Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 43. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 43.

Na yeye Vai usiku huo, kabla ya hilo juma kukatika, akawa akifutwa machozi vilivyo. Ukawa usiku wake haswa. Mawifi zake hao wawili wa pande zote, ambao ni marafiki, walimtengenezea tafrija nzuri sana wakisaidiwa na kina Magesa. Na yeye akajitendea haki. Hakuzembea swala la saluni baada ya uchovu kuisha. Hakuhitaji urembo mwingi ili kupendeza. Dada za James ni warembo wa kuzaliwa. Alipendeza Vai, akavutia kumtizama.
    Naye Bale akaeleza historia yao mwanzo mpaka siku hiyo. Tokea siku ya kwanza anamuokota juani, mwenzie akimwambia amuache tu nje ya kitengo cha mifupa, MOI. “Nikiwa na hasira, moyo umejaa uchungu, nikitamani kujiadhibu zaidi. Nipo juani. Nimetupa gongo ambalo lingenisaidia kusimama, naungua pale nilipokalia. Sina uwezo wa kuamka tena. Vai akashindwa kumsikiliza rafiki yake, akanisadia kusimama. Akaniingiza ndani, kwenye chumba fulani hivi. Akanisafisha kidondo na kunifunga.”

“Ilikuwa ni siku ambayo sikutakiwa kuwepo pale na kidonda ili wanijaribishe mguu wa bandia. Kwa hiyo nikajikuta nipo pale kwamba nitasubiria foleni ndefu vile lakini nikijua nitakachokwenda kuambiwa. Siwezi kupewa mguu wa bandia mpaka kile kidonda kipone tena. Vai ananisafisha kidonda ila moyoni nilikuwa nimejawa uchungu wa kupitiliza. Ila akazungumza na mimi kitu kilichonishangaza sana.”

“Ikawa kama anazungumza na mimi na vile mapungufu yangu yalivyo. Ikanifanya nijirudi kabisa. Nikapoa. Akaniacha pale baada ya kunisaidia. Yeye akidhania ni kile kidonda tu, kumbe akawa amezungumza na moyo wangu. Kufupisha habari ndefu, tukapotezana na Vai. Sikumuona tena. Mpaka siku moja.” Wakamuona ametulia kwa muda.

“Hakika ni bora ukosane na wanadamu ila si Mungu. Nilipita mahali nikaona ni bora kuondoka kabisa hapa duniani. Nikiwa nishatundika kamba, najiandaa kujinyonga, Joshua akanipigia simu nikiwa sitarajii simu yake. Kwanza ni usiku, na nilishajua mida ya usiku anakuwa na familia yake, huwa hatuzungumzi mida ile.” Naya alilia sana. Watu wote kimya.

“Ikabidi tu nipokee maana sikujua anataka kuniambia nini! Ila naye ikawa ametumwa na Mungu kama Vai tu. Kuzungumza na mimi. Akaniambia Mungu amemtuma aniambie, ‘hajamalizana na mimi’.” Watu wakazidi kushangaa.

“Yeye aliniambia hajajua ni kwanini ametumwa hivyo na kwa nini wakati huo ambao alikuwa na wageni. Ila alijua hataweza kusubiri tena, lazima apige na aniambie hivyo. Kufupisha hiyo habari, akazungumza na mimi sasa akijua ni mpweke. Akaja kunishauri kuwa lazima kutoka. Nitafute gym nifanye mazoezi mbali na ya hospitalini. Itanisaidia kutoka ndani na kujichanganya na wengine. Nikafuata ushauri wake.”

“Nikiwa nimempoteza Vai, sijui hata nitampatia wapi tena. Kwanza hata sikuwa nikimtafuta. Ni Vai, binti anayejielewa. Mrembo, halafu mimi mlemavu. Mbaya zaidi wakati huo sikuwa hata na kazi! Nalishwa na kutunzwa na shemeji. Sikutaka hata kujisumbua naye. Nilijua sina hata nafasi kwake.

“Sasa wakati natembea na gongo langu, nachechemea, natoka gym nikasikia mtu ananiita nyuma yangu. Kugeuka alikuwa Vai na yeye anatoka maeneo hayohayo ila saluni. Alikuwa amependeza sana.” Watu wakacheka vile alivyoweka msisitizo.

“Mimi mwenyewe nilibabaika kwa sekunde kadhaa. Ndipo nikamkaribisha kwangu nikijua yeye ni mwanafunzi, halafu tukakutana akiwa na njaa. Akawa anakwenda kununua chakula. Na mimi nikawa nimepika mavyakula mengi, sina mtu wakula naye kipindi kile cha sikukuu za krismasi. Nikamkaribisha kwangu ale, kisha nimfungie kingine abebe. Kama shukurani tu. Hapakuwa na wazo jingine, kwa sababu kama nilizotangulia kusema hapo awali, yeye ni Vai mimi bado mlemavu, sina hata mguu bado nachechemea, sina kitu. Hapakuwa na hata wazo mtu kama yeye anaweza hata kunifikiria.”

“Basi, kwa jinsi alivyokuwa amependeza, ikabidi tu nijikaze, nikodi taksii mpaka kwangu. Bwana Vai amejawa shukurani! Ndipo ikawa kama Mungu kazini. Mimi nikiwa na kilema kibaya cha kutoridhika. Macho yangu wakati wote kutizama nisicho nacho, yeye anaona hata maji ni kiburudisha cha ajabu sana. Akikushukuru kwa jambo, mpaka unatulia na wewe na kuanza kufikiria ulichompa. Ukimwambia jambo ambalo huna, yeye anakurudisha kwenye kilichopo hapo.”

“Siku yetu ya kwanza nilimsimulia ukweli wote juu ya historia yangu. Sikujua ni kwa nini. Lakini nilijua kwa hakika angetishwa na kukimbia. Lakini nikashangaa amejawa utulivu mpaka nikajikuta nazungumza mambo ambayo sikupata nafasi kujieleza kwa watu wengine na wao wakaweza kusikia na upande wangu na mimi. Au niseme sikupata mtu ambaye alitaka kusikia upande wangu, ila yeye.”

“Vai akanisikiliza kwa kutulia mpaka ikabidi nimuulize mbona hashituki na kukimbia! Kufupisha habari ndefu, siku ile ndipo kwa mara ya kwanza, baada ya mateso mengi hapa duniani, ndio kama Mungu akajidhihirisha kwangu kwa wazi kabisa kupitia Vai. Akawa rafiki, ndugu na faraja ambayo sikujua kama nastahili.”

~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini nabii hana heshima nyumbani kwao. Vai alishakosea sana nyumbani. Ndoto za wazee wao ilikuwa afike mpaka chuo cha udaktari. Amalize na awe daktari. Akakataa chuo alipomaliza tu kidato cha nne, kitu kilichowaumiza sana wazazi. Wakati Nanaa akisoma wao walikuwa ni wale binti wasioshikika. Mjeuri, haambiliki. Ndugu zake walikuwa hawaamini wakati Bale akieleza mazito na makubwa ya Vai kwenye maisha yake. Wakati wengine wakishangilia na vigelegele, wao walijinyamazia tu wakijua anapambwa. Kwanza ni usiku wake. Kimya wakijiangalizia.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Kuanzia hapo tukajikuta ni kama mchana na usiku lakini tunaohitajiana kwenye mapungufu yetu. Tunafuatana kila mahali kama marafiki tu, mpaka nilipojua kwa hakika, sitakujapata mwanamke mwingine kama Vai. Lakini atanikubali kweli!? Ndio ikawa hofu yangu. Majaribu ya maisha yakaja kumsogeza na yeye karibu yangu, na kujua mimi ndiye mume wake. Lakini tena kwa vile nilivyokuwa nimeharibu kwenye jamii ya wanao nifahamu, ikawa ngumu kuaminiwa na Vai.”

“Tukatulia tukimsubiria Mungu, tupate kibali sasa kwa hao ndugu ambao nilishawaumiza kupita kiasi, huku Joshua akituongoza kwenye kusubiria, tukiwapa watu nafasi, bila kuwazonga ila tukimwamini Mungu, atawagusa na kuridhia kuniamini na Vai.”

“Haikuwa rahisi hata kwa Vai ambaye anazungukwa na vishawishi vingi, halafu ananisubiri bila tumaini. Lakini alikubali kusubiri na mimi. Tukifunga na kuomba mpaka Mungu alipojibu.”

“Huwa namwangalia Vai nakujiambia, wakati Mungu akimuumba yeye, aliweka vitu vilivyopungua kwangu.” Watu wakashangilia.

Akapata nafasi ya kupiga goti tena, wakichukuliwa video vizuri. Akamvalisha pete, Joshua akabaki akiangalia kwa hamu ajue kama ameamua kupata kiss kwa mara ya kwanza au la. Alitulia Joshua akifuatilia kwa makini sana hatua kwa hatua. Mwanzo mpama mwisho anamaliza kumvisha pete.

Lakini akamuona anasimama, akamkumbatia vizuri, kisha kumbusu shavuni, basi. Hata yeye hakuamini! Akapotea pale kabisa mawazoni akitafakari wakati watu wakishangilia. Bale akaamua kusubiri! Alimtia Joshua wivu wa hali ya juu. Akapatwa wivu wa ajabu! Akajisikia kupitwa mbali sana na Bale. Kwamba Bale ameweza kusubiri, yeye alishindwa! Akabaki kimya kabisa akiangalia watu wakiwapongeza. Kula na kunywa, kisha kikao cha kwanza kikaanza.

Joshua akashindwa kujizuia, wakati wakitoa pledges yeye akasema mbali na mchango, lakini pia atalipia fungate yao. Popote watakapochagua na kwa siku zozote watakazotaka. Mpaka Naya akamtizama kwa mshangao. “Hiyo ni zawadi yangu kwa Bale.” Hakuna aliyeelewa, ila Bale alihisi. Jinsi alivyomshukuru Joshua, Joshua akajua amejua ni kwa nini amefanya hivyo. Ikamuongezea hali ya kusubiri mpaka hiyo siku ya fungate yao.

Pale Majibu Ya Maombi Yanapochanganywa Na Ugumu Mwingi Wakuumiza Na Kushawishi Kutoshikilia Muujiza Wako.

Wakiwa wamegawana kama mwanzo. Kila mmoja kwenye ukumbi walipofunga viti, usiku huo na yeye Junior akiwa na kijana mwingine wakichangamka ili kutoa hivyo vitu vya Jelini kwa haraka ila kwa usalama, akasikia simu ikicheza kwenye mfuko wa nyuma. Akajua ni ujumbe umeingia. Akidhania ni simu yake. Akaona isubiri mpaka amalize. Ikanguruma tena. Baada ya muda, ikanguruma tena. Kisha tena. Kwamba zimekua jumbe nne. Ikabidi atoe. Akagundua si simu yake, aliondoka na simu ya Emelda.

Akafungua kuona. Zilikuwa jumbe za maneno tatu na sauti moja kutoka kwa Ester. Ile ya sauti ilionekana kubwa. Akaunganisha na bluetooth yake. Kwa kuwa alikuwa na kazi, akaendelea kusikiliza huku akifanya kazi na huyo kijana. Ulikuwa ujumbe mzito. Ester amemrikodia Emelda na kumtumia. Yalikuwa maneno makali. Kama ingekuwa anaambiwa, asingeamini kama dada yake anaweza kumwambia hivyo Emelda.

Alimkumbusha Emelda tokea siku ya kwanza anafika kwao. Jinsi alivyokuwa duni. Akitumia vitambaa vilivyochakaa kipindi cha hedhi yake. Vile alivyokuwa akinuka harufu mbaya. Alimsema mengi mpaka Junior mwenyewe akasimamisha kwanza. Ilikuwa ngumu kusikiliza moja kwa moja. Akaendelea kufanya kazi. Hata aliyekuwa naye alijua amebadilika.

Alikuwa akitetemeka kwa wazi kabisa na jasho kumtoka. Wakamliza na kupandisha vitu vyote kwenye gari. Akamwacha huyo kijana wa Jelini aondoke, akaingia kwenye gari yake. Akajitumia ule ujumbe wa maneno bila kumalizia. Akafungua jumbe za maneno na kujitumia pia. Kisha akaondoa gari kurudi alipomuacha Emelda na Jelini kwani hapo ndipo walipokubaliana kukutana.

Njiani akaona amalizie tu ule ujumbe wa sauti. Alisikiliza mpaka akajikuta machozi yakimtoka huku akiendesha. Ezra akapiga. “Sisi huku tumeshamaliza. Nimemruhusu Teri arudishe vitu, naelekea walipokuwepo kina Jelini au unahitaji msaada nikufuate?” “Na sisi tulishamaliza muda tu. Nimetingwa tu ndio maana nimeshindwa kukutaarifu. Ila nipo njiani kuelekea walipo kina Emelda.” Jinsi alivyozungumza akajua si kwema.

“Vipi, kuna nini?” Alijua hawezi kujificha kwa Ezra. “Daah! Natamani haya ninayoyasikiliza yangekuwa hayatoki kwa Ester, aisee. Nimeshindwa hata kukutumia! Aisee nimeshindwa.” “Umekutumia wewe?” “Hapana. Emelda. Sikujua kama niliondoka na simu yake. Sasa wakati nipo ukumbini ndio jumbe zikaanza kuingia. Nikataka kupuuza mpaka nikimaliza lakini kadiri zilipokuwa zikiingia, nikahisi ni muhimu. Kutoa, kumbe ni simu ya Emelda, jumbe zinatoka kwa Ester. Ni chafu sana. Ni za kumdhalilisha kupita nitakavyokwambia, sitaweza kukutumia Ezra. Ni picha mbaya, ingekuwa Emelda hatakuwa mke wangu, ningekutumia.” “Aisee pole sana Junior. Pole sana kaka.” Junior akabaki akijifuta machozi.

Ezra akajua ameumia sana. “Utafanyaje?” “Cha kwanza nitahakikisha Emelda mwenyewe hataona wala kusikia hizi jumbe.” “Ila atajua kama umefuta jumbe zake.” “Nitamwambia nimezifuta. Lakini Ezra, inatosha. Emelda hatarudi kuishi pale. Itakuwa ni kama namtelekeza mahali ninapojua atateseka tu.”

“Ester amemuhakikishia kumlipiza kisasi. Na kumwambia kama anadhania ndio ameondoka pale nyumbani sasahivi atatawala yeye, asahau. Yeye ni mtoto wa baba, na hata leo ametuhakikishia kwamba yeye bado ni mmoja wa familia. Anao uhuru wa kuingia na kutoka pale nyumbani muda na wakati wowote. Amempa usiku wa leo tu, kesho awe ameachana na mimi. Lasivyo atahakikisha maisha yake ni machungu.” “Haiwezekani Junior!” Ezra hakuamini.

“Nakwambia ninapotamani haya yangekuwa yamesemwa na mtu mwingine na si Ester dada yangu, niamini aisee. Nakutumia vitisho vyake maana amevituma kwa maneno. Matusi ya nguoni ndio yapo kwa ujumbe. Na ameapa kumtangaza Emelda pale kanisani kila mtu amjue hila, ufitini na uchawi anaotumia hata kwa wanaume maana anahisi hata Edwin si akili zake, amemfanyia mambo ya kishirikina. Ili amtunze yeye huku pesa zake akitumia kwa mambo ya kiushirikina akiloga wanaume wengine.” Ezra mwenyewe akaanza kutetemeka.

“Mungu wangu! Hiyo itakuwa mbaya sana Junior!” “Itabidi sasa kuingilia kati. Kujulisha wazazi kabla hajachafua kanisa.” “Kama bado hatujachelewa!” “Na huo ndio wasiwasi wangu. Maana ukimsikiliza, ni kama aliyepagawa! Si Ester ninayemfahamu aisee! Amejawa na uchungu! Hasira kali! Sasa katika hili huwezi jua umbali gani atakwenda. Tafadhali nisaidie kufikiria ni wapi pakumpeleka Emelda usiku huu. Lakini hatarudi nyumbani na wala si kwa kina Jelini. Inatosha kumangamanga kwenye majumba ya watu. Acha apumzike.” Ezra akafikiria kwa haraka.

“Upo wapi?” Akamwambia. “Sasa nina wazo. Tumtafutie full funish apartment. Itakayomtosha yeye na mama yake, pamoja na mdogo wake wakati tukitafuta sehemu ya kuwaweka mpaka ndoa.” Hilo likakaa sawa. Wakapanga pakuanza kutafuta hizo apartment usiku huo.

“Basi wewe wapigie simu kina Jelini, waambie wakimaliza watusubirie, tutawaambia sehemu ya kutufuata, wakati mimi nazungumza na mama kumtaarifu juu ya Emelda.” “Akikusihi Emelda arudi?” “Anarudi kwenye mazingira gani, Ezra? Hapana. Ninachojua atataka kujua sababu. Itabidi niwaambie na kuwaonyesha jumbe zote. Itakuwa kesi ambayo baba atamtetea Ester. Ester atarudi kwake na kumuacha Emelda kwenye ile nyumba ambayo baba yupo. Unafikiri kutakuwa na amani tena?” Ezra akavuta pumzi kwa nguvu akifikiria huku akigeuza gari kuelekea walipokubaliana na Junior, kutafuta malazi ya Emelda.

“Hamna jinsi. Lazima tuzungumze na Ester usiku huu. Ili kuzuia hii sumu.” Junior naye alikuwa akitafuta sehemu ya kugeuza ili kuelekea huko walipokubaliana. Wakakubaliana kuwa ni jipu lazima kulitumbua tu. Wakaagana, kila mmoja akipiga simu kama walivyokubaliana. Ezra kwa Jelini, Junior kwa mama.

Kwa wazazi.

“Samahani mama. Najua mnajiandaa kulala. Lakini nilitaka kukutaarifu kuwa Emelda hatarudi tena hapo nyumbani. Namtafutia sehemu ya kuishi. Na nashukuru kwa moyo wa kutaka kusaidia ndugu zake, lakini wataishi na Emelda huko atakapokuwepo. Nitakusaidia kutafuta msichana wa kazi kuziba pengo lake. Lakini naomba kwa sasa uhesabu ni kama yupo likizo. Mama Leti aendelee kuja tu.” Huyo mama alishituka, usingizi wote ukapaa. Akajua historia inataka kujirudia na kwake. “Naomba usikate simu. Tafadhali Junior.” Mama yake akamsihi.

“Nipo mama.” “Kwa nini umeamua hivyo?” “Nakutumia sababu 5, ambazo naomba usikilize kwa makini na kusoma kwa kutulia. Ukiwa umejitoa kwenye nafasi ya mama yetu, ila kama mama mchungaji wa mtu kama Emelda ambaye umeishi naye hapo. Halafu uniambie kama ungekuwa wewe, ungefanyaje? Na nakuomba hakikisha hazimfikii Emelda japo nimetoa kwenye simu yake.” “Kwamba hajui?!”

 “Nafikiri ni Mungu tu mama yangu. Nilijikuta nimeondoka na simu ya Emelda. Ndio zikaingia nikiwa nayo. Yeye hajui hizi zilizoingia usiku huu. Na nimekusudia ibakie hivyo. Tafadhali.” “Sawa. Ila nitakapokupigia tena simu, tafadhali pokea Junior mwanangu. Usiniache hivi usiku wa leo.” “Siwezi mama.” Akakata na kazi ya kumtumia jumbe zote alizotuma Ester kwa Emelda ikaanza.

Alipomaliza tu, simu ikaingia kutoka Ester. Junior akapokea bila ya kusema kitu. Ester akaanza kwa matusi, kaka yake akimsikiliza. Alipoweka kituo tu, Junior akamjibu. “Kwa bahati nzuri nimejikuta nipo na simu ya Emelda. Kwa hiyo…” Kabla hajamalizia simu ikakatwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Maji Yanazidi Kutibuka.

Ni Nini Kitaendelea?

Usipitwe

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment