Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 33. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 33.

    “Tafadhali twende Emelda.” “Nilikuwa naoga kaka, nimevaa haraka ili nisikuweke mlangoni. Lakini sijapaka hata mafuta! Na ngozi ya kichwa inaniuma! Nahisi wamenivuta sana wakati wakunisuka. Nashindwa hata kufunga nywele ndio maana zipo hivi! Nitatokaje hapa?” “Kwanza nilisahau tu kukwambia. Umependeza sana. Hivyo ulivyo tu umependeza.” Emelda akacheka kwa aibu. Hajawahi sifiwa naye hata mara moja!

    “Sikudanganyi. Umependeza sana, na imekufanya uzidi kuvutia.” Hapo ndipo akamshangaza zaidi, ila akajikaza akishindwa kumuangalia. “Asante.” “Na pole kwa maumivu. Ila hivyo ulivyo sasahivi, umependeza. Wala huna haja yakugusa hizo nywele, ziache hivyohivyo. Ila naomba mafuta ubebe halafu utaenda kupaka kwenye gari.” Akabembeleza akimshangaza Emelda. Ila akasimama na kukimbilia chumbani, akakwapua lotion na kutoka nayo. Wakaondoka hapo kwa kasi.

    Akampigia simu Ezra akiwa njiani. “Nakuja Ezra.” “Sawa. Ila taratibu, usipate ajali.” “Nashukuru na samahani.” “Naelewa. Hamna neno. Utatukuta.” Akahema kwa nguvu akiendelea kukanyaga mafuta.

Safari Ya Jelini, ‘Wake Wa Peke Yake’,

Inaendelea.

    Walifika nyumbani kwa kina Jelini wakakuta  ndio wanamalizia kula. Mama yao kimya akiwatizama walipokuwa wakiingia ila mzee ndio akawa kama amevurugwa! Jelini akawaambia waende mezani moja kwa moja wajichukulie chakula. Junior akamnong’oneza Emelda. “Nikupakulie?” Akashituka, hakutegemea. “Mimi ndio nikupakulie kaka!” “Hapana. Wewe ni mgeni wangu hapa. Nakuhudumia mimi mwenyewe. Vinginevyo twende ukachague kitu unachopenda.” Akaona bora waongozane. Akamtanguliza.

    Kama kawaida yake, Emelda alipopakua chake, akatafuta sehemu ya kujitenga ili ale akijua lazima Junior atakwenda kukaa na walio wamaana. Ila Junior alipomaliza kupakua akamfuata, “Twende tukakae pale kwa kina Ezra na Jelini.” Akaingiwa hofu. Akasita. “Twende. Nipe na hiyo sahani yako nikusaidie kubeba.” Junior akasisitiza na kunyoosha mkono kabisa kumpokea sahani yake. Akamkabidhi na kusimama, akamfuata mpaka sehemu waliyokuwa wamekaa kina Ezra.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

    “Mgonjwa naona mambo yako si mabaya!” Jelini akamchokoza akiwa mwenzie anatetemeka. Kula na kina Ezra! Emelda hajazoea. “Nimepona.” Akajibu na cheko la wasiwasi. “Na ukapendeza. Umependeza sana.” Akamfanya aone aibu maana Junior na Ezra wote walimwangalia. “Asante.” “Mwaya wewe mpole! Kuanzia leo naanza kuwa kama wewe.” Junior na Ezra walicheka. Wakacheka sana mpaka wengine wakawageukia.

“Nyinyi sio watu wazuri! Sasa mnacheka kwamba siwezi au? Maana nataka pia niwe naongea kama Emelda!” Mpaka Emelda mwenyewe akacheka.

    “Mnacheka nini?” Mama mchungaji akauliza. “Wanao watu wabaya, mama! Mimi nawaambia kuanzia leo nabadilika. Nakua mtu mpole kama Emelda na nitakuwa nikiongea taratibu kama yeye. Lakini…” Mpaka mchungaji akacheka. Kila mtu akabaki kucheka.

    “Hakika mimi siamini! Yaani na wewe mama unacheka!?” Akimuuliza mama Jema. “Huyaweze. Wewe jiachie tu. Huyu binti mpole sana. Mimi namfahamu. Si yupo upande wa watoto kule kanisani?” Mama Jema akaongeza na kuuliza na kujijibu. “Alikuwa akiwafundisha kina Jeremy. Mtaratibu sana.” “Sasa mama hapo wewe unamaanisha nini?” “Wewe huyawezi, jiachie tu.” Wakazidi kucheka, Jelini akanyanyuka kutoa vyombo eti kwa masikitiko.

    “Kweli adui wa mtu, ni wa nyumbani kwake. Mimi siamini!” Akawa analalamika akikusanya vyombo, wengine wakicheka.” Alipokuwa akitoa sasa hivyo vyombo alivyokusanya hapo mezani kama kusafisha, Ezra akaenda kumpokea vile vyombo na kuvirudisha mezani.

    Jelini akacheka. “Nasafisha ili niweke dessert! Naona mchungaji kama amechoka, anadalili za kuondoka wakati mimi sijamaliza kumlisha. Nataka ale full-corse.” Akaongea kwa kunong’ona asijue wameshaanza kuchukuliwa video.

    Akashangaa Ezra anapiga goti na kutoa pete. Jelini alifurahi huyo na kuanza kurukaruka. “Jelini bwana! Sasa wewe umejua ni nini?” Junior akamfanya atulie. “Muone! Umeshaingiwa na hofu!” “Mimi nilijua anataka…” Ezra akamdaka mikono yote miwili. “Utulie sasa. Usikilize.” Junior akafanya wote wacheke. Akacheka na kutulia.

    Ndipo Ezra akaendelea akiwa magotini. “Nakupenda hivyo ulivyo Jelini?” Akacheka. “Hivihivi na maneno mengi?” Akamuuliza, wote wakacheka. “Hivyohivyo ulivyo, sitaki ubadilike.” “Kama hivyo, nakubali. Halafu mimi nakupenda Ezra! Wala sijivungi.” Watu walicheka wengine mpaka machozi. Ezra mwenyewe alicheka akiwa amepiga bado magoti akionyesha wazi hakuwa amemaliza alichotaka kumwambia, lakini biharusi alishakubali kabla hata hajaombwa!

    “Wewe mvalishe tu yaishe. Naona hakuna ustarabu mwingine tena.” Junior akamwambia Ezra. “Sasa kwani nilitakiwa kufanya nini na wewe Junior?” “Havina hata maana tena. Wewe vaa pete, tuanze mipango ya harusi.” Akacheka hana mbavu huku kanyoosha mkono tayari avalishwe pete, hataki mengi mwenyewe.

“Nimefurahi Ezra! Sasa mbona hata nilikuwa sijui!” “Kuna kitu kinaitwa surprise Jelini!” Junior akamjibu huku Ezra akimvalisha, yeye hana mbavu mpaka akamaliza. Akambusu huo mkono na kumuachia.

    Jelini akaiangalia ile pete akawa tena kama haamini. “Mwenzenu naolewa na Ezra!” Akaongea akijiangalia kidole huku akicheka, gafla akaanza kulia. “Tena? Sasa unalia nini?” “Mimi siamini bwana! Sasa kama ni ndoto?” Kila mtu anacheka. Ezra akamsogelea na kumshika mikono yote miwili. “Nakupenda Jelini wangu. Hata ukiamka kwenye hiyo ndoto, ujue mimi bado nipo. Na ni wako.” “Kweli? Na hutabadilika?” Akamuuliza kwa sauti ya chini akilia.

    “Sithubutu. Nakuhitaji Jelini. Umeleta furaha na faraja kwenye maisha yangu, siwezi kukupoteza. Una upendo wa kweli kwangu na kila mtu anayenizunguka. Na ahadi ya kubaki peke yako kwangu itabakia hivyohivyo mpaka kifo changu. Utabakia wewe kuwa dharula yangu ya kwanza daima.”Akalia huyo! Akamkumbatia. Vigelegele kwa mama mchungaji.

Mpenda mikono akatulia hapo akajisahau kama yupo mbele za watu. “Njoo nione pete.” Mpaka Jema alipomuita maana walimjua. Akajitoa hapo kwa Ezra na kwenda akijifuta machozi. “Na mimi nimepata wangu wa peke yangu.” Mama yake akabaki akimtizama. “Nzuri sana. Hongereni.” Akaenda kumuonyesha na mama yake. “Mwenzio naolewa na Ezra.” “Hongera mama yangu mzazi.” Akaanza kucheka kwa furaha.

    Kisha akamgeukia Junior. “Ujue Junior mimi sikuelewi kabisa? Mbona sikusikii sasa!” “Nachukua video Jelini! Nitafanya mangapi?” “Sasa si uchukue video huku useme hongera!” “Haya mama. Hongera sana Jelini.” “Naolewa na Ezra mwenzio.” “Na mimi naona. Umependa pete?” “SANA. Sisi tunapenda vitu vizuri. Ila hii ni sana. Halafu nimevalishwa na Ezra!” Pakawa na furaha ya namna yake. Huyo Jelini kila mtu akahakikisha anaona pete yake kidoleni.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Wakati wanakula keki, Emelda akamuuliza Junior. “Wifi Hope yuko wapi?” “Hapa hayupo.” Akamjibu hivyo akijua wazi silo jibu alitakiwa kutoa. Emelda akanyamaza.

    Wakasherehekea hilo, wakaagana wakiwa wamekubaliana kinachofuata ni mahari lakini uchumba lazima kutangazwa siku ya jumapili kanisani, na tafrija fupi kwa mchungaji. Sio jambo geni, hata Junior alifanyiwa hivyo.

     Mchungaji akafanya maombi, akaomba Jelini na Ezra wapige magoti kisha watu wote wawazunguke, wakawawekea mikono. Wote wakawaombea. Mchungaji akatamka baraka kwao mpaka watoto wa watoto wao. Jelini alifurahi sana.

    Ndipo wakawasindikiza nje. Kabla hajapanda kwenye gari, akamgeukia Ezra na Junior. “Mkitoka hapa, safari iwe ya nyumbani. Sitalala, nawasubiria.” Ezra na Junior wakaangaliana. “Nikimaanisha msichelewe.” “Tumeelewa baba. Tunakuja sasahivi.” Mzee akaondoka. Ila vile alivyowatizama, walijua kinachoendelea.

    Junior akaondoka na Emelda kama kuwapa nafasi hao wawili hapo kwenye gari la Ezra. Wakakiss kwa muda tu wakisherehekea uchumba wao, ndipo Ezra akaondoka kuwahi nyumbani, akiwa amemuacha Jelini na familia yake wakiwa wamefurahi.

~~~~~~~~~~~~~~~

     Zaidi mama Jema. Alifurahia kwa heshima ya kufuatwa na mchungaji na mkewe siku ya jumatano na kuombwa rasmi kuposwa binti yake. Hilo lilimgusa sana. Ndipo akaonyesha na zawadi walizokuwa wamempa. Jelini hakuwa akiamini jinsi mama yake alivyomficha. “Basi mimi sikuwa hata najua kama wana huo mpango leo!” “Mchungaji alikuwa akisema unajiandalia uchumba wako mwenyewe. Wema wako umelipa.” Wakabaki kucheka.

    “Wewe si ulisema hutaki wa kanisani wewe?” Jema akimkumbushia siku yake ya kuchumbiwa yeye, jinsi alivyomuomba asimuombee apate mume mlokole. “Huko duniani wa peke yangu nimekosa dada yangu.” “Naona mpaka umefunga!” Wakazidi kumcheka. “Nampenda Ezra! Mtaratibu sana. Na naona wamefurahi kweli yeye na Junior nilivyokubali kuwa nao kwenye maombi leo. Ezra alikuwa ananiambia pale kanisani, eti imemfurahisha sana mchungaji na mkewe. Kwao ni watu wa maombi sana.”

     “Sasa sio uishie leo.” “Siwezi Jema. Sasahivi naongeza juhudi kwenye mambo ya kanisani, ili niwe nao. Ni watu wazuri sana.” “Na kuanzia sasa ndio fungu lako hilo ulilochagua na kulikubali. Huna jinsi. Taratibu tu, utakuwa kama wao. Na naona wenyewe wanakupenda.” Mama Jema akaongeza. “Katika hilo namshukuru Mungu. Wazazi wao wana upendo sana. Hawana neno.” Ikawa faraja kwao.

Kwa Wazazi.

    Walipofika nyumbani Junior hakuingia ndani akabaki garini akimsubiria Ezra mpaka alipofika ndipo akashuka. “Emelda yuko wapi?” “Nimemwambia aende chumbani kwake moja kwa moja.” Wakasimama hapo kwa muda. Kimya, kisha wakajikuta wanaongoza njia kuingia ndani. Wakakuta wanasubiriwa. Ule ukimya ukaashiria si shwari.

    “Tumepanga kesho ndio nihitimishe rasmi na Hope.” Akaanza Junior hata kabla hajakaa vizuri na mzee hajaongea. “Ezra ameshaandaa mazingira mazuri. Nitakwenda kuzungumza naye, ili tuachane kwa ustarabu japo natamani iwe kwa amani pia.” Kimya mzee akimtizama.

“Nataka kuishi kwa amani baba. Na niwe na mwanamke anayenipenda na kunijali. Hope anaweza kuwa mke mzuri tu, lakini kwa mwanaume mwingine, si kwangu. Nikiishia kumuoa yeye, maisha yangu hayatakuwa na furaha. Na naona si sawa kwangu na kwake. Tumejitahidi kwa muda mrefu, au niseme nimefumbia hiyo hali kwa muda mrefu, lakini naona sipo tayari kuendelea kuishi hivyo. Sina sababu.” Kimya.

    “Ni hilo tu  nimeona nikwambie mzee wangu na mama najua utaelewa. Najua unataka niishi kwa furaha.” Junior akamalizia, mzee akamtizama mkewe. “Umeshindwa wapi na hawa vijana wako, mama?” Wote walitegemea kutupiwa mama yao hiyo lawama.

    “Mbona kama nimesikia kuna mipango ya kueleweka tu! Au sijaelewa?” Wote walishangazwa na mama yao jinsi alivyochukulia hilo jambo. Junior akajiweka sawa sasa. “Mama Junior!? Hivi wewe umefikiria pale kanisani?” “Mimi nafikiria mwanangu kwanza. Hayo mambo mengine ni baadaye. Wewe mwenyewe ulinionya hata mimi nisiwahi kuingilia chaguzi zao kwenye maswala ya mke.” “Lakini huyu amechumbia na kanisa zima linajua! Tutasema nini?”

    “Sasa imeshindikana! Tufanyaje?” Akajibu mama bila wasiwasi. “Kweli mama?!” Mumewe akashangaa sana. “Kwani ile ni ndoa? Si ndio maana kuna kuwa na uchumba ili wasomane! Umemsikia hapa amesema amemsoma, Hope si kwamba hafai, lakini si mke wake yeye! Sasa ulitaka mwanangu ndio aoe mke wa mtu!” Mama huyo akaongea kwa mshangao kabisa.

    “Hapana! Furaha ya mwanangu kwanza ndio mengine baadaye! Kweli mimi nianze kufikiria hisia za watu wengine halafu mwanangu ndio akateseke! Hapana baba Junior. Mbona wao walilifurahia swala la mwanangu kuachwa? Wakambariki yule binti na watoto wake wakizungu, wakashangilia pale na uchumba ulikuwa karibu kabisa na ndoa! Hawakujali mwanangu. Wakamuacha Ezra anasononeka peke yake!” Mama Mchungaji akaendelea.

    “Kwanza wakati wote umekua ukisifia akili za Junior. Kwa nini katika hili uone hajafikiria?” Mzee akanyanyuka. “Kuna jambo jingine.” Ezra alishituka, asiamini. “Kwa nini usisubirie kwanza Junior!?” Akamtizama Ezra, akafikiria kidogo ila akashindwa. “Siwezi tena Ezra. Acha tumalize hili jambo.” Akasimama kama baba yake.

    “Naomba ukae baba. Na nakuomba katika hili usimame na mimi kama baba na si mchungaji. Sasahivi nakuhitaji wewe kama baba yangu. Unajua kwenye huduma sisi wote hapa na kila mtu humu ndani tunasimama na wewe baba yangu. Iwe mchana au usiku tuko na wewe tukitumika pamoja. Leo nakuhitaji usimame na mimi kama baba.” Mzee akakabwa, akarudi kukaa.

    Na yeye akarudi kukaa. Akamtizama Ezra, naye akabaki akimtizama. “Ni jambo la kushitua kidogo, ila kabla hamjasema hapana na kukataa, tafadhalini naomba mpate muda wakufikiria, tunaweza kuzungumza zaidi kesho. Naomba msiwe na haraka mkataka kunijibu sasahivi. Mnaweza toa jibu ambalo hamjafikiria. Naomba ufikirie kwanza baba.” Mzee kimya akimtizama.

    Akatulia kidogo kama ambaye anatafuta pakuanzia, Ezra akimtizama pembeni yake. “Nampenda na nataka kumuomba Emelda awe mke wangu.” Palizuka ukimya hapo. Kama ambaye hakuna anayehema. Mpaka mama yake akaishiwa maneno.

“Kwa kuwa nimeanza, acha tu nimalizie. Emelda ndiye anayenitunza hata huko ninakoishi. Nimeondoka hapa, lakini bado ananifikiria na kunihudumia. Ni, kwa nini sasahivi na si wakati ule hata kabla ya kumchumbia Hope? Najua mnaweza kujiuliza hivyo.” Kimya wakimtizama. Anajiuliza mwenyewe, na kuendelea kujijibu.

    “Sikuwa nikijua kama nafungia macho upendo mkubwa wa namna hii. Sasa matatizo yangu na Hope ndiyo yalinifanya nikapata muda wa kutafakari na kutamani kama ningepata mwanamke anayenijali hata nusu ya Emelda. Nikajaribu kufikiria usiku kuchwa, nikagundua sitakuja pata mwanamke kama Emelda. Mbali ya kuniheshimu na kunijali. Ananifikiria, anani…” Akaanza kuwatajia wazazi wake mambo anayofanyiwa na Emelda kana kwamba hawamjui Emelda. Kimya wakimtizama.

    Akaendelea tu kama anayekamua jipu. “Ndio nikaona bora nitulie kwa Emelda ambaye kwanza sio kwamba nahitaji kumsoma. Wote tunamjua. Amejawa upendo, mtaratibu, anajiheshimu, hana kiburi,...” Akaendelea kutaja sifa zake mpaka Ezra akamshitua. “Nafikiri wanamfahamu Emelda.” “Kabisa. Ni binti wa hapa nyumbani. Kwa hiyo kwa sababu yeye namfahamu vizuri, akikubali, ndani ya miezi mitatu, tunafunga ndoa. Ni hilo tu.” Kimya, hao wazazi wamepigwa na butwaa hata hawasogezi mkono. “Sasahivi nimemaliza.” Akajitahidi akimeza mate. Kimya.

    “Na swala la safari.” Akaongeza Ezra. “Asante Ezra. Nimemuomba kesho asisafiri. Na naomba asianze likizo yake kesho. Ili nikitoka kuhitimisha na Hope ndio nizungumze naye sasa. Akikubali ndio nafikiri kutakuwa na chakuzungumza. Maana hata sasahivi mkikubali au mkikataa bila mimi kuzungumza na Emelda mwenyewe, haitasaidia. Ni bora tudhibiti hisia zetu na neno lolote mnalofikiria kuniambia sasahivi mkiwa na mshituko, mpaka tupate jibu lake Emelda. Hapo nimemaliza. Au kuna nilichosahau?” Akamuuliza Ezra.

    “Naona kwa sasa itoshe, wazee wakapumzike. Tuendelee ukishazungumza na Emelda hiyo kesho ambayo nafikiri sio wazo baya akawa off, ili apate muda mtulivu wakujiandaa na mazungumzo.” “Wazo sio baya. Nashukuru mama kumuomba mama Leti aje asaidie kazi kwa kesho pia. Maana kila kitu kikienda sawa, tutakuwa na chakula cha usiku cha pamoja pia. Sisi wanne. Tukiombea safari yetu.” “Inamaana mimi, Junior, Jelini na Emelda.” Ezra akaongeza. Wawili hao wakabaki kupokezana maneno na mipango, wazazi kimya wakiwatizama. Pakatulia kwa muda. Kimya.

    “Naona kweli tuache wazazi wakapumzike.” “Kabisa. Lakini kabla hatujaondoka, ili mpumzike, naomba niwashukuru wazazi wangu kwa kufanikisha hili la usiku wa leo. Naona safari yenu inakaribia kufika mwisho kwetu. Tukishaweka sawa la Junior, ndani ya miezi mitatu, tunaoa kabisa, huu ukurasa tunafunga, wote mpumzike.” Kimya. “Na kweli ilifana.” Akaongeza Junior.” Kimya. Ezra akasimama.

    “Twende Junior.” “Naomba nizungumze na Emelda mara moja ili kuweka sawa mipango ya kesho.” Wote wakamtizama mama yao. Kimya. “Naona tuondoke tu, utazungumza naye kwa simu ili wazazi wakapumzike. Siku ishakuwa ndefu.” “Ni kweli. Wazo zuri. Usiku mwema.” Wakaaga. Kimya. Wakaondoka hao wawili bila yakujibiwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alipofika tu kwenye gari akakumbuka vile Emelda alivyokuwa amependeza. Akafurahia moyoni, ila akakumbuka kumwambia ngozi ya kichwa inauma kwa kuvutwa akiwa anasukwa. Akaona aanze kumtafutia dawa ya maumivu usiku huo. Ezra akampigia. “Mbona sikuoni nyuma yangu?!” “Natafuta dawa ya kupunguza maumivu kwa Emelda. Wamemvuta sana wakati wakumsuka. Wewe tangulia kulala.” “Kwamba unapango wa kurudi tena nyumbani!?” “Siwezi kulala bila ya kumpelekea dawa. Najua si muhimu, lakini nataka kumhakikishia kuwa nimebadilika na sasahivi namsikia.” Ezra akatulia.

“Ujue ameniambia ni kweli aliniaga siku ya jumapili?” “Ikawaje?” Akamsimulia jinsi alivyoambiwa na Emelda. “Daah!” “Nimejisikia vibaya! Mpaka nimebaki nikijiuliza nimekuwa nikimfanyia hivyo mara ngapi!” Ezra akabaki akimfikiria huyo binti. “Sasa sijui kwa kuwa na yeye ni mkimya sana na sauti yake ni ndogo pengine ananikuta nakuwa na mambo mengi, kwa hiyo naishia kumuitikia hata kitu ambacho sijaelewa!” “Hapana. Tukiri tu kuwa tumekuwa tukimpuuza. Hakuna jinsi ya kujitetea katika lolote lile, Junior. Na nakuunga mkono kwa hichi unachotaka kufanya, japo sijui unarudije nyumbani!” “Sina jinsi, itabidi tu nirudi. Nitajua chakufanya nikifika pale mlangoni.” “Nijulishe kama utafanikiwa.” “Sawa.” Wakaagana, kazi ya kutafuta dawa ya kupunguza maumivu ya ngozi ya kichwa ikaendelea.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kila duka aliloingia usiku huo akieleza tatizo lake linalohitaji dawa, walibaki wakimshangaa. Mwishoe akaenda duka kubwa la madawa Mikocheni, akapata muhudumu aliyesomea mambo ya madawa. Akamuhisi ndiye mmiliki mwenyewe. Maana alimkarimu vilivyo na kumpa muda wa kutosha kumsikiliza na kumshauri. Akampa dawa ya kupulizia ya kupunguza maumivu. Akamwambia pengine itasaidia. ‘Pain relif spray’. Akalipia na safari ya kurudi kwao ikaanza.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia simu Emelda. “Umeshalala?” “Bado.” Akajibu. “Nakuletea dawa ya kupunguza maumivu ya kichwa kwa ajili ya kusukwa. Kwa hiyo usilale, nisubiri.” Alishituka Emelda hakutegemea kabisa. Kwanza hakujua hata kama amemsikia au hata kutilia maanani alichokuwa akisema. Hakuzoea kabisa. “Utanifungulia mlango?” “Naogopa kaka! Unajua baba ndiye anayefungua milango usiku.” “Basi acha nimpigie simu anifungulie.” “Au tufanye tu kesho kaka. Usisumbuke.” Akaongea kwa hofu. Mpaka aamshwe mzee kwa ajili ya msuko wake! Haikuwa imekaa yakueleweka.  “Hapana. Sisumbuki, nataka ulale vizuri. Na usiogope. Umesikia?” Akatulia. “Nakuja. Usilale, unisubiri.” “Nitakusubiri kaka. Asante.”

~~~~~~~~~~~~~~~

Alifika kwao akaingiza gari mpaka ndani. Junior mtoto wa nyumbani na walinzi wanamfahamu. Akampigia simu baba yake. Ilishapita lisaa tokea atoke hapo. “Samahani sana baba yangu. Kuna dawa nataka kumpa Emelda.” “Ambazo haziwezi kusubiria kesho?” “Haziwezi. Nimeshafika, nipo hapa mlangoni kwako. Naomba nifungulie.” Simu ikakatwa, akajua anakwenda kufunguliwa.

Baada ya muda mlango ukafunguliwa. “Ni usiku sana sasahivi Junior, nahitaji kupumzika.” “Sitakaa sana.” “Tafadhali usikae kabisa. Mkabidhi na uondoke.” “Sawa.” Akampita hapo mlangoni akiwa hajasogea kabisa kumuashiria anamsubiria.

Akagonga mara moja tu, kama aliyekuwa amesimama mlangoni akafungua akiwa na wasiwasi. “Pole kwa usumbufu.” “Usijali. Ni ya kupuliza. Kwahiyo jipulizie kwenye ngozi ya kichwa, itafanya ngozi kuachia na kutulia. Vingine humo ndani ya mfuko mwingine ni vyako. Tutaongea zaidi kwenye simu au unalala sasahivi?” “Nitasubiri mpaka tuongee. Uwe nasafari njema ukiwa unarudi nyumbani.” “Asante. Nitakupigia muda si mrefu.” “Sawa.” Akatoka kwa haraka, akamkuta baba yake palepale alipokuwa amemuacha.

“Nashukuru baba. Usiku mwema.” “Asante na wewe. Na uwe makini huko barabarani.” “Nitajitahidi.” Akatoka, mzee akafunga mlango, huku nyuma Emelda anafurahia kama arukeruke. Mfuko mmoja ulikuwa na hiyo dawa, na mwingine chocolate nzuri sana. Zikaonekana za kiwango cha juu haswa. Akabaki akijichekesha hata asipulize dawa. Simu ikamtoa kwenye furaha.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Kaka?” “Umepuliza dawa?” Ndio akakumbuka. “Bado.” “Nataka uipulizie nijue kama itasaidia au tutafute nyingine.” “Itasaidia tu. Asante. Nimefurahi! Sikujua hata kama ulinisikia!” “Nipo kwenye kupunguza kelele zote zilizokuwa zikinifanya nishindwe kutulia na kukusikia. Narekebisha ili niweze kukusikia wewe Emelda. Nivumilie kidogo tu. Kila kitu kitakuwa sawa.” Alivyokuwa akimbembeleza, ikamfanya atulie kabisa.

“Nashukuru kukubali kubaki na kuwa na mimi kwa kina Jelini. Uliumia?” “Safari hii sijaumia sana, kwa kuwa tulikuwa wote kaka. Na angalau ulijua kama nipo pale.” Junior akamuhurumia. “Samahani kama huwa inaonekana ni kama nakupuuza Emelda. Sikudharau.” “Ila huwa unashindwa kabisa kuniona kaka, au hata kunisikia. Wakati mwingine hata nikikusalimia unakuwa mbali, huitiki.” “Naomba unisamehe. Nakuahidi nitabadilika. Na nimeanza kuchukua hatua kwenye mapungufu yangu.” Akatulia.

“Kesho naomba uje nyumbani. Nimeshakuombea ruhusa kwa wazazi. Au unaratiba ingine?” “Hapana kaka. Nitakuja. Ulitaka iwe saa ngapi?” “Nitatuma mtu aje akuchukue saa nne na nusu asubuhi. Mpaka mfike nyumbani, nitakuwa nimesharudi, nakusubiria wewe tu. Ulitaka kula nini ukifika?” Akashangaa kidogo ila akajibu. “Utakachotaka nipike, nitapika na mimi nitakula.” “Kesho mimi ndio nakuandalia chakula.” Akamsikia akicheka.

“Nitakuandalia chakula kizuri. Na usiku tutakuwa na Ezra pamoja na mchumba wake.” “Kwamba na mimi nitakuwepo!?” “Ndiyo. Tupate nao chakula cha usiku.” “Sitaweza kukaa huko muda wote huo. Natakiwa kurudi kusaidia kazi. Mama Leti huwa anawahi kuondoka, na baba ni lazima apate chai ya saa 10.” “Nimezungumza na mama. Hamna shida. Kesho ni mapumziko yako. Nitakurudisha nyumbani usiku.” Akafurahia moyoni ila na wasiwasi ukizidi kumnyemelea. Wifi Hope! Maana hanaga utani. Akatulia na kuaga. “Usiku mwema kaka.” “Na wewe. Nitakuona kesho.” “Asante.” Wakakata simu.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment