Hali ilipokuwa mbaya sana, akamuachia na kumlaza ubavuni kwake akimtoa mwilini mwake, ila kichwa akamvutia kifuani. Akamchungulia. Emelda akajificha kifuani. Akacheka taratibu. “Asante kunisubiri Emelda. Ningesikitika kuja kurudi na kukuelewa, halafu nikawa nimechelewa.” “Kwamba ningekuwa nimepata mtu mwingine?!” Akamuuliza taratibu ila kwa mshangao wa aibu.
“Ndiyo. Inawezekana kabisa.” “Nisingeweza.” Junior hakutegemea, mpaka akamgeukia vizuri kwa kulala ubavu. “Sasa ungenisubiri mpaka lini Emelda!? Hivi unajua nilikuwa nikikaribia kumuoa Hope?!” “Najua.” Akaanza kulia. “Lakini nilikuwa nikimuomba sana Mungu. Bila kuchoka. Wakati mwingine kila nilipokuwa nakuona huna raha, na muda wa kufungua umefika, nilikuwa nashindwa kabisa kula, naona niendelee tu kuomba. Hata siku tatu nakaa bila kula.” Kwakwe Junior zilikuwa habari za kumshangaza sana!
Hakujua kama kuna mtu anaweza mfanyia hivyo! Kwanza hakutegemea mtu kufuatilia hisia zake hivyo kwa karibu! Alijitahidi kuzificha na kuwa mstari wa mbele kwenye kila kitu anachohitajika, akitaka jambo lisiharibike. Na Hope wakati wote wimawima na mipango yakutelekeza kwa haraka. Sasa kuja kusikia hayo kutoka kwa Emelda, akashangazwa haswa.
“Pole na nakushukuru Emelda. Hakika sikuwa hata nikihisi! Kweli hukukata tamaa kabisa!?”“Kuna kipindi nilikata tamaa. Ila nikaja kujiambia nitakusubiri mpaka uoe kabisa ndipo nitajua haikuwa bahati yangu.” Junior akamfuta machozi na kuanza kumkiss tena. Ila safari hii taratibu.
Kisha akamuachia kama aliyekumbuka au aliyepitwa na ujumbe. “Kwa hiyo wewe unaona kuwa na mimi ni bahati!?” Akajificha akicheka. “Niambie Emelda!” “Mimi naona kama hakuna anayeweza kukaa vizuri na wewe kama mimi mwenyewe.” Junior alicheka sana. Emelda akajificha kabisa chini ya ubavu.
“Hawakuwezei, wanakunyima raha bila sababu! Mimi naumia bwana!” Akamsikia akiongea huko alikokuwa amejificha. “Hawawezi kukupenda kama mimi mwenyewe.” Junior hakutegemea. Emelda amefunguka kama aliyekuwa akisubiria hiyo nafasi ya kujieleza. Moyo ulijawa furaha, akaibariki hiyo siku na kumshukuru Mungu wake kwa kumtunzia huyo binti.
“Mimi nakupenda.” Akaongeza taratibu. “Hujui ni kiasi gani nafarijika kusikia hivyo. Asante kwa kunipenda kwa dhati Emelda.” Akanyamaza.
“Niangalie nikwambie kitu.” Akajitoa hapo alipokuwa amejificha na kujiweka sawa. “Sasa hivi nimeamua kutulia na wewe tu. Na ukikubali, tunafunga ndoa. Tunabakia sisi wenyewe wawili.” “Kweli unioe mimi!?” “Nakutaka wewe Emelda. Sitapata mtu atakayenipenda na kunijali kama wewe. Na mimi nimeahidi kubadilika. Kuanzia sasahivi nitakuwa nikikusikia.” “Umeshaanza kunisikia. Sikutegemea ulivyokumbuka swala la kuvutwa wakati nikisukwa. Nilifurahi! Sikuwa naamini. Nikala na chokuleti. Nikasahau dawa kwa furaha, mpaka uliponipigia kunikumbusha. Nilikuwa siumwi tena.” Junior alicheka sana. Na jinsi alivyosema chokuleti akazidi kucheka.
“Sikutegemea! Nikaona umenijali.” “Na nakuahidi kuendelea kukujali na kukupenda Emelda. Sitataka nikuoe unitumikie, ila tushiriki pamoja mapenzi yetu. Kitu kikiwa hakijakaa sawa, wewe niambie. Usikinyamazie ili tukirekebishe kwa haraka tuendelee kuishi kwa amani. Sawa?” “Nikuulize kitu, kaka?” “Juu ya nini? Na uache kuniita kaka.” Emelda alicheka sana.
“Nishazoea.” “Niulize.” “Unafikiri wazazi wako watakubali kweli? Maana mimi sio kama wifi…” “Tafadhali usimtaje kwa leo. Na usimtambue tena kama wifi yako, maana sio.” Hapo akamuona amebadilika. Emelda akamwangalia, akajua ndiye aliyemuudhi.
“Na swala la wazazi usiogope. Nishazungumza nao.” Emelda alishituka mpaka akakaa. “Kwa hiyo mama anajua!?” “Ndiyo.” Akamuona kama anayevuta kumbukumbu. “Nini?” “Ujue yeye ndiye aliyeniambia nianze kujitayarisha nije huku? Kwa hiyo nilivyo andaa kifungua kinywa kwa wote nikaingia kuoga nikavaa. Akanifuata chumbani, akaniambia hajapenda nguo niliyokuwa nimevaa. Akanichagulia hili gauni na kunisaidia kutengeneza nywele!” Junior akafurahi sana.
“Si umeona tuna mbaraka za wazazi?” “Mchungaji je!?” “Usiwe na wasiwasi naye. Tumfikirie mama yako kwanza. Nilikuahidi tutamtumia pesa. Naomba tufanye hivyo kabla siku haijawa na mambo mengi. Halafu tutajipanga twende pamoja na Ezra.” Alifurahi Emelda lakini akamuona kama aliyekumbuka kitu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona umebadilika tena?” “Kwetu mafukara kaka. Nitawaweka wapi?” Junior akatulia. “Aina ya nyumba uliyonayo wewe kichwani sipo kwetu. Hakuna mazingira mazuri na nimeshindwa kubadilisha kwa sababu pesa ninazowatumia zote zinakuwa zikisubiriwa kila mwezi. Yaani kabla mimi sijapokea mshahara huku, ujue mimi na Mika tushapigia mahesabu mpaka mshahara ujao, na hautoshi.” “Nipe muda nifikirie. Lakini usiwe na wasiwasi juu yangu na Ezra. Kama hakuna vyumba, sisi tunaweza lala hata kwenye gari ilimradi tu tufike nyumbani. Ila tutume pesa kwanza?” Akajua bado hajamuelewa kabisa hali ya kwao, akaona amuache tu.
“Zinamfikiaje?” “Huwa namtumia Mika ndio ana simu. Tena hiyo simu alinipa Noah, nikampelekea yeye Mika. Akipata pesa, anaondoka shule, anafanya manunuzi yanayohitajika nyumbani na nyingine anampelekea mama na hivyo vitu.” “Yeye mama hana simu?” “Hana simu na wala hakuna mazingira ya kuwa na simu pale.” Junior akawa hajaelewa. “Atachaji wapi?” “Kweli. Basi mtumie Mika.” “Asante kaka.” “Acha kuniita hivyo bwana!” Emelda akacheka na kujifunika na mto.
“Sasa watasema nimeoa dada yangu!” Emelda alicheka sana mpaka dimpozi zikaonekana. “Emelda wewe ni mzuri!” Hapo ndio akajificha kabisa. “Unapendeza sana ukicheka.” Akabaki amejificha. “Tuma hela kwa mama, bwana.” Akatoka hapo kochini maana walikuwa kama wamejilaza, yeye amelala ubavuni mwa kochi. Akamruka na kufuata pochi.
Wakati anatoa simu, akashangaa pesa zinaanza kuingia. Maana alijua atumie zake tu, atakuja kumpa baadaye. Akamwangalia Junior kwa mshangao baada ya kuona hiyo pesa aliyomtumia. “Ndio nimtumie zote hizi!?” “Kwa sasa fanya hivyo wakati tukijipanga.” Akahisi kuishiwa nguvu, akakaa kochi la karibu taratibu na kurudisha macho kwenye simu yake. Hakuwahi kushika pesa nyingi hivyo.
“Naomba nizungumze kwanza na Mika. Anaweza akashituka sana.” “Unataka nikupishe?” “Acha mimi ndio nitoke.” Akanyanyuka pale kochini. “Hata hivyo acha nimwangalie Ezra. Wewe endelea tu. Naenda kumpigia simu nijue alipofikia.” Akaondoka kabisa hapo na kumuacha Emelda haamini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda akarudi na kumkuta amejiinamia kama ambaye amepotea kabisa pale, simu ameshikilia mkononi, kama ambaye hajui chakufanya tena. Akasimama kwa muda akimwangalia wala asijue kama yupo pale. Akajua kuna kitu hakipo sawa. Hajapata taarifa nzuri.
“Kwema?” Akasimama kwa haraka kama ambaye amefumaniwa. “Kuna nini?” “Hamna kitu. Kaka Ezra anahitaji msaada?” “Tumalize moja baada ya jingine kwanza. Vipi nyumbani?” “Salama.” Jinsi alivyojibu akaamini kuna kitu hakipo sawa ila hataki kumwambia.
“Umezungumza na Mika?” “Ndiyo.” “Amekupa hali ya nyumbani?” “Ndiyo.” “Mbona kama humalizi kuniambia kinachoendelea!?” “Ameshukuru kwa pesa.” “Naweza kuzungumza naye?” “Mika!?” Akauliza kwa mshangao mkubwa.
“Si ndiye mwenye habari za nyumbani aliko mama na Mateo?” Akamuona anapoa ila akaitika. “Ndiyo.” “Kama unaona sawa, naomba unitambulishe kwake na mimi niweze kuwasiliana naye. Au unaona haupo tayari kunitambulisha kwake?” “Hapana.” “Naona kama itasaidia mawasiliano kati yetu. Isiwe lazima kuwasiliana naye kupitia wewe tu.” Akamuona kama anasita.
“Kuna nini? Mbona kama unasita?” “Au muwasiliane wakati mwingine?” “Na kwa nini isiwe leo!?” “Hana habari njema. Ndio naona labda tusubiri kwanza.” “Kwamba mpaka kuwe na habari njema ndio unitambulishe kwake!?” Akamuona amefikiria mpaka huko kichwani kwake kumeafikiana. Akampigia.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Mika?” Akajua kule ameitika. “Junior anataka kuzungumza na wewe.” Sasa akashangaa sio kama anamtambulisha kwa mara ya kwanza ni kama Mika anamfahamu yeye. Akashangazwa ila akapokea simu.
“Hujambo Mika?” “Shikamoo.” Akamsikia akimsalimia kwa heshima kubwa, akajua anamfahamu mpaka umri. “Marahaba. Vipi huko, mnaendeleaje?” Emelda kimya amerudi kukaa amejiinamia. “Ndio nilikuwa nikimwambia Emelda. Hali sio nzuri. Alinituma kwenda kumwambia mama hatakuja tena kama alivyopanga. Akanipa na pesa ilikuwa ikihitajika. Nilipoenda kwa mama, nilikuta upande mmoja wa nyumba umechukuliwa na mvua, maji yanaingia mpaka anakolala na Mateo. Godoro wanalolalia limeloa kabisa kama limeoza tayari. Na ni godoro jipya Emelda alituma hela nikawanunulia maana walikuwa wakilala…” Akamsikia amesita.
“Haikuwa nzuri. Kwa kuangalia lile godoro nikajua inamaana wamelala pale kwa muda mrefu, sisi hatujui. Nilikuwa nimebanwa na mambo ya shule, tokea nilipowapelekea matumizi mwisho wa mwezi uliopita alipotuma pesa Emelda, nilipanga nirudi nikimaliza mitihani. Kwa hiyo sikuwaona zaidi ya mwezi.”
“Nikawahamishia jikoni. Sasa kwa kuwa pesa ilikuwa ndogo, nisingeweza kutafuta mjenzi. Ikabidi nibaki mwenyewe kutafuta udongo mzuri wa kujengea na fito. Imenichukua siku nzima ya jana na leo mpaka saa nne asubuhi kuziba upande waliokuwa wanalala. Ila sio pote. Pesa haikutoshea fito na yakuwaachia ya chakula. Udongo ilinilazimu kwenda kuchimba mwenyewe, mbali kidogo na pale. Na pia muda haukutosha.” “Poleni sana.” Junior akajikuta anaumia.
“Asante. Lakini nimepata matatizo shuleni. Muda ule niliokuwa nyumbani, nilitoroka shule, imejulikana. Huwa natoroka asubuhi siku za jumamosi, nakwenda kumuona mama na Mateo, jioni nakuwa nimerudi shule. Sasa nilishindwa kuwaacha vile wanalala kwenye matope. Kuja kumaliza ujenzi mpaka kufika shuleni ikawa saa 6 mchana wa leo. Kumbe mwalimu wa nidhamu aliitisha rokoo mida ya saa 4 asubuhi. Ndio ikajulika kuwa sikuwepo shuleni. Nikaitwa ofisini kwa mwalimu wa nidhamu. Kesi inaendelea. Wanamsubiria mwalimu mkuu, amesafiri. Lakini wanasema naweza kusimamishwa shule kwa kuwa nilitoroka au kufukuzwa kabisa.” Junior akamuhurumia sana.
Lakini ndipo akamuelewa sasa Emelda. Inamaana hata nyumba wanayoishi niya tembe! Full suit. Udongo juu mpaka chini. Maana hakuwa amesikia kama alinunua paa au makuti au nyasi ya kuezekea! Akasikia kuumia zaidi.
“Ulieleza shuleni mazingira uliyoyakuta nyumbani?” “Hapana.” “Hudhani kama ungeeleza ukweli ingefungua mwanya wa kueleweka?” “Au kufanya maisha yangu pale shuleni nako kuwa magumu zaidi, kama pale kijijini wanavyotuchukulia. Nilitamani kuwaeleza ukweli, lakini huwa hakuna anayetusikia.” Junior akashituka sana. Kaka yake akaongea kama Emelda.
“Kila anayetufahamu kwa ukweli, wanatukejeli na kutudharau. Wanatugeuza kichekesho. Sikutaka na mazingira ya pale shule ya sekondari yawe kama vile kijijini. Kote huko shuleni, mimi na Emelda tumekuwa tukinyanyaswa mpaka na walimu. Angalau Mateo wanamuheshimu sasahivi sababu mimi ndio mwanafunzi wa kwanza kufaulu pale kijijini, na tokea mimi nifaulu, hakuna tena mwanafunzi amefaulu pale kuja sekondari. Ndio hata na wao wakaanza kumwangalia na kugundua hata Mateo anaakili sana.”
“Lakini vinginevyo sio mazingira natamani kuendelea nayo na huku shuleni. Inanipotezea muda wa kupambana na vitu vidogo vidogo kutoka kwa wanafunzi wenyewe hata na walimu. Wakishatujua sisi ni kina nani, hawatusikilizi na kutuangalia tena kama wanafunzi wengine.” Junior alitamani akae. Ni kama alikuwa akimsema na yeye.
“Emelda alikuwa na akili sana pale shuleni. Darasani kwao alikuwa akifaulu sana. Lakini kwa sababu ya kutudharau, muda mwingine walikuwa wakimtoa darasani na kumtuma kazi majumbani kwao.” “Muda wadarasani!?” “Kabisa. Wenzake wakifundishwa au wakifanya mitihani, yeye anakuwa kwenye majumba ya walimu akifanya kazi. Wakati mwingine nilikuwa nikienda kumsaidia ili amalize haraka akafanye mitihani kama wenzake wasipate sababu ya kumrudisha darasa. Kwa hiyo sikutaka tena hilo linipate kwenye hii shule.” Junior akaumia sana.
“Pole sana. Nimekuelewa. Sasa tufanye jambo moja baada ya jingine. Kwanza ulichofanya ni kitu kizuri sana. Nakupongeza. Isingekuwa vizuri kumuacha mama kwenye ile hali.” “Halafu yupo na maumivu. Dawa alizosema Emelda ni mnunulie wakati ule, naona zimemuishia. Mguu unamuuma. Mateo anasema usiku kuchwa anamsikia akigugumia maumivu. Nisingeweza muacha na maumivu halafu wanalala kwenye matope! Nisingeweza.” Akamsikia kama analia.
“Sisi tutakuja huko. Tunajipanga. Naweza kuanzia shuleni kwako tuzungumze na walimu tuone wanachosema. Usiogope, kila kitu kitakuwa sawa.” “Nitafanyaje nikifukuzwa shule?” Akamuuliza kwa wasiwasi.
“Vitu viwili. Wakishindwa kabisa kukusamehe, wakakusimamisha. Kwa huo muda watakao kusimamisha, tutahakikisha hurudi nyuma. Tutalipia mwalimu atakayekufundisha mpaka utakaporudi shule. Na wakikufukuza, tutaomba matokeo yako mpaka hapo ulipofikia kisha utahamia kwenye shule ya kulipia mpaka utakapomaliza.” Hapo hata Emelda akavuta pumzi kwa nguvu. Junior wa mipango alishafikiria mbali hao ndugu wawili angalau kwa mara ya kwanza wakapata matumaini.
“Sasa kwa kipindi hiki unachosubiria hitimisho, tulia kabisa. Ila sasahivi nilazima uende ukaonane na mwalimu wa zamu atakayekuwepo, mwambie lazima uende nyumbani ukapeleke dawa za mama, utarudi kesho. Umueleze ni muhimu kwenda kumsaidia mama na mdogo wako, hawana msaada mwingine ila wewe. Utakachofanya ukienda, umtoe mama pale. Kama kuna nyumba za wageni, muweke hapo.” “Kule ni kijijini, hakuna nyumba za wageni.” Junior akafikiria kwa haraka.
“Basi rudi nao mjini na watafutie chumba kwenye nyumba za kulala wageni. Wakae hapo mpaka sisi tutakapokuja. Emelda atakutumia pesa.” “Ila Mateo yupo shule. Mama anaweza kukataa. Wanaweza pata sababu ya kumfukuza shule na yeye.” “Nakuahidi ni kwa muda tu Mika. Wakati tukijipanga. Maana kwa mazingira hayo hata Mateo mwenyewe atasomaje?” “Anasoma. Lazima asome.” Akajua yeye ndiye mwenye shida kuliko hata mama yao.
“Mika hawezi kukubali.” Akamsikia Emelda akiongea kwa sauti ya chini. “Nikuulize kitu Mika?” “Hamna shida.” “Unafikiri kwa mazingira hayo Mateo anaweza akasoma?” “Ndiyo mazingira sisi wote tumesoma. Tena bora yeye hata amekuwa akiweza kupata hata mlo mmoja kwa siku. Mimi na Emelda tulikuwa tukishinda njaa na tumesoma. Mateo lazima asome ndio maana tunahakikisha angalau anapata chakula.” “Basi naomba nikuahidi kuwa lazima atasoma. Lakini isiwe kwenye mazingira hayo. Tafadhali Mika. Mimi mwenyewe nitahakikisha anasoma. Lakini usiache mama akateseka. Mlete mjini. Mtafutie dawa za maumivu. Waachie pesa ya kununua chakula hapo kwenye nyumba ya kulala wageni. Kwa siku chache tu, tunakuja kuweka suluhu ya kudumu.Tafadhali naomba ufikirie Mika.”Kimya.
Junior akafikiria kwa haraka, akajua udhaifu wake ni mama yake. Aliweza acha shule anayopenda na kukaa akimjengea nyumba mama yake! Akaona atumie huo udhaifu wake. “Hata mama mwenyewe hawezi kuendelea kuishi kwa dawa za kupunguza maumivu tu. Ni lazima apelekwe hospitalini, wachunguze huo mguu kujua nini kinamsumbua. Kama kuna madhara makubwa yatibiwe kabla hayajasambaa na kumdhuru kabisa au kumletea tatizo la kudumu.” “Nilimwambia hivyo hata Emelda. Lakini pamekua hakuna uwezo.” “Kama kukipatikanika pesa, pale kijijini kuna hospitali?” Akamfanya kufikiria.
“Hakuna hospitali. Ni kijijini sana.” “Inamaana ni lazima mama aje mjini, si ndiyo?” Akapoa. “Ndiyo.” “Basi tuanze sasahivi. Kaage, rudi kijijini. Andika barua kwa mkuu wa shule ya kina Mateo, kuwa hatakuwepo shuleni kwa muda, sababu ya matibabu. Hivyo tu.” “Wanaweza kataa.” “Hutakuwa ukiomba ruhusa ila kuwataarifu. Waachie barua kama ushahidi. Uwe na nakala yako na wewe pia. Kisha watoe kwenye hayo mazingira mabaya. Hilo ndilo la msingi na la kwanza. Mengine hatuwezi kuwa na majibu yoke kwa sasa. Lazima tutembee kwa hatua.” “Ni kweli.” Hapo akakubali.
“Emelda atakupa namba yangu. Tuwasiliane kwa kila hatua. Tukianzia kama utaruhusiwa hapo shuleni kwenda kwa mama. Ila nashauri uhakikishe unaruhusiwa. Ukamtoe mama kwenye yale mazingira.” “Sawa. Junior?” Akamuwahi kabla hajakata. “Bado nipo.” “Nilitaka kukushukuru. Nilikwama, sikujua kitu chakufanya.” “Poleni sana Mika. Mungu atasaidia.” “Naamini hata sasa ameshasaidia. Nakushukuru.” “Karibu. Nategemea kukusikia baada ya muda mfupi ukitoka kuaga.” “Sawa.” Ndipo wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hapohapo kwa kutumia simu ya dada yake akamtumia namba yake. Akamgeukia Emelda, akamkuta ametulia. “Pole sana Emelda.” Akasimama kama aliyemtoa mawazoni. “Naomba tukae.” Wakarudi kukaa. “Uliposema mama anatembea kwa kuchechemea, sikujua kama ni kwa maumivu.” “Nafikiri baba alimvunja mguu, hakupona vizuri. Vipindi vya baridi ndio inakuwa mbaya zaidi. Sasa Mateo aliposema anahisi anamaumivu, ila hataki kusema, ndio ikabidi kumnunulia dawa za maumivu. Tukawa tukimsaidia hata kulima. Akichukua kazi, Mika na Mateo ndio wakawa wao wanaenda kulima hayo mashamba ya watu. Na mimi nikiwepo nawasaidia. Kidogo akapata nafuu. Sasa nahisi imerudi. Na mama ni mkimya sana. Atakuwa alianzwa muda mrefu ameshindwa kusema.” Junior akabaki Akifikiria.
“Sijui chakufanya tena.” Akaongea kwa sauti yake ya chini kama aliye lemewa kweli. “Naona kama kila baya linatupata sisi na sijui kwa nini!” Akaanza kulia. “Mimi na Mika tunaomba sana, kaka.”“Mimi sio kaka yako, Emelda.” Ikabidi Emelda acheke akilia. “Lakini naona sasahivi ndio kama kila kitu kinaparanganyika. Nyumba imeenda na maji. Halafu wanataka kumfukuza shule Mika! Sijui itakuaje?”
“Kuna usemi unasema it gets worse before it gets better. Unaelewa?” “Ndiyo.” “Basi kama nilivyomwambia Mika, ndio na wewe. Sikuwa nikimfariji tu. Tutembee kwa hatua. Hatutakuwa na majibu yote kwa wakati mmoja. Ila ninachojua kwa sababu anataka kusoma, atasoma tu. Na kwa kuwa mama ni mgonjwa, nilazima apate matibabu. Acha akamtoe kwanza kijijini. Na sisi tukaombe ruhusa jumatatu, kisha twende wote tukamchukue.” “Utamuweka wapi huku mjini?! Mama asijeona nimeanza matatizo akanifukuza kazi.” Junior akahisi hata pale kwao hawajui ukweli juu ya maisha ya huyo binti. Kama kaka yake, na yeye pia hajizungumzii ili wasimdharau.
“Emelda, wewe ni mpenzi wangu. Utakua mke wangu. Sehemu yangu mimi. Mama wa watoto wangu.” Mpaka hapo akainua kitu ndani yake. Na alifanya makusudi ili kumleta karibu. “Huna jinsi ukawa matatizoni, ukaumia, mimi nisiumie. Ndivyo ninavyoishi na Ezra, na wewe umekua sehemu yangu na wewe itakua hivyohivyo. Kuanzia sasa, tatizo lako ni letu. Nitazungumza na wazazi kujua jinsi yakumsaidia mama yako mpaka apone kabisa.”
“Na najua kuanzia nilipowaambia nataka kukuomba nikuoe, wakijua kama umekubali. Najua kwa hakika mama ataanza kutafuta mtu mwingine pale. Au huna uhakika na sisi?” “Mimi ndio nina wasiwasi na wewe. Nahisi utalemewa mapema. sikutaka ujue mengi usije ona unajiingiza matatizoni. Ila mimi nakupenda Junior. Nakupenda sana. Hata Ester alinigundua.” Junior akashituka.
“Ester?! Mbona hakuniambia chochote na sisi tupo karibu sana au niseme tunazungumza mengi?” “Nilimsihi asinisemee hata kwa mama. Na nikamuomba asimwambie mtu. Ila yeye akaniambia wewe umemchumbia Hope na anakujua wewe unamsimamo, nisimkatae Edwin. Nikijipa..” “Subiri kwanza. Edwin yule wa kanisani anayefanya kazi na Ester?!” “Ndiyo.” “Kwamba alikutaka!?” “Alimtuma dada Ester." Akaanza kubadilika sura. Wivu tayari.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kumbe Emelda aliyeshindwa kumuona yeye tokea mwanzo, alishaonwa na kijana wamaana tu, anayejielewa. Lipi lililokuwa likiendelea wakati yeye amefumbia macho mapenzi yaliyokuwa yakililiwa na wengine.
INAENDELEA…
0 Comments:
Post a Comment