Kwa Mara ya kwanza Jelini nyumbani kwa Ezra.
Alimrudisha nyumbani mtoto mapema tu. Akaanza maandalizi ya
kwenda kwa Ezra. Kama kawaida yake, hakuna makosa kwenye mwili wake.
Akajitengeneza vizuri mpaka akaridhika. Ndipo akampigia simu kumwambia yupo
njiani kwenda. “Nitakuwa na wewe kwenye simu, ili
usipotee.” “Nashukuru.” Akamuelekeza mpaka akafika kwa Junior. “Sasa kuwa kama unazunguka ukuta wa Junior kwa mbele. Nyumba
zimepakana kabisa.” Jelini akacheka. “Nyinyi
wawili sijawapatia mfano wenu!” Ezra akacheka akitoka ndani ili
kumsubiria.
Kampuni ya ulinzi inayolinda kwa Junior ndio hiyohiyo
akakuta sare zao hapo getini kama alivyokuta kwa Junior, ila wamemfungulia geti
kabisa kama waliokuwa wakimsubiria yeye. Jelini mwenyewe akacheka akiwatafakari
mapacha hao wa nje. Akasalimia hapo getini na kuvuta gari ndani. Akamuona kwa
mbali kwenye ngazi za kuingilia ndani kama anayemsubiria.
Akasogeza gari mpaka karibu yake, akaenda kumfungulia mlango
na kubaki akimtizama. “Mpaka naona vibaya kukugusa Jelini!” “Kwa nini tena?!”
“Jinsi ulivyopendeza na kuvutia! Unaonekana wa thamani sana. Mpaka nahisi
nikikugusa nitakuchafua!” “Basi ujue nakutengenezea kitu kizuri chakushika.
Wewe hustahili kushika vitu vibaya. Vizuri tu. Ndio maana.” Akamdaka kwa uchu wote. Likawa kiss la
msamaha, karibu nyumbani, na nashukuru kunipenda. Kiss kilo likavuta kwa
muda wake wakutoshea tu, ndipo akamuachia.
“Nimefurahi umetenga muda kwa ajili yetu.” “Na mimi
nimefurahi umenikaribisha kwako.” “Karibu sana.” Akamshika mkono kumuongoza
ndani.
Kila kitu, kuanzia nje mpaka kitasa kweli ilikuwa kama kwa
Junior. Utafikiri upo nyumbani kwa Junior! Jelini akaanza kucheka alipoingia
ndani. “Ni nini?” “Mimi uliponiambia nyumba zenu zinafanana, nikajiambia
pengine thamani za ndani, labda makochi ni tofauti. Kwamba nyinyi mpaka makochi
vinafanana!” Ezra akaanza kucheka.
“Imekua kama kasumba. Junior akinunua kitu, au mimi, hata
wazazi imekua hivyohivyo, lazima kununua viwili. Wakijua kimoja changu na
kingine Junior. Huna kitu utaona humu ndani, kisiwepo kwa Junior. Zaidi vitu
vikubwa. Na vyombo.” Akafikiria. “Na baadhi chumbani. Maana mama huwa anapenda
sana mashuka. Kwa hiyo yeye ndiye mleta mashuka.” Akafikiria zaidi. “Hata
mapazia na..” “Mimi nahisi ni kila kitu.” Ezra hana mbavu.
“Karibu. Hapa ndio nyumbani.” “Asante. Ila nyinyi hamfananii
na uhalisia wenu, kabisa! Kuna nyumba nilishaingia. Nikaishangaa nikidhani ndio
nyumba nzuri ya mwisho nitakuja ingia hapa mjini, ila nimekutana na hizi zenu,
nimewanyanyulia mikono! Hongera Ezra.” “Asante. Sasa twende nikupe tour.
Upafahamu vizuri.” Akamzungusha humo ndani, Jelini mwenyewe akapakubali.
Kisha akamrudisha sebuleni akiwa amemshika mkono na
kumuongoza kwenye kochi. Yakaanza tena makiss mengine, maana alishamuona
Jelini amebabaika mpaka akajuta kumzungusha humo ndani. Alimkiss kwa
kumkumbatia kwa muda mrefu mpaka akasikia sauti ya Junior ikimuonya. “Usije
zidisha.” Ezra akaanza kumuachia taratibu maana ni kweli alikuwa anaanza
kuzidisha. Na alivyo Jelini, alishalegea hapo mikononi mwake. Akawa anamalizia
taratibu juu ya midomo, mpaka wakatulia.
Akabaki akimwangalia na kumwambia kwa upendo kama
anayebembeleza. “Naomba zawadi yangu.” Jelini akacheka akijitoa hapo mikononi,
ila alijawa wasiwasi sana. “Naamini utapenda.” Akavuta pochi yake na kutoa
vimfuko viwili, vilivyofungwa vizuri. Ezra akabaki kusubiria kwa hamu.
Akamkabidhi vyote. “Kila moja ina herufi ya majina yenu.” Akamkabidhi kama
aliyemaliza. Ezra akapokea akijua anaficha hiyo ingine.
Akafungua na kukutana na cufflinks nzuri sana,
maalumu kwa mashati yasiyo na vifungo vya mikono. Wenye umaridadi hununua
mashati hayo maalumu na kuweka hizo cufflinks zinazoongeza umaridadi.
“Ni nzuri sana. Na zinaonekana zimekugarimu, maana na mimi huwa napenda sana
kununua. Asante Jelini.” “Karibu. Nimefurahi kama umependa na kama zitawafaa.”
Ezra akabaki kuziangalia akizegeuzageuza kwa kuvutiwa nazo ila akitafuta jinsi
ya kudai ingine.
Akamwangalia akakuta ametulia tu. “Asante.” “Karibu.”
Akacheka kwa wasiwasi kama anayejaribu kujituliza. “Nasubiria zawadi yangu ile
uliniambia ungenipa kama si kukuudhi.” “Hapana. Sio kuniudhi. Ila sitaki
unielewe vibaya. Ukadhani labda nakurupuka. Au kwa kuwa nimekuona upo vizuri, nyumba
yako nzuri, halafu nikawa nimeshasema sijawahi ishi gorofani, ndio maana nataka
kukufunga. Sikuwa nimefikiria vizuri. Ndio maana naona hiyo ifae tu. Nisiwe
kama wale wanawake wanaolazimishia mambo kwa wanaume ili wajinufaishe wao tu.”
Akaongea sana akijitetea kwa hofu.
“Kama ningekuwa kama ulivyonifikiria. Kwamba mimi ni mission
town. Siishi kwenye mazingira kama haya, ungenipa na kuniambia nini?” Jinsi
alivyouliza kwa kutulia bila paniki, ikamfanya Jelini atulie. Akavuta pochi
yake. Akatoa kimkebe kama kilichotoka kwa sonara. Akakishika kwa mikono yake
yote miwili, ila akaonekana kama anatetemeka. Ezra akafikiri pengine ni pete. “Sasa
itakuwa ya ndoa! Maana wanawake hawachumbii!” Akajiuliza akiangalia kile
kimkebe kizuri tu chakuvutia kwa macho.
Kisha akamtizama na yeye, akagundua anajishauri. Akahisi
anatafuta jinsi ya kubadili alichotaka kumwambia. “Tafadhali usibadili
kitu cha kwanza ulichokusudia kuniambia wakati ukinipa. Usirekebishe wala
kutengeneza. Niambie vile ulivyokusudia mwanzo. Na nakuahidi kwangu upo
salama.” Akamuona kama anatulia.
“Nilitengeneza cheni yenye majina yetu.” Ezra akatoa macho kwa hamasa. “Lakini nilitaka kukuomba ufikirie kwanza kabla hujaivaa. Unaweza kuiweka usiivae mpaka ukawa tayari na ombi langu, na ukishindwa unaweza nirudishia tu, usivae.” Akaendela taratibu akijihami. “Nilitaka kukuomba kama unaona nafasi kati yetu ya mpaka uzee wetu, ndio uvae.” Akamtizama kwa hofu. Alipomuona ametulia, akaendelea. “Na kama utaivaa, basi ilete maana. Kwamba kila ukiiona au ukiikumbuka ipo shingoni kwako, umkumbuke Jelini tu. Na asiwepo mwanamke mwingine unayemfikiria ukijua mimi nipo, ni wako na nakuhitaji wewe. Lakini sio kwamba nataka kukufunga ili…” Ezra akamuwahi midomo kwa kumvamia kwa uchu kama ambaye ameamsha kitu ndani yake.
Jelini akaanza kucheka akijivutia kwake zaidi akifurahia
kwamba hajamfikiria vibaya. Amependa. Akambusu kwa muda wa kutosha. Wakanogewa.
Jelini akazidi kujiachia hapo kochini maana hisia zilipitiliza, Ezra naye hisia
zikaendelea kupitiliza. Jelini mtamu mikononi bwana! Harufu nzuri na
mihemo akipata midomo mitamu sawia, vikamfanya Ezra kuhama kabisa kihisia. Hapo
alishasahau amri zote za Mungu, ila penzi la kimwana Jelini.
Uzuri alishaweka ulinzi kwenye maisha yake. Wanalindana hata
kiroho, siku hiyo ikasaidia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Simu ya Ezra ikawatoa kwenye hiyo hali. Kwa upande fulani
akashukuru sana Mungu. Akamuachia Jelini akihema, na kusimama kuifuata mezani.
Alikuwa Junior. Akatulia kwanza ili pumzi zikae sawa, ndipo akapokea. “Nimepata dessert, naweza kuwaletea?” Alijua
wazi hilo sio lengo, ila alishukuru sana nafsi mwake.
Hawa wawili walilindana kiroho tokea wanafahamiana. Kila mmoja akawa mlinzi wa mwenzie. Na kwa kuwa Ezra alishavuka mpaka wa kumkiss Jelini, Junior akaongeza umakini kwake. Hakutaka kosa litokee kwa rafiki yake. Ikawa kama Roho wa Mungu amemshitua Junior kuwahi. Maana Ezra alishafika hatua ambayo, kama Junior angechelewa kidogo tu, pengine wangeharibu. “Aisee nakushukuru sana. Njoo.” Junior akacheka vile alivyoshukuru maana alimuelewa alicho maanisha. Akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Junior anatuletea dessert. Kuna sehemu tunapata dessert
nzuri sana.” “Afadhali aje nimpe na zawadi yake.” “Kwanza naomba yangu.
Nimefurahi Jelini!” “Sasa umefurahia nini? Mwenzio naona ni kama sikufikiria
vizuri!” “Nisikilize Jelini. Mimi nimemaliza kwenye swala la kutafuta.
Sitarajii kuanzisha mahusiano mengine mbali na wewe, na mimi najijua. Ni kama
Junior tu. Hatuna udhaifu kwenye eneo hilo.” “Wanawake?” Jelini akauliza.
“Tamaa za wanawake au tamaa kwa ujumla wake. Kitu
tunachotaka, tunahangaika kukipata kihalali. Na tukishapata, tukajua ni chetu, tunaridhika
nacho na kutulia kabisa. Nini nataka kukwambia?” Jelini akajiweka sawa
kusikiliza. “Kwenye haya mahusiano yetu, mimi na wewe, mimi binafsi nimemaliza
na kufunga kabisa. Sijawahi na sitarajii kukifanya hichi ninachofanya na
wewe kwa mwanamke mwingine tena.” Hapo akamchanganya Jelini. Kwamba na mchumba
wa kwanza hawakuwa wakikiss! Akajiuliza na kutulia.
“Kwako imekua tofauti. Nakupenda Jelini.” Ikawa kama
anayemjibu mawazo yake. “Na natamani nisije shika mwanamke mwingine tena
hivi. Kwa hiyo nikikusikia na wewe unajifunga kwangu kwa kiasi hiki,
hujui inanifariji kwa kiasi gani. Inanituliza na kunihakikishia
kuwa sijakosea hata kukushika hivi na kuwa wewe ndio mwanamke wangu wa kwanza
kukukiss.” Hapo Jelini akatoa macho waziwazi na kumfanya Ezra acheke.
“Ezra!” “Hukumbuki nilikwambia niliokoka nikiwa kidato
cha kwanza, na kumbuka nilitokea kijijini?” “Sasa na mchumba wa kwanza!?” Ezra
akafikiria kwa muda akawa kama amekosa jibu. “Labda nikwambie kuwa, hakuwa kama
wewe.” Jelini akawa hajaelewa. “Vile unavyomuona Hope, ni kama kwa haiba
wanafanana kidogo. Si watu wa kuweka mikononi.” Jelini alicheka. Akacheka mpaka
akajifunika na mto.
“Wewe unapenda mikono, Jelini. Msichana kama Hope ni mipango
wakati wote. Mnunue nini na mfanye nini. Au umsaidie nini. Wapo kiuchumi
zaidi. Wakati wote mkikaa wanafikiria kitu cha kufanya tofauti na wewe,
unamfanya mtu anatulia na kupumzika. Rahisi kufikiria upande mwingine wa
mapenzi. Huna mahitaji ya kufanya mtu afikirie kiasi cha pesa cha kukupa.”
“Kwani ulikuwa ukimsaidia kifedha?!” Ikamchanganya tena. Maana alisikia hata
Hope amesoma na anakazi nzuri. Anasaidiwaje tena!
“Unafikiri kwa nini nilichanganyikiwa? Maana hata nauli
yenyewe ya kwenda huko ni mimi nilimpa. Na pesa ya kuanzia maisha huko
pia nilimpa, nikijua nawekeza kwenye ‘chetu’, kama unavyopenda kusema
wewe. Sasa kuja kusikia tena amepatikana mwanaume mwingine, mimi tena sipo
kwenye picha, ndio kujua kumbe nilikuwa nikijenga kwenye mchanga, na
mapenzi ya dhati hayakuwepo tangia mwanzo, nilikuwa nikichezewa tu.” “Pole
Ezra.” Mara kengele ikalia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Junior huyo!” Akaenda kumfungulia. Akasikia wakinong’ona.
“Aisee nakushukuru. Umeniokoa kupita nitakavyokueleza. Hakika ungechelewa,
ningeharibu vibaya sana.” Jelini hakuwa akijua au kusikia wanachozungumza. Ila
akasikia Junior akicheka sana wakiwa wanamfuata sebuleni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akasimama walivyofika pale. “Kama kawaida yako, umependeza.”
“Asante Junior. Nimefurahi kukuona. Nikupokee? Boski lenyewe linavutia!” “Na
vilivyopo humo ndani vinafurahisha pia. Nilitaka mlo wako wa kwanza hapa, ukamilike
na uufurahie.” “Hapa nimeshafurahia! Si tutakula pamoja?” Junior akashangaa,
hakutegemea. Akamwangalia Ezra na kusema. “Sitaki kuwaingilia. Huu usiku
ni wenu.” “Basi nikwambie, utakuwa unapitwa. Ezra mwenzio ameniandalia
chakula kizuri. Na nina zawadi yako nzuri.” Wote wawili wakacheka.
“Unauhakika Jelini? Sitaki kuwavurugia.” “Kwanza nataka uwe shahidi
yangu. Acha nikupokee kwanza, halafu nije nikwambie kitu.” Akampokea. “Asante.”
Ezra na Jelini wakashukuru kwa pamoja. “Karibuni sana.” Akamkabidhi hilo boksi
lenye dessert, Jelini akawa mwenyeji akikumbuka jikoni. Akapeleka huko,
huku akipaangalia mara mbilimbili jinsi palivyo pazuri na kuvutia. Alidhania
kwa mzee Kasa ni pazuri, akakutana na vijana hao waliotulia, wanajituma
kanisani mpaka kufuta viti halafu sasa ni wa kisasa. Kila kitu hapo
ndani kwao ni kizuri na chakuvutia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anarudi akasikia wakinong’ona tena. Akajichekea
nafsini kwake. “Hawa wapo kama watoto!” Akawafikiria akisogelea
alipowaacha sebuleni. Akakuta bado wamesimama. “Ezra ameshindwa kukushawishi
ubaki?” “Hapahitajiki nguvu nyingi kunishawishi kubaki. Sina chakula cha usiku,
kwa hiyo acha tu ni doee kwa watu.” Wakacheka sana jinsi alivyozungumza
kama mtoto wa mtaani mtaka kula kwenye majumba ya watu, wakaa.
Shahidi.
“Mimi shahidi mzuri sana, Jelini.” “Na huruki watu?” Wakacheka
sana jinsi alivyouliza. “Sitakuruka.” “Hata ikiwa kati yangu na Ezra?” “Mimi ni
mwenye haki wa Mungu. Na Ezra ananijua. Akikosea huwa namwambia waziwazi.”
Jelini akacheka. Akatulia kidogo, wakaona anaanza kuogopa.
“Chochote unachotaka kuniambia mimi, ujue kipo salama
Jelini. Usiogope.” “Umejuaje!?” Akauliza akicheka kama anayetaka kujituliza.
“Usiogope.” “Haya. Unakumbuka siku ile usiku nilikwambia na mimi nitakuwepo
sana kwenye maisha ya Ezra. Nikakuomba na wewe uwe unamkumbusha asiniumize?”
Junior akacheka na kujibu. “Nakumbuka.” “Sasa mwenzio ameniahidi nitabaki
peke yangu.” Wakacheka sana, kama ambao hawakuwa wametegemea aseme hivyo.
“Jelini!” “Kweli tena. Na ndivyo ninavyotaka. Ukimuona tu
anaanza kumfikiria mtu mwingine, mkumbushe yupo Jelini.” “Japokuwa nina
uhakika na Ezra kwa asilimia 100. Kwa kuwa namfahamu na yeye kama ninavyofahamu
kiganja changu, kwamba hatatafuta mtu mwingine, na leo nakuibia siri, Ezra
anakupenda sana Jelini. Sana.” “Kweli?” Akauliza kwa deko akimtizama
Ezra aliyekuwa ametulia akiwasikiliza, kwenye hilo kochi walilokuwa wamekaa
pamoja.
“Nakuhakikishia. Anakupenda kwa asilimia zote
utakazotaka kujihakikishia. Anakupenda kwa moyo wake wote. Na nakuhakikishia,
kama hutabadilika, jua utabakia peke yako daima.” “Mimi sibadiliki. Ujue
nilikuwa nikitamani mtu kama Ezra?” Junior akacheka akimsikiliza.
“Mtu mwaminifu, halafu nataka nibaki peke yangu.” “Nakuongezea
kitu kingine, ujue kwa Ezra utajaliwa sana, na utapendwa kupita
utakavyofikiria. Kwa kuwa Ezra anakua akikufikiria wewe tu, wakati wote.
Mimi ni shahidi. Usiwe na wasiwasi, na ndipo inapokuja ahadi yangu kuwa,
mimi nitakuwa shahidi wako daima. Ila ujue mimi nasimamia haki Jelini.
Sitapendelea kati yako au Ezra. Nitakuwa mkweli kwenu. Si naruhusiwa?” “Mimi
hivyo ndio nataka.” “Basi umejipatia shahidi.” Akacheka na kufuata tena kile
kimkebe.
“Nilimtengenezea cheni ya majina yetu, kama kumkumbusha
‘sisi’. Sasa sijui ni sawa kwa wadhifa wenu pale kanisani halafu akaonekana
amevaa cheni yenye majina yetu?” Akawa tena na wasiwasi akimuuliza Junior.
Wawili hao wakaangaliana. “Mimi nafikiri si tatizo. Itakuwa kama pete ya
uchumba kwake, watu wajue amejifunga kwako.” Jelini alifurahi huyo!
“Basi ni vile sijawazoea, bado nawaogopa. Ila
ingekuwa ni watu wengine, ningesema hivyohivyo kwamba ni kama mimi nakua namchumbia
Ezra.” Walicheka mpaka wakacheka. Akajifunika na mto wa makochi. “Jelini!”
“Kweli tena. Sema mimi nawaogopa, ndio maana sitasema hivyo.” “Kwamba
unamchumbia Ezra?” “Sasa hayo ni maneno gani na wewe Junior, mwanamke kumwambia
hivyo mwanaume? Si ndio maana sisemi!” Hawana mbavu.
“Basi usiseme Jelini. Ibaki tu siri yako. Ibakie kuwa ni
kumbukumbu, kumkumbusha kuwa Jelini yupo.” “Mimi naona ibakie tu hivyohivyo. Na
ingekua ni kuchumbia, ningemvalisha mwenyewe.” Ezra akacheka zaidi akitingisha
kichwa. “Ila nafikiri ukimvalisha ndio italeta maana kabisa.” “Eti eeh!”
Eti akafurahia hilo wazo. “Kabisa. Aikumbuke hii siku, ili siku tukimkumbusha
akumbuke kwa urahisi. Na mimi nashukua video kabisa, nije niwaonyeshe
mpaka watoto wenu.” “Mimi ndio maana nampenda Junior.” Wakazidi kucheka. “Nitakupa
zawadi nzuri, tena sana.” “Nashukuru Jelini.” Basi akasimama akitaka kumvalisha
ila Ezra akamuwahi.
“Naomba kwanza niishike mkononi kabla hujanivalisha.
Inaonekana nzuri sana na pesa nyingi.” “Sisi tunapenda vitu vizuri sana.”
Wakaanza kucheka tena. Junior na yeye akasimama kuiangalia na kuhamaki.
“Jelini! Hii cheni umetengeneza wapi!?” “Kwa sonara wangu. Huwa ananijulia
sana. Kila kitu ninachomwambia anitengenezee, anatoa kama ninavyotaka na
anampenda sana Yesu. Yupo pale Magomeni. Mtu mzuri sana.”
Ezra akabaki akiitizama, wote kimya macho kwenye hiyo cheni.
“Kwanza nzito ya hadhi. Imezungushiwa alama ya moyo iliyokerezwa vizuri sana,
ikabeba herufi E
iliyobeba J.
Nzuri sana inavutia.” Akaithaminisha Junior na yeye akiitizama kwa makini pale
mkononi kwa Ezra. “Halafu jinsi ilivyokerezwa kwa ustadi! Haichoshi kuitizama
ilivyo. Dhahabu safi tena ya kiwango cha juu. Daaah!” Akasikika Ezra kwa hisia
za kutosadiki na kumtizama Junior, akacheka na kurudi kukaa akiweka sawa kamera
yake ya simu.
“Asante Jelini wangu. Nashukuru mpenzi wangu.” Ikawa kama
Jelini amewawahi kwenye kuchumbia. Tena
kwa kiwango cha juu. “Nimefurahi kama umependa.” “Mbali na uzuri wake wa
kiwango cha juu, maana yake ndio imenifurahisha zaidi. Nashukuru
kujifunga kwangu, na nakuahidi nitakuwa mwaminifu kwako Jelini. Nakuhakikishia
usiwe na wasiwasi wa mapenzi yangu kwako. Niwahi au nichelewe kupokea simu
zako, jua Ezra ni wako tu.” Jelini alicheka kwa aibu.
“Hata asipokutaarifu yupo njiani kukufuata, ujue popote
alipo wewe ndio upo mawazoni.” Junior akaongezea. “Kabisa. Wazo hata lakufiria
kama nimekusahau lisiwahi kupita akilini mwako tena. Jua
nakufikiria, na safari yoyote niliyopo ujue ni ili kukufikia wewe.” Akatingisha
kichwa kukubali kwa kuridhika.
Akamrudishia hiyo cheni, akajua ndio anampa amavalishe. Basi
akazunguka nyuma ya kochi pale alipokaa, akaenda kumvalisha kwa makini. Kisha
akaiweka sawa mbele akilaza vizuri zile harufi zao kisha akambusu hapo chingoni
kidogo tu, akarudi kukaa pembeni yake. Ezra akamsogelea na kumkumbatia tu. Bila
mengi. Junior akichukua video na kuwapiga picha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ila hilo tukio lilimmaliza sana
Junior. Jelini ni mgeni kabisa kwao, lakini akaweza kujichanganya na kuweka
kumbukumbu nzito sana kati yao, halafu ikavutia. Akabaki akijiuliza ni lini
Hope amempa zawadi zaidi ya kuomba pesa na misaada mizito! Hakukumbuka. “Halafu
hana hata heshima!” Akazidi kujiumiza moyoni, akiangalia zile picha
alizowapiga.
Ezra akamgundua amepotea. Akaelewa anachofikiria. Jelini na
wanawake waliokuwa nao, ni mchana na usiku kabisa. Ikawa tena kama Jelini
amekwenda kumchongea Hope, ila kumfuta machozi Ezra. Akashukuru
hata kuachwa na mchumba wa kwanza. Akamuhurumia Junior akielewa alipo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Usiache kunitumia na
mimi.” Akamtoa mawazoni kusudi, na Junior akajua. Akagutuka na kurudi pale
kimawazo. “Aisee nzuri sana. Nyinyi wawili mnapendezana mno. Nina
ujasiri wa kusema mmebahatika.” Wakacheka kwa furaha, Jelini asijue
kinachoendelea. “Asante. Basi tupige na wewe pia Junior. Iwe kumbukumbu yetu.”
“Jelini! Hutaki kurukwa baadaye?” Ezra akafanya wacheke. “Acha niweke ushahidi
wangu wa baadaye, asije sema hakuwepo.” Basi Junior akategesha kamera.
Akategesha. Na kuzunguka nyuma ya kochi, akasimama nyuma yao. Wakapata picha za
kutosha tu. Ndipo wakahamia mezani.
Hao wawili ndio waliiandaa hiyo meza wakisema Jelini mgeni
siku ya kwanza. Wakatengeneza utafikiri imeandaliwa na mama yao! Safi kwa
ustadi mpaka napkins. Kama mama mchungaji anavyoandaa meza ya chakula
nyumbani kwake, kwa wageni wanaofika kuwatembelea. Wakaiga kwa mama yao. Pakapendeza.
“Ila hiki chakula sijakipika Jelini. Imebidi kununua.
Uliponiambia nirudishe akili kazini, ndipo nikagundua nina mengi sijafanya.
Kuja kumaliza, muda ulishakwenda, nikajua nitakuchelewa tena.” “Mimi nataka
muda na wewe Ezra. Hivi vyakula vipo tu.” “Ndio maana nakupenda Jelini wangu.
Huna makuu.” Wakacheka wakikaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakala kwa pamoja, Junior asiamini kama kweli Jelini
ameridhia kujumuika naye usiku huo uliokuwa maalumu kwa ajili yake na Ezra! Akabaki akimsoma kwa tahadhari, akagundua yupo
sawa tu, si kwa kujilazimisha. Tena alionekana kumfurahia na kumshukuru kuwa
nao usiku huo. Akimshukuru kuwa kuja kwake na kukubali kuwa nao, kumefanya
waweke kumbukumbu yao ya kudumu, kitu kilichozidi kumvutia na kumpenda Jelini, akiona
Ezra amebahatika kwelikweli.
Yaliendelea mazungumzo yaliyojaa vicheko tupu. Wakaweza
kufahamiana hao watatu kwa karibu. Maswali mengi na majibu. Junior alipomaliza,
akaaga kwenda kupumzika. Lakini hata Ezra alijua ameondoka akiwa si kama
alivyoingia hapo. Zawadi ya Jelini imemfanya afikirie yake zaidi.
Jelini na yeye hakukaa zaidi, akijua kesho yake ni siku ya
kazi. Akawa muungwana. Akaondoka bila mengi ila busu tu la mdomoni tena kwa
kifupi, akaondoka akiwa amemuachia furaha ya ajabu huyo Ezra. Kila wakati mkono
shingoni.
Msingi.
Wakati anakaribia kupitiwa na usingizi wa furaha, yake
na Jelini yamekaa sawa, ujumbe ukaingia. Akadhania ni Jelini, akakwapua simu
kwa haraka asije haribu tena. Akakuta ni Hope. ‘Tunaweza
kuzungumza?’ Ezra akampigia. Alijua amefanya makusudi mida hiyo akijua
hata kama wanafuatana vipi na Junior, mida hiyo Ezra atakuwa peke yake
akipumzika kwa kazi kesho yake.
“Upo mzima?” Akaanza Ezra. “Nimeharibu
Ezra, na sijui jinsi ya kurekebisha.” Akaanza, Ezra kimya. “Ni kama niliyejifunga kwenye kamba mara nyingi, sijui
najitoaje! Naomba msaada wako tafadhali.” “Wakufanya nini?” Akamuuliza
taratibu tu kama kawaida yake, hana papara. Mtulivu.
“Nisaidie kurekebisha. Najua unajua
kinachoendelea. Nimeharibu. Sijui nitafanya nini.” “Unajirudiarudia Hope. Bado
sijajua unataka mimi nifanye nini!” Akaanza kulia. Akalia hapo kwa muda,
Ezra kimya. “Najua na wewe nimekukosea Ezra.
Nimemtenda ubaya Jelini. Nafikiri kuanzia hapo ndipo nilipoendelea kuharibu.”
“Maadamu umemtaja, naomba tuanzie kwake. Unatatizo gani
na Jelini? Na kuwa huru tu kuniambia chochote kile.”
“Nafikiri nilibeba kinyongo tokea kwenye shuguli
za Ester. Ni kama kwa namna fulani alinipuuza wakati najua kila mtu anajua mimi
ni mchumba au niliyekuwa mchumba wa Junior kama bado hajaniacha. Nilitegemea
angalau anitambue na kunisalimia. Sasa aliponiacha tu, nikajenga kinyongo.” Akamshangaza kidogo Ezra. “Wewe ulitegemea Jelini
ambaye ni mgeni pale kanisani, afahamu kila kitu kinachoendelea pale kanisani?!”
“Kila mtu anajua Ezra.” “Kwamba wewe unadhania ni mashuhuri kiasi hicho pale kanisani,
kwamba kila anayefika pale ni lazima apate habari zako na uheshimiwe kwa kuwa
unamahusiano na Junior!? Kweli Hope?” Hope akapoa.
“Unakumbuka vizuri habari za malikia Vashti?” Hope kimya
akiendelea kulia. “Tafadhali pata muda rudia kusoma
kitabu cha Ester. Vashti alibweteka katika nafasi yake, akashindwa kumkubalia
mfalme, ambaye ni mumewe, jambo dogo sana. Kujitokeza mbele ya watu, ili
mumewe ajivunie uzuri wake. Lakini kwa kuwa alishalewa sifa, Vashti alikataa.
Unaifananisha hiyo stori na tukio lolote lile?” Kimya.
“Eti Hope? Hiyo habari unaifananisha na tukio
lolote lile lililotokea hapa karibuni? Maana kwa kukataa kwake kujionyesha
mbele ya wageni, akiwa amejiamini sana, alisababisha nafasi yake apewe
Ester, mtoto yatima ambaye hakuwa hata na hadhi ya kuwa malikia. Kirahisi sana bila
kutarajia, akidhania jambo kama hilo haliwezi kumpata mtu kama yeye
kwa vile alivyo jidhania na ambayo ameshakwisha fanya kwenye ule
ufalme wa Ahasuero. Ukumbe na yeye aliwafanyia wanawake sherehe kubwa sana
kwenye jumba hilohilo la mfalme, ikafana sana. Lakini si aliondolewa?” Hope akazidi kulia.
“Umejisahau Hope. Umesahau alipokukuta
Junior. Umesahau mtu uliye naye, ukamdharau kwa kuwa ni mpole
sana. Ukasahau kuwa kila mtu anao mwisho wake. Ukabweteka
kwenye mafanikio anayoyasimamia Junior. Wote tunajua jinsi Junior anavyosimama
na wewe. Hata ukipewa jukumu la wanawake, Junior hataondoka ulipo, akisubiria
umtume kwa chochote mpaka jambo likamilike bila ya wewe kulemewa au usijikute
peke yako! Huna utakapomtuma Junior akakukatalia Hope. Mchana na usiku
yupo na wewe.”
Taratibu bila jazba, alihakikisha anamfungua macho.
“Haya, jiulize umekuwa ukikwama mara ngapi
kifedha, Junior akakupa mamilioni ya pesa bila hata kufiria mara mbili?
Unaendesha gari nzuri na kuishi kwenye nyumba nzuri, akikulipia yeye mwenyewe
bila ya kujali au kuumia mapesa anayowekeza kwako! Kweli leo unamdharau
hadharani kabisa na kuonyesha watu baki ni muhimu kuliko yeye!” Hope akazidi kulia.
“Kana kwamba haitoshi, upo kwenye maamuzi yake
mchana na usiku. Tena mimi nakujua Hope. King’ang’anizi mpaka kwenye
mambo yake ukitaka unachoshauri wewe akikubali! Napo pia amekua akikusikiliza,
na bado unashindwa kuelewa utii ni bora kuliko dhabihu!
Utatoa nini chakumlipa mwanaume kama Junior kama sio kumtii,
tena wala hana makuu! Huwa hatakagi mengi. Vitu vyake vidogovidogo tu! Kweli
napo unashindwa!”
“Kweli leo useme Jelini alikupuuza kwenye shuguli
za Ester, eti ndio uje umuadhibu Junior!? Ushindwe kumzungumzisha vizuri
mbele za watu, halafu eti ushindwe hata kukaa naye meza moja kwenye shuguli ya
dada yake! Siku muhimu kama ile kwake, kweli ulishindwa kujikana
kidogo tu ukiheshimu jambo muhimu kama lile kwa familia yake, unazua tension
isiyo na msingi, tena kwa jeuri ya wazi kabisa kwa kiasi kile?!”
“Ingekugarimu nini kukubali kupiga picha na sisi?
Ingekuchukua muda gani? Ingekugarimu nini kutuvumilia kukaa na sisi meza moja
kwa muda mfupi ule tena karibu ya mwisho wa harusi! Unamuhama mezani, mbele ya
mgeni anayemuheshimu kama Jelini?!”
“Halafu eti unajivua madaraka kwa kupitia barua
pepe, moja kwa moja kwa baba yake, yeye hana taarifa! Dharau ya wapi hiyo Hope?
Umejiaminisha kwa kipi?” “Nimekosa Ezra. Hakika
najuta. Naomba msamaha. Nipo tayari kujirekebisha. Nisamehe. Na naomba nisaidie
kuzungumza na Junior.”
“Hapana Hope. Unatakiwa wewe mwenyewe uzungumze naye.”
Ezra akajitoa.
“Nitengenezee mazingira. Tafadhali Ezra.
Nimeingiwa na hofu ya ajabu. Siwezi hata kumsogelea. Najua wewe atakusikiliza.
Junior amekasirika sana. Na najua amekata tamaa na mimi. Lakini mimi namtaka
Junior. Nakuahidi nitabadilika. Nimekosea.” Ezra akapoa.
“Tafadhali Ezra. Nampenda Junior, na sitaki
tuachane. Wala sitakudanganya. Sitaki kuachwa na Junior. Na kabla ya kesho
kukabidhisha uongozi kwa mzee kama alivyoniomba,” “Hapana
Hope. Ni kama ulivyoomba. Wewe ndio umeomba kuacha uongozi effective immediatly.
Ndicho ulichotaka na ndicho unachopewa kwa heshima kabisa. Tafadhali usianzishe
jambo jingine litakalozua mkanganyiko pale kanisani. Hilo usilibadili
kwa watu. Maana umeanza kwangu niliyeona barua pepe yako, hutashindwa
kwa washirika wengine. Usisambaze habari ambayo siyo.” Akajua amebanwa kila
kona.
“Nimekosea kusema Ezra. Sijamaanisha kitu
kingine. Na hata katika hili nakiri kwako nimekosa na naomba nizungumze na
Junior kabla sijaenda kukabidhisha.” “Sasa hivi
ameshalala. Nimetoka kuzungumza naye muda mfupi kabla hujanipigia, tumeagana,
analala. Naomba iwe kesho. Nitaweka mazingira mkutane kwa chakula cha mchana.”
“Nashukuru Ezra. Na wewe umenisamehe?” Ezra
akacheka kwa masikitiko.
“Nimekosa Ezra. Na nakuahidi nitazungumza na
Jelini pia.” Alimshitua
Ezra, kama aruke. “Hapo hapana Hope. Tafadhali usimsogelee
Jelini. Ameshaingiwa hofu na wewe. Kwanza umemuharibu akili kwa kudharau
anachokifanya.” “Sikukusudia.” “Lakini umeshafanya. Kwa hiyo HAPANA. Achana na
Jelini. Wewe tengeneza yako na Junior. Jelini niachie mimi.” Hapo napo
Hope akalia sana. Akajua bado kutakuwa na matabaka asiyoyataka Junior. Leo
kusiwe na Ezra na Jelini kwenye maisha yao, akajua hayo mahusiano hayatakaa
yakafaa.
“Nisamehe Ezra.” “Hakika nakusamehe
kabisa! Ila Jelini hapana. Hapo utanisamehe Hope. Mimi nakufahamu na
namfahamu Jelini. Unaweza zungumza jambo, likabaki kwake, wewe huna
taarifa au usijali au ukaja omba msamaha kama hivi, lakini
lishamwingia yeye. Hapana Hope. Nitafanya chochote ila si Jelini.
Acha muda uje utuweke pamoja, lakini si kwa wewe kumtafuta Jelini. Hapo HAPANA.
Usiku mwema. Nitakutaarifu kesho.” Simu ikakatwa na kumuacha Hope bila
ya tumaini.
Alitamani arudi kwa Junior angalau kuna taarifa za
kutengeneza na Jelini pia. Lakini hakuwa na chakufanya. Kila alipokumbuka
maneno ya Ezra kwenye mahusiano yake na Junior, akazidi kukata tamaa.
Jeuri aliyokuwa akimfanyia hata kabla ya hapo. Kumpuuza kwenye mambo
madogomadogo! Hofu ikazidi kumuingia kila akifikiria sababu inayoweza mfanya
Junior amsamehe, alikosa.
Akajikuta ni mzigo ambao Junior atakuwa na nafuu
ya kuutua. Hawakuwa na historia/msingi mzuri ya kimapenzi, ila ni kweli walifanikisha
mengi kwa pamoja. Ila akakumbuka yote waliyofanikisha, hayakuwa yao. Kanisa
si la Junior, ni la baba! Junior hana cha kukumbuka hapo na kumfanya
atake warudiane! Usiku huo ukazidi kuwa mbaya kwa Hope. Maji yalishamwagika muda mrefu sana, asijue hata yalishakauaka. Hakuna cha kuzoa wala
kudeki. Anajirudije!
~~~~~~~~~~~~~~~
Tusijisahau, kila tunachopewa ni dhamana na kuna garama
ya kutunza.
TUSIBWETEKE.
Umama, ndoa, mahusiano, hata undugu ni DHAMANA, na
kuna GARAMA. Siku
utakapochoka tu, na kuamua kuzembea, UHARIBIFU UNAANZA
KUNYEMELEA.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment