Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 44. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 44.

Huku kwa Ezra yeye akiwa anaendelea kukanyaga mafuta, akampigia Jelini na kumwambia wakimaliza, wawajulishe watawaambia sehemu ya kukutana. Nakumuomba amwambie Emelda, Junior aliondoka na simu yake, asiitafute. “Lakini na sisi tumemaliza Ezra. Tutawafuata muda si mrefu.” Akafikiria, ila akawa hana sababu ya kuwazuia. Akakubaliana nao, kwamba wakishusha viti, wawafuate. Hilo likakaa sawa.

    Wawili hao wakaanza kusaka sehemu ya kuishi ya Emelda usiku huo. Kukiwa hakuna wasiwasi wa pesa ila sehemu tu. Wasijue kinachoendelea kwao. Ukawa usiku mzito haswa.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Sitageuka kuwa mama yako. Na Ester hatakua dada zako. Nimekataa.” “Mbona kama hii kesi imekua yangu gafla!?” “Kwa kuwa wewe ndiye unayemuendekeza Ester. Msichana yule wa mwisho kabla ya Emelda, hakutuambia juu ya Ester ukamkania? Sasa leo umesikia na sauti yake kabisa, akikufuru kwa msichana kama Emelda aliyekuwa akimzolea matapishi! Unataka alaaniwe?” Kimya.

“Au na hiyo sauti utasema si yake amesingiziwa!?” Kimya. Akamkabidhi simu yake. “Mpigie Ester, mwambie namuhitaji hapa, sasahivi.” “Hata mimi nimeshituka mama! Najua ni kufuru mbaya sana. Na nimeingiwa hata hofu mbele za Mungu. Natamani hata hayo maneno yasingepitishwa hapa kwetu. Lakini huyu mtoto yupo kwenye ndoa changa, mama J. Kweli tumtoe kwake usiku huu ili tuanzishe kesi?! Hivi mumewe atatuonaje sisi?” “Kwa jumbe hizi, za mpaka muda huu, inaonekana anao muda wa ziada. Nashauri hiki kikao kifanyikie hapa na si kwake.” “Kwamba utamfuata!?” Mama akakaa vizuri.

“Nimekwambia sitampoteza Junior kwa mwanamke. Sitamsusa kama KWENU walivyonisusia wewe. Maana ni hivi, Emelda atakapotoka hapa bila maelewano, ujue zile siku chache nilizokuwa nikibahatika na kina Junior, zitahamia kwa Emelda. Sitawaona tena hapa. Halafu, kwa kuwa Ester ameahidi kumchafua hata kanisani, inamaana atahama kanisa. Ujue ndio na Junior atahama. Alipo Junior ndipo alipo Ezra. Ndio Jelini. Halafu na familia ya kina Jema itahamia huko alipohamia Emelda, ambapo yupo Ezra na Jelini. Mpaka hapo unanielewa ninachozungumzia?” Mzee kimya.

“Mimi si mjinga kumkubali Emelda, kwa sababu najua madhara ya kupinga mapenzi. Ni kuwaweka wale wapenzi karibu zaidi, kama kweli wanapendana. Kama kilichotokea kwetu. Kadiri mama yako na dada zako walivyokuwa wakinichukia na kunifanyia visa, ikatusaidia kutusogeza sisi karibu zaidi. Mwishowe kwakuwa walishindwa kuwa na sisi wakati ule, sasahivi wanaona aibu kujirudi.”

“Ndicho kinachotaka kutokea sasahivi kwa Junior. Lakini mimi nimekataa. Mke atakayeolewa na Junior, atapendwa na kuheshimiwa humu ndani kama Ester. Kwa kuwa, narudia tena. Sitampoteza Junior, mtoto niliyekuwa nikishinda naye njaa wakati tukiwa sisi si kitu. Maana  hawa wengine wametukuta tukila milo yote na kusaza tukichagua nini tule, lakini si Junior.”

“Mtoto asiye na makuu ila kusaidia kila mtu akijinyima yeye! Amemwaga mamilioni ya pesa kwenye huduma pale kanisani bila kutaka kulipwa.” “Mama J, mke wangu, mimi nipo upande wako na Mungu wangu ni shahidi. Hizi jumbe zinanitisha mpaka naogopa. Tafadhali katika hili tusimame pamoja. Ninachozungumzia ni jinsi ya kushugulikia hili bila kuharibu zaidi.” “Basi chagua. Kikao ni hapa au nimuite Junior na Ezra nyumbani kwa Ester?” Mzee akafikiria kwa haraka akapata jibu.

“Mimi nina wazo.” Mama kimya akimtizama. “Nafikiri sisi tukae tuyazungumze halafu Ester tuzungumze naye kesho mida mizuri ya heshima hata kwa mumewe. Hatatuelewa kuanza kumuita binti tuliyemkabidhi kwa heshima tena mbele za Mungu usiku huu! Sidhani kama ni sawa. Emelda hana haja ya kuhama hapa.” Akamkabidhi simu. “Ya nini sasa?” “Hayo uliyoniambia mimi, mwambie na Junior. Akimleta Emelda hapa, ndipo tutajua baada ya hapo.” Akasita.

“Kwa hiyo tunakutana kwa Ester?” Mama akaendelea kusimamia pakali. “Unajua Junior hatanisikiliza kama ambavyo anakusikiliza wewe!” “Kwa sababu mimi namsikiliza na kumuheshimu. Huwezi kumpeleka Junior kama mtoto mdogo huku ukimuonyesha upendeleo wa waziwazi kwa Ester! Hawezi kukubali. Ukiongea naye kwa kuheshimu mawazo yake, hawezi kukataa. Mimi ameniambia ananitumia sababu 5 za kutorudi kwa Emelda hapa. Wewe unampa sababu gani za kumrudisha Emelda hapa?”

Kwa Emelda.

Emelda anakutana na kina Junior anaona jinsi walivyopaniki asielewe kulikoni. Akaomba kuzungumza na Junior nje ya ofisi walipokuwa wakisubiria jibu la meneja kujua kama kuna sehemu, yaani apartment ya Emelda. Wakatoka.

“Ni nini kinaendelea mbona unaonekana haupo sawa!?” “Nakutafutia sehemu ya kuishi wewe na kina mama wakija.” “Kwa nini sio tena nyumbani!? Mama amegairi?” Akamsimulia juu ya jumbe alizotuma Ester ila  hakumwambia kilichoandikwa au kurekodiwa. Akashangaa Emelda bado anasubiri sababu ya kutorudi nyumbani kwa mchungaji.

Nimezifuta kwenye simu yako, sitaki uzisikie.” Emelda akabaki anasubiria. “Kwamba mchungaji ameona ndio amekataa nisirudi kwake?” Yaani yeye Emelda bado akawa anasubiria sababu, Junior amemaliza.

“Sijawasiliana na baba ila mama.” “Kwa hiyo ndiye amesema nisirudi au!? Sijaelewa!” “Mimi ndiye nimeonelea usirudi. Inatosha Emelda.” Akabaki amemkodolea macho. “Huwezi kuendelea kunyanyasika.” “Juu ya jumbe za Ester!?” Jinsi alivyouliza akamfanya Junior kutulia kama sasa na yeye haelewi tena! Alijua atajipatia sifa kuwa anajali, akashangaa Emelda ametulia kama hajamsikia na alijua wazi amemuelewa.

“Sidhani kama wewe leo umesikia jambo jipya ambalo mimi sijawahi kumsikia Ester akiniambia, Junior.” “Sio hizi.” Emelda akacheka. “Katika hizo jumbe hakuna inayosema nilikuja kwenu nanuka na nikitumia mavitambaa yaliyochakaa kwenye siku zangu za hedhi mpaka yeye aliponisaidia pedi?” “Haiwezekani Emelda!” “Hajasema, nilikuja kwenu nanuka kwapa mpaka akawa hawezi kulala usiku?” “Naomba acha Emelda. Tafadhali usirudie.” Mpaka macho yakabadilika yakawa mekundu kama alie.

“Junior, kwa miaka yote hiyo nimekua nikiishi na Ester chumba kimoja. Na Ester ni yule akiwa kwenye hedhi anatapika nakuumwa tumbo, hata kama una roho mbaya vipi, huwezi lala jinsi anavyougulia tumbo na kutapika. Utamuhudumia lakini maneno atakayokuja kukupa baadaye! Unaweza sema siye yeye!”

“Atakukumbusha jinsi ulivyomuuguza akiwa kwenye siku zake. Nilivyomdekia matapishi yake na kufua mashuka yake ya damu, tena taratibu kama unavyomjua Ester, kisha anakuuliza, ‘utaendelea kuishi hivi mpaka lini?’. Yaani kama vile nilivyomfanyia ni haki yake!” “Emelda!!” Akacheka wakati mwenzie ana hali mbaya ya kupitiliza.

“Mimi mbona nishamzoea! Na najua huwa anachukia sababu huwa namnyamazia, simjibu.” “Kwa nini uishi hivyo Emelda!?” “Sababu, ya kwanza na kubwa ni mama yako. Sijawahi ishi na mtu akaniheshimu na kunipenda bila unafiki kama mama yako. Na kumbuka ni kama alinilipia garama au kuninunua au weza sema kununua uhuru wangu kutoka kule nilikokuwa nikifanya kazi mwanzoni na hajawahi nidai ile pesa.”

“Kingine nilikwambia Junior, nina majukumu ya familia ambayo siwezi ruhusu hisia zangu ziingilie. Nategemewa kwetu. Watu watatu wananiangalia mimi. Shule ya Mika na garama zake zote, ni mimi kufanya kazi ili alipe ada na michango yote ya shule pamoja na matumizi yake binafsi.”

“Bado shule ya Mateo ambayo inavijimichango vidogovidogo ambavyo bila hivyo wanakuwa wakimnyanyasa mbele ya wanafunzi wote. Siwezi pata usingizi nikifikiria hajalipa hiyo michango, inamaana atapitishwa na wale walimu pale kijijini pale tulipopita mimi na Mika. Fedheha ya hali ya juu. Unakuwa unachekwa na wanafunzi wote kama ambaye unatembea na kinyesi wakati wote. Bado kula yake na mama!”

 “Halafu pia najijua na kuwajua wanadamu. Sitaweza kwenda sehemu ingine nikapata mama mwenye nyumba mwingine kama mama yako, Junior. Nina uhakika kwa kuwa nimeishi naye na kuishi na watu wengine nikaona jinsi wanavyo nichukulia. Wanaoweza kusema, ndio kama kina Ester. Na wengine ndio hata hawahisi uwepo wangu hata nikiwa karibu yao, ni kama sipo tu. Lakini si mama yako.” Junior akazidi kuumia akijisuta na yeye.

“Leo asubuhi amehakikisha nimeondoka kwakwe kuja kwako nikiwa nimependeza. Mimi msichana wake wa kazi! Hanitambui mbele za watu kama msichana wake wa kazi! Ananitambulisha kama binti yake, tunaye nyang’anyana ziwa na Noah! Ndio usemi wake popote kule. Na ndiko hata Ester naye alikopata huo usemi. Na si uongo. Hatanifanya nikajisikia mimi kama kijakazi wake.”

“Ikifika kipindi cha ada ya Mika, namkopa mshahara wa mpaka mbeleni! Mika yupo shule leo, nakuhakikishia ni kwa sababu ya mama yako. Hanipunji mshahara wangu wala hanicheleweshei. Ukimfanyia jambo, anashukuru kama hastahili, wakati ananilipa!”

“LiNoah likiniomba nimfulie, mama alikuwa akijua nimemfulia au kumsafishia chumba, anamlazimisha anilipe mpaka na yeye amefanya mazoea. Huna utakachomfanyia Noah, na ulevi wake ule, sema nahisi kama limeacha! Siku hizi simuelewi vizuri. Amejaa pale ndani kazi uchokozi asubuhi mpaka usiku!” Junior akacheka kidogo vile alivyojiuliza, maana aliwajua hao wawili.

“Lakini vyovyote baba anavyomchukuliaga Noah, lakini huna utakachomfanyia asikushukuru kwa dhati, tena anakupa kabisa pesa. Mwenyewe anasema sio kama ananilipa, ni ananipoza. Lakini yote hayo ni kwa sababu ya mama yako. Alikuwa akimwambia Noah kama wewe ulivyokuwa ukimuomba akufanyie jambo kisha unampa pesa, ndio na yeye afanye hivyhivyo kwangu. Sasa hembu niambie, nampata wapi mimi mtu kama yeye?” Kimya.

“Ndipo narudi kwenye sababu yangu ya kwanza na ya msingi, sina jinsi ya kumlipa mama yako kwa kuishi na mimi kwa namna anayoishi na mimi isipokuwa kumsaidia. Mama yako ni mtu mzima, halafu na mama Leti ana matatizo ya mgongo. Kuna mambo mle ndani hayawezi kufanyika bila mimi. Yaani hata mama akinipa ruhusa kwenda kwetu, nikirudi nakuta hayajafanyika kwa sababu mama yako amekwama. Na yeye unamjua, si mvivu ila hana uwezo.”

“Kwa hiyo, kama yeye hajanifukuza, sitaondoka kwake mpaka tumpatie mtu. Tafadhali Junior. Tusimuadhibu mama kwa ajili ya Ester. Si mgeni kwangu. Ananiumiza, lakini sio wakumkimbia.” Junior akachoka kabisa.

“Tusijivuruge. Kesho ni siku muhimu sana kwa Ezra na Jelini. Twendeni tukalale, tuendelee na mipango yetu kama kawaida. Tusimpe shetani nafasi. Atatuvuruga mpaka sisi wenyewe tupoteze malengo. Tujikute tunaendana na ratiba zake, akiwa ameshatutoa kwenye kalenda ya Mungu.” Wakati Junior amepigwa na baridi kali hata hajajibu, Ezra akawafuata.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Naona hapa tumefanikiwa.” Junior akamwangalia. Emelda kimya. “Ni nini tena!?” Akawa kama ameshamsoma Junior. “Emelda hataki kuondoka nyumbani.” “Sio kwamba sitaki. Natamani sana, ila isiwe kwa kukimbia. Tutamuadhibu mama yenu. Mimi najua ninachozungumzia. Mama anahitaji msaada jamani! Hatuwezi kumuacha hivihivi eti sababu ya Ester! Hapana jamani! Na naomba muwe na amani.” “Hivyo sitaweza.” “Basi naomba umfikirie mama pia. Halafu naomba niwe muwazi kwenu, kwa hakika sioni sababu.” Ezra akamtizama Junior kama aliyemuuliza swali aliloelewa.

Akamjibu. “Japokuwa sijamuonyesha jumbe zenyewe, amerudia mwenyewe neno kwa neno mpaka nimemuomba aache.” “Haiwezekani Emelda!?” Ezra akahamaki kwa hofu kubwa mpaka ikaonekana usoni.

“Aliyoyasikia Junior leo, sio mageni kwangu. Ni kama wimbo tu. Na sina sababu yakumsingizia Ester, mpaka huwa namuhurumia, nasema anakufuru. Ni hivyo baba yake anasema anamuombea sana. Lakini hakuna jipya. Kwa hiyo nashauri tukapumzike, kesho ibadani.” Ezra naye hoi.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akatoka na Jelini. “Naona kikao kimehamia nje!” “Na naona kinaisha. Emelda anataka kurudi nyumbani.” Wakamsimulia kwa kifupi sababu ya kutaka kumtoa hapo kwa mchungaji na yeye kukataa, Jelini naye hoi. Emelda akawacheka taratibu kama alivyo.

“Nyinyi nendeni mkapumzike, kesho siku yenu. Naomba unisaidie usafiri wa kurudi nyumbani.” Hapo akamwangalia Junior. Ikabidi tu wakubaliane naye. Wakaomba pamoja na kuiweka siku ya kesho mikononi mwa Mungu. Wakaombea mipango yao mpaka kusema ‘Amen’. Kidogo Junior akawa ametulia.

Penzi Ambalo Halijachanganywa.

{kama tui la kwanza}

“Sasa kesho ni kama mnatangaza uchumba kwa mara ya kwanza. Ezra atakuvalisha pete kwa upya.” Jelini akachekelea bila kufikiria. “Lakini si unajua inamaana itabidi utupe hiyo pete twende nayo, ili kesho akuvalishe pale kanisani mbele…” Alimshitua Jelini! Kabla hajamaliza akaficha mkono wenye hiyo pete. Kisha akakataa. “Hakika sitaweza kulala Junior. Hapo mtaninyima raha kabisa.” Hawakutegemea, maana na machozi yalishaanza kumtoka.

“Jelini! Anakuvalisha kesho pale kanisani!” Wakaharibu mudi yote ya Jelini. “Siwezi kulala bila hii pete. Hivyo mimi sitaki. Mnanirudisha nyuma, wakati huko nilishatoka.” Akaanza kulia. “Basi Jelini. Basi.” Ezra akambembeleza. “Ila ujue kesho ningekuva…” Akapandisha mabega kabisa kukataa akijisogeza pembeni.

“Mimi najijua. Bahati zangu huwa haziji mara mbili. Utashangaa chochote kinatokea, hii pete haitakaa ikarudi tena hapa kidoleni. Nitarudia yale maisha ya zamani, ya upweke. Nawasihi katika hili mnielewe jamani. Nina hofu ambayo hamuwezi kunielewa.” “Basi Jelini. Basi.” Na Junior naye akamtuliza akikumbuka yake alivuliwa na kuwekewa mezani.

“Tunaweza ichukua tukishafika kanisani, pale mkiwa mnaitwa mbele muombewe na wazee.” Hapo napo ikawa shida. “Mimi nilijua tu jambo lazima litokee jamani! Sijui kwa nini mimi!” Akalia kabisa.

“Jelini, hiyo pete mimi nitahakikisha inarudi kidoleni kwako. Chukulia ni kama unachumbiwa kwa mara ya pili na unapata nafasi ya kujipanga vizuri mbele ya watu wengi! Ni sifa.” “Mimi sitaki sifa. Sitaki kuchumbiwa tena. Nataka ibakie vilevile mara moja. Kwanza mimi sihitaji watu wengine. Mimi watu wangu wote wa muhimu siku ile mlikuwepo. Inatosha. Napenda surprise yangu ya kwanza na ibakie tu vilevile, ila naombeni msinitoe tena pete kidoleni. Haitakaa ikarudi hapa. Mimi najijua.” “Basi haitoki.” Ezra akamsogelea na kumkumbatia kabisa.

“Basi Jelini. Na samahani. Basi tutamwambia mchungaji awaite tu pale mbele. Atangaze uchumba, picha zenu ziwekwe pale mbele kwenye screen ili watu wengine waone mlivyo chumbiana, basi muombewe.” Hilo akakubali.

“Samahani Junior. Najua mna mipango yenu. Lakini hii pete kwangu ni zaidi ya kuchumbiwa. Nilipita kipindi kigumu sana kabla hajaja Ezra. Nikimaanisha Ezra aliponirudia kwa mara ya pili. Ni zaidi ya faraja au tumaini. Ameniongezea kitu ambacho sina jinsi nikawaeleza mkaelewa. Nikiwa popote, hata nikiamka usiku usingizini, nikiiona na kuanza mawazo yanayoninyima raha, nikiiangalia, najua Ezra wangu wa kuaminika yupo sehemu. Ni umbali wa simu tu. Narudi kulala bila shida au nafanya yangu kwa utulivu. Hapa maombi yangu ni Mungu ajalie iongezeke ya pili na si kupungua.” “Nimeelewa Jelini, na samahani sana.” Junior akamuhurumia kwa jinsi alivyoongea kwa hofu. Ujanja wote ulimuisha Jelini cha maneno, Ezra akambusu hapo mbele yao.

“Nakuahidi ya pili inakuja muda si mrefu. Tuvumilie kidogo tu.” Jelini wa mikono, alishajaa hapo mikononi na kujilaza kabisa kifuani, Emelda akapotelea mawazoni kabisa, Junior akamuona. “Acha nimrudishe Emelda akapumzike. Naamini kesho kila kitu kitakuwa sawa.” Wakaagana.

“Jelini!” Emelda akawa kama amekumbuka kitu. “Nashukuru sana kwa mavazi ya kesho.” “Emelda naye! Kila saa unashukuru tu!” Akacheka na kurudia. “Asante. Naenda kufanyia mazoezi viatu.” Jelini akamcheka. “Tutakushika mkono usianguke.” “Mpaka kesho nitakuwa nishaviwezea.” Wakataniana hao wawili ndipo wakaondoka lakini Junior akamshukuru Jelini kwa kumjali Emelda.

Junior&Emelda.

Junior akawa anamrudisha Emelda, wakawaacha hapo hao wachumba wakiagana. “Nikuulize kitu Emelda?” “Ndiyo.” Akamwangalia. “Unaamini kama najutia muda niliopoteza bila wewe?” “Mimi nakuamini Junior. Tafadhali usiishi kwa hukumu.” “Siwezi. Ila nina swali jingine.” Akamwangalia. “Unaamini kama nakupenda kwa dhati?” “Nakuamini Junior! Usingekuwa na mimi sasahivi kama si upendo. Na mimi nikuulize kitu?” “Niulize tu.” Emelda akamgeukia kabisa.

Kisha akamuuliza. “Utaishi na mimi kwa hukumu mpaka lini?” Akanyamaza. “Furaha yangu ni kukuona unafuraha, Junior! Hapo ndio naweza hata kula. Tafadhali naomba mimi na wewe tuanze ukurasa mpya. Ndio nitajisikia kama maombi yangu yamejibiwa kiukweli.” Junior akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha, kimya.

“Usitishwe na Edwin wala Ester. Wewe ndio umewajua kwa undani leo. Lakini mimi nimekuwa nikiishi nao hivyohivyo lakini bado nikabaki nikikupenda wewe.” “Basi Emelda. Ila naomba unielewe na mimi. Leo imekuwa siku ngumu sana kwangu. Sana. Tokea asubuhi mpaka sasa, napata habari mbaya tu zakuniumiza, kasoro wewe kunikubali.” “Basi naomba hiyo itoshe kukufanya ulale na kuamka vizuri kesho.”

“Noah ameniambia unaongoza sifa kesho.” Ikawa kama ndio anamkumbusha. “Daah! Nimesahau kabisa! Alitaka nimtumie nyimbo nitakazoimba, nimekuwa na mambo mengi sijafanya hivyo.” “Basi nitakukumbusha kabla hujalala.” “Nashukuru.” Mara simu ikaingia.

~~~~~~~~~~~~~~~

USIKU WA HEKAHEKA.

INAENDELEA.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment