Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 41 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 41

Akaitoa simu mfukoni. “Ni Mika.” Akaongea akiangalia simu yake akitaka kupokea. “Nakupenda Emelda. Na nakuahidi macho na masikio yangu vitabaki kwako tu na mimi nifikie moyo wako kama ulivyofikia wangu na kuweza kuusoma kwa kiasi kikubwa hivi. Nitakupenda mpaka kusubiri kwako kutaleta maana.” Emelda akacheka na kuinama. Akambusu juu ya kichwa na kurudi kukaa. Simu ilishakatika.

Ukipenda Boga,…

Akapiga tena. “Anakusumbua. Pole. Nitazungumza naye.” “Hata kidogo. Na yeye alikuwa na wasiwasi huohuo, mimi ndiye niliyemwambia muda na wakati wowote anipigie.” Akakata na kumpigia yeye. “Simu bado ina ule muda wa maongezi ulionitumia. Naweza kupiga mimi.” Akawahi Mika, akisikika kujawa kutosheka. “Usijali. Vipi mama?” “Nakushukuru sana. Nimeweza kuwaleta mjini. Wote wameoga, wamekula vizuri, naona mama maumivu yamepungua, hapa anakoroma.” Junior akacheka. 

“Na Mateo anamcheka. Ila tumefurahi! Anasema hajalala hivi kwa muda mrefu.” “Ndio maana amechoka! Poleni sana. Vipi Mateo na yeye anaendeleaje?” “Ni kukohoa tu. Ila nimehisi ni sababu ya kulala kwenye unyevuunyevu na baridi. Nimempa sweta langu, amevaa. Wakilala kwenye mazingira kama haya hata siku mbili tu, atapona. Yeye sina wasiwasi naye sana.”

“Sasa kwa upande wangu huku na mimi naona kwa sehemu kubwa panaendelea vizuri. Nimefanikiwa kupata mazingira ya kuwaweka mpaka watakapopona.” Emelda akashangaa sana. Hakuwa na taarifa. “Bado tu maswala ya ruhusa kazini. Tukifanikiwa kwa haraka tunakuja kuwachukua. Ila nina wazo sijui mtalionaje! Nipo na Emelda hapa. Na yeye anakusikiliza.” Wakasalimiana tena.

“Umemchukulia mama nguo zakutosha?” “Hali haikuwa nzuri. Mama hana nguo kabisa zaidi ya niliyomkuta amevaa. Ilibidi nimnunulie gauni pale duka la Ushirika. Angalau kumtoa kwenye yale mazingira.” Emelda akashangaa sana. “Nguo zote nilizokuwa nikimpelekea zilienda wapi!?” “Anavyosema Mateo eti kuna zilizoharibika kabisa na matope ya mvua. Wakaziokota na kuosha, hazikufaa ila anasema mama alitunza. Ila sasa anasema kuna siku walitoka na mama kwenda dukani, waliporudi wakakuta wameibiwa kila kitu.” Emelda akaumia sana.

“Ila pale palikuwa panavutia kujichukulia kitu chochote unachotaka. Upande uliokuwa umebakia ni kama nje kabisa. Yaani ni ukuta mmoja ulikuwa umebakia wa nje na ndani kuzunguka chumba kile anacholala mama na Mateo, tena nusu. Basi. Paa lote lilikwenda na maji, ikabakia kidogo ndio hapo walipokuwa wakijibanza usiku.” Emelda akanyamaza.

“Ila anakuulizia.” “Nipigie akiamka ili nizungumze naye. Na mnunulie dawa nyingine za maumivu ili maumivu yasirudi tena. Na huyo Mateo sio baridi tu. Amekaa kwenye baridi na unyeuvuunyevu muda mrefu inawezekana kifua kimepata shida. Naomba umnunulie dawa ya kifua na yeye. Mwambie mama namsubiria Junior. Akiruhusiwa kazini tunakuja kumchukua akatibiwe.” “Nilishamwambia.” “Asante Mika. Na pole kwa hekaheka.” “Mimi ndio nakushukuru kuniwezesha. Nilikwama kabisa nikawa sijui chakufanya. Nakushukuru dada yangu. Wote nawashukuru. Yaani hata nikisoma sasahivi nitaelewa aisee!” Wakacheka.

“Nilikuwa na hali mbaya! Hata nikipiga magoti kuomba nilikuwa nashindwa chakumwambia Mungu. Naishia kulia tu. Lakini sasahivi nikimwangalia hivi mama, ameoga maji masafi! Niliwanunulia chakula kingi. Amekula, ameshiba. Halafu akanywa na soda ya baridiii!” Ikabidi tu wacheke akisikika kweli huyo Mika amefurahi. “Sasahivi nina raha. Nahisi hakuna nitakachosoma nisielewe tena. Nawashukuruni sana.” “Karibu Mika.” Akajibu Junior.

“Lile wazo lako?” Emelda akamkumbusha alidhani wamesahau. “Ilikuwa juu ya shule ya Mateo. Nilikuahidi Mika kuwa Mateo atasoma. Sasa najua anakuja huku na hatujui matibabu ya mama yatachukua muda gani. Ni sawa akiwa anamsubiria mama awe anaendelea na shule?” Pakazuka ukimya hapo. Hao ndugu wawili wote wakapatwa ububu.

“Emelda?” “Kwangu ungekuwa muujiza, Junior! Lakini ni wapi huko utawaweka wawe sawa na mgonjwa pamoja na mtoto anayetakiwa shule!?” “Nyumbani.” Emelda akabaki amemkodolea macho. “Nimeshazungumza na mama. Yeye mwenyewe ametaka wafikie nyumbani na si kwingineko. Ile nyumba ni kubwa Emelda, na unajua kuna vyumba vitupu kabisa, havitumiki mpaka tupate wageni. Mama amewakaribisha kwa moyo wake wote.” Emelda akanyamaza.

“Usiwe na wasiwasi.” “Hautakuwa mzigo mzito sana? Sitaki walemewe.” “Hata kidogo. Maadamu mama mwenyewe amekubali, usiwe na wasiwasi. Turudi kwenye swala la shule. Mika unasemaje?” “Naona mimi nipo kama Emelda. Kwetu utakua muujiza. Muulize huyo Emelda maombi tuliyokuwa tukiomba.” Akaendelea Mika.

“Ungetusikia ungeweza sema tumechanganyikiwa. Tulikuwa tukiomba vitu havilingani kabisa na sisi. Kwa hiyo chochote kile Mungu atakachotupa, sisi tunapokea kwa shukurani kubwa sana. Na nakuahidi huku nyuma nitaendelea kuweka mazingira ya nyumba yakufaa kuishi tena. Ili mama akipatiwa tu matibabu, basi arudi hata kama atajiuguzia huku itakuwa sawa, ili asilemee huko. Mimi mwenyewe nitakuwa likizo, akirudi huku nitamsaidia mpaka apone kabisa ili Emelda aendelee na kazi huko.” Kaka mtu hakujua ameshapata shemeji. Habari imeshabadilika. Emelda amepata jina jipya.

“Tutazungumza hayo tukifikia hapo. Sasahivi ni mama afikishwe hospitalini. Na Mateo asome. Kwa hiyo jitahidi katikati ya siku za shule urudi shuleni kwao umuombee matokeo yake.” “Ninayo.”Akajibu Mika kwa haraka sana mpaka akamshangaza Junior. “Natunza ripoti zake zote tokea yupo darasa la kwanza. Ninazo mpaka na za Emelda. Natunza. Sijatupa. Naamini Mungu siku moja Emelda na yeye atarudi tu shule. Hataishia hapo. Anaakili sana. Alikuwa akifanya vizuri sana shuleni.” Emelda kimya wakati Junior amepatwa ububu.

“Ukija nitakukabidhi za Mateo. Na yeye ana ripoti nzuri sana. Utaona. Sio kwamba nawasifia tu ndugu zangu! Na yeye anajitahidi shuleni.” Junior akacheka. “Unafanya vizuri sana Mika. Hiyo itasaidia. Na pia nitaulizia kama kuna kitu kingine kitahitajika ili kusaidia ahame shule kiurahisi ili ufuatilie.” “Sawa. Asante sana. Nakushukuru.” Alijawa shukurani huyo Mika, kama dada yake. “Usiache kunipigia simu mama akiamka.” “Nitafanya hivyo.” Ndipo wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akamwangalia akamkuta ameinama kama anayefikiria kitu. “Unawaza nini?” akamwangalia. “Niambie.” “Nilitamanai kuzungumza na dada Ester kesho akija kanisani. Sijapenda alivyokuwa akinipokelea hongo. Si sawa kwangu wala kwa Edwin! Tena nikiwa nilimjibu waziwazi kuwa simtaki! Si sawa, Junior. Aliweka matumaini yasiyo kweli kwa Edwin na nafikiri ndio maana Edwin alibakia akinisubiria, wakati alitakiwa aendelee na maisha yake. Hakunifanyia vizuri. Maana ni kweli inamaana nimemgarimu sana huyo Edwin bila ya mimi kujua!” Wivu kwa Junior.

“Ukisema ‘sana’ unamanisha nini?” “Yaani sasahivi nikifikiria ndio nazidi kuumia na kujisikia vibaya muda niliokuwa nakuwa naye karibu huyo Edwin nikimchukulia kama kaka wakati tukitumika, kumbe ananitunza! Inaniuma sana. Sio sawa Junior. Nilikwambia kuna kipindi kilifika sikuwa na matumizi kabisa na pesa yote nikawa nikimtumia Mika maana dada Ester alikuwa akinipa kila kitu?” Junior akanyamaza akikumbuka vile Ester alivyosema mpaka vitu vya kike vya mwezini alikuwa akipewa na Edwin. Ikamkera kupitiliza.

“Yaani kila kitu mpaka lotion, sabuni nzuri za kuogea, miswaki hii ya maana! Nguo za ndani zile za garama na sidiria zake mpaka nikawa namshangaa dada Ester upendo huo ni kama umepitiliza! Ila nikajua ni kwa sababu umemuunganishia kazi Devin huko mnakofanya kazi nyinyi na kaka Ezra, na mama naye alikuwa na furaha kuwa maisha yao yamewabadilikia, sasahivi wanapesa sana na anajua kumtunza sana dada Ester. Basi mimi nikawa nikipokea nikijua vinatoka kwake yeye mwenyewe dada Ester! Ila kwa vile yeye alivyo na ninavyomjua kwangu, hakika kuna wakati mwingine nilikuwa nikimtilia mashaka na vitu alivyokuwa akinipa. Ila sikujua jinsi ya kumuuliza. Kumbe nilikuwa sahihi.”

“Ila kwa upande wa nguo ndio mara chache sana kunipa mpya. Mara zote alikuwa akinipa zake, nakwenda kupunguza na kuvaa. Sasa kuja kujua ni yeye Edwin! Hakika sijapenda Junior. Sijapenda kabisa, lakini basi.” Junior akamwangalia.

“Basi kwa nini!?” “Sasa hivi nataka amani ili mama yangu atibiwe. Tatizo la mama ni zaidi ya hisia zangu zilizojeruhiwa. Kwa jinsi sasahivi ilivyo, inamaana ni kama nimekua msaliti kwake dada Ester na Edwin ambaye sijui kama alipewa jibu la kweli kutoka kwangu na dada Ester. Nitakapomuuliza dada Ester na kumtibua kwa namna yeyote ile ujue nitakuwa nimemgusa moja kwa mojamchungaji/baba yenu, ambaye hataki Ester hata atoe chozi! Na mama pamoja na Mateo ndio hao wataishi pale wakisaidiwa matibabu. Huoni nikianzisha jambo sasahivi nitaharibu hata majibu ya maombi yetu? Inamaana itamgusa mama moja kwa moja, Mika na Mateo pia. Nitaacha tu.” Wakatulia wakitafakari.

“Ila naona wazo lako la kuzungumza na Edwin sio baya. Itabidi nitafute mazingira mazuri ya kuzungumza naye.” Hapo akamshitua Junior. “Kwamba utafute muda na sehemu ya kuzungumza na Edwin?! Aliyekuwa akikutunza kwa garama yote hiyo! Ana watu wakumuombea akuoe! Na mchungaji wake yupo upande wake! Mkakae nyinyi wawili mzungumzie jinsi alivyokuwa akikutunza na yeye akuelezee kwa ufasaha jinsi anavyokupenda!?” Mpaka hapo Emelda akawa amekwama. Akanyamaza.

“Wewe unataka kunichanganya Emelda!” Akasimama kabisa. “Lakini ndivyo ulivyonishauri wewe mwenyewe Junior!” “Kabla sijajua hila za hongo zake kwako! Huyu mtu yupo kwenye maisha yako kwa karibu sana kuliko mimi! Anakufahamu kwa karibu kuliko mimi mwenyewe. Inamaana najua mpaka size za nguo zako, tena mpaka za ndani, wakati mimi mwenyewe sijui, Emelda!” “Labda ni dada Ester ndiye aliyekuwa akienda kununua, yeye anampa tu pesa. Hajui.” “Unajuaje?” “Nahisi.” Kisha akakumbuka. Akawaza kwa sauti. “Ila anasemaga anapenda sana shopping.” Hapo alimtibua Junior akabaki akimwangalia.

“Ni katika mazungumzo yake.” “Nyinyi mnakuwa mnafundisha watoto pale kanisani au mpo date?!” “Sio hivyo! Ukumbuke huwa inabidi kuwahi ili kupokea watoto na tubakie wa mwisho mpaka kila mzazi aje achukue mtoto wake. Halafu kunabakia kusafisha mle ndani na kupaacha pazuri. Ndio huwa anapita kila darasa kusaidia.” “Kila darasa au anaishia kwenye darasa lako wewe anayekutumia neno la Mungu kila siku asubuhi na kukujulia hali?” Emelda akafikiria kwa haraka akasimama pale alipokuwa amekaa, Junior amesimama. Wivu mpaka kwenye kope.

Akamshika mikono yote miwili. “Mimi nina wazo Junior. Leo ndio siku yetu ya kwanza mimi na wewe kutoka, pamoja na kina Jelini. Tutulie na kufurahia siku ya leo wakati tukifikiria pamoja kitu cha kufanya juu ya hili. Au unasemaje?” Kimya akianza kutulia. “Mimi napenda kukuona unafuraha Junior! Sitaki mimi ndio niwe chanzo cha kukunyima raha. Itakuwa haina maana tena ya mimi kuwepo.” “Sio wewe. Wewe walikuwa wakikuzunguka tu. Hata mimi Ester ameniumiza.” Akajirudi kwa haraka.

Akamuachia mikono na kumkumbatia kiunoni. Emelda akajisogeza karibu. “Nakupenda Emelda. Sitaki kukupoteza.” “Huwezi nipoteza. Nakuhakikishia Junior.” “Basi sitaki kuingiliwa kwenye maisha yako.” “Sasa kwa kuwa tumeshajua ukweli. Kuanzia sasa, sisi tunaendelea na yetu na mimi nitaishi kwa akili. Au unasemaje?” 

“Nakupenda Emelda.” “Namimi nakupenda. Usiwe na wasiwasi na Edwin.” “Hapo siwezikuepuka.” “Basi usiwe na wasiwasi na mimi. Wewe niangalie mimi tu, acha kuweka macho yako na masikio kwengine, itakusaidia. Au na mimi imeshakuwa ngumu kuniamini?” “Wewe nakuamini.” “Basi tutulie.” Simu ya Junior ikaanza kuita.

 ~~~~~~~~~~~~~~~

Akaitoa tena mfukoni. “Ezra huyu! Atakuwa akitutafuta.” Akapokea. “Chakula.” “Tunakuja.”Wakaanza safari ya kurudi hotelini. Ila wote wakionekana wametulia sio kama walivyotoka hapo.

Wote waliagiza chakula kila mtu akapata alichopenda wakaanza kula. Mara ujumbe ukaingia kwenye simu ya Emelda. Akatoa simu mfukoni ikisindikizwa na macho ya Junior. Alikuwa Edwin. Akasoma mpaka akamaliza na kuirudisha kwenye mkoba wake bila ya kujibu akijua majibu yoyote yale si kwa Junior tu hata Edwin mwenyewe yalibeba maana nyingi. Akaona atulie tu. Kimya. Akaendelea kula kumbe Junior roho inamtanga anataka kujua mtuma ujumbe.

Jeremy alikuwa akila taratibu kama ambaye alishachoka. Na muda wa kuja kuchukuliwa ulishakuwa umekaribia. Mama yake alishamtoa majini. Ezra akampeleka upande wa kiume kuoga. Akamsadia na kubadili nguo. Hapo alikuwa tayari kuja kuchukuliwa. “Malizia chakula au nimwambie akufungie?” Jelini akamuuliza. Ila Ezra akaona sio wazo baya kufungiwa.

Wakamuita muhudumu na kuomba chakula kingine na cha mama Jema akijua Jelini angefanya hivyo. Jelini akashukuru. Wakaendelea kula muhudumu akiwa amendoka. Kimya kimya tu, Junior akili na mawazo yapo kwenye ujumbe ulioingia kwenye simu ya Emelda.

Mara ujumbe mwingine ukaingia tena kwenye simu ya Emelda. Akatoa tena simu yake na kuanza kusoma. Ila huu wa safari hii ukaonekana mrefu sana. Akasoma kwa muda. Ila safari hii Junior akagundua anabadilika sura sio kama ujumbe wa mwanzoni. Wakati akiendelea kusoma muhudumu akarudi na chakula kilichofungwa vizuri na simu ya Jelini nayo ikawa ikiita. Mama Jema amefika, anamtaka Jeremy. 

“Haya aga twende, bibi amefika.” “Asante anko Ezra kunisaidia bafuni, kuoga, na kuvaa. Halafu kuniangalia kuogelea nisizame, halafu nini tena?” Akawa anacheka akimwangalia mama yake amkumbushe kitu cha kushukuru. Jelini akaangalia mezani. Akakumbuka akicheka. Wote wakacheka. Alikuwa mzuri huyo mtoto, ungependa kumuangalia. “Halafu tena asante kwa chakula kizuri, juisi, halafu saa ile ukaniletea na maji ulisema jua kali sana, ninywe maji ya kunywa wakati nikiogelea. Sasahivi sijasahau kitu.” Maneno mengi kama mama yake! Wakacheka. “Karibu Jeremy. Wewe ni mtoto mzuri, unashukurani na heshima.” Akacheka kama mama yake.

“Bye anko Junior na anti Emelda.” Wakacheka. Wakimwangalia mtoto wa bibi. Wakamuaga. “Acha nikusaidie kubeba vyakula na pia nikamsalimie mama na kumshukuru kutupa Jeremy.” Wote wakaona sio wazo baya kwenda kusalimia. Akawashukuru sana kumsaidia Jelini.

 “Na kama isingekuwa nyinyi, leo angechemka huyu. Alipata bahati ya kazi nyingi, akazikubali huku hajui atajigawaje. Lakini mmemuokoa. Nawashukuru sana. Asanteni.” Wote watatu, Ezra, Junior na Emelda wakaitika. Hawakukaa sana hao wawili wakaondoka na kuwaacha Ezra, Jelini na Jeremy hapo na mama Jema.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Nashukuru kwa kutuamini na Jeremy.” Akachomekea Ezra kwa mama Jema. Akacheka akifikiria kidogo. Kisha akaona aseme tu. “Wewe unaonekana unajielewa na unajua unachokifanya. Unasimama na anachokiamini Jelini na kumsaidia kukifanya hata kama kinaonekana kipo chini ya wadhifa wako au kitu duni.” “Jelini hafanyi kitu duni mama yangu. Anajitahidi sana.” Ezra akamsifia.

“Sasa ndio hayo ninayoyasemea mimi. Sio wote wanaona hivyo! Wewe umeona na kumtia moyo ukithamini juhudi zake. Na ndio maana hata wenzio kina Junior wanamthamini na kusimama naye pia. Sio wote wanafanya hivyo Ezra! Si Jelini ni mwanangu na nimeona wengine waliotangulia kwenye maisha yake jinsi walivyoishi naye!”

“Wewe umesimama naye, unamsifia, unamtia moyo, ukamfanya na yeye atulie. Ukisema jambo, unatekeleza. Sio mbabaishaji tu. Maneno maneno mengi yasiyo na vitendo! Ndio maana sina wasiwasiukiwa na Jeremy. Najua yupo na mtu wa kuaminikaanayejielewa. Inamaana na yeye ataona na kujifunza maisha yanayofaa kuishi. Sitaki awe kama hawa wahuni wa hapa mjini. Na sitaki mtu amchanganye.” Akamwangalia Jelini. 

“Sasa mimi hapa nimefanyaje? Si umesema saa 12:30 awe ameshakula na yupo tayari? Sasa hapa tokea unipigie simu kuwa umefika na kumtoa hapa kwani imechukua muda gani?” “Sitaki ayumbishwe huyu.” “Hata yumba mama yangu. Nakuahidi. Jeremy ni mtoto mzuri sana. Na anaonekana mmemlea vizuri.” Akaingilia Ezra. “Sasa sitaki hapo katikati achanganywe kama alivyochanganywa hapo nyuma. Sitaki ajifunze kwa wababaishaji wanaosogezwa karibu yake. Sitaki na katika hilo sitayumba.” Jelini akanyamaza akijua bado ni Colins tu.

“Mwishoe ataanza kujua tabia fulani ni sawa kuziishi kumbe sio sawa. Lakini wewe na James nimeona mnajielewa. Sina shida na nyinyi. Ila sasahivi lazima arudi nyumbani. Sitaki akazunguke huko kwenye makumbi na Jelini. Atakutana na waliofurahia sherehe, wamelewa. Wakianza fujo hawatambui cha mtoto wala mtu mzima. Bora yeye akatulie nyumbani.” “Nashukuru mama yangu hata kwa muda mzuri tuliokuwa naye leo. Naamini amefurahia. Eti Jeremy?” “Nimefurahia. Siku nyingine tena si na mimi nitakuja tena?” “Tutapanga na bibi, halafu tutakwambia.” Jelini akajua amempenda Ezra ndio maana anataka kutoka naye tena. Ila kwa kuwa alikuwa ameshanuna akanyamaza.

“Sasa umekasirika nini?” Mama yake akamuuliza. “Mimi hapa nimetulia lakini sasahivi wewe huoni tena! Kwani mimi nimemyumbisha Jeremy?” “Jelini!?” Kama mama yake anayemuuliza unataka nikuhesabie? Akamuelewa. “Lakini sasahivi si nimetulia!?” “Si kwa sababu upo na Ezra ambaye anajielewa? Kila mtu ametulia sasahivi sababu kichwa chako kimetulia.” “Sasa hapo ingekuwa mama mwingine anayempenda mtoto wake angemsifia kwamba mtu amebadilika, ndio ametulia. Lakini wewe huoni!” “Ndio utulie. Na hapo uliposimama usiyumbe.” “Mimi siyumbi tena. Sasa kwa nini hunisifii hata kidogo?” Ezra akabaki hajui chakufanya.

Mchumba analalamika, yeye amesifiwa. Hajamzoea mama Jema, hataki kumuudhi, hajui aingilie vipi hayo mazungumzo. “Mimi kila ninachofanya kinaonekana bado!” Akaendelea kulalamika. “Mimi simyumbishi Jeremy tena. Na nimeshasema natulia lakini bado! Mimi hapa sipendwi. Nakua mtoto mbaya kila siku! Sisifiwi hata nikifanya kitu kizuri.” Akaanza kulia.

“Mbona unafanya vitu vizuri sana, mama yangu mzazi? Shida yangu Jeremy.” “Sasa tokea Colins, kwani mimi nimempeleka wapi huyo Jeremy kama sio kwa Ezra tu na Jeremy mwenyewe amempenda kama wewe! Mimi najua tu hunipendi.” “Basi mama yangu mzazi. Kwanza leo umeingiza pesa nyingi. Najivunia kweli! Hata Jema nimemringishia. Nikamwambia mama mzazi leo ame..” Sitaki sifa hiyo.”Akakataa na mabega kabisa na machozi mpaka kidevuni.

Ezra akamshika. “Mimi hapa ni mama mzuri. Nimebadilika. Na nimetulia.” “Usilie.” Ezra akamtuliza kwa kumshika kabisa. “Basi nipe muda kuthibitisha hayo. Tulia hapo ulipo mpaka na kwenye ndoa. Hakuna kuyumba uone mimi kama sitakuwa na imani na wewe. Kwengine kote unafanya vizuri mama yangu mzazi. Unasimamia jambo mpaka unakamilisha. Tena unakamilisha vizuri sana. Umeachana na marafiki wabaya. Unakwenda kanisani. Unasimamia biashara vizuri. Leo viti vyako vyote vimetoka. Unajitahidi mama yangu mzazi. Hapo nakusifu.” Wakati huku Jelini akiendelea na mama yake, Junior akapata mwanya.

~~~~~~~~~~~~~~~

Waliporudi walipokuwa wamekaa. Akamuomba simu yake. Emelda akasita. “Ni nini unachokataa nisione?” “Mama anaweza kunipigia muda wowote kuanzia sasa.” “Akipiga nitakurudishia simu yako, usiwe na wasiwasi.” Akawa amekwama. Akamkabidhi. “Chukua simu yangu uwapigie kina Mika kujua wanaendeleaje.” Akajua anamfanyia kusudi kama kumwambia yeye hana chakuficha. Emelda akapokea na kubaki ametulia.

Moja kwa moja akaenda kwenye jumbe. Ujumbe wa juu kabisa au wa mwisho kuingia kwenye simu ya Emelda akaona unatoka kwa Ester. Akashituka ila akaufungua na kuanza kusoma. 

‘Ulipokuja kwetu, tulikupokea kwa mikono miwili. Tukakufanya kama mmoja wa familia. Kumbe wewe ni nyoka katikati yetu ukitambaa polepole mtu asisikie sauti yako kila unapotaka kufikia. Nilipogundua hila zako za usaliti, nilikuonya Emelda. Umekataa kunisikiliza. Umemwaga sumu katikati ya familia uliyokuta imejaa amani na upendo. Tukiheshimiana na kubebana katika kila jambo. Umeweka ufitini. Kwa mara ya kwanza familia yetu imegawanyika kwa sababu yako.’

‘Kwa mara ya kwanza tokea nazaliwa, leo namuona baba na mama wakipishana, wewe ukiwa umesababisha. Mama ananigomba mimi, na kuwa kinyume yangu kwa sababu yako! Ndoa iliyokuwa inakaribia kufungwa kati ya Hope na Junior, umefanikiwa kuivunja bila hata hofu!’

‘Umesambaza uongo huko kwa kaka zangu, sasahivi wote wananichukia mimi na kuniona mimi ni mbaya. Unamkataa Edwin ukitoa sababu za uongo kumbe ulishapiga mahesabu kujua nani mwenye nazo zaidi ambaye utanufaika naye, ukagundua Junior anauwezo mkubwa kifedha kuliko Edwin, ndio ukamchagua yeye kumlisha mavitu ya kichawi kutoka kwenu mpaka ukafanikiwa kumuharibu akili. Anamuacha mwanamke mzuri kwa ajili ya kumfunga akili.’ Junior alikuwa akitetemeka mpaka Emelda alimuona mikono ikitetemeka na kuzidi kumtia hofu akijua Ester amemmaliza kwa hakika.

Akamwangalia Emelda. “Mwee! Kisicho ridhiki kweli hakiliki! Kweli huu ndio mwisho!”Akawaza Emelda na yeye akitetemeka mpaka tumbo likaanza kunguruma. “Junior atajua kweli nilikuwa nikimlisha mauchawi. Mungu unitetee.” Akajisalimisha kwa Mungu akiwa amejawa hofu ya ajabu. Hakutaka Junior asome huo ujumbe.

Junior akaendelea kusoma. ‘Tulikuwa tukikupa ruhusa kwenda kwenu kusalimia, kumbe tulikuwa tukikupa nafasi kwenda kuchukua mauganga ya kwenu ili uje umuharibu akili Junior! Tukakuachia uwe unampikia tukidhani ni upendo, kumbe ulikuwa mwanya wa kumlisha madudu yako akukubali wewe!’

‘Emelda, Mungu anakuona. Na sitatulia mpaka mbingu zimtetee Junior. Akombolewe kutoka kwenye mauchawi yako. Awe huru na kila kifungo ulichomfunga. Aoe mwanamke aliyekusudiwa na Mungu. Na kila baya ulilotupia familia yetu, nakurudishia wewe mwenyewe. Umeshindwa.’ Junior akamaliza kusoma na kuvuta pumzi kwa nguvu.

~~~~~~~~~~~~~~~

PALE MUNGU ANAPOJIBU MAOMBI ULIYOSUBIRI KWA MUDA MREFU, KISHA KULETEWA YAKIWA NA MAJARIBU NDANI YAKE.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment