Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 17. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 17.

Bado Colins akajisikia mzigo na Kamila akishindwa kujisaidia. Akaacha majukumu mazito yanayomkabili hapo kazini, japo usiku ulishakuwa umeendelea, lakini bado alikuwa na yakufanya, akaacha kila kitu akaanza kazi ya kumtafutia sehemu ya kulala wageni.

Akapata sehemu ambayo ni njiani kwenda nyumbani kwao. Akaona patamfaa, yeye na Kamila mwenyewe. Akalipia chumba, akamsindikiza chumbani akiwa amepoa.

  “Utakuwa sawa hapa?” “Nashukuru. Asante.” “Nataka kujua kama utakuwa sawa.” “Naogopa. Lakini panaonekana pako salama.” “Nikikwambia usiogope, itasaidia?” Akatingisha kichwa kukubali.

“Usiogope. Lala ukiwa umewasha taa. Usifungue mlango kwa sababu yeyote ile mpaka papambazuke, na pia kwa yeyote atakayegonga, muulize kwanza kabla hujamfungulia.” Akakubali. “Kingine, nashauri kesho ujiweke sawa kabla hujarudi kazini.” “Unamaanisha nini?” “Si bado unaishi na ndugu zake Mike?” “Ndiyo.”

“Basi nashauri ukaage. Isiwe umeondoka kimyakimya. Na uchukue mizigo yako pia, ili uanzie pazuri.” “Walichukua vitu vyangu karibu vyote. Vilivyobakia nikafungia kwenye gari. Luca aliponipokonya gari, nikamuomba nichukue vitu vyangu lakini akakataa. Akasema kila kitu ni mali yao.”

“Kwa hiyo huna kitu ulichobakiza kule?” “Hamna. Ila nina hela benki. Naficha kadi yake. Mike alinifungulia kwa jina langu akaniambia nisiwahi tumia mpaka iwe dharula kweli, akiwa yeye hayupo. Maana kadi nyingine za benki zilizokuwa na jina langu na Mike, walininyang’anya. Wakaenda mahakamani kudai pesa. Wakapewa wakagawana, mimi wakaninyima. Ila sikuwaambia kama nina akaunti ingine. Nilinyamaza tu.” Colins akabaki kimya.

“Ninachotaka kukwambia, hata kama wamechukua, nitanunua vingine. Halafu naweza kutafuta pakuishi, ila sema naogopa. Sijawahi ishi peke yangu hata mara moja!” “Basi usiwe na wasiwasi. Zipo sehemu nyingi tu ambazo utakuwa salama.” “Kweli?” “Kabisa. Usiogope. Tutatafuta taratibu. Na ukitaka kitu chochote. Ukiwa na swali. Muda na wakati wowote, chukua namba yangu, tuwasiliane.” Akatoa simu yake. Colins akampa namba yake ya zamani.

“Ni sawa nikikupigia ili utunze namba yangu?” Akamuuliza kwa hofu kidogo. “Ili ikitokea nakutafuta, ujue ni mimi. Na pia sitakusumbua mpaka iwe lazima sana.” Asijue Colins alishakuwa na namba yake tokea hawajakutana!

“Wazo zuri. Na naomba usiogope Kamila. Mwanzo ni mgumu kwa yeyote yule. Na kuuliza si ujinga. Halafu ni kweli nipo busy, lakini si kiasi chakushindwa kukusikiliza. Umenielewa?” “Nimeelewa, sema kesho niliwaahidi nitapika.” “Wanahitaji msaada hata kesho kutwa na siku zij azo.” Akamfanya atulie.

“Pata muda wa kesho kujiweka wewe mwenyewe vizuri. Kuanzia usafi wako binafsi. Mavazi na vitu vingine. Nina uhakika ukiwa sawa wewe mwenyewe, kwa kuanza hatua ya kwanza, utashangaa jinsi itakavyokuwia rahisi kuendelea kuchukua hatua zingine.” “Asante. Eti wewe unaitwa Colins?” Colins akatoa tabasamu.

“Ndiyo. Naitwa Colins.” “Mimi naitwa Kamila. Nitatunza jina lako.” “Ulikula?” “Sina njaa. Bado nipo kama nime…” Akasita. “Moyo wangu umekataa kuamini kama sitamuona tena Mike! Nashindwa kuweka kitu chochote mdomoni.” Akanyongea kabisa.

“Bado siamini kama Mike ameniacha!” “Unafikiri ukienda kuona kaburi lake itasaidia?” “Sidhani. Nitajuaje kama yeye ndio yupo humo ndani?” Colins akakwama.

“Nahisi kama yupo mahali ananitafuta ila hajui jinsi ya kunifikia! Mike ananipenda sana. Hawezi ishi bila mimi. Hatujawahi kuwa mbalimbali hata siku moja! Alikuwa hata akipata safari ya dharula vipi, lazima anifuate twende wote. Alikuwa anasema hawezi kulala, kama sipo naye! Sasa sasahivi nipo najifikiria. Nakua namuonea pia huruma! Nahisi amekwama mahali, hajui jinsi yakunifikia! Sijui! Nipo na wakati mgumu!” “Pole sana.” Akamuona ametulia.

Kisha akaongeza. “Nammiss sana. Natamani kama ningeweza kuzungumza na Luca, anihakikishie kama kweli waliyemzika alikuwa Mike!” “Sasa kwa nini usifanye hivyo?” “Chochote kitakachosikika ni kunisaidia mimi, hawezi kukubali. Anatamani sana kuwa na mimi. Kitendo cha kumkataa, kinamuuma, ndio anataka kuniumiza na mimi makusudi. Wakati mwingine ananibembeleza anasema hata nilale naye tu! Kwa hiyo najua nikimuendea kwa lolote, atataka kwanza mapenzi.”

“Ndugu zake wengine?” “Kwa sasa wanamtegemea yeye kifedha. Ni kama wote wanaishi kwa rehema zake Luca. Hawakusoma na wala hawana kazi za kueleweka. Kwa hiyo chochote anachosema Luca, wanamsikiliza.  Na hawawezi fanya chochote bila ya kumuuliza yeye. Ashasema mimi ni mtu mbaya kwao, nataka kuja kuwageuka baadaye, nidai haki kama mke wa Mike. Yaani nichukue mali zote za baba yao, halafu niwadhulumu. Mimi nikawaambia sina nia hiyo. Ndio akasema basi anioe ili kweli mali zao zibakie kwao. Nikakataa. Ndio akawaambia ndugu zake ni kweli nia yangu ni kuwadhulumu mali za baba yao.”

“Halafu kwa jinsi nilivyosikia, mmoja wao aliropoka tu. Nasikia walipokwenda mahakamani, waliulizwa kama Mike hakuacha mke na watoto. Wakakataa. Wakasema nilikuwa nikiishi naye tu. Wakaambiwa hata kama hatukuwa tumefunga ndoa, lakini nimeishi naye kwa muda wote huo, kisheria mimi ni mkewe, natakiwa mimi ndio niwe mrithi. Nasikia walidanganya kama eti mimi nilishaondoka kwenye maisha ya Mike hata kabla ya kifo au sijui walidanganya nini, nakusema hata hivyo sikuwa hata nimezaa naye.”

“Sasa nasikia wanaogopa kunifukuza kwa nguvu, nisije nikawashitaki. Wanajua mimi nina haki kama mke wa Mike.” “Ambayo ni kweli.” “Kumbe kweli!?” “Kisheria kama mmeishi nyumba moja kwa zaidi ya miezi 6 nafikiri, mnatambulika kama mke na mume.” Akatulia akifikiria.

“Lakini, acha tu niondoke. Kwa sababu kwa uhalisia, Mike aliaminiwa tu na baba yao, kuendeleza mali zake. Sasa kwa kuwa mimi nilikuwa nikinufaika kupitia kwa Mike, ambaye ni kama alikuwa mfanyakazi tu, haitakuwa sawa leo kuanza kudai mali za baba yao.”

Simtaki Luca, wala hatakaa akawa mume wangu. Acha nisimuabishe Mike. Mike alikuwa mtu wa haki. Hata wao wanajua ndio maana pia walikuwa wakimuogopa sana na kumuheshimu japo walikuwa wakimuonea wivu. Hakuwahi kuchukua kitu kisicho halali yake. Na mara kwa mara alikuwa akiwaambia kila faida anayotengeneza kwenye mali zao, na kuwapa wenyewe wagawane. Ila nafikiri wivu ndio ulikuwa ukiwasumbua.”

“Acha tu niondoke kwa amani, ili pia wasije nifuata nyuma na kunidhuru. Siwaamini. Na naamini ukweli utakuja jitenga. Kama kweli Mike wangu amekufa kweli, najua nitajua tu. Na Mungu atanipa nguvu ya kuendelea mpaka nije kukutana naye kwenye huo ulimwengu ujao.” “Hapo umeongea sahihi. Pata muda upumzike.”

“Nashukuru sana Colins. Si ni sawa nikikuita hivyo au nitakuwa nikikuvunjia heshima, nikuite bosi kama wengine?” “Huna sababu yakufanya hivyo. Colins inatosha.” Akacheka. “Kesho nikikamilisha kila kitu, kesho kutwa nitakuja kazini.” “Sawasawa. Na naweza kukupitia nikiwa natoka kazini kujua ulipofikia. Ni sawa?” “Nitafurahi.” Wakaagana, Colins akasubiria nje ya mlango mpaka akafunga milango yote, akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alipofika tu kwenye gari akaona anampigia. “Kwema?” “Samahani. Nimejikuta na funguo mbili za mlango. Kwa kuwa wewe ndio sasahivi kama mdhamini wangu, na ndio mtu pekee unajua nilipo. Naomba ukae na funguo moja. Ili hata ikitokea naanguka ndani, basi kuwe na mtu mwingine wakuweza kuingia ndani.” “Wazo sio baya kabisa, japo najua hakuna baya litakalo kupata. Usiogope. Narudi kuja kuchukua.”

Akafurahia hilo wazo, akarudi kuchukua funguo, akamkuta anamsubiria. Akamkabidhi. “Nakushukuru na samahani nakusumbua.” “Usijali kabisa. Hivyo unavyo zungumza, ujue ndio itakusaidia. Muda na wakati wowote, wewe nipigie tu.” Akaonekana kuridhishwa na hilo, ndipo akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati analala kumalizia hiyo siku ndefu ya jumapili, ujumbe ukaingia kwenye simu yake mpya. Akajua kuna Kamila anachotaka kumwambia Mike.

‘Siamini kama umeondoka Mike wangu. Nina ombi moja kubwa kwako. Nipo na wakati mgumu sana. Siamini kama umeondoka katika ulimwengu huu ambao mimi nipo. Ila kama kweli upo popote mpenzi, tafadhali nijulishe kwa njia yeyote ile, nijue bado upo katika ulimwengu huu. Natamani kujua kwa hakika Mike. Nashindwa kuamini mpenzi. Kweli walikuzika! Kweli muda mfupi tu ule nilipokuacha pale hospitalini eti ndio uwe mwisho wa kuonana mimi na wewe! Bado siamini. Ule hauwezi ukawa ndio mwisho wetu wa kuonana.’

‘Lakini hata hivyo, nakwenda kuagana rasmi na ndugu zako. Naogopa wasije niua sababu ya mali. Luca amepandwa na hasira mbaya sana dhidi yangu tokea nilipomkataa. Acha niwapishe. Ila sitabadilisha namba ili popote nitakapokuwa, unifikie Mike. Tafadhali usinyamaze mpenzi. Kama unanisikia, tafadhali nijibu.’

‘Ila nahisi nimepata mtu mwingine mwenye moyo kama wako Mike. Ni yuleyule, amesema kweli jina lake ni Colins. Amenisaidia kuhama pale hospitalini. Anaonekana ni mtu mzuri. Na yeye ananisikiliza kama wewe. Ila yeye namuogopa.’ Akamalizia hapo na kumuacha Colins akitafakari mpaka kupitiwa na usingizi.

Jumatatu.

 Asubuhi na mapema, akaamkia hapo hotelini. Alitoka kwao alfajiri sana akiwa amesahau kuwa waliagana na ahadi ya kumtafuta jioni akiwa anatoka kazini ili kujua siku yake iliendaje. Lakini alimka akili ikimtuma kwenda kumuangalia yeye tu.

 Akakanyaga mafuta kama anayewahi kitu. Haraka mpaka mlangoni. Naye Kamila akafungua mlango kwa haraka akionekana kama ambaye hakuwa amelala. “Mbona kama hujalala kabisa?!”  Akamuona amenyamaza. Akajua tu ni sababu ya Mike.

“Eti Kamila?” “Mimi siwezi kulala sehemu yote hii peke yangu. Naogopa, ndio maana Mike alikuwa haniachi peke yangu usiku. Na ndio maana pia nimeshindwa kuhama pale aliponiacha Mike.”

Akaendelea taratibu tu bado akionekana na majonzi. “Japokuwa wananisumbua pale, lakini najikuta sipo peke yangu. Nalala hata kwenye kochi.” Akaanza kutokwa na machozi.

“Na pia nashindwa kulala kwa kuwa bado inaniwia ngumu kuamini kama Mike hatarudi tena. Naogopa sana. Imekua ni kama kufumba na kufumbua tu jamani! Yaani siku ile tulikuwa na wakati mzuri tu! Gafla anaumwa tumbo. Nampeleka hospitalini akiwa anatembea mwenyewe! Eti namuacha kwa muda mfupi tu, tena kwa kumuaga yeye mwenyewe, ndio iwe basi! Hakika siamini. Moyo wangu unauma, sijui chakufanya.”

“Bado nahisi kuna kitu hakipo sawa, lakini sijui ni nini!” Colins akatulia na kubaki akitafakari.

“Najua unaweza usinielewe kwa kuwa umeshapita muda mrefu, utashangaa kwa nini nilie mpaka leo, lakini Colins, moyo wangu upo na wakati mgumu! Sijui jinsi ya kuelewa hili jambo. Nimemtafuta Mike kila nilikohisi wanaweza mficha! Nimeenda mpaka kijijini kwao kabisa na nikakaa huko siku 10 nikipeleleza kama wamemuona! Huko nako nimemsaka mpaka kwenye mashamba yao!”

 “Nilishakwenda mpaka nyumbani kwa Luca na kwa ndugu zake hata kabla hawajahamia pale nilipokuwa nikiishi na Mike. Nilikuwa nikienda kwa kuwashitukiza, namtafuta mpaka chini ya uvungu, wananiona ni kichaa. Sina ninapopafikiria, sijaenda kumtafuta Mike. Na bado nahisi pengine ipo sehemu, nimeshindwa kupajua!” Kimya akijaribu kufikiria jinsi ya kumsaidia.

 “Najua unachoka na mimi, lakini siwezi kujisaidia.” “Hapana, Kamila. Mimi naelewa kabisa. Naweza nisijue maumivu yako kwa kuwa kila mtu anahisia zake, ila hiyo hali ya kutokukubaliana na ukweli, nilishakaa hapo kwa mateso makali, akili ilikuwa inashindwa kuelewa. Lakini tofauti yako na yangu, mimi nilikuwa na vithibitisho vyote kuwa nimepoteza na sitakaa nikampata tena. Kwa hiyo naweza nikaelewa hali unayopitia. Nilishakuwepo hapo.”

“Na sitakushangaa kwa kulia mpaka sasa au kumtafuta. Hata kidogo. Unahitaji kumuombolezea Mike na kujiridhisha kwa hakika juu ya sehemu sahihi alipo. Na linapofika swala la kulia, usijizuie. Na pia ukifikiria sehemu nyingine unayodhania unaweza kwenda kumtafuta, niambie mimi nitakusindikiza mpaka uridhike kabisa. Chukua muda wowote ule mpaka utakapo pata nafuu nafsini kwako na mawazoni. Sita kuhukumu.” “Nashukuru, Colins. Na asante kunielewa.” “Kabisa.” Akajaribu kutulia.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa kuhusu swala la kulala hapa, unafikiriaje? Au unataka kurudi kule ulipokuwa ukiishi?” “Hapana. Acha nitajaribu tena na leo. Ningumu, lakini lazima nianzie sehemu. Nimekua kwenye nyumba ya watoto yatima. Nikafaulu kwenda bweni, kisha nikahamia kuishi na Mike, alipoondoka wakahamia ndugu zake. Kwa hiyo ni kama sijawahi ishi peke yangu.” Colins akabaki akifikiria.

“Nina wazo ambalo nataka nilifikirie kwanza kabla sijalitekeleza. Kwa sasa tupate kifungua kinywa utoke hapa ukiwa umeshiba, na mimi niende kazini.” “Kichwa kimevurugika Colins, siwezi kula.” “Naomba jikaze Kamila. Itakusaidia kufikiria na kuchukua hatua sahihi tena kwa haraka. Niambie unataka kula nini?” Akambembeleza hapo mpaka akakubali kula. Wakaagiza kifungua kinywa, wakala pamoja hapohapo chumbani huku wakiangalia taarifa yahabari asubuhi hiyo.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Nikikusubiria hapa, unaweza kulala kidogo angalau upunguze usingizi kabla hujatoka?” “Sasa na wewe kazini? Acha tu.” “Usijali. Lala kidogo. Nikihakikisha umelala kabisa, ndio nitaondoka taratibu. Au utaogopa?” “Nikishapotelea usingizini sitakuwa na shida. Nashukuru.” Akawa kweli amebanwa na usingizi. Akapanga kitandani, akihakikisha macho yake yanamuona Colins. Akageukia kabisa upande aliopo akimtizama kama anayejihakikishia hayupo peke yake. Hakuchukua muda mrefu akalala Colins akiwa amepotelea mawazoni.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Miaka miwili bado Kamila anamsubiria na kumtafuta mpenzi wake!?” Wivu ukaanza kumsumbua Colins. “Ningepata bahati hiyo mimi!” Akazidi kuwaza akijiumiza moyoni. Mengi yalipita kichwani. Kumbukumbu za kipindi amechanganyikiwa hajielewi zikamjia.

“Inamaana na mimi ningekuwa na mwanamke kama huyu, angenitafuta, nakujua nipo matatizoni akanisaidia mapema tu. Jelini alinikatia tamaa.” Akaendelea kuwaza na kuumia, mpaka akakumbuka anamajukumu mazito yanayomsubiria. Juma ndio limeanza. Kuangalia, Kamila alishalala kitambo! Akatoka kwakunyata.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akabakiwa na kazi ya kufikiria pakumuweka huyo Kamila. Alimtafutia hoteli nzuri, tulivu yakisasa akidhania angefurahia, ndio hakulala! Yeye hana nyumba, anaishi kwa wazazi. Hasira zikampanda akawapigia simu wazazi wake wote na kuwaweka kwenye conference call. Wote kimya wakitaka kujua safari hii ni nini tena!

“Nataka nyumba yangu.” “Tafadhali kuwa na subira Colins. Yule mpangaji ana mke na mtoto mchanga. Siwezi kuwafukuza. Katika hilo tafadhali naomba fikiria.” “Siwezi kufikiria kama nakuwa na wageni wangu, wana shida, halafu mimi nashindwa kuwasaidia.” “Kwa nini usimkaribishe pale nyumbani?” Mama yake akatoa wazo.

“Ili na yeye mumfanyie kama mlivyomfanyia Jelini? Mnataka kuendelea kunitesa mpaka lini jamani!?” “Colins, nimekosa baba. Nakuahidi sitarudia kosa. Safari hii nita..” Wakasikia simu imekatwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini huko alipobakia akabaki akifikiria pakumuweka Kamila, lakini mwishoe anaishia wazo la mama yake si baya. Kwao kumetulia sana. Mbali na hasira alizobeba kwa mama yake, alimjua ni mtu mzuri sana. Mpole ndio maaana mama Simba alikuwa akimuonea.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akapiga tena. Wazazi wote wakapokea kama wanaofanya kazi kwenye kampuni za simu, wakihudumia wateja. “Lakini akija hapo kuna masharti.” Wakajua amekwama, ila jeuri kama baba yake.

“Unataka nini?” Mzee akauliza. “Hakuna kumuongelesha kabisa. Hata salamu sitaki.” Kimya. “Mnanisikiliza?” “Nina swali.” “Hapana mama.” “Sasa ikitokea anasalimia?!” “Usiitike.” “Hapana Colins. Hivyo mimi sitaweza. Itakuwa..” “Mbona baba akikulazimisha kufanya jambo unakubali, mimi nakuomba jambo dogo tu, unashindwa?” “Basi kama wewe na baba yako hamjui, nyinyi wawili ndio mnafanya maisha yangu kuwa magumu sana hapa duniani, mpaka naumwa, na najua kwa hakika mtaniua siku si nyingi.”

Akaanza mama Colins na kulia juu. “Hivyo ulivyo sasahivi na hasira, ndivyo alivyokuwa baba yako mpaka tukamtoa Jelini kwenye picha. Akapoa. Sasahivi umerudi wewe, umempokea, hasira zilezile unaniadhibu bila kunifikiria wala…” “Mbona wewe hujanifikiria!?”

“Nimekwambia kwa sababu baba yako yupo kama wewe. Na yeye alinipitisha hapahapa unaponipitisha wewe. Nimebaki na mapressure, naumwa, mwili hausikii dawa, wasiwasi, sina raha! Acheni nife, mpumzike. Labda utakuja kupata mama mwingine ambaye ni mwema kwako, na hakosei kama mimi.” “Mimi sijasema nataka mama mwingine.” Mzee akajua tayari ameshakamatika.

 “Ila sidhani kama mama ambaye anampenda mwanae angeweza kumtelekeza kama wewe.” “Nimekosa Colins. Na nipo tayari kutengeneza.” “Jelini wangu anaolewa. Unatengenezaje hapo?” Akaongea kwa uchungu ila sio ukali na hasira. Wote kimya kwa muda.

“Najua haitasaidia, lakini nimekosa Colins. Nimekosea sana. Tafadhali tafuta jinsi ya kumsamehe mama yako, hata kama kwangu utashindwa, mimi nitakuelewa. Yeye ndio aliye gutuka na kujua kuna kitu hakipo sawa kwako. Japokuwa kina Simba walikuwa wakituficha hata kujua ulipo wakitudanganya umesafiri kikazi au upo na majukumu mengi, mwishoe mama yako akashindwa kabisa kusadiki.”

“Alikuwa na kazi ya kukutafuta kila mahali alipokuwa akidanganywa na kuhisi upo. Ofisini na huko Kigamboni. Kazi pia zilimshinda kwa ajili ya kukutafuta wewe. Alishashinda huko Kigamboni akikusubiria mpaka usiku ndipo akajiridhisha kuwa kuna kitu hakipo sawa, ndipo nikaingilia kati. Hana hatia.” Hapo hakujibu ila akaendelea.

“Nitarudi na mgeni wangu jioni.” “Unataka nimtayarishie chumba?” Mama yake akaongea kwa kujikomba. “Bado siwaamini, nitalala naye chumbani kwangu.” “Kama mkeo?!” “Kwani nimesema ni mwanamke?” “Kwa hiyo hutuamini sisi na rafiki yako wa kiume, unataka ulale naye chumba kimoja, na kitanda kimoja!?” Kidogi akacheka.

“Na hakuna kumuongelesha mama. Mwacheni kabisa. Kwanza nitakuwa nikija naye na kuondoka naye. Hakuna kumsogelea na kumpa wakati mgumu. Ni yatima. Hana ndugu, amefiwa na mtu wake wa karibu ambaye alikuwa kama mume. Alimleta hapa hospitalini.” Akawaeleza kwa kifupi ilivyokuwa mpaka kifo cha Mike.

“Nipo tu kumsaidia maana ni kama amekwama. Na hata akili yake bado haijarudi kuwa sawa. Na ndugu wa Mike wanamsumbua sababu ya mali. Kwa hiyo naomba hapo nyumbani kuwe na mazingira mazuri jamani. Sio kuanza zile tabia zenu za kulazimishia mambo yenu.”

“Sitaki hata mumshauri kitu. Niachieni mwenyewe. Nakwenda naye taratibu mpaka akiwa tayari ataendelea na maisha yake.” “Sawa. Unafanya vizuri kumsaidia.” Akatulia kidogo bila ya kujibu, wote kimya kwa muda, mwishoe akakata simu. Lakini ndio yakawa mazungumzo ya kwanza waliyozungumza angalau na kufikia mwafaka tena baada ya muda mrefu sana.

~~~~~~~~~~~~~~~

INAENDELEA.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment