akaona ajinyoshe kidogo
wakati akimsubiria alale. Akasikia kutulia hapo pembeni ya Kamila, akapitiwa na
usingizi kabisa asijue alipo.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alikuja kuamka saa 11:30
alfajiri. Akamuona Kamila amelala vizuri, hana habari. Akanyata kutoka hapo na
kukutana na mama yake koridoni. Alishituka akabaki kama amepigwa ganzi. Mama
yake akacheka tu na kuelekea jikoni. Akamfuata. “Haipo kama unavyodhania mama.”
“Kwani mimi nimesema nini?”
“Alishindwa kulala, ndio
nikaenda, nikapitiwa na usingizi. Siwezi kujichanganya. Kwanza bado
anamuombolezea mpenzi wake. Namsaidia tu. Ame…” “Basi utachelewa kazini.”
“Unaweza sema..” “We Colins! Tulia bwana. Sasa huko ulipoenda kumbembeleza na
wewe umelala salama?” Colins akacheka akitingisha kichwa.
“Nini sasa? Maana hamna
salamu!” “Mimi sijakwenda kumbembeleza mama! Ila..” “Ulipitiwa na usingizi.
Sasa umeamkaje?” “Basi bwana. Hata nikikwambia hutanisadiki. Bora niache tu.”
Mama yake hana mbavu.
Akatoka na kurudi.
“Hujanifumania mama.” “Yote hayo unayasema mwenyewe. Mimi nimeuliza jinsi
ulivyoamka, basi.” “Niambie pressure yako kwanza.” Akajua ameingiwa
hofu. “Naendelea vizuri.” “Na hakuna kufa.” “Wewe na baba yako ndio mtulie.”
Akamuona amesimama pale mlangoni kama anayefikiria.
“Usirudi nyuma Coly. Nyuma
ni pabaya, siku yako nzima itaharibika. Natamani ningekuwa na jinsi ya
kurekebisha, lakini sina. Naomba tuendelee.” “Jelini anaolewa mama. Mmenikatilia
vibaya sana. Na mimi nilipata mwanamke anayenipenda kwa dhati, lakini mmemtoa kwenye
maisha yangu. Hilo linaniuma. Sina jinsi ya kufanya. Nafikiria eti
mwanaume mwingine ndio anamuoa Jelini! Mimi ndio nimemkosa!” Akaongea kwa
uchungu na kuondoka. Mama yake akabaki kimya akimuandalia mumewe kifungua
kinywa akishindwa cha kujibu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mix feelings.
Hisia zimeshaanza kuchanganyikana. Kamila kama msaada na hisia za namna yake, halafu Jelini mapenzi yaliyosubiriwa kwa hamu, nakushindwa kutokea.
Akidhania anamsaidia Kamila, Colins anajikuta taratibu anajisaidia yeye mwenyewe. Moyo umeanza kufunguka hata kuweza kumfikiria mama yake. Kuna mambo yanamlazimu kuyafanya, kuweka mazingira rafiki kwa Kamila, nyumbani kwao. Ameweza hata kuanza kujirudi kwa mama yake.
INAENDELEA
0 Comments:
Post a Comment