Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 31. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 31.

Ilipofika mida ya saa mbili kasoro Ezra na Jelini wakafika hapo. Junior alishamwambia tokea wapo kwa wazazi kuwa anampeleka hospitalini. Alichofanya ni kwenda kumchukua Jelini na kwenda naye huko. Akabakia yeye ndio dharula yake ya kwanza hata hapo hospitalini. 

“Vipi?” “Aisee homa ilikuwa kali sana na anatapika kweli!” “Malaria hiyo!” “Kama kawaida ya mama, kaanza kumpa dawa hata hajapimwa!” Wakacheka kwa masikitiko. “Mama! Hajaacha tu?” “Naona ni kasumba iliyokataa kutoka. Ndio amechukuliwa damu, tunasubiria majibu. Vipi Jelini, mbona leo umepoa?” “Mimi maneno mengi nje ya hospitali. Nikishaona hivi halafu na sindano ipo mwilini mwa mtu, ndio nazidi kupoteza uchangamfu. Haya sio maeneo yangu kabisa.” Wakaanza kumcheka.

    “Ila poleni.” “Asante.” “Ila huyu kama mimi namfahamu. Si anakuaga kule kwa watoto siku za jumapili?” Jelini akauliza akimwangalia Emelda. Ezra na Junior wakatizamana. Hawana uhakika maana huyo ni mtu wa mwisho kabisa waliyekuwa na taarifa naye japo ndiye aliyekuwa akiwalisha kila siku ya ijumaa baada ya maombi ya siku nzima.

“Au nimekosea? Maana mwanzoni pale kanisani walitaka Jeremy awe anakwenda kwa watoto. Huyu akampokea. Nilipoenda kumchukua Jeremy,  akaniambia ni mtoto mwenye tabia nzuri. Nikamtania nikamwambia ni kama mama yake. Akacheka na kuniambia tumefanana naye pia. Ni mtaratibu sana huyu dada. Au nimemfananisha?” Kimya.               Akaendelea kuvuta kumbukumbu. “Na nilishamuona na mama mchungaji, kwenye harusi ya Ester. Akicheka mashavu yake yanabonyea hivi.” “Basi ni yeye.” Wote wakaitika kwa pamoja na kucheka. Maana Jelini alipiga ikulu. Kweli Emelda akicheka anabonyea mashavu.

“Nilijua tu! Poleni sana. Kumbe ni dada yenu anaishi kwa mchungaji!?” Kimya wakishindwa kujibu hilo. “Poleni.” “Asante. Vipi kazi lakini?” “Namshukuru Mungu, mambo si mabaya. Na wewe?” “Siwezi kulalamika. Nipo.” “Njoo tukae hapa Ezra, tusiongee sana, mgonjwa apumzike.” Wakaenda kukaa kochi la pembeni, refu. Wakatulia. Ezra na Junior wakaangaliana, Ezra akatingisha kichwa kama ambaye haamini, Junior akacheka kimyakimya.

Hope.

    Huku kanisani baada ya bible study mchungaji na mkewe wakaelekea ofisini ili kukutana na Hope. Hakuwepo kwenye mafundisho, ila akafika hapo kama aliyevizia muda wa kipindi uishe, akutane na mchungaji. Hakutegemea kumkuta na mama mchungaji. Akampokea kwa furaha tu japo alionekana amenyongea. Mchungaji hakutaka mengi. Akamshukuru kwa huduma yake hapo kanisani, kujitolea kwake na kumwambia, “kama kungekuwa na watenda kazi kama wewe hata wanne tu katika kila kanisa, hakika tungekuwa mbali. Wewe ni mtenda kazi unayefanya kana kwamba unafanya kwa Bwana kabisa. Kwa hakika Mungu wangu asikupungukie.”

    “Na tuna zawadi yako kutaka kukushukuru.” Akaongezea mama mchungaji, lakini kwa Hope akashangazwa kwa nini hata haulizwi ni kwa nini anaacha! Alitarajia mazungumzo ili apate pakujieleza na kuomba abakie.

    Asijue usiku huo una mengi, wanawahi kwa mama Jema. Na pengo lake limeshazibwa. Hawakumuulizia la kheri wala la shari zaidi ya shukurani kubwa sana kwake na hiyo zawadi. Na yeye akakabidhisha funguo zote, ila kabla hajatoka, mama mchungaji akamuwahi. “Hope binti yangu, milango hapa ipo wazi. Na hapa ni nyumbani mama. Ukipumzika. Ukajisikia unayo nguvu ya kuendelea, tafadhali usiache kurudi. Sisi bado tunakuhitaji. Hii kazi ya Mungu ni kubwa mwanangu, na watenda kazi ni wachache. Tunakuhitaji binti yangu.” Hilo likamfurahisha sana Hope. Angalau akajisikia vizuri. “Nimeelewa mama. Acha niweke mambo sawa, akili ikitulia, nitarudi tena.” Wakambariki na kuondoka wakiwahi kwa mama Jema.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Wakiwa kwenye gari ujumbe ukaingia. ‘Nimemkuta Emelda anatapika sana na homa ipo juu, tupo hospitalini.’ Mama yake akasoma kwa sauti. “Wapigie na waambie tukitoka huko, tutawapitia.” Mama mtu akapiga, akaweka spika kama kawaida yake ili asijirudie kwa Ezra akijua lazima wapo pamoja. Wote wapate ujumbe kwa pamoja. “Tukitoka kwa mama…” “Tupo na Jelini hapa.” Junior akawahi asije toa siri. Akacheka.

    “Na mimi nimekuja kuona mgonjwa mama.” “Afadhali. Ndio maana kanisani sijakuona!” Akamchokoza akijua haendi kanisani vipindi vya katikati. “Mwenzio naanza ijumaa hii, na nafunga na Ezra.” “Na mimi Jelini!” Junior akamuwahi akilalamika. “Sijakusahau Junior! Na Junior pia, halafu sisi wote watatu tunakuja kanisani kwenye kipindi cha maombi.” Wakacheka.

    “Ingekua mimi, ningemwambia mchungaji ijumaa hii ndio iwe siku ya kutoa ile ahadi yake. Tunafunga pamoja, halafu mnakuja kufuturu kwa mama Jema.” Wote wakacheka kwa pamoja na mchungaji.

    Jelini!” “Sasa mama wewe umeshawahi kula ndizi iliyopikwa na mchanga mwenyewe? Machalali?” “Sijawahi Jelini, mwanangu.” “Umeona? Ningekuwa mimi ningembembeleza mchungaji na kumpaga mpaka akubali. Unabakiwa na kazi ya kufunga tu, nakuomba. Chakula mnakula kwa mama Jema, halafu mnaenda kulala tu. Au wewe unaona wazo baya?” “Naona wazo sio baya. Acha ‘nimpange’ mchungaji.” Akamuigilizia. “Ndio maana mimi nakupenda.” Wote wakacheka.

    “Jelini? Wewe si umesema hospitalini panakuogopesha huongei sana?” “Mimi mwenzio nataka kutembelewa na mchungaji, nyumbani  kwetu, ndio inabidi kuchangamka. Ila na wewe unakaribishwa Junior. Wewe wangu.” “Sawa Jelini.” Wakacheka na kuagana kwamba watawapitia na hapo, Jelini asijue anajipangia surprise yake mwenyewe.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Ilipofika muda wa saa nne usiku mchungaji na mkewe wakawa wanaingia hapo. Wakasimama wote kusalimia. “Kumbe bora ulivyomleta wewe! Mimi alinikatalia huyo! Alikuwa anatapika kuanzia asubuhi. Kila nikimwambia twende wakakuchome sindano, hataki.” “Sasa kwa nini umwambie mambo ya sindano wakati unajua anaogopa?” “Sasa ameishia wapi? Si yaleyale tu. Hapo si ana sindano!” “Usingemwambia sindano, angekuja mama! Halafu ndio aje akutane na sindano huku.” Kama kawaida ya Ezra hakosi neno la kuchangia kwa Junior.

    “Acha nikwambie Jelini mwanangu. Huyu na Noah wote hawataki sindano. Ukiwatajia tu hospitalini, akili inakimbilia kwenye sindano.” “Basi na mimi nipo hivyohivyo mama yangu. Hospitalini sipapendi, nipo hapa mpaka sasahivi sababu ya Ezra na Junior. Ila si vinginevyo.” Stori zikaanza, Ezra, Junior na mchungaji wakatoka nje. Wao wakabaki hapo ndani wakisubiria dripu iishe, waondoke.

Baba na Vijana wake.

    “Mambo yamekwendaje kwa mama Jema?” “Kule unajina kubwa!” “Acha baba!” Wote hawakuamini, maana alinyimwa kuwepo kwa Jeremy. Ikawapoozesha, kumbe! “Yule mama anaonekana amekufurahia na yupo tayari kwa wewe uoe binti yake wakati wowote. Anasema humdharau binti yake. Unampenda na kumjali kwa dhati. Umemfanya atulie na anasema Jelini anakupenda sana. Tukampa wazo hilo la ijumaa. Amelipenda kwa sababu anasema kwao jumamosi ndio siku kubwa ya biashara zake na binti yake. Kwa hiyo ataandaa mazingira mazuri nyumbani kwake, ili ufanye unachotaka.” Ezra alifurahia sana.

    “Asante baba yangu.” “Kwako naona kunakaa sawa. Ila naona kwa Junior tunaanza tena upya! Ni nini kinaendelea Junior? Kwa nini urudishiwe pete ya uchumba ambayo Hope alikuwa akijivunia nayo sana?” Ezra akamtizama kama kumkumbusha aseme ukweli.

    “Yeye alipenda vitu vyangu kuliko mimi mwenyewe baba. Na hilo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu nikiendelea kulifungia macho mpaka siku ya jumapili ndio kama nimefunguliwa macho. Hope amenipuuza kwa muda mrefu sana akiamini sitaweza kuja kumuacha kwa sababu ya jinsi nilivyo, na anajua nitahofia kuchafua sifa pale kanisani. Akajiaminisha na kunidharau huku akinitumia atakavyo. Lakini baba, na mimi nataka kupendwa na kuheshimiwa kama wanaume wengine.”

    “Unataka kuniambia Hope haku..” “Kile ulichokiona siku ya harusi ya Ester ni muendelezo wa mambo mengi na mimi kufumbia macho baba yangu. Muulize Ezra kama nasingizia. Ana jeuri fulani hivi ambayo unaweza kuifananisha na ujasiri lakini sio ujasiri. Ni kujiaminisha. Sasa safari hii naona ni kama amenisaidia kunifikisha mwisho.” “Junior! Mwisho tena!?” Baba yake akashangaa sana.

    “Hakika ile pete haitarudi kidoleni mwake tena.” Mzee akamwangalia Ezra. “Na mimi nasikia sasahivi mzee wangu.” “Kwamba wewe hukuwa ukijua?” “Kwa sehemu na alikubali kesho tuzungumze akiwa amenipa muda wa kufikiria kwanza. Hivi sasahivi na mimi ndio nashangazwa na haya maamuzi.” “Nimegundua moyo wangu umehama kabisa. Na tafadhali kumbuka maneno yako baba. Ulisema hutatutafutia mke.” “Umepatwa na nini Junior!?” “Baba, na mimi nataka ndoa kama yako! Hilo ni kosa!?” Akauliza kwa ukali kidogo. Mzee akabaki akimtizama.

    “Ila swala la ndoa ni la maisha yote yaliyopo hapa duniani. Nafikiri Junior ana haki yakupendwa na kujaliwa baba yangu. Hope ni kama tu Hellen. Tulimfungia macho tukidhani ndivyo inavyotakiwa kuwa, kwa kuwa kwanza hatukuwa na mfano mzuri wa mahusiano, ndiye alikuwa msichana wangu wa kwanza, tukadhania pengine nikijitahidi kumuonyesha upendo kwa kumpa na kufanya kila anachotaka na nikija kumuoa itabadilika.”

    “Lakini kumbe alikuwa akinitumia, na akaniacha kikatili kiasi kile! Mtu anayekupenda kwa dhati anakuheshimu na kujali hata hisia zako. Haiitaji kumfundisha kukujali au kumuonyesha upendo mwingi ili kukupenda. Nimeliona kwa Jelini. Kama mapenzi yapo, yapo tu baba yangu. Kwa hiyo nafikiri Junior ndiye ana haki ya kusimamia anachojisikia.” Ezra akamtetea huyo Junior japo naye ndio anasikia hapo kama ndio MWISHO Hope. Lakini bado akasimama naye akimtetea.

    “Hivi nyinyi mmehesabu garama ya hayo maamuzi yenu lakini?” “Japokuwa maamuzi ni ya Junior. Na wote tunakubaliana muoaji ni Junior, anahaki na kuchagua mke wake. Kama na wewe mzee wetu utakubaliana na hilo na ukakumbuka ulituahidi hutatuchagulia wake, basi kwenye madhara ya hili tunaomba utusaidie kusimama na sisi.” Ezra akawa anazungumza, amemkingia kifua Junior kama yeye ndio muoaji.

“Tunajua si kwenye jamii tu, hata kanisani hapatakuwa sawa. Tunahitaji msaada wako kusaidia hili liishe vizuri japo inaweza isiwe kwa amani.” Mzee wao akawatizama na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

    Junior akahema kwa nguvu. “Nashukuru Ezra.” “Hapana Junior. Naomba tuzungumze. Na tafadhali nisikilize. Maana umenibadilikia.” “Utanisamehe Ezra. Ila nimeshindwa kuendelea kumfumbia macho Emelda. Nimejisikia kuumia na kuona nimemtelekeza kwa muda mrefu wakati yeye hajawahi kunikatia tamaa! Nimemkuta mgonjwa, yupo peke yake wakati mimi nipo! Hakika sitaendelea kumfumbia macho tena. Kwanza sina sababu yakufanya hivyo. Kwa nini!? Kama niliweza kuweka muda wangu mwingi kwa watu baki, ni zaidi kwake.”

    “Hope hakuwa mtu baki. Ni mchumba ambaye ulimchumbia kanisani.” “Alikuwa mchumba. Tafadhali tusirudi tena nyuma. Na katika hili nakuhitaji Ezra.” “Lakini taratibu Junior! Tafadhali, taratibu.” “Siwezi tena. Kwa hiyo tutafute njia ingine. Lakini ‘taratibu’ hapana.” Junior akaweka msisitizo.

    “Kwamba umeshampenda?” “Nafikiri.” “Junior?” Akaanza kucheka. “Acha kunichanganya.” “Mimi nahisi nimepatwa na hisia za tofauti, na sijawahi jisikia hivi. Hakika siwezi kujisaidia Ezra. Akilia, nasikia kuumia kupita kiasi! Mimi si mtu wa kushika matapishi, lakini yake nimeshika, tena bila ya kufikiria! Mwili mzima ulisisimka nilipomshika kumpima homa.”

    “Junior!” “Sasa si ndio nakutoa kwenye kuchanganyikiwa? Hapa nakusaidia wewe. Halafu alipokuwa amelala nikamshika kidogo, hakika sijawahi jisikia hivyo! Nusura nimpakate kichwa nimbeleze alale akiwa miguuni kwangu.” Ezra alimtizama kama anayeshindwa kummaliza, Junior hana mbavu.

    “Kumbe kupenda ndio raha hivi!” “Naomba tuhitimishe na Hope kwanza.” “Sawa. Kwa hiyo wakati wewe ukiweka mipango ya kuhitimisha, mimi naendelea na Emelda.” “Umepatwa na nini Junior?!” “Wewe ndio unashindwa kunielewa Ezra na unanisikitisha. Nimekwambia sitaendelea tena kumpuuza Emelda. Sitapoteza muda wangu kwa watu baki. Emelda kwanza, ndio mengine baadaye. Au hutaki tuoe tena?” Mara daktari akawa anaingia chumba alichopumzishwa Emelda.

    Junior akataka kikimbilia, Ezra akamuwahi. “Naomba usubiri kwanza.” “Ni nini tena!?” “Emelda ataruhusiwa kurudi nyumbani.” “Najua.” “Najua unajua, kwa hiyo?” “Nitamru..” “Hapana Junior. Hutamrudisha wewe nyumbani. Acha wazazi warudi naye.” “Ezra!” “Subiri kwanza Junior. Kesho wanapotoka mida yao ile ya saa nne, wewe ndio urudi nyumbani ukamwangalie. Lakini usiku wa leo, tafadhali naomba uishie hivi. Tafadhali Junior. Baby steps.” “Hapo hapana.” Akamtibua.

    “Basi, basi! Sio baby steps. Tutembee hatua moja baada ya nyingine.” “Hapo sawa. Ila si kwa kunichelewesha.” “Sawa Junior.” Hapo wakakubaliana, na kurudi ndani.

    Daktari akamruhusu, akiwa ameridhia arudie dawa ya malaria usiku huo baada ya kula. Ilikuwa ni ya kunywa mara moja tu, ila akaandikiwa dawa za kuzuia kutapika tena. Wazazi wakaondoka na Emelda. Ezra na Jelini. Junior akaondoka peke yake.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Alipofika tu nyumbani ujumbe ukaingia. Alikuwa Emelda. Safari hii akaona. Akataka kumsikia na kuelewa. Akaweka kila kitu pembeni, kisha akaenda kukaa kabisa ili asome asije akokosa ujumbe mzima. Ila ujumbe ulikuwa mfupi tu. ‘Nashukuru kaka.’ Junior akarudia tena na tena akitamani kama angeandika zaidi.

    Akaamua kumjibu kwa swali. ‘Naweza kupiga?” ‘Mama ananiandalia chakula. Pumzika tu kaka. Sisi huku tupo salama. Ila usiache kula.’ Emelda akajibu. ‘Nataka kuzungumza na wewe.’ Moyo wa Emelda ukajaa furaha, japo hakujua anataka kuzungumza nini. Ujumbe mwingine ukaingia. ‘Au nakusumbua, unataka kupumzika?’ Ni Junior, kaka yake wa siku nyingi. Huo ujumbe ukawa si kawaida yake. Kwanza huwa hajibu jumbe zake. Usiku huo anawasiwasi wa kumsumbua! Emelda akapatwa na sintofahamu.

    ‘Hapana kaka. Hunisumbui kabisa. Nakuonea huruma, najua unatakiwa kuamka alfajiri sababu ya kazi.’ Junior akasikia kujaliwa huyo, kana kwamba ni mara yake ya kwanza wakati ni kawaida ya Emelda ila hakuwahi kumuelewa wala kumsikia. Akamjibu huku akimfikiria. ‘Usijali. Naomba kuongea na wewe kabla hujalala na pakiwa pametulia. Nijulishe.’ ‘Nitafanya hivyo.’ Akajibu na kuficha simu chini ya mto ili mama yao akiingia asione.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Akaamua kuoga kabisa na kujiweka kitandani akisubiria simu ya Emelda. Baada ya muda akaona simu yake. Akakata, kisha akampigia yeye. “Umekula vizuri?” “Ndiyo.” Akajibu kwa utulivu. “Na umeshiba, hujatapika?” “Sijatapika. Asante kunipeleka hospitali. Nilikuwa namkatalia mama.” “Usiwe unaugua peke yako. Uwe unanijulisha.” “Unakua na mambo mengi kaka. Wakati mwingine inakuwia ngumu kunisikia.” Emelda akazungumza kwa upole, lakini Junior akamuelewa.

    “Nakuahidi kubadilika. Kuanzia sasa nitakuwa nikikusikia. Ni ahadi nakupa.” Emelda hakuamini! Akajisikia machozi kumtoka. Alishamfungia huyo Junior, akimuomba Mungu amfungue macho kwake, lakini wapi! Mpaka akakata tamaa. Akajua amebakia kumchukulia ni msichana wa kazi za ndani tu. Hamuoni kama ni mwanamke anayeweza kuwa zaidi ya hivyo.

    “Umenisikia?” “Ndiyo.” Akajibu kwa heshima. “Kesho nitakuja kukuona. Nikuletee nini? Niambie chochote unachojisikia kula. Na hunisumbui.” “Unamjua mama anavyopika. Kutakuwa na vyakula vingi. Usihang…” “Sio usumbufu. Huna hamu na kitu chochote?” “Sina kaka. Pengine sababu ya kuumwa. Sina hamu na chakula kabisa.” “Basi nitakuletea hata matunda. Pumzika. Nitakuona kesho.” “Asante kaka. Uwe na usiku mwema.” “Na wewe pia, Emelda.” Simu ikakatwa na kuwaacha hao wawili wote mapigo ya moyo yakienda kasi.

Alhamisi.

    Asubuhi hiyo alimkuta Ezra alishafika ofisini. “Nimezungumza na Hope, nimemuomba leo mchana mkutane tena.” “Hapana Ezra. Leo mchana nina ratiba ya muhimu sana.” Akakataa bila ya kufikiria. “Hivi unafikiri utamalizaje swala lako na Hope?” “Sijakataa, ila isiwe leo mchana.” Akafikiria kwa haraka, kisha akaongeza. “Na kesho pia sitaweza.” Ezra akabaki akimwangalia.

    “Ni nini sasa?” Umepatwa na nini Junior!?” “Mbona sijakataa! Ila si leo wala kesho. Pengine tufanye jumamosi, mida ya saa nne asubuhi.” “Hapo sasa unaongea. Sasa utamwambia nini?” “Kwamba naahirisha uchumba.” “Hivyo tu?!” “Basi niambie wewe unavyotaka nikamwambie, nitamwambia. Ila kwa sasa sina sababu ingine. Na nataka kumaliza majukumu yangu hapa kwa haraka ili saa nne niende kwa Emelda kama ulivyosema jana.” Hapo akamkazia sauti kama usinigeuke.

    “Kama unakwenda saa nne, inamaana mida ya saa sita utakuwa umesharudi!” “Hapo sasa unanigeuka Ezra, na si kawaida yako. Jana uliniambia nini?” “Wewe unataka ukakae nyumbani mpaka ukutwe pale na wazazi!?” “Sina ninachoficha tena.” “Hapana Junior. Mpaka uhitimishe kwanza na Hope, ndipo uanze jambo jingine. Mfikirie mama.” “Sawa. Lakini sasahivi nina mgonjwa, siwezi kukutana na Hope. Mwambie jumamosi.”

    “Sawa. Jumamosi saa nne asubuhi. Nyumbani kwako?” “Hapana!” Akashituka kabisa. “Kwa nini afike kwangu na tunaachana!? Tafadhali iwe sehemu ingine tena nashauri iwe ya wazi kabisa. Tunaweza kwenda wote.” “Hatutafanya hivyo! Huo hautakuwa ustaarabu. Ulitongoza mwenyewe, nenda kaitimishe mwenyewe.” Akamkatalia.

    “Sawa. Lakini sio nyumbani kwangu. Hapo hapana Ezra.” “Kwa nini?” Akamuona anasita. “Junior?” “Sasa anafuata nini kwangu?” “Junior?” Ezra akasisitiza akiwa anajua kuna anachoficha. “Nitakuwa na Emelda. Nataka mida ya saa sita, aje nyumbani tuzungumze. Sasa sitaki aje akute hata dalili za Hope.” Ezra akachoka kabisa.

    “Yaani ile saa nne ninapokwenda kukutana naye kwa kuhitimisha, nampelekea kila kitu chake alichoacha kwangu, tunaagana kwa amani. Simdai, hanidai. Hakaribishwi tena kwangu.” “Hope atajua kwa hakika ule utabiri wangu juu yenu haukuwa utabiri, nilijua kinachoendelea. Nikabaki kumsanifu tu!” Akawa amemchanganya Junior.

    “Utabiri gani tena!?” “Umeniponza Junior!” “Nini tena!?” “Mimi nilimwambia juu ya mfano wa kitabu cha Ester. Juu ya malikia Vashti…” Kabla hajamaliza, Junior akawa ameelewa. Acha acheke. “Wewe nabii aisee!” “Acha kucheka Junior! Hope atajua muda wote mimi namuwekea mipango ya kukutana na wewe, lakini najua yupo Emelda!” “Huna jinsi ya kurekebisha hilo.” Ezra akabaki akimwangalia.

    “Wewe endelea na mipango ya saa nne, ya siku ya jumamosi. Kama hataweza, basi tena mpaka jumatatu. Na isiwe kwako.” “Unajua kwangu siwezi kumruhusu tena, sababu ya Jelini.” “Basi na mimi sababu ya Emelda.” “Unaiga Junior!” Hana mbavu kama mazuri.

“Wewe changamka, tuoe, tutulie. Tengeneza mazingira mazuri, jumamosi tufunge ukurasa wa Hope. Kesho unachumbia wewe. Jumapili tunatangaza uchumba. Mnaombewa. Watu wakishamaliza maneno kati yangu na Hope. Pakipoa tu pale kanisani, namchumbia Emelda. Ndani ya miezi mitatu, tunaoa, tuanzishe familia. Au unasemaje?” Hapo akampata Ezra.

    Junior wa mipango, Ezra akacheka. “Hatutakuwa tumeharakisha sana?” “Pesa tunayo. Wanawake wanaotupenda tunao, tatizo ni nini?” “Namaanisha kwa upande wako na Hope, mpaka Emelda, kisha ndoa? Watu hawatakuelewa Junior!” “Nani amekwambia sasahivi wananielewa? Mimi shida yangu Emelda. Akinielewa yeye, akukubali ndoa, naoa. Mengine nitajua mbele ya safari. Kwanza nimeshapata jibu la swali lako.”

    “Kwamba kama unampenda?” “Ndiyo. Nikiongea naye najisikia tofauti. Furaha ya ajabu! Bwana yule binti ananipenda na kunijali Ezra!” “Kwamba baada ya pale ulimpigia simu tena?” “Sio kwa haraka! Mama alipoenda kulala! Wewe vipi Ezra!” Ezra akatingisha kichwa kwa masikitiko, Junior hana mbavu.

~~~~~~~~~~~~~~~

Itaendelea….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment