“Ndiyo.” Mzee akaweka
msisitizo alipoona wameshangaa. “Yupo kwenye maombi na ameshirikisha
wazee wawili na mimi pia. Wakati wewe upo na Hope, mwenzio alikuwa akimwamini Mungu
kwa ajili ya Emelda. Leo unataka kumtoa Emelda kwenye njia sahihi, kisha na
yeye ukamuache?” Mzee akauliza kwa ukali kidogo.
Edwin anamfahamu Emelda kwa kufanya naye kazi kwa karibu sana. Wakati wewe ukiwa na Hope, Edwin alikuwa akitumika na Emelda. Amemuona kwa muda mrefu tu wewe ukiwa umemfungia macho huyu binti! Sasahivi unarudi kinyumenyume ukimtaka Emelda ambaye alikuwepo na hajawahi kubadilika! Si sawa kwako, Edwin ambaye naye ni kijana wa pale kanisani na aliyemuwahi Emelda tokea mwanzo na kushirikisha wazee tumuombee na Emelda mwenyewe.”
“Acha nikuulize kitu
baba.” “ Uliza tu maana hapa hatugombani na safari hii naomba Ezra usiingilie
kabisa ili tumsikie Junior mwenyewe.” Kimya. “ Umenielewa Ezra?” “ Ndiyo baba.”
“Haya uliza Junior.”
“Katika nyinyi mnayemuombea
Edwin au Edwin mwenyewe, kuna ambaye alishazungumza na Emelda kujua
anachotaka?” “Hapo sina uhakika ila najua wapo sehemu nzuri tu. Na Edwin
anajiandaa kumchumbia.” “Basi acha nikupe uhakika. Edwin alimtuma Ester kwa
Emelda, na Emelda alishamwambia hamtaki Edwin. Mpigie simu Ester kuthibitisha.”
“Ester yupo mapumzikoni na mumewe, siwezi kufanya hivyo.” “Mapumziko yao
yameisha jana. Na kesho watakuwepo kanisani kwa sababu jumatatu wanatakiwa
kazini. Tafadhali mpigie simu muulize ujue alichomjibu Emelda hata kabla mimi sija
mchanganya kama unavyodhania na naomba umuulize ni nani anapendwa
na Emelda?” Mzee akatulia.
“Najua upo radhi
ukosane na mimi kuliko kumsumbua Ester, japo niswali dogo tu ambalo hutachukua
muda mrefu.” “Unaanza lawama Junior!” “Ni kweli baba. Hapo hutaki kumsumbua tu
Ester.” Mama yao kimya.
“Mimi ninachokuonya
ni uwe muangalifu Junior.” “Hapana baba. Unataka kumaliza kesi ili
usimwingize Ester. Ila ujue nina kesi naye kubwa sana na safari hii
hutaweza kumkingia kifua kwa sababu umeonyesha upendeleo wa waziwazi, na
kushindwa kuwa upande wangu.” “Huu upande niliopo mpaka sasa ni wako
Junior. Na ndio maana unaona imenibidi kuzungumza na wewe.” “Kama kweli upo
upande wangu basi uwe unajua ukweli wote wa huu upande niliopo. Haitajalisha
kwangu kama utaupenda au la, ila ujue ukweli. Na hutajua ukweli
bila kumsikia Ester mtu unayempenda na kumuamini. Tafadhali mpigie
baba.”
Akamwangalia mkewe,
kimya akimtizama. Ezra akabaki akimtizama kama anayesubiria kuona atafanya
nini. Na ukimya ule wa mkewe, akaona apige. Ester akapokea kwa haraka. “Nilitaka kukupigia leo baba yangu. Nishakuwa na hamu na wewe.
Shikamoo.” “Marahaba mama. Umekuwa na wakati mzuri?” “Sana. Na
nimekuletea zawadi.” Huwa akifika kwa huyo binti, hawezi jisaidia. Gafla
akajawa furaha kama sio yeye. Akacheka kabisa kwa wazi, wote pale wakamtolea
macho wakimshangaa. Akajirudi.
“Asante
mama. Sasa hapa nipo na mama yako, Ezra na Junior. Tuna swali.” “ Wewe ndiye mwenye
swali.” Junior akamrekebisha. “Sawa. Nina swali juu ya
Edwin na Emelda. Unajua chochote juu yao?” “Kuna nini tena?!” Ester
akashituka. “Tafadhali jibu swali Ester.” “Mbona kama
Junior amenikasirikia mimi bila kosa!?” “Unalo na umenikosea Ester. Ila kwa
sasa tafadhali mjibu baba.” “Mimi Ninachojua ni Edwin anaamini Emelda ni mkewe.
Anaamini hivyo hata ofisini haachi kumzungumzia Emelda na sifa zake.”
“Hakukutuma
wewe ukamtongozee kwa Emelda?!” Junior akauliza. “Ndiyo na Hapana.”
“Acha kunichezea akili Ester maana huu sio wakati wake.” “Mbona mimi sina
kosa!? Hata baba anajua kama Edwin anampenda Ester! Tena hata Noah anajua. Ni
wewe peke yako ndiye uliyekuwa hujui kwa sababu ulikuwa ukimpuuza Emelda upo na
mchumb...” “Ester!” “Kwani uongo? Nimekuta jumbe zake kibao kwenye simu yako,
alizokuwa akikuandikia mchana hadi usiku, na hujawahi mjibu hata mara moja.
Bisha.”
“Na kabla
hujapoteza muda wa kuuliza nimejuaje, nimejua kutoka kwenye simu yako wewe mwenyewe
nilikuomba siku moja nimpigie simu baba anifuate kwako. Simu yangu iliishiwa
chaji.”
Ester akaendelea akisikika kujitetea tayari wala si kujibu tena swali.
“Wakati
nazungumza na baba, ujumbe wa Emelda ukaingia. Nikashangaa sana. Nikasoma kujua
anakwambia nini! Na kabla hujakasirika ni kwa nini nilisoma, jua
nilikuwa kwenye kumchunguza kwa nini alimkataa mwanaume kama
Edwin, japo nilishamwambia anao uwezo, akamkataa nikijua wazi Emelda kwao wana shida,
mtu kama Edwin anayempenda kwa dhati na hampuuzi, ANGEMFAA.”
Alikuwa akiweka
msisitizo kwa makusudi ili kumkumbusha kaka yake.
“Ndio
nikaona jumbe zote anazokutumiaga halafu wewe HUJIBU hata moja. Ndio nikaumia
sana. Na hata mama anajua hili.” Wote wakamgeukia mama yao. “Japokuwa Emelda aliniomba nisimsemee, lakini nilishindwa.
Nilikuwa naumia kuona anaweka mategemeo kwako wewe unayekaribia kuoa, na
humwambii mtoto wa watu. Unakula vyakula vyake tu, humjibu
chochote. Anabaki na tumaini ambalo linamchelewesha kwenye upendo
wa kweli. Edwin anampenda Emelda na anamfuatilia kwa karibu sana.
Akiona kitu chochote kizuri, anamnunulia yeye mwenyewe au ananituma mimi
nikamnunulie na akaniomba nisiwe namwambia kama vinatoka kwake.” “Ester!
Ester!”
“Sasa
unakasirika nini!? Wewe hujui kama wanawake wanahitaji matumizi hata nguo za
ndani?”
Kimya. “Sasa wakati wewe ukihudumiwa na Emelda, humjali,
Edwin alikuwa akimfikiria. Mpaka nguo za ndani alikuwa akinituma
nimnunulie. Lotion, sabuni nzuri za kuogea na deodorant ilikuwa kazi yake
kukumbuka na kununua hata kabla hajaishiwa. Sasa hapo kosa langu mimi ni lipi?”
“Tafadhali
turudi kwenye swali la msingi Ester. Ulipomwambia Emelda juu ya Edwin, alijibu
nini? Na samahani baba, nimeingilia nikitaka kusaidia turudi kwenye mstari,
naona tunapotea, mazungumzo yanavuta na wewe umesema bado unaratiba ndefu ya
siku.” “Wala si kupotea. Najua unamtetea Junior kama kawaida yako bila
kufikiria. Mnatafuta lawama kwa watu kama nyinyi wote hamkuwepo wakati
mlikuwepo, na Emelda alikuwepo akiwahudumia bila hata kumlipa!”
“Na kwa
taarifa yenu alikuwa akitumia kihela chake kidogo cha mshahara na
vyakula vya mama pale nyumbani kuwalisha nyinyi wenye mihela isiyo na kazi,
halafu Edwin anamuhudumia. Sasa kabla hamjamnyooshea mtu kidole
mjiangalie nyinyi wawili mliokuwa mkimdharau na kumfanya amsubirie
Junior akiamini ipo siku atamuoa.” “Na nitamuoa Emelda.” “Haaaah!” Ester akashituka
sana.
“ Japokuwa hutaki
kujibu, alikujibu nini, lakini…” “Unaoa mke wa mtu Junior na SIO sawa.
Edwin amemsubiria huyo binti wakati wewe ukichumbia wanawake wengine.” “Sikukwambia mimi
Junior?” “Baba, Emelda si mke wa Edwin na Ester unajua ukweli.
Labda afiche.”
“Mimi
sifichi kwa kuwa sina hila. Nilijuaga nimachokita, nikatulia
nacho mpaka ndoa.” “Sawa Ester. Wewe mtoto mzuri. Lakini jibu. Emelda alikujibu
nini juu ya Edwin? Na
mama naomba hakikisha ananijibu.” “Mimi najua alichojibu ila najua nikisema
hapa, mtasema namtetea Junior, ndio maana nimenyamaza. Lakini mnavyofanya si
sawa!” “Umeenza mama!” “Kwani huyu Emelda yeye ni mtoto
mdogo na hana hisia hajui anachokifanya?” Mama mchungaji akauliza
kwa ukali kidogo.
“Kama kweli
angekuwa mke wa Edwin si angemkubali basi na kuacha kufunga na kuomba
kwa ajili ya Junior?” Akauliza.
“Nani amekua karibu naye kati ya Junior na Edwin!? Si
Edwin? Kutwa yupo naye huko kanisani! Na wewe Ester kutwa kumuuza Edwin kwake! Mbona
asimkubali, halafu amekuja kumkubali Junior mara moja tu alipomtongoza?”
Kimya.
“Mnataka
kumchanganya Junior, na hakika sitawaruhusu.” Hapo akawa mkali
kabisa. Mama mchungaji akabadili gia angani. Mbele ya kifungua mimba! Hapo
akawabadilikia. “Kwani ilikuwa lazima Junior amtunze
Emelda ndipo aje amuoe? Hapana kwakweli!” Akajijibu hapohapo kama
ambaye asiyetaka kuingiliwa. “Kama Mungu amemuandikia
Emelda, itabaki hivyo. Na naomba muache kumtisha mwanangu. Yeye
sio mtu wa kwanza kuvunja uchumba! Watu wanavunja ndoa, ije kuwa uchumba!
Mnataka mwanangu aingie kwenye ndoa asiwe na furaha! Hapana kwakweli.”
“Nilijua tu
mama atamtetea Junior!” “Tena Ester binti yangu nakuonya mama, usikufuru.
Kama yako yamekuendea vizuri, tulia mshukuru Mungu. Wako mabinti kama wewe, wamesubiri
na kuishia kuachwa. Mifano unayo. Mmoja wapo ni Ezra huyu hapa tunaye
mfano ulio hai. Alitulia kwa yule binti akimwaga pesa kumtunza, mbona aliachwa?
Na mbona hamkusema? Leo imekua Junior ndio mnamkaba hawezi kuhema! Wakiachwa
wao ni sawa, ila wao wakiacha ndio sio sawa. Acheni kumnyima raha
Junior.” Mama
akaendelea kama aliyepata jukwaa.
“Wakati
wote mmekuwa mkimpongeza ana akili za kufikiria. Kumbe ni wakati akiwafanikishia
yenu tu?!”
“Mama Junior unafika mbali.” “Kabisa acha nifike. Huyu
Junior na mwenzie Ezra mlikuwa mkiimba sifa zao kutwa kwa sababu waliinua
huduma pale kanisani kwa juhudi zao. Kifedha ndio sitaki kuhesabu. Kiroho ndio
kutwa wapo kwenye maombi wakiombea huduma na hii familia na maisha yao yote wameyatoa
kanisani.”
“Na wewe
Ester ni mara ngapi huyu Junior amekua akikusaidia wewe na Devin mpaka
akasimama? Si huyuhuyu alijitoa mpaka akafanikisha mumeo kupata kazi BOT?
Amesimama na nyinyi bila kuchoka akiwatia moyo mpaka mkafanikiwa kuoana,
leo unamkejeli mwenzio!”
“Aliona ubora
wenu mkiwa chini sana. Akawashika na kuwatia moyo mpaka hivi leo! Tafadhali
msije sahau hilo. Na sitaacha kusema japo ni kukufuru, lakini
Ester, bila Junior mumeo mpaka leo angekuwa akihangaika mtaani.
Bisha, ukamuulize Devin. Kama atakuwa na yeye amesahau tutamkumbusha barua yake
ya shukurani kwa Junior na Ezra.”
“Haya, alipo
mchumbia rafiki yako na kukufanyia yako yakaenda, mlikuwa mkiimba sifa
zake kila mahali! Kweli leo mwanangu anawaomba msimame naye katika hili ambalo
kwanza hajuagi kulia shida mwanangu! Katika hili, kwa mara ya kwanza
ndio anawafuata, halafu kweli nyinyi ndio mnamchagua Edwin badala ya
mwanangu? Kweli!?”
Wote kimya.
“Ester ukijua ukweli
kabisa juu ya msimamo wa Emelda kwa Edwin, bado unasimama kinyume na kaka
yako!? Na nakuonya Ester, usijerudia tena hata siku moja kujifananisha na kaka
yako. Mbali ya kwamba amekupita mbali sana, Junior amesimama na wewe tokea
mdogo mpaka sasa. Alikuwa akikesha kukufundisha hesabu ulizokuwa huelewi
popote baba yako alikokuwa akikupeleka ukafundishwe, lakini alikuwa hachoki kukutia
moyo mpaka ukamaliza chuo. Leo unajilinganisha na Junior na kuona umempita
wewe! Hakika Mungu akusaidie usijisahau Ester. Acheni kumnyima raha
mwanangu!”
“Hee! Imekua nongwa! Sasa
na huyo Hope wenu amemuacha. Yupo kwenye uchumba na Emelda. Na hata yeye
akiona hafai, basi.” “Mama Junior!” “Hakika katika hili sitataka mtu
amchanganye. Akili hiihiii iliyokuwa ikisifiwa kwenye kuendeleza kanisa,
kusaidia wengine, ndio nataka iachwe, ifikirie mpaka itoe mke. Msimchanganye.”
“Haya. Tuambie habari
njema na mbaya. Na Ester usikate simu ubaki hapohapo na uache kulia. Maana
sasahivi zamu yako imepita, waachie na wenzio.” “Zamu yake inapita vipi tena?! Bado
ni mmoja wa hii familia na mawazo yake yanatakiwa sana.” “Yeye ameshaolewa,
habari iliyobaki kwa sasa ni ya Junior na Ezra. Atulie na awe
msaada kwa wenzie kama alivyosaidiwa yeye.”
“Mnaninyanyasa.” Akazidi kulia.
“Unakumbushwa ulipotoka, ili usijisahau. Na nakuomba unyamaze Ester sio uzidi
kulia ukijua baba yako hatasikiliza hapa, atabaki akikubembeleza wewe. Sio
sasahivi. Tulia tumalize kilichomleta Junior na mwenzie hapa ofisini.” “Hakika
humtendei haki mtoto! Umemnyanyasa kwa wazi kabisa!” “Naomba hayo tuendelee
nayo baadaye. Tunakusikiliza Junior.” “Acha tu mama. Nitatafuta msaada
kwengine. Twende Ezra.” Wakasimama.
“Ester, umekosa sana.
Na familia huwa haziwi hivyo, na wewe unajua. Huwa tunasimama pamoja wakati
wote. Mimi na Junior tumekua kwenye maisha ya kila mmoja wenu bila ya
kulalamika wala kuchoka. Tumejitoa kwa hali, mali mpaka kuwasaidia kufunga na
kuomba hata kwenye yale magumu yaliyokuwa yakionekana hayawezekani kwa macho.
Leo mnashindwa kusimama na sisi katika hili ambalo Junior ametoa sababu za wazi
tu!” Ezra akaendelea.
“Mlitaka aoe halafu yeye ndio akateseke wakati wengine wakipata
sifa!? Kwa wazazi kwa sababu wameozesha kijana wao. Na kwako wewe Ester kwa
sababu rafiki yako uliyemuunganishia kwa kaka yako, ameolewa bila shida. Ndivyo
mlivyotaka itokee ili Junior abakie kama mlivyozoea nyinyi, kwamba abakie
wakati wote akilipa garama ya furaha yenu!? Binafsi sikutegemea! Nilitegemea tofauti. Sidai, lakini nilidhania kipindi cha shida yetu
na nyinyi mtasimama na sisi! Lakini mnachagua watu baki kabisa!
Si sawa. Twende Junior. Nitampigia simu mama Jema nimuombe yeye msaada.”
Wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
INAENDELEA…
0 Comments:
Post a Comment