“Lakini pia nikamwambia mimi simtaki Eddy.” “Usianze kumuita kimapenzi.” Wivu tayari. “Ndivyo dada Ester anavyomuita!” “Naomba kwako abakie tu kuwa Edwin.” “Sawa. Lakini kile kitu ni kama dada Ester hakupenda kabisa. Maana ni kama alinibadilikia kwa muda fulani hivi.” “Kitendo gani tena?” “Kumkataa Edwin. Yeye akasema nachezea bahati, nitajuta.” “Mlishakuwa mkiwasiliana na Edwin?” Akanyamaza. Akapata jibu.
“Mnawasiliana kwa njia gani!?” “Mimi nahisi anakuwa anatumia watu wote wenye namba zao. Maana ni kila siku asubuhi, zile jumbe za neno la Mungu.” “Kila siku asubuhi?!” “Ni neno la Mungu!” “Mbona mimi hanitumii hilo neno la Mungu na ana namba yangu ya simu?” “Basi itakuwa kwa wale ambao tupo wote kule kwenye huduma ya watoto.” Ndipo akakumbuka Edwin ni kiongozi kwenye huduma ya watoto pale kanisani, na alimudu haswa hicho kitengo mpaka wazazi walikuwa wakifurahia kupeleka watoto wao huko. Aliandaa masomo maalumu ya watoto kulingana na umri wao, kisha akapata wasadizi wa hayo madarasa. Kwa hiyo yeye akawa amekishika hicho kitengo vizuri sana.
“Ni jumbe za neno la Mungu tu.” Akajaribu kumtuliza. “Mimi hivyo sitaki. Wewe una bibilia yako. Utasoma kwenye bibilia. Sitaki atumie mwanya huo kuwasiliana na wewe. Hivyo hapanakwakweli.” Swala la ugonjwa wa mama mkwe likawa limeshasahaulika tayari.
“Tuone jinsi anavyokuandikia.” Akamkabidhi simu yake. Akaanza kusoma. “Mbona na salamu kabisa?! Yaani mnakuwa kama mna chat?!” Akaendelea kusoma akilalamika. “Yaani kumbe ni kila siku asubuhi!” “Ila nahisi hizo jumbe ni za kundi. Sio zangu peke yangu. Ukisoma vizuri utaona.” Emelda akaendelea kumjibu kwa utulivu tu kama kumtuliza asijue kuwa anasikika kumtetea.
“Za asubuhi Emelda!? Ndio salamu ya kundi zima, kukutambua kikaribu hivi!?” “Eti mimi nikahisi pengine akifika kwenye salamu anakuwa ana edit jina anaweka kwa kila anayemtumia.” Junior akabaki akimtizama.
“Au wewe unafikiriaje?” Akajirudi kwa haraka. “Anaendelea kukuvuta karibu akijua siku moja utamkubali. Hivi mimi sitaki Emelda.” “Sawa.” Akawa hajaridhika.
Akarudi kusoma. “Na wewe unaonekana unamjibu!” “Ni salamu tu! Na wakati mwingine ukifuatilia vizuri kwenye hayo mazungumzo utagundua ni mazungumzo ya Sunday school. Nafanya kama msaidizi wake.” Hapo akasimama kabisa na kuondoka. “Wakati wakimzuia asiwasiliane na mimi huku, kumbe Ester amehamisha mawasiliano kwa Edwin!” Akawaza moyoni akichukia kabisa kana kwamba alikuwa akichati naye yeye huyo Emelda wakati hakuwa hata na mpango naye. Alipoondoka Emelda akamcheka moyoni. Hakujua kama ndio anawivu hivyo!
Baada ya muda akarudi. “Kaka Ezra anahitaji msaada?” “Oooh! Yeah. Nilisahau. Lakini wewe unaweza baki. Tutarudi baadaye. Chakula kipo. Ukisikia njaa unaweza kula. Kuwa huru. Tukimaliza tu, tutarudi.” “Nilifikiri umesema kuanzia leo tatizo lako ni letu!” “Ndivyo itakavyokuwa.” “Sasa kwa nini na mimi nisiende kusaidia? Naweza nikasaidia chochote kile. Nimemuona Jelini ni mtu mzuri. Hana shida. Na mimi naweza saidia.” Hilo likamfurahisha Junior. Kama maombi yake na Ezra yanajibiwa vile! Kama kuna dalili za wanawake zao kupatana! Hilo akalitunza moyoni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakatoka hapo. “Naomba kuwa makini na Edwin. Anaonekana yeye hajakukatia tamaa.” Akaanza tena wakiwa wanaondoka hapo. “Sawa.” Emelda akakubali bila shida. Hakuridhika. “Maana kama mtu alishakataliwa, alitakiwa kuwa mstaarabu. Aelewe na kukuacha. Maana wewe uliwaambia wazi humtaki. Sasa kwa nini anaendelea!” “Labda ameacha ndio maana unaona amesimamia mambo ya kiroho.” “Mbona kama unamtetea sana!?” Emelda akashituka kidogo, hakutegemea kama ataonekana anamtetea.
“Au si kwamba umemkataa moja kwa moja?” “Nilimwambia dada Ester.” Hapo akamtibua zaidi. “Kwamba jibu la hapana analo Ester na si yeye!?” “Yeye hajawahi kunitongoza! Ni dada Ester ndiye aliyesema na nikamjibu yeye.” “Hiyo haijakaa sawa kabisa na sijamuelewa kabisa Ester. Maana hapo huwezi jua alimjibu nini! Unaweza kuta yeye Edwin anajua umejibu utamfikiria au unaomba juu ya hilo kwa hiyo anakua yupo kwenye kusubiria. Mimi hivyo sitaki, Emelda.” “Sawa.” Akawa bado hajaridhika.
“Utafanyaje sasa?” Akamuuliza na kumuangalia kabisa akimtizama huku anaendesha. “Labda wewe unishauri chakufanya maana mimi siwezi kuanzisha jambo ambalo halikuwepo kati yetu! Itakua kama mimi ndio naanza kumtongoza sasa.” Hapo akamfanya atulie.
Akajua yameisha. Wakaendelea kwenda yupo kimya kisha akaanza tena. “Lakini lazima wajue kama wewe umenichagua mimi. Hata kama mimi nimechelewa kuelewa lakini sasahivi mimi mwenyewe nipo na nakupenda. Na utakua mke wangu mimi. Sitaki kuingiliwa. Kwanza sio sawa kujisogeza karibu na wewe kwa kujidai yupo kiroho. Wewe uhitaji kutumiwa neno la Mungu kila siku asubuhi! Huko ni kuniingilia kwa waziwazi. Na hivyo sitaki. Itabidi kuzungumza na Ester.” Emelda akamtizama.
“Kwanza namuhisi amekua msaliti. Kwa nini aingilie mambo yangu? Yanamuhusu nini? Alitakiwa aniambie, mimi mwenyewe ndio nichague. Nani namuoa, haimuhusu kabisa. Anamuuza mke wangu kwa wanaume wengine! Hiyo sio sawa. Nitataka kujua alimjibu nini Edwin baada ya kumkataa. Asijekuwa hajampa jibu la kueleweka.” Emelda akatulia kimya maana alijua akiongeza anaweza onekana anatetea. Wakawa wamefika kwenye ukumbi wa harusi alipokuwepo Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakaenda walipoelekezwa atakapokuwepo Jelini. Ezra alikuwa amepeleka vitu kwenye ukumbi mwingine wa harusi. Akafurahi sana kumuona Emelda mpaka Emelda mwenyewe akajisikia vizuri. “Tumekuja kukusaidia.” Emelda akamwambia akicheka taratibu. “Nimeshaanza kuwa kama wewe. Naongea taratibu mwenyewe!” Junior hana mbavu. “Mwaya Junior sijui yukoje!” “Wewe tupe kazi.” Junior akamwambia. “Mbona nawashukuru! Nakimbizana na muda. Sasa naomba niachie Emelda.”
Akafikiria wakamuona amekubaliana na mawazo yake. “Naomba wewe uende na huyu kijana pamoja na vitu vilivyopo kwenye gari. Anajua chakufanya. Naomba ukamsaidie kufunga hicho kiti kikubwa na marembo yake. Sio kazi kubwa sana. Hamtachukua muda mrefu, ila mtanisaidia kuweka uwaminifu kwa wateja wangu. Kuwawekea vitu kwa wakati bila kuwachelewesha.” “Usijali.” Junior akakubali bila shida, akaondoka na huyo kijana kama alivyofanya Ezra.
Emelda na Jelini wakabaki hapo kwenye huo ukumbi wakiendelea. Hapo palikuwa na kazi kubwa kidogo, na pesa nyingi. Hakutaka kumuachia mtu mwingine. Akaanza kwa kumuelekeza Emelda cha kufanya. Akaelewa kwa haraka sana! Wakawa wakienda vizuri tu tena kwa haraka mpaka akamshangaza Jelini kama ambaye alikuwa na uzoefu wa hiyo kazi tayari.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya kama masaa mawili wote wakajikuta wamerudi hapo walipokuwepo Jelini na Emelda. Akaruhusu vijana wake waondoke, wakabakia wao wanne nje ya ukumbi. “Nyie Emelda anaakili jamani! Yaani ukimwambia jambo mara moja tu ameshaelewa na kufanya, tena vizuri! Mimi nahisi ameelewa haraka kuliko hata mimi!” Wakacheka vile alivyomalizia kwa manung’uniko.
“Sasa mbona kama unasikitika tena?” “Mimi nahisi wivu. Ilinichukua muda mrefu kweli kuelewa kufunga hivi na mpaka leo amenifanya nione ndio maana nachukua muda mrefu kwenye makumbi ya watu! Yeye yupo mwepesi! Kote kule amefunga mwenyewe ndio maana mmetukuta tumemaliza. Asante Emelda.” “Nilikwambia usijali. Na wewe ni mwalimu mzuri Jelini.” “Mmmh! Mimi nahisi nitaanza kujifunza tena kutoka kwako. Natamani kumzidi mahesabu mama mchungaji, ni hivyo tu nampenda. Ningemuomba aniachie wewe.” Ezra na Junior wakaangaliana.
Emelda akacheka. “Kweli! Hii kazi inaweza onekana kama duni, kwa sisi tusio soma, lakini inapesa! Nikiwaambia pesa ninayoingiza leo tu, kwa hichi tu mlichonisaidia kufanya. Hamtaamini. Halafu bado viti ninavyokodisha.” “Kumbe una viti unakodisha pia!?” Junior akamuuliza kwa mshangao kidogo.
“Bwana vina pesa! Halafu uendeshaji wake si mgumu kabisa. Naviweka anakofanyia mama biashara zake. Ananisaidia kusimamia. Wakianza kukodisha alhamisi kwenye kitchen paty zao, lazima wanirudishie ijumaa asubuhi. Ujue jioni hapo vitatoka kwenda kwenye sendoff au hata kwenye maharusi. Jumamosi asubuhi lazima warudishe. Ndio napata wateja wengi tena wanang’ang’aniana kwa mashuguli ya jumamosi. Kwa hiyo viti hivyohivyo vinaingiza pesa siku tatu kwa juma, mfululizo. Na nilivinunua vile viti vizuri ambavyo haviharibiki kwa urahisi. Na meza zake pia huwa wana kodi. Ni biashara ambayo inaonekana duni lakini…” Akawa kama anajitetea.
“Nisikilize Jelini. Usimsikilize Hope na wala usikubali maneno yake yakuingie akilini. Aliyokwambia ni maneno ya mtu asiyefikiria mbali.” Emelda akamwangalia Junior kama asiyeamini anachokizungumza juu ya Hope. Maana sifa za huyo Hope zilikuwa zikiimbwa na kila mtu. “Kuna faida gani ya kusoma halafu unaishi kwa kuombaomba?” Kimya Jelini akicheka taratibu.
“Mtu kuweza kumudu mazingira yake kwa kiwango chako, ni zaidi ya elimu ya darasani. Binafsi imeniongezea sana heshima kwako. Unaakili yakufikiria Jelini. Unajuhudi. Halafu unaupendo. Sina hata wasiwasi ikija kutokea Ezra hana pesa, wewe utayamudu maisha bila shida.” Wakacheka.
“Kabisa Jelini! Una moyo mzuri sana na nafikiri ndio maana unafanikiwa. Usikubali kukwama kwenye elimu ya darasani ambayo watu wanayo lakini haiwasaidii. Binafsi najivunia sana wewe. Achana na Hope. Kwanza hayupo tena katikati yetu.” Akawa hajaelewa.
“Hivi unavyotuona sasahivi, ndivyo itakavyokuwa mpaka mmoja wetu aondoke hapa duniani.” Akamfafanulia na kumuacha Jelini ametoa macho. Akamtizama Ezra. “Leo wamesitisha uchumba.” “Kwamba mmeachana!?” Akamuuliza Junior akiwa kama haamini.
“Ndiyo. Hapa nasububiri mmalize swala la uchumba wenu, na mimi nimchumbie Emelda.” Bwana Jelini alifurahi akashindwa kujizuia. Mpaka akarukaruka. “Jelini!” “Sasa nikwambie mimi na Emelda tunaendana na tunazungumza lugha moja. Uongo Emelda?” Hawana mbavu. “Halafu mimi Emelda nampenda.” Wakazidi kucheka.
Kisha akajirudi na kutulia kinyonge kama mtoto mzuri. “Ila mimi mtu mbaya! Sasa kwani nilitakiwa kukupa kwanza pole au hongera? Nilijisahau.” Wakazidi kucheka. “Ushachelewa.” “Mwaya Junior! Niambie mwaya Ezra. Nilijisahau. Mimi nampenda Emelda bwana! Nilitakiwa nimpe Junior hongera au pole?” “Vyote.” Akajibu Ezra akicheka.
“Pole kwa kujichelewesha. Na hongera ya kumpata Emelda.” Ikawa na maana kubwa sana kwa Emelda kwamba na Ezra amempokea. Akafurahi akicheka ameinama. “Nyie, hongereni sana. Ila sasahivi nimetulia ndio naanza kufikiria.” “Nini tena?!” Junior na Ezra wakauliza kwa pamoja wakiwa na wasiwasi kidogo.
“Watoto wetu sisi wote wanne wakiingia sehemu. Tatizo likitokea tu watakuwa wanauliza, ‘Watoto wa Jelini na Ezra wameharibu nini?’ Maana…” Walicheka hapo mpaka machozi. Jelini alizungumza kwa masikitiko kweli.
“Mimi nawaambia ukweli na mtakuja kuona. Kila wakiwepo watoto wetu, watu watajua wetu ndio watundu, sio wenu. Na watasema wamefuata kwa mama yao. Nyinyi wote wapole! Ndio maana mimi naanza kuwa kama Emelda.” “Jelini na mawazo yake!” Wakazidi kucheka. Wakapata wakati mzuri hapo wafuraha.
“Sasa hapa tumemaliza. Nitarudi tena usiku kufungua na kuchukua vitu vyangu. Nawashukuru sana kwa kunisaidia. Isingekuwa nyinyi, hapa ningekaa mpaka jioni.” Wakaangalia muda. “Bado mapema. Si tutakuwa pamoja mpaka usiku?” Akauliza Ezra akimwangalia Jelini. “Mimi sina neno. Mmenisadia kufupisha siku yangu ya kazi. Sina lakufanya sasahivi mpaka usiku. Lakini lazima nikaoge kwanza. Mlitaka twende wapi? Naweza kuwafuata huko.” Wakaangaliana.
“Tutafute sehemu yenye vyakula vizuri na mazingira mazuri tutakayoshinda huko tukisubiria kwenda kutoa viti ukumbini.” Akatoa wazo Junior lililomshangaza kidogo Jelini. “Kwamba mnampango wakunisaidia tena na usiku?!” “Kabisa! Au wewe ulikuwa ukiwazaje?” Junior akauliza kama ambaye hajaelewa. “Msije anza kunikimbia kwa kunichoka. Nyinyi pumzikeni. Mmeshanisaidia vyakutosha.” “Sisi ndivyo tunavyoishi Jelini. Hata Emelda nimemwambia. Kila kitu chetu sisi tunafanya pamoja. Na kwakuwa na nyinyi mmeongezeka kwetu, itakuwa hivyohivyo. Au nimekosea Ezra?” “Kabisa. Hakuna jinsi mmoja wetu akaumia sisi tukawa sawa. Tunasimama pamoja kwa hali, mali, hata kwa kusaidiana kimawazo. Lako ni letu wote. Ndivyo tunavyoishi.” Ezra akaendelea.
“Ila binafsi, hili hata sijamwambia Junior, nimefurahia moyo wako Jelini. Umemfanya Emelda ajiunge kwetu kirahisi!” “Kabisa. Na nina uhakika amefanya vizuri leo kwa ile thamani uliyoweka kwake. Umempenda na kumuheshimu bila kumdharau! Na kwa hilo nitakushukuru daima.” “Mpenzi wako anapendeka bwana!” Wote wakacheka.
“Sio kwa wote Jelini. Junior yupo sahihi. Tokea umenipokea hapa na jinsi ulivyonielekeza hukunielekeza kama wengine wanavyonichukulia. Wewe nimekuona tofauti Jelini, ndio maana ulivyonielekeza nikajiongeza na mimi nikijua unanichukulia vizuri. Tena ukijua mimi ni nani, wadhifawangu kwenye jamii, halafu wala bado hukujua kama nipo na Junior! Ukanipa heshima ya tofauti na wengine wanavyonichukulia. Ukanifanya kama nipo sawa tu na wewe, kwa heshima! Ulinishangaza kwakweli. Nakushukuru.” “Mwaya wewe unaongea vizuri!” Walicheka wasiamini. Mpaka Emelda akajificha kwa aibu.
“Jelini! Yaani maneno yote hayo wewe umebakiwa na hilo tu!?” “Mimi si nilisema anapendeka! Sasa mmeamini! Ila nyinyi mmenifurahisha! Asanteni kwa kuniunga kwenye ummoja wenu. Kukitokea na nyinyi mnataka msaada wangu, muwe mnaniambia. Ndio nitafurahi.” “Wala usijali. Tupo pamoja.” Akaongeza Junior.
"Basi naomba iwe karibu na baharini na kwenye pool.” Jelini naye akatoa wazo. “Na mkikubali naweza kumuomba mama, nikaja na Jeremy. Ili apate muda wa kuogelea pia. Asikae ndani peke yake kwa muda mrefu.” Likawa jambo zuri. Ezra akafurahi sana. “Mwambie mama tutakuwa waangalifu naye.” Akaongeza Ezra. “Sawa.” Akakubali Jelini.
“Mkikubali tena naweza kwenda na Emelda pia akaoga na kubadili. Na yeye ametokwa jasho. Halafu tukawafuata huko mtakapotuambia.” Hilo hata Emelda akalifurahia. Wakaondoka Jelini na Emelda. Ezra akaondoka na gari yake, na Junior hivyohivyo.
Katika Hali Zote.
Hakuna litatokea kwa mmoja wao hao wawili, mwingine asijue. Na wakiwa mbele za watu, watakingiana kifua mpaka mwisho, ila huwezana wenyewe sirini. Akiwa njiani amempigia simu Ezra akilalamika juu ya Ester na Edwin, simu ya Mika ikaingia. “Acha nimuunge na wewe usikilize. Hali sio nzuri kama nilivyokwambia.” Wakiwa wanafanya kazi huko ukumbini, tayari alishampigia simu Ezra na kumueleza hali ya kwa kina Emelda. Na Mika alishampigia simu kumwambia imebidi kuzungumza kwa undani na mwalimu wa nidhamu. Amemuelewa na kumpa ruhusa kwenda kumfuata mama yake amlete mjini.
Akapewa hiyo siku ya jumamosi lakini akaambiwa jumapili awe amerudi shuleni. Likawa limekaa vizuri na hata kusamehewa kabisa. Alichoshangaa Mika kwa pale kwenye shule ya sekondari akaonekana kama kijana mwenye hekima sio kama vijana wengine. Akapongezwa na huyo mwalimu wa nidhamu akionekana ni kijana anayejielewa na anayejali mambo ya nyumbani. Ikamfariji sana kuona hajadharaulika.
Akamuunganisha Mika. “Uko na Ezra pia kwenye hii simu.” Akawa muungwana kumjulisha ili kama yupo huru kuzungumza na Ezra naye akiwepo iwe sawa au amtoe Ezra wabakie wao wawili. Ila akaonekana hana tatizo. “Shikamoo kaka Ezra.” Wote wakashangaa maana ni kama yeye aliwafahamu vizuri tu! Ezra akaitika na kumuuliza. “Vipi mama?” “Nimefika huku. Lakini nimemkuta mama mgonjwa! Mguu unamaumivu, hawezi tembea kabisa. Anasota. Kwenye basi hawawezi kumpisha akakaa. Na kwa jinsi alivyo, hawezi simama kwa safari ya masaa mawili. Nilikuwa nikiomba nitumie pesa zaidi kukodisha pikipiki.” “Nashauri akodi gari, Junior.” Ezra akasikika.
“Gari itakuwa garama sana!” Mika akajibu kwa wasiwasi. “Mama ni muhimu, Mika. Hukuwa na dawa zozote za maumivu?” Junior akauliza. “Zilisha isha.” “Hakuna hata maduka ya madawa hapo karibu? Mnunulie za kupunguza maumivu na kitu chakula wakati wewe ukishugulikia usafiri. Kodisha gari tafadhali. Ukifika mjini umpeleke hata kwenye dispensary. Wamchome sindano ya maumivu. Sisi tutakuja kumfuata kumpeleka hospitalini kwa matibabu kamili.” Ukawa muujiza ambao hakuutegemea.
“Nawashukuru sana. Acha nichangamke ili nimtoe hapa.” “Poleni sana. Ila katika yote usijesahau chakula. Wale kwanza ndipo umpe mama dawa.” “Na usiache kuwasiliana kwa kila hatua, Mika.” Akaongeza Junior kwenye pole na maelekezo ya Ezra. “Haitakuwa usumbufu?” “Hata kidogo. Muda na wakati wowote, wewe piga. Na ukishampandisha kwenye gari ndipo tumtaarifu Emelda.”Ikawa kama anamuonya asimtie wasiwasi kwa wakati huo hawajafikia suluhu ya jinsi ya kumtoa hapo kijijini. Akaelewa. “Jamani mimi nawashukuruni sana. Asante.” “Tupo pamoja.” Akamalizia Junior na kukata.
Kwa Jelini&Emelda
Alichokifanya Jelini ni kutafuta nguo ya Emelda kwanza. “Mimi mwenzio napenda kupendeza na sinaga dogo. Popote nikitoka lazima nipendeze.” Emelda akacheka akimsikiliza. “Na kweli huwa unapendeza.” “Sasa na wewe lazima upendeze. Twende tukatafute nguo nzuri. Simple casual. Halafu tukitoka hapo tunakimbilia saluni. Waku style hizo nywele kiufukweni ufukweni ndio twende sasa ukiwa umependeza sanaaaa. Mpaka akikuona Junior azidi kuchanganyikiwa.” Emelda hana mbavu kwa furaha. Hajui kinachoendelea kwa mama yake.
Kwa Ezra&Junior
Huku kwa kina Junior wao mipango ikawa inaendelea. Wakawatafuta wazazi, mida hiyo walikuwa kanisani. Wote wawili wakawafuta. Wakajikuta wanaingia kanisani pamoja na kuegesha sehemu moja. Wakiwa wamejawa hamasa, zaidi Junior wakakimbilia ofisini kwa mzee wakijua na mama atakuwepo huko akiwasubiria. Cheko limemjaa Junior asijue yajayo yanayo msubiria.
“Nina habari njema na mbaya.” Akaanza Junior wakimtizama. Ila baada ya kuwasoma vizuri akagundua si shwari sana, zaidi mzee. “Mbona kama…” “Wewe siku hizi hutabiriki bwana! Anza na habari mbaya kwanza halafu uje utupooze na hiyo njema kama kweli ni njema.” “Baba amekosa imani na mimi!” “Kwa sababu umenipa sababu, je!” “Nimekua mtumzima baba.” “Sawa. Tuzungumze basi maana bado nina ratiba ndefu.” Akajiweka sawa. Ezra kimya akimwangalia hapo ofisini kwa mzee wao na yeye alishayosoma hayo mazingira akahisi upepo unavuma isivyo.
“Naona nianze njema kwanza.” “Sikukwambia siku hizi hutabiriki? Zamani ungefuata ushauri wangu bila shida.” “Kwa sababu habari ya kwanza inategemeana na ya pili baba! Ila sio ukaidi! Mbona kama nakuhisi huna furaha na mimi?” “Ulikuwa ukitabirika Junior. Sasa hivi maamuzi yako yanategemeana na siku unavyojisikia.” “Baba!” “Nisikilize tu. Nilivyokuzoea wewe tokea unakua ni huongozwi na hisia.” Akaendelea.
“Junior wa sasahivi anajua kukasirika na kutendea kazi hasira zake.” “Najua unampenda Hope, baba. Lakini mimi sikuwa na furaha naye!” “Kwa nini sasa?! Huyu Emelda ambaye unataka kutupa habari zake njema kama amekubali, si alikuwa hapa siku zote akikuhangaikia mchana na usiku!? Kilichobadilika nini?” Kwamba hata na mzee alikuwa akizijua juhudi za Emelda kwa kijana wake.
Lakini kabla Junior hajajibu, mzee akaongeza swali jingine. “Utafanya nini ukishamchumbiahuyo Emelda uliyekuja kumgundua juzi, ukakuta na yeye anayo mapungufu yake? Utatafuta tena mwingine aliyekuwa mwema kwako na kumchumbia na yeye?” Junior akawa ameshakasirika ila akatulia.
“Nakuuliza Junior? Maana hawa mabinti unachumbia na kuwaacha ukumbuke unawatoa sokoni. Edwin anampenda sana Emelda na yupo tayari kumuoa.” Walishituka hao wawili wakaangaliana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
BADO juma halijafanikiwa kukatika. Ndani ya hilo juma kulijaa MENGI Mno.
Na Mzee Naye Amembadilikia Junior.
Je, Hapo amevaa hofia ya Ubaba au Kiuchungaji Kwa Waumini wake!? Au Vyote?
Anaonekana kujua ukweli zaidi juu ya Edwin kwa Emelda.
Junior akidhani ni ‘neno la Mungu’ tu, kumbe mpaka mchungaji wa Edwin anataarifa za Edwin kwa Emelda.
Nani wa Nani? Nani Atapokonywa Tonge Mkononi Kabla hata Hajaweka Mdomoni!?
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment