Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 36. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 36.

“Vile mchungaji anavyo mpenda na kumuheshimu sana mama, haikuwa hivyo kwetu.” “Na nafikiri hiyo ndio siri ya mafanikio yao wale. Tokea nina akili zangu, wapo hivyohivyo. Wanaelewana na kuvumiliana bila manung’uniko. Baba yako wewe yuko wapi?” 

“Alitufukuza na kututelekeza moja kwa moja, ila baada ya mateso mengi sana kwetu. Alikua akianza kumpiga mama, unaweza hisi atamuua. Na akimaliza alikuwa anamtupa nje na kutufungia sisi wote na mama yetu.” “Pole sana Emelda.” “Asante. Na mbaya inakua pengine ni usiku. Hakuna pakwenda. Na ile ilishamfanya mama akawa wakudharaulika, hakuna wakutufungulia mlango na mama hawezi rudi nyumbani kwao, mbali na aibu kwenye kijiji alichotokea. Na bibi hakuwa na uwezo kabisa. Fukara. Naye aliachwa na babu, mama akiwa mdogo, babu alipofariki.”

“Kwahiyo mama alikuwa mtoto wa peke yake. Akaolewa na kuhama kijiji kingine, ukoo mwingine ambao hawakumtaka mama kabisa. Mateso yakaendelea. Hapo tulikuwa mimi na Mika. Mdogo wangu huyo wakiume anayenifuata. Mama alipokuja kumzaa Mateo, ndio ikawa mbaya kabisa. Alikua akianza kumpiga mama, ujue basi mpaka na sisi tutapigwa.” “Kosa nini!?” “Hata sijui kaka! Halafu kama nilivyokwambia, mama yangu ni mpole sana, ni rahisi kumuonea. Alimtesa mpaka mama akawa mtu wa hofu kupita kiasi. Ila nafikiri Mungu alituhurumia, mwishoe siku moja usiku baada ya kutupiga, akatufukuza wote. Ndio ikabidi sasa kurudi kijijini alipokuwepo bibi. Ikawa fedheha ya kuachika kwa mama, shida, hamna hata chakula huko kijijini kwa bibi lakini angalau kukawa na utulivu, japo nyumba yenyewe ni ndogo sana.”

“Ndio mama akawa anachukua kazi kwenye mashamba ya watu, tunasaidiana kulima, anapata pesa, maisha yanaendelea. Bibi aliachwa na mashamba pamoja na mifugo, lakini babu alipofariki, ndugu zake babu walimpokonya bibi kila kitu, mpaka nyumba. Walisema hastahili kurithi kwa kuwa hakuzaa na babu mtoto wa kiume wa kuendeleza jina la babu.” Akasikika na sauti ya uchungu.

“Tulikuwa tukisoma shule za palepale kijijini. Mimi nilipomaliza darasa la saba, sikufanikiwa kuendelea. Ila Mika alifaulu kwenda shule ya wanaume ya sekondari ya bweni, Songea. Ikawa ndio mtu wa kwanza kufaulu pale kijijini kwetu. Akawa anaweka, juhudu ya shule, mimi na mama tunamsaidia kutafuta ada na michango ya shule. Akiwa likizo na yeye akirudi nyumbani basi anasaidia kazi.” Akaendelea taratibu tu.

“Ndio likizo moja bado akiwa kidato cha kwanza akarudi na nauli, akasema kuna rafiki yake anaishi huku Dar, mama yake anatafuta msichana wa kazi za ndani, alipomwambia ana dada yake anaweza faa, ndio akawasiliana na kwao, wakatuma nauli ili mimi nije huku Dar. Sasa wakati huo mimi na mama tulikuwa hatuna simu. Hawezi kutuma hiyo pesa ya nauli wala kuwasiliana mpaka aliporudi likizo ndio akatuambia. Mama akaniruhusu nije mjini. Mika alipowasiliana nao kuwa nipo tayari kuja huku kwa kazi, wakawa wameshapata msichana mwingine. Ndio akawasihi wanitafutie kwengine. Baada ya muda wakasema nije huku.”

“Ndio kwa mara ya kwanza nikafika mjini. Walinipokea na kunipeleka kwa mama mmoja alikuwa na watoto wawili wadogo. Naye akawa kama baba yetu tu. Ana mkono wa kupiga.” “Kwamba na wewe anakupiga?!” “Sana kaka. Mtoto akicheza akijiumiza, kosa ni langu. Ananipiga. Chombo kikivunjwa na mtoto, basi ni mimi, ananipiga. Hakuna mshahara, kila mwisho wa mwezi ananihesabia vitu vilivyoharibika hapo ndani kwake kwamba natakiwa kulipa. Kwa hiyo eti akawa anakata kwenye mshahara, nabakiwa na deni kila siku.” “Aisee pole sana!” Akazidi kumuhurumia.

“Asante. Akawa ananipiga mpaka majirani wakawa wanajua. Hanilipi mshahara na wakati mwingine hanipi chakula. Nilikaa kwake kama miezi sita, hajanilipa hata mara moja. Siwezi saidia nyumbani na pia kurudi nyumbani siwezi nilikuwa najitahidi naamini ipo siku atakuja tu nilipa, bila mafanikio.”

“Ndio kuna sehemu nilikuwa nikitumwa mara kwa mara kununua mkaa, huyo mama mumewe alikuwa mlinzi nyumbani kwenu. Na mwenyewe aliniambia analinda kwenu kupitia kampuni ya ulinzi. Ila akasema mama yenu mtu mzuri sana, ni mama mchungaji. Huwa anawapa chakula mara kwa mara na kuwatengenezea chai kila siku usiku. Akasema akipita getini atamuomba aniulizie kanisani kama kuna mtu anataka msichana wa kazi. Ndio baada ya kama siku mbili akasema anipeleke kwake.”

“Mara ya kwanza nilitoroka sababu yule mama niliyekuwa nikiishi naye alikataa nisiondoke, akasema eti ananidai. Alipwe kwanza ndio niondoke.” “Jamani! Si hakuwahi kukulipa mshahara wako?!” “Hata shilingi kaka. Ndio nikatoroka. Nilipokuja kwenu yule mlinzi akawaambia ukweli wazazi wako kuwa imebidi nitoroke, wao wakanirudisha kwa yule mama.” Junior akashituka.

“Wakaomba kujua ananidai kiasi gani ili tuachane kwa amani. Wakamlipa.” “Namshahara wako!?” “Mama yenu alisema nimuache tu, Mungu atakuja nilipa kwa njia ingine. Wakamlipa yeye, wakaandikishana, ndio nikaishia kwenu.”

“Ila nikashangaa mama yenu akaanza kunilipa hela, tena mshahara mkubwa tu. Halafu Ester akawa ananisaidia kazi, na bado wakamleta na kijana wa nje! Kazi yake kufua na kupiga pasi! Siku za usafi anasaidia kuosha madirisha na mambo mengine! Nikawa nashangaa hela kubwa halafu kazi sio nyingi! Halafu mchungaji anataka ikifika saa nne kila mtu awe ndani na kumetulia.” Akamuona anacheka.

“Nini?” “Nilikuwa nafurahia kaka! Kazi mwisho saa nne usiku! Halafu mama yenu hataki mtu angie chumbani kwake! Anasafisha chumba chake mwenyewe! Hugusi kitanda chake na mumewe! Hataki kabisa mpaka umbembeleze kweli kumsaidia kusaficha hata choo chake na bafu, ndio mara moja moja anaweza kukubali. Ila hataki mtu chumbani kwake. Wakati kwa yule mama nilikuwa mpaka namtandikia kitanda! Wakati mwingine unakuta kitanda kichafu kabisa wametoka kutumia! Uchafu! Halafu ananipiga! Pale kwenu nikawa nafurahia. Sina kazi nyingi, unakula wanachokula wengine, huhesabiwi chakula, halafu nalipwa!” Junior akacheka.

“Hela ikawa haina matumizi kwangu. Ester ananipa nguo zake. Akinunua nguo za ndani akiwa na hela na mimi ananinunulia. Na mama hivyohivyo. Kwa hiyo ule mshahara wote nikawa namtumia Mika. Analipa ada yake na michango ya shule ya Mateo kisha ikibaki ni ya mama. Ndio mpaka leo.” “Pole.” “Sasahivi sio mbaya. Kazi yangu inasaidia. Na mama yenu hana neno. Ikitokea nahitajika pesa nyumbani, namuomba, ananikopa, nawatumia nyumbani halafu anakuja kunikata kwenye mshahara unaofuata. Kwahiyo inasaidia.” Junior akatulia akitafakari.

“Unakumbuka kuna kipindi nilikuaga nakwenda nyumbani kuna mgonjwa?” Junior akamwangalia huku akipika. Hilo jiko na vifaa vyake ungependa kuwepo hapo. Kulikuwa na island nzuri sana katikati ya hicho chumba cha jiko. Yenye jiko la umeme katikati yake na mbele ilizungukwa na viti vizuri sana. Ndipo alipokuwa amekaa Emelda akila, Junior akipika mbele yake. Hiyo island  ilikuwa kama kwa Ezra tu kulikombambaisha Jelini.

“Ulinipa pesa kaka! Hukumbuki?” “Nakumbuka Emelda.” “Basi mama alikuwa akiumwa. Ndio nikaenda. Ile pesa ilisaidia kaka! Ila mama akapona. Halafu wakati huohuo akaugua bibi, wala hakuugua sana, yeye akafariki. Nikawataarifu huku kuwa itabidi nikae kule zaidi mpaka mama apate nguvu. Alitoka kuugua na mama yake akafariki. Lakini mama yako akawa na wasiwasi kuwa naweza nisirudi. Ila akanitumia pesa ya mazishi. Ilisaidia kaka, sina jinsi nikakwambia ukaelewa! Maana pale kijijini hawamsaidii kabisa mama akipatwa na tatizo. Lakini ile pesa ikasaidia, tukamzika bibi. Baada ya siku chache nikarudi.”

“Mika yupo kidato cha ngapi?” “Cha tatu sasa.” “Na Mateo?” “Yupo darasa la tano. Ila sijui tutafanyaje akimaliza darasa la saba! Anaakili sana, ila yupo na mama kila mahali. Hataki kwenda mbali kama vile Mika na mimi. Tukimwambia akifaulu lazima aende shule, analia. Na pale kijijini hawana sekondari bado.” “Kama Noah?” “Wewe ndio umepatia. Huwa namfananisha na Noah! Li Noah lipo kama linanyonya!” Junior akacheka.

 “Eti anasema yeye ataolea palepale nyumbani. Ili akae na mkewe pamoja na mama.” Junior akatingisha kichwa kwa masikitiko akicheka. Akatulia.

“Na kama ungepata nafasi ya kujiendeleza, ungependa kuwa nani?” Akashindwa kujibu. “Basi labda niulize. Darasani ulikuwa ukifaulu masomo gani?” “Yote.” Junior akashangaa sana. “Emelda!” “Kweli kaka. Mimi nilikuwa nakuwa wakwanza kwenye kila somo, ila sema nilijua sitakwenda mbali ili kumsaidia mama. Kwa hiyo sikuwa nikifikiria mbali na pale mama alipo.”

 “Nilikuwa nikimuhurumia kumuacha. Mama yetu ni mnyonge sana. Si mtu anaweza jitetea kwa yeyote na kwa chochote. Kijijini kwetu sisi, nikimaanisha na mama yetu ni wale watu wakudharaulika. Hakuna sehemu akazungumza wakamsikiliza. Hata akienda dukani yeye, anaweza kuwa wa mwisho kuhudumiwa. Wakati mwingine anaweza akawa amefika yeye wa kwanza, akaja mtu nyuma yake akahudumiwa, yeye akaachwa.” Junior akaumia.

“Halafu baba alimpiga mpaka akamuharibu mguu. Anaweza tembea, lakini yupo kama mlemavu! Anachechemea au niseme anatembea kwa kupinda. Pale kijijini wanakuwa wakimuigilizia anavyotembea, hata shule tulikokuwa tukisoma walikuwa wanatukejeli wakimuigilizia jinsi anavyotembea. Kusudi tu, kutuchokoza. Kwa hiyo nilikuwa najua nitabaki naye daima ili kumsaidia pale.” Akamalizia kama aliyekumbushwa mbali. Akatulia na kupotelea mawazoni.

 “Pole sana Emelda. Lakini unajua mimi si kwamba nilikuwa nikikudharau?” Kile kitu kilimuuma Junior akawa kama akijitetea. Emelda akacheka na kuinama.

“Mungu wangu ni shahidi Emelda, sikuwa nikikudharau sema…” Akasita. “Sijawahi kukudharau. Nafikiri ni ni ni…” Akakosa kabisa jinsi ya kujitetea. Gafla akajikuta anajifunga kila kona. Kila akifikiria sababu ya kujitetea kwa mtu kama yeye aliyekuwa akimfanyia yote hayo asiyaone, akajua akiongea ukweli anaweza akaharibu zaidi.

“Naweza nisiwe na sababu nzuri ya kutosheleza. Ila najua unaniamini mimi si muongo. Eti Emelda?” “Najua wewe sio muongo kaka.” “Basi na katika hili nakusihi uniamini. Sijawahi kukudharau hata mara moja. Sikuwa nikikufahamu. Na kwa jinsi nilivyokuwa nikikuona na kuzisikia sifa zako kuwa ni binti mzuri. Kwa kuwa wasichana pale ndani walikuwa wakimsumbua sana mama, mpaka ulipofika wewe. Ukajawa heshima na ukawa umetulia. Zaidi kilicho tushangaza ni ukakubali kwenda kanisani!”

“Kwani wengine hawakuwa wakienda kanisani!?” “Hapana. Na tulipokuwa tukienda kanisani, huku nyuma ndio ulikuwa wakati wao wakufanya mambo yao. Mnarudi nyumbani wanakuwa hawapo na hawafanyi kazi. Kwa kifupi ni wasichana ambao hawakuwa wametulia, mpaka ulipokuja wewe. Ukawa binti mdogo, lakini ukamudu ile nyumba na kila mtu.”

“Halafu Emelda wewe ni mpole sana. Huzungumzi. Halafu ukaweka umbali kabisa kati yako na mimi pamoja na Ezra, tofauti na ulivyomzoea Noah! Nafikiri ili tusikutie wasiwasi na sisi tukawa kama tunakupa nafasi. Na hapo nakiri ndipo tulipopitiliza. Lakini sio dharau hata kidogo. Au unahisi kuna jinsi nimekuonyesha dharau? Na tafadhali niambie ukweli. Usiogope?” “Hapana.” Junior akafikiria kwa haraka.

“Niambie vile ulivyonifikiria nakuchukulia.” Akafikiria kisha akamwangalia. “Niambie tu.” “Najua ulinichukulia kama msichana wa kazi za ndani tu.” Hiyo ikamuuma zaidi Junior! Haina tofauti ya kumdharau. Kwamba alikuwa akimuona si kama wasichana wengine. Ni mfanyakazi duni, hawezi kuwa zaidi ya hivyo.” Akaona ajishushe.

“Naomba unisamehe Emelda. Lakini haikuwa na nia ya dharau hata kidogo. Na naomba uniamini.” Akacheka taratibu akiwa ameinama. Na kujibu. “Hamna neno kaka.” Wakatulia lakini Junior hakuwa ameridhika. Ila akaona aipe muda.

“Acha nimuite Ezra aje tule. Naona hapa nakaribia kumaliza.” “Basi nioshe hata vyombo!” “Ataosha Ezra. Wewe leo mgeni. Zamu yako tukutumikie.” Akamtumia ujumbe Ezra.

Akaendelea kupika akiandaa sahani. Alipanga vyombo mezani, Emelda akimwangalia anavyofanya kama mama yao. Baada ya muda akamuona anaanza kusafisha alikokuwa akitumia huku akimalizia kuivisha.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mara Ezra akaingia. “Upo Emelda?” “Shikamoo kaka.” Akasimama kabisa. “Marahaba. Mzima lakini?” “Mzima.” “Tunahamia mezani nini? Mimi nataka nile nichomoke kwa haraka, naenda kumsaidia Jelini. Naona leo amepata kazi kubwa!” “Ukitaka msaada, niambie. Nitakufuata.” Ezra akabaki akifikiri.

“Itatusaidia kumaliza haraka ili tupate muda wa pamoja baadaye.” “Wazo sio baya. Basi acha mimi niende kwanza, nikaangalie, tutawasiliana.” Wakahamia mezani.

“Umependeza sana Emelda!” Ezra akamfanya apatwe na aibu, Junior akamwangalia na kucheka. “Asante.” Ezra akacheka vile alivyojibu akijificha.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Vipi mambo yalikwenda vizuri?” “Aisee zaidi ya nilivyotarajia, halafu ikapitiliza mpaka upande wa pili!” “Acha masihara!” “Si hata Muhubiri 10:19 kwenye bibilia inamalizia kwa kusema, ‘Fedha ni jawabu la mambo yote?’ Au?” “Acha Junior!?” “Nakwambia, nakupitiliza.” Akamuona anabadilika na sura.

“Mbali na ahadi ya kurudishiwa cheo na kulipwa mshahara, bado kunahitajka kadi ya gari na funguo.” “Haiwezekani!!” “Nakwambia hapakuwa na habari ya kushitua wala kushangaza ila wasiwasi wa pango na usafiri tu!” Ezra akatingisha kichwa kwa masikitiko. Junior akacheka na kuendelea kupakua. Emelda hajui wanazungumzia nini.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Hiki ni chakula chako Emelda. Nakupakulia wewe. Kwa hiyo niambie niongeze nini.” “Naona inatosha. Nitaongeza nisipotosheka. Asante.” “Mambo yangu matupu hapa!” Akaongea Ezra akijipakulia. “Mtengenezee na Jelini sahani yake. Nilinunua vitu vingi sana.” “Sawa. Tena sasahivi atakua na njaa. Ameanza kazi mapema sana leo. Nitampelekea. Nakushukuru.” Wakaomba na kuendelea kula wakizungumza wao wawili maana walishajua wakimuongelesha Emelda, hatakula kwa aibu. Wakajifanya kama wamemsahau. 

Alikula kwa haraka. Bila ya kuambiwa, kama anayejua anachotakiwa kufanya, akakusanya vyombo vichafu na kurudi jikoni kusafisha mpaka masufuria. 

Akahakikisha Emelda hafanyi kitu. “Karibu sebuleni! Nakuja.” Akajua ndio anatakiwa kuhamia huko, akaondoka akimuacha anamalizia kusafisha meza. Akatulia hapo sebuleni akiangaza macho. Akabaki amekodolea macho picha ya Junior na Hope.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akamfuata Ezra jikoni. “Nisikilize Junior. Najua haijakaa vizuri, lakini kama hivyo vitu vitaleta amani, tafadhali mpe tuachane naye tu.” “Aisee nimekereka Ezra!” “Najua na nakuelewa. Ila acha iishie hivyo. Tuhesabu ni kama tumelipia ada kwenye shule tuliyofundishwa kwa machungu. Acha yaishe. Hatuna shida ya gari sisi, ila amani. Hiyo ni garama ndogo sana unalipa kulinganisha kama ndio ungeingia kwenye ndoa ya namna hiyo. Fanya kama sadaka.”

“Unafikiri basi nilikuwa na hata wazo la kumnyang’anya! Ila jinsi alivyonidai ndio imenikera Ezra. Hana hata utu! Yaani yeye hajali ila mali tu! Imeniuma sana kujichelewesha ambako mbali ya kwamba sikuwa nikitakiwa, pia nilikuwa nikidharaulika!” “Tafadhali usijiumize zaidi Junior. Emelda yupo ndani, anakusubiri wewe. Achana na ukurasa uliopita. Tutajichelewesha wenyewe.” Kidogo akatulia.

“Kesho ndio ametaka tumalizane naye kwa kumkabidhi funguo ya pili na kadi ya gari.” “Basi kesho tufunge huo ukurasa kabisa, tusirudi nyuma.” Junior akaridhia. Akamalizia usafi. Akamchukulia na Jelini chakula, akatoka kwa haraka.

 Junior&Emelda.

 Junior anafika sebuleni ndio anagundua aliondoa kila kitu cha Hope kasoro hiyo picha yao ya siku alipomvalisha pete. Ilikuwa picha nzuri ya kuvutia. Aliikuza na kuiweka kwenye framu ya kuvutia sana. Emelda alikuwa amezama mawazoni, macho pichani.

         Alisikitika na kuona amejirudisha nyuma kwenye kuanza kwa Emelda. Kwani walipofika jikoni angalau mazungumzo yalimfanya atulie hata kuweza kuongea. Kwa mara ya kwanza akajihisi hofu ya kuzungumza naye ilipungua. Hapo alikuwa akitengeneza mazingira mazuri arudi kujitetea tena juu ya kutomdharau. Amuweke sawa, atongoze.

Lakini alipomuona amemuona akiingalia picha yao, akainama kinyonge. Akarudi Emelda yuleyule wakufinyiliwa. Furaha yote ikaisha. Mnyonge. Ndipo akaweza kumsoma kuwa hayo mahusiano yalikuwa yakimuuliza. 

Juhudi ya kutoa hiyo picha ikaanza tena. Akatafuta stuli kabisa kuifikia hiyo picha. Akaondoka nayo hapo, Emelda akiwa amejiinamia. Akaenda kuiweka mbali kama mashariki na magharibi na hapo alipo Emelda. 

Wakati anarudi, Emelda akasimama, macho mekundu. “Naenda chooni, kaka.” “Nakusubiri.” Akamwambia kwa upendo, kama anayembembeleza. Emelda akampita na kuelekea chooni. Akakaa, baada ya muda akatoka akionekana aliosha uso kabisa. Akaenda kukaa kochi la mbali kabisa na pale alipokuwa Junior amemfuata kwenye kochi alilokuwa amekalia mwanzo.

La Moyoni!

Alichofanya Junior ni kuhamia kwenye kochi alilokuwa amehamia. Tena akamsogelea karibu kabisa, akapandisha mguu mmoja kwenye kochi akaukunja juu ya kochi na kumgeukia yeye. Emelda akakalia mikono yake na kuinama.

“Nilitaka uje mida hii kwa kuwa nilitaka tuzungumze Emelda.” Akamwangalia na macho yaliyojaa machozi. “Ulipofika hapa na kunikosa, nilikuwa nikikutana na Hope.” Akainama, ila akamsikia akivuta kamasi, akajifuta machozi kwa bega, akiwa bado amekalia mikono yake. 

“Niliweka hiyo miahadi, ili nikazungumze naye. Na kuhitimisha.” Emelda alishituka na kumwangalia. “Kuhitimisha?! Kama kuachana!?” Akawa kama hajaelewa. “Ndiyo.” Akabaki akimwangalia Junior kama haelewi, kisha akamuuliza taratibu tu. “Kwa nini tena, wakati mpaka baba aliwaombea na watoto wenu?” Na safari hii machozi yakadondoka mpaka kifuani.

Maana maombi aliyofanyiwa Ezra na Jelini, na mchungaji, baba yao, yalikuwa kama aliyofanyiwa Hope na huyo Junior. Junior hakuamini kama bado anakumbuka hayo maombi! Akazidi kuamini kuwa huwa anamfuatilia kwa karibu sana.

“Hope hakuwa mke wangu.” Na yeye akamjibu kwa utulivu akimwangalia kama anayejaribu kumsoma zaidi. Emelda akapigwa na butwaa, akaduaa. “Umeshawahi kusikia ule usemi wanasema mpumbavu anapotumbukia majini. Usimtoe mpaka amalize kutapatapa. Akishakunywa maji, akalemewa kabisa, hapo ndipo msaidie kumtoa. Vinginevyo anaweza kukuzamisha na wewe?” Emelda alikuwa kwenye butwaa, hakujibu.

“Ndio ilikuwa mimi. Nilihitaji kupita kote nilikopita na Hope, kutambua, au nikubali kuwa hakuwa mke wangu. Japo nilishaona dalili kwa muda mrefu na kufumbia macho. Mwishoe ndipo nikakubali kuwa, yeye kama yeye si mtu mbaya, ila hakuwa mke wangu.” Akawa kama amehitimisha, Emelda ndio akagutuka na kutoa mikono kule alipokuwa amekalia mapajani na kuanza kuisugua taratibu.

“Nimepoteza muda mrefu kwenye mahusiano ambayo nilishajua si yangu, lakini nilikuwa nikilazimishia na nimejichelewesha.” Emelda akamtizama kwa macho yaliyojaa upole. Kama anayemuomba amuone na yeye. Junior akamsogelea karibu zaidi.

Kisha akamuuliza. “Katika jumbe zako. Pengine niwe nilisoma vibaya. Maana zote ninazo Emelda. Sijawahi futa ujumbe wako hata mmoja.” Akashangaa sana. “Kwa nini umezitunza na hukuwa ukinijibu?!” Akamuuliza kwa upole, machozi yakiendelea kutoka taratibu. 

“Kwa sababu sikuwa nikipuuza, ila nafikiri nilishindwa kukuelewa mpaka nilipojipa muda wa kurudia kusoma tena na tena. Ninazo jumbe zako zote na naweza kukwambia hata ujumbe wako wa kwanza kwangu.” Akainama.

“Nakiri nimekua mzito kwenye kukuelewa. Na hata sasahivi nina hofu na nilichokielewa mpaka nihakikishe kutoka kwako mwenyewe.” Alishindwa hata kumuangalia. “Eti Emelda? Au nimeshachelewa?” Alilia huyo binti, akalia kwa uchungu sana mpaka Junior akamuhurumia, ndipo akajua alikuwa akimaanisha kila alichoandika, na amemuelewa.

Junior akajisogeza kwake, akamzungushia mikono, bwana akamkumbatia Emelda! Aisee kama penzi lipo, lipo tu. Emelda akajiweka vizuri, wakajikuta wamekumbatiana kwa n wa ajabu sana. Junior alijawa hali ya ajabu, akaelewa alichosema Ezra hali aliyoipata alipomkumbatia Jelini!

Akambembeleza hapo akiwa ametulia mkononi, kochini. Emelda analilia shingoni na kuamsha hisia kali sana kwa Junior. Akambembeleza mpaka akatulia, alipotaka kuondoka, akamuwahi ila sasa akajiweka vizuri na kuanza kumfuta machozi taratibu. 

“Nahisi ningekuelewa mapema, nisingehangaika kote huko Emelda. Au ukute ni kweli Mungu alitaka nikahangaike huko ili nije kuthamini alichokuwa ameniandalia.” Akaendelea kuzungumza naye taratibu. 

“Au nimechelewa?” Akatingisha kichwa kukataa kisha akaongeza. “Mimi bado nakusubiria wewe.” Alifurahi Junior, hakutegemea. Hapo akapitiliza. Na kwa alivyo Junior, hakujua kama anaweza kufanya hivyo kwa mwanamke asiye mkewe. Alikuwa amejawa maadili, hata Hope hakuwahi kufika umbali huo.

Hapo hisia zilikuwa zikizungumza kwa ajabu sana. Akajiegemeza kwenye kochi vizuri, akamvutia kwake. Akaanza kumbusu alipofikia, akamnyanyua uso, akapata midomo, akaanza kupata kiss. Emelda alikuwa akitetemeka! Mwili umekakamaa kama amepigwa shoti ya umeme. Hajawahi kufika umbali huo na yeyote, sasa iwe kaka Junior! Akazidi kutetemeka.

Ila Junior alishindwa kumuachia akaendelea tu kung’ang’ana naye. Kadiri Junior alivyoendelea, akihangaika kupata midomo sawia, Emelda hajawahi kukiss, hajui chakufanya. Hajui anatakiwa kufanya nini! Hofu imemjaa na mshituko kushikwa vile na kaka Junior! Junior akaendelaea kunyonya midomo ya nje taratibu, yeye mwenyewe anasikia raha kupitiliza.

Sasa jinsi alivyomshika kwa uhakika, akimbusu tena na tena kisha kuendelea kunyonya midomo yake kwa nje, kwenye lips, Emelda akaanza kutulia. Junior hakuacha mpaka binti wa watu akalegea, akajiachia, na kujisahau akamkumbatia vizuri kama asianguke. Alipofanikiwa kupata ulimi, ungesema ananyonya pipi! Kwa jinsi alivyokuwa akifurahia huo ulimi wa Emelda.

Hapakuwa na hodi wala usumbufu. Junior akajinafasi. Alimjua hajui kwa kuwa Emelda mtoto wa nyumbani. Hatoki nje. Kanisani, ndani. Akitoka ni na mama mchungaji au Esther. Sifa zake zilikuwa zikiimbwa mpaka na Noah. Hapo Junior alijua ndio yeye anapita hapo kwa mara ya kwanza. Alijawa furaha akijua ni pipi anayoitoa kwenye ganda lake. Yeye wa kwanza, hakuna aliyeishika. Mtoto mbichi! Emelda umri karibu sana na Jelini. Mdogo. Ila hajapitishwa kwingi kama Jelini. Junior alikuwa akisikia raha! Na hivi anabaraka za mama yake tayari, alikuwa kwenye ulimwengu wake.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mwanzo Mpya, Muendelezo Wa Maisha, Mwisho Mpya Kwa Wengine. Wote Wanatakiwa Maisha Yaendelee.

Wengine Wanapanda, Wengine Wanashuka, Wapo Ving’anganizi Wanaokomaa Na Maisha Jinsi Yalivyo Bila kutetereka.

Mapenzi & Pesa…..

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment