Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 42. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 42.

“Aliwezaje kusoma yote hayo na kutulia hivyo!” Junior akajiuliza nafsini mwake na kumwangalia asijue hali anayopitia huyo Emelda. Hofu ya kitumbua kuingia mchanga. Lakini akazungumza kitu kilichomshangaza. Ikawa tofauti kabisa na matarajio yake, mpaka akamtuliza moyo. “Uliponiambia Ester ana maneno machungu, hukuniambia ni kwa kiasi hiki!” Emelda akacheka taratibu na kunyamaza. Junior alikuwa na hali mbaya! Ulikuwa ujumbe mmoja ila mrefu wakuumiza. Akajitumia na yeye huo ujumbe.

Emelda akaona ujumbe unaingia kwenye simu ya Junior. Kuangalia ulikuwa ule ujumbe. Akamtizama Junior. “Unataka kufanya nini Junior!? Sitaki haya mambo yazidi kwenda mbali.” “Kwa hakika kwa sasa hata mimi sijui Emelda. Ila nilihitaji kuwa na huo ujumbe na mimi kwenye simu yangu.” Akaomba simu yake. Akamtumia na Ezra. Ila kutoka kwenye simu yake mwenyewe si ya Emelda.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kutoka kwenye ujumbe mzito hivyo, hakuwa amesahau ujumbe wa kwanza. Yeye shida yake ni Edwin. Alishajua ujumbe uliokuwa umeingia kabla ya wa Ester utakuwa ni kutoka kwake tu. Na akawa amepatia.

Akafungua. ‘Naamini upo mzima Emelda. Kabla ya kumuomba mchungaji kupata muda wa mazungumzo na wewe, nimeona nianzie kwako wewe mwenyewe kwanza. Naomba kesho baada ya ibada, tutoke twende mahali tukazungumze. Kuna jambo nililitunza kwa muda mrefu moyoni, nikimuomba Mungu anipe wakati muafaka wa kuzungumza na wewe. Naona sasahivi ndio limepata kibali machoni kwa Bwana. Naamini tutapata wakati mzuri. Kama ni sawa kwako, tafadhali nijulishe ili nizungumze na mchungaji.’ Tayari wakawa wameshamvuruga Junior.

“Yaani wakati kwangu ndio panavurugika eti huyu naye ndio anasema amepata kibali kutoka kwa Bwana! Wanataka kunizidi mahesabu, hakuna bwana yeyote hapa. Ester ndiye aliyemwambia huu ndio wakati wa kumtongoza Emelda.” Akabaki akiwaza. Akajitumia na huo ujumbe na kumtizama Emelda. Ametulia kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Kwa hiyo unaamua nini juu ya Edwin?” “Hata sijui!” Kwa hakika hilo halikuwa jibu sahihi kabisa. “Emelda! Kwamba hujui chakufanya na Edwin!?” “Tafadhali nishauri Junior. Sijui cha kufanya.” “Katika lipi? Maana ni kama uliniambia umenichagua mimi!” “Na ndivyo ilivyo!” “Sasa mbona tena hujui chakufanya?!” “Namjua ninayemtaka. Ila sijui jinsi ya kufanya maana wewe hutaki nizungumze na Edwin. Sijui atajuaje msimamo wangu kama hatanisikia mimi mwenyewe! Maana kama ulivyosema, hatujui Ester alipokuwa akipokea vitu kutoka kwake alikuwa akimwambia nini!” Akatulia akifikiria. Ila na huo ujumbe pia akamtumia na Ezra.

~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda Ezra na Jelini wakarudi hapo, Jelini akiwa ametulia furaha, zote kama aliyetoka kubembelezwa na huyo Ezra. Wakakaa ila moja kwa moja akawasoma usoni akajua hawapo sawa. “Naomba mnisikilize Junior na Emelda.” Wote wakamwangalia. “Kwanza Emelda pole sana. Hukustahili maneno kama haya. Na mimi bila hata kufikiria mara mbili siamini chochote ulichotuhumiwa hapa.” “Unajuaje kaka yangu?” Akauliza Emelda kwa upole.

“Kwanza mimi si kaka yako tena. Labda uwe unamkataa Junior.” Wakacheka. “Mimi natamani kubaki naye. Na ndiyo yalikuwa maombi yangu.” “Basi turudi kwenye swali lako kwamba mimi nimejuaje! Kila chakula ulichokuwa ukipika na kukiacha kwa Junior, jua na mimi nimekuwa nikila naye mpaka chai na juisi.” “Lakini kweli.” Junior akaafiki.

“Hakuna ulichopika kwa Junior, mimi sijala. Kwa sababu kwanza kila mlo uliokuwa ukileta kwa Junior ulikuwa ukitupunguzia shuguli ya kupika au kununua chakula. Mpaka juisi tulikuwa tukigawana na chai vilevile. Sasa kama kweli kulikuwa na uchawi, mbona na mimi sinitake kukuoa.” Bwana Jelini alicheka, kama mazuri.

“Si umeona? Ni jambo la kufikiria kwa haraka tu. Wote sisi sasahivi tungekuwa tukikung’ang’ania, kama kungekuwa kuna uchawi kwenye chakula chako. Halafu kingine, kweli huyu Mungu tunayemtumikia kweli aweze kutuponya na mabaya yote kasoro uchawi wako tu!? Yaani uchawi uwe na nguvu dhidi ya nguvu za Mungu, kweli!? Au ndio kusema hata huyu Ester anatuona na sisi hatuna Mungu! Kwani bibilia inasemaje?” “Hata mkila vitu vya kufisha, havita wadhuru.” Akajibu Junior kwa haraka.

“Sawasawa. ‘Aliye ndani yetu ni mkuu kuliko wa dunia hii’. Halafu, ‘hakuna silaha itakayonyanyuka juu yetu ikafanikiwa’. Hizo zetu ni ahadi zetu sisi wana wa Mungu. Inawezekanaje zishindwe kutimia kwetu sisi tu, mimi na Junior halafu, zikatimie kwa wengine?” “Si kweli.” Akajibu Junior.

“Haya yote nakutaka wewe Emelda uyafikirie na ndipo ujue, shetani NI KAMA, na wala SI. ‘Ni kama’ simba AUNGURUMAYE. Ni kelele tu. Hana meno ya kula. Anapiga kelele tu, kukutisha uone kuna jambo zito linaendelea. Ufikiri nyumbani wote ndivyo watakavyoanza kukuona na mengine mengi, kukutisha tu. Lakini sio kweli.”

Ezra akaendelea. “Leo sisi tulikwenda ofisini kwa wazazi kuomba malazi ya mama yako na Mateo. Hatukwenda kugombana! Na japokuwa habari yako ilishajulikana kabla ya leo, tuliwakuta wazazi wapo sawa wakiweka mipango yao kwa amani kabisa. Sisi tulitaka Ester apigiwe ili aseme ukweli mbele ya mchungaji juu ya msimamo wako tokea mwanzo juu yako na Edwin. Basi. Hapakuwa na jambo la tofauti. Kilichoendelea baada ya pale ni juu ya Ester, wewe hauusiki. Umenielewa Emelda?” Emelda akatulia kwa muda.

Wote kimya wakimwangalia. Mwishoe akaongea kama anayefikiria. “Hata sijui chakufanya! Nisingependa mama aje kwenye mazingira kama haya!” “Tafadhali niamini nikikwambia kuwa, hii ni kelele tu ya simba. Wala wazazi hawakuchukulii hivi. Simba anataka kukutisha tu. Ni mama mwenyewe ndiye ameomba mama yako afikie pale. Tafadhali usikubali kutishwa na kelele za simba. Hilo ni moja.”

“La pili, Junior na Emelda, kuna vita zingine tunashinda kwa kutojibu mashambulizi kabisa. Kunyamaza kimya. Maana wakati mwingine, unapojibu mashambulizi unakuwa unampa adui mambo mawili. Anagundua kule ulikojificha, maana ataona kule mshale au risasi ilipotokea. Kwa hiyo atajua eneo ulipo na kuweza kufanya mashambulizi kwa urahisi. Na ndipo atajua hata aina ya silaha unayotumia. Inamsadiaa kujipanga na kutumia silaha yenye nguvu zaidi.”

“Lakini mtakapotulia mlipo sasahivi. Ila mkiwa mmenia mamoja, mnammaliza kwa urahisi sana. Hatajua mlipo wala mnachofikiria. Hatajua mnatumia silaha gani. Atabaki akipiga kelele mpaka anajikuta anachoka na kunyamaza. Nyamazeni kimya.” Hapo hata Emelda akajisikia kutulia.

“Japokuwa Ezra amenisimulia kwa kifupi tu. Lakini poleni.” Akaongea Jelini na kuendelea. “Mimi hapo alipo Emelda nilipita. Nilimsimulia Ezra. Kumbe haya mambo hayana kanisani wala mtaani! Shetani ni mvurugaji popote anapopata nafasi. Lakini uzuri wako wewe Emelda, umezungukwa na watu wawili wa muhimu sana. Junior mwenyewe anaonekana anakupenda kwa dhati na ana msimamo. Halafu unaye Ezra ambaye tayari ni mtetezi wako anayejua ukweli. Mimi ningekuwa wewe, nisingeogopa wala kukimbia. Ningesimama kama alivyosema Ezra. Amekushauri vizuri sana.”

“Na ujue wazi kabisa, hata ukikimbia sio kwamba huko utakapokimbilia utakuta shwari! Unaweza ukaona hapa maji marefu, ukakimbilia kwa Edwin ndio ukakutana na familia yake wote hawakupendi! Unaishia kupendwa na Ester tu ambaye wala si ndugu wa Edwin na Edwin mwenyewe.” Yaani gafla chati ya Emelda ikapandishwa.

“Mimi nataka kubaki na Junior. Wala si jambo nalifikiria. Nilishaamua. Ila sema niliingiwa hofu nikidhani aliyosema Ester, hawa wawili wanaweza kuyaamini. Zaidi kuwawekea vitu vibaya kwenye chakula. Mungu wangu ni shahidi sisi kwetu hatujui uchawi.” “Wala huhitaji kuapa au kujitetea. Hata kama ungekuwa na uchawi, kwa asilimia 100, nakuhakikishia usingenipata. Mimi namjua Mungu ninayemtumikia. Sihitaji ulinzi wa mafuta wala chumwi au maji ya baraka, kulindwa na huyu Yesu. Kazi iliyofanyika msalabani ni kweli na amina. Maisha yangu yamefichwa ndani ya Kristo Yesu. Wala uchawi haunitishi mimi. Kwanza tusipoteze muda hapo. Turudi kwenye swala la msingi.”

“Jelini na Ezra tunawashukuru kwa kusimama na sisi. Najua tutaomba kabla ya kutoka hapa. Lakini nafikiri swala la kutulia, mimi naafikiana na Ezra. Usimjibu kitu Ester, na najua anajua huu ujumbe naweza nisione kwa vile anavyokujua umsiri au mtulivu hutaki ugomvi. Na mimi sitamtafuta kwa hili wala chochote kati yetu. Tunyamaze tu tukijipanga na yetu.”

“Niwaulize swali?” Jelini akaingilia. “Karibu.” “Kwani wewe Junior ulipanga kuoa lini?” Akashangaa Ezra na Junior wanaangaliana. Kisha kucheka. “Nini? Au pia kuoa mnataka muoe siku moja?” Jelini akauliza kwa utani asijue ndio maombi yao hao.

Alipowatizama akapata jibu. “Jamani nyie haiwezekani! Kwamba mnataka muoe siku moja pia!?” “Kama mtakubali lakini. Katika hili hatutakuwa wabinafsi tukijua ni siku yenu na nyinyi. Ila sisi tuliomba tusimamiane harusi zetu na iwe siku moja, mchungaji mmoja. Baba. Tunaenda honeymoon pamoja.” Hao warembo wawili wakabaki wamewakodolea macho. Junior na mwenzie mbavu zao! Cheko.

“Mjue nyinyi mnashangaza sana!” “Tunajua.” Wote wakajibu kwa pamoja. Emelda akacheka. “Tuanze na Jelini, wewe una ndoto za harusi gani?” Ezra akamuuliza. “Mimi nataka kuolewa na wewe. Basi.” Wakaangaliana tena. Kisha wakaona wamuweke sawa, labda hajaelewa. “Labda niulize zaidi maana sisi tuna wasiwasi na wewe, Jelini. Kwamba wewe hutaona unapokonywa siku yako tukiwa sisi wote wanne na si nyinyi tu wawili? Kwamba watu wote wawaangalie tu nyinyi siku nzima sio tena iwe na sisi pia? Mimi na Emelda?!” Jelini akatulia akifikiria.

“Pana ukweli. Lakini niwaambie, tunaweza fanya ikawa kitu cha kupendeza sana, tukaweka historia nzuri.” Hao wawili walifurahi mpaka kushangilia. “Sasa wewe umepita. Emelda je?” “Ila mimi siamini! Pengine ndio maana mnafanikiwa sana! Kwamba kweli haya yote yanayoendelea kati yangu na Junior kweli hamjali tena?!” “Yapi!?” Wote wakauliza kwa pamoja na Ezra kuendelea.

“Ester anaendelea na ndoa yake. Edwin si atakayekuwa mumeo. Sisi ndio tumeshika hatima yetu. Hatuna mwanya wa kuyumba. Umenielewa Emelda?” “Ndiyo.” “Ukiyumba tu sasahivi, ujue umetukwamisha sisi wote watatu. Kuanzia sasahivi sisi tunasimama kama tulivyo, dhidi ya kila silaha au ulimwengu. Huna utakapopita sisi tusisimame na wewe. Usiogope. Na kama umetishwa na hili, basi simamia miguu yetu, sisi tutakubeba. Tulia na usijibu kitu.” “Ila kesho nitakuwa nikihudumu na Edwin. Nitamjibu nini?” Wote wakamwangalia Junior. Akabaki kimya.

“Kwani nyinyi mlipanga uchumba wenu mtangaze lini?” Ikabidi Jelini aulize. Simu ya Emelda ikaanza kuita. Alikuwa Mika. “Mama atakua ameamka. Acha nisogee pembeni nizungumze naye.” “Sawa.” Junior akajibu. Alipoondoka tu, Junior akajibu. “Baada ya uchumba wenu nyinyi ndio nilitaka kumvalisha pete.” Akajibu Junior macho kwa Emelda aliyekuwa akizungumza huku akiondoka hapo.

“Kungekuwa na pete, eti mimi ningeshauri msivute zaidi ya hapa. Sababu kwa jinsi nilivyosoma ujumbe wa Ester, huwezi jua amezungumza nini tena na Hope na kumfanya arudi kinyumenyume, akaanza kulalamika na kutibua hali ya hewa pale kanisani. Pili tungekuwa tukimjibu Edwin na kumnyima sababu ya kukaa tena na Emelda.” Wakaangaliana.

“Kwamba wewe usingejali na kesho pia siku yetu ya kutangazwa uchumba na wao watangaziwe?!” “Hata kidogo! Nyinyi hamfikiri kama ndio itapendeza zaidi? Tunaanza safari yetu pamoja!” Walifurahi hao wawili wakashindwa kuamini utayari wa Jelini waliyekuwa na wasiwasi naye sana.

“Kwa hakika nimefurahia  utayari wako Jelini. Lakini naomba nimfanyie Emelda na yeye surprise. Amenisubiri kwa shida sana, tena nikimpuuza. Naombeni katika hili nimtendee haki. Edwin asiniharakishe nikamnyima kitu kizuri. Tuache kesho iwe siku yenu. Mama anaandaa tafrija nzuri sana kwa ajili yenu nyinyi wawili. Acha kesho iwe kwa ajili yenu tu. Mimi nikamchukue mama yake. Nizungumze na Mika, ambaye ni kama anayeongoza mambo ya kwao na mama yao, ndipo nimchumbie. Au mnasemaje? Tusiwe tunamuharakisha kwenye hili.”

“Halafu pia, acha watu wajue kama uchumba wangu na Hope umeisha, kabla sijaanzisha jingine. Lasivyo hichi anachozungumza Ester usije geuka mtazamo wa kila mtu. Wakamchukia Emelda wakati maamuzi ni yangu mwenyewe.” “Sio wazo baya.” Akaafiki Ezra.

“Na kesho akikutana na Edwin?” Jelini akauliza tena. “Hakika hatatoka na Emelda. Hapo hapana. Tafadhali fikiria njia ingine Ezra. Lakini sitaki Emelda ampe masikio yake. Nataka abakie kunisikia mimi tu.” “Hata hivyo kesho kuna shuguli nyumbani. Hawawezi kutoka kwenda kokote. Baada ya ibada watu walioalikwa watakaribishwa nyumbani. Hawawezi kutoka.” Hapo akamtuliza Junior ila ukabaki wivu.

Hawa wawili wanatumika kanisani pamoja. Upande wa madarasa ya watoto. Inamaana hata kama hawatatoka, lakini watakuwa pamoja kabla, wakati na baada ya ibada, tena peke yao, huko kwenye madarasa ya watoto! Akabaki akiwaza Junior ambaye hajawahi kujihusisha hata mara moja na huduma ya watoto.

~~~~~~~~~~~~~~~

Emelda akarudi. “Mama anataka kukusalimia na kukushukuru.” Junior akapokea simu kwa heshima huyo, mpaka akamshangaza Emelda. Junior kama apige goti! “Shikamoo mama.” Akasikia sauti kama ya Emelda ila ya kiutuuzima kidogo ikiitika upande wa pili. “Nilikuwa kwenye shida. Nashukuru kunitoa.” Junior akaumia.

 “Karibu mama na poleni sana.” “Asante. Ila mguu umetulia kidogo, msiwe na wasiwasi. Msisumbuke. Usije acha kazi kwa ajili hii. Mimi nitapona tu.” “Hiyo nafuu unayosikia ni ya muda sababu ya dawa za kupunguza maumivu. Lazima kutafuta suluhu ya kudumu. Na hutusumbui kabisa. Hata hivyo na sisi tulitaka kuja kukuona.” “Kama ni hivyo sawa. Karibuni sana.” “Asante. Tunashukuru.” Kimya.

Huyo mama kumbe akawa ameshamaliza. Akamtizama Emelda. Akamcheka. “Ujue hapo ameshamaliza. Tena ameongea sana. Acha tu nimuage.” “Basi muwe na usiku mwema huko.” Akashangaa anaitika kwamba alikuwepo ila kweli hana tena cha kuzungumza. Ikabidi tu arudishe simu kwa Emelda. Akaondoka pale.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Mbona nimesikia safari mimi sijui!” Akalalamika Jelini. Ezra na Junior wakaangaliana. “Mimi nimetengwa!” Akalalamika kwa unyonge. “Hapana mpenzi wangu. Kwanza nikuombe msamaha na nikwambie jinsi ilivyo. Maana haya yametokea mimi mwenyewe nikiwa ukumbini leo tukifunga lile kochi.” Wakamsimulia mwanzo mpaka mwisho. “Kama kungekuwa na uwezo na mimi ningeenda. Nataka kwenda na wewe Ezra.” Alivyoongea mpaka Ezra akajikuta anampa kiss ya juu ya mdomo.

Kisha akamuuliza. “Ukizungumzia uwezo unamaanisha nini?” “Usafiri. Maaana kama mtakuwa nyinyi watatu, na wao wawili si gari imejaa!” “Safari ndefu kama hiyo huwa tunatumia gari kubwa ambayo inauwezo wa kubeba watu 8 na mizigo. Zikiwa za milimani inatulazimu kutumia Range ile yenye gia nzito. Hizi za karibu tukiwa tu sisi ndio tunatumia gari ya kawaida.” “Kwamba inabidi mkodi kwa safari?!” Ndio akakumbuka Jelini bado hajawafahamu vizuri.

Ikabidi amueleze. “Katikati ya nyumba yangu na Junior ndipo tunaegesha magari yote.” Jelini akapatwa na ububu wa gafla. Akameza mate. “Kwa hiyo kama shida ni usafiri, hilo usitie shaka.” Junior akamalizia. “Ila swala la kazi Jelini?” Akamrudisha kwenye kushangazwa na hao vijana wawili. Walionekana wa kawaida mno. Siku nzima wakifunga viti vyake huko ukumbini. Wamesoma na shahada mbilimbili, kisha wanaajira ya kueleweka. Tena ajira ya muda mrefu! Ila wakafanikiwa kujishusha, mali zao zikawa ni msaada tu kuwafanya waishi na watu kwa ukarimu! Akazidi kuvutiwa nao.

Akarudisha akili hapo. “Siku zangu ninazohitajika sana ni kama leo. Mengineyo hata mama anaweza nifanyia. Ningependa kwenda na mimi.” “Basi acha tukaangalie jumatatu kazini. Tukiweza tutoke na kurudi kabla ya jumamosi.” “Hata hivyo hatutakaa. Tunakwenda kuwachukua na kugeuza. Tutakuwa tukipokezana kuendesha.” “Kama ndio hivyo naenda kuzungumza na mama. Akionyesha hamna shida, na mimi nitaongozana na nyinyi.” Mipango ikazidi kukaa sawa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Juma hilo moja tu likajawa na mengi mno. Kuna waliopata na kukosa. Kuna walio dhania ni vyao, wakijua ni majibu ya maombi yao, wakatunza kwasiri, kumbe sivyo! Kuna waliojibiwa maombi yao waliyosubiri kwa muda mrefu, wakajua wamejibiwa. Kuna ambao walishajibiwa ila kushindwa kutunza muujiza wao. Kuna waliojibiwa wasijue kama walishajibiwa, wakabaki kusubiria. Kuna waliojibiwa, wakapokea na kushindwa kutuliza macho kwenye miujiza yao wakaweka macho yao kwengine. Halafu kuna waliojua wamejibiwa, wakapokea, na kutunza waking’ang’ania.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment