“Nisikilize Kamila. Eti mimi naona nikinyume na hivyo!
Nisikilize tu tufikirie pamoja. Usilie, nisikilize tu.” Akamfanya amsikilize.
“Wewe umesema Mike alikupenda sana. Ulimuona akiishi kwa juhudi zake na
kufikiria. Kwa nini hayo yote usiyaenzi kwa kupambana uishi vile angependa
uishi kuliko kutoa maisha yako ambayo yeye aliyahangaikia mchana na usiku ili
uwe na furaha? Kuutoa uhai wako kwa namna hiyo ni kupuuza juhudi
za Mike.” Akamuona hapo anasikiliza.
“Kuanzia sasa, ishi kama mtu uliyependwa sana na
kuonyeshwa njia maishani. Sidhani kama Mike alikutoa sehemu moja ili uangamie!
Maana kwa kujiua ujue unamkosea Mungu, na hawezi
kuja kukuweka sehemu moja na mtu kama Mike. Huko unakofikiri unamfuata
Mike, hutamkuta. Mungu atakupeleka pabaya ambako utakutana na uasi
mbaya zaidi ya huu unaoukimbia hapa duniani, na kamwe mtu mwema kama
Mike hutakuja kumuona tena maishani.” Akamuona anaanza kutulia kabisa kama kimeanza
kuingia akilini.
“Kama kweli unampenda Mike, anza kuishi kama yeye ili
ukiondoka hapa duniani, ukakutane naye huko.” “Sijui pakuanzia!” “Unakumbuka jana uliomba kazi na ukapata?” Akakubali.
“Leo ulitakiwa kuanza kazi, lakini umelala hapa, ukijaribu kuharibu
juhudi zote za Mike! Sidhani kama ikitokea leo Mike anarudi, anakukuta na hali
hiyo, atafurahia!” Akakataa akilia.
“Wewe unakipaji kikubwa sana. Hicho kikusaidie
kuendesha maisha yako. Acha kulala kwenye makochi, au kwenye gari. Maisha
aliyokuachia Mike, sisemei nyumba na gari, hapana. Ramani aliyokuachia ya
maisha, hiyo ndiyo nazungumzia, ukipambana, unaweza kuja kuyaishi. Tena vizuri tu.”
“Na auhitaji kujua kila kitu kwa wakati mmoja. Chukua
hatua moja moja kama ulivyosema jana usiku. Utafanikiwa tu.” Akamuoana
anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Akamuona anajishika shingoni.
“Panauma?” Akamuuliza kwa kujali. Akatingisha kichwa
taratibu kukubali. “Moyo wangu unauma zaidi. Natamani kama ningeondoka na
Mike hapa duniani.” “Pole sana. Pole Kamila.” Akajifunika na
kuendelea kulia kwa sauti ya chini, ila kwa uchungu sana. Akakumbuka kilio kama
hicho kukisikia kutoka kwa Jelini. Akamsogelea pale kitandani, tena akakaa
kabisa.
Alikuwa akigugumia kwa uchungu kana kwamba anakatwa
sehemu. Akamtoa mkono ndani ya shuka
akamvuta karibu yake. “Sijui unavyojisikia. Ila ninajua kwa hakika, ‘it’s
going to get better.’ Nakuahidi hivyo. Jipe tu muda. Umesikia?” Akatingisha
kichwa kukubali.
“Pata muda wa kupumzika, kisha utoke kitandani, nenda
kule jikoni. Nimekuona jana. Ni kitu unafurahia sana kufanya. Ukiwekeza mawazo
yako hapo, utajikuta akili inawaza mambo sahihi na utaweza tu. Sawa?” Hapo
anazungumza naye akiwa amemshika mkono. Akambembeleza mpaka akatulia.
“Tuone shingoni.” Akawa
anasita. “It’s okay. Nionyeshe tu.” Akamuona machozi yanamtoka tena.
Akajisahau akamfuta kwa upendo. “Nionyeshe.” Akajifungua amtizame shingo nzima.
“Nitaulizia kama kuna dawa ya kupunguza maumivu.” Akatingisha kichwa kukubali
na kurudi kujifunika. Akabaki akimwangalia mpaka akajishitukia mwenyewe.
“Acha nikuulizie dawa.”
Akaona atoke tu. Baada ya muda akarudi. Macho yakagongana. “Najua hunifahamu
Kamila. Lakini ni sawa nikuombe uniahidi kitu?” Akavuta tena pumzi kwa nguvu na
kuzishusha taratibu kama anayejaribu kutulia, kisha akatingisha kichwa
kukubali.
Akarudi kukaa tena na
kumshika mkono. Kamila akajiweka sawa. “Niahidi hiki ulichokifanya leo, yaani
kujidhuru, hutarudia tena.” Akaanza kulia tena kwa uchungu.
“Tumekubaliana utamuenzi Mike kwa kuishi kile alichotamani kuona kwako.
Si ndiyo?” Akatingisha kichwa kukubali.
“Nina hamu naye! Hakika nina hamu naye sana!
Mungu anajua jinsi ninavyomuhitaji. Mike ananipenda sana jamani, hakuna mwanadamu
atakuja kunipenda kama Mike! Sijui maisha mengine bila yeye Mike. Moyo wangu unauma
sana. Nimejawa hofu, naogopa, nahisi nitakosea sana. Sijui maisha yanakuaje
bila Mike!”
“Nilikuwa nikivumilia hata pale ninapoishi
sasahivi nikijua atarudi tu. Siamini kama ndio basi tena, jamani!” Akalia hapo kwa
uchungu kisha akaongeza. “Ila sitarudia tena kumfedhehesha Mike wangu. Sitajidhuru tena.” Akamfuta machozi. “Usiwe na haraka.
Hatua ndogondogo kama mtoto. Endelea kupokea kila siku kama ulivyosema jana.
Hata sasahivi usiache. Fanya hivyohivyo.” Akakubali.
“Pumzika. Watakuja kukuletea dawa ya kukupaka hapo
shingoni. Kisha ulale kabisa. Ukiamka unaweza kwenda jikoni. Si unapakumbuka?” “Nafikiri.
Nikishindwa nitauliza.” “Au nipigie simu, nitakuja kukufuata
nikupeleke. Wana maagizo yako. Ukifika tu, watajua ni wewe. Usiwe na wasiwasi.”
“Asante.” Akashukuru na kutulia. Colins akaona aondoke tu.
“Nitakuwa ofisini. Ukikwama popote usisite kunitafuta. Vinginevyo nitakuona
baadaye.” Akatoka.
Dhahabu Inapopitishwa Kwenye Moto.
Jelini alivyokuwa
amepania hiyo siku ya mwenzie! Alihakikisha anapendeza. Na kwa kuwa alijua
wangeanzia kanisani, basi akambebea nguo nyingine. Nzuri sana inayoendana na
kaumbile kake na mpambaji, Emelda hajui.
Wakati wanamaliza
kikao, kina Junior wanatakiwa kanisani wajiandae na ibada ya sifa, akamwambia
Junior amwambie Emelda amfuate garini. Bila kujua akamfuata. “Sasa wake za twins,
kazi yetu ni kupania kupendeza.” Emelda akaanza kucheka.
“Sasa mbona hata
huulizi kikao kiliendaje?” “Tushakubaliana kuna harusi, hayo mengine
stori za baadae. Ingia garini, badilisha nguo, upambwe. Sitaki mazoea na
Junior. Sio kwa sababu amekuona asubuhi, basi ajue ndio utakua hivyohivyo!”
Emelda kucheka meno yote nje.
“Gauni zuri sana Jelini!
Asante kipenzi.” “Sasa ukichanganya na kaumbile kako, rangi! Mate
yatamtoka Junior.” Kazi ya kumtengeneza ikaanza wakiwa wamejificha nyuma
kabisa, wamekaa kiti cha nyuma, Jelini maneno mengi kiti cha mbele cha dereva,
mwenzie anacheka mbavu hana.
~~~~~~~~~~~~~~~
Waliingia kanisani
baada ya kipindi cha sifa kuanza. Kwa hakika Emelda alionekana nadhifu. Mchungaji
alikuwepo kwenye kupiga gitaa la bezi, Junior ndio muongoza sifa, safari hii
Ezra alikuwa akipiga kinanda. Mama mchungaji alikuwa akicheza mpaka jasho.
Ungejua Junior ndiye anayeimbisha. Na yeye alizijulia nyimbo anazopenda mama
yake. Basi lazima aziimbishe hizo kama kuchanganya ni chache tu. Basi hapo
ibada hukamilika kwa mama yake. Na akimuona mumewe anapiga gitaa, basi vigelele
vyake husikika, mwanzo mwisho.
Muda aliokuwa
akingojea Emelda kwa maombi akifunga bila dalili za kuja kujibuwa, ukawadia.
Ila akitamani sana kujua aina ya pete atakayovalishwa. Mchungaji akasimama.
Akatoa matangazo yote. Kisha akafika kwenye wakati wenyewe.
“Kuna maombi
unaomba kwenye umri fulani. Na unamsihi Mungu, yatokee ukiwepo hapa
duniani, isiwe kama ahadi ya Ibrahimu ya uzao mwingi lakini akafa hajaona.”
Kanisa zima kimya.
“Sasa na mimi Mungu
ameanza kunijibu na kunipa fulsa ya kuanza kushuhudia kwa macho. Ezra na
Junior njooni hapa mbele.” Wakasimama na kukimbilia mbele. Lakini jinsi
alivyorudi Junior, amebadili nguo, amependeza kirasmi kama mwenzie Ezra, watu
wakahisi jambo. Maana alivaa kitanashati kijana wakati akiimbisha
ili kuweza kucheza kwa uhuru wote.
“Hawa wawili bwana!
Wanaweza kukuchonganisha na Mungu hivihivi!” Watu wakacheka. “Unaweza
ukawaombea jambo. Likifanikiwa kwa mmoja halafu mwingine hajafanikiwa,
ujue kwao wao hayo maombi hayajajibiwa bado. Unabakiwa na deni la kuendelea
kuombea. Hapatatulia mpaka wote wapate.” Watu wakazidi kucheka wengine
wasielewe ila kuhisi.
“Sasa siku chache
zilizopita, Ezra alijibiwa.” Mchungaji akaendelea. “Jelini mama upo wapi?”
Akasimama cheko, meno yote nje! “Njoo mama.” Alivyokuwa amependeza, naye Ezra
hana dogo, akaenda kumpokea na kumshika mkono kabisa, watu wakipiga vigelegele
mpaka juu madhabahuni.
“Sasa msifikiri
kwangu hapo nilimaliza kazi! Nilikuwa na deni nikikumbushwa kuombea mchana na
usiku, mpaka na Junior naye alipojibiwa.” Wengine wakashangaa.
Maana huyo Junior ametoka kuvunja uchumba na kutangaza mpya ndani ya juma moja
tu! Mpaka Hope akashangaa na kutaka kumjua huyo mchumba mpya!
“Sasa safari hii
nimewaambia hata wao. Zege hailali. Hawa wachumba tutakao ombea
safari hii ndio kina mama wa wajukuu zangu!” Watu vigelegele haswa, zaidi mama
mchungaji.
“Leo Junior anachumbia,
na tangazo lao la kwanza la ndoa linatoka leoleo. Wote wanne. Kwa hiyo
mwenye kipingamizi na wao, awahi haraka na ushahidi wa kueleweka. Vinginevyo,
jumapili ya nne kuanzia sasa, nawatoa hawa wanne wote sokoni.” Kelele na
miluzi kutoka kwa vijana.
“Nitasimama hapahapa, niwatamkie baraka, mpaka
kifo kiwatenganishe, nibakie na kazi ya kuombea wajukuu. Hakuna kurudi
nyuma tena.” Vigelegele.
“Haya Junior, kazi
kwako.” Wote macho kwa Junior. Wakamuona anavuta pumzi kwa nguvu kama anayetaka
kufanya kazi nzito. Watu vigelegele wakijua ndio anachumbia sasa. Ezra na
Jelini wanamcheka. “Jikaze.” Ezra akamrushia neno. Akatingisha kichwa akicheka
kisha kuchukua kipaza sauti na kuanza kutoka hapo jukwaani, akiongea.
“Kuna watu hupita
kwenye maisha yetu kutukumbusha sisi ni wa kina nani, kisha wanaondoka.
Wanaweza kukuacha na maumivu lakini wanakuwa wametimiza kusudi lao na hufanyika
msaada kwenye maisha yako yote.”
“Halafu kuna viatu vya watu wengine, sijui
Mungu aliumba vipi miguu yao! Yaani viatu vyao, huwa vinawaenea
wao wenyewe tu. Hata ukijaribu kumvalisha mtu mwingine, havienei.
Unabakia kuwaachia wengine malengelenge ya miguu au madonda kwa kulazimishia
viatu visivyo vyao.” Hapo Junior anaongea huku anasogelea upande aliokuwa
amekaa Emelda, kila mtu akitaka kujua kwa hamu huyo anayekwenda kumchumbia.
Lakini Emelda, msichana wa kazi za ndani, hakuna hata mmoja
aliyemdhania.
“Imenichukua muda,
nikiwa na hicho kiatu mkononi, nikimpita mwenye nacho, mpaka
Mungu akanihurumia kama Hajiri kijakazi aliyezaa na Ibrahimu, baba wa
imani, alipokuwa na kiu kali jangwani, akijua mtoto wake atakufa tu,
akiwa anamkimbia Sara mke wa Ibrahimu. Kumbe hakuwa mbali na maji, ila
hakuwa ameyaona. Macho yake yalifungwa na mengi, mpaka alipoonyeshwa
na malaika.” Vikasikika vigelegele vya mama mchungaji.
Bado Jelini na Ezra
walikuwa wamesimama mbele madhabahuni, Ezra amemshika mkono Jelini. Wamependeza
haswa. Wapiga picha na wachukua video, walikuwa wakimfuata Junior kwa karibu tu
kupata tukio zima.
Akaenda mpaka
alipokuwa amekaa Emelda, akampita mama yake na mdogo wake akaenda mpaka
alipokaa yeye, akapiga goti mbele yake watu wakahamaki wasiamini! Kwamba
Junior anaoa msichana wa kazi wa nyumbani kwao!
Akamshika mikono yote
miwili. “Nakupenda Emelda. Na naomba uwe mke wangu.” Hivyo tu Emelda
akihisi yupo ndotoni. Akatingisha kichwa kukubali. “Niambie kwa maneno
basi!” Akaongea kwa kubembeleza. “Wewe unajua ninavyo kupenda Junior!” Wengine
wakabaki mdomo wazi, wengine vigelegele wakishangilia. Akambusu
mikono yote miwili kwa muda mrefu tu kwa hisia zote, watu wakishangilia, ndipo
akamvalisha pete, na kusimama.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hata Hope hakuamini!
Junior hakumvalisha pete kwa namna hiyo. Kwanza walikwenda naye kwa sonara
kupimisha pete yake. Ilikuwa nzuri sana na ilimgarimu sana Junior. Hakutaka
kuisubiria. Akaenda ifuata yeye mwenyewe punde sonara alipowatumia ujumbe kuwa
ipo tayari.
Akaanza kuivaa kabla
ya jumapili, akitangaza ufahari kazini na kwa mashoga zake, ndipo jumapili
yake wakaombewa! Leo Junior amepiga goti na kutangaza anampenda Emelda
na Emelda anasema Junior anajua ni kwa kiasi gani anampenda! Ndoa
ndani ya majuma manne! Upendo huo ulianza lini? Kiroho kikaanza kudunda
hapo alipokuwa amekaa. Hasira na wivu.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Haya naomba mje hapa
mbele.” Nyimbo zikaanza kupigwa watu wakishangilia. Jelini na Ezra wakaenda
kuwapokea wakiwapongeza mpaka kukumbatiana wao wote wanne. Hakika walipendeza
na kuvutia haswa. Watu walicheza hapo wakishangilia, wengine wasiamini.
Jelini akamvuta mkono kuona pete. Wote
wakacheka kuona zinafanana. Emelda kama ya Jelini! “Hakika mimi sijawapatia
wenzenu!” “Na ibakie hivyohivyo Jelini. Kwanza ulikuwa ukiwatafutia
wapi hao wenzetu!?” “Mwaya Junior naye! Si usemi tu!” Ezra na Emelda mbavu
hawana. Wakicheka hapo mbele, watu wakiwashangilia.
“Yaani hawa wanne
wakirudi kuja kusimama tena hapa mbele kama hivi walivyo, jamani ni kuwafunga
pingu za maisha na kubariki watoto wao. Mmesikia Junior na Ezra! Hili zoezi
Mungu asaidie lifike mwisho.” Wengine wakazidi kucheka na wao wakacheka
wakitingisha vichwa.
“Safari hii muoe.”
Akaweka msisitizo akiwa anasikika kwenye
kipaza sauti. “Tunaoa baba mbona hivyo!?” “Nataka watu wapumzike!” Vigelegele
wao wanacheka. Hao wawili wote walishachumbia kwa mara ya kwanza, hiyo
ya pili.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Jamani! Junior anaoa
binti yangu.” Mchungaji akafanya washirika watulie. “Maana hawa waliondoka,
tukabakiwa na viziwanda wawili. Noah na Emelda, wakinyang’anyana ziwa, sasa
naona amebakia Noah peke yake!”
“Hongera kwa kujitunza
Emelda binti yangu. Mungu wa
mbinguni akubariki wewe na uzao wa tumbo lako.” Akaita watumishi wengine
pale mbele akataka na wao wapige magoti, kina Ezra nao pembeni.
“Watoto wako na watoto wa watoto wako wakaitwe heri.
Ubarikiwe uingiapo na utokapo kwa vile ulivyotupenda, kutuheshimu, na kututunza
mimi na mke wangu, na watu wa nyumba kwangu. Tumbo lako libarikiwe, litoe
watoto bora, watakao kutunza wewe na mumeo mpaka kifo chenu.”
“Nakataa uharibifu
wa mimba. Kwako, Jelini na watoto wa watoto wenu. Utasa usitajwe
kwenu. Kisiwepo kifo cha bahati mbaya katika nyumba zenu na nyumba za
watoto wenu.”
Bwana mchungaji aliomba huyo, mpaka ibada ikageuka ikawa ya maombi.
Gafla nguvu za Mungu
zikatawala kila mmoja akiguswa na hayo maombi ya mchungaji kwa Emelda. Na
wenyewe wakaanza kuomba. Wakageuka kuungana mkono na mchungaji kumbariki huyo
Emelda. Ungejua huyo binti amegusa moyo wa mchungaji. Alitamka baraka
bila ya kumpunja.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mungu hanaga kikao
wala wakumuuliza ni kwa nini anapofanya jambo lake. Siku hiyo Emelda alilipwa
na Mungu hadharani, hata mama yake asiamini
kama ni mwanae! Alivyo badilika Emelda, ungedhania alizaliwa kwenye neema, kumbe Mungu alimtumia kunguru wake,
ambaye ni Jelini aliyemuumba na moyo mzuri, ampige msasa.
Kwa muda mfupi tu,
Emelda alikuwa nadhifu, na neema ya Mungu ikawa juu yake. Hana anachoweka mwili
mwake kisivutie! Fumba na kufumbua, akawa mama mjengo. Jumba la Junior lililokuwa
likimtoa roho Hope, leo fukara Emelda ndio atamiliki!
Akiwa anaishi kwenye
nyumba ya tembe, akidharaulika na kunyanyaswa huko kijijini kwao, huku
mjini Mungu alikuwa akimuandalia makao nadhifu na ya hali ya juu sana.
Lakini ilikuwa lazima ampitishe kwenye moto kwanza ili kung’arisha
dhahabu yake.
Kupita kuwa mtumwa wa
kudharaulika, kutukanwa na kudhulumiwa mpaka kufikishwa
pale Mungu alipo muandalia.
Mwanaume mwenye hofu
ya Mungu, msomi, mwenye pesa na bado anampenda haswa. Kwa
hakika dhahabu iliyopitishwa kwenye moto, siku hiyo iling’aa.
Je, angekimbia majaribu yake? Angekimbia
pale Esther alipokuwa akimnyanyasa? Pengine leo asingekuwa ameinuliwa
hadharani! Emelda akawa amemaliza mitihani yake ya maisha kwa kipindi
hicho, Mungu anampa cheti hadharani. Ilikuwa furaha ya ajabu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini kinachokuumiza na kukufanya ukimbie?
Yapo majibu mengine kutoka kwa Mungu, yamefungamanishwa na majaribu.
SIMAMA ILI UPAMBANE, UVUKE. Kukimbia
ni kujichelewesha.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment