“Duuuh!” Akasikika Ezra baada ya kumaliza kusoma na kurudia
“Kama nilivyo mwambia Jelini, narudia tena kuwakumbusha na nyinyi na ninaomba tubaki tukikumbushana mpaka kifo chetu sisi wote. Hizi ni kelele tu. Haijalishi nani anazileta, sisi tusonge mbele kwenye safari yetu. Iwe watoto wenu au hata wangu na Jelini, watakapo leta jambo la kutufarakanisha, tukumbuke ni kelele. Sisi tutaendelea kuishi hivi tulivyo, ila njia ndio zinaweza kubadilika kwa sababu tutakazo kubaliana pamoja.”
“Emelda, nasikitika Edwin amekuharibia surprise yako kesho. Maana ni kweli, sisi wote watatu na wazazi tumekuandalia kitu kizuri sana. Lakini narudia tena, hatutapoteza lengo kwa sababu ya hili, ila njia.” “Kivipi tena, wakati na yeye ametangaza vita? Si tutakuwa tukiharibu huduma nzima!?”
“Hapa nilipokaa sasahivi, muda huu, sitakuwa na majibu yote Emelda. Ninachojua kwa hakika, tuna harusi kubwa sana, tena nzuri na ya kifahari inatusubiria sisi wote wanne. Kisha mapumziko mazuri sana, ambayo sisi wote tunayastahili baada ya harusi yetu. Ila tunafika vipi hapo, ndio naomba tutulie kabisa. Hakuna paniki. Tunabadili gia hukohuko angani, tena bila kutetereka wala kubadili muda wetu.” “Hapo afadhali. Mimi sasahivi nataka tuishi wote Ezra.” Jelini akajilalamisha kwa deko.
Akampa kiss hapohapo. Naye hakulilazia damu. Wakaanza kupeana ndimi wenzao wanawaangalia. “Kweli!?” Junior akashangaa sana, ikabidi waachane, Emelda akacheka kwa aibu. “Sasa si tumesema hizo ni kelele tu, na wewe Junior! Na Ezra amesema hakuna kitakacho badilika. Mimi nataka kuolewa na Ezra.” “Na mimi nataka kukuoa Jelini, tena haraka.” Alipotaka tu kumsogezea Ezra mdomo, Junior akawawahi. “Acheni kwanza bwana! Nyinyi vipi!?” Wakaanza kucheka.
“Mwaya Junior!” “Wewe hutamaliza.” “Si tunabadili gia angani? Au unasemaje Junior?” “Wasiwasi wangu ni kuwa, anaonekana kuna anakotoa taarifa zetu za ndani, kiasi kwamba hata tukibadili, atajua tu na anaonekana amekusudia kuniharibia! Tujiulize tu, yeye amejuaje kama kesho ndio nilikuwa nikitaka kumchumbia Emelda?! Na nilimuonya kabisa mama asimwambie yeyote yule. Na ndio maana nilikataa tafrija pale nyumbani, nikakubali kuingia garama zaidi tufanyie hotelini ili Emelda asijue. Wameniharibia mipango yote!” Junior akaongea kwa kulalamika.
“Wewe Junior usifikirie ndio tumeishiwa. Na wala usifikirie eti ndio Emelda amejua halafu ndio basi! Nitawaambia nyinyi wawili mpango mwingine mpaka utalalamika kwa nini sijakwambia huu kwanza. Wewe Junior mimi mtu wako. Siwezi kukuangusha. Na wewe Emelda tulia wala usipaniki. Jua mambo mazuri yanakuja. Na tunakuwazia mema mazuri.” Kidogo wakatulia.
“Sasa mchungaji!? Maana hizi shutuma ni nzito jamani! Hatuwezi muacha akaaibika kwa kushitukizwa kwa jambo ambalo hana hatia. Tafadhali naomba tumshirikishe.” “Emelda anapointi Junior. Tumshirikishe tu, tuone atakavyo tushauri. Ila naomba wakati hiki kikao kinahamia nyumbani, Jelini akapumzike.”
“Sawa. Ila sasa nawaomba kuagana kwenu kuwe kufupi. Usiku sasa.” Jelini na Emelda hawana mbavu. “Sasa nyinyi mngeanza kuondoka na kumuwahi kumuomba mzee kikao kabla hajalala.” “Mbona hilo halina shida! Ombi ni mmalize kuagana hapa. Msikeshe mkiagana.” Junior akaongeza na kumgeukia Emelda. “Twende mke wangu.” Ilimgusa Emelda, hakutegemea.
Akaitunza moyoni, ila akajisikia fuhari kweli! Kwanza hakuwa anajua hata kama Junior atakuja kumchumbia hadharani kama alivyomfanyia Hope. Alijiona hastahili.
Akasimama, Junior akamshika mkono. “Ezra, tunakusubiri.” “Junior naye! Hata hamjatoka, unaanza kumrusha roho mpenzi wangu! Namuaga mara moja tu, anakuja huko.” “Na iwe hivyo Jelini.” Wao wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona ametulia hapo garini, kama hayupo pale. “Unawaza nini?” Akamgutusha. “Niambie Emelda. Itanisaidia.” “Nikwambie ukweli?” “Ndio ninachotaka kusikia.” “Sikuwa hata na wazo kama unampango wa kunichumbia hadharani kama vile Hope!” “Sasa wewe ulikuwa ukifikiria ningekuchumbiaje?” “Nilijua ndio basi tena. Kwa sababu ulishafanya kwa Hope, nikajua umeshamaliza.” “Emelda!?” “Kweli Junior. Kwanza nilijiona sistahili. Mimi sio wa hadhi hiyo.” “Tafadhali usiseme hivyo Emelda. Unaniumiza.”
“Ndivyo nilivyojisikia Junior. Halafu hapakuwahi hata na kuropokwa juu ya hilo, kwa hiyo moyoni nikakubali iende vile ilivyo.” “Nilifanya hivyo makusudi ili kukufurahisha. Sikutaka hata waropoke. Kila mtu nilimsihi asiseme.” “Kwamba mpaka mama anajua!?” “Tena yeye ndio ilibidi nizungumze na Mika kabisa, ahakikishe anaelewa. Nilitaka ufurahie Emelda. Wewe nimekupenda kutoka moyoni. Furaha yangu, ni ufurahie na nataka ujue nakuoa kwa kuwa nakupenda. Au unamashaka na hilo?”
“Huna sababu yakunidanganya. Lakini sasahivi kwa kuwa nimejua, eti roho inaniuma Junior! Naona kama Edwin amenikatili! Kwa hakika zingetimia ndoto ambazo nilisita hata kuzifikiria kuota. Ningehisi nipo usingizini. Ningefurahi sana. Eti na mimi kuchumbiwa kanisani mbele ya kila mtu!” Akawa kama anayevuta picha kujaribu kufikiria vile ingekuwa na kumuumiza Junior.
Mwishoe akajirudia tena kama aliyejihakikishia. “Edwin amenikatili vibaya sana.” Junior akatafuta sehemu, akaegesha gari. Akashuka kabisa garini, Emelda asielewe anataka kufanya nini. Akaenda kufungua mlango alipokaa.
Akamfungua na yeye mkanda, Emelda akimtizama tu, na kumgeuza. Na wao siku hiyo angalau wakapata kiss. Bwana Junior aliitendea haki. Ilikuwa ya muda wakutosha, halafu amesimama nje ya gari, Emelda amekaa ndani miguu nje. Alimshika vizuri na kuendelea kwa muda bila haraka.
Kisha akamuachia. “Tutakuwa na ndoa nzuri sana Emelda.” “Leo umeniita mke wangu, nimefurahi!” Junior akarudi tena midomoni kwa kujinafasi, kisha akamuachia. “Na ndivyo itakavyokuwa. Mimi na wewe mpaka kifo. Mungu atakapotujalia watoto, wataongezeka kwetu, lakini tutabaki hivihivi.”
“Na tafadhali usivunjike moyo. Mimi nitakuoa, na tutakuwa na harusi nzuri sana, hata kama uchumba haitakuwa kama nilivyo panga.” Akamuona ametulia. Na yeye ikampata hali kama ya Emelda. Akafikiria akivuta picha vile ingekuwa kesho yake. Furaha ambayo angefanikiwa kuiweka kwa Emelda!
“Daah! Nafikiri mimi ndio amenikatili zaidi. Nilijiandaa eti! Nilijiandaa haswa. Nilitaka ufurahi.” Emelda naye akajiongeza kama Jelini. Akampa kiss ya kumtuliza, hawakuishia hapo. Wakaendelea kwa uchu mpaka kujisahau kama kuna kikao kwa wazazi.
Furaha ya kujua kama Junior anamfikiria kama Hope tu tena zaidi, ikamuongezea hamasa. Midomo yake ikazidi kuwa mitamu asitake kumuachia mpaka Junior akamshangaa. Si Emelda wa aibu tena. Ametulia akitoa ushirikiano wa aina yake, tena akimpapasa nyuma shingoni mpaka sehemu ya nyele kwenye kichogo kama alivyomuona Jelini akimfanyia Ezra.
Wakaamshana wasitake kumaliza. Mwishoe ndio kama Junior akagutuka. “Twende tuone baba atatushauri vipi.” Wakatoka hapo wakijaribu kutulia wakielekea nyumbani kwa wazazi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakamkuta Ezra alishafika. Akawatizama kwa kuwasuta. “Na kwa taarifa zilizo rasmi, baba hakuwa anataarifa za ujio wetu. Yaani mimi ningechelewa kidogo tu, ningekuta ameshalala.” “Nilipitiwa kupiga simu bwana! Shikamooni.” Akawasalimia wazazi wake huku wakikaa. Na Emelda akasalimia.
Jungu Kubwa Lisilokosa Ukoko.
“Kwema?” Mzee akauliza. “Kuna habari sio nzuri. Tunaomba ushauri wako jinsi ya kuendelea.” Mama mchungaji akashituka. “Ni nini tena?!” “Ezra atakupa simu yake, mimi nitampa baba. Msome ujumbe alitumiwa Emelda na Edwin. Mkimaliza ndipo tuendelee.” Wakafanya hivyo.
Mzee akasoma. Wakamuona ametulia kwa muda kisha akamrudishia Junior simu yake. “Mungu wangu huyu kijana!” Mama mchungaji yeye akahamaki baada ya kumaliza kusoma. “Subiri kwanza mama J. Nyinyi mlitaka ushauri juu ya nini?” “Si umesoma ujumbe huo baba!? Tunaendelea vipi?” “Kama tulivyo panga na kumuomba Mungu.” Wakashangaa.
“Kabisa. Labda kati yenu awepo wakubadili mawazo, au mmoja wenu asiamke mzima, tena awe amekufa. Ila kama wote tutaamka kama hivi, kama Mungu wangu aishivyo, kesho unachumbia, na mtaoa kanisa lilelile. Na mimi nitatamka baraka juu yenu.” “Baba J!?” Mkewe akashangaa sana.
“Hakika tena. Kuamka kwetu siku ya kesho, na kuwepo kwetu siku tuliyopanga hawa wafunge ndoa, ndio yatakuwa majibu na kibali cha Mungu juu yao hawa. Hakuna kelele, wala kitisho kitakachoingilia. Wala msitingishike.”
“Kinacho niuma tu, ni jinsi Junior alivyohangaika, kuhakikisha hizi taarifa hazimfikii Emelda mpaka siku ya kesho. Hicho tu. Haya mengine, ni kilio cha wivu.” Ezra akaanza kucheka kwa furaha na kishabiki.
“Hakika tena. Kwani sisi tulishawahi kumfungia Emelda humu ndani? Kila siku jumapili alikuwa naye huko kanisani. Kilichomshinda kutongoza mpaka kukubaliwa ni nini?” Emelda alifurahia kweli.
“Sikatai alitushirikisha kwenye maombi. Sasa kwani mimi ni Mungu wake mpaka anilaumu kwa kutojiwa kwake! Kwanza alishindwa mwenyewe kutongoza, akabaki kumtumia Esther akimuhongea. Leo ananilaumu mimi na kunitisha!? Hata kidogo!” Ezra hana mbavu. Junior akabaki akimtizama kama ambaye baba yake hajaelewa ukubwa wa madhara yake.
“Sasa na huduma yako baba!?” “Wala huduma si yangu mimi. Mwenye nayo ataitetea. Na mimi niliitwa kama wewe na Edwin. Aliyetuita atatetea kazi yake. Hilo halinitishi. Akashitaki popote. Akatangaze popote. Siibi pesa hata shilingi. Sadaka zao zinapokelewa na watunza hazina. Na mimi nalipwa mshahara kama yeye anavyolipwa pale kanisani! Sidhulumu mtu, siibii mtu hata kwa kuwadanganya kwa kutumia imani yao kwa Mungu wao. Halafu leo atake kunitisha mimi na mwanangu! Hakuna wakumtisha mwanangu mimi labda Mungu, aache ujinga wake.” Hapo akaupata moyo wa mkewe. Ni Junior tena! Mama akafurahi na tayari usiku wa mchungaji ulishabadilika. Mama alikuwa tayari kwa shuguli ya nguvu usiku huo, kumpongeza mumewe kusimama na kifungua mimba wake.
“Junior, usikubali akakuingia kichwani hata kidogo. Umechumbia mara moja tu! Na uliyemchumbia umeachana naye kwa amani tu. Tena kwa garama ndogo tu ya gari.” Wote wakacheka wasiamini.
“Baba! Kweli hili halikutishi hata kidogo!?” “Atanitisha nini mimi? Siogopi umasiki, kwamba eti washirika watanikimbia kwa maneno yake ya uongo! Hata kidogo. Najua kuwa na njaa, najua kuwa na karamu nyumbani kwangu. Najua kutokuwa navyo, najua kuwa navyo kwa kipimo cha kiMungu. Uzuri wangu ni huu, aliyenijaza nipo upande wake na hatujakosana.” “Safi sana baba.” Ezra shabiki akaendelea kushabikia kwa furaha.
“Ebo! Yaani eti sisi watu na akili zetu tubadili mipango yetu kwa ajili ya kukosa kwake yeye! Hata kidogo. Nyinyi nendeni mkapumzike. Pole Junior, surprise imeharibika, lakini msichana unaye. Emelda, hakuna kilicho haribika.” “Nashukuru baba yangu. Nimefurahi! Na mimi natamani uniombee kama ulivyomuombea Hope na Junior!” Wakajisikia kupoa.
“Sijayasahau yale maombi mchungaji! Nakumbuka neno kwa neno. Au kama kwa Ezra na Jelini. Na mimi natamani.” Akaongea kwa unyenyekevu. “Basi na ikawe kwako mara dufu. Wewe na watoto wako na watoto wa watoto wako. Na kesho, tutawatamkia baraka wewe na mwenzio huyu. Nenda kapumzike, ukijua kesho ni siku yako muhimu sana, tumeiandaa kwa ajili yako. Na hata Junior amesema, kesho ni siku yako. Usikubali kuvurugwa. Haya, nenda ukalale.” Emelda alifurahia huyo, akaondoka akicheka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alipoondoka tu mchungaji akajikuta akiwaza kwa sauti. “Huyu Edwin anaonekana anapata taarifa zetu kutoka ndani kabisa. Swali ni nani anayempa taarifa za ndani zilizofanyika juhudi za kufichwa!?” “Yaani hilo ni swali na mimi nimejiuliza baba!” Wakatulia kwa muda kama wote wakitafakari, kisha wote wakajikuta wakisema kwa pamoja mpaka mama yao. “Ester.”
Hapohapo wakamuona mchungaji anapiga simu. “Kesho, saa moja kamili. Uwepo ofisini kwangu, kanisani, bila kukosa. Na hakikisha unafika na Edwin. Umenielewa Ester? Na hata kama ni mgonjwa, meza dawa uje. Utarudi kwako kupumzika baada ya hapo.” Simu ikakatwa.
“Hiki kikao kitahamia kanisani. Saa moja bila kukosa. Acha niwaombe na wale wazee waliokuwa wakimuombea Edwin, waje naye. Tumalizane ofisini. Sitaki fujo kwenye nyumba ya ibada.” Hapo likakaa sawa. Ndio wakatawanyika.
Ukweli Juu Ya Mike Kwa Kamila
Akamfikisha mpaka kwenye hicho chumba cha kulaza wagonjwa wenye pesa zao, alichopewa. “Kuna kitu nataka kuzungumza na wewe. Naruhusiwa kuingia ndani?” Akamuona amepatwa na wasiwasi. “Unakumbuka nilikwambia sitakudanganya?” Akakubali. “Basi naomba tuzungumze.” Wakaingia ndani.
“Kaa hapo kitandani.” Akakaa kwa wasiwasi. “Unakumbuka jana mimi kukurudisha kutoka getini, nikakukaribisha ofisini kwangu ukiwa umefukuzwa na walinzi?” Akabaki kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu.
“Uliniomba nikusaidie kutafuta taarifa kamili za Mike.” Akabaki akimwangalia akawa tena kama amemchanganya. “Kamila?” “Nafikiri!” Hapo akaridhika, alitaka tu uhakika kama anamsikiliza au amempoteza.
“Basi ulinipa taarifa zake, yaani jina lake na tarehe yake yakuzaliwa. Nimefanikiwa kupata taarifa zake kamili.” “Yuko wapi!?” Likawa swali la haraka sana.
“Kwanza nataka kujua, kabla ya kumleta hapa, mlikuwa wapi?” “Luca alitukaribisha nyumbani kwake kwa chakula cha usiku. Sisi na ndugu wengine. Tuliporudi nyumbani, akaanza kulalamika tumbo. Alipozidiwa ndio nikamleta hapa. Nikawa nilitoka nyumbani kwa haraka, sikuchukua pochi na yeye alikuwa ameshabadili nguo. Alikuwa amevaa tu nguo za kulalia. Kwa hiyo hakuwa na walet yake.”
“Walipompokea mapokezi kwa kuwa alikuwa akilia sana tumbo, tukapewa chumba cha kupumzika wakiandaa kumpa huduma ndio nikamuacha kwenye hicho chumba au sehemu karibu na mapokezi akisubiria matibabu na mimi nikakimbia kufuata pochi maana hatukuwa hata na vitambulisho.”
“Mike yuko wapi?” Akaongeza swali kwa haraka. “Ulikuwa sahihi kabisa. Mike alipokelewa hapa. Lakini haikuwa jana, Kamila. Mlikuja hapa miaka miwili imeshapita.” Akamuona anakunja sura, kama anamshangaa.
“Na kweli mlifika hapa usiku wa saa sita. Inavyoonekana ulipoondoka ndio akazidiwa zaidi. Taarifa ziliandikwa, hata madaktari walishindwa kumpa huduma.” “Sababu ya pesa!?” “Hapana. Inavyoonekana alikula kitu ambacho kilikuwa kikiharibu viungo vya ndani. Akaanza kutapika damu na nyingine kutoka masikioni na puani. Majira ya saa 7 kasoro usiku, siku ileile ulipomleta, Mike alifariki.” Akabaki ameduaa.
“Nilikuangalia na wewe. Siku hiyo inaonekana ulilazwa hapa majira ya saa 10 alfajiri. Ninavyohisi, ulirudi, ulipoambiwa, ulipoteza fahamu. Taarifa za wauguzi wameandika baada ya siku tatu uliruhusiwa. Na mwili wa Mike ulikuja kuchukuliwa siku hiyohiyo, nikimaanisha kwenye majira ya saa 6 mchana wake akiwa alifariki alfajiri au usiku wa tarehe hiyohiyo. Sasa nafikiri walimzika wewe ukiwa hapa hospitalini huna fahamu.” Kimya amebaki ameduaa.
“Nasikitika mimi kuwa ndiye nakupa hizi taarifa Kamila. Lakini ni kweli Mike alifariki. Ila sijui alipozikwa.” Hapo akaanza kulia. Dada alilia kwa kunung’unika huyo, akimuita Mike. Alilia mpaka manesi wakaingia. Pressure nayo ikalipuka, ikabidi achomwe sindano, alale.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ikabidi sasa Colins kuwaweka kikao ili kuzungumza nao hao wauguzi wote wa upande huo, waliokuwa zamu muda huo. “Huyu dada amepoteza mtu wake wa muhimu sana hapa. Na inavyoonekana, ni hospitali ambayo imeshindwa kumtoka akilini.” Akawasimulia tokea alipomleta Mike.
“Kitendo cha kutomzika mpenzi wake, kimemuacha kwenye nafasi ya kufikiria bado yupo hai, mpaka hivi leo ndio ameamini ukweli. Si kichaa. Ila nafikiri kila mwaka inapofika tarehe aliyokufa mpenzi wake, kuna kitu kinamlipuka ndani, ndio anakua hivyo.”
Kidogo akaona wameanza kumuhurumia. “Sisi kama wahusika hapa, tuna uwezo wakumsaidia nakufanya hii hospiatali kuwa adui au sehemu iliyoweza kumpokea yeye na mpenzi wake, na kuwa na mpenzi wake mpaka safari yake ya mwisho hapa duniani. Ukarimu wowote tutakao muonyesha baada ya hapa, utamsaidia sana. Kwa muda mfupi niliozungumza naye, ni yatima asiye na pakwenda, ndio maana leo yupo hapa.”
“Mimi narudi nyumbani. Ila chochote kitakachotokea, tafadhali naomba mnipigie.” “Sawa. Na usiwe na wasiwasi. Tutapita kuwa tukimwangalia. Na sasahivi tumeelewa. Tutamchukulia taratibu.” Hilo likamfurahisha Colins, nakutoka sasa kurudi nyumbani. Ilishakuwa ikikimbilia majira ya saa 7 usiku.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kichwa kilijaa Kamila tupu, akimuhurumia asijue jinsi ya kusaidia. Akalala akiwa ameshiba chakula kizuri alichomtayarishia. Akapitiwa usingizi mzito kwa uchovu wa mawazo. Ilipofika majira ya saa 10 alfajiri simu ikamtoa usingizini. Akaiangalia, ni kutoka hospitalini.
Akapokea. “Samahani bosi wangu. Uliniachia maagizo kuwa chochote kikitokea kwa Kamila, tukujulishe.” “Kwema!?” “Sisi tulidhania amelala, kumbe aliamka akajining’iniza.” “Kwamba amejinyonga!?” “Ndiyo.” Alishituka Colins, akatamani iwe ni ndoto.
~~~~~~~~~~~~~~
Mchungaji amekusudia zege isilale. Mipango inaendelea kama kawaida.
Edwin atafanya nini?
Bado Love yupo Lupango. Wazazi wakisaka pesa ya dhamana kwa udi na uvumba. Itakuaje?
Kamila naye Kitanzini.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment