“Na mimi nashauri mkutane. Naomba mpe nafasi.
Msikilize tu kisha utaamua. Nitaweka reservation.” Akamtajia kimgahawa
kizuri, chenye utulivu na kinachoendana na hadhi yao anachojua Junior anapenda
chakula cha hapo. Kimya. “Nitamwambia saa sita na nusu awepo hapo. Utamkuta.”
Kimya, hata kumwangalia hakuwa akimwangalia. Ezra akamuacha akiwa na uhakika
amesikia, na atakwenda.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika saa 6:10 mchana, akamuona ananyanyuka. Akajua ndio
anakwenda huko. “Nikuletee nini?” Akamuuliza. “Na mimi nakutana na Jelini saa
saba kamili kwa chakula cha mchana. Ameniomba anitoe kwa lunch.”
Akafikiria kidogo, akatoka.
Palipomwagika Maji.
Alifika hapo ili asichelewe kama kawaida yake, lakini akakuta
Hope akimsubiria. Alikuwa kama mgonjwa, mpaka Junior akashituka. “Unaumwa!?” Akamuuliza.
“Hapana. Ila nashukuru kwa kuja kunisikiliza.” Hope alikuwa amenyongea. “Najua
nilikuomba msamaha siku ya jumapili na nikakuahidi nitabadilika. Lakini nimekosea tena.” Akaanza kulia. “Tunaweza
kuagiza kinywaji kwanza?” Junior akauliza wakati muhudumu akiwasogelea.
Akaagiza juisi ya embe, Hope akajifuta machozi na kuagiza maji ya kunywa.
Muhudumu akaondoka akiwa amewaachia menu ya chakula.
“Nimekosa na kujichanganya kupita kiasi na
sijui chakufanya.”
“Labda nikuulize Hope, tatizo ni nini?!” “Hakuna
tatizo Junior. Mimi ndio tatizo. Nilikosea tangia mwanzo wakati unanionya juu
ya Jelini. Nikashindwa kuchukulia zile taarifa vizuri, nikaendelea kuharibu.
Nimekosa Junior. Nimekosea hata kuacha uongozi bila ya kukutaarifu. Nimekosea
jinsi nilivyoacha. Nimekosea hata kwa Jelini. Najua nimekuumiza, ila nakuahidi
kuanzia leo nitakua nikikushirikisha, na kukusikiliza. Nisamehe Junior.
Nimekosa.” Junior akabaki kimya.
“Nimekosa Junior. Nisamehe.” Ubaya wa Junior
hakuwa amemtafuta tokea aombe msamaha na kuahidi kujirekebisha na kesho yake
kuharibu zaidi, pia hakumtafuta. Alinyamaza kimya. Na hapo akawa amenyamaza
kama anayefikiria. Muhudumu akaleta vinywaji, wakaomba asubiri swala la
chakula.
“Naomba usinikatie tamaa Junior! Nimekosea, na
nakuahidi nitajirekebisha.” “Labda nikuulize swali. Na naomba ufikirie kabla hujajibu.”
Hope akatulia. “Ni kwa nini unataka kuwa na mimi?”
Hope akababaika kama ambaye hakutegemea hilo swali. Lilikuwa swali rahisi, ila
akashangaa kwake limemuia gumu. Junior akaendelea kunywa kinywaji chake kisha
akaongeza.
“Nashauri kabla hatujaenda mbali, kapate muda wa kufikiria. Maana
haya yanayoendelea kwako, ukiwa kwenye mahusiano yaliyofika mbali kama hivi, sidhani
kama ni kunijali hata kidogo.” Hope akashituka sana.
“Nakujali Junior!” “Kama ungekuwa
ukinijali hata kidogo, ungenifikiria ile fedheha uliyoniachia mbele ya
watu siku ya jumapili. Tena zaidi ya mara moja! Yaani kwa kurudiarudia, hadharani!
Binafsi nisingeweza kumfanyia hivyo hata mtu baki tu. Halafu kana kwamba
haitoshi, tunazungumza usiku, kesho yake unamuadhibu baba yangu kwa
mazungumzo ambayo umekiri hutarudia tena kwa kuwa ulikosa! Sasa na
sasahivi tunarudi palepale kuwa ‘umekosa, hutarudia tena’. Unamaanisha
nini!? Pengine mimi ndio nashindwa kuelewa?” Hope akashindwa kujibu kabisa,
akabaki akilia.
“Tafadhali tuzungumze Hope. Maana hapa tunazungumzia juu ya hatima
ya maisha yetu yote ya hapa duniani. Sitataka uishi na mimi kwa kulia,
na mimi sitataka kuishi bila furaha na amani. Hatuna sababu ya kufanya
hivyo. Kwa nini?!” “Nakuahidi sitarudia tena
Junior.” “Kwa nini?” Junior akaendelea kuuliza.
“Nakupenda Junior. Natamani tuishie pamoja. Na
sidanganyi. Ni vile tu sijui jinsi ya kutenda sawasawa. Nimekukosea adabu wewe
na mzee. Ila nimekuja kufikiria, na mimi nimegundua nimekosa Junior. Nimekosa,
naomba nisamehe. Nimekua na haraka ya mambo, nimekosa muda wa kujitafakari. Ila
nimepata muda wa kujifikiria, nimegundua makosa mengi hata ambayo hutayataja
hapa, lakini nimepata muda wakujifikiria, nimegundua nimekukosea kwingi na
unahaki ya kunichoka Junior.”
“Nimerudi kwako, nimekiri makosa yote. Kuzembea kote ambako
nimekufanyia. Naahidi nitabadilika, tena kwa vitendo. Najua huwa nakulazimisha
kufanya maamuzi. Lakini safari hii nakuacha kabisa. Na pete yako nakurudishia
kabisa. Ukiona nastahili nafasi ya pili, na upo tayari na mimi kwa mara ingine,
basi naomba unitafute. Ila kama unaona huna nafasi yangu nyingine, basi Junior.
Mimi ndio nimekosa. Nimevunja mahusiano yetu. Sitakulaumu. Ila ukinirudia,
hutajuta tena. Na ujue utakua huanzi upya. Upo na mtu anayekufahamu. Hutapata
shida..” Akaweka pete mezani Junior asiamini.
“Unafanya mchezo wa hatari Hope wewe!” “Hamna maana ya hii
pete kama nitakukosa wewe mwenyewe Junior! Umenipa vingi. Vingine siwezi
kurudisha maana kama gari ndio miguu yangu hapa mjini na ile nyumba ndio naishi
hapo?”
“Najua umekasirika, kuniacha haitakuwa shida. Ila ujue mimi
nipo, na nakusubiria. Na ukinirudia hutajuta tena. Nitakuwa
nikikusikiliza na kukupa nafasi hata uwe unafanya maamuzi yako bila
kukuingilia. Na…” Aliendelea kutaja mapungufu yake hapo, Junior akimtizama tu.
Kisha akaaga na kuondoka hata chakula hakula ila aliacha pete juu ya meza. Junior
akaagiza chakula, akaendelea kula taratibu. Kimyakimya, akitafakari maisha
yake.
Ofisini.
Ezra anatoka kula anarudi ofisini akiwa na furaha, akidhani
pengine wametengeneza, akaenda kumuwekea matunda aliyomjia nayo hapo mbele
yake, pembeni ya kompyuta aliyokuwa akitumia. “Jelini anakusalimia.” “Asante.
Mmekuwa na wakati mzuri?” Jinsi alivyokuwa akiuliza si kama aliyekasirika ila
aliyekuwa mbali kimawazo. “Utamuweza Jelini!” Akajibu akienda kukaa mezani
kwake. Ndipo akagundua kuna pete ya uchumba ya Hope. Alishituka hakutarajia.
Ilikuwa kama ameachiwa yeye hapo mezani kwake. Akaichua na kubaki
akiitizama kisha akamtizama Junior. Busy na kazi.
“Ni nini kinaendelea Junior!?” Ikabidi aulize. “Hope
amenirudishia.” Ezra akashindwa kuelewa. Ikabidi aulize tena. “Kwa makubaliano
gani?” Akamuona anacheka kwa masikitiko. “Yaani mimi namvalisha pete kwa
heshima mbele ya wazazi wangu, ananirudishia mgahawani! Eti ananiambia, nitakapoona
nipo tayari na yeye tena, eti mimi ndio nimtafute! Umeona wapi hiyo!?”
“Subiri kwanza Junior. Kwani ilikuaje?” Junior akamueleza mwanzo mpaka mwisho.
“Nilitamani kumsikia anapambania mahusiano yetu Ezra!
Leo ananirudishia mimi pete, na kuniambia nije kumtafuta tena, kana kwamba eti
mimi ndio nina shida kubwa sana na haya mahusiano! Yeye nafasi yake ni
ipi sasa? Kwa nini akimbie pakiwa pametibuka, asibaki akitengeneza kama kweli
ananipenda?” Ezra akatulia akitafakari.
“Hivi unajua alishindwa kabisa kunijibu ni kwa nini anataka
kuwa na mimi!” Ezra akakunja uso kama ambaye ameshindwa kuelewa. “Exactly!
Na mimi nikashangaa hivyohivyo kwamba alishindwa hata kudanganya kwa
kusema pengine ananipenda! Kitu ambacho wachumba huambiana hata kama
hisia zinakuwa ziliisha, japo kwetu sidhani hata kama zilikuwepo!” Junior
akaendelea kulalamika.
“Nilimchumbia mbele ya wazazi na kanisa, tukawekewa mikono,
na mimi nilimpa hii pete nikiwa sijaribishi. Na yeye nilimwambia huu
ukurasa nafungia kwake, sitatafuta tena. Sasa sijui akajiaminisha sana, ameishi
na mimi kama unavyojua. Kiburi wakati wote. Amenikosea. Kwa kuwa anajiamini
sana, anarudisha pete akiwa na uhakika ni lazima itarudi tu kwake!”
Junior akacheka na kutingisha kichwa.
“Pengine hakuwa amemaanisha hivyo! Sijui! Simtetei. Maana
jinsi nilivyozungumza naye ni kama hataki kukupoteza.” “Na mimi
ameniambia anataka kuwa na mimi. Ndio nikamuuliza kwa nini, huwezi amini hilo
swali likawa gumu kwake.” “Junior!” “Hakika siongopi. Si nimetoka kukusimulia
hapa? Ndio ikabidi nimwambie akapate muda wa kufikiria kabla hatujaendelea.
Halafu eti baadaye ndio anakuja kusema ni kwakuwa nanipenda. Yaani kama
aliyekuwa akitafuta jibu! Kweli Ezra! Mpaka nahisi yupo na mimi kwa sababu ya pesa,
misaada ninayompa, na si mapenzi.” Hapo hata Ezra akaanza kuumia.
“Ezra, mapenzi hayajifichi jamani! Hufikirii
kumwambia mpenzi wako kama unampenda! Inamuwia ngumu hata kuropoka tu kama
ananipenda!” Ezra akapoa kabisa.
“Hapana Ezra. Kuna tatizo kati yangu na Hope, au nimekuwa nikilazimishia
kitu ambacho hakipo kwa muda mrefu sana. Nimekaa nikifikiria na kuona
hata anashindwa na Emelda!” Ezra akakunja uso.
Ukisema Cha Nini, Wapo Wanaolilia Kukipata.
“Emelda yule wa nyumbani!?” “Kabisa Ezra. Hope amenifanya
nijifikirie sana. Amenifanya nitulie na kutafakari na usiku nikashindwa kulala.
Hope ambaye ni mchumba, anapitwa mbali sana na Emelda, msichana wa mama.
Haya unayomfanyia Jelini wewe, ndiyo anayonifanyia Emelda ila
nikipuuza nikichukulia ni wajibu wake au nikidhani mama anamtuma, kumbe ni yeye
tu mwenyewe.”
“Usiku nimerudia jumbe zake, mpaka nikashangaa.” “Junior!”
“Hakika sizushi Ezra. Nikikwambia sikulala jana usiku, ujue sijalala nikijaribu
kutafakari na kujiuliza nilishindwa vipi kuelewa?” Junior akakaa sawa.
“Unakumbuka miaka miwili iliyopita mama yake alikuwa
mgonjwa?” Ezra akabaki akimtizama, pete aliyovua Hope ameshika mkononi. “Acha
kuniangalia kama niliyechanganyikiwa.” “Hakika naomba nielewe na mimi Junior.
Mambo mengi yanapita kichwani mwangu sasahivi ila wewe ulishapata muda wa
kuyatafakari usiku kuchwa. Najaribu kuyaweka sawa. Wrapping my head around
it. Endelea.” Junior akakubaliana naye. Zilikuwa ni taarifa nyingi kwa
wakati mmoja.
“Mama alimpa pesa na kumwambia arudi kwao, akamuuguze mama
yake. Alinifuata tukiwa kanisani siku ya jumapili. Sema sikutilia
maanani. Ndio sasahivi kumbukumbu zinanijia kana kwamba nilifunga macho, ndio
yanafunguka. Ila aliniambia hivi, ameshindwa kuondoka mpaka aniage.
Akaniambia anarudi kwao, hajui atarudi lini, mama yake ni mgonjwa, anakwenda
kumuuguza mpaka apone. Mimi moja kwa moja nikajua anataka nimuongezee pesa.
Bila ya kufikiria nikampa pesa na kumwambia akiwa na shida yeyote akiwa
nyumbani, asiache kuwasiliana, sisi ni ndugu, asiuguze peke yake. Nakumbuka
mpaka sura yake jinsi alivyofurahia kusikia hivyo na wala si pesa.” “Kwa hiyo
mlikuwa mkiwasiliana alipokuwa nyumbani?” Akampa simu yake.
“Hayo ni mazungumzo yangu na yeye, tokea wakati ule mpaka
majuzi analeta chakula nyumbani.” “Subiri kwanza Junior! Inamaana
anayetuleteaga chakula nyumbani si mama ni yeye?!” “Ndivyo na mimi nilivyodhania
muda wote. Kumbe wala mama hajui au hausiki. Yeye anapika, kisha
anamtuma Noah au dereva atuletee. Vinawekwa kwangu ndio tunakula kama vile,
nikijua ndio utaratibu wa mama kwa kuwa siku za ijumaa anajua tunakua tumefunga.
Kumbe mama hausiki kabisa.”
“Sasa wewe umewezaje kujua kama si mama?” Ezra akazidi
kudodosa. “Cha kwanza hata wewe ukisoma hizo jumbe kwa kutulia, utagundua ni
wazo lake, na utagundua anapika vitu vile anavyojua napenda, na
ndio maana utagundua anajirudiarudia kwenye vyakula anavyotuletea. Pili, jana,
ilibidi kumuuliza mama kwa umakini huku nikimchanganya na habari zako za
kuchumbiwa na Jelini.” Wote wakacheka.
“Amesemaje?” “Kwanza amefurahi sana. Ila amesema tumetia
aibu, tumepitwa. Leo wanakwenda kuzungumza na mama Jema, tujipange. Ila
sasa nikamchomekea kuwa sasa si itabidi atuletee chakula cha pongezi? Akanijibu
hivi, yeye alitubembeleza sana tusihame nyumbani, mpaka tuoe. Tukakataa
tukijiona tumekua. Akasema wazi kabisa, tukitaka chakula chake twende tukale
kwake, tena kile anachompikia mumewe, ndio na sisi tule hichohicho. Vinginevyo
tuoe, tuache kuchosha wake za watu.”
“Haiwezekani Junior!” “Hakika. Ndipo nikajua huyu Emelda
anapika kwa siri hata mama hajui. Na ndio maana vyakula vyake vinakuja mchana
wazazi wakiwa hawapo nyumbani na sisi tupo kazini. Kama anayejiiba. Au mama
anajua, amelifumbia tu macho.” Ezra akazidi kushangazwa.
“Sasa pesa huwa anapata wapi?” “Mimi sijui anajinyima vipi
mpaka anapata pesa yakupika vyakula vyote hivyo. Pengine hizi pesa ndogondogo
tunazompa. Sijui.” “Mmmh! Hii imenifanya nimfikirie kwa tofauti, aisee na
kunifanya nikumbuke mengi!” “Mimi zaidi mpaka najuta.” Ezra akamtizama
kama mwenye swali.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kosa la Mchumba, limefungua mwanya wa
KUWAZWA msichana anayefanya kazi za ndani kwa muda mrefu kwa mama mchungaji. Hatimaye
wema wake UMEFIKA akilini kwa Junior. Ni nini kitaendelea? Hope atarudishiwa pete ya
uchumba?
Mkakati wa kuchumbiwa
Jelini unaendelea. Watafanikiwa?
Usikose
muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment