Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 34. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 34.

SUBIRA INAPOVUTA KHERI.

Vai  alikuwa akimalizia mtihani wake wa mwisho wa vitendo siku hiyo ya

jumamosi asubuhi. Kama lilivyo jina lake, herufi ya mwishoni kwa hiyo akawa amepangiwa wa mwisho kwenye mtihani huo. Alilala chuoni karibu majuma mawili kwa ajili ya mitihani hiyo ya kumaliza mwaka wa kwanza. Walishakuwa na hamu na kila mmoja wao, wakabaki wakihesabu siku mpaka masaa watakaporudi kuwa pamoja nyumbani.

Wenzie walifanya mitihani mapema kwa zamu, mpaka ikafika zamu yake. Alikuwa amechoka na mitihani mfululizo. Akili na mwili vilikuwa tayari kwa mapumziko ya shule ya mwaka mzima. Akafanya kwa umakini akijua anamuwakilisha na Bale wake aliyekuwa akisoma naye bila kuchoka na kumtia moyo usiku na mchana bila ya kumkatia tamaa.

Alipomaliza tu na kuridhika amefanya vizuri akamtumia ujumbe Bale hata kabla hajatoka kwenye jengo alilokuwa akifanyia mtihani huo. ‘Kwa mwaka huu, tumemaliza mpenzi wangu. Tunapumzika mpaka mwakani. Na HAPANA, sijakuabisha. Ninauhakika nimekuwakilisha vizuri.’Akautuma huo ujumbe. Akafikiria tena mtihani jinsi alivyofanya, hofu ikamuingia. Akaandika ujumbe mwingine. ‘Nafikiri.’ Akautuma.

Hapohapo Bale akampigia akicheka. “Sasa tena mbona unatia mashaka nesi wangu?” “Mimi sijui bwana! Ila nafikiri nimefanya vizuri.” “Mimi nina imani na wewe.” “Basi nasimamia imani yako. Naamini nitafaulu. Ujue sasahivi nina hamu ya nini?” “Kulala tu.” Bale akajibu kwa haraka bila ya kufikiria na kumfanya Vai kucheka. 

Kisha akamuuliza. “Umejuaje?” “Umenitumia ujumbe saa nane usiku. Tukaongea saa 10, ukiwa umechangamka tu, ila hofu ya mtihani. Saa 12 asubuhi ukatuma ujumbe mwingine kuwa tumbo la hofu linakuuma. Tukazungumza mpaka saa moja.” Vai hana mbavu. “Kwa hiyo najua hujalala.” “Na nataka kulala sehemu ambayo wewe upo. Ukitoka kazini nipitie.” “Sitakuweka. Nakuja. Na ujue nimekuandalia mazingira mazuri ya kulala na kupumzika. Nakusubiria Vai wangu.” “Jamani Bale wangu! Nashukuru. Na mimi nina hamu kweli na wewe.” “Nakuja.” Wakaagana kwamba anakwenda kumalizia kufungasha, akifika ampigie aanze kushuka na mizigo yake. 

Ilikuwa likizo ndefu. Kuanzia huo mwisho wa mwezi wa tano mpaka kurudi tena mwezi wa 9. Hata magodoro walikuwa wakirudisha stoo. Hakuna kuacha kitu hosteli. Alishapunguza asilimia kubwa sana ya vitu na kuhamishia nyumbani kwa Bale na wala si kwa mama yake. Wawili hao walishazoea maisha ya kuishi pamoja. Hakuna aliyeweza kuishi tena bila mwenzie japo bado hapakuwa na kufanya mapenzi. Hapo ndani wanafuatana mpaka kusubiriana bafuni. Wanaongea huku wanasubiriana. Mmoja nje ya bafu, mwingine anaoga ndani wakiongea na kucheka.

Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,Kwa paa na kwa ayala wa porini,

Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.

Uzalendo ukamshinda. Alishakuwa na hamu na Vai, akili haifanyi kazi. Akaona ampigie simu Joshua. Akapokea kwa haraka tu. “Kwema?” “Kwema. Nina swali. “Karibu.” Akafikiria jinsi ya kuuliza swali lake, akasita. “Mbona unanitisha wakati kila kitu na kila mtu yupo tayari?” “Hapana. Kila kitu kipo sawa. Ni swali binafsi.” “Oooh!” Joshua akasikika kutulia sasa, maana alifanya maandalizi ya nguvu maalumu kwa siku hiyo.

“Karibu.” “Eti ni dhambi kukiss!” Joshua akaanza kucheka. Hakutarajia. “Sijawahi kumkissVai hata mara moja! Leo kwa mara ya kwanza nilitamani kufanya hivyo. Au niseme nimekuwa nikitamani sana. Nampenda Vai.” “Naelewa. Kiss kama Kissing, yenyewe haina shida ila swali la kujiuliza ni je, una KIASI?” Bale akatulia.

“Maana kissing kwa mtu unayempenda lazima itaamsha hisia kali ndani yenu. Utaweza kujizuia usiendelee zaidi! Hayo ni maswali inakupasa ujiulize wewe mwenyewe na uwe mkweli kwako.” Joshua akaendelea.

“Mimi nilikiss kabla ya ndoa. Ninachotaka kukwambia, ni kweli si kitu rahisi. Ila binafsi nilisaidiwa na mambo makubwa matatu. Maana na mimi ni binadamu kama wewe tu Bale. Kwa vyovyote utakavyoniona na kunichukulia, nina mwili wenye hisia kwa asilimia 100.”

“Kwahiyo pale nilipozidiwa, moja, nilikuwa nakumbuka kuwa nimechumbia binti ya mtu, ambaye alikuwa akimchunga binti yake kwa maombimacho yake na maneno hata kwangu. Ikaongeza hofu na heshima kubwa sana kwa mchumba wangu. Nisingethubutu kuvuka mipaka wakati baba yake alikuwa akitufuatilia hata kiroho na wakati mwingine hata kuomba na mimi.”

“Kingine kilichokuwa kikinisaidia pale ubinadamu ulipokuwa ukinizidia, hisia zimepanda sababu ya kuchochea mapenzi, ni MAZINGIRA. Hapakuwa na mazingira rafiki. Wengi wanaishia kuzini sababu ya mazingira kuruhusu. Kama hayo mazingira yako wewe na Vai. Mnayo faraghayakuwatosha. Ndipo unapotakiwa kujiuliza bila kujidanganya, Je utaweza kuendelea kuishi na Vai nyumba moja, peke yenu, halafu ukaishia kwenye kukiss tu?”

“Maana nihisia ambazo sina jinsi nikakueleza ukaelewa pale zinapokuwa zimepanda! Hazizimiki kwa urahisi na ukumbuke kwa wakati huo hutakumbuka maombi kabisa.” Bale akacheka akisikiliza. “Nakwambia ukweli maana hapo ulipo na mimi nilikuwepo. Bibilia inaposema usiyachochee mapenzi, niamini haiongopi. Ni moto unaoweza zimwa kwa kitendo chenyewe. Je, utaweza? Unayo hiyo stamina?”

“Yaani uwe umewakwa tamaa kabisa. Mazingira yanaruhusu. Vai yupo chumbani. Amelala. Hakuna anayekuzuia. Hata ndugu wanajua anaishi kwako! Ndio jiulize, utaweza kuishia hapo tu kwenye kissing na kurudi kulala kwenye kochi ukamuacha Vai?” Bale kimya.

“Na kingine, najua hapo ulipo sasahivi utajiambia itakuwa LEO tu.” Bale akashangaa ni kama aliyeyasoma mawazo yake. “Nasikitika kukwambia, SIO kweli. Kila siku kuanzia mara ya kwanza mkianza, hutakosa sababu ya kwa nini msikiss tena! Ukitaka kumpongeza, utabakiwa na njia moja tu. Kissing. Ukitaka kumshukuru, kueleza hisia zako kwa namna yeyote ile, chochote kile kuanzia hapo, njia ya kuwakilisha hisia zako nzuri kwake itabakiwa ni hiyohiyo. Kwa hiyo nakuhakikishia haitakuwa mara moja tu. Mtaendelea. Ndipo rudi kwenye swali langu la kwanza ambalo usinijibu mimi ila wewe mwenyewe. Je, unalo TUNDA la kiasi kwa kiasi gani?”

“Jambo la mwisho lililonisaidia mimi, ni mimi si kama watu wengine Bale. Kuna mahali Mungu aliponitoa, kiasi ya kwamba hata nikishawishika kumtenda Mungu dhambi, napatwa hofu ya ajabu sana. Sisemi mimi ni mkamilifu, ila nilikopitishwa na maisha, kumenijengea nidhamu ya hali ya juu na hofu ya Mungu. Ninahofu ya kukosana naye, sababu sina kimbilio.”

“Kwangu ule mtindo wa kutubu na kutenda dhambi tena na tena, ukijua utatubu tu tena, hauna nafasi kwangu kwa sababu sina kimbilio jingine ila kwa familia ya pekee niliyokuwa nayo, ya mbinguni. Mchezo wa kujichafua na kutubu, sijabahatika hiyo nafasi kwa sababu nataka kila anayehusika na mimi huko mbinguni nikiita, waitike kwa haraka ili nisibaki tena peke yangu, na kuharibikiwa. Maana mimi najijua Bale. Si mkamilifu ila mimi si kitu kabisa.”

“Kwa hiyo japokuwa nilishaanza kukiss. Ilipokuwa hali ni mbaya, japo nilikuwa nikijitahidi sana nisivuke mipaka kwenye kissing zangu. Sikumshika mchumba wangu kwa undani mpaka ndoa. Lakini pia kile kitendo tu chakumkiss mwanamke ninayempenda, tena najua ni wangu, Mungu amenipa kuwa mke wangu, kilipokuwa kikiibua hizo hisia kali, sikuachwa kukumbushwa mimi ni nani na nilipotolewa na huyu Mungu. Kwa hiyo hofu ikawa inanifanya najirudi kwa haraka sana, ila nikisaidiwa na zile sababu za mwanzoni.”

“Utamchezeaje binti ya mtu kama baba Naya? Anaomba na kutembea na binti yake kila wakati! Halafu ndipo inakuja swala la mazingira. Sikuwa au sikuweka mazingira rafiki. Kwa hiyo iwe kwa kupenda au kutopenda kwangu, sikufanikiwa kuvuka mpaka. Ninachojaribu kusema ni kwamba, hilo ni swali ambalo ni LAZIMA ujiulize mwenyewe, na uwe mkweli kwenye kujijibu.”Bale akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha.

“Vipi lakini, upo tayari?” “Aisee nipo tayari Joshua. Nashukuru sana. Hii siku nimekuwa nikiisubiri kwa kufunga na kuomba. Naamini nipo tayari kabisa.” “Tupo pamoja. Naona na Naya atakuwa anakaribia hapo. Mimi sipo mbali. Tulitaka tuwepo hapo kabla ya wengine ili kuwapokea na kuwapa muongozo.” “Nawashukuru kwa kila kitu.” Wakaagana na kukata simu. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akamuacha Bale njia panda, vibaya kuliko alivyofikiria. Maana alijua kwa Joshua pengine angepata jibu la ndiyo au hapana. Lakini akaachiwa yeye mwenyewe. Akabaki garini akifikiria mpaka Naya alipomgongea kioo. 

“Toka sasa hapo niachie gari.” Bale akashuka akicheka. “Si ungenisalimia tu?” “Utanipotezea muda. Ondoka Bale.” “Sawa. Ila ujue nashukuru. Na nimekuachia hapo nyuma ya gari pasafi kama ulivyosema.” Maandalizi yakaanza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kila kitu kilipokaa sawa ndipo akamtumia ujumbe. ‘Nipo hapa nje nakusubiria.’ Vai akasoma na kuendelea kukusanya vitu vyake kwa haraka bila ya kujibu. Nia akitaka asimuweke sana hapo nje akimsubiria. Akafanya yake mpaka akamaliza. Akaanza kusombelea vitu garini. Akaanza kwa kubeba vichache akashuka kuelekea anakojua Bale hupenda kuegesha gari.

Akamuona amesimama kwa mbali, akaongeza mwendo akicheka. Na Bale akawa anamfuata. “Eti moyo wangu umejawa furaha gafla baada ya kukuona! Nilikumiss bwana Bale!” Bale akacheka akiendelea kumsogelea. “Na mimi nilikumiss. Afadhali shule imeisha. Nikupokee baadhi.” Akamkabidhi baadhi wakawa wanaelekea garini.

Kugundua gari ilishafunguliwa maana nyuma palikuwa wazi, Vai akaongeza mwendo kulifikia, asijue amemuacha Bale nyuma. “Nafanya haraka ili nisikuweke sana. Tunaondoka hapa sasahivi.” Kadiri alipokuwa akisogelea gari akagundua hapo nyuma si patupu. Akakunja uso akijiuliza ni wapi aweke mizigo yake! 

“Gari ipo kama ina vitu tayari! Itatosha kweli na mizigo yangu au niweke kiti cha mbele?” Akashangaa Bale hamjibu, akageuka. Akamuona amepiga goti. Yeye Vai akili ikamwambia ameanguka. Akatupa kila kitu alichokuwa ameshika na kurudi kwa haraka pale juani alipokuwa amepiga goti Bale. 

“Pole sana. Umeumia?” Akawa akimsogelea kwa haraka na huruma tayari. Maana na vile alivyokuwa amempokea aliweka chini, yeye akili yake ikamwambia vimeanguka alipoanguka.

Akamfikia. “Pole. Nakushika chini ya kwapa nikunyanyue.” “Sijaanguka bwana Vai! Mbona unawasiwasi?” Vai akawa hajaelewa. “Sasa wewe naku surprise vipi mpenzi wangu!?” Pia bado akawa hajaelewa. Anachotaka asimame pale alipokuwa juani.

“Vai! Najua umechoka. Lakini tulia, fikiria. Sijaanguka. Na pale nyuma kwenye gari…” “Kuna mizigo, nimeshindwa kuweka hivi.” “Basi naomba nenda kaangalie kwanza.” Akaenda hatua chache akamgeukia. Bado amepiga magoti! 

“Sasa kwa nini ukae juani bwana!” “Usiwe na wasasiwasi na mimi. Nipo sawa. Naomba nenda pale kwenye gari. Kaangalie kwanza.” Akamuona anaondoka lakini kama aliyechanganywa, na hajafurahia. 

“Moyo wangu hauna amani hapo ulipo juani. Siwezi kukuacha Bale.” Akasimama kabisa kama aliyegoma kuondoka. “Nipo sawa Vai! Nenda bwana. Ni kitu kizuri SANA, utafurahia.” “Siwezi kama wewe upo juani. Hivyo mimi sipendi. Moyo wangu hauna furaha. Njoo twende wote.” “Daah! Mchaga wangu kumsuprise ni kazi! Haya mama.” Ikabidi asimame maana aligoma kabisa kuondoka na ni kweli jua lilishakuwa kali. 

“Sasa ni surprise gani hizo za juani! Basi nikwambie huo ndio ushamba.” “Sawa Vai. Mimi ndio mshamba.” Akaanza kucheka na kurudi pale ili kumsaidia kubeba. “Hivi vitu nilikupokea Vai! Tafadhali acha.” “Bale naye hajui kupendwa! Basi hapo mtu mwingine angefurahia.” “Anafurahia kupokelewa mzigo ambao alikusaidia?” Akaanza kucheka wanarudi garini.

“Na uwe unakumbuka hapa ni hospitali kuu ya Taifa. Kuna kila gonjwa. Shauri yako kushikashika chini.” Akaanza kuokota vitu vyake, ikabidi tu Bale abaki amesimama pembeni ya gari na mizigo mkononi maana Naya alihangaika kweli kupamba hilo gari ili wamsurprise Vai.

Akamaliza na kusimama akamuona bado Bale amesimama na mizigo yake mkononi. “Sasa si uweke ndani ya gari!?” “Siwezi sababu hapo ndani ya gari nimekuandalia zawadi yako. Mpaka uchukue ndipo tutaweka mizogo.” Akaanza kucheka ila akakubali maana hapo amesimama naye.

“Kumepambwa vizuri, mpaka naona shida kuweka mizigo yangu!” “Ndio usiweke.” Akaangalia na kugundua ni matawi ya maua ya roses. Yamepangiliwa vizuri sana. Alama ya moyo. Yananukia vizuri. Ikamchanganya. 

“Acha tu nikubali kama mimi ndio mshamba. Maana haya maua ni mazuri sana, na yanavutia. Asante mpenzi wangu. Ila sasa kwani natakiwa kuyafanyaje?” Alimfanya Bale aangue kicheko nakushindwa kujizuia. “Sawa Bale! Ila ujue hapo nimekwama. Hizi surprise nyingine uwe unaniandaa hata kunionyesha movie kwanza. Maana hapo nafikiria sijui nichukue mfuko niyazoe na kuyaweka humo! Au natakiwa kufanyaje?” Bale hana mbavu. 

“Mwaya Bale!” Akaweka mizigo yake chini. Akili yake ya usingizi ikamwambia kweli ayakusanye yale maua, ayaweke kwenye pochi yake. Akaanza kuyazoa anaweka kwenye pochi aliyokuwa amening’iniza begani. Bale hana mbavu. “Ukumbuke hii siku Bale. Unapofika mahali, hujui chakufanya, halafu nimebaki mimi ndio mkali wako.” Akaendelea kuongea akikusanya maua akiweka kwenye pochi mpaka akafikia kimkebe.

Bale akamuona amekunja uso wakati akikitoa. Akaona kimkebe cha sonara. Akacheka akijua ni hereni tu kama alivyomzoesha kumnunulia dhahabu. Akamwangalia akicheka kama aliyegundua sasa. 

“Bale siku hizi umepanda chati! Zawadi unaniwekea kwenye maua! Jamani mimi Vai napendwa!” “Ushamba tu.” “Bale naye! Taratibu, nitazoea.” “Fungua sasa Vai, mbona hivyo!” Akacheka akianza kufungua.

Akashituka sana kukutana na pete ya uchumba. Kumgeukia Bale akamkuta amepiga goti, ndio akaelewa. “Bale!” “Nakupenda Vai wangu. Muda wa Mungu umefika, na sisi tufunge ndoa.” Vai hakuamini. Machozi. “Kwa hiyo tumekubaliwa nyumbani?” “Ndiyo. Sasahivi umebaki wewe tu. Ukikubali, tunafunga ndoa kabla hujarudi chuo.” Alifurahia Vai. Akaweka pete pembeni na kumkumbatia mwenzie amepiga goti.

“Pete kwanza Vai, lakini mbona hivyo!” “Acha nifurahi kwanza Bale. Siamini!” “Basi nipe hiyo pete nikuvalishe.” Akamuachia akicheka huku akijifuta machozi. “Nimefurahi Bale! Kweli nimeamini kuna wakati wa Mungu.” “Umeona eeh! Marufuku kukata tamaa.” Akamvuta mkono na kuanza kumvalisha. Mara Vai akashangaa watu wanashangilia mpaka na vigelegele na kuwasogelea. Alishituka! Hakujua kama kuna watu wengine. Alishajizoelea maisha yake na Bale tu.

Ila siku hiyo alikuwa Naya na mumewe. Familia ya Magesa wote mpaka watoto wao na mama G. Kaka yake na mkewe{Jema}. Viola na mtoto wake, pamoja na wazazi wao. “Mpaka baba!” Hapo Vai akashindwa kujizuia. Akalia kwa furaha. Mzee wa migombani-mjini! 

“Usilie sasa.” Bale akajaribu kumtuliza. “Mimi sikujua! Sijategemea!” “Hongereni sana.” Kila mtu akawapongeza na kuvuta macho na masikio ya wanachuo wengine waliokuwa wamezagaa hapo wakifurahia kumaliza huo mwaka wa shule na wengine wakipakia mizigo yao na wao tayari kuondoka hilo eneo la shule kama Vai.

Ndipo wakaanza kumcheka Vai vile alivyokuwa akiokota maua na kuweka kwenye pochi. Walicheka mpaka machozi. “Mimi nilikuwa sijui chakufanya bwana!” Watu wakazidi kucheka. “Shida kumsuprise huyu!” Bale akaongeza na kufanya wazidi kucheka jinsi alivyoshindwa kuelewa tokea mwanzo.

“Mimi nilijua ishashindika vile alivyomtoa pale juani alipokuwa amepiga goti.” Mama G akaongeza na kufanya wazidi kucheka. “Mimi mwenyewe nilishamwambia Joshua, tuwasogelee tu, ishashindika vile alivyogoma kurudi tena kwenye gari. Joshua akasema tusubiri tu mpaka mwisho tuone.” Wakazidi kucheka.

“Kwani wewe hujui mtu akitaka kuvalishwa pete, mwanaume anapiga goti?” “Najua kaka. Lakini pale mimi akili iliniambia ameanguka. Nikashindwa kufikiria vingine kabisa, nikaingiwa hofu.” “Ndivyo tulivyokutana naye huyu kwa mara ya kwanza. Aliniokota juani, nikiwa nimeanguka kule kitengo cha MOI. Sasa naona ile ilimuingia akilini na moyini. Ningekumbuka hilo tusingefanyia maeneo haya.” 

“Ila kweli Vai anakupenda Bale! Mpaka Joshua amesema! Anakupenda ile yakutoka rohoni.” “Hata Geb amesema hivyohivyo kuwa Vai anaonekana kumpenda sana Bale. Japo ameambiwa kuna zawadi garini, lakini ameshindwa kufuata zawadi kabisa, akili zimebakia kwa mwenzie pale juani!” Vai akacheka kwa aibu akishindwa kuwaangalia.

“Hongereni sana.” “Asante baba. Sijategemea kabisa kukuona hapa! Nimefurahi! Asante umekuja baba yangu. Wote, nawashukuruni kuja. Nimefurahi! Nilikuwa hata sijui, maana kulikuwa kimya, na kaka hakurudisha jibu na hakuwa akizungumzia kabisa. Nikajua baba umekataa.” “Nilimrudishia jibu Bale, mapema tu. Ila akaomba tusubiri kwanza umalize mtihani, tusikuchanganye. Haya maandalizi yote yalikuwa yakiendelea kwa muda tu, tokea umeanza mitihani. Joshua ndiye aliyemuomba baba kama anaweza kuja na yeye kuhudhuria kwenye shuguli nzima. Juzi ndio baba akatoa jibu kuwa atakuja. Ila yeye hatukuwa tukimtegemea.” Vai alikuwa na furaha yakupitiliza. 

Bale naye akapata nafasi ya kuwashukuru wote. Joshua na Naya wakawakaribisha wote nyumbani kwao kwa chakula cha jioni kama tafrija, kumshukuru Mungu kwa hilo na kujipanga na mambo ya mahari pamoja na harusi. Hata hilo likamshangaza Vai. Hakujua hata kama kuna maswala ya tafrija!

Ndipo wakatawanyika. Lakini Naya akataka kuzungumza na Vai. “Ukishapumzika, nashauri uende saluni. Utengenezwe, upendeze, maana tafrija yako itakuwa na watu wa maana watupu. Na..” “Lakini sina hata nguo ya maana Naya! Si nitatia aibu? Sikuwa najua.” “Ndio nilitaka kukwambia. Nilijua imekua surprise, nimekununulia magauni matatu. Hata Jema ameyapenda. Uwahi uje ujaribu. Utakaloona umependa wewe zaidi, ndio uvae kwenye tafrija yako.” Vai hakuamini, akamtizama Bale. 

“Asante Naya.” Yeye Bale akashukuru. “Asante Naya! Sijategemea! Nashukuru sana kunifikiria na kujali, wifi yangu. Nitaenda kupumzika kidogo kupunguza usingizi, ndio nikimbilie saluni ndipo nije kwako. Muda gani mzuri?” “Muda na wakati wowote leo njoo. Maana nikirudi tu maandalizi yanaanza.” “Hutaki msaada?” “Nina jeshi langu hilo, wote uliowaona hapa, wanahamia kwetu kwa maandalizi. Nyinyi leo ni siku yenu. Kajitayarisheni, mpendeze ndio mje.” Wakaachana.

~~~~~~~~~~~~~~~~

MAMBO YANAENDELEA…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment