Akatoa simu yake mfukoni. “Mama huyu! Naomba kuzungumza naye.” “Hamna shida.” Junior akapokea. “Mnaweza kuja nyumbani sasahivi? Wote watatu na Ester naye anakaribia kufika.” “Hata hivyo sisi tupo njiani, namrudisha Emelda, amekataa kuhama mpaka akuachie msichana wa kazi.” Huyo mama hakuamini.
“Kweli Junior!?” “Tulisha mpatia mahali, lakini amekataa, anasema labda kama wewe ndio unataka aondoke.” “Nilivyo na shida naye huyo binti! Hakika Mungu wa mbinguni amkumbuke na yeye siku ya uhitaji wake, na uzee wake ukawe wa heri.” “Amina mama. Atasikia ila nimemuacha Ezra na Jelini.” “Ni muhimu Junior, unajua nisingewaingilia mida hii.” “Basi nitamwambia.” Akakata na kumtaarifu Ezra.
“Hata hivyo nimeshamruhusu Jelini akapumzike. Na yeye amekuwa na siku ndefu, hapa tupo barabarani.” “Afadhali. Sikutaka kuwaingilia.” “Usijali. Nakuja.” Wote watatu safari ya kwa mchungaji ikaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba nikuombe kitu Junior.” “Hutaki kesi?” Junior akawa ameshamuelewa. “Kabisa. Ila nitaomba kujua kwa hakika, Ester alimjibu nini Edwin.” “Basi nitaliwekea msisitizo, maana mchana amekwepa kabisa kujibu. Amekua akizunguka na maneno mengii! Sijui ana nini! Kwa hakika leo ndio nimetambulishwa Ester ambaye sikuwahi mfikiria kabisa!” Akapotelea mawazoni, naye Emelda akanyamaza mpaka nyumbani.
Wakawa kama wameongozana na Ezra tu. Hakukawia. Wakaanzisha kikao chao hapo nje. “Hatutaki kesi, ila kujua alimjibu nini Edwin. Hilo tu.” “Sawa.” Ezra akakubali na kuongozana ndani.
It gets worse, before it gets better.
{Usikimbie.}
Wakakuta ni kama wanasubiriwa wao. Emelda akakaa, akashangaa Junior na Ezra wanakaa pembeni yake. Akawekwa mtu kati. “Kabla hatujasikiliza mlichotuitia, naomba niwaombe jambo la kwanza. Maneno yote aliyozungumza Ester kwa jumbe na kurikodi, nikuombeni wote, kwa Ester nitazungumza naye baadaye, ila hapa, na kwengine kokote kule, yasijewahi rudiwa tena. Iwe mwisho. Niombi.” “Wala huna haja ya kuomba, hata jumbe zenyewe nimefuta kwenye simu yangu, kwa hofu.” “Nashukuru mama. Kingine, hatutaki kesi. Kama ndicho mlichotuitia, sisi hatutaki kesi na Emelda hivyohivyo, ila ana ombi moja tu kutoka kwa Ester.” Kimya wote wakimwangalia Junior.
“Anataka nini?” Mama yake akauliza. “Kujua ukweli wa alichomjibu Edwin juu yake. Na katika hilo sitayumba mama. Maana mchana alituzungusha, tukaondoka bila ya jibu. Lakini sasahivi NATAKA Emelda ajibiwe.” “Sema ni wewe ndio unataka kujua.” Ester akaongea kwa kiburi. Wote wakamtizama.
“Halafu zidhani kama ni sawa eti niwaambie mazungumzo yangu na Edwin! Hayamuhusu mtu. Ni kati yangu na yeye.” Walishangaa, wasiamini. “Ester mwanangu, umepatwa na nini wewe!?” “Maana wamekuja kama kunisuta wakati na mimi sina baya nililofanya! Nimefanya kama wewe tu mama ulivyonifanyia mchana. NIMEMKUMBUSHA Emelda alipotoka, asije jisahau.” Walibaki wamepigwa na butwaa, wasiamini.
“Sasa mnashangaa nini?! Mlipo nikumbusha mimi mchana mpaka mkaniliza, mliona sawa. Akikumbushwa huyo Emelda ndio sio sawa?! Kwa nini?!” “Kwa kuwa sasahivi umekua, una kwako na maisha yako, sitataka kukupotezea muda usiku huu. Ila na mimi naomba unijibu jibu moja tu, na lisiwe refu Ester mwanangu. Kutoka ndani ya moyo wako, jumbe ulizotaka zimfikie Emelda, zikaishia kwa kaka yako,..” “Wala hazijaishia kwa bahati mbaya, amempa makusudi ili kunichonganisha na kaka zangu. Lakini mimi sijali. Yeye si anataka kuwa mtawala wa hii nyumba? Abakie akipendwa yeye mwenyewe, sasa tutamuona atafika wapi.” Emelda kimya.
“Ipo roho imekuingia Ester mwanangu, si kawaida hata ya asiyewahi kumsikia Mungu hata mara moja! Huwezi kuzungumza vile kwa kiumbe kilichoumbwa na Mungu! Umepatwa nini Ester mwanangu?!” “Najua tu utamtetea kwa sababu sasahivi ni mwanamke wake Junior.” “Acha nikuombe kitu Ester binti yangu.” Kwa mara ya kwanza mchungaji akaingilia.
“Kwa jinsi nilivyokusikiliza hata ukimjibu mama yako, nahisi, hiki kikao kizima kwako tutakupotezea muda tu. Nataka kukuruhusu uondoke tu, acha sisi tutamalizana na Emelda. Ila nataka kukuomba jambo.” Wote kimya wakitaka kumsikia mzee kwa binti yake kipenzi. Hata mama mchungaji safari hiyo akataka kusikia kwa hamu sana.
“Kwa kuwa upande uliosimamia unaamini ni sahihi, hutaki kuhama hapo,” “Kwa sababu..” “Tafadhali usiniingilie, Ester binti yangu, nivumilie tu nitamaliza na wewe utaondoka. Nakuahidi sitakuchelewesha.” Wote kimya. Kwa mara ya kwanza hao wawili kusikika kama wanaanza kuwa kambi mbili tofauti! Hata Ester akaonekana kushitushwa kidogo.
“Kama kile ulichoandika kwa Emelda juu ya kanisa, unakusudia kukisimamia, nakuonya ACHA. Hapa nasimama kama mchungaji, nakusihi acha kazi ya Mungu, iliyoanzishwa kwa machozi, mifungo, tukikesha na kuomba.”
“Huyu Junior ameanza kukesha kanisani akiwa bado ananyonya hana hata mwaka! Tupo naye tukimuomba Mungu kwa ajili ya huduma hii, tena tukiwa tunafanyia sehemu ya dhiki kwelikweli, wala nikikueleza hutaelewa. Mazingira yasiyo faa. Lakini tulikuwepo hapo usiku kuchwa tukiombea kazi ya Mungu.”
“Kama unavyojua maombi peke yake hayatoshi, Mungu hana benki anayotuma watu wake wakachukue pesa. Hapo napo nikaona watu kujitolea mpaka visenti vyao vya mwisho, ili Mungu atengenezewe nyumba ya kuabudiwa. Hao kaka zako unaowaona hao, wamemnunulia Mungu kile kiwanja kwa pesa yao bila kunikopa au kukopesha kanisa. Hawajawahi dai hata shilingi. Mpaka mimi nilipopewa zawadi ya kile kiwanja, ndio nikawapa na wao, angalau waanze kujijenga. Lakini mpaka kwenye ujenzi wa lile kanisa, walikuwa wakitoa pesa yao bila kujali malipo.”
“Leo watu wamepata jengo nadhifu, wanakutana na Mungu wao. Wanafarijika. Wanapokea uponyaji. Wapo waliopata kimbilio, kuanzisha familia zao kwenye ile huduma. Wanakutana kwa ushirika na mengine mengi. Usihusike kwenye kuharibu ile kazi ya Mungu kwa maneno ambayo hayatajenga ila kubomoa.” Akajiweka sawa akionekana kubadilika kabisa, sio kama walivyomzoea kwa huyo binti yake.
“Nimesema hapa nazungumza kama mchungaji. Na ndipo nakuja kwenye ushauri wangu wa mwisho kabla hatujakuruhusu, kama huu ushauri wangu utaona hautakufaa, haukubaliani nao, HAMA KANISA.” Walishituka, hawakutegemea.
“Yaani baba unanifukuza kanisa sababu ya Emelda!” “Unazungumza nini Ester binti yangu!?” Akakaa sawa akijivuta mbele kabisa ya kochi. “Ile kazi si yangu, mama. Na mimi nimeitwa na kupakwa mafuta. Aliyeniita hana upungufu ya watenda kazi. Nikishindwa mimi, atanitoa kama alivyomtoa Sauli na kumpa Daudi! Kwani Sauli yeye hakupakwa mafuta kuwa mfalme wa Israel? Si alipakwa! Tena si ni kwa ruhusa ya Mungu? Alipojiinua kinyume ya Mungu, Mungu akaenda kutafuta mchunga kondoo, akaamuru apakwe mafuta, akawa yeye mfamle! Tena huyu mfugaji akawa mfamle bora na mzuri kuliko mfamle Sauli aliyetambulishwa kwenye bibilia kuwa ni mzuri kwa muonekano!”
“Ester, nimetubu mbele za Mungu kwa machozi kabla hujaingia hapa. Muulize mama yako. Niliogopa hata kutubu nikiwa nimekaa. Nimelia mbele za Mungu, nikimsihi akusamehe na atusamehe na sisi hata kwa kuona hizo jumbe!”
“Mama, huyu Mungu ametutoa pabaya! Hata ni bora ya Emelda amekuja hapa kwetu na viatu! Mimi nimekutana na viatu na utuuzima wangu. Shule nimekwenda bila viatu! Kuwe na mvua kuwe na jua, miguu tupu, Ester mwanangu. Hakuna chakula siku nzima mnashinda maporini kula matunda kama ndege!”
“Muulize mama yako huyu hali aliyonikuta nayo. Mbaya. Tunakutana kanisani, nimetoka kulinda. Usiku kuchwa nipo kwenye majumba ya watu nikilinda. Ikitokea ni jumapili ujue natoka kazini, sijaoga, nakimbilia kanisani kusafisha. Naandaa kanisa ili watu wafike pasafi, kisha kupiga gitaa ili wamuabudu Mungu wao. Amenikuta mama yako nina kiatu aina moja tu. Hichohicho kila mahali panaponilazimu, kwengine navaa kandambili!”
“Kama isingekuwa kunipenda huyu, asingekubali kuolewa na mimi. Sikuwa na kitu. Sijawahi kukutana naye nikiwa nimetoka kuoga. Wakati wote natokwa jasho nakimbizana na maisha. Kwengine natembea zaidi ya masaa ili nifike mahali. Hapahapa Dar ambako watu wanamiliki magari.”
“Natoka kulinda kwenye majumba ya watu yakifahari kama haya mliyokulia nyinyi, nakwenda kulala sehemu mbovu haifai! Nimeoa ndio nikahamia kwenye chumba chenye taa! Kimoja tu. Tunaishi hapo mpaka tumempata na Junior. Tumejibana hapo wote sisi watatu. Na si siku moja, wala miaka miwili. Hatuna kitu, ila tumaini kwa Mungu tuliyekuwa tukimtumikia. Wakati mwingine tunafunga si kwa ajili ya maombi, hamna chakula! Mnataka kufungua, hamna chakula, mnaongeza siku ya kufunga.”
“Junior huyu ameanza kufunga hata miaka 10 hakuwa amefikisha! Yeye anajua ninachozungumzia, maana ameyaishi maisha yangu na mama yake. Na Mungu naye akatujalia, hakuwa mtoto wakulia. Si kwa njaa, si kwa ugonjwa. Muulize mama yenu mpaka majirani walikuwa wakishangaa kama kuna mtoto ndani. Alikuwa akimnyonya mama yake, hakuna kitu kinatoka, mama ananjaa, chakula hakuna, maziwa yamekoma, lakini ni kama alizaliwa akijua hali yetu, aisee! Kimya, anaishia kulala na njaa yake.”
“Kipindi kile kama hata malaika angetumwa na Mungu kuniambia nitakuja kuishi kwenye nyumba kama hii, na kuaminiwa kwenye huduma kama ile, kwa hakika nisingesadiki. Mama yako anajua ninachozungumzia.”
“Nimekwambia nimeomba toba kwa machozi, tena kwa kutetemeka mbele za Mungu. Ester, mama, huyu Mungu anampa amatakaye, na hakuna wakumuuliza kwa nini! Niamini mimi, najua ninachozungumzia. Amenipa mimi! Yaani Mimi! Niliyekuwa duni, sistahili! Acha kucheza na huyu Mungu.”
“Mbaya zaidi, hichi ulichofanya wewe kwa Emelda, ndicho kilimpata mama yako kwa dada zangu. Wakiona kale kamshahara kaulinzi, eti binti ambaye alikuwa huyu mama yenu, eti ndio amenipendea hicho! Mwanamke niliyemkuta mjini! Kila nikikutana naye, mwenzangu msafi na mke wangu ni mzuri bwana.” Mpaka kina Ezra wakacheka.
“Sijivunii, mpaka leo mke wangu mzuri. Wanaume walikuwa wakihangaika mpaka ndani ya ndoa walikuwa wakimuulizia wakimtaka aniache mimi mlala hoi, wamchukue. Sio mchezo! Kama hamuamini, muulizeni mwenyewe mkiwa peke yenu.” Wakawaangalia wakicheka taratibu.
“Lakini nataka kukwambia, kwa ile dhiki ya kwetu, nilikotoka kwa wazazi wangu jinsi ilivyokuwa duni, yaani eti mimi na ile hali yangu, eti ndio nikaonekana tajiri. Ndio ujue nilikotoka ni pabaya, siwezi hata kujilinganisha na Emelda.”
“Nimemuomba Mungu asiyatazame maneno yako, zaidi hapa kwetu yalipoingia. Mimi siwezi wala sithubutu kukufuru, mama. Nimetoka kubaya kuliko huyu Emelda. Tena kubaya sana. Ndio maana siku zote, mimi na mama yako hatuthubutu kumuangalia mwanadamu aliyeumbwa na Mungu kwa jicho ambalo Mungu hamtizami nalo.”
“Kwa kuwa tumetoka chini, sanaa. Na kwa hakika, hapa tulipofika hata sisi tunasema ni muujiza ambao tunaushikilia kwa unyenyekevu sana tukijua Mungu, hajaishiwa wahitaji na hata watumishi. Sijui kama umenielewa?” Kimya.
“Katika hili, tafadhali nitataka unijibu, tena kifasaha maana sitakuruhusu uharibu kazi ya Mungu, kwa sababu yeyote ile. Umenielewa Ester?” Mzee akawa mkali kabisa. Ila akawa kama ameshindwa kumjibu. Junior akafikiria kwa haraka, akahisi kitu. “Au umeshaanza kusambaza?” Kimya. Hapo ndipo waliposhituka sana.
“Mungu wangu Ester, mwanangu wewe! Umezungumza na nani?” Mama akahamaki kwa hofu, lakini akabaki kimya. Kwa haraka sana, kama kufumba na kufumbua Junior akasimama na kwenda kukwapua simu yake.
Na yeye akasimama kama amrukie kaka yake achukue simu yake. Junior akamuwahi. “Hutapata hii simu kwa sababu, na wewe ulichukua simu yangu ukasoma jumbe zangu kwa siri bila ya ruhusa yangu. Kaa chini utulie.” “Rudi kukaa Ester.” Baba yake akamuamuru.
Junior akaenda kwenye jumbe, akakuta amewasiliana na Hope pamoja na Edwin. Akaanza kusoma za Hope mapigo ya moyo yakienda kasi. ‘Usikubali kumuachia Junior. Sio akili zake. Emelda amemloga ili amchukue yeye. Ila Junior anakupenda wewe. Tutamuombea mpaka afunguliwe. Na kesho tutajipanga vizuri.’ Akaona Hope alimjibu. Akakimbilia kusoma. ‘Mimi nimezungumza vizuri sana na Junior. Sijaona kama anatatizo la akili. Tumekubaliana vizuri tu. Hapa nasubiria anikabidhi kadi ya gari na funguo zake. Amenitia moyo kwenye huduma. Narudi kutumika kanisani. Sitaki kujichanganya tena, Ester. Acha nitulie nisije kosa kotekote.’ Hayo yakawa majibu ya Hope, kidogo Junior akaridhika. Ni kama swala juu ya Emelda akawa aidha hajalielewa au moyo na akili zake vipo kwenye mali tu. Ila akashukuru kwa hilo.
Akahamia kwenye jumbe zake na Edwin. Akakuta moja tu ya siku hiyo. ‘Changamka Eddy! Huu ndio wakati wako na Emelda. Chelewachelewa utakuta mwana si wako. Ushaomba vyakutosha, sasa chukua hatua.’ Junior akapata jibu lililokuwa likiwasumbua wote. Edwin hakuonekana kujibu.
“Kwa kujibu swali la kila mmoja wetu hapa, zaidi Emelda, kwa ujumbe huu ambao Ester amemtumia Edwin, inamaana hakumpa jibu lako. Huyu mtu alikuwa akipokelewa vitu vyake akiwa na tumaini kwako. Na si sawa.”
“Kwani amewasiliana na Edwin pia?!” “Yaani mama, wakati baba akisita kumtafuta Ester akidhani bado yupo honeymoon, kumbe yeye yupo busy kuvuruga watu.” Junior akawasomea jumbe zote.
“Umepatwa na nini Ester, binti yangu?!” “Baba unanilaumu bure bila sababu. Uchawi upo. Iweje kama kweli huyu Emelda amemlisha mavitu ya kichawi Junior? Sio hata wewe umelalamika kuwa Junior amebadilika? Sasa unafikiri mabadiliko hayo yanatokana na nini? Sisi tuombe, kama hakuna uchawi si basi!” “Sasa kama ni uchawi aliolishwa Junior, kwa nini na mimi usinipate?! Maana kila alichokula Junior, kutoka kwa Emelda, na mimi nimekula!” Ezra akaongeza kwa kumshangaa kabisa.
“Na kweli! Halafu jamani, huyu Mungu tunayemtumikia, tunamwamini kwenye kusamehe dhambi tu, kwenye kutulinda na mabaya yote hapo ndipo hawezi!? Kwamba kweli leo huo uchawi wa Emelda ndio una nguvu kuliko ulinzi wa KiMungu?!”
“Asante mama. Maana na sisi tulijiuliza swali hilohilo.” Ezra akawapitisha kwenye maandiko yote juu ya ahadi za Mungu. Kisha akamalizia na Mathayo 16:18 Nami nakwambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu,’ na hapo ndipo inapokuja ahadi ambayo watu wengi wanaikosa sana na kutaabika na uongo wa shetani juu ya uchawi.”
“Ahadi yenye nguvu, lakini wamechagua kuamini uongo wa ibilisi kupitia vinywa hata vya watumishi wa siku za leo, kuliko kumuamini Mungu mwenyewe, au ahadi ya Yesu. Maana amemalizia kwa ahadi yenye nguvu sana kuwa, ‘wala milango ya kuzimu, haitalishinda.’ Anazungumzia hilo kanisa lililojengwa kwenye huo mwamba ambao ni yeye mwenyewe Yesu Kristo.”
“Sasa kwa nini wewe utishwe na uchawi!? Kama upo na Emelda anafanya, si muache mwenyewe kuliko kuvuruga watu kanisani! Sisi hatuna hofu kwa kuwa huku kwa Yesu, hatubahatishi. Imani yetu imejengwa kwenye mwamba. Hatuogopi kulogwa, kwa sababu madhara yake si SEHEMU YETU. Hofu yetu sisi ni hiki unachokifanya sasa hivi wewe Ester. Wala si uchawi hata kidogo. Ila hichi unachokifanya ndio kina madhara na hata bibilia imeandika. ‘Chachu ndogo, huchachua donge zima.’ Hicho ndicho tunachohofia.”
“Na wala si hivyo tu, Kitabu cha Yakobo pale mlango wa 3 kimezungumzia sana juu ya ulimi. Wewe unatafuta habari za uchawi zinazotungwa na watumishi wanaotaka kutia hofu watu ili kuwafanya mateka wao, kwa kitu ambacho HAKINA MADHARA KWETU KABISA! Unaacha mambo ya msingi unahangaika na vitu visivyo maana!”
“Mstari wa 6 hapohapo mlango wa 3 kwenye kitabu kichohicho cha Yakobo kinasema, ‘Nao ulimi ni moto, ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwasha moto na jehanamu.’ Soma mlango mzima jinsi unavyoeleza kwa undani tena kwa kutisha kuliko hata huo uchawi!”
“Hakuna sehemu imeongea ubaya wa uchawi kwenye bibilia kama ubaya wa ulimi. Una nini Ester!?” Junior akamuuliza kwa kuumia sana kisha akaongeza swali jingine japo hata la kwanza hakuwa amejibiwa.
“Acha nikuulize swali la msingi Ester dada yangu. Najua umezaliwa kwenye dini. Wokovu, kazi ya msalaba, hofu ya Mungu, umekua ukivisikia vikiongelewa tokea unaakili zako ndogo kabisa, kiasi ya kwamba pengine umezoelea, au unaona ni maneno ya kawaida. Umebatizwa kama wengine tu. Lakini leo nimepata nafasi ya kukufahamu dada yangu, hivi kweli wewe binafsi. Mbali ya kwamba ni mtoto wa mchungaji, ulishawahi kukutana na Yesu kibinafsi? Kwamba ukapata wakati wakumtambua jinsi alivyo na nguvu zake, ndipo ukaamua kumfuata?” Kimya. Wote wakimwangalia.
Kisha akajibu. “Mimi nimeokoka.” “Kila mtu ameokoka siku hizi. Swali la Junior ni la msingi sana Ester. Wewe binafsi, umebahatika kumfahamu huyu Mungu kwa uhalisia, sio wa kufuata familia?! Maana kama kweli ungekutana na Yesu, na uweza wa nguvu zake, hata kama Emelda angekuwa ana dhambi za namna gani, usingemtizama na kumuongelesha kwa namna hii!” Ezra akaendelea taratibu tu bila ya jazba.
“Usingemtizama kwa jicho unalomtizama nalo na kumpa maneno mabaya ya kiasi hichi! Ni swali la msingi unatakiwa kujiuliza Ester. Upo uhuru wa kweli na pumziko ambalo hutayumbishwa hata kwa mahubiri haya ya siku hizi. Utamjua Yesu na nguvu zake. Mambo haya yanayowatisha watu na kuwafanya wasilale, wewe ndio yatakupa usingizi. Wenye dhambi utawaangalia kwa jicho alilowaangalia nalo Mungu mpaka akamtoa mwanae wa pekee aje awakomboe. Utawakimbilia na kuwapenda, ukitaka watubu, wawekwe huru. Si kwa namna hii.” Ezra akamalizia.
Mchungaji akapokea. “Na ndipo nakuja kuweka msisitizo. Wakati ukijitafuta upande uliopo. Na ukifanya maamuzi yako ya kiroho, ACHA KAZI YA MUNGU. Kokote utakapoenda, chini ya mchungaji yeyote yule, kaa mbali kabisa na kazi ya Mungu. Usivuruge watu kwa hila zako. Umenisikia sawasawa Ester?” Kimya.
“Angalia kama kuna aliowapigia simu ili tujue jinsi…” “Mama, huko kwengine usiende. Ester hatakiwi KUJUA kabisa mipango ya kanisa, mpaka nitakapomuona amekaa sawa na Mungu. Chochote kinachoendelea kuanzia sasa, asihusishwe tena. Ila naomba Junior angalia aliowasiliana nao. Akiondoka ndipo tutajua chakufanya. Ila kuanzia sasa, Ester asihusishwe kwa chochote juu ya kanisa.” Hapo Ester akalia sana.
“Kwamba unanitoa kwenye hii familia!?” “Hii familia na kanisa ni vitu viwili TOFAUTI mama. Hapa mimi ndio kichwa cha familia. Ila kule kanisani, wote tumeajiriwa. Na Aliyetuajiri anao watenda kazi wengi sana. Na unavyotuona hapa, hayupo ambaye yupo tayari kustaafishwa. Sasa wewe usituponze. Umesikia Ester?” Akamuuliza kwa ukali kabisa. Kimya akilia.
“Hapa nyumbani sisi tutabebana kwa kila hali. Unakaribishwa kuingia na kutoka vile utakavyo. Lakini si kwenye kazi ya Mungu. Hapo sitakuruhusu Ester. Binafsi nimekataa kuwa kama Eli aliyeponzwa na watoto wake mpaka akapokonywa nafasi yake ya unabii na kupewa mtoto mdogo kabisa, tena aliyekuwa hata hajui sauti ya huyo Mungu, Nabii Samweli. Lakini Mungu akamtoa Eli aliyekuwa akimjua vizuri, akaenda kumpa nafasi Samweli! Kijana mdogo tena aliyekuwa akimtunza yeye mwenyewe nyumbani kwake na Samweli aliishi pale akitumwa kazi na Eli! Lakini kama mchezo hivi, Mungu akapindua nafasi zao! Mimi nimekataa.”
“Na ndio maana unaona siku hizi hata mdogo wenu hafiki kanisani amelewa. Nimemwambia akirudia hivyo, basi. Asifike tena pale kanisani. Hata sisi watatu hapa tunajua kupiga vyombo. Na nina uwezo wa kuajiri watu wakupiga vyombo, watu wakamuabidu Mungu wao kwa amani.”
“Muulize mama yako kama naongopa, na kama Noah amerudia kukanyaga kanisani akiwa na pombe kichwani. Msitake kunitia matatizoni kwa Mungu wangu. Mimi namjua. Na nina mwamini, ndio maana nilikuwa nikitembea masaa, kwenda kukutana naye na kumuabudu na watu wake. Namjua kwa hakika ninaye mtumikia. Ni mwingi wa rehema, lakini pia ni MOTO ulao. Mimi najifunza kwa walio tangulia. Msinikosanishe na Mungu. Haya Junior, kama umemalizana na simu yake, mkabidhi awahi kwake.” Junior akamkabidhi.
“Kama unavyojua, kesho Ezra anachumbia. Kama huna tatizo na Jelini naye, na unakubali kutii, hutasambaza sumu zako kwa watu na kuwavuruga, basi karibu kanisani. Na hapa nyumbani kutakuwa na tafrija nzuri sana. Haya usiku mwema.” Mama yake akamalizia. Ester akachukua pochi yake na kuondoka bila yakusema kingine.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mchungaji akamgeukia Emelda. “Mungu wetu ni shahidi, na atatutetea kwako Emelda binti yangu. Sisi hatujawahi kukuona tofauti. Au kuna jinsi yeyote tumekwisha kukuonyesha ubaya wa aina yeyote?” “Hapana.” Emelda akakataa. “Au hata dharau, kubaguliwa, kitu chochote ulichoona kimetokea hukupenda?” “Hapana. Hakuna baya mlilonitendea. Na naomba muwe na amani kwangu, hiki kilichotokea kwa Ester kwangu si kigeni kabisa na ndio maana nimerudi.” Wazazi wakashangaa.
“Kwamba alishakwambia kabla!?” “Wala si mara moja mama yangu. Nimeshamzoea. Mimi sina neno kabisa. Labda mnisaidie tu kufikiria jinsi ya kumkabili Edwin. Naona si sawa kwake. Amekuwa akitoa vitu vyake kwangu wakati nilishamrudishia jibu la hapana!” “Tutafika huko Emelda. Lakini kwa nini hukuwahi hata kumwambia mama yake!?” “Kwa sababu ulikuwa ukweli. Katika yote hayo hakuna alilodanganya kasoro tu la uchawi. Mimi sijui hata mlango wa mganga jamani! Sisi kwetu ni mafukara lakini si uchawi. Ila mengine yote yupo sahihi.” Walipoa hapo kama kuna msiba. Kimya kwa muda.
Emelda akamtingisha Junior kidogo. “Daah! Najua umesema tuwe na amani, lakini wote imetuchukua kwa mshituko Emelda. Tafadhali tusamehe hata kukuacha kwenye hayo mazingira ukinyanyasika. Si sawa.” “Mimi naona nikiwaambia nimewasamehe naona ndio mtapata amani.” Emelda akaongea akicheka.
“Hakuna amani katika hili Emelda, binti yangu. Hakuna. Ila maadamu umeamua yaishe, basi, mama. Tupange yajayo.” Mchungaji akaongea akisikika mawazoni.
“Ila kesho kabla ya kutangaza uchumba wa Jelini na Ezra, lazima nitangaze kuvunjika uchumba wa Junior na Hope. Na kabla ya hayo yote, lazima nipate muda na nyinyi wote wawili tuzungumze kabla ibada haijaanza. Ili nimsikie na Hope pia.” Wakaona wazo zuri.
“Na nafikiri Edwin anastahili kumsikia Emelda mwenyewe. Sio sawa kwake. Alikuwa akitoa kwa matumaini.” Junior mwenyewe akaongeza na yeye akisikika mawazoni. Wakapanga mipango mizuri.
Wakaomba kwa pamoja. Wakaombea siku ya kesho yake na usiku huo. Akashangaa na mchungaji anamuombea mama yake na mdogo wake. Hilo likamfariji sana Emelda na kufurahia kutokukimbia usiku huo. Akajisikia kukaribishwa kwa mama yake hapo nyumbani kwa mchungaji, tena kwa upendo! Moyo ukajawa furaha na kumtukuza Mungu. Angalau huo usiku uliotaka kuisha vibaya ukaisha kwa utulivu.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Najua ni usiku sana wote tunahitaji kupumzika.” Kimya wote wakamgeukia Junior kama usianze tena.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment