Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 30. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 30.

“Unajuta nini?” “Kumpuuza na kushindwa kumuelewa kabisa! Unakumbuka nilivyougua kipindi kile mpaka nikalazwa hospitalini?” “Ndio hayo nayakumbuka sasahivi na kuanza kuyapa picha ya tofauti na nilivyokuwa nikidhani!” “Kabisa. Alikuwa akija kila siku asubuhi na mapema kuniona na vyakula, bila wazazi. Nakumbuka ulikuwa ukimuuliza mbona hasubirii usafiri, akawa anasema anawahi kuja ili awahi kurudi asichelewe kazi nyumbani.” “Aisee kumbe kweli umepata muda wa kufikiria Junior! Alijibu hivyohivyo!”

    “Nakwambia sijalala usiku nikimfikiria yeye na aliyokuwa akinifanyia. Alihangaika kweli, lakini kinachoniuma, nakumbuka siku ya mwisho karibia natoka, alinikuta peke yangu pale chumbani wewe umeenda kulipia au sijui ulikuwa wapi! Aliniomba rasmi kuwa anaomba nikitoka pale, nikakae nyumbani kwa siku chache mpaka nipate nguvu.” Junior akatingisha kichwa kwa masikitiko.

    “Nini?” “Aisee mpaka najichukia. Maana alijitahidi kabisa kuniomba, ila alijawa hofu, mimi nikapuuzia.” “Yeye alisema ni kwa nini alitaka ukaugulie nyumbani?” “Alisema ingekuwa rahisi ‘kwa mama’ kuniona na kuhakikisha nakula vizuri na nakupata mapumziko yakutosha.” “Alimtumia mama?” “Ndivyo alivyoniambia. Sasa ukumbuke wakati ule ndio nimeanzana na Hope, akili ilikuwa haipo kabisa. Nikamjibu tu kwa kifupi, nitakuwa sawa. Akapoa kabisa, hakuzungumza tena, akaondoka.”

    “Sasa iliyokuwa mbaya, ambayo nakumbuka ilikuwa siku ile namchumbia Hope. Yaania nilikumbuka jana, hakika nilishindwa kulala.” “Ilikuaje?” “Yule binti hakula Ezra. Maana kwanza nilimuona pale kanisani kama macho mekundu sana. Kama  aliyekuwa akilia. Sasa kulikuwa na hekaheka watu wakitupongeza, nikashindwa kabisa kuzungumza naye. Jioni si ndio mama akawa amealika marafiki, familia ya kina Hope na wale majirani kwa chakula kwa ajili ya kufahamiana zaidi. Sasa kuna kitu nilikuwa nafuata jikoni, nakumbuka kumsikia mama akimwambia ni lazima ale. Hawezi kuendelea kufunga siku muhimu kama ile.”

    “Sasa mimi nikawapuuza nikijua ni kawaida ya mama na wale wanae pale. Noah na Emelda. Kutwa kuwabembeleza. Nikafanya yangu, nikarudi sebuleni. Sasa soma hizo jumbe ndio utakubaliana na mimi kama aliumia baada ya kuona nimechumbia, na utagundua huyu binti bado ananisubiria mimi.” Kazi ya kusoma hizo jumbe ikaanza. Ezra alianzia mwanzo kabisa, taratibu akisoma. Junior akabaki ametulia.

    Ezra alisoma mpaka mwisho na kubaki ameduaa. “Haiwezekani Junior! Uliwezaje kutoelewa!?” “Hapo unazungumza kwa sababu nimekwambia haya. Lakini simama upande wangu, na vile Emelda alivyo na anavyotuheshimu. Angalia jumbe zake zilivyojaa heshima. Ni ‘kaka’ wakati wote. Hata akiwa ananipa maji kanisani, au akileta zile juisi pale kanisani unaweza fikiria ametumwa na mama.” “Kwamba na juisi zile wanazotuma kila jumapili wakija kanisani ni yeye?!” Ezra akawa bado haamini. “Nakuhakikishia ni yeye. Na zile chupa zakutopooza anazowekaga mle, ni yeye. Mama yako hana habari hata.”

    “Sema zilituchanganya maana ni ladha kama juisi anazotengeneza mama kabisa. Na chakula akipika Emelda ni kama amepika mama, ndio maana inakua ngumu kugundua. Na upaji wake wa kitu ni rahisi kufikiria ametumwa. Maana anaweza kunikuta nipo busy pale kanisani, anapenyeza chupa mkononi mpaka nimgeukie. Ndio ananipa na yako, napo nashukuru na kuendelea na yangu nikijua mama ndiye amemtuma maana mama ndiye…” “Anayependa kusisitiza maswala ya kunywa maji.” Akamalizia Ezra.

    “Sasa kumbe ni kwa mwanae yule mnywa pombe, ndiye anamsisitizia maji na chakula. Na kuhakikisha baba hapungukiwi maji kanisani. Lakini sio sisi.” Ezra akacheka akifikiria. “Na imekua kasumba yake. Kila maji unayoona nakupa siku za jumapili ni yeye Emelda anakuwa amenipa.” “Na haachi kuja na chai yetu kila siku ya ijumaa kwenye maombi!” “Ewaaah! Sasa usifikiri ni mama. Ni yeye mwenyewe.” Ezra akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha.

    Akamwangalia, wakabaki wakiangaliana. “Sasa utafanyaje Junior!?” “Ninachojua sasahivi ni mgonjwa, naenda kulipa fadhila.” “Subiri kwanza Junior. Naomba fikiria kabla ya kuanzisha jambo jingine.” “Wewe umesoma hizo jumbe?” “Ndiyo.” “Haya, fungua na kwenye chat zangu zote na Hope, kisha tulia fikiria mahusiano yangu na Hope. Kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kisha nakupa nafasi ya kuja kunishauri. Ila sio leo. Nataka upate muda wa kutafakari. Halafu uje uniambie kama naanzisha jambo jipya, au napokea jambo ambalo nililifungia macho.”

    “Junior?!” “Unashangaa nini na wewe umepewa nafasi ya kunishauri? Mimi siendi kufanya jambo la ajabu. Emelda ni mgonjwa.” “Anaumwa nini?” “Mama ameniambia eti baba anamlaumu Noah, amemuambukiza malaria ya baa.” Wakaanza kucheka.

“Kwa hiyo ni malaria. Sasa mimi nawajua pale nyumbani, wanaweza wakawa wamepuuza, wanamuombea tu. Nataka niende nikamuone mimi mwenyewe.” Ezra akabaki akimwangalia, Junior akaanza kucheka kama sio yeye aliyekuwa amekasirika.

    “Acha kunitizama hivyo!” “Unauhakika Junior?” “Kadiri ninavyoendelea kufikiria, ndivyo ninavyopata uhakika Ezra. Huyu binti amenijali kama hivyo unavyomfanyia Jelini. Tofauti yetu ni mimi nimekosa shukurani.” “Nafikiri si kukosa shukurani, ila ni kutambua,kutoona na kumwambia yeye mwenyewe kwamba unathamini anachokifanya.” Ezra akatulia na kurudia kusoma jumbe moja iliyokuwa imemgusa.

    “Junior!” Junior akamwangalia. “Ni kama huyu binti anakusubiria!” “Ewaah! Kuna ujumbe hapo ni kama ameniambia kwamba hatachoka kunisubiri.” “Na unakumbuka hata Ester alimwambia kwamba na yeye akue, aondoke pale ndani, aache kunyang’anyana ziwa na Noah, unakumbuka alimjibu Ester kuwa yeye atakuwa mtu wa mwisho kuolewa mle ndani? Tena akasema hivi, wote tukishaoa, ndipo atajiridhisha kuwa zamu yake ndio imefika, anatakiwa kuondoka. Unakumbuka Junior?” “Nakwambia ndio ilikuwa kazi ya jana hiyo. Nimekumbuka mengi, nikashindwa kulala. Na Emelda ni mzuri tu. Asingeshindwa kuolewa na kuondoka pale ndani.” “Sawasawa. Najua najirudia Junior. Lakini tafadhali niambie utafanya nini?”

    “Nimeshakwabia na najua huna tatizo la kukumbuka.” “Acha kucheka Junior! Ujue hili jambo ni zito sana? Umeliangalia kwa kona zote?” “Mpaka kanisani, wazazi, Hope na wengine wote. Ila ninachojua kila jambo linatokea kwa sababu. Mimi sikutaka Hope anirudishie pete!” “Junior! Unajua hilo halikuwa lengo lake.” “Then, too bad. Hainihusu. Maandiko yanasemaje?” “Tafadhali acha kunukuu maandiko kwenye kipindi kama hichi! Mimi nimeshachanganyikiwa.” Junior hana mbavu.

    “Maandiko yanasema, ‘everything, works together for good, for those who loves God.’ Sasa..” “Junior!?” “Sasa mimi ndiye niliyeandika bibilia jamani!? Unamzuiaje Mungu kufanya yake katika kunipatia mema? Au wewe huamini katika maombi tunayoomba kila siku?” “Tafadhali taratibu Junior. Please.” “Sawa.” Akakubali akicheka.

    “Naomba niagizie matunda kama unayomnunulia Jelini.” Ezra akabaki akimtiza. Junior amebadilika, anacheka kama siye yeye aliyekua amepoa. “Kwamba wewe umefurahia kurudishiwa pete au? Mbona sikuelewi?!” “Soma andiko hilo Ezra.Warumi 8:28 ‘nasi twajua ya kuwa katika mambo YOTE Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia MEMA, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake’. Hilo ni neno la Mungu. Sasa mimi kosa langu ni kufurahia neno!? Tena naomba ongeza na maua.” “Maua hapana Junior. Hapo HAPANA. Peleka matunda kwanza.” “Sawa.” Akakubali na kurudisha macho kwenye kompyuta yake, akicheka.

    Ezra akatulia kama amepigwa na butwaa. “Sikusikii ukiagiza matunda Ezra! 9:45 mimi natoka hapa, navizia muda wa wazazi kutoka pale ndani, ili kuepusha maswali mengi.” “Hapa namuwazia mama na kumuhurumia. Maana hiki ndicho kile kipindi mzee anakabidhisha watoto wakiume wote ni wa mama. Na huwa hajui alikosea wapi, maana yeye amekamilisha kazi yake vizuri kwa Ester.” Junior hana mbavu.

    “Ila mama anampenda sana Emelda.” Akaongeza Junior mwenyewe. “Hilo tu ndilo la kushukuru Mungu, ila sasa ushajiuliza katika hili atalichukuliaje?” “Mimi hilo halinitii wasiwasi kama pengine nimemsoma Emelda vibaya.” Akamuona anaanza kuvunjika moyo.

“Iweje niwe nimemfikiria sivyo kwa sababu mawazo tu yalinipelekea huko? Maana katika kuwaza kama na mimi nilishabahatika kujaliwa hapa duniani na mwanamke, ndio nikaishia kwa Emelda. Nikajivunja moyo nikijiambia pengine alikuwa akifanya hayo yote kwa kutumwa na mama! Ndio ikabidi kuanza kufanya uchunguzi.” “Sasa hayo mashaka ndio yanata kukupokonya furaha yako Junior.” Akamuhurumia tena.

    “Nisikilize. Naona umewaza vizuri. Nenda muda ambao pale nyumbani mtakuwa peke yenu, umsome. Kwanza akikuona umekwenda kwa ajili yake, jua itamshitua. Lakini hakikisha unatuliza hiyo hali ili kuweza kumsoma moyo wake. Msichana akikupenda na kama ni wako utajua tu, Junior. Japokuwa Jelini alikuwa kitisha, kama ni wa viwango vingine kabisa, na…” “Hata mimi nilikukatisha tamaa ili usije umia.”

    “Ewaa! Lakini ndani ya moyo wangu nilijua nampenda na kumtaka yule binti. Haikuwa kwa haraka, lakini ona ilivyokuwa sasahivi. Sasa kwako kama ni kweli, ndio ujue itakuwa rahisi kabisa sababu anakusubiri. Usiogope.” “Nashukuru Ezra.” Tayari Ezra akawa tena upande wake, hataki kumuona tena anarudia ile hali ya kutokuwa na furaha.

~~~~~~~~~~~~~~~

    “Nikwambie kitu lakini usishituke?” “Husubiri hili likae sawa kwanza Junior ndipo tuanze bomu jingine?!” Junior akazidi kucheka. “Hope aliponiacha pale, baba alinipigia simu kunitaarifu kuwa anakutana na Hope leo ndipo wakutane na mama Jema jioni. Sikumficha. Nilimpigia picha ile pete juu ya meza, nikamwambia Hope amenivulia na kunirudishia. Sikumwambia mengi ila mzee amesikitika sana. Akasema hivyo sivyo alivyodhania mwisho wetu.” “Ila utamwambia ukweli.” Hapo akamtibua kidogo.

    “Ukweli kwamba ameniachia mimi jukumu la kutengeneza, akijipa yeye thamani kwamba nilazima nitamvalisha yeye tena hii pete? Kwamba ni yeye tu amebakia hapa duniani? Na mimi nina jukumu la kunyenyekea yeye akinidhalilisha! Kwa nini? Hana hata chembe ya kunijali kama Emelda ambaye nimekua nikimpuuza!” “Sina nia ya kukuudhi Junior. Na mimi nataka upate kitu kizuri. Ila nataka kusiwe na hila. Tafadhali Junior. Uchumba si ndoa. Unaweza kuvunjika, lakini nataka kama tunamalizana na Hope, tumalize kwa heshima. Ni sawa?” “Sawa.” Akatulia.

    “Mbona sasa ni kama umeshafanya maamuzi yako?” “Ndiyo.” “Junior! Sio kwamba umesema kesho tutazungumza?” “Kwani ni mara ngapi nakua nimeamua jambo na kubadilisha? Wewe njoo na hoja zakueleweka bila kuangalia jamii na watu watasemaje, ila mimi kama Junior. Ukinifikiria furaha yangu hapa duniani, na kile ninachostahili. Watu wengine mpaka wazazi hao najua hatutashindwa kuwakabili endapo sisi wawili tutaamua kusimama pamoja.” “Sawa.” Ezra akamkubalia. Hapo akatulia.

Penzi.

     Alijikuta amewahi kidogo. Kwa hiyo akaegesha gari pembeni ya nyumba mpaka alipoona gari ya wazazi wake ikitoka, ndipo na yeye akaingia. Akasalimia mlinzi getini na kuvuta gari yake mpaka sehemu ya kuegesha magari. Akashuka kama akimbie na matunda yake mkononi.

     Akashukuru Mungu kukuta hata Noah hayupo. Akayaweka jikoni na kuelekea chumbani kwa Emelda. Akagonga mara kadhaa na kusubiria, baada ya muda akamsikia anafungua. Alishituka sana kumuona Junior pale.

    “Shikamoo, kaka.” “Marahaba. Vipi? Pole nimekuamsha.” “Hamna neno. Pole na kazi.” Akamwambia kwa kujali. “Asante. Pole na wewe kwa kuumwa.” “Nashukuru. Kama hujawakuta kina mama, waliniambia wataenda kanisani, na baada ya hapo kuna mahali watapitia, watachelewa kurudi. Labda ukakutane nao kanisani kabla hawajatoka.” Akamwambia akijua wazi yupo pale kwa ajili ya wazazi.

    “Mama ameniambia unaumwa, ndio nimekuja kukuangalia.” Akawa kama hajamuelewa. Junior akaelewa ila akajua ni haki yake. “Unajisikiaje?” “Ni kutapika ndiko kunanichosha. Hakuna kitu kinakaa ndani. Hata nikinywa maji tu, natapika. Umekula mchana?” Akabadili mazungumzo.

    “Nipo hapa kwa ajili yako Emelda. Nataka kujua unavyoendelea.” Jinsi alivyozungumza, akajua imemuingia, kwani alimwangalia na kuinamia mlangoni. “Kwa nini husemi ukiwa unauma?” Kimya akiwa ameinama, wamesimama hapo mlangoni. Lakini ikawa hali si ya kaka na dada tena. Junior huyu amekuja kivingine.

    “Umekunywa dawa ya kuzuia kutapika?” Akatingisha kichwa kukataa na kuongeza. “Kila kitu nikiweka mdomoni, natapika. Hata nahisi dawa zenyewe za malaria, nimezitapika. Ndio mama amesema tusubiri tuone, kama mpaka kesho homa itakuwa kali, anipe dawa zingine.” Junior hakupenda hilo.

    Akatoa mkono mfukoni na kumshika kipanda uso. “Una joto kali! Mama amekupima?” “Amenipa dawa, nikatapika ndio akaniambia nipumzike, akirudi atanipa zingine.” “Pole sana. Twende nikupeleke hospitalini. Angalau wakuchome sindano ya kuzuia kutapika, ndipo uweze kutumia dawa za malaria.” “Mimi naogopa sindano, kaka. Umesahau? Bora nijaribishe vidonge tena.” “Si umeniambia umejaribisha umekua ukitapika?” “Acha nijaribu tena.” “Unayo maji?” “Mama ameniachia hapo chumbani. Wewe nenda kapumzike kaka. Najua unachoka. Mimi nitakuwa sawa.” “Usijali. Tuone dawa unazotumia.” Wakaingia ndani.

Akaangalia hizo dawa, kweli zingemsaidia kushusha homa. Akampa na chupa ndogo ya maji aliyoikuta hapo pembeni ya kitanda, Emelda akimwangalia kwa kujificha asiamini kama ameingia hapo na ametumia muda wote huo kwake! Akawa hajui ni nini kinaendelea.

    Akameza akitarajia baada ya hapo ataondoka, lakini wapi! “Jipumzishe tuone kama hazitatoka. Usipotapika, nitakupa na matunda. Nimekuletea.” Emelda akahisi pengine malaria imempanda kichwani, anasikia na kuona mazingaombwe. Junior akiwa anamuelewa kabisa kwa jinsi alivyoishi naye kwa kumpuuza, akajiongeza. Akamnyooshea mashuka ya kitandani kwake, akaweka kama nafasi ya kulala na kumuwekea mto. Akamgeukia maana alizubaa akimtizama. “Panda ulale. Mimi nitakuwa hapa na wewe.” Akapanda bila ya kuongeza, akashangaa anamfunika kabisa, akalala ubavu ila akimwangalia.

    Akashangaa anakaa hapohapo kitandani na si kwenye kitanda cha pembeni ambacho kilikuwa cha Ester au kuondoka kabisa. Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi. Akamshika kipanda uso. “Unajoto kali! Acha nikuletee taulo la maji.” Wakati Junior anasimama, na yeye akaruka kitandani kukimbilia bafuni kutapika. Kilikuwa chumba chake na Ester, na bado vitu baadhi vya Ester vilikuwemo humo.

    Akamfuata na kwenda kumshika mbavu akiwa anatapika ili asiumie zaidi. Emelda alitamani asimalize kutapika. Hatimaye ameshikwa na Junior! Ikawa mix feelings. Kilio cha furaha na uchungu kikaanza. “Pole sana.” Akambembeleza. Alitapika kidogo nje ya choo. Wakati anajisaficha uso na mdomo, akashangaa Junior anaanza kusafisha matapishi yake. Kwa hakika hakuwa akielewa. Akamaliza na kurudi chumbani wakati Junior akimalizia kusafisha hapo bafuni. Akabaki amekaa kitandani hata haelewi.

    “Nakupisha ubadili nguo, twende hospitalini. Pole.” “Asante.” Akatoka na kwenda kumsubiria sebuleni. Baada ya muda akatoka. “Vipi?” “Nikitapika najisikia afadhali. Ila nachoka! Hapa natamani kulala tu.” “Pole. Twende. Wakishakupa dawa, utalala.” Wakatoka hapo kuelekea hospitalini.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Sasa Emelda akashangaa sana aina ya hospitali aliyopelekwa. Viwango vyake na yeye haviendani kabisa. Kulekule alipokuwa amelazwa yeye Junior ndio akampeleka na yeye. Akashangaa sana. Lakini kwa kuwa usiku huo kulikuwa na mengi ya ajabu, akaona atulie tu. Yeye mwenyewe Junior akaandikisha kila kitu, ndipo wakaenda kumuona daktari. Muda huo tayari giza lilisha ingia, wagonjwa si wengi. Wakabaki kusubiria nje, baada ya muda mfupi na wao zamu yao ikafika. Wakaingia.

    “Natapika. Hata mama aliponipa dawa, hazikukaa sana, nikatapika.” Akamwambia hivyo daktari. “Unatumia dawa gani?” Akamwangalia Junior. “Mama amempa za malaria.” Junior akamsaidia. “Ulipima?” Hilo swali likamfanya na Junior kumwangalia. “Noah alikuwa na malaria, ndio nilivyoanza kutapika na homa wakasema itakua malaria tu. Wakanipa dawa kama za Noah.” Hayo anamwambia Junior, daktari akisikiliza, mpaka Junior akaishiwa nguvu. Ila aliwajua wazazi wake. Akajua hata huyo Noah naye atakuwa hajapimwa alipewa tu dawa.

    “Ni sawa akifanyiwa full blood picture. Ili tujue ni nini?” Ikabidi tu Junior aombe. Wakaandikiwa vipimo, wakaenda maabara kutolewa damu. “Naogopa kaka! Siwezi kabisa sindano.” Junior akacheka akimwangalia. “Wewe usiangalie. Wakiwa wanakuchoma na kutoa damu, usiangalie mpaka watakavyokwambia wamemaliza.” Akatulia lakini wazi akionekana hajaridhika.

    Wakatafuta sehemu na kukaa baada ya Junior kuweka kikaratasi walichopewa na daktari sehemu ya dirisha la maabara. Tena akaenda kukaa karibu yake kabisa, Emelda akainama pembeni yake akijichezea mikono yake. Na yeye akainama pembeni yake kabisa kama anayemchungulia pale alipojiinamia. “Siku nyingine ukiumwa, usiache kuniambia. Umesikia?” Akamwambia kwa upendo, na kuzidi kumchanganya Emelda.

    “Kuanzia leo, ukiumwa na chochote, unijulishe.” “Upo na majukumu mengi na muhimu, kaka. Kazini na kanisani, hupumziki! Nakuhurumia. Naona mengine upunguziwe.” Junior akasikia kujaliwa huyo, moyo kwatu, kama aliyekuwa na kiu, anapewa maji.

    “Sio katika ugonjwa wako. Nalo ni muhumu kwangu. Usiache kunitaarifu. Sawa?” Akatingisha kichwa kukubali, wakatulia mpaka walipoitwa na kutolewa damu. Akapatwa hali ya kichefuchefu tena, akakimbilia kutapika. Akatapika mpaka watu wa nje wakabaki kusikiliza, Junior akaingia ndani kumsaidia. Baada ya muda wakatoka. Akaenda kumuombea apate angalau sindano ya kuzuia kutapika wakati wakisubiria majibu.

    Kwa kuwa alikuwa ametapika sawa, wakaona wampe na dripu kabisa. Akapewa chumba cha mapumziko, akawekewa hiyo dripu akiwa ameshikwa na huyo Junior, kaka yake. Wakamuweka sawa, na kuwaacha hapo, Emelda alishapitiwa na usingizi. Junior akabaki amekaa hapo akimtizama kama asiyeamini wakati ni Emelda yuleyule ambaye alikuwa mbele ya macho yake, akimtunza bila kuchoka ila hakuwahi kumuona!

~~~~~~~~~~~~~~~

Junior anacheza karata nyingi kwa wakati mmoja. Huku akiwa ameshika pete ya uchumba, moyo umeshahamia kwa msichana wa kazi za ndani wa mama yake, aliyeshindwa kumuona wakati wote.

Pete itawekwa kidoleni kwa nani? Inarudi kwa Hope anayejulikana mpaka kanisani na kwa wazazi, au kwa  Emelda?

Uchumba wa Ezra na Jelini?

INAENDELEA. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment