Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 27 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 27

Wakati jumatatu hiyo iliyokuwa imejaa mengi upande wa kina Jelini, huku kwa Colins majira ya saa 11:30 alfajiri Chaz akawa amewasili hapo mpaka akamshangaza Colins ila akafurahi sana. Akajua James amemwambia awahi. Akafika hapo na kushika usukani kumsaidia Colins ambaye bado alikuwa kimya tu kwa watu wa nyumbani kwao, hazungumzi nao isipokuwa kitu cha muhimu sana, tokea James aondoke hapo siku iliyopita na kuwapa onyo la kutomsogelea tena Jelini.

    Jioni Connie alipomletea laptop zake kutoka Kigamboni, akamuuliza akiwa amekaa anafanya mazoezi madogo kwenye kiti hapo chumbani. “Love alijua kama unachukua laptop zangu?” “Kama ulivyonituma, nilimwambia nahitaji vitu vyako baadhi. Alitoka na kunipisha kwenye chumba alichohamishia mizigo yako. Hizo nikazificha kwenye nguo. Ameshangaa kusikia kama ndio umenituma, akishindwa kuamini kama umepona. Aliponiuliza kama unampango wa kurudi kule, nikamwambia akupigie mwenyewe, mzungumze. Ila anaonekana vizuri tu. Na simu yako amenipa. Kila kitu kipo ndani la hilo begi.” Begi dogo tu akaliweka pembeni yake.

“Nashukuru. Ila nikwambie ukweli tu, mimi, nisingekukimbia.” Connie akaanza kulia. “Hata kama ungekuwa umeolewa ndoa ya kanisani kabisa tena yenye furaha na amani, nisingeacha kukutafuta kukujulia hali kwa muda mrefu hivyo. Miezi zaidi ya 7! Hujui nilipo wala ninafanya nini au ninaendeleaje! Umenisikitisha na kunihuzunisha sana Connie. Mimi nisingekufanyia hivyo hata iweje.”

    “Ni kama nimerudishwa duniani nione nina zungukwa na watu wa namna gani! Kweli natembea mimi kama mwenda wazimu mtaani, Love akinitesa atakavyo, nyinyi mpo hapahapa Dar, hamna taarifa wala hamjali! Yaani unakuja kugundua yangu, kwa kumkosa baba wodini kwenye hizo round zenu! Unamsaka baba, ndipo unakutana na mimi, lakini inamaana kama ungemuona baba, inamaana mpaka sasa usingejua kinachoendelea kwenye maisha yangu na usinge jali.” Colins alijitahidi kuzungumza naye kwa sauti ya kueleweka, lakini wazi ilisikika imejaa uchungu.

    “Tafadhali nenda kaendelee na maisha yako Connie. Usipoteze muda sasahivi, kwa sababu huna unachokifanya hapa, ila kupoteza muda wako wa thamani usiotaka matatizo, na kutaka kuja kufeli, uje usingizie ulikuwa hapa kwa ajili yangu, wakati si kweli. Funga mlango nyuma yako.” Connie akajua ndio anamfukuza, aliondoka hapo kwao akilia sana. Hakujua azungumze nini tena na Colins. Na alijua neno ‘samahani’, halitoshi.

Kwa Mzee wake.

    Hakutaka tena msaada kutoka kwa baba yake. “Huna haja ya kuja kuniangalia kila mara na usiku. Najua dawa ninazotakiwa kutumia, na natumia kwa wakati. Ninaye Chaz ambaye ananisaidia mchana, usiku nakuwa nalala. Tafadhali usikwame hapa kwa ajili yangu wakati wote tunajua una mambo muhimu sana yakufanya, kuliko mimi.”

    “Na Mungu akinirudishia tena nguvu za mwili, nitahakikisha nafanya kama unavyotaka. Kukuingizia pesa ili uzidi kuwa tajiri, ufe ukiwa na mali unazotaka kumiliki hapa duniani. Kwa hiyo naomba nipe muda na nafasi. Kila kitu kitaendelea kwenda kama ulivyopanga.” Mzee naye akatoka kimyakimya.

Mama Yake Naye.

    Mama yake alipomletea supu, Colins akabaki akimwangalia akiiweka mezani. “Hivi ulipita muda gani tokea uliponiacha mpaka kuja kugundua kama mimi nipo matatizoni?” Akamuwahi kabla hajatoka. Kimya. “Nenda tu, nisikupotezee muda wako. Nitakuja kumuuliza mama Simba.” “Nilijaribu Coly, mwanangu. Nilijaribu sana, lakini ikawa nagonga mwamba.” “Lini? Nikimaanisha, tokea mara ya mwisho unione na kuzungumza na mimi, kisha kuja kugundua nipo matatizoni?” Mama yake akabaki kimya.

    “Na bado ulikuwa unaamani tu!? Japokuwa ulijua ubaya wa Love kwangu, lakini uliridhia kuniacha naye na kunitelekeza kabisa!? Hivi uliweza vipi hata kupata usingizi mama wewe!? Tuseme ulidanganywa juu ya Jelini. Lakini kweli hukukumbuka yote niliyokwambia juu ya Love hata kabla Jelini kufika kwenye maisha yangu, kweli?! Unaacha niangamie sababu ya mali! Kweli?! Unakubali mimi nitolewe kafara kwa urafiki wenu na mali!”

    “Hivi tokea mnirudishe hapa nikiwa na hii hali, ni mara ngapi mama Simba amekutafuta kunijulia hali?” Kimya. “Mungu akinirudishia nguvu, hakika nitawatafutia mali nyingi sana. Muwe nazo mpaka mkinahiwe kama kupo kukinahiwa na pesa. Nitahakikisha kafara yenu inawalipa. Maana mmemuua kijana wenu kwa garama kubwa sana! Tena bila huruma, kikatili kabisa eti sababu ya mali na marafiki! Basi nitawatumikia mama, ili furaha yenu ikamilike.”

    “Sasa nashukuru kwa chochote ulichokuwa ukikifanya hapa. Chaz atakupokea. Huna haja yakurudi tena hapa. Endelea na maisha yako na usingizi mzuri kama uliokuwa nao uliponitelekeza kwa Love. Na usiwe na wasiwasi, nikipona tu, nitarudi kule ulikotaka niwepo. Kwa hiyo nivumilie uwepo wangu kwa sasa. Nikiweza tu kujitegemea, nitaondoka. Ila tafadhali usirudie kunidanganya kwa kuonyesha unajali kwa kunihudumia. Usipoteze muda wako na usije hapa kunikejeli. Inatosha.” Mama CJ akaondoka. Colins akajivuta na kuanza kunywa supu aliyoletewa, tena bila ya kujivunga.

Ezra.

    Alitaka kwenda kwa Junior, lakini akaona Junior mwenyewe ana yake na mchumba wake, amuache apumzike. Akabaki amekaa sebuleni kwake akaona atoe simu yake angalau amjulie hali Jelini na kujua kama alifika salama. Ndipo akakutana na jumbe za Jelini. Mbaya zaidi akakutana na missed call ingine ya dakika chache zilizopita kutoka kwa huyohuyo Jelini. Kwamba ndio ametoka tena kumpigia, hajapokea. Ezra alitamani kulia. Kikampata cha Colins. “Ni nini kinaendelea kwenye hii simu! Kama nahujumiwa!” Akajiuliza kwa uchungu kana kwamba analaumu hiyo simu.

    Haraka akaenda kwenye jumbe wanako chat na Jelini. Mbali na hiyo simu aliyotoka kumpigia hapo na hakupokea, kumbe baada ya kumkosa, Jelini akamuachia na ujumbe mwingine tena. Asione. ‘Nilitaka kukutakia usiku mwema na kukutaarifu kuwa nimemuomba mama off kwa siku ya kesho. Sijawahi kuwa off tangia nianze kazi. Nitakuwa na mapumziko siku nzima, nitafunga kabisa simu ili nipate muda wa kumpumzika na kujitafakari. Na samahani niliondoka bila kushukuru kwa chakula. Asante. Usiku mwema na siku njema kesho. Ni mimi Jelini. Kama ulipoteza namba yangu.’ Mpaka vidole vilikuwa vikitetemeka wakati akisoma huo ujumbe wa mwisho.

    “Jelini anahisi napuuza simu zake kama niliyefuta namba yake! Mungu wangu usiniache. Nitetee Baba yangu.” Akajikuta amechanganya na maombi hapohapo. Akaangalia hizo jumbe alizotumiwa na Jelini akiwa nyumbani kwao, usiku huo kabla hawajakutana. ‘Unafikiri bado kuna uwezekano wa kuonana usiku wa leo?’ Huo ulikuwa ujumbe wa kwanza na ilikuwa saa mbili na nusu. Akasoma mwingine. ‘Upo sawa Ezra?! Tafadhali nijibu, nina wasiwasi na siwezi kujisaidia. Nataka tu kujua kama tunakutana leo au nirudi tu nyumbani nisiendelee kukusubiria hapa? Nataka kutumia bafu kwa haraka na hapa tumeshafunga. Nilisharuhusu wafanyakazi wote, nimebaki peke yangu.’ Huo ukawa ujumbe wa pili. Muda ulipoingia huo ujumbe ilikuwa ni saa nne kamili usiku huo. Hapohapo akaamua kumpigia simu. Hakuwa hewani. Akajaribu zaidi ya mara kumi kama ambaye hajaelewa ujumbe wa Jelini kuwa anafunga simu kwa mapumziko. Huo usiku ukawa umeshaharibika kwa Ezra.

  Kwa Colins.

    Alichokifanya usiku huo, huyo Colins baada ya kushiba vizuri na kukaa kitandani kwake ni kuanza kupitia akaunti zake huko benki. Akagundua mahela aliyokuwa akilipwa kama mshahara. Mwenyewe alitoa macho. Lakini akashangaa ile pesa ilikuwa kama ikipita tu hapo kwenye akaunti yake na kupelekwa kwingine. Mjuzi huyo wa mtandao akaanza kufanya uchunguzi zilipokuwa zikipelekwa. Akagundua zilikuwa zikihamishwa kwenye moja ya akaunti ya Love. Akacheka na kutingisha kichwa kwa  masikitiko.

    Akaanza sasa kufikiria namba ya siri ya Love kuingia kwenye akaunti yake. Akatulia zaidi ya nusu saa akiandika namba za siri anazofikiria anaweza Love kutumia. Akiwa anaandika, akaanza kwa kubadili namba ya siri ya akaunti yake huko benki. Akaweka namba ya siri ambayo alijua hata afanye nini huyo Love hawezi rudi tena ndani ya akaunti yake. Kisha akarudi tena kwenye akaunti ya Love. Kwa vile anavyomfahamu Love, alijaribu mara ya kwanza, ya pili akafanikiwa kuingia.

    Uzuri Love ni wale wanawake wanao jua kutunza pesa. Si watapanyaji. Kwa hiyo akakuta mamilioni ya pesa yakutosha tu huko kwenye akaunti yake, hakushangaa. Love ni wa mahesabu na mtu wa kufikiria sana kesho. Akapiga mahesabu. Tokea mshahara wake wa kwanza aliochukua mpaka siku hiyo. Hakuacha hata shilingi. Pesa yote akajirudishia kwenye akaunti yake bila ya kuzidisha hata shilingi. Lakini jinsi alivyofanya, alionyesha ni yeye mwenyewe Love amefanya marekebisho ya makosa aliyofanya kujihamishia hiyo pesa. Kila pesa aliyohamisha, aliirudisha moja baada ya nyingine, vile ilivyo kila mwezi si kwa jumla. Moja moja mpaka akamliza. Akafunga akaunti ya Love na kuicha na pesa yake tu. Akafurahia kuangalia ile akaunti yake. Ikarudia uhai wake. Akafunga komputa na kulala akiwa ndio amechukua hatua ya kwanza.

Jumanne.

    Alfajiri na mapema, akajaribu kupiga simu kwa Jelini. Akakuta bado imefungwa. Akajaribu tena na tena bila mafanikio. Njia nzima kwenda kazini akawa na kazi ya kumpigia simu Jelini bila ya kuchoka. Anaingia kazini akawa kama ambaye hajalala kabisa. Junior akashangaa. Maana Ezra waliyeachana naye akiwa anakwenda kwa Jelini kupewa zawadi yake, tena yenye ahadi kuwa ni nzuri sana, siye aliyetegemea kukutana naye asubuhi hiyo. Junior akamuuliza kulikoni.

    “Mimi sijui kinachoendelea kwenye hii simu Junior! Ni kama nahujumiwa kabisa.” Akamsimulia Junior na macho yaliyokuwa mekundu haswa. “Naomba simu yako Ezra. Lazima umecheza na setting, umezima notification zote.” Akampa huku Ezra akijaribu kufikiria ni muda gani amefanya hivyo, bila kukumbuka. Junior kuingia ndani ya simu yake, akakuta alichodhania ndicho. Akamrekebishia na kwenda kwenye chati zake na Jelini. Akaanza kusoma. Mwanzo mpaka mwisho.

    “Hii haijakaa vizuri, Ezra!” “Najua Junior. Na wewe unajua siwezi kunyamazia simu za Jelini hata iweje! Nafanyaje? Imekua kama nina mkosi kwenye swala la mahusiano jamani!” “Acha kusema hivyo. Nakosea wapi, sijui! Nakua kama nimeandikiwa kufa peke yangu!” “Niseme nini Junior kama si hivyo!” Junior akabaki ameshikilia simu ya Ezra akitafakari. “Ila hata mlipoachana usiku, bado alikutafuta na kukuachia ujumbe ambao hauonekani kama amekasirika!” “Lakini hakunipata, Junior! Huyu binti mpaka ameanza kusamehe makosa kama haya aliyokuwa akifanyiwa na Colins! Kitu ambacho ndio ilikuwa nguvu yangu kwake. Sasahivi ni kama nacheza sana chini ya kiwango.”

    “Nikuulize kitu Ezra? Ila naomba ufikirie kabla hujanijibu.” Ezra akatulia, akimtizama kama anayemwambia uliza. “Hutapenda kumuoa Jelini, akiwa anayafahamu mapungufu yako? Namaanisha akubali kuolewa na wewe akikujua wewe ni nani, kama wewe ulivyomfahamu kupitia Jema, na bado ukampenda? Hutaki hiyo na wewe? Akupokee kama ulivyo sio kama Ezra mtakatifu asiye na makosa?” Ezra akatulia kabisa. Hakika alishindwa kujibu. Alishamtaka huyo Jelini, hakutaka tatizo litokee katikati yao.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Alitoka kabisa hapo na kwenda nje kuendelea kumpigia simu Jelini bila ya kuzungumza tena na Junior. Muda ukazidi kwenda bila matokeo na harudi ndani kufanya kazi. Junior alipoona kimya, akatoka kumtafuta. Akamkuta amekaa sehemu ya peke yake akipiga simu. Akamsogelea. “Umefanikiwa?” “Aisee nachanganyikiwa Junior.” “Hudhani kama pengine amelala?” “Sasa hivi siwezi kufikiria kabisa. Nahisi nimeshapaniki.” “Mtumie ujumbe. Mueleze ukweli na muombe akiamka akutafute japo umjulie hali.” Kazi ya kuandika huo ujumbe ikaanza.

    Junior akamuona anaandika kisha anafuta. Hilo zoezi likaendelea kwa muda wa kutosha, akaona aombe yeye hiyo simu. “Unataka kumwambia nini?” Junior akamuuliza akitaka kumsaidia kuandika yeye huo ujumbe. “Nampenda, na yeye ni mtu wa mwisho kabisa nataka kumuumiza.” Bila ya kutarajia chozi likamdondoka mwanaume mzima, na wadhifa wake. Akalidaka kwa haraka na kuondoka kabisa pale kuelekea chooni.

    Junior akaanza kuandika. Akatengeneza ujumbe mzuri, akampelekea simu chooni. “Angalia huu ujumbe kisha usifute ila niambie wapi nirekebishe kabla sijatuma.” Ezra akasoma kwa kurudia rudia. “Sioni msisitizo wa kama nampenda.” “Ni zaidi ya neno ‘nakupenda’, Ezra. Hayo maneno ameshazoea kuyasikia. Anachotaka ni vitendo kitu alichokikosa jana, na ndio unataka kumuhakikishia si kwamba umempuuza, na haitakaa ikatokea ukampuuza. Atabaki kuwa dharula yako ya kwanza na hakuna kitabadilisha hilo. Mkumbushe hili nalo ni jaribu lenu la pili, na wewe safari hii umekosea, unahitaji msamaha wake. Itamfanya atulie na kujifikiria.” Hapo akakubaliana naye, akamtumia. Akamuona anaanza kutulia. “Twende tukamalizie kazi.” Wakarudi ofisini akiwa ametulia kidogo. Ndio mida hiyo akaweza kuanza kufanyakazi. Pakawa kimya hapo kila mmoja akiwajibika kivyake.

Kwa Jelini.

    Huku kwa Jelini akaamka mida ya saa sita mchana. Usingizi umemuisha kabisa. Nyumba nzima yupo peke yake. Akabaki akijifikiria. Kitendo cha Ezra kutojibu jumbe zake na asipokee simu yake, si kwamba kilimkasirisha, ila kumnyenyekeza vibaya sana. Ile hali ya kufikiri anatakiwa kubabaikiwa, ikamuisha kabisa. Akapoa na kuanza kujiona si kitu. Akabaki akijifikiria maisha yake, akajiambia arudishe akili kazini, swala la mapenzi kwake limeshakuwa zito. “Sina sababu ya kujilaza hapa siku nzima kama mgonjwa.” Akaingia bafuni kuoga na kutoka ili ajiandae kurudi kazini. Kama kawaida yake hakujikosea. Alipendeza tu.

    Akatamani kumsalimia Ezra, ila akakumbuka usiku uliopita. Mara kadhaa kumtafuta na kushindwa kuitika simu yake hata jumbe! Akapoa na kuona ni bora amuache tu. Akajiandaa, wakati anatoka akaamua kuwasha simu yake moja ili kumtaarifu mama yake kuwa anakwenda kazini. Ndipo akakutana na ujumbe wa kwanza mrefu sana kutoka kwa Ezra.

Alibaki ndani ya gari akisoma. ILA ukweli ilimfariji sana, kuona bado anasoko na mtu kama Ezra bado anambabaikia! Kutoka kujikatia tamaa akiona ameshotoka sokoni, na kusoma ujumbe wa kutetemekewa hivyo! Moyo wake ukaanza kuinuka.

     ‘Tafadhali nipigie Jelini. Nina hali mbaya. Siwezi kufikiria nikiwa nimekuumiza. Nisamehe mpenzi, na tafadhali usifikirie kuniacha. Hesabu hili ni jaribu letu la pili.’ Mbali na ujumbe huo mrefu wa kwanza, huo nao ukawa wa pili. Inamaana baada ya kutuma ule wa Junior, akaona atengeneze na wa kwake utakao muwakilisha vizuri.

Jelini akiwa anaendelea kusoma huo ujumbe wa pili, kumbe kule kwa Ezra alitegesha simu kwamba Jelini akipokea tu jumbe, apewe taarifa. Simu ikaingia akiwa anasoma hizo jumbe garini, asiamini zinatoka kwa Ezra.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Na yeye akapokea bila ya kuchelewa. “Ezra!” Alivyosikia akimuita hivyo kwa upole, hakuamini. Akajikuta anafunga macho na kuvuta pumzi kwa nguvu. “Nilikuwa nimelala Ezra, na usiku nilikutaarifu kuwa nitazima simu kabisa ili nipumzike bila muingiliano. Maana simu zangu zipo busy sana kila wakati. Pengine uwe hujaona tena.” “Nimerekebisha simu asubuhi hii mpenzi wangu. Nimegundua tatizo. Sijui imekuaje, nilizima notification zote na kuweka silence. Kwa hiyo kama sikuwa nimeona simu ikiingia, basi haitabakia juu kuona missed call. Na jumbe hivyohivyo. Yaani nimefika nyumbani nikiwa nataka kukutafuta nijue kama ulifika nyumbani salama, ndio nakutana na jumbe ambazo ulinitumia tokea nipo kwa wazazi na njiani kuja kukuona.” Ezra akaendelea kujieleza kwa hofu kama anayejitetea.

    “Inatokea Ezra.” “Hapana. Si kwangu, na si kwako. Nakuthamini Jelini, kuliko nafsi yangu. Wewe ni mtu wa mwisho hata kufikiria kukuumiza. Nisamehe mpenzi.” “Hamna shida Ezra. Kuwa tu  na amani.” Ezra akawa bado hajaridhika. Ikawa kama bado hajaupata moyo wake.

    “Unaendeleaje?” “Naendelea vizuri.” Akajibu tu hivyo. “Tumbo?” “Nipo sawa kabisa. Hapa naelekea kazini. Nimelala mpaka usingizi umeisha, nimejikuta sina chakufanya, nikaona ni bora tu niende kazini.” “Naweza kukuona jioni? Leo nitawahi. Sitakuweka kama jana.” “Naomba iwe wakati mwingine au hata kesho kama tutaweza. Leo nina mipango mingine.” Hilo halikukaa sawa kwa Ezra. Mipango mingine“Nakuahidi sitachelewa na sitakuchelewesha. Nataka tu kukuona Jelini. Jana haikuwa nzuri, nisipokuona na leo, nitashindwa kabisa kufikiria.” Jelini akatulia.

    “Nataka nikupikie chakula kizuri, uje kula nyumbani. Leo ufike nyumbani kabisa na tukae tule pamoja.” Akawa kama anaye bembeleza. “Nilimuahidi Jeremy nitatoka naye nimpeleke akaogelee maana mama amemuanzishia mafunzo ya kuogelea. Nimekua busy, sijawahi kumuona akiogelea hata mara moja ndio leo nimemuahidi nitampeleka nimuone akiogelea na tupate chakula pamoja sababu nitakuwa off. Hata huko kazini ninapokwenda sitakaa sana. Ninaenda tu kuchungulia. Na kumuwahi nyumbani. Jeremy anakaa sana ndani. Ndio hata shule wameshauri aingie kwenye mchezo wowote atakaopenda yeye. Amemwambia mama angependa kufundishwa kuogelewa, ndio mama amemuingiza huko. Nataka na mimi nimuunge mkono. Wanasema anajitahidi na huko kwenye kuogelea.” Hapo Ezra akakwama. Maana alishaambiwa jicho la mama Jema lipo hapo kwa huyo Jeremy na hataki utani na mtu.

    “Nashukuru kwa ukaribisho wa nyumbani na utayari wa mpaka kunipikia Ezra. Lakini nilishaweka mipango mingine.” “Uliniahidi nini Jelini? Sisi kwanza, mengine yanafuata. Sio kwamba nakataa usiwe na Jeremy lakini mbona hujanishirikisha kwenye mipango ya leo?” “Ningekupataje Ezra!? Simu zangu hukuwa ukipokea na jumbe hujibu! Maisha lazima yaendelee. Mwenzio ni mama. Nina majukumu mengine ambayo nimekua nikizembea sana, nikimuachia mama. Na wewe nilikwambia, nataka kubadilika.” “Na mimi nakuunga mkono Jelini. Lakini umeelewa sio kwamba nimekufanyia makusudi?” Akazidi kuzungumza kwa kubembeleza mpaka akawa anatia huruma na kumfanya Jelini kujisikia hastahili. Ni kijana Ezra! Sio kwamba yupo hovyo! Anajielewa na anajiweza.

“Nimeelewa Ezra. Najua unanipenda, huwezi kunifanyia makusudi.” Ezra alitamani kulia. Hakutegemea. “Nashukuru kunielewa Jelini. Asante. Na nashukuru kutambua kama nakupenda. Umeshakula chakula cha mchana?” “Sijala. Nilitaka niende kazini. Nikachungulie ndio niende kumfuata mama, nikale naye kama angekubali. Huwa anakua busy sana, lakini ukimuwahi anaweza kutoka na kula.” “Basi naomba leo nichukue nafasi yake.” Jelini akacheka akifikiria.

    “Tukutane nyumbani, nitakuja na chakula. Kwa hiyo unaweza kwenda kazini kwako, ukaweka mambo sawa, kisha tukutane nyumbani.” “Sasahivi nimapema sana Ezra, usiache kazi kwa ajili ya kuweka sawa mambo ya jana. Mimi nimeelewa.” “Lazima nikuone leo, Jelini. Kwa garama yeyote ile. Tafadhali.” “Basi akitoka kaka shule, anikute nikimsubiria. Nimpeleke kula na kuogelea. Mpaka ikifika saa kumi na mbili atakua amechoka. Nikimrudisha nyumbani, ndio nije kwako.” “Hapo sawa kabisa. Nakushukuru Jelini. Na samahani sana.” “Yameisha Ezra. Wewe fanya kazi kwa amani.”

    “Kwa hiyo nisubirie na ile zawadi yangu?” Akanyamaza. “Eti Jelini? Au ndio nimeharibu sana, sistahili tena zawadi?” “Yameisha Ezra. Ila ile zawadi nimeifikiria, nimeona nimekosea.” “Kivipi tena!?” “Sijui Ezra! Ila moyo wangu umeingiwa na hofu, naona kama sikutakiwa kukupa aina hiyo ya zawadi! Maana pia ilikuwa na maana yake. Ila kuna ingine nzuri pia, nilikununulia wewe na Junior. Zinafanana. Nitakuletea. Usiwe na wasiwasi.” Ezra akamtizama Junior, Junior akamuandikia kikaratasi. ‘Zawadi ya kwanza.’ Ezra akasoma na kuelewa.

    “Kama si kuchelewa kwangu jana na kushindwa kurudisha jumbe zako kwa wakati, hiyo zawadi ambayo imekufanya ufikirie na kukuingiza hofu imebeba maana gani?” Jelini akatulia kama anayesita, maana alikuwa akikwepa, akajua bado Ezra anang’ang’ania japo amemwambia ipo ingine. “Eti Jelini? Tafadhali naomba kujua.” Akasikika kubembeleza. “Nilitaka kukwambia au kukuomba kitu kwanza ndipo nikupe. Lakini si muhimu. Ila ninayo ingine ambayo inafanana na ya Junior. Nilinunulia maalumu ya kuvalia hayo mashati yenu ya kazini. Nilitaka nimpe na Junior. Kwangu amekua mtu mzuri sana, halafu ni rafiki yako. Sitaki muoneane wivu. Utapenda. Ni nzuri.” Ezra akacheka lakini akijua anakwepa zawadi ya kwanza kwa kuendelea kuzungumzia zawadi ya pili.

    “Nyinyi mnafanya kila kitu pamoja. Nimejiambia nikikununulia kitu cha kuvaa, kama nguo nitafanya kama mnavyofanya nyinyi wenyewe, kununuliana.” “Nashukuru Jelini. Ila hiyo nyingine ya kwangu maalumu, natamani kujua hicho ulichokuwa umepanga kuniambia.” “Hata kama nitakuwa nimeharakisha?” “Hata kama utakuwa umeharakisha. Natamani kujua.” Akamsikia akicheka kwa wasiwasi.

    “Ni nini?” “Si muhimu Ezra!” “Nilishajiandaa nayo. Japokuwa umeniambia imeharibika, bado nataka kujua ilikuwa ni nini na kupata hiyo maana yake.” “Kwanza ujue jana nilikuwa nimekasirika kidogo ndio maana nikasema itakua imeharibika, lakini si kitu chakuharibika. Nilikuwa nimetengeneza maalumu kwa ajili yako.” “Pole nilikuudhi mpenzi wangu.” “Yameisha Ezra.” “Lakini bado ni yangu. Na bado naitaka na maana yake pia. Tafadhali Jelini. Usigairi kwa makosa ya jana. Umesema yameisha, na kama unajua nakupenda basi naomba tusonge mbele, tusirudi tena nyuma.” Akamlainisha kabisa, mpaka akamuweka kwenye mstari.

    “Basi acha nikija jioni, nije nayo maana nilitaka kukupa na ndio nikwambie maana yake. Ila usinielewe vibaya nikikupa.” “Hata kidogo. Nasubiria kwa hamu sana.” Jelini akacheka. Alitamani kuendelea kuzungumza, lakini Junior akamwandikia kikaratasi kingine tena kwa herufi kubwa kabisa. Akakisoma kutoka mezani kwake. ‘INATOSHA. UTAHARIBU.’ Akajua ndio anamwambia akate simu. Asiendelee kuzungumza sana. Akaaga na kukata.

Full Swing.

    Akamuona anaandika tena ujumbe. Junior akajituliza tu. ‘Naomba tuzungumze hata dakika moja.’ Mara akasikia simu yake ikiita mara ya kutuma huo ujumbe. “Nina dakika 10 tu kabla sijaingia kikaoni.” “Asante. Najua mama yenu yupo sana makini na Jeremy.” Akahisi safari hiyo anazungumza na Jema. “SANA. Ni roho yake.” Jema akajibu. “Tafadhali niombee ruhusa leo niwe na Jelini akiwa anampeleka kwenye kuogelea.” “Mmmh!” Jema mwenyewe akaona pamekua pagumu.

    “Tafadhali dada Jema. Mimi unanijua. Sitamkimbia Jelini. Nipo naye mpaka uzee wetu. Na wazazi watamtafuta mama nafikiri kama sio kesho, basi kesho kutwa ili kuweka mipango ya kuchumbia. Ni siri tu nakudokeza, na sitaki Jelini ajue. Maana tunamuandalia surprise nzuri sana. Nimekudokeza wewe sababu nataka ujue sio mchezaji wala mbambaishaji. Nitakuwepo kwenye maisha ya Jeremy si leo tu, mpaka tunamuoza.” Jema akacheka, kwa kuridhika ila na wasiwasi wa hilo ombi.

    “Kama utaniruhusu kumdokeza mama mpango wa wazazi kumtafuta kwa posa, angalau nitakuwa na kijinafasi cha kukuzungumzia angalau uwe karibu na Jeremy. Macho, akili na moyo wa mama vyote vipo kwa Jeremy. Huwa tunasema na James, tunafikiri yale yote aliyotamani kuyaona na kufanya kwangu na Jelini, anahakikisha anayafanya kwa Jeremy. Hataki kuruhusu kosa hata kutoka kwa Jelini mwenyewe.” “Naahidi na mimi nitakuwa makini, dada yangu. Tafadhali niombee kwa mama ili leo niwe nao.” “Sikupi ahadi Ezra. Na usijisikie vibaya akikataa.” Akamtahadharisha.“Sawa. Nijaribishie tu.” Wakaagana.

Kuliko Ng’atwa Na Nyoka. Jani Likitikisika Tu, Anashituka.

    Jema akampigia simu mama yake. Akamueleza mwanzo mpaka mwisho. Hapana Jema.” Hakutaka hata kuzungusha. “Unanielewa? HAPANA. Mwambie atakuwa naye wakati mwingine, mambo yakikaa sawa. Huyu Jeremy ndio ameanza kuogelea. Hataishia leo. Inamaana ratiba kama hizi zakuogelea zitaendelea tu. Kutakapokuwa na picha yakueleweka kati yake na mama yake, ndio tutamsogeza kwa Jeremy. Msitake kumchanganya huyu mtoto.” Akaanza kubadili gia.

    “Mnataka haya wanayofanya hawa wanaume wahuni wa hapa mjini ndio aige Jeremy? Awe anachezea binti za watu hovyo? Nataka awe kama James. Anaanza jambo kwa heshima, na kulisimamia mpaka kwenye ndoa na hadi sasahivi ni baba pia. Sijamuona akiyumba. Ndio maana unaniona sina shida na Jeremy kuwa nyumbani kwako, kwenye mwanaume anayejielewa. Haya mambo ya katikati unayotaka kuyaruhusu TENA, hapa katikati ni kutaka kumchanganya huyu mtoto, na sitakuruhusu tena Jema. Maana ulimtetea hivihivi Colins. Vikaishia wapi?” Moyo wa Jema ukashituka, asijue kumbe mama yake anamlaumu na yeye pia.

    “Mtoto amebaki akijenga treni zenye maswali, alizofundishwa kujenga na huyo Colins, hakuna anayejua kumjibu maana alianzisha mambo kwa Jeremy, akiwa na ahadi kemkem, akaishia barabarani.” Jema akajua kibao kimemgeukia. Mjumbe anauwawa. “Nimeelewa mama. Na samahani.” “Kwa heri.” Simu ikakatwa. Jema akabaki ameduaa. Anarudishaje majibu!

~~~~~~~~~~~~~~~

Zawadi gani hiyo Jelini amemuandalia Ezra? Na Inamaana gani?

Ipi mipango ya Colins?

Ameanza na pesa yake, na ahadi ya kumfanya mzee na mkewe watajirike sana, huku akisisitiza wamemtoa mtoto wao kafara.

Uhusiano wao utabakia kwa picha ipi?

Love atafanya nini?

Wanasema ogapa mtua siye na chakupoteza. Colins.

Maisha yake wakiwa wamemtoa Jelini kwenye maisha yake, yatakuaje?

Nani atawajibishwa? Nani atahimili gadhabu yake?

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment