Wakati wengine wakiendelea kwa furaha na mipango ya maisha, na Colins alikuwa akijenga ramani mpya ya maisha yake akiwa na maumivu ambayo hajui anayotoa vipi
Kazi ya kutengeneza orodha ya wanao mzunguka, na kuwaweka kwenye makundi wanayostahili ilikuwa ikiendelea bila kuchoka. Akiwahamisha kila mara kwenye hayo makundi kwa aina ya adhabu zao alizowafikiria bila kuridhika.
Kuna ambao waliingia na kutoka akiwahamisha kwenye kila kundi, akihakikisha wanapata adhabu wanazostahili bila kuwapunja kutokana na dhambi zao dhidi yake.
Jinsi ya kumfikia kila mmoja wao ndio ikabakia kazi inayomsumbua. Akasaka taarifa zao kwa kina huko mtandaoni bila kuchoka na akitumia akili nyingi kukumbuka jinsi walivyo na walivyohusiana naye. Chochote alichopata juu yao, hata kutoka kwa wao wenyewe, hata kwa muda mfupi tu walipomsogelea kipindi wakimuumiza, alitunza kwa kuandika kila alipokumbuka au kupata taarifa zao, akiwa anaongezea kwenye kila jina. Maana kila mmoja wao alimtengenezea profile yake kwa vile alivyomtenda.
Kichwa kilikuwa kikifanya kazi mchana na usiku. Hata akikumbuka taarifa ndogo ya namna gani juu ya hao watu, bila kupuuzia, hata akiwa usingizini, au anakula. Akakumbuka chochote juu yao, iwe salamu na jinsi ulivyoitika, ataacha kila kitu na kwenda kuandika kwenye ukurasa wa huyo mtu, ndani ya kompyuta yake iliyokuwa ikifunguka kwa face id yake tu. Aliweka hivyo makusudi akitoa kufungua kompyuta yake kwa namba ya siri, ili kujihakikishia hakuna anayeweza fungua bila yeye kuwepo akitizama kompyuta zake zote.
Mtumishi aliyemuombea mpaka kumgeuza kichaa. Huyo akabaki kusaka habari zake pamoja na Kemi. Japokuwa walikuwa wakionana mara nyingi na kumfanya apoteze fahamu, lakini katika machache aliweza kuunganisha mchana na usiku huku akivuta kumbukumbu za Kemi pia.
Na ili sasa asimtibue Love kabla hajamalizana naye, akafikiria jinsi ya kurudisha pesa aliyochukua kwenye akaunti yake, akihofia siku akija tafuta kujua salio la akaunti yake huko benki akajua hiyo pesa haipo, angegutuka na kuomba benki statement ambayo alijua ingemfanya aanze uchunguzi na kumpotezea na yeye muda kwenye yake. Alitaka akiwa ametulia hivyohivyo, anajiona mshindi, basi ampige mpaka paume kabisa.
Sasa kwa kuwa ni mtaalamu wa mambo ya kompyuta na amefanya kazi kwenye kampuni ya simu tokea anarudi nchini, akaanza yake. Akaingia kwenye simu ya Love, akapata tu jina la Mtumishi ila akapata namba na kuanza kutafuta iliponunuliwa na kusajiliwa. Alikuwa akijiuguza, huku akifanya yake kila anapokuwa peke yake.
Alitafiti mpaka akapata jina lake kamili. Akafanya hivyohivyo kwa Kemi. Alishituka sana alipogundua kuwa Kemi ni mtoto wa Kasa. Akafikiria amemfikiaje yeye! Kwa nini aungane na Love katika kumuangamiza! Ndipo akajua wazi ni sababu ya kuwa na Jelini. Hasira zilimpanda Colins! Chuki ya ajabu dhidi ya Kemi ikainuka ndani yake. Akamuhamishia kwa haraka sana kwenye kundi la Love. “Hakika atalipa na dhambi za baba yake pia.” Colins akaapa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alipojiridhisha amepata taarifa zao kamili ndipo akarudi sasa kwa Love. Kwa kutumia IP addressya Love, akaingia kwenye kampuni anayofanyia kazi Love. “Hawakuwa wakiniita Guru kimakosa.”Akajipongeza alipoweza kuyafikia mamilioni ya pesa ya kampuni hiyo.
Hakuiba hata shilingi moja. Alichofanya, kwa kutumia hiyo IP address ya Love, kuonyesha kama ni yeye mwenyewe Love ndiye amefikia pesa ya kampuni, kwa kutumia kompyuta yake, akajihamishia pesa. Kiwango kilekile alicho muibia kutoka kwenye mshahara wake, si jumla yote ili asimshitue Love mwenyewe na hata wahasibu wa kampuni, akakigawa. Kiasi kidogokidogo kulinganisha na mamilioni ya kampuni, ila kiwango kilekile mpaka akatimiza kiwango alichomuibia kwenye kila mshahara wake. Ikawa amemrudishia Love, Ila akawa sasa Love ameibia kampuni yake na si Colins.
Alifurahi Colins, mpaka akajawa nguvu ya ajabu. Akili ilikuwa ikifanya kazi kiasi ya kwamba kila mafanikio yake yakamuongezea nguvu za mwilini. Akaitizama akaunti ya Love, na kucheka akimuhurumia.
Akatamani itoshe, lakini akaona aanze kulipiza kisasi chake kwa kupitia hiyohiyo tekinologia. Vita yake apigane kiteknologia bila yeye kuhusika moja kwa moja.
Akarudi tena kwenye kompyuta yake lakini akiwa kama Love. Kwamba akatumia tena IP addressya Love.
Usiombe kupigwa na anayekufahamu, halafu moyo wake umejeruhiwa, hakosei. Anapiga anapojua huwa panakuuma sana.
Kazi ya kuchota mapesa ya kampuni ya Love kumuhamishia Kemi na Mtumishi ikaanza. Na wao akaonyesha ni kama Love alikuwa akiiba pesa ya kampuni na kuwahamishia mamilioni ya pesa ila kwa wakati tofauti tofauti. Alicheza na tekinologia hiyo, kiasi ya kwamba hata kama uwe nani, ukiangalia, utajua ni Love ndiye aliyekuwa akiiba pesa ya kampuni na kujilundikizia yeye na kuwapa watu wake.
Mbaya zaidi, kuna ambazo zilionyesha ni kompyuta ya Love ya ofisini kwake pia alitumia kwenye kujihamishia pesa mwenyewe yaani akiwa ofisini kwake mida ya alfajiri kama anavyojua huwa anapenda kuwahi kazini. Love hajui kuchelewa popote. Akatumia na hiyo sifa yake kumuumiza.
Na pesa zingine alionyesha aliiba kwa kutumia kompyuta yake binafsi akitumia IP address ya nyumbani. Akaonyesha alikuwa akiiba pesa akiwa pia nyumbani Kigamboni. Hayo yote anayafanya yeye Colins, nyumbani kwa wazazi wake, kwenye chumba alichopewa hifadhi.
Alipotengeneza hayo yote kwa akili, na umakinifu akatulia sasa akisubiria za mwizi zije kufika 40ambayo alijua itachukua muda, kwa jinsi alivyofanya kwa makini. Lakini alijua ipo siku LAZIMA itajulikana tu.
Uchumba Si Ndoa.
Wote wawili walifika hapo kwenye hicho kimgahawa bila ya kuchelewa. Ila wote wakiwa na matarajio ya tofauti. Kwa hakika yeye Hope alitegemea ndio anarudishiwa pete yake. Huku Junior akiwaza jinsi ya kuhitimisha bila kuchafua kanisa la baba yake.
Wakasalimiana. Ila Hope akaanza kuingiwa na wasiwasi. Hapakuwa na uchangamfu. Akajipa moyo pengine bado alikuwa na hasira ila watatengeneza tu. Wazo la kuachana alijua wazi sio chaguzi kwa sababu alijua fika, Junior hatataka kutia doa kanisa la baba yake kwa kashifa ya kuvunja uchumba mkubwa vile.
“Unaendeleaje?” Akamuuliza kwa kujali. Junior akamtizama kama ambaye hajaelewa. “Nakuuliza maendeleo yako!” “Nzuri kabisa. Samahani tulishindwa kukutana siku ya alhamisi. Ratiba ziliingiliana.” “Naelewa kabisa. Hamna shida.” Akajibu kiuugwana, kitu ambacho si kawaida yake.
“Naomba nisikupotezee muda wako zaidi. Kuna jambo nataka tuzungumze.” “Hata hatuli!?” Akauliza na tabasamu akiwa ametulia. “Samahani. Unaweza kuagiza chochote unachotaka, acha na mimi nipate juisi.” Akaagiza supu na chapati. Junior akaomba juisi ya ukwaju. Wakatulia.
“Vipi lakini majukumu?” Siku hiyo Hope akaonyesha kujali haswa. “Tunaendelea. Sio vibaya. Unakumbuka tulipoanza swala la uchumba?” “Nakumbuka.” “Nilikuomba unichunguze na mimi nipate muda na wewe, tuone kama tunaweza kuja kuishi pamoja.” “Ushaona mapungufu yangu?” Akauliza kwa utani.
“Mapungufu, hapana. Wewe Hope ni mtu mzuri sana. Unampenda Mungu na utumishi upo ndani yako. Hata baba anasikitika kuacha kwako madaraka.” “Niliwaahidi nikiweka mambo sawa nitarudi. Nilijichanganya sana Junior, mpenzi wangu. Nikafika mahali nikawa hata mimi mwenyewe sijitambui, nakosea tu. Nikaona ni bora nitulie, nijitafakari kwanza. Kweli sisi ndio tunatakiwa kujipa kipaumbele. Sisi wenyewe tusipokaa sawa, hata tukiwa na mamilioni ya pesa, hatutakuwa na raha nayo.” Hapo napo Junior hakupenda. “Anawaza tu mali!” Akajiambia moyoni.
“Kwa hiyo kwa vyovyote tulivyo na chochote tutakachoshika, sisi kwanza. Yaani maelewano kati yetu, ndio mengine yafuate. Tujenge utaratibu mzuri wa kuwasiliana. Kama kuna kitu hupendi, tafadhali niambie Junior. Usikae nacho muda mrefu. Na mimi hivyohivyo.” Akawa amempokonya maneno. Hajui tena aendelee vipi. Akabaki ametulia akimsikiliza.
“Na nakuahidi safari hii itakuwa tofauti. Sitafanya jambo bila ya kukushirikisha. Na pia sitakuingilia kwenye mambo yako, labda utake mwenyewe ushauri. Mtindo wa kulazimishia mambo, naacha. Tutakuwa tukishauriana.”
“Halafu nimepanga kuandaa chakula kizuri kwa Ezra na Jelini. Waje pale kwako kwenye nafasi nzuri, tule nao pamoja ili tupate mwanzo mzuri kati yangu na Jelini. Na nitamuomba msamaha. Nafikiria jumapili hii ndio nifanye hivyo. Nikitoka tu kanisani, nikimbilie pale kwako, niandae kwa haraka, jioni ndio tukutane.” Junior akacheka. Ila jinsi alivyocheka, wazi alionekana si kwa furaha.
“Kwani na hapo nimekosea? Niambie tu.” “Huwa unamipango mizuri sana Hope. Inakuwa imekaa vizuri na mikakati inayoeleweka.” “Lakini?! Maana nimehisi kama kuna lakini hapo.” Junior akamwangalia kama anayetaka kugairi akiona haina maana tena, lakini akaona amwambie tu.
“Umetoka kuniambia kuanzia sasa utaanza kunishirikisha kwenye maamuzi yako. Hata dakika 5 hazijapita, unanipa mipango iliyokamilika, bila hata kuniuliza!” “Si ndio nimekushirikisha mpango mzima bila ya kukuficha na kukwambia tokea mwanzo kama una jambo useme usiweke moyoni!” “Umeniuliza kama nimekubaliana na mpango wako bila kujali ratiba yangu wala ya Ezra! Hatujaonana kwa takribani siku tatu sasa. Hujui nina ratiba gani, hujui kinachoendelea kwenye maisha yangu wala ya Ezra! Ndio tumekutana sasahivi, lakini tayari unaratiba yako, yangu na ya Ezra! Tena ambayo unataka sisi wote watatu, mpaka Jelini ambaye ni mgeni kwetu, tuifuate hiyo ratiba yako!”
“Lakini bado tulikuwa tukiendelea kuzungumza Junior!” Akafikiria, akaona haina maana tena. Moyo wake ulishahama kwa huyo mrembo, akili zipo kwa Emelda. Akatulia akifikiria.
“Basi nishauri wewe kitu gani chakufanya.” “Mimi sidhani kama unanihitaji kwenye mipango yako Hope.” “Nakuhitaji Junior. Nakuhitaji sana tu.” “Pengine hivyo ndivyo unavyodhani na labda kwa upande mwingine wa kukutekelezea hiyo mipango yako, kihali na mali, lakini si vinginevyo.” Hope akashituka kidogo.
“Kwamba unaona mimi nakutumia tu?” “Ninachotaka kusema ni hiki kilichotokea hapa sasahivi ndio imekua sehemu ya maisha yangu tokea naanzana na wewe Hope. Unapanga na kuendesha ratiba zako na zangu. Na wakati wote unazisimamia kuhakikisha nazifuata bila ya kukosea. Sikumbuki kwa wewe kuniomba ushauri kwa lolote, au hata mimi kukushauri jambo, ukalipokea kirahisi.”
“Wakati wote ninapokushari jambo, utalitolea kasoro na sababu, na hutafanya. Ila kutaka mimikukufanikishia lako bila ya kujali garama ya fedha, kama ninayo hiyo pesa kwa wakati huo au la. Na pia hutajali hata hisia zangu. Utataka nifanye tu.” “Nitab…” “Subiri kwanza Hope. Usijirudierudie ukitoa ahadi za kubadilika, kisha unafanya tofauti.” Kidogo akawa mkali kwake kumtuliza ili amsikilize mpaka mwisho.
Kweli akatulia. Akaendelea. “Ni kwa muda mrefu sana, tokea tumeanzana na wewe, mimi kupanga jambo langu na kulifanya kwa uhuru. Imekua ni shida, mpaka nahisi ninapoteza uwezo wa kufanya maamuzi yangu na kuyasimamia mimi kama mimi Junior na mtoto wa wakiume wa kwanza kwa mzee wangu. Maana mara zote wewe umekua ukinikosoa na kubadili kila mpango wangu. Hivyo si sawa kwako na kwangu.” Hapo akawa tofauti kabisa na Junior aliyemzoea. Hapakuwa hata na hisia za kimapenzi. Ikawa kama yupo mahakamani akitoa hukumu!
“Unauwezo mkubwa sana wa kufikiria Hope. Na uzuri, unajuhudi. Na kingine ambacho namshukuru Mungu, japokuwa unaongoza mambo mpaka yangu, kwa asilimia kubwa unapatia. Hilo nakupongeza.” Hapo akampuliza baada ya kumng’ata.
“Ungekuwa ni msichana mwingine na hiyo haiba yako, nafikiri ningeharibikiwa vibaya sana kwa kuwa nimekuwa nikikusikiliza kwa kila jambo na kufanya kwa kila namna ili tu kukufurahishawewe.” Kimya, Hope amepoa kabisa.
“Nimefikiria na kufika sehemu, nikatambua akili yako. Upo vizuri sana. Kiukweli hunihitaji mtu kama mimi, na mimi sipo tayari kuendelea kuishi maisha ya kuongozwa na wewe.” Hope akashituka sana.
“Nina ratiba yangu ya maisha. Na ramani ambayo niliiweka kabla ya wewe kuja kwangu. Nasikitika haijawahi kuendana na yako. Na mimi sipo tayari kubadili, na pia sitaki kukubadilishaHope. Hivyo ulivyo, wewe huna kasoro. Najua upo hivyo ulivyo, Mungu amekuumba hivyo kwa ajili ya mwanaume mwingine, lakini si mimi. Ukibadilika tu kwa ajili yangu, utajiharibia maisha yako, na sipo tayari kuona haiba nzuri kama hiyo inabadilika sababu ya ramani yangu ya maisha ambayo kwanza, sijui hata kama ulikuwa tayari kuifahamu. Na kwa bahati mbaya sana, hata kwa sehemu ndogo niliyojitahidi kuifunua kwako, ulionyesha wazi bila kuficha kuwa haupo tayari nayo.” Hope kimya.
“Nashukuru kunivumilia kwa muda wote huo, lakini naomba kusitisha swala la uchumba.” “Mmmh! Kwa hiyo unanipokonya vitu vyako vyote?” Hilo swali lilimuumiza sana Junior. Hakutegemea katika yote, hilo ndilo lingekuwa la msingi kwake.
“Tafadhali nifikirie Junior. Ukinitoa kwenye ile nyumba, au ukinidai pesa uliyonichangia kwenye gari…” “Nilikuchangia au nililinunua mimi na pesa yangu!?” Hapo akamtibua. “Lakini kumbuka mimi ndiye niliyelitoa bandari Junior! Japo niliweka pesa chache, ila kumbuka na mimi nimechangia.” Junior akacheka kwa masikitiko.
“Basi naomba niseme unifikirie. Na hata ukitaka nikulipe, nitakuja kukulipa, ila naomba muda.” Junior alipoona moyo wake upo kwenye vitu na si yeye akaumia, ila akafikiria kwa haraka, akaona katika hilo pia anaweza kulimaliza hilo kwa amani bila kutibua hali kanisani.
Akaona atumie mali zake kuleta amani. “Tunahitimisha uchumba Hope na si mahusiano. Sitegemei tuwe maadui kuanza kunyang’anyana vitu!” “Kwa hiyo hata pale ninapoishi hutataka niondoke?” Akamshangaza sana Junior. “Nitamwambia mwenye nyumba mkataba huu unapoisha, kama utapenda kuendelea kuishi pale basi mtaandikishana naye. Mimi najitoa kabisa kwenye hiyo nyumba.” Akaumia na kushindwa kunyamazia hilo, akaona aulize tu.
“Hivi kweli kwa muda wote umeishi na mimi Hope, umeshaniona mimi moyo wangu upo kwenye mali na si mtu?” “Sasa mtu si ndiye huyo mnaachana!?” “Tafadhali kuwa na amani. Hatugombani ila mahusiano yetu yanachukua sura mpya. Na kingine cha mwisho cha msingi. Usiache kumtumikia Mungu kwa ajili yangu. Wewe umeitwa na Mungu, Hope. Unayo karama na uwezo mkubwa sana wa kuendesha mambo na kukaa sawa. Usiache kumtumikia Mungu. Na pale usihesabu kama ni kanisa la baba yangu, hesabu kwamba ni shamba la Mungu na watenda kazi ni wachache. Unahitajika.” Akajishusha ili arudi kwenye nafasi yake, isijeonekana amefukuzwa kazi sababu si mchumba tena wa Junior. Hapo Junior akataka asimchafue baba yake au kumuharibia kwa watu.
“Kwamba wewe huna shida mimi niendelee kutumika pale na tumeachana!?” “Hata kidogo! Ile huduma hata mzee akiondoka leo, Mungu atanyanyua mtu mwingine. Na hilo baba amekua akilihubiri wakati wote. Yeye ni mtenda kazi pamoja na sisi. Pale ni nyumbani kwako pia Hope. Na tutafanya kazi pamoja kama zamani. Na safari hii ukirudi, nitahakikisha na wewe unalipwa maana unastahili kama wengine wote wanaofanya kazi pale na kulipwa. Unatoa muda wako mwingi sana pale. Unahitaji kuangaliwa na wewe.” “Kama ndio hivyo, sawa.” Junior hakuamini ikawa rahisi kuliko alivyotarajia.
Lakini akamtibua tena. “Maana hapa nilishaanza kufikiria kodi inayofuata ya ile nyumba. Nilijua ndio mwanzo wa kukimbia mji.” Akacheka kabisa kwa furaha. “Nakushukuru Junior. Kwa hiyo utazungumza kila kitu na mchungaji? Maana sitaki aone narudi sababu ya pesa.” Japokuwa alishamboa vyakutosha, akaona ahitimishe tu. Haina maana tena.
“Usiwe na wasiwasi, ukija kanisani kesho, utarudishiwa kila kitu chako.” Kwa hakika hilo lilimfurahisha Hope. Furaha ya pengo la msaada aliokuwa akipokea kutoka kwa Junior kuzibwa na mshahara wa pili atakao anza kulipwa kanisani, alishindwa kuificha kabisa. Alifurahi kupitiliza.
Junior akamuaga kuwa kuna majukumu mengine ni lazima akayakabili. Akamuomba waongozane kwenye gari akachukue vitu vyake. Hakuwa na shida. Akaomba muhudumu amfungie baadhi ya vitafunwa alivyomtajia. Wakatoka hapo kuelekea garini kwake.
“Naomba usinielewe vibaya Junior.” Junior akamtizama. “Naulizia na swala la gari. Maana umesema sio kwamba unaninyang’anya vitu ulivyonipa. Inamaana na gari si unaniachia?” “Mbona unawasiwasi sana wa hilo gari Hope!? Ni nini?!” “Sio wasiwasi ila ni kutaka tu kuweka mambo sawa.” Akabaki akimtizama Junior kama anayetaka akumbuke kitu.
Na yeye Junior akabaki akimtizama kama hamuelewi lakini alishamkera vyakutosha. Hope akajikaza na kuchangamkia. “Nazungumzia gari bado ipo kwa jina lako. Sasa kwakuwa tumehitimisha na umesema hutaninyang’anya kitu. Ikiwepo na gari, nilikuwa naomba na kadi ya gari unipe na tubadilishe kabisa jina.” Junior alichoka mpaka uso ukanyongea.
“Ni kwa nia nzuri tu ili kuweka mambo sawa. Tena tunaweza tumia kijana yuleyule ambaye alitusaidia kulitoa. Anaonekana anafahamiana na watu wengi sana TRA.” “Sawa.” Akajibu tu hivyo na kufungua gari yake.
Akamkabidhi vitu vyake, baadhi akamsaidia kubeba mpaka kwenye hilo gari analodai. Akamsaidia kuvipanga. Akajua amemaliza. Wakati anataka kurudi garini kwake akamuwahi. “Kwa hiyo nitegemee hiyo kadi ya gari na vitu vingine kesho kanisani? Maana hata funguo yake ya pili bado unayo.” “Tutawasiliana Hope.” Akaondoka akiwa ameumia asijue anaumizwa na nini!
Pengine kudhania alikuwa anakwenda kumuacha Hope, lakini akagundua hata huyo Hope hakuwahi kuwa naye. Hope alikuwa na mipango yake ya maisha na yeye akajiongeza kwenye maisha yake, akafanyika msaada uliomsogeza kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Basi.
Alitaka uchumba uishe kwa amani, akajikuta yeye ndio hana amani. Hope hana wasiwasi. Ikawa kama amekutana na Hope mwingine kabisa. Hakuonekana kupoteza chochote kile kati yao, ila hakutaka kuvunjika kwa hayo mahusiano, kumrudishe nyuma kimaendeleo. Alionyesha wazi kuachana kwao si tatizo ila abakiziwe mali. Tena hakuuma maneno. Hope akachangamkia kwa nguvu zake zote bila ya kulazia damu.
Hilo likamuuma Junior kuona alidhania alikwenda kuvunja, kumbe hapakuwepo na chakuvunja. Maana tokea mwanzo wawili hao kumbe hawakuwa wameungana! “Hope hajawahi kunipenda kabisa!” Akaendelea kusononeka akirudi kwake ila Hope akiwa na tumaini kama jina lake. Maisha yataendelea vizuri. “Hapa ni kujipanga tu. Na hivi pale kanisani wataanza kunilipa! Siwezi shindwa kujitegemea. Wala maisha yangu hayatayumba. Asante Mungu wangu, umeona juhudi zangu, umenilipa kwa wakati wako.” Wakati Junior analizwa na yake, yeye Hope amepokea muujiza wake. Mshahara wa kazini na wa kanisani! Tena kanisa la baba Junior! Anajua watu huwa wanalipwa pesa nzuri tu. Sasa leo na yeye atakuwa miongoni mwao! Akabaki akimtukuza Mungu wake na yeye akirudi kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alichotamani Junior anakipata. Mambo yanaweza isha kwa AMANI kabisa kama alivyokuwa akitamani. Ni kiasi cha yeye kukabidhisha funguo za gari na kadi ya gari kwa kukubali kusaini karatasi kisheria, kuonyesha amemkabidhi Hope gari. Litoke kwa jina lake liwe la Hope moja kwa moja. Basi. Hope hana jingine. Ashindwe yeye tu.
Na yeye hakuwa na shida na hilo gari, lakini jinsi alivyodaiwa, ubinadamu ndani yake ukanyanyuka. Hasira! Uchungu kuona alikuwa akitumiwa tu! Hope hajaumia kuachwa! Vyote hivyo vikamfikisha kwenye his last nerve. Akawa amekereka kupitiliza. Hajui tena chakufanya.
Kila Jambo Na Wakati Wake.
Hakutaka kuendelea kujichelewesha. Palepale Mgahawani alipokuwa na Hope, alishaagiza vitafunwa. Sambusa, chapati, kababu, egg chops, na bajia nyingi tu. Akaomba afungiwe vizuri na kuondoka akiwahi nyumbani aandae mazingira ya kufika Emelda. Ukweli alibeba kila kitu cha Hope alichoacha kwake na kumrudishia. Hakutaka apate sababu ya kurudi kwake.
Wakati anaingia getini akamuona Emelda amekaa kwenye ngazi. Alishituka, hakutegemea. Maana ndio alikuwa ametuma dereva kwenda kumchukua. Akivizia kwamba mpaka awe amerudi naye atakuwa ameshaandaa mazingira ya pale.
Akaongeza mwendo karibu agonge. Lakini kadiri alivyokuwa akimsogelea, ndio uchungu ulivyokuwa ukipungua kwa furaha ya kumuona. Akaegesha gari na kushuka kama akimbie. Emelda akasimama wakati akipandisha ngazi.
“Shikamoo kaka.” Akasalimia kwa heshima akitaka kumpokea. “Pole umekaa juani! Sikujua kama utakuja sasahivi! Maana ndio nimemtuma dereva akufuate.” “Ni mama huyo! Na mimi nilimwambia tusubirie maana ulisema utatuma dereva, akasema niwahi, wewe hupendi kuchelewa. Akamwambia Noah anilete!” Junior alifurahini nusura ashangilie, ila akajikaza. Akabaki akiwaza. Maana huo ulikuwa ujumbe mzito sana kutoka kwa mama yake. Na alijua amefanya makusudi kama kumwambia ana baraka zake.
Sasa kwa vile alivyokuwa amekerwa na Hope, usoni hakuwa sawa. Mbaya zaidi hapo akanyamaza akimtafakari mama yake. Ikamtia wasiwasi Emelda ambaye anamfahamu huyo Junior kwa kumwangalia hata kwa mbali, atajua tu kinachoendelea ndani yake. Iwe ni huzuni, hasira, furaha au hata kuchoka, Emelda atagundua tu hayupo sawa au kila kitu kipo sawa. Na hapo akamsoma hayupo sawa, akajua ni kufika kwake hapo mapema.
“Samahani kama nimeharibu ratiba. Naweza nikarudi baadaye.” Emelda akamtoa kwenye mawazo ya furaha yanayozidi kumtuliza roho iliyokuwa imechafukwa. “Hapana! Nimefurahi upo hapa. Ila sikutaka ukae juani ukinisubiri! Na ningejua kama utafika kabla yangu ningekuachia nyumba wazi. Pole.” “Hamna neno, kaka. Acha nikupokee.” “Hapana. Leo nataka mimi ndio nikutumikie.” Emelda akacheka kwa aibu.
“Wewe mgeni wangu leo. Na nataka unitume chochote unachotaka. Hata maji ya kunywa ukitaka, nitume.” Akacheka na kujificha uso. Kisha akamuuliza. “Kwa nini sasa?” “Kwa sababu kuanzia leo, na mimi nataka kukutumikia kama wewe. Najifunza kutoka kwako.” Akawa anamwangalia, akaona aibu na kujificha nyuma yake. Junior akacheka na kuongoza njia.
“Twende ndani nikakuandalie brunch nzuri! Au unanjaa sana hutaweza kusubiri?” “Hapana. Nitasubiri, hamna neno.” Akafungua mlango akamkaribisha akiwa anamsubiria mlangoni. Akampita. “Umependeza Emelda!” Akazidi kumpa wakati mgumu. “Umependeza sana.” “Asante. Ni nguo ameniachia dada Ester.” “Basi na hiyo imekukaa vizuri. Dawa imesaidia kidogo?” “Imesaidia ndio maana nimeweza hata kufunga nywele. Asante kwa kunifikiria.” Akafurahi huyo Junior, kwamba amejipatia pointi.
“Twende unisindikize jikoni. Nisubirie wakati natengeneza chai na kukaanga firigisi na maini.” Emelda akaacha kipochi chake sebuleni na kumfuata jikoni. Akakuta amemuandalia glasi ya juisi, na sambusa moja. “Kula hivyo kidogo wakati napika.” “Kweli hutaki nikusaidie hata kidogo!?” “Hapana. Utanipokonya furaha yangu yote ya leo. Leo nataka mimi ndio nikutumikie.” Akacheka kama mwenye maswali anayeshindwa kuuliza. Akakaa.
“Nashukuru kaka.” “Kwa nini tena!?” “Kwa hiki chakula, kunikaribisha kwako na kunipikia. Asante.” “Karibu japo kwa kuchelewa. Nafikiri ilitakiwa iwe mapema zaidi ya leo. Najihisi nimejichelewesha mwenyewe. Ila hata sasa, karibu.” Akamfanya Emelda ashindwe kujibu. Akaanza kuandaa vitu vyakupika ila akamuona kama aliyekumbuka kitu na uso kunyongea tena.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Ni nini kimekuudhi?” Junior alishituka, hakutegemea. Alijitahidi kuficha kinachoendelea ndani yake na hapo anamuuliza akiwa anakusanya vitu sio kwamba walikuwa wamekaa karibu wanaangaliana na kuzungumza. Alipotelea mawazoni akijishugulisha, akijua Emelda anakula.
“Nipo sawa Emelda. Umependa juisi?” “Nimependa juisi ila najua kuna kitu kimekuudhi. Pole.” Aliongea kwa upendo na kujali, ila kwa uhakika kama anayemwambia nakufahamu kwa kukuangalia tu. Ilimgusa Junior mpaka akasimama kama anayefikiria kitu. Kisha akamwangalia. “Na mimi naomba kukufahamu zaidi Emelda.” Kisha akasaidia kufafanua.
“Najua yupo mama na wadogo zako wawili. Baba yuko wapi? Wadogo zako wapo na umri gani? Wanasoma? Unao ndugu wakubwa? Bibi, babu na ndugu wengine. Umesomea wapi? Mpaka elimu gani? Mbali na unachofanya sasahivi, ulikuwa ukitamani kufanya nini? Na kingine chochote unachoona kitanisaidia kukufahamu zaidi.” Emelda hakutegemea.
Akacheka kwa wasiwasi. “Vipi? Maswali ni mengi sana?” “Hapana.” Kisha akatulia. “Tuna siku nzima pamoja. Hamna haraka.” Akamuona amenyamaza tu. Akamuacha.
“Umependa sambusa?” Akavunja ukimya maana hata hakuwa akila tena ila akichora chini kwenye maji yaliyochuruzika kutoka kwenye glasi ya juisi. “Asante kwa chakula.” Junior akacheka kama kumtuliza. “Ulishashukuru bwana! Ila hauli!” Ndipo akang’ata sasa sambusa.
“Ni nzuri! Wewe umekula?” “Nazifahamu. Ezra ndio mpenzi sana wa vitafunwa vya pale.” Akaanza kula sasa. Junior akaendelea kupika.
Ila akamtumia mama yake ujumbe. ‘Nakushukuru sana mama yangu. Asante.’ Mama yake akamjibu bila ya kuchelewa. ‘Utafanikiwa tu. Nakuombea.’ Junior alifurahi huyo. Hata hayo mawasiliano hapo kati yake na mama yake, yalibeba maana kubwa sana. ‘Amina mama.’ Akajibu na kuendelea kupika, furaha imejaa moyoni. Ndipo akamkumbuka bibi harusi mwenyewe.
Akamtizama, macho yakagongana. “Picha ya baba uliyonayo wewe, vile anavyowapenda nyinyi na kuwajali. Anavyombembeleza dada Ester kama katoto kadogo sio kama baba yetu.” Junior akacheka taratibu akimsikiliza. Alielewa anachozungumzia. Ester alipendwa na baba yao na kumlinda kama mboni ya jicho lake.
“Na taswira ya maisha ya pale kwenu sio kama kwetu, ndio maana sijui nikueleze vipi ili uelewe.” Akaendelea taratibu. “Unaweza usiamini hili, lakini mimi nayajua maisha ya kila namna, tena kwa kuyaishi.” Ikamuia ngumu Emelda kuamini. Akamuelewa.
“Wewe umeanza kuishi na sisi maisha yakiwa yamebadilika sana. Ni Noah peke yake ndiye aliyezaliwa kwenye aina ile ya maisha na kwenye ile nyumba pia. Ester naye amekua angalau akakuta maisha ya wazazi yameanza kuwa na aghueni. Lakini mimi nimezaliwa kwenye maisha na mazingira duni sana. Na nikakua kwenye aina hiyo ya maisha mpaka nina akili zangu kabisa. Hata Ezra tumeanza kuishi naye wazazi wakiwa bado maisha yanasumbua. Na hatukuwa tukiishi pale. Kwa hiyo huna lugha ya kuongelea maisha yeyote yale nikashindwa kuelewa.” Emelda akabaki akifikiria.
Wazazi wa Junior wanaishi kwenye jumba linalokaribia kufanana na vijana wao, sema yao ni ramani ya kawaida na hawakuweka vitu vya thamani kama hapo kwa vijana wao. Ila huyo Emelda anaishi kwa mchungaji geti kali. Jumba la kifahari kwelikweli. Na jinsi walivyo utafikiri walizaliwa kwenye hizo mali. Si malimbukeni hata. Kama waliozaliwa kwenye neema na kukua nayo. Familia nzima hata huyo Noah aliyesema amezaliwa kwenye mazingira hayo, ukikutana naye sehemu, unaweza usidhanie anatoka kwenye aina ile ya maisha. Ester naye yupo hivyohivyo. Wakiongozana na Emelda, unaweza sema ndugu wa damu. Mnyenyekevu kama mama yao. Mali zao hazijawabadilisha. Ngumu hata kufikiri kwamba wamekutana na hizo mali ukubwani!
~~~~~~~~~~~~~~~
IPI HISTORIA YA EMELDA?
Je, Junior atamaliza vipi uchumba?
Adhabu za Colins akiwa anaendelea kujiuguza inaendelea. Usiache kumfuatilia Faru aliye jeruhiwa.
0 Comments:
Post a Comment