Mama yao akawakimbilia. “Subirini.” Wote wakasimama. “Twendeni kule nje
mkanieleze vizuri. Kuanzia kwa Emelda na hili mlilotaka kuniomba mimi mwanzo.” “Acha tu mama.” “Hapana Junior. Sitapoteza nafasi yangu ya umama kwenu kirahisi hivi. Nitaumia sana kuona eti mama Jema ndio ananibebea majukumu yangu! Hapana Junior. Msiniadhibu wanangu.” “Sio kukuadhibu, naona tukupunguzie mzigo.” “Sijalemewa na mzigo wangu. Twendeni.” Wakatoka kabisa hapo kanisani na kwenda kusimama nje kwenye kivuli.
“Tuanzie kwa Emelda.” “Nakiri nilimfumbia macho mama. Lakini si kwa kumdharau ni vile ambavyo nilimchukulia kama Ester tu. Kwa hiyo kila jumbe zake nilisoma na kutafasiri kwa jicho la Ester. Sijitetei lakini na Emelda mwenyewe anatuogopa sana mimi na Ezra. Kwahiyo tukajenga kama umbali ili tusimnyime raha. Nakiri hapo ndipo nilipopitiliza mama. Lakini si dharau au kumpuuza.”
“Sasa umemwambia Emelda mwenyewe?” “Nimemwambia na kumuomba msamaha. Yeye amesamehe hata kama atakua hajaelewa. Emelda amenipokea na hilo kosa langu.” “Acha nikwambie ukweli Junior. Yule binti amekusubiria bila kuchoka mpaka nilikuwa nikimuhurumia! Yeye ndiye aliyenifanya kuongeza manunuzi pale ndani ili asiendelee kuingia mfukoni.” “Kwa nini hukuniambia mama!?” Junior akalalamika.
“Kwa sababu hii hii niliyowapa pale ofisini. Tunakuamini kwenye mambo yote. Kwanini na hili tusikuamini nalo? Niliacha ili ufanye maamuzi yako mwenyewe. Na uzuri Emelda mwenyewe alikuwa akiomba sana. Na mimi pia. Nilijua Mungu hawezi akakuacha katika hili. Wewe na mwenzio huyu mmechangia kwa asilimia 80 kununua lile eneo la kanisa kabla ya hawa washirika wote hawajajiunga na sisi! Mishahara yenu ya mwanzoni kabisa. Kweli Mungu awaache hivihivi tu? Si rahisi. Na mimi nilikuwa nikimdai Mungu kwa machozi nikimwambia akumbuke sadaka yenu na nikawa namwambia mlimjengea nyumba, mpaka leo watu wamepata pakumwabudu ni akili yenu na mioyo yenu ya kumpenda yeye, nyinyi wawili kwa pesa yenu bila kushulutishwa.”
“Mimi na baba yenu tulikuwa hatuna mpango wa huduma kubwa hivi! Kwanza tulijua tumeitiwa watu wachache kwa vile uwezo wetu ulivyokuwa. Lakini nyinyi mkatuchemsha mpaka tukasimamia imani yenu. Tukanunua hapa wakati huo hapa hapaonekaniki kama ni sehemu ya maana. Sasa kweli Mungu atawaachaje!? Ndio maana hata Helen alipomuacha Ezra, nilijua ameumia sana. Lakini hata baba yenu nilimwambia, hakuwa mke wa Ezra Mungu aliyemwandalia. Mwache aende. Ezra ataumia, lakini Mungu atamjibu kwa wakati wake. Ona sasa mwanamke uliyepata!” Wakacheka.
“Mpaka Noah mwenyewe amemsifia kwamba anaonekana ana moyo mzuri!” “Nashukuru mama. Asante kusimama na sisi.” “Asante mama.” Junior naye akaongezea kidogo akisikika ametulia.
“Haya niambieni kinachoendelea.” Ndipo wakamsimulia hali ya kwao kina Emelda na mama Emelda mwenyewe. “Mleteni nyumbani tumtafutie matibabu. Lakini Junior amini huyu binti anakupenda wewe. Kwa hali ya kwao kwa jinsi mlivyonisimulia na alivyokusubiria japo hapakuwa na tumaini! Hakika anakupenda. Usije sahau hilo.” “Siwezi mama. Nimejikuta nampenda Emelda. Na sina shaka kuwa ndiye mke wangu.” Akafikiria kidogo kama anayevuta hisia.
Kisha akasema. “Kuna jinsi najisikia kwake, sijawahi jisikia hivyo kwa mwanamke mwingine yeyote wala hata kwa Hope aliyekuwa mchumba wangu! Mpaka nasema pengine Mungu alikuwa akiniandaa kwa ajili yake ndio maana akanifunga macho hata nisimuelewe mpaka nipite kote huko nijifunze ndipo anipe yeye.” “Mungu atawasaidia. Usiogope wala usijitilie mashaka. Wewe unaombasana. Amini hata katika hili Mungu atawasaidia.” “Amina mama.”
“Lakini kuna jambo jingine.” “Nini?” “Na huyo mdogo wao wa mwisho ambaye anaishi na mama yao naye atahitaji hifadhi.” “Mungu alituweka kwenye lile jumba kwa makusudi. Kuna vyumba mle japo ni kwetu lakini kwa hakika sio vyetu. Nafikiri naona ndio wakati huu mwenye nyumba ndio anataka kuvitumia. Acha waje. Mungu wao atawatunza hapo mpaka atakapowafungulia mlango mwingine. Emelda amekua msaada sana kwetu. Anafanya hata usiku tena bila ya kulalamika.”
“Ester huyuhuyu alipokuwa akiumwa lile tumbo lake alikuwa akikesha naye usiku kuchwa akimuhudumia mpaka kusafisha matapishi yake, tena bila ya kulalamika! Hakika ufike wakati wake wakulipwa. Alijitoa sana kwenye hii familia.”
“Wasiwasi wangu ni mahali pakupata binti kama yeye. Hapo ndio nakwama. Alinifanya nikapumzika shida za wafanyakazi kwa muda mrefu sana!” “Mungu atakupa mwingine mama. Usiogope.” “Nashukuru kunituliza Ezra mwanangu.” Wakajipanga hapo hao wawili wakaondoka.
Penzi Halikuchanganywa Na Pesa.
Na wao wakaelekea majumbani kwao kujisafi. Wakakutana kwenye hoteli nzuri sana kama walivyokubaliana, tena kwa wakati. Emelda alipendeza mpaka Junior na Ezra wakabaki wameduaa. Jelini alijua. Alicheka mpaka basi. “Sasa hiyo trela, bado muvi lenyewe.” Akawaambia akijigamba. “Msicheze na Emelda. Mambo yake si madogo!” Emelda alikuwa akicheka kwa aibu.
“Haiwezekani!” “Sasahivi habari ya mjini ni Emelda. Mnamuona?” “Acha bwana Jelini!” Emelda akamzuia akicheka kwa aibu sana. “Si umeona wamepatwa na ububu gafla! Sasa na hapo bado!” “Kwamba tumtarajie Emelda mwingine zaidi ya huyu!?” “Huyu!? Bado kabisaaa! Kwanza sisi tunapenda vitu vizuri. Ila sana! Na hapo tulikuwa na haraka. Kwa uzuri wa Emelda, hapo ndio juujuu.” Mpaka Emelda akajificha.
Walimtengeneza vizuri. Akavaa gauni refu mpaka chini, la pinki lakini na maua meupe yaliyopendezesha sana mwili wake. Lilimshika kaumbile kalikoonekana sita ya nguvu ila nyembamba iliyonona. Mikono ya kamba lakini iliyoweza kuziba mikanda ya sidiria. Jelini alimpa hereni na cheni, dhahabu safi. Kubwa ikamkaa vizuri. Alimnunulia miwani ya jua na kofia ya beach, rasta aliyosuka ikamwagika chini ya kofia mpaka mgongoni ila juu wakaisokota vizuri, ikaweza kukaa ndani ya hiyo kofia na akitoa kofia pia alipendeza. Jelini akamfundisha jinsi ya kuchomekea hiyo miwani ya juu hapo juu ya nywele atakapovua. Akavaa na sendozi nyepesi za pinki. Bwana alipendeza! Ungejua ni rafiki wa karibu sana na Jelini jinsi walivyotokea vizuri pamoja.
Kama kawaida yake yeye Jelini hakujikosea. Alivaa gauni la njano lenye kamba zilizopita shingoni. Likajimwaga kuanzia juu mpaka chini kama mapazia yaliyojiachia kwa muundo mzuri sana na kumpendezesha. Akajipangilia haswa kama mwanae Jeremy. Wakatokea kitajiri.
“Kwa hakika mmependeza sana.” “Asante. Na nyinyi mmependeza na pensi zenu na mashati meupe. Halafu mchumba wangu mimi akapendeza zaidi yako Junior! Yeye anacheni, wewe huna!” “Jelini!” Wote wakacheka. “Nakutania bwana! Mimi nafurahia kuona jina langu kifuani kwake. Ila wote mmependeza sana. Halafu nimefurahi tupo pamoja.” Wakatafuta sehemu wakakaa.
“Sasa sisi hapa hatujaja kukaa. Si eti Jeremy?” Akaanza kucheka. “Mimi nataka kuogelea tu mpaka baadaye bibi akija kunichukua.” Wakamwangalia Jelini kwa mshangao. “Mama amesema saa 12:30 jioni mwisho. Na amesema anakuja kumchua mwenyewe ili nisimpe kiswahili kirefu. Kwa hiyo saa 12:30 awe ashatoka majini, ameoga na kubadili nguo na awe amekula kabisa.” Ikabidi wawe wapole.
“Basi tuanze siku. Naweza kumsindikiza kuogelea.” “Wala si wakumsimamia. Maadamu pool ipo pale mbele ya macho yetu, nampeleka kubadili nguo. Akitumbukia majini narudi kukaa.” “Ni sawa mimi nikimpeleka?” Ezra akauliza. Jelini akamwangalia mwanae akamuona anacheka huku akimwangalia na yeye. “Ezra ni mtu mzuri sana. Usiogope.” “Njoo nikunong’oneze kitu.” Jelini akacheka akimsogezea sikio. Alifanana na mwanae kama mapacha.
“Nipeleke wewe!” Akamwambia mama yake. Jelini akacheka akifikiria jinsi ya kuweka hilo sawa, kisha akamwambia basi twende na Ezra pia.” Hapo akakubali na Ezra kuridhika. Wakaondoka hapo hao watatu na kumuacha Junior na Emelda.
Emelda&Junior.
“Umependeza sana Emelda.” “Asante. Lakini haupo sawa.” “Emelda! Kwamba kwako siwezi kujificha hata kidogo!?” “Niambie nini kinakusumbua.” “Hamna bwana! Kila kitu kitakua sawa.” Akamuona ameinama kama anayefikiria. “Nakuahidi kila kitu kitakua sawa, Emelda. Usijali.” “Najali na siwezi kujisaidia.” Akaongea taratibu kwa sauti yake tulivu, na kuendelea.
“Naweza nisiwe kama kaka Ezra. Lakini naomba na mimi uwe ukinishirikisha. Hata kama sitaweza kukusaidia hata kwa mawazo tu, basi nitajua nini chakuombea! Najua ni ngumu kufanya hivyo kwa mtu kama mimi, lakini naomba ujaribu.” Ikamuingia Junior na kujisikia vibaya jinsi alivyoiweka. Akajishauri jinsi ya kumshirikisha.
Akamwangalia, akakuta ametulia tu. “Twende tukatembee baharini. Acha viatu ili visikusumbue mchangani.” Emelda akatoa viatu kama yeye Junior na kofia akaweka pembeni. Akabakia na miwani ya jua kama Junior. Wakatoka hapo wakifuatana mpaka ilipokuwa bahari pembeni ya hiyo hoteli, si mbali. Wakaanza kutembea taratibu, kimya kwa muda.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kisha akaanza. “Sikujua kama mambo yako na Edwin yana picha kubwa kwa namna niliyosikia leo!” Emelda akamwangalia akiwa na sura ya sijui unazungumzia nini. “Tulikutana na wazazi ofisini kwa baba na Ester akiwa kwenye simu. Wakaniambia kinachoendelea.” “Ni nini hicho kinachoendelea!?” Emelda akauliza taratibu bila paniki.
“Inavyoonekana yeye anaamini kwa asilimia zote kuwa wewe ni mke wake.” Akamsimulia kila kitu. Akashangaa Emelda ametulia tu. “Nimekwama.” Emelda akamwangalia. “Niambie ulipokwama.” “Sijui Emelda! Sijui natakiwa kufanya nini!” “Kwa upande upi?” “Sijui! Ndio maana nimechanganyikiwa.” Kimya wakiendelea kutembea kwa muda. Wakafika mbali kidogo na upande waliokuwa wamekaa hotelini.
“Naomba tukae kidogo nikwambie kitu.” Emelda akavunja ukimya. Wakatafuta sehemu kuna mwamba, wakakaa. “Japokuwa sijapenda dada Ester alivyokuwa akinipokelea hongo kutoka kwa Edwin na kunipa, lakini mimi nitakwambia vile nilivyofika hapa.” Junior akamwangalia na kuzidi kuvutiwa. Emelda alitulia vizuri na akapendeza haswa.
“Emelda wewe ni mzuri sana. Najutia mengi! Najilaumu. Najihisi nimekwama kabisa.” “Mimi nilijua kitu nataka. Japokuwa ilikuwa ni kama ndoto ambazo hata ngumu kuthubutu kuota, nikiwa najua hata watu watajua sikustahili hata kidogo lakini moyoni nilijua kwa hakika mimi ndio nastahili kuwa na wewe.”
“Kwa hofu ya watu, nikajitahidi kupuuza. Halafu hata jinsi ulivyokuwa ukinichukulia haikuwa ikitia moyo kabisa. Nikajitahidi lakini nilishindwa. Moyoni nilikuwa nipo tayari kwa lolote na kukusubiria wewe tu.” Akaendelea taratibu.
“Edwin alipoanza kutuma ishara kwangu hata kabla ya dada Ester hajaniambia, mimi nilijua. Maana ukweli nipo naye karibu kule kanisani. Edwin anajali sana, Junior. Naomba nisikudanganye. Ni yule mtu anayeweza kukufikiria na kukufanyia jambo mpaka ukashangaa. Au kama ulivyosikia leo. Sijashangaa alichokuwa akifanya kwa kupitia dada Ester. Ndivyo alivyo Edwin. Amejawa upendo na..” “Naomba kwa sifa za Edwin tuishie hapo.” Wivu. Roho ikazidi kumuuma.
“Sawa. Ninachotaka kukwambia, ni japokuwa alichoniambia dada Ester alikuwa sahihi ila aliniambia kwa jinsi ambayo sikupenda.” “Alikwambia nini?” Emelda akasita. “Sijakuficha kitu, na wewe usinifiche. Tafadhali Emelda. Umeomba ‘nijaribu’ kuzungumza na wewe. Mimi nimechukua hatua ya kwanza, zamu yako na wewe.” Akajirudi.
“Nafikiri alichoka kunibembeleza, usiku mmoja niliporudi chumbani baada ya kazi aliniambia hivi, badala nimkubali Edwin nikaishi kwangu, nakupumzika, mimi nang’ang’ania kutumika kwenye majumba ya watu. Inakua kama nimeandikiwa shida, nakimbizana na jua.” Junior alishituka sana.
“Haiwezekani Emelda!” “Sina sababu ya kumsingizia. Najua ni dada yako na wote mnamwamini sana kwa sababu ni mkimya, lakini Junior, Ester ana maneno machungu sana.” Haikuwa shida kumuamini Emelda. Na yeye siku hiyo kwa mara ya kwanza alikutanishwa na aina hiyo ya Ester. Alimtolea uvivu mbele ya wazazi na Ezra bila ya kumbakisha.
“Alikuwa akiniambia mengi juu ya Edwin vile anavyonisifia hata ofisini kwao mbele za wafanyakazi wenzao na mengine mengi akisema ananipenda kwa dhati, na ametulia. Yupo radhi kuwa na mtu kama mimi, mwenye kama hadhi yangu, na kuacha wanawake wa maana. Na mengine mengi tu. Haukuwa ushawishi wa siku chache na utulivu. Alianza kwa kunibembeleza. Akaja kwa ukali. Ndipo akamalizia kwa vitisho.” “Pole sana Emelda.”
“Nakwambia hivi ili nikuonyeshe kile kilichonisaidia mimi katikati ya kelele nyingi. Katikati ya wanaume wengi na shida za kwetu, na ahadi ya misaada kutoka kwa wanaume zikionekana kuwa msaada kwetu, hizo zote niliweza kuzimudu na kukusubiri mpaka sasa kwa sababu nilifuata moyo wangu.” Junior akashangazwa sana.
“Kulikuwa na sababu 99 za kukata tamaa, lakini ilibaki sababu 1 tu yenye nguvu iliyonifanya kukusubiria Junior. Sasa lazima na wewe ujiulize bila kuangalia watu na ufungie masikio kelele zote. Ni nini unataka! Ukishajua hilo, itakusaidia kwengineko. Utapita tu. Hutapotea njia maana utakuwa na ramani inayokuongoza kwenye kile kilichopo moyoni mwako. Haitajalishi wakati, muda wala mtu. Ukishajua wapi unaelekea, huwezi simama au kuishia njiani. Utakaza macho mpaka ufike unakotaka. Itakua rahisi, hapana. Kuna kujeruhiwa sana hisia. Wakati mwingine hata mtu wako wakatibu anaweza asikuelewe kabisa. Lakini wewe unajua unapokwenda, na njiani si kituo chako cha mwisho.” Ndio kwa mara ya kwanza anamsikia huyo Emelda.
“Kumbe ndio maana Edwin anayekufahamu anakung’angania hivyo!” “Mimi sijui Junior! Ila nimetuliza macho yangu kwako tu. Ndio maana hata ukiwa unazungumza sebuleni, mimi nipo jikoni, najua kinachoendelea moyoni mwako.” “Haiwezekani Emelda!” “Na sijawahi kukosea. Hata wakikuomba uongoze sifa pale mbele kanisani. Mkawa mpo na Ezra akikusaidia kupiga vyombo. Mkachangamsha kanisa zima kama kawaida yenu mkiongoza sifa. Mama anachezaga sana. Lakini kama kuna kitu hakipo sawa, nikikuona tu hata kwa mbali, jukwaani, najua Junior. Najua.”
“Na huwa nakuja kuthibitisha kutoka kwa mama, Ester, Noah, au hata kwenye mazungumzo yako na Hope. Hata kama utamwitikia Hope kitu anachokutuma, au kukutaka umpe na kumwambia utafanya, huwa najua kama unakwenda kufanya kwa kupenda kwako au unafanya ili usimuudhi. Hata kama utakubali na kutabasamu au kicheko kabisa, nitajua.”
“Na uzuri kwa kuwa wewe hukuwa ukiniona kabisa hata nikiwa karibu yako, nilikuwa nikiweza kuthibitisha mengine, kutoka kwako wewe mwenyewe, unapokuwa na Ezra. Mtazungumza kwa uwazi kabisa, ila kwa mafumbo kama mlivyozoea kwa lugha yenu nyinyi wawili, mkijua mpo peke yenu au hata kama mpo na mtu, mkijua huyo mtu hawaelewi. Lakini pia nilikuja kujifunza lugha yako na Ezra.”
“Mwanzoni iliniwia ngumu kwa sababu maana nzima ya neno mlikuwa mkiweka habari nzima ya kwenye bibilia. Au mtataja mstari wenye bibilia kwa namba tu. Lakini mkimaanisha nusu ya mnachotaka kuzungumza.” Junior alishituka sana. Ni lugha waliyojifunza wao wawili tokea wapo sekondari. Wakaiboresha mpaka na utuuzima huo. Kwa hakika hakutegemea kama mtu anaweza kuwaelewa. Maana jambo la baadaye wanaweza kulizungumza kama lilishatokea. Hutakuta wakimtaja mtu jina. Ila alichokifanya watakibadilisha na kutaja tukio la kwenye bibilia au tukio walilokwisha liona kwenye maisha yao. Ngumu kujua. Wanaweza kukusema ukiwa mbele yao, usijue.
“Haiwezekani Emelda!” “Sikudanganyi. Mkiwa nyinyi wawili mkizungumza, sasa hivi nawaelewa. Na kwa kuunganisha matukio, huwa najua ni nani mnayemzungumzia. Ndipo huwa nathibitisha pia nilichohisi ni sahihi.” Junior aliishiwa nguvu kabisa, na kushangazwa.
“Lakini sikuwa nikikudharau Emelda.” “Ninachotaka kukwambia, ni baada ya kujua ninachota. Moyo na macho yangu nikaelekeza kwako tu, ndio maana nikaweza kukusoma na kukufahamu vizuri bila shida. Watu na kelele havikunifanya niishie njiani. Na nipo hapa nakuahidi kukubali matokeo. Ukiniambia unataka kuishia hapa na mimi, sitajilaumu. Nitajua kumbe hapa ndio kilikuwa kituo changu cha mwisho, kama nilivyokuwa nikisubiria harusi yako. Nilijiambia nitasubiri mpaka uoe. Ukioa, ndio nitakua nimefika mwisho, sina jinsi ingine.” Junior akavuta pumzi kwa nguvu na kuinama akitafakari.
Kisha akamwangalia. “Nikuulize kitu Emelda? Na naomba uwe mkweli kwangu.” Emelda akatulia tu. “Ukinilinganisha na Edwin, huoni kama mimi nimepelea sana?” “Hampo kwenye mashindano Junior!” “Hata kama Emelda, huyu jamaa ameanza kukutunza muda mrefu kiasi ya kwamba mpaka Ester anasema nikikuoa mimi nitakua naoa mke wa mtu!” Emelda akanyamaza.
“Eti Emelda?” “Mimi sitaweza kuusemea moyo wako Junior. Naujua moyo wangu na hapo ndipo nitasimamia. Nyinyi mmefanikiwa kumfahamu tu Edwin kwa sababu yupo karibu ya Ester. Lakini haipo hivyo!” “Kwamba kuna wanaume wengine pale kanisani?!” Wivu. Emelda akacheka taratibu na kunyamaza.
“Nakupenda Emelda. Naogopa kukupoteza.” Emelda akamwangalia na kutulia. “Nimeingiwa hofu ya ajabu! Najihisi kupokonywa mkononi nikiwa hata sijashika vizuri.” “Nilikuwa nikikusubiria wewe, ukiwa huyajui yote haya. Yaani haya uliyoyasikia wewe leo ndio maisha nilikuwa nikiishi nayo kila siku, lakini nilikuwa nikikusubiria wewe Junior! Kama wewe unajihisi bado hujanishikilia vizuri, amini mimi nimekushikilia na hakuna mtu atanitoa kwako ila wewe mwenyewe.” Ilimuingia Junior mpaka akapatwa vipele vya baridi.
“Emelda!” “Nakupenda Junior. Nimekuwa nikimuomba Mungu wakati wote akufungue macho unione japo sikuwa mbali na wewe. Ila nasikitika amekufungua macho na masikio pia. Unasikia kila kitu na kuona kila mtu, isipokuwa mimi.” Akashituka sana. “Nakusikia Emelda! Amini nakusikia.” “Basi sauti yangu inamezwa na kelele nyingine, zenye nguvu kuliko sauti yangu.” “Hapana Emelda! Nakusikia.” Emelda akacheka taratibu na kutulia.
“Nakusikia Emelda!” Akanyamaza akiangalia chini. “Niamini nakusikia.” “Kwa hiyo ni umeshindwa kuniamini?” “Hapana!” “Basi naomba upokee moyoni kwako kile nilichokwambia mimi tokea asubuhi. Mimi nakupenda wewe. Nataka nibaki na wewe. Mimi nitakupenda na kukujali kama zawadi niliyopewa na Mungu na ndivyo nilivyomwambia Mungu. Kama endapo atanipa wewe nita…” Akashindwa kumalizia akainama na kuvua miwani, nakuanza kulia huko alikokuwa ameficha uso.
Junior akapiga magoti mbele yake, mchangani, akamgeuza kichwa upande alipo akapata midomo. Ikaanza kissing. Ilikuwa ya muda mrefu wakutosha. Akamuachia kwa muda. “Nafunga macho na masikio nabakia kwako tu. Nakuahidi Emelda. Maadamu nishathibitisha kutoka kwako mwenyewe, vita ingine nitapigana nikijua nipo na wewe. Na sio kwamba sijui ninachotaka ila nafikiri hukumu inanisumbua. Naona kama nilikupuuza sana. Ni kama sasahivi sikustahili tena!” “Hapo ulipo na mimi nilikuwepo. Nilikuwa na sababu za msingi nikijiona sikustahili, lakini nilisubiri Junior!”
“Nashukuru kunituliza moyo wangu. Asante. Sasa sasahivi wewe kazi yako imeisha. Pumzika ukijiandaa kwa harusi yetu. Mambo mengine ni zamu yangu kupambana nayo.” Emelda alifurahi mpaka akacheka. Alimpa Junior ujasiri na kujiamini kwa aina yake. Hakujali tena baba, Ester, Edwin wala wazee wanaomsaidia Edwin kuomba kwa ajili ya Emelda. Akajiambia ni vita ya siku nyingine. Kissingzikaendelea mpaka simu ilipowatoa wakiwa kwenye huba nzito.
~~~~~~~~~~~~~~~~
INAENDELEA…
0 Comments:
Post a Comment