Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 14. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 14.

Mapigo ya Colins yalikuwa yakienda kasi, akili imeganda kwa muda, bado simu sikioni. Akitamani kuwe na taarifa ya tofauti alfajiri hiyo ya siku ya jumapili. “Masikini Kamila!” Akajikuta akiongea kwa sauti. “Bosi!” Upande wa pili akasikika kama anaye muwahi asikate. “Nipo! Ila nasikitika tumeshindwa kuwa msaada kwake.” “Hapana bosi wangu. Tulimuwahi. Ndio dokta ametoka sasahivi kumalizana naye. Amerudi kulala.” Zilikuwa taarifa zilizo amsha nguvu ya ajabu kutoka kwenye mwili wa Colins uliokuwa usingizini.

 “Nakuja huko sasahivi. Tafadhali uwe unapitia hapo mara kwa mara.” “Nitafanya hivyo. Japo amepewa dawa za usingizi, sasahivi amelala kwa hakika. Na sasahivi wote tupo naye makini.” Na kweli safari hii akasikika kwa sauti ya kujali sio kama mwanzo walivyokuwa kwa huyo Kamila. Akashukuru kama anayehusika haswa na huyo mrembo, na kukata simu na kuanza kujiandaa kwa haraka kisha akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Moja kwa moja akakimbilia alipolazwa Kamila. Akasimama akimtizama vile alivyokuwa amelala pale. Kwa jinsi alivyokuwa mweupe, alama nyekundu za alipojinyongea zilibaki kuonekana bayana shingoni kwake. Akamuhurumia sana.

Akavuta kiti na kukaa hapo pembeni yake. Akaona haitoshi, akamshika kabisa mkono! Akaanza kuuminya, mwishoe akajishitukia. Akajua atafumwa na manesi. Akamuachia na kujivuta pembeni kidogo. Alikaa hapo mpaka majira ya saa moja asubuhi.

Akakumbuka kwanza ilikuwa siku ya jumapili. Yeye ni mkristo, tena ngazi ya juu sana hapo. Wote watamshangaa kuweka kituo kwa mgonjwa mmoja tu, muda huo na siku kama hiyo ambayo angalau basi angeanzia kanisani kabla ya kazi na si wodini kwa Kamila. Akatoka kwenda ofisini kwake.

Kanisani.

Ilipotimu majira ya saa moja kamili, familia ya mchungaji wote akiwepo Emelda walishakuwa wamewasili hapo ofisini kwa mchungaji. Esther hakuwa amefika bado. Baba yake akampigia. “Upo wapi?” “Ndio naegesha gari hapa kanisani. Nakuja baba!” Akakata.

Baada ya muda akaingia hapo akiwa amependeza haswa, akitangaza utajiri na neema ya maisha. Utulivu usoni hana baya na mtu. Akawatizama wote aliowakuta pale, akawasalimia na kukaa.

“Unaendeleaje Esther mwanangu?” Mama yake akaanza. “Vizuri japo sijategemea kuulizwa! Maana tokea jana simu mnazonipigia ni za amri tu! Kijeshi bila salamu.” “Mama yako alikupa taarifa za kuchumbia kwa Junior leo. Si ndivyo?” Baba yake akamuuliza bila ya kujibu malalamiko yake. “Ndiyo.” “Ulimwambia nani?” “Edwin.” Akajibu bila hofu, wote wakabaki wakimwangalia kwa mshangao.

“Kwani vipi?” “Sikukwambia mimi kama ni siri!?” Mama yake akamuuliza akimshangaa. “Ulisema ni siri, Emelda asijue. Sasa kwani Edwin ambaye ni rafiki yangu mimi ni Emelda!?” Kaka zake wakabaki wakimtizama kwa masikitiko.

“Umeingiwa na nini Esther mwanangu wewe!?” “Kwani mimi kosa langu hapo ni lipi!? Mbona kama mnanipania tu mimi kila wakati?!” Mara mlango ukagongwa, wakaingia wale wazee waliokuwa wakimuombea Edwin pamoja na mchungaji. Wakakaribishwa na kukaa. Baada ya muda mfupi na Edwin naye akaingia akiwa na sura ya tofauti si waliyomzoea nayo. Na yeye akaonekana amejipanga vilivyo.

Wakafungua kwa maombi, mchungaji akaanza kikao. “Nimewaomba mfike kwa sababu tulianza jambo, Edwin akiwa ametushirikisha kwa heshima. Sisi.” Akijionyeshea yeye na wale wazee wengine.

“Alitaka tumuombee kwa ajili ya kutaka kumchumbia Emelda.” Mchungaji akaendelea. “Sasa kwa kuwa alituamini sisi kama viongozi. Naomba kwa heshima kabisa, nimpe nafasi azungumze juu ya hilo. Maana ukweli tuliomba hata na yeye akiwepo. Sasa baada ya hapo, ni nini kiliendelea?” “Junior amenipora mchumba wangu.” Akajibu kwa jazba na kuchanganya wale wazee walioomekana hawajui kinachoendelea.

“Kumbe mwenzetu ulishajibiwa, halafu hukurudisha majibu, ukatuacha sisi tunaendelea kuomba!?” Mzee mmoja akauliza kwa utani kidogo. “Hilo swali ni la msingi japo najua wewe hujaona uzito wake. Na ndio sababu tupo hapa leo. Tafadhali Edwin jibu.” Edwin akaanza kwa jazba kali.

“Haikuwa siri kabisa. Hata Esther ni shahidi yangu kwamba mimi ndiye niliyekuwa nikimtunza Emelda, wakati Junior akiendelea kuchumbia wanawake wengine! Alipoona Emelda niliyekuwa nahangaika naye amependeza ndio tamaa ikamuingia, akahamia kwa mchumba wangu.” Wote kimya wakisikiliza.

“Anatumia cheo cha baba yake vibaya. Akichumbia mabinti hapa kanisani na kuacha. Leo mimi niliyejitunza na kubakia na mchumba mmoja tu, amenipora!? Hakika sikubali.” “Kidogo mnanipoteza jamani!” Mzee mwingine akadakia.

“Hivi huyu Emelda tunayemzungumzia sio yule binti wa mama mchungaji?” “Ndiye huyohuyo na ni huyu hapa.” Mama mchungaji akamuonyeshea wote wakamgeukia. "Ewaa! Kumbe mwenyewe yupo! Sasa kwa nini ni kama tunamzungumzia kama hayupo!?” Akaongeza.

“Ni lini wewe ulimchumbia huyu binti!? Kwa hakika mimi sina taarifa!” Akauliza swali kiuungwa tu. Wote wakamgeukia Edwin. Aliongea mengi sana na kuzidi kuwachanganya wale wazee waliokuwa hawana hata fununu ya kinachoendelea.

“Subiri kwanza Edwin. Huyu binti ulimchumbia au hukumchumbia!?” “Sio kwa hapa kanisani kwamba tulitangaza! Ila Esther ambaye ni kama dada yake anajua na Emelda mwenyewe anajua.” Wote wakabaki kama hawajaelewa.

“Wanachofanya ni kunidhulumu.” “Na kweli Edwin alimtunza sana Emelda. Mimi ni shahidi.” Esther akaongeza. “Tena kwa Edwin kunitumia mimi mwenyewe, kumfikishia Emelda matunzo.” “Wakiwa kwenye mahusiano?” Baba yake akamuuliza Esther vizuri tu.

Ndiyo. Maana walikuwa wakitumika pamoja.” “Esther, acha kujibu swali la jumla. Na acha kuzungusha maneno, tuna ibada na hawa wote wanahuduma huko ibadani. Nakuuliza swali nataka unijibu moja kwa moja bila kuzungusha. Nauliza hivi, wakati ukitumwa vitu na Edwin, umpelekee Emelda, je, walikuwa kwenye mahusiano, na Emelda alijua vitu vinatoka kwa Edwin?” “Mahusiano yana hatua baba.” “Tafadhali jibu swali.” “Si ndio najibu?! Mbona kama hamtaki kusikiliza mnakuwa kama mna majibu yenu!?” Mpaka wale wazee wakashangaa nakuhisi kuna kitu hakipo sawa.

“Tafadhali tumsikilize Esther tuone ana kipi chakujibu! Maana mpaka hapa sasahivi ni kama bado sijaelewa sawasawa.” “Asante! Maana naona ni kama hamtaki ukweli wa mambo! Mimi nasimamia haki, hata kama mtanichukia.” Esther akaendelea. Wote kimya.

“Wote tunajua kabla ya uchumba kuna hatua. Moja wapo ya hizo hatua ni kufahamiana ikiwemo na kujaliana. Ndicho alichoanzia Edwin. Alianza kwa kufahamiana na Emelda. Alipoona anamfaa ndipo akawahusisha kumuombea. Na sisi wanawake huwa tunajua hata kama mwanaume hajasema kitu, unajua wazi kabisa kinachoendelea. Emelda asijidai hakuwa akijua kinachoendelea kati yake na Edwin! Alijua na kukipenda. Edwin si mjinga kuwekeza sehemu ambayo anajua mtu hamtaki. Emelda alijua na kupokea matunzo akijua vinatoka kwa Edwin. Asijidai kupinga sasahivi sababu ya tamaa.”

 “Ameona Junior anapesa kuliko Edwin, ndio akaweka ufitini na kufanya njama ya kuvunjika uchumba kati ya Junior na Hope, yeye ndio akajiingiza kwa njia zake.” Akazidisha jazba.

“Nafikiri kuna swali la msingi sana bado sijapata jibu lake! Tafadhali naomba kumsikia Edwin mwenyewe. Nashukuru Esther. Lakini hili naomba ajibu Edwin mwenyewe.” Yule mzee akaweka msisitizo.

“Swali langu ni hili, wakati ukifanya hayo matunzo kwa Emelda, ulishakuwa kwenye mahusiano naye kwamba mlishazungumza kabisa, akakubali, si kihisia, kwamba akakubali muanze hii safari ya mahusiano, mzidi kuomba ndio mrudishe jibu kwetu, au mlisharudisha jibu kwamba mmekubaliana, mimi sikuwepo?”

“Nilikuja kumwambia. Japo Esther alishaniambia alishazungumza naye, Emelda akakubali kabisa kuwa na mimi, na ndio maana akawa akinitajia uhitaji wa Emelda, nampa pesa akamnunulie au vingine namnunulia mwenyewe kisha nampa Esther ampelekee.” “Bado narudia swali. Wakati huo unapofanya hayo yote, ulishakuwa umezungumza na Emelda mwenyewe?” “Huwa…” “Samahani Esther binti yangu. Naomba Edwin atujibu yeye mwenyewe.” Akamkatisha, asimuingilie.

“Karibu Edwin.” “Najua tu mtamtetea mchungaji, kwa sababu mnataka kuwepo kwenye hii huduma. Mimi siogopi mtu. Nasema kweli. Na sikubali kudhulimiwa.” Wote wakashangaa. “Binafsi kabla sijaonyesha upendeleo wangu, kwanza ningependa kuelewa. Mpaka sasa sijaelewa kinachoendelea!” Edwin akaongea mengi akilalamika huku akiwatisha kwa mengi, wakimwangalia.

Na ubaya wa Junior na Ezra wakikuamulia kukuanika ujinga wako, lazima utaumbuka tu. Hunyamaza kimya wakikuangalia. Sasa kama una jazba na maneno machafu, lazima yatakutoka tu, halafu wao kimya mpaka utulie mwenyewe au uamue kuondoka. Ndicho kilichompata Edwin. Aliongea kwa sauti zote, wao kimya tu wakimtizama.

 Mwishoe mmoja wa wazee akauliza. “Kwa hiyo Junior ndiye anayemchumbia Emelda!? Maana mnazidi kunichanganya.” “Ndiye aliyepewa ndiyo ya Emelda, na leo ndio tulipanga kutangaza uchumba wao.” Mama mchungaji akajibu.

“Na wamefanya kwa siri sababu ya hila.” “Kwani uchumba ni ndoa tayari!? Hii ilikuwa maalumu kwa ajili ya kumfurahisha Emelda. Junior alitaka kumfanyia surprise, amvalishe pete hadharani, mbele ya watu wote, kisha kutangaza tangazo la ndoa yao, akiwepo Ezra na Jelini, maana wataoa siku moja, walikuwa wakisubiriana. Kisha baada ya tangazo, kuruhusu mwenye kipingamizi chochote ajitokeze na ushahidi wake. Sina ninachoficha. Sina mkato kwa kijana wangu. Nilichofanya kwa wengine, ndio nitafanya kwake na kwa Ezra.” Mchungaji akaendelea taratibu tu.

“Kikao hiki nimefanya kwa heshima yako Edwin, kwa kuwa alianzia kanisani. Sikutaka kupuuza malalamiko yake, baada ya kusikia hili, japo bado anaruhusiwa kutoa ushahidi kama anapingamizi kwenye hili. Ninachoomba tu, ni tumsikie Emelda mbaye nahisi atawapa picha yakueleweka, maana Esther na Edwin, wameshindwa kutoa majibu ya moja kwa moja. Na tafadhali tusimuingilie.”

“Emelda anawaogopa.” Edwin akadakia. “Kwamba una wasiwasi hataweza kuzungumza au!?” Yule mzee akamuuliza Edwin. “Analazimishwa mambo.” “Sio kweli, na mimi si mtoto mdogo, na sitasema uongo.” Kwa mara ya kwanza Emelda akaongea.

“Mimi sijui Edwin amepata wapi hilo wazo kwamba naogopa familia ya mchungaji, wakati mimi naishi nao pale kama anavyoishi Noah! Hapajawahi kuwekwa mazingira ya kunifanya niogope na ndio maana japokuwa Junior alikuwa amemchumbia Hope, hisia zangu kwake sikuzificha hata kwa mama yake! Ndio muamini ule ukaribu na mazingira ninayoishi nayo pale kwa mchungaji.”

“Wakati Esther akinitisha kuwa mama yao akijua nampenda Junior akiwa amechumbia, atanichukia, ikawa kinyume. Mama alikuwa akijua nampenda Junior. Na aliheshimu kitendo cha mimi kutowaingilia. Nilibaki kuomba tu nikimsihi Mungu kama Junior ni andiko langu basi anipe, ila kama sio, basi awabariki yeye na Hope.”

“Mungu na Hope ni shahidi, Hope hajawahi hisi kutoheshimiwa au kutopendwa na mimi. Nilimchukulia kama wifi kabisa.” “Na mimi ni shahidi.” Mama mchungaji akaongeza.

“Asante mama. Na kipindi hicho chote, nilikuwa nikitumika na Edwin vizuri tu, hakuwahi kunitongoza wala kunipa ishara yeyote ile ila heshima kama mtumishi mwenzie. Na hapo Esther akinipa vitu kama dada tu, na akatae hapa. Si kwa maneno mengi. Kama hata siku moja alishanipa kitu akasema kinatoka kwa Edwin. Sema ukweli Esther.”

“Sasa wewe ulifikiri nakupa vitu mimi kama nani yako!?” “Subiri kwanza Esther. Kwamba wewe hukuwa ukimwambia Esther kama vitu na pesa zinatoka kwangu!?” “Alijua sana aache unafiki.” “Alijua kwa kumwambia au kama ulivyosema ni hisia?” Wakaanza wao wawili sasa kubishana. Kimya wengine wakisikiliza.

“Alijua sana tu.” “Esther, tafadhali usinichanganye zaidi. Maana wewe mwenyewe ulikuwa ukirudisha majibu ukisema Emelda amenishukuru sana na anapenda ninavyomjali.” “Kwani uongo? Kama angekuwa hapendi si asingekuwa akipokea?” “Umemdanganya Edwin, na wewe ndio umemchanganya. Na kingine, nimesikia ukisema ulinipa na pesa!” “Wala si mara moja.” Emelda akashangaa sana.

 “Mungu ni shahidi Edwin, sijawahi pewa pesa hata shilingi na Esther dhidi ya nguo za ndani, na matumizi ya siku zangu.” “Usijidai unafiki Emelda. Sikukwambia kama Edwin anakupenda wewe!?”

“Subiri Esther, pesa nilizokuwa nikikupa ili umpe Emelda zimeenda wapi? Na perfume. Sijamsikia akizitaja!” “Wewe hukumsikia akinukia?” “Kwa kunipa niwe najipulizia siku za jumapili, tena akinisisitiza akisema nisije nukisha watoto wawatu na kuua huduma pale kwa wazazi kushindwa leta watoto wao.” Wote wakaumia sana, akaendelea.

“Ila sikujua kama ni ili Edwin ndio ajue umenipa perfume alizokuwa akikutuma kwangu!” Akaanza maneno mengi akijitetea kwa hili na lile ila akawa amekamatwa.

“Wazee wangu naombeni mnisikilize na mimi. Naahidi sitadanganya.” “Ongea Emelda.” “Nashukuru. Esther alikuwa akinipa vitu kama nilivyovitaja. Samahani kurudia. Ni nguo za ndani na vitu vyakutumia kwenye siku zangu. Nguo alizokuwa akinipa ni zake, alizokuwa ametumia, yaani ilikuwa ikinibidi kuzibana ili zinienee. Na nilikuwa nikimshukuru kwa sababu ni kweli nilikuwa na uhitaji na nguo.”

“Unataka kuniambia kweli hujawahi pata nguo mpya kutoka kwangu!?” “Mungu ni shahidi Edwin, na mama atanitetea. Sijawahi vaa nguo mpya mimi tokea nina akili za kukumbuka yaani mtoto, mpaka alipokuja Junior kwenye maisha yangu. Na Jelini, kwa kutumia pesa yake, ndiye mtu wa kwanza kuninunulia nguo mpya ya kwanza.”

“Tokea mtoto, mpaka majuzi, ndio kwa mara ya kwanza kumbukumbu zangu zinanihakikishia, na sijasahau jamani, nimevaa nguo mpya kutoka kwa Jelini. Yaani nguo ambayo haijawahi valiwa na mtu mwingine mimi ni wa kwanza. Ni Jelini alininunulia na sitasahau. Maana hata sare za shule, ilikuwa navaa za watu. Tunakwenda kuwafanyia kazi majumbani kwao, mama anaomba malipo wakati mwingine iwe sare za shule za watoto wao, sababu hata wakitulipa unakuta pesa haitoshi kununua sare mpya. Sidanganyi, muulizeni mama yangu mzazi yupo.” Ofisi nzima kimya. Edwin akazidi kuumia.

“Na swala la pesa, mama mchungaji huyu hapa. Ilibidi anianzishie kitabu cha madeni. Nilikuwa nikichukua mshahara hata ambao bado sijafanyia kazi, ili nisaidie kwetu. Sasa kama kweli mimi ningekuwa nikipokea pesa kutoka kwa Edwin, kulikuwa na ulazima gani wa kumkopa mama kila wakati!?” Wote kimya.

“Na nasema kutoka ndani ya moyo wangu, na Mungu nishahidi, kila kitu alichonipa Esther nilijua ni yeye ndio ananipa. Na hata alipozungumzia swala la Edwin. Tena hapo ni baadaye sana akiwa anaendelea kunipa, maana aliniambia Edwin ni mtu mzuri, anafaa kuwa mume.” “Muongo.” “Subiri kwanza Esther. Mwache amalize.” Mzee akamuwahi.

“Hivyohivyo wala siongezi. Mimi nilimjibu kuwa, Edwin naheshimiana naye sana. Namuona kama kaka au mtumishi mwenzangu tu. Kwa heshima kabisa, nilimjibu hivyo Esther. Kama kweli ingekuwa ikikaa ndani yake, angekubaliana na mimi. Lakini najua atabisha.” “Siwezi kukubaliana na uongo wako.”

“Sawa Esther dada yangu. Lakini hata mpaka hapo hata Edwin mwenyewe hakuwa ameniambia! Edwin ameniambia majuzi tu, nikiwa nimetoka kukubaliana na Junior, ndoa. Hapo tukiwa tumeshajipanga tayari na kina Ezra na Jelini mpaka maisha yetu ya ndoa na baadaye na watoto wa watoto wetu, ndio Edwin ananiambia maswala ya kunichumbia! Ukipunguza hasira Edwin, utakubaliana na mimi kuwa ni siku chache zilizopita ndipo umeniambia.”

“Ni kweli. Emelda hajadanganya. Mimi binafsi nimemwambia jumapili ya juzi tu. Esther umenidanganya. Umenipotezea muda na pesa zangu. Pengine isingekuwa kukusikiliza wewe ningemuwahi Emelda mapema sana.”  “Wewe acha kus…” “Hapana Esther. Wewe ndio umeniponza. Ulinifanya nikuamini! Yaani hapa huyu mzee ameuliza maswali na wakati Emelda anazungumza nimetulia, nakufikiria kweli nimejiona mjinga.”

“Nilikuwa nikikuhonga wewe wala si Emelda! Ulinifanya niamini kila kitu kati yangu na Emelda kipo sawa, nijiandae tu kwa harusi, kumbe Emelda hana taarifa!” “Kwani mimi nilikukataza usizunguze na Emelda mwenyewe!? Kama ulishindwa kutongoza ni wewe, acha kulaumu watu. Yamekushinda mwenyewe ndio unatafuta wakumlaumu! Kwani kuomba na kutuma hongo ndio kutongoza!? Wewe umeshindwa kusimama kiume, acha kutafuta mchawi wako.” Wakashangaa Edwin hajibu kabisa, amenyamaza mpaka Esther mwenyewe akaishiwa maneno. Kukabaki kimya.

“Kwa heshima yenu jamani, naomba nizungumze na Edwin. Kwa hakika, wakati nazungumza na Emelda, sikuwa nikijua kabisa habari zako, na Emelda hivyohivyo.”

 “Binafsi imenichukua mapito fulani, na ukweli fulani kwa Hope, kufiki muafaka, mimi nafumbia macho upendo mkubwa ulio kuwa mbele yangu ukinisubiria, na kwa Hope kugundua, hawezi kuvaa viatu vya atakayekuja kuwa mke wangu.” Junior akaendelea.

“Alikiri yeye mwenyewe mbele ya wazazi wangu, hawezi kuja kuwa mke wangu kwa vile nilivyo na maisha ninayotarajia kuja kuyaishi. Yeye mwenyewe, ambaye ni mwanamke pekee niliyekwisha chumbia maishani, akiwa amekaa kwenye kiti hicho alichokaa Esther sasahivi, alikiri kuwa, kwake kuwa mke wangu ingekuwa mateso. Tukahitimisha hapa kwa amani. Hope hana tatizo na mimi.”

“Ukitaka kujua Emelda ni mke wangu, Mungu alinipa, mimi nikimchukulia kama dada tu pale nyumbani, yaani kama Esther, nisiweke wazo la mapenzi na wala si kumdharau, tumeanza muda si mrefu, lakini yale mapungufu aliyoyaona Hope, kwa Emelda si tatizo hata hafikirii, mpaka mimi na Ezra tunashangaa! Maana na Jelini naye ni hivyohivyo! Hakuna kati yao anayelalamikia maisha yetu na ndoto zetu. Mimi na Ezra. Wapo wakituunga mkono na kuongeza ladha kwenye mahusiano yetu. Ndio maana tumeona tuoe tu, maana hakuna jingine tunasubiri kutoka kwa Mungu.”

“Ni hilo tu Edwin. Binafsi nakuheshimu na nina hofu mbele za Mungu. Kwangu ndoa si kitu cha kujaribisha ndio maana hata baba yupo makini sana na kila jiwe tunaloweka kwenye msingi wetu, mimi na Ezra, kwenye ndoa. Kazembei akihakikisha tunaweka msingi wa kiMungu. Hapakuwa na hila au mchezo niliokuchezea.”

“Ila dada yako amenichezea Junior. Na amenichezea mchezo mbaya sana.” “Ni wewe mwenyewe Edwin. Acha kujiliza.” “Acha nilie Esther. Ila na wewe Mungu atakulipa. Kama kweli hujanitenda hila, Mungu ataamua kati yetu.” “Mwache aamue. Usinitishe.” “Sawa. Mimi naondoka kabisa kwenye hili kanisa.” Hapo wale wazee wakahamaki.

“Acha kukimbia Edwin! Hizi ni changamoto ambazo utakutana nazo kila mahali. Ukikataa kufudhu hapa, ujue Mungu atakupitisha kwengine mpaka aone umeelewa na kuhitimu.” “Lakini itakuwa kwengine sio hapa kwa mwanamke pekee niliyewahi kumpenda. Siwezi ona Emelda anaolewa na mtu mwingine, mimi nikawa sawa. Siwezi. Bora niondoke tu.” Akasimama na kuondoka kabisa hapo ofisini. Kimya kwa muda. Mwishoe mchungaji akahitimisha kwa maombi.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye majira ya saa nne na nusu akarudi tena pale. Bado alikuwa amelala. Akaulizia hali yake kwa manesi walioingia asubuhi, wakamwambia madaktari wamepita, wamemwangalia, anaendelea vizuri. Akaona akae tena kidogo.

Haukupita muda mrefu akafungua macho. Alipomuona tu akaanza kulia. “Pole sana Kamila.” “Nataka kwenda aliko Mike. Hapa mimi sitaweza kuishi tena. Bora wangeniacha tu niende kwa Mike. Huko alipo atakuwa ananisubiria, haelewi kwa nini nakawia.” Colins akajua kazi itakuwepo.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mapenzi&Pesa!

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment