Baada ya muda akaambiwa amefika. Akamruhusu aingie.
“Naitwa Christopher ni wakili wa familia ya Simba.” “Umemsahau na Kemi.”
Akamuonyesha anamfahamu. Akamtizama kidogo kisha akaendelea. “Lakini hapa
nawawakilisha familia ya Simba, zaidi mdau wa hii hospitali, Love.” Kimya
akimsikiliza.
“Love kama mmoja wa wamiliki
wa hii hospitali na kampuni kwa ujumla, anahaki na mali za hapa. Kisheria
anaruhusiwa kutumia mali zake atakavyo.” Colins akabaki akimwangalia tu.
“Sasa basi, kwa kuwa sasahivi ana uhitaji, anataka
kutumia sehemu ya mali yake na wazazi wake pia ambao ni wamiliki au waanzilishi wa hii kampuni, wanaunga
mkono.” Akatulia akimwangalia.
Akamuona anatoa karatasi kwenye mkoba wake na kumkabidhi,
Colins hakupokea. Akaziweka mbele yake. Kimya akimtizama. “Hizo ni
karatasi zilizowekwa saini na wamiliki wote wanne kwa upande wa Simba
kuidhinisha kutolewa pesa benki. Akiwepo Love mwenyewe, wazazi wake na Loreta.
Hundi itahayoandikwa, itaenda moja kwa moja kwenye kumuwekea dhamana
Love. Atakaposhinda kesi, hiyo pesa itarudishwa kwenye akaunti za kampuni.” “Hapana.”
Akajibu Colins na kumshangaza sana.
“Wewe unakataa kama nani? Maana kama sijakosea,
wewe ni mwajiriwa tu, ila una hisa
baadhi kama Love au Loreta. Hii ni kampuni ya wazazi wenu.” “Kufupisha hiki
kikao ambacho kinanipotezea muda,
nitakujibu mimi nakataa kama nani. Kisha nakuruhusu ukashitaki popote
unapotaka, tutakutana mahakamani. Ila nina uhakika, hutataka kushindana na mimi Chris.”
“Unanitisha wewe bwana mdogo wa juzi tu! Hudhani kwa
mpaka hapa nilipofika nishatishwa
sana na wenye uwezo wao na wanaoogopewa hapa nchini! Acha ubabe wa kitoto.”
Colins akacheka kwa kumsikitikia.
“Acha dharau.” “Nakusikitikia sana Chris. Kama hujajua,
hao unao watetea mpaka kutaka kumdhulumu mtu asiye na hatia, mwenye ile
hoteli, ambaye wewe kwa kupitia Love na Kemi, umemshitaki bila hatia, wamekutoa kafara.” “Acha kuni…” “Unaongea sana Chris, hunisikilizi. Nakwambia
hivi, hao unao watetea, kwa kutaka watu wengine wasio na hatia, walipe
garama yao, nakwambia hivi, wamekutoa kafara.
Umejiingiza pabaya sana, mpaka nakusikitikia.”
“Acha kunitisha mimi. Nafuata sheria. Hakuna mtu yupo na
kosa mpaka sheria iamue. Love na Kemi hawana
hatia. Wewe ni nani mpaka uwahukumu? Na kama huyo mwenye hoteli hana hatia,
basi mahakama itaamua. Usinipotezee muda wangu. Ninachotaka ni hundi.”
“Hutapata pesa hapa.” “Unakataa wewe kama nani!?” “Mimi
kama mmiliki mkuu wa hapa. Na kukusaidia tu, karudishe majibu kwa
waliokutuma kuwa, mbali ya kwamba nina mkataba wa ajira ya hapa,
basi wajue, kwa sasa mimi nina hisa kubwa sana kuzidi kila mtu kwenye
hii kampuni. Nina miliki zaidi ya asilimia 60 kwenye hii kampuni
na katika hao uliowataja hapo juu kama wamiliki hapa, Loreta si
mmoja wao. Hana hisa hata moja hapa.” Kabla hajajibu akaendelea.
“Kwa kifupi ili usizidi kunipotezea muda, hii kampuni ni
kama yangu. Na unapozungumza na mimi, jua nina zungumza kwa niaba yangu mimi mwenyewe kama mdau mkuu, wazazi wangu na dada
yangu, ambao wote hao pia na wao ni wadau hapa. Kwa kukusaidia tu, sisi kina Komba ndio tuna kauli ya mwisho
ya nini kiendelee kwenye hii kampuni.”
“Jambo la msingi nataka usisahau. Usiwahi kurudi
hapa kama unaingia chooni. Weka miahadi. Upewe muda wa kuja. Kama ni
karatasi, huna haja ya kuniona mimi. Mwachie sekretari. Na nilikuwa nikikuonya,
sijui kutisha kama wengine. Siku ingine utakapoingia hapa kama leo, jua
nitakutoa na polisi. Uwe na siku njema.”
“Haiwezekani!” “Wewe si umesema unakwenda na sheria? Acha
kujiliza hapo kama mtoto mdogo wa kike, nenda kanishitaki,
tukutane mahakamani. Vinginevyo acha
kunipotezea muda kwa mambo ya kijinga. Umeona wapi mambo yanafanyika kama hivyo
unavyotaka kufanya wewe na hao walio kutuma!?”
“Eti kampuni iliyo na wabia kibao, eti baadhi tu
ndio wanaidhinisha pesa itolewe benki! Tena kwa matumizi binafsi! Mpaka
unanitia wasiwasi na kiwango chako cha kufikiria na utendaji wako kazi! Unakimbizwa
kama upepo tu!” “Najua ninachokifanya.” “Una uhakika?” Colins akamuuliza kwa kumdhihaki.
“Nakuuliza wewe, unao uhakika?” “Ndiyo.” “Unajua hata
sheria na mikataba ya hii kampuni au umekurupuka tu nakuja hapa kama
kondoo unayepelekwa machinjioni, tena siku ambayo hata si ya kazi!?”
Kabla hajajibu, akamfukuza. Alikuwa na hasira naye kupita kiasi. Mbali ya
kumsaidia kumuweka Kemi uraiani, akakumbuka unyama aliomfanyia
Zulfa. Hapo alikuwa na hasira naye kupitiliza.
“Kwanza toka hapa ofisini kwangu. Unanipotezea
muda.” Akawa ameshabonyeza kengele aliyokuwa imejengewa kwa kufichwa chini ya
meza yake, maalumu kwa kuita walinzi.
Chris akaanza kugomba. Akitetea haki ya familia ya Simba
kwa jazba walinzi wakaingia wakamkuta ameng’aka, anawaka kwelikweli kuwa
Colins hajui anachokifanya, na atamuonyesha yeye alizaliwa kabla yake na
anajua anachokifanya. Colins kimya akimtizama pale mbele ya wale askari wake
ili kutoa sababu ya kukamatwa.” Askari akamsogelea.
“Huwezi kutoa vitisho ndani ya ofisi ya mtu.” Kwa kuwa
alikuwa ameshapandwa na jazba, akataka kumjibu yule askari, wakamuwahi na
kumvuta nje.
“Hakikisheni mnapata taarifa zake kamili, mziandike
na apewe onyo kabisa.” Akarushia neno wakimtoa pale. Hapo akawa
amemtibua Colins. Akajiapia kutumia nguvu zote, kumfikisha magotini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akatafuta picha zote za Zulfa akiwa peke yake. Binti
aliyekuwa naye kwenye mahusiano. Akaziweka pamoja, kisha akaingia kwenye uwanja
wake wa mapambano, hiyo laptop yake, akamtumia kwa email kama salamu tu. Akahakikisha haachi email yake wala ip address yake.
Ili asijue inapotoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa amerudisha akili kazini na akili imeshatulia kutoka
alivyotibuliwa asubuhi hiyo, hata asijue ni saa ngapi, akasikia hodi taratibu
kama mtu asiyetaka kumsumbua. Kuangalia ni Kamila. Akatoa tabasamu kwani
alikuwa amebeba chakula. “Nimeambiwa leo una kazi nyingi. Sitakuongelesha.
Nakuachia tu chakula.” “Usijali. Ingia. Nimekua na mambo mengi lakini naweza
chukua mapumziko mafupi.”
Akaweka kila kitu pembeni na kugeuka vizuri. “Vipi naona
mambo yako si mabaya?” “Nilikuwa jikoni na wapishi. Wazee wazuri sana.
Wastaarabu, wacheshi na wachokozi.” Colins akacheka.
“Wana maneno mengiii!” “Ndio vizuri. Na chakula kinanukia
vizuri! Asante.” “Nimejua hujala, nikaomba kidogo cha wagonjwa,
nikakutengenezea pembeni.” Akakipokea na kukiangalia. “Unajua kuweka chakula
kwenye sahani! Mpaka kinavutia.” “Asante. Nikuache ule. Nisikuingilie.” “Hamna
shida. Nimefurahi umechukua hatua Kamila. Itakusaidia.” Akamuona ameanza
kuingiwa hofu. Anabadilika rangi. “Ni nini? Niambie tu.” “Kula kwanza, nitakwambia
baada ya kazi. Acha nirudi kule kazini.”
“Kamila!” Akamuita kabla hajatoka, akageuka. “Ni nini?”
“Nataka kukuomba kitu lakini kinaweza subiri.” “Nini? Niambie tu,
usiogope.” “Waliponituma nipeleke vyakula vya madaktari, wakati napita, niliona
chumba cha wauguzi. Wanabadilishia nguo. Kuna kitanda, nilitaka.” Akasita.
Akamuona anaanza kutetemeka mikono. Ashapaniki.
“Niangalie Kamila. Unaweza kuzungumza na mimi kitu chochote. Na kama
kitashindikana, nitakwambia tutafute suluhu nyingine. Kwa hiyo niambie tu, usiogope.
Niambie.” “Naomba nikae hapo kwa muda wakati najipanga, kuliko kukaa kwenye
kile chumba cha wagonjwa. Wameniambia ni garama sana! Halafu kinanifanya
nijisikie kama mgonjwa!”
“Sawa. Japo garama isikutishe. Ni wagonjwa
wachache sana wanamudu vile vyumba. Kwa kuwa ni kweli ni garama, ndio maana
unaona kipo wazi mpaka sasa. Ila kama kina kufanya ujisikie kama mgonjwa, hilo linaeleweka.”
“Nashukuru. Na nakuahidi nikijiweka tu sawa, nitaondoka.”
“Sawa.” Akaitika hivyo tu kwa kifupi na kuanza kula. “Unaondoka saa ngapi?”
Colins akamtizama. Akameza na kumjibu. “Inategemea. Vipi?” “Nauliza tu.” Kisha
akatoka. Alimgundua ni mtu aliyejawa hofu, akaona amchukulie taratibu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika majira ya saa 3 usiku, akashituliwa na ujumbe
kwenye ile simu yake mpya ambayo Kamila humtumia jumbe Mike, na kushindwa
kabisa kugawa hiyo namba na kuiacha kwa ajili hiyo tu. Akaacha kila kitu na
kuanza kusoma. ‘Kifo chako kimeacha pengo ambalo sijui litakuja kuzibwa vipi hapa
duniani! Ni wewe pekee ndiye unanielewa na kuweza gawa muda wako kwa ajili
yangu. Nipo mpweke Mike! Mungu anajua jinsi ninavyojisikia.’
‘Natamani
urudi hata kwa muda mfupi tu, unisaidie kimawazo. Nimekwama, naogopa
sana. Najaribu kuchukua hatua, kama alivyonishauri Colins. Nimeambiwa ndio jina
lake. Ila yeye hajaniambia. Kumbe yeye ndio kiongozi mkubwa wa hii hospitali
nzima! Wamenimbia anamamlaka yote, kwa hiyo anamajukumu mazito, siwezi kuwa
nikienda ofisini kwake kila ninavyo jisikia. Siruhusiwi tena. Nimekwama.’ Colins akashituka asijue ni nani amemkataza asimuone!
Akagundua hata hakurudi kuchukua vyombo.
Akajaribu kuvuta kumbukumbu kama kweli hajawahi
kujitambulisha kwake! Akagundua mazingira hayajawahi kuruhusi, wakati wote wamekutana
kukiwa na mazingira ya hekaheka. Akafikiria kidogo, akaendelea kusoma. Maana
ulikuwa ujumbe mrefu sana.
‘Huwezi
amini Mike, nimeomba kuishi hospitalini! Lakini usiwe na wasiwasi, wamenipa na
kazi. Nitatoka tu hapa. Halafu usiwe na wasiwasi na hawa ninaofanya nao kazi
sasahivi. Ni watu wazima. Wacheshi na wanajiheshimu. Hawana mambo mabaya, na
wanataka kesho mimi ndio nipike. Nimefurahi! Narudia kazi yangu ninayoipenda.’
‘Luca amenipokonya
pete uliyonivisha na gari. Wamenichukulia nguo zangu zote. Lakini usiwe na
wasiwasi. Nipo tu sawa nitaenda kununua nguo zingine, bado nina akiba. Nishauri
nikaishi wapi baada ya hapa. Nitumie tu hata ishara. Sijui kabisa wapi patakuwa
salama. Tungekuwa wote najua ungeniambia nisiogope, kwa kuwa tupo wote. Popote
tutaishi. Ila naogopa vibaka njiani. Nisaidie.’
Alipomaliza tu kusoma akatoka kama akimbie. Akaanza kumsaka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akaenda mpaka kwenye chumba alichoomba aishi, japo hakuwa
ameingia ndani, lakini kulisikika na hekaheka! Kuingia na kutoka kusiko isha
kwa kila muuguzi wa kike. Akajiuliza huyo Kamila atalalaje humo, na kukosa
jibu. Akazunguka mpaka kwenye chumba alichokuwa amelazwa, akaambiwa kule
alishatoka na kuaga mapema sana. Ndipo wazo likamjia kuangalia jikoni. Akatoka
hapo kama akimbie tena, safari hii akiwa na uhakika atakuwa huko.
~~~~~~~~~~~~~~~
Na kweli akamkuta amekaa peke yake ametulia kama yupo
darasani. Hata hakujua kama Colins ameingia. “Mbona umekaa huku peke yako?” Akashituka
sana. “Samahani, sikukusudia kukushitua.” “Hamna neno. Nimekaa tu. Nasubiria
kule kutulie ndio niende nikalale.” “Hapana. Hutalala pale.” Akaingiwa na
wasiwasi.
“Kwenye kile chumba ndio sehemu wanabadili nguo na
wengine kupumzika kwa muda mfupi ili kuendelea na kazi. Kwanza sidhani kama
utapata kitanda wazi.” Akamuona amekosa raha. “Twende tukatafute sehemu ya
kulala kwa muda wakati tukitafuta sehemu ya kudumu.” “Wameniambia una mambo
mengi! Sitaki kukusumbua.”
“Ni nani amekwambia hivyo?” “Sekretari wenu. Aliniona
napita na chakula kuingia ofisini kwako, nilipotoka akaniita. Alikasirika
anasema namfanyia dharau. Niliingia bila ya kumuomba yeye ruhusa. Mimi sikujua!
Ndio nikamuomba msamaha. Ila akasema nisirudi tena. Kama nimesaidiwa
mara moja, niwe na shukurani nisiendelee kusumbua.” “Pole, lakini usijali.
Hunisumbui. Twende.” Wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa na mengi yanayoendelea kwenye maisha yake, bado Colins anajiona
anawajibika kwa Kamila. Ni Nini Kitaendelea kwao na Kamila mwenye Mike nyingi
mdomoni?!
Jelini, Ezra, Junior na Emelda yao?!
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment