Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 12. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 12.

Colins kimya na yeye akawa kama anasubiri. Wakabaki wakiangaliana.

“Unamaanisha nini?” Ikabidi amuulize. “Sehemu ya mwisho niliyokuwa nikiwafanyia kazi, yule mmiliki na meneja wake walikuwa wasumbufu. Wanachanganya kazi na mambo mengine, halafu wanakuwa wanashindana. Kila mmoja ananipangia kazi kutokana na muda yeye atakao kuwepo pale. Ukiwaambia mimi nina mtu wangu, hawaelewi wanakuwa wanakufanyia ukorofi.”

“Ndio Mike akasema niache tu kazi, nishapata uzoefu wakutosha. Nikishamalizana na uzazi, alisema atanifungulia biashara ya catering, niwe nafanya mwenyewe, niajiri watu, kuepuka mambo ya mabosi. Ndio haijakuwa mpaka leo. Ila hapa mnawapa wagonjwa chakula.” Akamaliza.

Colins akajaribu kuelewa. “Kwa hiyo unaomba kazi ya upishi!?” “Najua kupika. Na nilivyokula chakula cha hapa, naona kama kinaweza kutengenezwa kwa ubora zaidi!” “Kwa hiyo wewe unaweza?” “Kuliko nilale tu hapa, naweza saidia. Mkiona nafaa, na mnanafasi mnaweza nipa mimi kazi, angalau nianzie hapa. Nakuahidi nitafanya vizuri.” “Sawa.” Akawa tena kama haamini.

“Twende ukaone jiko lenyewe. Lakini kwa sasa wapishi wameondoka, watarudi saa 11 alfajiri. Nitawaachia maagizo kuwa utakuwepo ili siku ya kwanza uangalie tu jinsi wanavyofanya. Halafu ikifika jioni, tutazungumza tena uniambie vile unavyofikiria, kama bado ni kitu unafikiria kufanya.” Wakatoka pale pamoja.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alipofika jikoni akamuona amefunguka kabisa. Akapafurahia sana. Yaani yeye ndio akaanza kumuelezea Colins vile vifaa. Akajieleza mpaka Colins akajua kweli jikoni ni eneo lake analofurahia. Hapo alionekana anajielewa kabisa. Anazungumza vizuri tu.

Akabaki akimsikiliza kisha akamuuliza. “Umeshakula?” “Hapana.” Akamjibu akiwa hana uhakika na kwa nini anauliza! “Kama ungekuwa na muda, mimi ningekutengenezea chakula kizuri sana.” Colins akacheka akimwangalia. “Hapa kuna gesi. Haitachukua muda mrefu. Nakuahidi utapenda. Nishaona baadhi ya vitu ninavyoweza changanya mpaka kutoa sahani yako.” Akaamua akae hapohapo jikoni.

“Kama upo na mambo mengi sana, naweza kukuletea ofisini kwako.” “Hamna shida. Hapa nipo sawa.” Akamuona anaanza kuandaa vitu hapo jikoni. Mkono mwepesi kweli! Akapotelea mawazoni asijali hata muda. Macho kwa Kamila.

Vikaanza kunukia vizuri hapo jikoni, akionekana amezama kwenye upishi. Akapata wasaa wakumtizama sasa na umbile. Ukweli alivutia. Alitulia akimtafakari. Mdomo wake ulijaa Mike! Hana sentensi isiyo na Mike, na aliamini Mike anarudi. Akatulia kabisa akimtizama na kumtafakari.

~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda akamgeukia. “Nionjee chumvi. Halafu uniambie kama niongeze kidogo au unapenda iwe hivihivi. Nataka kutengeneza kutokana na unavyopenda wewe. Najua ladha ya Mike, kwa hiyo huwa najua nitengeneze vipi chakula chake.” Akamsogelea pale alipokuwa amekaa na mwiko.

“Kuwa mwangalifu, ni mto kidogo.” Akashangaa anamsogezea mwiko mdomoni. Kwamba aonjee hapohapo! Akawa hajaelewa, lakini akamsogezea mpaka mdomoni, ikabidi afungue na kuonja. “Waw!” Hakuamini. “Kumbe kweli unajua kupika!” Akacheka na kuvutia sana. “Umependa?” “Sana. Na nakiona kipo sawa kabisa.” Akashangaa anamfuta pembeni ya mdomo kwa mkono wake, vizuri na taratibu. “Nimekuchafua. Pole.” Ikabidi Colins ajishike kama kujifuta vizuri zaidi. “Hamna shida. Asante.” Akacheka na kuondoka hapo.

 “Kama umependa hivyo basi nimemaliza. Upo tayari kwa chakula?” “Kuonja kumeniongezea njaa.” “Sasa uandae tumbo. Nimepika kingi.” “Wewe hutakula?” “Nimeshakula. Na nilikula sana nikijua naondoka, naweza nisile tena.” Akampakulia na kumuwekea mbele yake. “Nashukuru. Asante. Hata ulivyokiweka kwenye sahani, kinavutia zaidi.” Akacheka kwa furaha. Akawa Kamila wa tofauti na aliyekuwa naye ofisini. Hapo alijawa ujasiri wazi alionekana amefikishwa viwanja vya nyumbani.

Akala huku Kamila anasafisha pale alipotumia. “Chakula ni kizuri sana. Sana.” “Mike anapenda sana nikimpikia. Wakati mwingine kama akiwa na kazi nyingi, harudi nyumbani mchana, nilikuwa nampikia nampelekea ofisini kwake. Anakuwa anafurahia!” Akamuona amepoa gafla. Akamuacha tu. Mwishoe akamaliza.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akavuta kiti pembeni yake. Akamwangalia. “Wewe ni mgeni hapa?” Akamuuliza. “Namaanisha umeanza kazi hapa siku za karibuni?” “Ulitaka nini?” “Msaada wako. Nina uhakika nilimuacha hapa Mike. Nisaidie kupeleleza kujua kilichotokea.” Colins akamwangalia kama anayempima kujua kama yupo tayari na ukweli au la. Akawa hajaridhika na utayari wake.

“Ila kama unaona itakuwia ngumu, basi. Nisikusumbue. Ila natamani sana kujua. Nakua nipo njia panda. Moyo wangu unaniuma! Sijui kilichompata Mike, wangu. Mike ananipenda sana. Kama yupo matatizoni nataka kumsaidia. Kwa garama yeyote ile.” Akaona amkubalie tu. “Sawa.” “Kwamba utanisaidia kunichunguzia!?” “Taarifa hapa zipo wazi kabisa. Sio tatizo.” Akamuona ametulia.

Akaendelea kula. Kimya na yeye akiwaza yake. “Nikuulize kitu Kamila?” Akamwangalia. “Hunifahamu kabisa. Utaamini vipi taarifa nitakazokupa juu ya Mike? Nitajua vipi kama utaamini au utaniweka kundi moja  na watu usio waamini juu ya taarifa za Mike?"

Akamuona ametulia anafikiria. Kisha akamwangalia. “Kwani wewe unaweza kunidanganya?” Akamuuliza kwa upendo. “Hapana. Ila wewe utaamini vipi nitakayokwambia?” “Kwanza najua huna sababu ya kunidanganya. Hunifahamu mimi wala Mike. Halafu naona hunufaiki kwa chochote juu ya Mike.” Hapo akaongea vizuri mpaka Colins akaridhika na kuendelea kula.

“Au nimeongea si sahihi?” “Upo sahihi kabisa. Sina sababu ya kukudanganya.” Akamuona na yeye ameridhika. Akaendelea kula. “Chakula ni kizuri sana. Nashukuru, nimeshiba. Asante.” “Mike naye anashukurani sana. Ila mimi napenda nikipika, mtu ale kama hivyo! Ndio nafurahia.” Akaanza kuondoa vyombo akionekana kweli na furaha. Akasafisha hapo kisha akarudi alipokuwa amekaa Colins akamuona kama ameshakosa raha tena.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Kuna nini?” “Wale manesi kule juu nimeshaona hawanielewi. Nikirudi tu hivihivi unafikiri watanielewa?” “Twende nikusindikize, nitazungumza nao.” “Nakusumbua sana?” “Usijali. Twende.” Wakatoka hapo kimya tu ila ule uchangamfu na furaha aliyokuwa nayo jikoni ukawa umemuisha tena.

“Utakua sawa Kamila. Usiogope.” “Naogopa sana. Natamani kama Mike angekuja hata siku moja tu! Nahisi kuna mambo mengi nilitakiwa kumwambia lakini sijamwambia! Najuta. Ila sasahivi kila nikikumbuka kitu namwandikia kwenye ujumbe namtumia kwenye iliyokuwa namba yake ya simu, ili nisisahau tena. Eti nahisi ni kama huko alipo anasoma, lakini wanamzuia kunijibu! Mike ananipenda sana.” Hilo alilisisitiza kila wakati na kuzidi kuweka ugumu kwa Colins, kumwambia ukweli.

Alimuhisi kama hayupo tayari huku akimuhurumia akiona anazidi kupoteza muda akimsubiria mtu aliyekufa! Colins akazidi kubaki njia panda usiku huo.

Mwanzo wa Mike&Kamila.

“Utakua tu sawa.” “Ndio hata sijui kuwa sawa bila Mike ndio kukoje!” “Ulianza mahusiano naye kwa muda gani?!” “Mrefu sana. Tokea shule alikuwa ananipenda. Tulianza tu kama salamu. Mimi nikiwa kidato cha pili yeye cha tano. Alipokuja tu, tukakutana bwaloni, akaanza kunisaidia. Ananichukulia chakula, halafu ananisaidia kazi. Alipofika kidato cha sita ndio akaniambia niwe na yeye tu.” Akamuona anacheka.

“Nini?” “Mike ananipenda sana. Ila mimi nahisi nilimpenda tokea mwanzoni. Nikawa namsubiria aniambie mimi, asimwambie msichana mwingine, kama anampenda. Nikawa naogopa, asije akapata msichana mwingine mimi nikabakia tu kuwa rafiki. Ndio akasema yeye ananipenda mimi.” Akamuona anavyocheka kwa aibu kama ndio anatongozwa.

“Mike ananipenda sana. Ndio akamaliza shule, akafauli vizuri kwenda chuo. Akaniacha pale shuleni, nikawa tena sielewi, ameniacha. Akawa anakuja kunitembelea tu, vile mimi sikuweza tena. Nikafeli kidato cha nne, wale masista waliokuwa wakinilea wakakasirika kwa nini nimefeli. Wakataka niingie kwenye usista. Nikatoroka na kuja huku Dar kumtafuta Mike.”

“Akanipokea, akatafuta sehemu tukawa tukiishi naye lakini anaenda chuo, nakurudi. Ndio kuanzia wakati huo nikawa nikiishi naye. Ana upendo sana. Halafu ananijali.” “Ulirudi tena kwa wale waliokuwa wakikulea mwanzoni?” “Hapana! Nilijua watanifungia, nisirudi kwa Mike. Walikuwa wananikumbusha jinsi nilivyokuwa nataka kuwa sista tokea mdogo. Kila nikiwaambia mimi sitaki tena, wakawa wananisema eti nimebadilika! Nitulie ndani, nitakumbuka wito wangu. Ndio nikaondoka, sikurudi tena.” Akabaki kimya.

Mapenzi na Misukosuko Yake!

Wakati wanakaribia kuagana usiku huo, ndio kila mmoja akachukua sasa vitu vyake ikiwemo simu walizokubaliana siku hiyo iwe wao tu bila muingiliano. Kama ilivyo ada, ukishika simu unaanza kuangalia. Wengine wakajiridhisha hakuna cha muhimu ila Emelda yeye wakamuona kama amezama kwenye ujumbe, hamalizi.

Junior akaanza kusumbuka, Ezra akamuona. Kana kwamba haitoshi, Emelda akatoka kabisa hapo walipokuwa wamesimama wanakaribia kutoka mlango mkubwa, maana kama walikomea hapo. Hawatoki, stori zinaendelea tu ndipo hapo akapotelea kwenye simu yake, haongezi neno wala hacheki tena, kama ambaye hakuwepo pale. Mwishoe bila kujua kama Junior anamwangalia, ndio akaaga kuwa anarudi ndani atumie choo. Kisha akaondoka bila ya kuwatizama kama aliyetingwa na simu yake mkononi. Hapo ndipo Junior akavurugwa kabisa. Kulalamika hawezi, kila mmoja ameshika simu yake na walishaomba pamoja, wakawa ndio wanatawanyika.

Baada ya muda mfupi wakamsikia akitoka, Junior akageuka kabisa. “Kwema?” Akagutuka na yeye akawatizama kwa zamu. “Kwema?” Junior akarudia. “Ndiyo.” Junior akabaki akimtizama. “Kila kitu kipo tu sawa.” “Naomba simu yako.” Mpaka Jelini akashangaa. Emelda akabaki amepigwa na butwaa.

“Wakati nikitumia yako, wewe chukua yangu utumie kwa muda mpaka nitakapo kurudishia.” Junior akaongeza na kumnyooshea simu yake kabisa akimkabidhi. Emelda akabaki amesimama. Simu hapokei wala hatoi yake. Wote sasa kimya, pakawa kama kumetengenezwa tension.

“Emelda, nimekuomba simu. Au kuna kitu humo hutaki nione??” “Ndiyo.” Akajibu na kushangaza wote. “Ni nini!?” Kimya. “Emelda?!” “Nashauri acha tu Junior. Tumekua na wakati mzuri hapa, tumeomba, tukapumzike. Mengine tuendelee nayo kesho.” Akaongea taratibu wote wakimtizama. Junior ndio akaweka mikono mfukoni kabisa, kama anayemwambia hataondoka hapo.

 “Ni nini Emelda?!” Ezra akaongeza swali kwa wasiwasi. “Junior na Ezra, nyinyi mnataka kuharibu siku nzima nzuri ya leo. Naombeni tuhitimishe, mengine yaendelee.” Akamuona na Ezra naye ameweka mikono mfukoni kama mwenzie. Akawatizama wote wawili kwa zamu, akaona wamekusudia kuweka mgomo mpaka wapate hiyo simu. Akamkabidhi simu Junior kama anayewaambia, mkumbuke niliwaonya. Akapokea.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa haraka sana akaingia kwenye jumbe. Akakutana na jina la Edwin juu. Akajua huyo ndio mtuma ujumbe wa mwisho. Akafungua na kukutana na picha zake, Emelda na watoto wa pale kanisani wakihudumu. ‘Haya ndiyo yalikuwa maisha yetu. Na hizi ndizo zilikuwa ndoto zangu, tumtumikie Mungu kwa namna hii. Niliikuta hii huduma si kitu hata Junior mwenyewe hajui kinachoendelea. Nimeanzia chini kabisa na kutengeneza kundi langu la watu watakao tumika hapa, wewe ukiwa msaidizi mkuu, yeye anaingilia na kusambaratisha!’

 ‘Baba yake anafumbia macho kwamba mimi ndiye wa kwanza kumfuata kwa heshima na wazee wengine juu ya uchumba wetu! Tena wakaomba na mimi! Kweli ananigeuka kikatili hivi na kutoa baraka zake kwa kijana wake ambaye ana kazi ya kuchumbia mabinti hapa kanisani, na kuwaacha wakiwa amewaumiza!’ Junior akaanza kutetemeka mpaka akawa anaonyesha kabisa.

‘Mungu wanaye muhubiri yupo wapi? Basi hata kama hii huduma kwao ni biashara tu, kweli wamenyimwa kabisa roho ya ubinadamu! Mimi ambaye niliwaambia kabisa, nataka kukuoa. Kweli wananipokonya msichana mmoja tu niliyekuwa nimetulia naye, wanamkabidhi kijana wao ambaye anachafua tu mabinti hapa kanisa!’ Kwa kadiri alivyokuwa anabadilika, Ezra akajua hali ni mbaya. Akashauri warudi kukaa. Wakarudi wote sebuleni. Lakini kimya hapo kwenye makochi wakimwangalia Junior aliyeshindwa kukaa, na kubaki amesimama akiendelea kusoma.

‘Sasa tutaona hiyo kesho wakati na wewe akikuingiza rasmi kwenye msururu wa mabinti aliowakabidhisha kwa kijana wake awaharibie maisha, akitangaza uchumba, napo atamuomba Mungu yupi!’ Emelda yeye alibaki amejiinamia tu kimya, hata hamwangalii mtu akijua anachokipata Junior.

‘Kama wewe unawaogopa sababu wanakutunza hapo kwao, nilikwambia Emelda, milango ya kwangu ipo wazi. Muda na wakati wowote nakukaribisha na tunaweza kwenda kumtumikia Mungu wa kweli sehemu ingine sio kwa hao matapeli.’

‘Kama wewe unawaogopa, mimi sitakubali. Nitapambana mpaka pumzi yangu ya mwisho. Waache uonezi kwa sababu wana pesa. Kwanza hizo pesa zote ni sadaka zetu tu. Sitakubali wanidhulumu. Walikuwa wakijua fika nakutunza, wakati wao wamekutelekeza, macho kwa wasichana wengine. Sasahivi wanaona vinang’aa ndio wanaanza kukimbilia!? Walikuwa wapi muda wote huo, wakichumbia binti wengine na ulikuwa ukiishi nao nyumba moja!? Hakika sikubali. Nitapinga hata mahakamani, wasilete habari zao zakibabe. Nitawashitaki mpaka kanisa lao lifungiwe na serikali. Wasituone tumenyamaza, wakafikiri sisi ni wajinga.’ Ikawa mwisho.

Akajitumia huo ujumbe yeye na Ezra. Simu yake ilipoingia ujumbe tu, akajua unatoka kwa Junior, haraka sana na yeye akafungua na kuanza kusoma. Jelini kimya anasubiria. Emelda akabaki amejiinamia vilevile, kimya. Yeye Junior akaanza kusoma tena kutoka kwenye simu yake.

~~~~~~~~~~~~~~~

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment