Connie yeye zaidi alitumia app hiyo kumfuatilia
baba yake hapo kwenye hospitali kuu ya Muhimbili. Akimchungulia alipo, akajua, na
yeye ananafasi, basi anamfuata hata kwa kumshitukiza tu. Atakaa naye
akimwangalia anavyotibu au kupata mlo wa pamoja ofisini kwake, kisha kumuacha
aendelee na kazi.
Wazazi wao walikuwa watumiaji sana, wakati watoto hao
walipokuwa shuleni nchini Marekani. Kutaka kujua walipo na wanachokifanya. Zaidi
kipindi cha ukuaji wao. Walipoona watoto wenyewe wametulia, hawapo kwenye
makundi mabovu, wanapotakiwa kuwepo ndipo walipo, basi kikaanza kukosa kazi
kubwa sana kwao. Ila bado kilitunzwa kwenye simu ya kila mmoja wao kwa miaka
mingi tu.
Colins alikuwa amekisusa. Amezira familia baada ya
kumtelekeza kwa Love. Lakini siku hiyo akaangalia.
Akamuona mama yake yupo kazini.
Kwa mara nyingine tena baada ya muda mrefu wa uchungu na
hasira, akamtuma mtu akanunue kikapu kizuri sana, kilichojazwa matunda yaliyotengenezwa
vizuri kwa ustadi. Na kupendezesha hicho kikapu. Fruit basket. Akamtuma
ampelekee mama yake, bila ujumbe.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mama Colins alishakuwa amenyongea kazini kwake. Kwa asili
ni mpole sana. Lakini matatizo ya nyumbani yakamfanya mnyonge asimwambie mtu.
Ila mama Simba anayejulikana kama mtu wake wa karibu sana kwa miaka mingi,
aliyempita wadhifa, akaanza kutoa siri zao kwa kumsanifu yeye kama yeye na
kijana wake huyo Colins.
Maneno yakawa yanaenea kutoka kwa mama Simba vile anavyojazwa na mwanae Love juu ya
Colins, manesi wenzie wakajua kinachoendelea kwenye familia yake kwa kutoka
upande mmoja tu, mama Simba. Yeye aliposikia hakuwahi kukanusha wala kumsema vibaya mama Simba. Kimya tu ila pressure ikimsumbua.
Nyumbani wanakoishi na Colins ni moto. Na kazini nako kukawa si rafiki tena. Maneno yasiyoisha.
Nguvu yake ikabaki mumewe ambaye alikuwa na jina zuri, mwanaume wa nguvu,
lakini hakuwahi mvua nguo mwanamke
yeyote hapo hospitali nzima ya Muhimbili, isipokuwa mkewe tu. Si wanafunzi wa
mafunzo ya udaktari anakosoma mwanae Connie, wala si warembo wanaosomea unesi.
Mzee akawa muaminifu kwa miaka yote, akimuheshimu mkewe, akijikaza
na tamaa.
Sasa ndio baba Colins akawa faraja kwa mkewe akijua yeye
ndiye anampitisha hapo. Basi mara chache atapita hapo kumwangalia mkewe akiwa
kazini. Atakaa naye kidogo akimfuata nyuma, mwenzie akitumika hapo wodini,
akifanya hiki na kile kisha kuondoka, ilimradi tu kumfanya asiwe peke yake na
kuhakikisha hiyo pressure anaiangalia
kwa karibu. Connie na yeye ikitokea anakijinafasi atapita hapo na kitu kidogo
hata chupa ya maji, atamsalimia mama yake na kwenda kufanya kituo kwa dad
wake. Colins hakuonekana tena hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~
Sasa siku hiyo, majira ya saa sita ndio akaitiwa mgeni
aliyekuwa na hicho kikapu kinachopiga kelele ‘zawadi’ maalumu. Akaambiwa
kinatoka kwa Colins. Akakipokea na kuanza kutafuta ujumbe kwa haraka kujua
amemwambia nini, akakosa.
Mwishoe akaenda kukiweka ofisini kwao, akaenda chooni
kulia. Alilia mama Colins, asiamini. Maana ni kama mwanae alimtangazia msamaha
usio ramsi. Ila alifurahi sana nafsini kwake na kujua maneno ya asubuhi yake
yalimuingia na kumuogopesha kuwa mama yake atakufa. Angalau uso ukapata
nuru.
Kamila kwa Colins.
Kwenye mida ya saa kumi
akapata ujumbe kutoka kwa Kamila. ‘Nimekuja na chakula, tule
wote kama asubuhi. Ila kama upo na kazi nyingi, nitasubiri.’ Hapohapo akampigia. “Uko wapi!?” “Hapa chini.” Akawa kama hajaelewa. “Unamaanisha hapa
hospitalini?!” “Ndiyo.” “Sasa kwa nini hujaja huku juu ofisini?!” “Nimeogopa Colins. Sitaki kuwaudhi zaidi hao
wafanyakazi wako.” “Njoo, usiogope, nimeshazungumza nao. Au una mizigo mizito?”
“Hapana. Ni chakula tu. Vitu nishashusha hotelini. Nilikodi gari. Nakuja.” Baada ya muda, akatokea mlangoni, Kamila wa mtandaoni!
~~~~~~~~~~~~~~~
Alimzubaisha Colins, mpaka
Kamila akamuona. Alipigwa na butwaa la wazi kabisa. “Nilienda saluni waliyokuwa
wakinitengeneza zamani.” “Umebadilika! Kama sio wewe!” Akacheka. “Wananijulia
kichwa changu. Halafu sinaga nywele nyingi. Lakini wao huwa wananijulia sana,
ndio maana nawapenda.” “Na nguo pia zimekukaa vizuri sana. Umependeza.
Karibu.” Akaweka kila kitu mezani.
“Umenifanya nifikirie na
kuchukua hatua. Mike alikuwa akipenda sana nipendeze. Mwenyewe alikuwa anasema
mimi ni fahari yake. Akiniona
nimependeza basi anafurahia huyo! Sasa nikajiuliza kama ulivyosema, akija kurudi tena gafla, angenikuta vile, ningemuumiza sana. Nimejinunulia tena
vitu vya muhimu vyote na nguo nzuri tupu.” Colins akacheka.
“Sasa si utaishiwa?” “Mike
ameniachia pesa nyingi sana, kama aliyekuwa akijua! Na mimi pale kwa ndugu zake
nilijifanya mjinga kabisa, kama sina
kitu ili wasije nishitukia. Nilikuwa
nikienda kuoga na kadi yangu, nalala nayo kifuani. Siiachi popote. Wakawa wanasema nahangaika kumtafuta Mike kwa kuwa nimeishiwa, nataka arudi anipe maisha
ya hali ya juu, kumbe mimi mwenzao nina hela.”
“Sasa si leo watakuwa
wamekushangaa!” “Nimeogopa kurudi kwao. Nikasema wasije nifanyia jambo baya,
nikashindwa kujitetea. Wale ndugu zake Mike wakorofi sana. Ila sijapuuza ushauri wako. Nimempigia simu Luca, nimemuaga.” “Akasemaje?” “Hajasema
kitu. Amenikatia simu bila hata ya kuniaga.”
“Pole sana.” “Nitakua sawa.
Si ndivyo ulivyoniambia?” “Kabisa. Hata sasahivi unamatumaini makubwa. Tukae
tule nikupe habari njema.” Wakakaa kwenye makochi ya pembeni na meza yake.
“Nashukuru kunifikiria
chakula.” “Mwenzio najikomba Colins.
Nataka usinisahau. Naogopa.” Colins
akaanza, kucheka.
“Usicheke. Ujue sasahivi
wewe ndio mtu wangu wa karibu! Au ni tabia mbaya?” “Hata kidogo. Lakini asante
kwa chakula. Mimi huwa ni mlaji ila tu muda.” “Nimekuona. Huzembei kwenye kula.
Ila sasa mbona huna mwili mkubwa?” “Niliugua kwa muda mrefu sana. Nipo kwenye
kurudisha mwili.”
“Pole. Ila na wewe uniahidi kitu Colins.” “Nini?” “Usiugue. Nahisi safari hii
nitachanganyikiwa kabisa. Usiugue
hata kidogo. Sawa?” “Na wewe uniombee. Nina uhakika hata Mike hakupenda
kukuacha, Kamila. Tuombeane uzima.” Akanyamaza.
“Tule, na urudishe mawazo
hapa. Kuna kitu nataka kukwambia.” “Ni nini?” “Nimekupatia familia ya kwenda
kuishi nao.” “Watanikubali!?” “Nimeshazungumza nao. Hawana shida.” Akamuona amekosa
raha.
“Nina uhakika utapafurahia
Kamila.” “Kwa nini wewe hunichukui Colins? Au umeoa? Naona kama itakuwa rahisi!
Ushanielewa. Hunidharau!” Hapo akawa ameshapaniki, yule Kamila anayeonekana
kama amechanganyikiwa, akarudi bayana usoni mwake. Hofu tayari.
“Wewe hunioni
kichaa. Unanisikiliza ndio maana
nimeweza hata kwenda saluni leo. Kwengine naogopa. Nitakuwa kama naanza upya!
Naomba twende wote. Au sio vizuri? Mimi najiheshimu Colins. Sitakuvunjia hesh…” “Tulia kwanza Kamila. Acha kulia. Nyamaza.”
“Sitakupeleka sehemu ambayo
kwanza mimi mwenyewe sijajiridhisha nao. Ni kwa wazazi wangu. Na mimi
nitakuwepo hapohapo. Kwa hiyo tutakuwa wote.” Hilo akalifurahia, hata machozi
yakakauka.
“Kama hivyo ni sawa.
Mwenzio mimi muoga. Sio watu wote wazuri!
Naogopa.” “Tutakuwa wote. Usiogope.” “Halafu ukiwa unakuja kazini,
tunakuja wote. Si sawa?” “Kabisa.” Hapo akatulia na kuendelea kula.
Colins alikuwa akimwangalia
kwa kutulia, hachoki. Kwa hakika alipendeza. Uzuri alikuwa akila huku akiwaza
yake, hata hakuwa na habari kama anaangaliwa, kwa hiyo wakapata muda mtulivu
hapo ofisini wakila.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Nimefurahia chakula.
Asante.” “Nafurahia unavyokula Colins! Mpaka unatia raha kukuletea chakula. Ila
nina swali. Si umesema naweza kukuuliza chochote au nitakuudhi?” “Niulize tu.”
“Kwa nini unaishi kwa wazazi mpaka sasa? Au ni
kwa ajili yangu?” Akafikiria jinsi ya kumjibu, akaona aifupishe. “Niliugua sana.
Ikabidi kuishi nao wakiniuguza. Kipindi hicho ndio baba akaikodisha nyumba
yangu. Nimepona na kutaka kurudi kwangu, ndio nikagundua waliikodisha, na mbaya zaidi mpangaji ana mtoto mchanga. Ila
amechapewa siku za kuhama, anipishe kwangu.” Akamuona ametulia.
“Umeelewa?” “Ndiyo. Ila
nina swali jingine. Ni lini unahamia
kwako?” “Ni sawa tukitembea siku moja moja?”
Akatulia. “Itakusaidia kuishi leo, bila hofu ya kesho.” “Nataka
kujipanga. Kama utaondoka, ni bora nifikirie kununua nyumba yangu.” Colins
akawa amehisi hajaelewa.
“Ununue au upange?” “Naona bora ni nunue tu ili nitulie sehemu moja,
niache kumangamanga.” “Kwamba unahela ya kununua nyumba!?” “Nina hela Colins.
Mike alikuwa akinitunzia kama aliyeziona hizi siku. Hapa nina pesa kasoro tu Mike, ndio maana unaona akili
haijatulia.” Akatulia, akamuona anafikiria.
“Mike alikuwa na pesa ndio
maana watu walifikiri ndio sababu
nampenda. Lakini Colins, Mike alikuwa mtu mzuri sana. Sikuwa na sababu ya
kuhangaika. Alinifanya nikatulia,
nikajiona nina kila kitu. Ameniachia
mahela mengi, lakini najiona sina
kitu! Nikikwambia nilienda kumtafuta kijijini kwao, nilikuwa nikimsaka mpaka
usiku mashambani na kwenye majumba ya watu.” “Kwa nini usiku?”
“Akili yangu ilikuwa
ikiniambia mchana wanaweza kumfungia vizuri, lakini usiku wanaweza
kuzembea.” “Kwa hiyo wewe hukuwa umechanganyikiwa basi! Ulikuwa ukifanya yote
ukifikiria kwa makini sana!” “Sana Colins. Watu walikuwa wakidhani nimechanganyikiwa kwa sababu nitakosa maisha aliyonipa
Mike, kumbe mimi namtaka Mike
mwenyewe. Hata leo wakinirudishia Mike wangu bila pesa, nitamchukua bila kufikiria mara mbili. Ni bora Mike bila pesa, kuliko pesa bila Mike. Havina maana kabisa.”
“Usingenikuta naogopa hivi!
Mike alikuwa ananipa uhakika wa kila kitu. Nilikuwa tajiri wa nafsi, furaha wakati wote. Sijui kama nitarudia ile hali Colins.”
“Usikate tamaa.” “Sina jinsi.” Akamsikia akiguna mawazoni.
Kisha akaendelea. “Mike alijaa kwenye maisha yangu, sikuwahi
kuhitaji mtu mwingine. Naweza nikawa nipo nyumbani, yeye kazini busy, lakini ananipigia na kuacha bluetooth sikioni. Anaendelea na kazi,
na mimi nipo nyumbani. Ilimradi tu awe na mimi na nisijisikie mpweke!”
“Na akipanda tu kwenye
gari, simu. Tunaongea mpaka anaingia
ndani. Hatukuwahi kumaliza mazungumzo. Tunalala tukicheka. Stori za tangia
shule zilikuwa haziishi!” Akamuona anafikiria kidogo kisha akaongeza tena.
“Mmmhh! Kama kweli Mike hayupo hapa duniani, basi Mungu afanye haraka anichukue na mimi, anipeleke alipo.” “Acha kusema hivyo bwana Kamila!” “Nimejawa hofu Colins, siwezi kujisaidia. Kila nikiwaza naishi dunia hii bila Mike, moyo unalipuka kama kumepigwa bomu! Hakika sijui maisha mengine bila Mike.” “Leo umeishi Kamila. Umetoka, umejifanyia usafi na ukapendeza. Umeniletea chakula. Umekaa na mimi hapa. Kesho utapikia wagonjwa wenye uhitaji, chakula kizuri. Huoni kama maisha yako yanabariki wengine?” Akatulia.
“Pengine uniambie hofu yako ilipo, tuzungumze.” “Naogopa
kubaki peke yangu, ndio maana unaniona nakuganda.”
“Na mimi sitakuacha peke yako. Ni ahadi
nakupa.” “Kweli Colins!?” “Kabisa. Siwezi kukufanyia hivyo.” “Lakini umesema
mwisho wa mwezi unaondoka kwenu!” Hapo ndipo akaelewa hofu yake na mengi hapo
kumbe yaliletwa na hilo! Alikuwa ametulia mpaka alipojua atahama.
“Kwanza ujue nyumba yangu imepakana
na kwa wazazi. Nitakuonyesha. Sio mbali.” “Lakini sio sawa na kuwa nyumba moja!” “Milango ya kwangu, kwako iko wazi. Muda na wakati wowote
ule, unakaribishwa. Wakati nikihama, tutazungumza na tutajipanga kwa kadiri
tunavyoendelea, na kuamua pamoja. Ninachokuomba tu, uwe muwazi kwangu.” Akajiweka sawa.
“Mimi si Mike. Naweza nisifanye
kama yeye, kwa kuwa yeye amepata
muda mrefu sana wa kukufahamu, ndio maana kama ulivyosema, kabla hujalia shida,
alikuwa akikutimizia. Hiyo inaletwa na kufahamiana kwa muda mrefu.”
“Sitegemei uwe Mike, Colins!” “Kama ni hivyo nashukuru. Sasa ukilikumbuka hilo,
ongeza na kuwa unaanza. Ila unaanzia
pazuri, na mimi ambaye sikufahamu, ila nipo tayari kutembea na wewe kwenye hatua unazotaka kuchukua. Ila uwe unazungumza
na mimi. Kuwa muwazi kabisa kwangu.
Kama ni kitu cha kukushauri
nitashauri ila kama ni kitu cha kukuunga
tu mkono, jua upo na mimi. Na sitakuacha.”
Akamuona anatulia. Akamuacha afikirie anachokifikiria.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa njiani wanarudi
hotelini, akamuona ametulia garini. Ila sio tulia mbaya, kama aliyepumzika kwa
sehemu. “Colins!” Akamuita taratibu. Akamwangalia. “Asante, umenipa tumaini. Pale ofisini niliogopa!
Nilijua ungeniacha tena kwenu,
nianze tena upya. Nahisi mimi nina tatizo. Mgumu kuzoea watu. Inanichukua muda.
Halafu sasahivi watu hawanielewi.” “Ikitokea wakati mwingine umeingiwa hofu, na
kitu chochote, unaahidi kuniambia?” Akacheka na kutingisha kichwa kukubali.
Alivutia, mpaka moyo wa Colins ukafurahi.
“Ila sasa usinichoke, na kusema wewe sio Mike
nisikutupie matatizo yangu.” “Siwezi kusema hivyo kwa kuwa najua mimi si
Mike, na wala sitakaa kuwa Mike. Ila nimekubali kutembea na wewe kwenye
huo mlango mpya uliokubali kuufungua na kutembea huko.”
“Nashukuru. Na ukiona nakosea usiache kuniambia.” “Kama umeniruhusu, hamna
shida.” “Nakuruhusu.” Wakacheka taratibu Colins akiendelea kukanyaga mafuta
kuelekea hotelini.
Madonda Mabichi Yaliyofunikwa na Ngozi Kavu.
Walipofika hotelini,
akakuta Kamila amefanya shopping ya
nguvu. Mifuko iliyojaa hapo, yeye mwenyewe ikabidi atafute mahali akae. Kwa
kuangalia tu aina ile ya mifuko alionyesha ametoka kufanya manunuzi yake kwenye
maduka makubwa ya maana. Akajua kweli huyo Mike alikuwa na pesa na amemuacha
pazuri. Na bado kufikiria kununua na nyumba!
“Nahisi sasahivi angalau
nina vitu vya kuanzia.” Akawa akizungumza huku akishika ile mifuko yake na
kuangalia ndani kama anayetafuta kitu. Mwishoe akatoa mifuko miwili. “Hii ni
yako. Nilikununulia na wewe zawadi.” Colins akashituka kidogo.
“Usingefanya hivyo! Wewe
ndio unauhitaji!” “Sio vitu vingi. Vitu kidogo tu. Zaidi ni perfume
aliyokuwa akitumia Mike na soksi.” Hapo ndipo akamtibua Colins.
“Kwamba unataka mimi ninukie
kama Mike?!” Swali la kwanza ilionyesha kama hana uhakika sana na anachokifanya
mrembo Kamila. “Ni nzuri sana, najua utapenda.
Ilikuwa ikikaa kwenye nguo zake, mpaka mwili wake ulikuwa una hiyo harufu.” “Kuna tatizo gani na harufu yangu!?” Hilo swali la pili aliliuliza kwa
umakini sana mpaka Kamila aliyekuwa akicheka kwa hisia ikabidi atulie na
kumwangalia.
“Eti Kamila?!” Hapo
akauliza kwa ukali kidogo, asijue amekanyaga kwenye donda bichi.
“Ni perfume nzuri!” Akajibu kwa upole. “Kwa hiyo umeona yangu haifai,
unataka kunigeuza niwe Mike?” Kabla hajajibu, akaongeza.
“Umetoka kuniambia nini? Si
kwamba hutegemei niwe Mike?!” Hapo ameshabadilika na rangi kabisa. “Ndiyo.”
Kamila akajibu akionekana ameshaogopa
haswa.
“Nisikilize Kamila. Watu
wengi sana wanataka kunibadilisha
niwe vile wanavyotaka wao. Kila mmoja kwa matakwa
yake. Mwanamke niliyekuwa naye kwa muda mrefu sana, alikuwa kama hichi unachonifanyia wewe. Sijui kama unanisikiliza?” Akatingisha
kichwa haraka sana kukubali.
“Aliniendasha mpaka
nikachanganyikiwa kabisa, kwa kurukwa
na akili. Kila leo alinibadilisha
kwa hiki na kile na sikuwahi kumtosheleza.
Nilifanya kwa juhudi zangu zote, ili tu kumfurahisha. Kwa miaka yote niliyokuwa
naye, sikuwahi kufikia lengo hata
siku moja, kwa sababu kila siku
alikuja na kitu kipya alicholalamikia na kunilazimishia
mimi niwe.”
“Na mimi nikawa mtumwa
wake. Nikahangaika mpaka mwishoe akaona anigeuze tahira kabisa ili niweze kuwa mtumwa wake. Akaendelea kunibadilisha na kuniwekea matakwa
yake, nikaishia kuwa kichaa kabisa
yule anayetembea bila viatu barabarani. Ndipo aliponiacha na kunikimbia.”
“Wazazi wangu wenyewe wanataka niishi ndoto zao. Na wmewe
tumekutana juzi tu, umeshaona kuna
kitu chakunibadilisha. Unaona hivi nilivyo haitoshi, mpaka niwe Mike.”
“Ni mtu mmoja tu. Msichana
mmoja tu. Niliyekwisha kukutana naye hapa duniani. Alinipenda hivi nilivyo na hakuwahi
kutaka kunibadilisha.” Akaendelea kama ambaye amepata jukwaa na kipaza sauti.
“Jelini alinipenda yule msichana, hivi nilivyo.
Hakuacha kuvutiwa na mimi na hakuwahi kufikiria kunibadilisha ndio
maana moyo wangu umelia sana juu
yake. Na kwa mara nyingine tena, umenirudisha
kwenye yale maumivu.”
“Hata hunifahamu!
Hujachukua muda hata kujua nini napenda!
Kwa nini nipo hivi! Tayari unataka
nibadilike!” Kamila alikuwa akitetemeka asitegemee ile zawadi ingegeuka kuwa
tatizo kwa kiasi hicho, asijue amekanyaga jipu
lenye usaha.“Naomba katika hili usiwahi
kusahau Kamila. Unanisikiliza?” Akatingisha kichwa kwa haraka sana, akitetemeka.
“Mimi si Mike. Sitakaa kuwa Mike. Na kamwe maishani mwangu,
SITAKI kuwa Mike.”
“Sio sawa kwangu. Mike
alibahatika kuishi maisha yake mpaka amekuachia wewe kumbukumbu. Na anacho kitu
cha kurudisha mbele za Mungu. Ana hesabu ya maisha yake aliyoyaishi hapa
duniani.”
“Kweli unataka eti na mimi leo, niendelee kuwa Mike?” Kimya. “Halafu
ili nani ayaishi maisha yangu? Mke
wangu na watoto wangu waishie kuwa
na Mike kwenye maisha yao na si
mimi? Ili iweje? Kwa faida ya nani?” Kimya akiendelea kutetemeka amejikunyata
akiwa amesimama.
“Na kwa taarifa yako tu,
hata nikitumia hiyo perfume
leo na kuvaa soksi zake, utaona haitoshi.
Utataka nianze kuvaa kama yeye. Utakuja kutaka niwe na zungumza, kula, kuishi kama yeye. Mwisho wake ni nini kama si kunirudisha barabarani nikiwa nimechanganyikiwa kabisa?”
“Maana mimi sijawahi muona Mike akiishi maisha yake!
Sijui anavyofikiria au kutenda, halafu wewe unategemea niwe yeye! Mwisho wake
ni nini kama si na wewe kunigeuza mtumwa wako ukinizungusha kwa hiki na kile
bila kutoshea?” Kamila kimya akiendelea
kutetemeka na mifuko yake mkononi, Colins anawaka kwelikweli.
“Sasa, mimi ni Colins. Hii harufu unayoisikia
kwangu ni yangu. Narudia tena. Mimi si Mike. Sitakaa kuwa Mike. Sitakaa
nikajaza pengo lake. Na sitaki kuwa
yeye, wala kujaza pengo lake, au hata sitathubutu
kuvaa viatu vyake. Alikopita amepita yeye,
na kwa jinsi unavyomuimba, inamaana
ameitendea haki nafasi yake. Siwezi
na sitaki kuendelea kuyaishi maisha
yake.”
“Chochote unachokiona
kwangu, jua kinaniwakilisha mimi kama Colins. Hulazimiki
kukipenda, na sitegemei upende kitu chochote kutoka kwangu. Iwe kwenye
kumbukumbu yako au vinginevyo, usithubutu
kunibadilisha Kamila. Huo ni mstari nimechora. Sitaruhusu yeyote auvuke. Wazazi wangu ndio wa mwisho, lakini sasahivi, BASI. Atakayeweza kuwa na mimi kwa hivi
nilivyo, sawa, ambaye hawezi. Basi.
Unanielewa?” “Ndiyo.” Mpaka mdomo ilikuwa ikicheza.
“Swali la mwisho ukiwa umeelewa msimamo wangu. Bado unataka kuongozana
na mimi nyumbani, au unahitaji muda zaidi wa kufikiria?” Kabla hajajibu
akaongeza. “Hiki chumba kimeshalipiwa. Namba yangu ya simu unayo. Ukijifikiria
na kuona unanihitaji kwa msaada wowote ule, bado ahadi ipo palepale. Muda na wakati wowote, nipigie. Nikiona kimya,
nitaelewa umeamua kuendelea bila mimi. Uamuzi ni upi?” Akamuona anavuta mifuko
yake mpaka kifuani juu. Akaikumbatia akitetemeka kwa hofu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ingekuwa wewe Kamila Angechagua kipi!?
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment