Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 32. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 32.

 Kwa kuwa walijua ratiba za wazazi wao hakupata shida kujificha kwenda kwao. Ila akamkuta mama ambaye huwa anaitwa kumsaidia kazi mama yao endapo Emelda anakuwa hayupo, au kuna kazi nyingi kama tafrija hapo nyumbani kwa mchungaji. Kwa hiyo huyo mama huitwa kusaidia. Hilo likamfurahisha Junior. Akamsalimia na kuambiwa wazazi wametoka, Emelda amelala.

    Hakupoteza muda, akaenda kugonga chumbani kwake. Mara moja tu, tena taratibu. Alipoona kimya, akaingia kwa kunyata. Akamuona amelala kitandani. Moyo ukajawa furaha! Akaweka matunda aliyokuwa amemletea kwenye meza ndogo aliyokuta ina glasi ya maji na supu imefunikwa. Akajua hajala.

    Akaweka vizuri na kuamua kukaa hapohapo kitandani taratibu kama asimuamshe wakati shida yake ni aamke. Hakuamka. Akaanza kumshika kichwa taratibu. Yaani yeye ndio akawa anasikia raha kumshika. Akamshika kipanda uso kama anayempima homa, mpaka akamuamsha.

    Junior alitoa koti la suti na hakuwa na tai. Shati jeupe! Msafi kama kawaida yake. “Kaka!” Akashituka, hakutegemea. Akatoa mkono kama aliyefumaniwa. “Vipi?” “Najisikia vizuri. Sijatapika. Ila nahisi dawa za kuzuia kutapika ndio zinanipa usingizi. Nalala kama niliyezimia. Pole na kazi.” “Asante. Basi acha nikupashie moto supu, uje unywe. Naona mama amekuachia hapa.” “Usihangaike kaka. Nitakwenda tu. Wewe pumzika.” Junior akakaa vizuri na kumwangalia.

    “Mbona wewe huwa unanipikia na kuniletea mpaka nyumbani na wakati wote hujawahi ona ni usumbufu? Kwa nini kwangu unahisi ni usumbufu?” Alishituka hakujua kama amejua. Akakwepesha macho.

    “Eti Emelda? Kwa nini kwangu ndio iwe usumbufu nikitaka kukufanyia kitu chochote? Au ulidhani bado sijajua kama ni wewe ndio unaleta chakula nyumbani si mama?” Akabaki akiangalia shuka alilojifunika.

    “Nashukuru kunijali Emelda. Asante.” Mwili mzima wa Emelda ulikuwa ukisisimkwa. Ni Junior! “Ila nasikitika sikujua mapema.” “Upo na majukumu mengi kaka. Unajitoa kwa kila mtu, kila mahali. Mchana na usiku hupumziki. Ni rahisi watu kukusahau wewe.” “Mbona wewe hujawahi kunisahau?” Akanyamaza.

    “Eti Emelda?” “Kwa kuwa upo kama mama yangu. Ni mpole sana. Anajituma sana pale kijijini kwenye mambo ya watu, lakini huwa yeye akipatwa na shida, watu huwa hawamkumbuki kabisa. Inakua rahisi kumpuuza kwa sababu huwa anafanyaga yale mambo watu wengine hawataki kufanya.” Akaendelea taratibu tu.

    “Kukiwa kuna misiba au hata harusi pale kijijini, basi ujue mama atafanya zile kazi ambazo watu hawaoni au hawataki kufanya. Zakudharaulika. Kama kuchota maji na kujaza kwenye vyungu. Kuleta kuni wapishi wapike. Na watu wakishakula, basi atabakia kusafisha na kuosha vyombo. Zote hizo ni kazi ambazo hakuna mtu anaona wala kuthamini. Kiasi ya kwamba ikifika kwenye kushukuriwa, yeye hafikiwi. Kwanza hawajui kama alifanya.”

    “Hakuna anayemshukuru mchota maji, wakati wakunawa mikono, ila anaye mnawisha. Hakuna anayemshukuru mleta kuni, ila mpishi. Hakuna anayekumbuka kusafisha vyombo baada ya vyakula vya msibani na kwenye sherehe kwa kwa watu wanakuwa wameshaondoka, na kama wapo, basi wanakuwa wamekaa sehemu maalumu, mama yangu akifanya nyuma ya nyumba. Na wewe upo hivyohivyo kaka.” Junior hakuamini.

    “Pale kanisani unakua wa kwanza kufika na wa mwisho kuondoka. Kila siku. Upo kwenye kila huduma, kasoro ya watoto tu ndio huko sijawahi kukuona.” Akakumbuka maneno ya Jelini. “Ambako wewe ndio upo?” Akamuuliza. “Ninachotaka kusema, unafanikisha kila huduma pale kanisani. Kila mtu anajua wewe na kaka Ezra hamjui kukataa wala kulalamika mnapopewa jukumu, ndio maana wanawatuma bila kuchoka. Lakini linapofika swala la kushukuru viongozi wa kanisa, sijawahi ona hata mara moja nyinyi mnaitwa pale mbele na kushukuriwa au kupewa zawadi. Wanawashukuru wale viongozi ambao nyinyi ndio mnakuwa mnawafanikishia kazi. Hakuna anayetambua watu kama nyinyi kaka.” “Lakini wewe unatambua na kujali.”

    “Sio kama ambavyo mnastahili au unavyostahili, kaka. Wakati mwingine natamani kufanya zaidi ila nakua sina uwezo. Nakuwa natamani hata usikie nikikwambia pole, lakini mara zote inakua ngumu kunisikia hata nikikwambia ‘pole’.” Junior akajisikia kuumia. Kwa asili Emelda ana sauti ya chini. Mtaratibu sana. Pengine ndio sababu.

Akamwangalia. “Napunguza kelele ili niweze kukusikia Emelda. Pole na samahani.” Ilimgusa huyo mrembo, akashindwa kuamini. Maana hata alivyoisema Junior, ilijaa hisia za kumaanisha.

    “Umenielewa?” Akamuuliza akivuta shuka kama amfunike vizuri. Emelda akatulia akifikiria maana yake. Kelele moja wapo ni Hope, sasa atamfikiaje yeye! Akatulia msichana wa kazi, asije kujipa tumaini ambalo halipo. Akamwangalia akamuona yupo mawazoni, akaona Ezra yupo sahihi. Amalize la Hope kabla hajaanzisha jingine, tena kwa maneno tu.

“Pole kwa kujirudia rudia mara zote bila mimi kukusikia, na bado hujachoka na kunikatia tamaa. Na samahani kwa kushindwa kukusikia.” Akamvuta mkono kabisa. Akaushika vizuri katikati ya mikono yake. “Lakini nakuahidi kukusikiliza. Na unapoona unazungumza na mimi, sijasikia, tafadhali rudia tena, na hakikisha nakusikia. Na nakuhakikishia kuanzia sasa, utajua kama nimekusikia. Sawa?” Akatingisha kichwa kukubali. Wakatulia hapo kwa muda, amemshika mkono vizuri na kwa upendo, akitamani asimuachie, na yeye akitamani kama aubusu. Ila akajikaza na kumuachia taratibu.

    “Acha nikakupashie supu moto. Ule kabla sijaondoka.” Akatoka. Ila kwa hakika Emelda alishajua yupo pale si kama kaka. Akahisi habari inataka kubadilika. Ila Hope akabaki kumfanya atilie mashaka kila kitu Junior alichozungumza. Akapoa akiumia moyoni, akitamani kama angepata yeye bahati ya Hope.

    Akarudi na sinia ya supu. “Nikusaidie kula?” Emelda akacheka. “Nitakula kaka. Asante. Mbona sioni yako?” “Nataka wewe ule kwanza. Ezra atanipelekea chakula ofisini. Nitakula nikirudi, usiwe na wasiwasi.” Akatulia kama anayejifikiria.

    Akamgundua. Akamuacha tu akijua kinachoendelea kichwani mwake, ila akashukuru Mungu hataweza kumuuliza. Maana hata yeye hakuwa na majibu ya kumpa kwa wakati huo. Akatulia akimsubiria akila, macho kwenye simu yake ili asimfanye akashindwa kula. Akahisi na yeye anavuta simu yake na kutuma ujumbe. Akabaki kujiuliza anawasiliana na nani muda huo na yeye yupo! Kajiwivu kakaanza.

    Mara akaona ujumbe umeingia kwenye simu yake, akahama kwa haraka kutoka alipokuwa akiperuzi kuwahi huo ujumbe akijua unatoka kwake. Ikawa ni kweli. ‘Nimefurahi umekuja kuniona na kukaa na mimi katikati ya siku yako yenye majukumu mazito. Asante.’ Akacheka taratibu na kumjibu. ‘Sasa hivi nakuona na nakukusikia.’ Akamjibu akamuona anavuta tena simu yake. Akasoma, akamuona anajifuta machozi. Akarudisha bila ya kujibu. Akamuacha. Akaendelea kuperuzi simu yake. Kimya mpaka akamaliza.

    Asante kwa supu. Nimeshiba.” “Rudi kupumzika. Kazi zote zimeshafanywa na mama Leti. Hakuna kitu chakufanya tena. Pumzika kabisa leo.” “Asante kaka. Asante sana.” “Karibu.” Akasimama na kutoa vyombo, Emelda akishangaa. Yeye ndio huwa anawatumikia hapo ndani. Zaidi huyo Junior na Ezra, leo Junior anamtumikia yeye! Ikamgusa zaidi. Akarudi kujilaza akimtizama anavyojishugulisha hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~

    Akasafisha hapo, na kurudi kukaa hapo kitandani. Akamvuta tena mkono akishangaa anataka kufanya nini tena na mbona harudi kazini! “Nikuulize kitu Emelda?” Akatingisha kichwa kukubali.

    “Nilipokuwa nimelazwa hospitalini, unakumbuka ombi lako siku ya mwisho natolewa?” Jinsi alivyoshituka na kuinamisha kichwa, akajua amekumbuka. “Kwa nini hukuniambia kama ni wewe ndio unataka nirudi nyumbani ili uniuguze, badala yake ulimtumia mama?” Akanyamaza, ila akahisi mikono inatetemeka, maana aliokuwa ameushika ulikuwa ukitetemeka.

    Akamsugua viganja, akataka kuuvuta mkono wake akamzuia, akabaki ameushika. “Eti Emelda?” “Nilijua nikikwambia ni mama ungeona uzito wake, ungekubali.” “Kwa nini muda wote huo umeshindwa kuniambia kama ni wewe, umekua ukimtumia mama? Na si katika hilo tu, katika kila kitu! Kwa nini hukutaka nijue kama ni wewe ndiye unayenifanyia vitu?” “Isingebadili chochote kaka.” “Lakini mimi ningependa kujua! Nahisi ingenisaidia.” “Sidhani kaka. Sidhani.” Kwa upande fulani akakubaliana naye. Akaendelea kumsugua huo mkono taratibu, kwa muda akiwa mawazoni akifurahia uwepo wake mpaka ujumbe ulipoingia.

     Ukamtoa mawazoni akiwa na huo mkono wa Emelda akiuchezea, hana habari, mbali mawazoni. ‘Inatosha Junior. Tafadhali rudi kazini. Kiasi.’ Alikuwa Ezra. Akaangalia muda, akashituka na kuachia mkono. “Pumzika, tutawasiliana.” “Asante.” Akasimama kama afanye kitu, akaona kweli awe na kiasi, akaondoka.

Ijumaa.

    Jelini hakuwa na habari kama ni siku yake ya kuchumbiwa. Ila Ezra alimtaarifu kuwa mchungaji amekubali kufika kwao kwa chakula cha usiku, baada ya ibada ya maombi. Kwa hiyo akamwambia ajiandae, usiku huo watakuwa na ugeni. Mchungaji na familia yake wote watakua hapo. Akamwambia mama yake, asijue mama yake anajua na ameshamtaarifu hata Jema. Siku hiyo wakawahi kwenda kazini na kurudi kuanza matayarisho, kila mtu kwenye familia yake na mchungaji alijua kama anachumbiwa, kasoro yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Ilipofika jioni, Jelini alikuwa amefunga kama alivyokubaliana na kina Ezra akaenda kanisani kwa maombi kabla ya kufungua. Akakutana nao. Noah alishakuwa tayari akipiga kinanda hapo ibadani kuashiria alishafika. Sasa wazazi walipofika, Junior hakumuona Emelda. Akamtumia ujumbe, hapakuwa na majibu. Uzalendo ukamshinda, akamfuata mama yake. “Emelda yuko wapi?” “Alikwenda kusuka tokea asubuhi. Yupo kwenye matayarisho.” Yeye Junior akajua matayarisho ya shuguli baada ya pale. Akatulia.

    Ibada ikaisha safari ya kuelekea kwa kina Jelini ikaanza. Ezra akagundua hayupo sawa. Walipofika kwa kina Jelini, ikabidi amuulize mama yao. “Emelda anaendeleaje?” “Ameamka na nguvu, akaamua kwenda kusukwa. Ameshinda huko siku nzima. Sisi tumeondoka hapo nyumbani hajarudi ila aliaga tokea jana kuwa atachelewa.” Akamwangalia Junior, kimya.

    Wakakaribishwa ndani, salamu. Jema na familia yake pia walikuwepo hapo. Kukawa kumechangamka. Jelini maneno mengi akafanya kila mtu kujisikia nyumbani na kuzoeana kirahisi. Hofu ya mchungaji waliyezoea kumuona madhabahuni tu akizungukwa na maelfu ya waumini, Jelini akaipoozesha akawa baba hapo kwa muda mfupi tu. Vicheko akimchokoza mpaka mama mchungaji. Mpaka Noah alikuwepo.

    Vikaendelea vinywaji, zaidi chai kwakuwa walikuwa wamefunga. Junior akatoka nje. Ezra akaona harudi, akamfuata. “Vipi?” “Simpati Emelda!” “Pengine atakuwa ameishiwa chaji. Mama amesema alikwenda kusukwa tokea asubuhi. Tumsubirie, si amesema atakuja ila kwa kuchelewa?” Akakubali kuingia ndani.

    Mambo yakawa yanaendelea, Emelda haji. Kila kitu kikaanza kukosa ladha pale. Yupo kama hayupo wakati mwenzie anataka kuchumbia. Akamsogelea mama yake. “Nani anamleta hapa Emelda?” Akawa amemchanganya mama yake. “Si umesema atakuja ila kwa kuchelewa?” “Nilimaanisha atarudi nyumbani kwa kuchelewa! Emelda hatakuja hapa. Yupo na matayarisho ya safari.” Junior alishituka, Ezra akasogea.

    “Safari ya wapi tena!?” Ezra akauliza. “Si aliniambia amekuaga wewe siku ya jumapili?” “Mimi!?” Junior akashangaa sana. “Ndivyo alivyoniambia. Kuwa siku ya jumapili pale kanisani alikuaga kuwa anakwenda kwao. Hata hivi juzi alipougua alikuwa na wasiwasi anaweza shindwa kwenda. Kwa hiyo yupo kwenye maandalizi ya safari ya kwao. Noah amemkatia tiketi ya basi la asubuhi.” Junior na Ezra wakaangaliana.

    “Tafadhali endelea Ezra.” “Siwezi bila wewe. Nenda ila ujue nakusubiri.” Mama yao akawa haelewi. “Vipi?” “Narudi sasahivi mama. Ila Ezra tafadhali usinisubiri. Endelea.” “Unapoteza muda. Nenda lakini jua nakusubiri.” Junior akatoka akikimbia.

Maombi Ya Sirini, Yajibiwa Kwa Moto.

Ila Kwa Wakati wa Mungu.

    Moja kwa moja akikanyaga mafuta kwenda kwao. Akashuka akikimbia kama anayewahi wakati aliambiwa Emelda anaondoka kesho na si usiku huo. Akagonga kengele mara kadhaa maana mlango ulikuwa umefungwa. Akabaki akigonga kengele na kumpigia simu. Baada ya muda akasikia mlango unafunguliwa kwa ndani, akahema kwa nguvu.

    Akatoka Emelda amependeza, mpaka akamzubaisha Junior. Hakusukwa kitu cha ajabu, ila rasta za kimasai. Ndogondogo kama sindano. Na kwa kuwa zilikuwa zikimuuma, aliziachia, hakutaka kuzibana kabisa, ngozi ya kichwa ilizidi kuuma kwa kuvutwa wakati wakusukwa.

    Hakutegemea kumuona Junior pale tena usiku huo. “Shikamoo kaka! Nilikuwa bafuni nikashindwa kutoka kwa haraka. Pole.” Akampisha mlangoni. “Karibu.” Junior akaingia. “Nilijua utakua na kaka Ezra! Mama aliniambia leo na yeye anachumbia.” “Sasa kwa nini na wewe hukuja?” Akawa kama analaumu.

    “Nimerudi kwa kuchelewa kaka. Halafu huku kuugua siku mbili kumenipotezea muda, nimejikuta sijajiandaa kabisa kwa safari ya kesho. Nikaona nibaki nijiandae kwa safari. Naondoka alfajiri sana. Mambo yamekwendaje huko?” “Sijui! Nimekuja kukufuata wewe.” Akamchanganya Emelda akahisi hajamsikia sawasawa.

    “Naulizia uchumba wa kaka Ezra. Mama ameniambia na yeye anachumbia leo.” Junior akaona akae. Emelda akamsogelea akiwa na mshangao. Ila akamuuliza. “Nikuletee juisi?” “Mbona unasafiri bila kuniaga?” Akauliza kwa kulaumu. “Nilikuaga kaka! Pengine hukuwa umetilia maanani. Tulikuwa kanisani.” Junior akashangaa sana.

    “Kwenye harusi ya Ester?!” “Hapana. Kanisani kabla ya kwenda kwenye harusi.” “Nikasemaje?!” “Ulisema sawa. Halafu hapohapo na wifi Hope naye akaja, akakuchukua, mkaondoka. Mliniacha palepale nimesimama.” Junior akainama kwa uchungu. Emelda akakaa taratibu, kochi la mbele yake.

    “Nisingeweza kuondoka bila ya kukuaga kaka!” “Daaah! Hata sijui niseme nini!” Emelda akawa hajaelewa. “Kwa nini?!” Akauliza taratibu tu. “Sikujua kama unasafiri kesho Emelda! Samahani sikutilia maanani. Naomba unisamehe nahisi sikuwa nimeelewa, pengine nilidhani...” Akaona asijitetee, anaharibu. “Samahani.” “Hamna shida.” “Hapana. Si sawa. Si sawa kabisa! Nakuahidi nitabadilika.” Emelda akainama akiwa amekalia mikono yake.

    “Unakwenda nyumbani kufanya nini?” “Ni likizo yangu, mama amenipa. Ndio nakwenda kumsalimia mama na wadogo zangu.” “Kwa muda gani?” “Amenipa siku 15, kwa hiyo kama majuma mawili. Naenda kumsaidia mama kulima. Ndio msimu wa kupanda huu.” Anaongea hajui jinsi kaka yake alivyovurugikiwa.

    “Nikikuomba usiondoke kesho, mpaka tuzungumze na kujipanga pamoja, itakuwa sawa?” Emelda akabaki amekunja uso kama asiyeelewa. “Tafadhali Emelda. Ukiondoka tu, utanichanganya, nitashindwa kufikiria na hata mambo niliyotaka kufanya nitashindwa. Naomba ubaki ili nitulie. Halafu kama ni shamba, naomba tutume pesa, zitangulie kwa ajili ya vibarua. Mama alipie watu wakumsaidia shamba.” “Mama ndio kibarua mwenyewe.” Junior akameza mate, akapatwa na kigugumizi.

    “Msimu huu anakuwa anachukua kazi kwenye mashamba ya watu, ili kujipatia pesa za kumsadia na wadogo zangu. Kwa hiyo mimi na wadogo zangu ndio tunakuwa tukimsaidia.” Ki ukweli hakuwa akimfahamu hata kidogo huyo binti japo alikuwa akiishi naye nyumba moja mpaka akahama hapo kwao. “Basi tutamtumia pesa za matumizi. Halafu nitamuomba mama asogeze siku zako za likizo mbele. Mimi mwenyewe nitakupeleka nyumbani.” Alishangaa huyo binti, akabaki kama amepigwa na shoti ya umeme.

    “Ukiondoka tu kesho, jua nitaharibikiwa vibaya sana. Naomba ubaki. Nipo kwenye mabadilisho, na ili niweze kufanya vizuri ni nijue upo na mimi na upo upande wangu.” “Mimi nipo na wewe siku zote kaka.” “Nashukuru. Basi jua sasahivi nakuhitaji zaidi. Naomba ubaki, kesho tutazungumza zaidi.” “Ila na tiketi nilishakata, na baba pia anajua kama naondoka kesho.” “Nitazungumza nao. Usiwe na wasiwasi. Sawa?” “Sawa.”

    “Naomba nikuombe jambo la mwisho.” Emelda akatulia akimwangalia kama ambaye bado hajamuelewa sawasawa. Siku chache tu zilizopita alikuwa akiishi naye kama hayupo! Gafla anambembeleza! Emelda akabaki amevurugikiwa ila akimsikiliza kwa makini akihofia asije jichanganya. Asijue kwa Mungu miaka 1000 ni kama siku 1 tu. Hubadilisha mambo na kufanya kwa wakati wake.

    “Ezra anatakiwa kuchumbia sasahivi. Hatachumbia bila mimi kuwepo. Na mimi siwezi kuwepo pale bila wewe kuwepo.” Aliona wazi jinsi alivyomchanganya. “Tafadhali Emelda.” “Nilimuomba mama huko nisiende kaka.” “Kwa nini?” Akamuona ameinama. “Eti Emelda?” “Sijui! Ila sikuwa nikitaka kwenda. Naishia kuumia tu wakati wengine wakifurahia. Si sawa.” “Pole. Lakini nikikuomba twende wote?” Simu ya Ezra ikaanza kusumbua hapo. Akamwangalia anavyoangalia simu yake na kurudisha mfukoni. Kisha akamuona anatuma ujumbe mfupi na kurudisha tena mfukoni.

    “Kwani huko mlitaka msaada gani?” Akajua ni kazi. Wanataka akawafanyie kazi. “Naweza kwenda kusaidia chochote. Mimi nilidhani ni kuhudhuria tu, ndio nikakataa kwenda. Ila kama ni kazi, naweza kwenda.” “Hapana. Nataka uwe na mimi. Na safari hii hautakuwa peke yako, utakuwa na mimi. Nitaweka mazingira usiumie.” Hapo ndipo akamchanganya zaidi. Akabaki ameduaa.

     Na hapo napo Junior akazidi kumuangalia na kushangaa aliweza vipi kutooana uzuri wake. “Ni sawa tukizungumza kila kitu kesho? Ila usiku huu naomba twende ili Ezra achumbie. Huendi kufanya kazi, unakwenda kama mgeni wangu mimi. Mimi ndio nakuhitaji. Nataka uwe na mimi kwenye hili.” Mwili mzima wa Emelda ulianza kupatwa baridi. Kauli hii si ya kikaka kabisa! Hata yeye aliweza kugundua.

    “Emelda?” “Abee!” Wakati anaitika simu ya mzee nayo ikaingia. Ikabidi apokee. “Sikukwambia mimi kama usipoweka mambo yako sawa, unazuia ndoa mbili?” “Nakuja baba.” “Tafadhali uje Junior. Mwenzio ameshindwa kuchumbia, anakusubiria wewe. Na hapa mambo yamekaribia kuisha, wote tunaonekana watu wa ajabu tusio na mipango.” “Samahani baba. Nakuja sasahivi.” Akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment