Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 46. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 46.

 

Akacheka. “Ni ombi dogo tu jamani! Mbona mmetaharuki?!” “Kwa hakika nataka nikapumzike Junior.” “Sawa baba! Nilikuwa naomba dakika 5 tu na Emelda. Halafu Noah atafunga mlango, wewe nenda kapumzike.” “Kama kweli ni dakika tano, mimi nitasubiri.” “Baba bwana! Dakika tano zile za tano kisha unaongeza kama 10.” “Hapana Junior. Mimi najua mambo yanapoanza. Huwa hakunaga kutoshesha.” Walijikuta wakicheka mpaka Emelda akajifunika uso.

“Kwani na sisi si tumetoka hukohuko! Umekua na Emelda siku nzima. Unataka nyumba nzima ikeshe! Wewe kuwa na kiasi, kesho tena mtakutana. Dakika tano ya kiMungu. Haya nendeni nasubiria.” Junior akasimama akitingisha kichwa kwa masikitiko. Wengine wakicheka. “Acha mimi nitangulie. Usiku mwema.” Ezra yeye akaondoka.

Junior akamshika mkono Emelda wakaelekea chumbani kwake. Akaingia na kusimama tu mlangoni. Emelda akaweka vitu vyake vyote kitandani pamoja na alivyonunuliwa na Jelini. “Jelini anaroho nzuri!” “Hayo ya kesho. Sasahivi nataka muda na wewe. Hizi dakika tano, nikushike mpaka akili na moyo utulie. Leo nimekuwa na siku yenye habari zisizo nzuri kasoro wewe tu. Acha nikushike, nitulie ndipo nikalale.” Emelda akajichekesha na kumsogelea.

“Niambie ukweli jinsi unavyojisikia. Jumlisha yote mpaka na ya Ester. Na usinifiche.” “Moyo wangu umejaa amani na furaha Junior. Nimekupata wewe, halafu tunarudi wote nyumbani kwetu! Sirudi tena peke yangu. Umemtoa mama yangu kwenye dhiki! Yote hayo yananipa furaha. Na zaidi nina uhakika wanafikia kwenye mazingira ambayo wanamsubiria kwa hamu si kama mzigo. Asante.”

Akamkumbatia vizuri akiwa amepishanisha mikono nyuma yake. Akawa amemvuta karibu kabisa. Emelda alipotulia, Junior na yeye akaanza kusikia kutulia mpaka akafunga macho kabisa, kichwa akajiegemeza juu ya kichwa chake, wakatulia kimya. Emelda akamsikia akivuta pumzi mfululizo kwa muda.

Akawa mwaminifu. Baada ya dakika nne akamuachia. “Kesho nitakuja kukuchukua twende kanisani pamoja.” Emelda akacheka kwa furaha. “Sasa sio uondoke na Noah. Unisubirie.” Huwa mchungaji na mke wake wanawahi sana kanisani. Nusu saa kama wamechelewa ila lisaa kabla ya ibada ya kwanza kuanza, wanakuwa walishawasili kanisani. Kama Emelda akiwahi basi ataongozana na Noah ambaye huwahi na yeye kufunga vyombo lakini sio lisaa. Mara nyingi hufika dakika 20 kabla ya ibada, ndipo Emelda hujipatia usafiri hapo. Vinginevyo, daladala. Akapata kiss fupi na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akamsikia akimwambia baba yake huku akitoka. “Uaminifu na kiasi pia ni tunda ambalo na mimi sikunyimwa.” “Sasa aliyekwambia umetumia dakika 5 tu ni nani?” “Utakuwa umehsabia kutokea uliposema, na si tokea tumepata faragha na Emelda. Sijazidisha muda. Nashukuru baba yangu na usiku mwema.” Akajichekea mwenyewe chumbani. “Umakini huko barabarani tafadhali.” “Asante baba.” Kimya milango ikaanza kufungwa. Akajua ameshaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mara simu. Junior! Akajawa furaha na kujitupa kitandani kabisa kisha akapokea. Wakaanza kuzungumza kana kwamba hawajatoka kuagana. Cheko limemjaa Emelda kama sio yeye! Ndani ya masaa machache tu ndani ya hiyo siku, historia yake imebadilishwa. Alikuwa na furaha, yakupita maelezo. Hatimaye maombi yake yamejibiwa.

Jumapili.

Ikawa hivi. Emelda alifika na Junior hapo kanisani. “Tafadhali kuwa makini na Edwin.” Emelda akajaribu kufikiria. “Namaanisha sio tena unakuwa muda wa kubembelezana! Unamwambia tu kwamba ulishampa jibu Ester, ila umekuja kugundua hakumfikishia majibu. Usianze kusema juu ya vitu alivyokuwa akikupa. Halafu unamtaarifu. Sio kumuomba ruhusa. Mtaarifu kuwa leo ni ibada ya kuchumbia Ezra, utakuwepo ibadani na familia. Atafute mtu mwingine wa kushika darasa lako.” Emelda akashangaa sana, ila akashindwa chakusema.

“Mbona kama hujaridhika?!” “Watu wengi hawapendi kuhudumu kwa watoto Junior. Kila mtu anakuwa na visingizio kama hiki unachosema! Wakati mwingine tunajikuta tukichanganya madarasa sababu walimu ni wachache. Halafu hata hivyo hiyo sababu itakuwa si ya kweli, kwa sababu mara nyingine tukiwa tuna walimu wachache, huwa tunafanya ibada ya sifa pamoja na kanisa zima, kipindi tu cha neno ndipo tunaondoka na watoto.” Junior akafikiria kwa haraka.

“Basi na leo mfanye hivyohivyo, halafu wakati wa neno na mimi nakuja.” Emelda akazidi kushangaa. “Kuja, unamaanisha na wewe kufundisha watoto!?” “Ndiyo. Au unaona nitakuwa nikiwaingilia?” “Junior! Najua kwa hakika, mchungaji na mama mchungaji, ibada huwa haindelei pale bila ya kukuona wewe na Ezra.” “Nitawaambia na mimi nahamia kwa watoto.” Emelda akaona ugumu utakao kuwepo lakini hajui amwambie nini!

“Mbona kama hutaki?!” “Nataka Junior. Karibu.” Kisha akaanza kucheka. “Acha kunicheka Emelda!” “Unajua wazi mambo hapa kanisani hayaendi bila wewe na Ezra. Hata umeme ukisumbua katikati ya ibada, mchungaji ataita Junior au Ezra. Kipaza sauti kikikwaruza tu, kila mtu anawatafuta nyinyi! Sasa leo mhamie kule kwenye madarasa ya watoto, wewe na Ezra! Maana najua na yeye Ezra ibada haiendi bila kuwa amekaa na wewe. Mtajaa nyinyi wawili kwenye darasa moja.”

“Itakuwa usumbufu usio kifani. Kila mtu atakuwa anakuja kuwaita. Mwishoe na mama naye atakuja mwenyewe. Jelini atafuata. Watoto watabaki wakitushangaa sisi. Itakuwa ni vurugu ibada nzima!” “Nitahakikisha kila kitu kinakaa sawa ndio nakuja.”

“Saa ngapi na wewe unakikao sasahivi, kisha unaongoza ibada nzima ya kusifu na kuabudu?” “Mbona kama hunitaki kwenye huduma yenu!? Inakua kama unanitafutia sababu tu!” “Mimi nakukumbusha majukumu yako hapa kanisani, Junior. Nilishatamani sana kukuona ukihudumu na mimi. Lakini nikagundua nafasi yako hapa kanisani si moja, na unahitajika sana.”

“Ili kila ibada kuisha hapa kwa utulivu, ni lazima wewe na Ezra muwepo. Haya ninayokuuliza, mwenzio nilishayafikiria hata miezi sita kabla ya leo. Nikafikiria labda ufanye hili na lile ndio ungeweza hata kufika kule kwenye madarasa ya watoto, nikaishia kujua kutofika kwako kule si kwa kupenda. Mmebanwa sana. Sasa ukiweza, karibu. Nitafurahi kwa mara ya kwanza na mimi kupata bahati ya kuhudumu na wewe.” Alipoiweka hivyo, akamtuliza. Akapoa kabisa. Ndipo wakaweza kuagana.

Uchumba Si Ndoa.

Hope alipofika tu kanisani, mchungaji akaomba afike ofisini kwake. Ukweli alikuwa amependeza tu. Akakuta wote wakimsubiria. Ezra, Junior, mama mchungaji na mchungaji mwenyewe. Kidogo akaingiwa na hofu, wasijue hofu yake ipo kwengine kabisa. Junior kubadili mawazo. Mchungaji akamtaka akae.

“Mbona mnanitia wasiwasi, kwema!?” “Hakuna tatizo Hope, binti yangu. Tulitaka tu tuwekane sawa.” Akatulia akisikiliza. “Jana ulikuwa na kikao na Junior. Nimesikia upande wake, ninataka kukusikia na wewe juu ya makubaliano yenu. Na kama umeridhia. Una amani na makubaliano yenu au la?” Akaanza Hope.

Makubaliano ambayo Junior mwenyewe alikubali ni kwamba, pale alipoingia mkataba na kunilipia kuishi, hatanifukuza. Ataniacha nikae pale. Ataniachia gari. Tena kwa makubaliano ya kunipa kabisa funguo za gari na kadi yake. Yeye mwenyewe Junior, kwa kukubali kwake yeye mwenyewe. Labda kama anataka kunibadilikia. Lakini alisema yupo tayari hata kusaini kihalali kuwa gari amenipa mimi.” Akawa ameshapaniki tayari.

“Sasa haya mambo ya kurudi kinyumenyume na Ester kunitafuta eti kusema akili ya Junior sio yake, kwangu ni usaliti. Tena usaliti mkubwa sana. Maana wakati yeye Junior anaahidi kunipa lile gari na kuniacha niishi pale, hakuonekana na tatizo lolote la akili.” Wote hoi! Mpaka mchungaji akabaki amepigwa na butwaa. Anachozungumzia Hope sio kabisa walichofikiria angejibu. Wakabaki wote wamemkodolea macho.

Yeye Hope akaendelea. Tena akisikika kabisa na jazba. “Tena yeye mwenyewe Junior. Wala si mimi. Yeye mwenyewe, alisema hana shida ya kufanya kazi na mimi hapa kanisani. Nirudi kwenye uongozi kwa sababu nawezea madaraka yangu. Na akasema atazungumza na wewe mchungaji, pia niwe nalipwa. Kwa maneno yake mwenyewe, alisema na mimi nastahili kulipwa kama wengine. Sasa hayo anayoanzisha Ester akisema kaka yake hana akili vizuri au sio yeye, mimi hapo ndio naona si sawa. Inakua kama kugeukana. Na si sawa. Mimi nimetumika kwa uaminifu sana hapa….” “Hope! Hope!” Mchungaji akamuwahi.

“Tafadhali tulia, binti yangu. Hakuna lililobadilika na ndio maana tupo hapa kuwekana sawa.” “Samahani baba J.” Mpaka mama mchungaji akaishiwa uvumilivu. “Naomba niingilie kidogo.” Akaendelea akimtizama Hope kwa mshangao mkubwa.

“Hope! Hivi unajua kama uchumba wenu umevunjika! Na ndilo hilo mchungaji alikuwa akitaka…” “Najua. Na Junior mbona amenieleza vizuri tu. Na mimi nakubaliana naye na naona yupo sahihi. Sisi tunaweza kutumika pomoja lakini si kwenye maswala ya familia. Yeye anamisimamo yake ya maisha ambayo kwakweli imeshindwa kuendana na yangu na hapo ndipo tulipopishana. Lakini sio eti ni kosa langu ndio ninyimwe haki yangu! Hapo mtakua mnanionea kwakweli na si sawa.”

“Maana kwa mtu yeyote anayefuata haki bila upendeleo, akipima atagundua ni kama tumepunguziana adha ya baadaye. Zaidi kwangu. Ukweli kwangu ingeniwia vigumu hapo baadaye, na ingekuwa kama uonezi. Maana ukifikiria ni kama ningeingia kwenye ndoa mbili kwa wakati mmoja! Hapa kanisani inaonekana nimeolewa na Junior, kumbe kuna Ezra, halafu atakayekuwa mke wa Ezra! Hapo bado watoto watakao kuja kuzaa huyo Ezra na mkewe. Pia eti waje kuwa jukumu letu!” Akashangaa kabisa Hope, mbele ya wakweze na Ezra mwenyewe.

“Mwanzoni niligundua kajiudhaifu kwa Junior. Nikadhani ni mzito kwenye kuamua mambo. Maana mkiwa kwenye mipango ya muhimu kabisa, jibu analotakiwa kutoa hapohapo, anakwambia eti anataka apate muda wa kufikiria. Nikaja kumgundua kumbe ni mpaka akamuulize na Ezra! Yaani hakuna maamuzi ya kama familia! Lazima maamuzi yetu sisi wawili, eti na Ezra naye ayapitishe!”

“Ikaja kuwa eti mpaka na mwanamke wa Ezra hivyohivyo, aje aafiki maamuzi yetu sisi wawili! Ikitokea Ezra hajakubaliana na maamuzi yangu na Junior, eti hapo kuna tatizo! Kufanya chakula cha pamoja nyumbani kwa Junior eti pia, ni mpaka Ezra na mwanamke wake wakubaliane na wazo langu!”

“Halafu eti mimi natakiwa pia kumpenda na kumnyenyekea mpaka mwanamke wa Ezra ambaye kwanza hatuendani. Jelini ni wale wasichana…” “Hapa hatumzungumzii Jelini. Tafadhali, kwa upande wake naomba ishia hapohapo. Zungumza juu yangu utakavyo. Lakini kumtaja Jelini, kwa namna yeyote ile, hapa, ni kuniingilia vibaya sana, na sitakuruhusu.” Ezra akawa mkali kabisa.

“Lakini yeye ndio chanzo cha matatizo yote.” “Hapana Hope. Kwa jinsi nilivyakusikia hapa leo, sidhani kama Jelini aliyekuja hivi karibuni ndio chanzo cha kuvunjika kwa uchumba wenu.” Mama mchungaji akaingilia.

“Sio kwamba namlaumu yeye!” Akajirudi kidogo. “Na pia nilikuwa nikimwambia..” Akasita kumtaja huyo aliyekuwa akimwambia. Ila akaendelea. “Uchumba sio ndoa. Ni kipindi cha kuchunguzana kabla ya ndoa. Junior mwenyewe, kwa kinywa chake, amesema hajaona tatizo kwangu, ila tu mimi si mkewe. Akataja sifa zangu nzuri tu, na ni kweli.” Hope akajikubali.

“Sasa kwa jinsi nilivyo, na yeye alivyo pamoja na Ezra na zaidi mwanamke wake, ukweli hatuendani. Ingekuwa ni shida tu. Hata hivyo na mimi nisingeweza kuwa kwenye ndoa ya watu wanne. Nataka mtu ambaye tunapanga mambo yetu ya kifamilia, tunakubaliana sisi wawili. Basi. Sio kila uamuzi eti lazima upitie kwa rafiki! Sasa hapo kutakuwa na ndoa kweli!” “Ili tusikupotezee muda mwingi Hope, binti yangu, kama nimekuelewa vizuri, ni kwamba mpo kwenye makubaliano ya kusitisha uchumba?” Mchungaji akataka ukiri, wafupishe kikao kilichoonyesha dalili zote za kuvuta sana.

“Makubaliano yalikuwa leo anikabidhi ….” “Usiwe na wasiwasi juu ya mali zake. Hizo..” “Lakini ukiangalia kwa makini si mali zake peke yake, mchungaji.” Hapo akaongea kwa heshima kidogo.

“Gari na mimi nilichangia, hata kama ni kidogo, lakini..,” “Hope! Hope! Ninachotaka kukuhakikishia ni kwamba, yote aliyokuahidi kukupa, utapewa. Kasoro swala la uongozi hapa kanisani, juu ya ile nafasi uliyoachia ndio itabidi nipate muda wa kuitathimini kwa upya na kumuomba Mungu zaidi. Maana kwa sasa ni kama kuna utaratibu unaofanya kazi vizuri tu.” “Kwamba tayari mmeshamtafuta mtu mwingine!?” “Juu ya hilo naomba kukutoa wasiwasi. Hilo niachie mimi.” “Maana alisema pia nikirudi kwenye uongozi kwa sababu natumika sana, tena vizuri, pia nitalipwa.” Ikawa mpaka imekera. Ila mchungaji akajikaza.

“Tutawekana sawa, tutakapofikia hapo. Tafadhali turudi kwenye ajenda ya UCHUMBA. Je, mmeafikiana kusitisha uchumba? Kwamba na wewe umeafikiana na hilo bila manung’uniko?”

“Uchumba sio ndoa mchungaji, kusema ilitakiwa iwe ya milele. Sisi tumechunguzana, ukweli hatuendani. Na ndio maana tumeachana kwa amani kabisa. Na makubaliano yetu yapo palepale. Hatuachani kwa ugomvi eti kufilisiana. Hapana. Au Junior amebadili mawazo? Maana namuona yupo kimya tu muda wote!” “Hapana. Nilitaka kuwapa nafasi na wao wakusikie vizuri na kukuelewa kwa uhalisia wako.” Junior akaongea kama kuwafikishia ujumbe wazazi, yeye Hope asielewe anasemwa yeye.

“Mimi naona hatutafika popote mpaka Junior amkabidhi hilo gari. Haya Junior, mkabidhishe ndipo mchungaji amuulize maswali yake, tutoke hapa. Ibada ikaanze.” Mama mchungaji akaingilia akisikika amefika mwisho kabisa.

Junior akamkabidhi bahasha kubwa. Akapokea. Akakuta kadi ya gari na karatasi zingine. “Mbona hakuna funguo?! Maana funguo ya pil..” “Hope, kila kitu kipo ndani ya hiyo bahasha. Tafadhali angalia kwa makini.” Akamwaga kila kitu hapo mezani kwa mchungaji kama kuhakikishia wote maana alishapaniki tena. Funguo ilipodondoka mezani wakamuona anatabasamu.

“Huyu Ester alitaka kunichanganya bila sababu! Junior ni mtu wa kusimamia maneno yake tokea mwanzo. Akisema atafanya jambo, anafanya. Na ndizo akili zake tokea namfahamu mimi. Hayo mengine ni uzushi tu.” Wote hoi. “Sasa hapa tumehitimisha kwa amani. Hatudaiani chochote. Na pete yako nilishakurudishia. Hunidai Junior.” Junior kimya. Wote wakimtizama. Ni kweli alionekana kutulia kabisa.

“Kwa hiyo leo tutatangaza kusitisha uchumba wenu, ili kama kuna mtu alikuwa akitaka kukuchumbia akazuiliwa na Junior, basi ajue ni wakati wake.” Hope akacheka taratibu. Mchungaji naye akacheka. “Au tayari Hope binti yangu?” Akacheka kwa wazi kabisa. Tena akiwa amebadilika, mwema kama siye yeye!

“Habari njema zinakuja, mchungaji. Na amekubali kuhamia hapahapa kanisani. Nimemwambia Junior hana shida ya kuhudumu na mimi. Maana na yeye ni mtumishi. Acha tujipange, nitamkaribisha.” Mama J, hoi! Akataka kuuliza swali, mumewe akajua swali lake na akajua ameshakasirika.

“Mengine acha tuendelee nayo tu baadaye mama J. Acha tuombe na kutamka baraka juu yao, tuwahi ibadani.” Hakusubiri jibu. Maana hao watatu walibaki wamemkodolea macho kama wanao muuliza ‘umeona sasa?’. Hope alishafunga macho. Bahasha yake kwapani pembeni ya pochi yake. Mchungaji akawatizama vile wanavyomtizama, akafunga macho na kupiga sala fupi. Hope akashukuru na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Naona hili limekaa sawa.” Mchungaji akawaambia maana walibaki wakimtizama. “Naamini hata kwa Emelda huko kila kitu kitakuwa kilienda sawa.” Ndio akawa amemkumbusha Junior. Akasimama kama mchale. “Nahamia kwenye huduma ya watoto.” Wazazi wakapigwa na butwaa. Ezra naye akasimama. “Hiyo ni vurugu unayotaka kuianzisha Junior. Na hapana.” “Kwa nini?!” Akamuuliza Ezra kwa ukali kidogo.

 “Wewe unajua ni kwa nini, Junior. Tafadhali twende jukwaani. Noah ameshatuma ujumbe, anataka tukawekane sawa na waimbaji wengine, tuanze ibada. Huwezi kurudi kinyumenyume sasahivi. Utamchanganya Noah ambaye ni kiongozi wa sifa. Na najua kabisa sio lengo lako.” Wazazi kimywa wakiwasikiliza.

“Tafadhali twende.” “Sasa hata kama ni kwenda kwa watoto si ni baada ya ibada ya kusifu na kuabudu! Sijasema kama nakwenda sasahivi! Kwanza watoto wenyewe watakuwa huku kwenye ibada ya sifa. Wakiwa wanaondoka na mimi…” “Unarudi kwenye majukumu ya hapa kanisani. Wewe unajua ibada hapa haziendi bila sisi. Hata kipaza sauti kikisumbua ni sisi. Sasa unataka kwenda kumlinda Emelda kule huku ibada ikwame?” Akawa ameongea kama Emelda. Hapo akapoa kidogo.

“Twende Junior, tunazidi kumchelewesha Noah.” Ezra akatoka, akamfuata nyuma. “Na lengo si kuwa nakwenda kumlinda Emelda! Nimejihisi nimekuwa kwenye kila huduma, kasoro huko kwa watoto. Nataka kushiriki, na pia kumtia moyo.” Wakawasikia wakiongea wakiondoka. “Lakini sio sasa na sio kwa gafla, Junior! Na wewe unajua.” Wakabaki wakisikiliza mpaka wakapotea. Uzuri wenyewe wanawezana. Angeingilia mchungaji hapo, Ezra angemtetea Junior, siku hiyo kweli wote wangeishia hukudumu kwa watoto. Utabiri wa Emelda ungetimia.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Ndio maana wanawake wanawaacha hawa!” Mama yao akaongea na kucheka kwa pamoja kama wanao wasikitikia. “Ila katika hili, nilazima kumuomba radhi Junior. Huyu binti angemsumbua sana kwenye ndoa.” Mchungaji akazungumza akimfikiria Hope. “Hana habari na mwenzie kabisa, wala hajali swala la uchumba, yeye ni mali tu jamani!” “Lakini mama, acha hivi ilivyoisha kwa amani.” “Halafu na huyo mchumba atakuwa alimpata lini!?” “Nilitaka kujiuliza hilo lakini nikakumbuka na yeye Junior mbona ana Emelda tayari!” Wakajisuta na kunyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~~

Je, kwa upande wa Edwin yeye alichukuliaje taarifa za 'Hapana' akiwa ameshawekeza sana kwa Emelda?

Ester? 

Jelini amechumbiwa kihalali, Colins?

Inaendelea.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment