Jioni Ezra na Junior wakafika nyumbani kwa wazazi. Wakamkuta
kama mzee wao alikuwa akiwasubiria kwa hamu sana. Wakakaa baada ya salamu. “Nina
somo linaloendelea pale kanisani, kwa huu mwezi mzima.” Ezra na Junior wakaanza
kucheka. “Na sisi ni washirika kwenye kanisa unalochunga mzee wangu.” Ezra
akaongea akicheka. “Tena sisi kondoo wale waaminifu, baba. Inamaana tunajua
kinachoendelea pale kanisani.” Junior naye akachangia kama kawaida yake, hakosi
neno juu ya neno la Ezra.
Mzee akawaangalia kama aliyekuwa akiwasubiri wamalize, kisha akaendelea. “Kama nilivyokuwa nikisema.
Katika hayo mafundisho ya huu mwezi, Mungu hajanipa ujumbe kuhusu
mapenzi yako na Jelini, huku Junior akiwa mpambe wa karibu sana. Sasa basi, nataka siku ya jumapili ninaposimama
pale kanisani, nibakie kuhubiri ujumbe niliopewa na Mungu.” Ezra na
Junior wakacheka taratibu wakimwangalia anavyoongea kwa makini.
“Mimi naomba nimsubirie mama aje.” Ezra akaongea. Mchungaji
akajirudisha nyuma ya kochi kimya akiwatizama bila ya kujibu. “Mbona kama mzee
umetupania hivi!?” “Mimi nimeitwa na Mungu, na aliyeniita ndiye anayenipa
ujumbe. Sasa jumbe za katikati, tena za kujitetea ili kujibu
maswali ya watu wanaoshikana mikono, wakivutana na kunong’onezana
masikioni, uchumba hautambuliki popote, hizo sina uwezo nazo sana wa kuzihubiri.”
Junior alicheka mpaka machozi. Ezra yeye akasimama.
“Acha mimi nikamsaidie mama kumalizia huko jikoni, naona
nitarudi naye.” Erza akaondoka Junior akiendelea kucheka.
“Tuhuma zimekushinda?” “Ni mapenzi tu kwako mama yangu.
Nimeona ni muda kweli hatujapika pamoja.” “Sasa mimi huku nilishamaliza muda tu.
Narudi kulekule ulikokimbia.” “Au tupumzike kidogo kabla ya…” “Wewe
twende. Maana leo nilazima mseme mipango inayoeleweka. Si kwa vile mlivyokuwa
harusini Ezra.” “Ilikuwa imezidi sana?” “Sana.” “Twende basi nikakupe
mipango mizima, na mzee akisikiliza.” Wakarudi sebuleni, mchungaji akimwangalia
kama anayemwambia hapa ni mtakuja.
Junior hana mbavu. “Ukitaka kwenda kwao, unanitoa mpaka
madhabahuni. Sasahivi mambo yanakuendea sawa, unanikwepa! Sasa usirudi
kinyumenyume.” “Ni vile sikutaka kujirudiarudia mzee wangu. Mbona najua sisi
tupo pamoja sana tu! Au unataka turudi tena mlimani?” Mama mchungaji na Junior
hawana mbavu vile Ezra anavyojitetea.
“Na kwa yule binti alivyo, ukicheza tu, safari hii ni mlima
Kilimanjaro.” Junior akazidi kukaukiwa. “Usiwe na wasiwasi mzee wangu.
Tumejipanga.” “Sawa. Na iwe haraka.” Akawasimulia mwanzo wake na Jelini mpaka
hapo.
“Jelini ananipenda kwa dhati wazee wangu, sitaki kuchelewa.
Kwa hiyo naombeni msaada wenu kumchumbia. Na pete tumeshapata na nimeshalipia
kabisa, sema inapunguzwa kidogo, itakuwa kubwa kwake.” “Hapo sasa unazungumza
lugha ya kueleweka.” Mama yao akampongeza.
“Nina wazo. Nafikiri inaweza saidia.” Akaanza mchungaji.
“Tusaidie tu, mzee wangu.” Akaongea kinyenyekevu huyo muoaji. “Jelini
amenikaribisha kwao na ameahidi kunipikia vitu vingi. Na nimemsikia
akikumbushia, inamaana amemaanisha. Sasa kwa kuwa mama yake ameweka
msimamo wa waziwazi. Nafikiria sisi kama wazazi tuzungumze naye kwanza, na
ndipo kuandaa mazingira ya kwenda nyumbani kwao sisi wote kama familia na huko
ndiko ukachumbie, halafu jumapili kanisani ni kuwaombea tu.” Junior na Ezra
wakaangaliana kama walioambizana.
“Kwani nyinyi wawili ni lazima kila kitu muamue pamoja?!”
“Wazo zuri sana.” Wakajibu kwa pamoja na kucheka. “Aisee utakuwa umeweka heshima
kubwa sana kitu yule mama nasikia ndio lalamiko lake. Watu hawaheshimu binti
zake kwa kuwa wanamdharau yeye. Kitendo cha nyinyi kumfuata kwanza, itakuwa
jambo la…” Akamtizama Junior. “Kimsingi na kimaana.” Junior akamalizia.
“Kwa kuwa nyinyi akili yenu naijua, nilijua mtakubali tu.
Hapa nishaandaa zawadi ya kumpa mzaa chema wangu, siku nikienda
kuomba kuoa.” “Wewe mama mimi ndio maana nakupenda aisee! Akili yako ya kipeke
yako! Sijui uliumbwaje mama yangu! Kama kuna kijiupendeleo hivi ambacho Mungu
alikupendelea!” “Maneno yote hayo ni ya zawadi tu ya ukweni?” Mchungaji
akafanya wacheke sana. Wakaweka mipango yao vizuri wakahamia mezani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba niamshiwe mwanangu
Noah jamani! Aje na yeye kula.” “Leo hajatoka?” Akauliza Junior akikaa.
“Anaumwa mwanangu!” “Mbu za baa hizo.” Mchungaji akaongeza. “Sio lazima ikawa
ndiko alikopatia huko! Kwani kila anayeumwa malaria, anakwenda baa?” “Asante
mama yangu. Maana humu ndani kila kitu ni mimi na baa! Sio mambo yote mabaya yapo
baa. Yapo mema pia.” Noah akawa akiongea akiwa anakuja hapo mezani. Hakuna
aliyemjibu.
Mama yake akamuandalia kiti kama kawaida yake na bakuli.
“Nimekutengenezea supu, baba yangu. Labda utapenda.” Wote kimya wakimjua mama
yao na Noah. “Labda kama kungekuwa na limao, mama.” “Nimeweka. Na nyama
nyingi.” Wakamuona anacheka huku akivuta bakuli lake. “Udumu mama yangu.
Uishi milele.” “Jikaze ule. Utapona tu baba.” Mchungaji na wengine kimya.
Mbegu Zilizopandwa Kwenye Rutuba.
“Halafu bro?” Junior na Ezra wakamwangalia kwa pamoja.
“Nimesikia Hope sio kiongozi tena. Nataka kumtoa kwenye kundi letu la
mawasiliano la viongozi na kwenye viongozi wanao simamia kwaya. Nilitaka
kukutaarifu kabla sija mleftisha na kumrimuvu.” “Sawa.” Junior
akajibu bila wasiwasi na kuendelea kupakua. Wengine wakabaki wameduaa.
“Unauhakika Junior?” Ikabidi mama mtu aulize. “Yeye si
kiongozi tena, sasa anabaki kwenye kundi la mazungumzo juu ya mipango inayohusu
kanisa, yeye akiwa kama nani? Naona Noah yupo sahihi kabisa. Hakuna sababu ya
kuwepo huko. Kwanzia sasahivi mipango yote ya kanisa, haimuhusu tena.” “Yesss!”
Hapohapo akatoa simu yake na kumtoa Hope kwenye makundi yote. Akaridhika.
“Bora watu waheme! Alitaka kugeuza kanisa kama kambi
ya Jeshi! Na niwaambie ukweli kabisa, yule demu wa bro wivu ndio unamsumbua,
hana lolote. Mimi namjua Hope. Hapendi kupitwa na hataki ushindani.
Amemuona Jelini tu, akajua atakua tishio kwake ndio aka..” “Usiongeze neno
jingine lolote Noah. Na hakika Mungu akusaidie.” Mchungaji akamuwahi.
“Sasa mimi nimesemaje!?” “Nakwambia hivi, chochote
unachotaka kukisema juu ya Hope NAKUONYA. Na usirudie tena.”
Wakashangaa mchungaji amebadilika. “Yule binti amejitoa sana pale kanisani.
Tena amejitoa bila kuchoka, mchana na usiku akihakikisha mambo yote yanakaa
sawa! Mambo yamekuwa yakienda sawa pale kanisani na yeye akichangia, tena bila
ya kulalamika wala kutaka kulipwa! Alifanya kana kwamba anafanya kwa Bwana
kabisa, tena bila kujisingizia! Amekuvumilia wewe mara ngapi?” Akamuuliza
kwa ukali kabisa.
“Ulitaka akufanyie kama hivi mama yako anavyokufanyia hata
kwenye mambo yaliyokutaka uwajibike kwa haraka, tena ukiwa umelewa? Ulitaka
kazi ya Mungu iharibike sababu ya kubembelezwa wewe? Ulitaka afanye nini
kwenye vipindi vilivyohitajika majibu ya haraka na wewe unashindwa kutoa
ushirikiano?” Mchungaji hapo akawa mkali kabisa.
“Leo iwe mwisho kumzungumza vibaya Hope. Amekua
msaada mkubwa sana pale kanisani. Ni aliyekosa macho na uelewa tu, ndio anaweza
kupuuza juhudi za Hope. Ameshika usukani wa pale kanisani, vitengo vingi
havikuwa sawa kama sasahivi. Amesimamia mambo mengi kwakujituma, bila
kuchoka, tena ibada zote! Hajui kuchelewa kanisani, hajui kuwahi kutoka
kanisani. Atakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika pale na wa mwisho
kuhakikisha mambo yote yapo sawa. Kila jumapili, bila kukosa. Na ndio maana
unaona watu wazima pale, wanamuheshimu.”
“Hope anajua anachozungumza na anakisimamia. Anaongoza mpaka
wazee na wote wanamsifia anafanya vizuri. Sasa wewe ulitaka ndio umkwamishe
au ukwamishe utaratibu mzima wa pale kanisani kwa sababu ya
kubembelezwa? Utakua lini wewe!? Ni lini mambo ya msingi utayachukulia kwa
msingi na kutizama mambo kwa manufaa ya wengine na si kujitizama wewe peke yako
ukitaka hisia zako tu ndio zilindwe?” Hakuna aliyetegemea, maana gia
ilibadilishwa angani bila kutarajia.
Ugomvi wa Hope na Noah ulishazoeleka hapo ndani na mzee
hakuwa mkali hivyo. Kila mtu kimya mpaka mkewe. “Tafadhali sana ukue Noah. Kua
na utoe huo utoto akili mwako. Acha ujinga. Acha uzembe. Yapo
masaa mengi sana ya kuelewa. Hushindwi wewe kwenda kwenye pombe zako baada ya
ibada! Ibada ni masaa machache tu. Unashindwa vipi kujikaza na kufanya kazi
uliyopewa, kisha kwenda kunywa pombe zako? Au utapungua wapi kwenda mazoezini.
Masaa machache tu. Hata matatu hayazidi. Kufundisha watu, kisha kwenda kulewa
usiku kuchwa?”
“Jeuri hiyo ndani ya nyumba ya Mungu unapata wapi Noah!? Huogopi
wewe!? Leo unapata mtu anayekusaidia kukuweka sawa kwenye mstari, unamgeuza
kejeli mbele za watu! Hakika leo iwe mwisho Noah! Umenisikia mama
Junior?” Wakajua habari imeshageuka.
“Kaa naye huyu, uzungumze naye. Amekataa msaada wetu.
Na hata misaada ambayo Mungu anamtumia ya watu baki pia anatoa dhihaka!
Utacheza na Mungu mpaka lini, Noah? Unataka kugeuka kuwa kama watoto wa nabii
Eli? Unataka hasira ya Mungu kwenye maisha yako wewe? Noah!?” Akamuita kwa
ukali.
“Nimekusikia baba. Nitajirekebisha.” “Na ikawe hivyo hata
kwa Hope. Binafsi nimepoteza mtu muhimu sana pale kanisani. Hilo sitawaficha.
Hope alikuwa mtu wangu ninayemtegemea muda na wakati wowote. Hakuna wakati
nitampigia simu, nimuombe afanye jambo, akashindwa kutekeleza. Hajui kukataa
wala hana visingizio. Atahangaika na hilo jambo mpaka atakufanikishia!
Nitapata wapi mtu kama yeye? Na hata kama nitapata mwingine, si ingekua bora
kupata mtu wa pili yake na si kupunguziwa Hope! Tafadhali leo iwe mwisho
kumdhihaki Hope. Nisiwahi kukusikia tena. Unapomtizama, angalia hiyo
haiba yake kwa jicho jingine, utagundua si unachomfikiria wewe, ila ni miongoni
mwa watu wachache sana, wanaoweza kujitoa kwenye jambo, wakilisimamia kwa
garama kubwa, kuhakikisha mambo yanakwenda sawa. Tafadhali sana.” “Samahani
baba. Na nimeelewa.” Hapo ndipo pakatulia.
Hao watoto wa huyo mzee hata Ezra alipohamia hapo aligundua.
Sio wakorofi kabisa. Wapo kama mama yao tu. Noah alitulia kabisa hapo na
kuendelea kula.
“Baba yupo sahihi jamani. Sisi tumeanza hii huduma hata
nyinyi hamkuwa mmezaliwa, labda Junior. Sidhani kama tumeshawahi pata mtu
aliyesimama na ile huduma kwa kiwango cha Hope. Yule binti amepitiliza jamani!
Japokuwa ameacha nafasi ya uongozi lakini nafikiri tufikirie zawadi nzuri yakumpa.
Kitu kizuri cha kumwambia tumeona na kutambua juhudi zake.” Mama
mchungaji akaongeza kama anayejikomba kwa mumewe. Hapo akapata moyo wa mumewe.
Junior kimya.
Ezra akadakia. “Wazo zuri mama. Tufanyeni hivyo, tena bila
ya kuchelewa.” Angalau wakabadili mazungumzo, wakala kwa utulivu. Mazungumzo
mengine yakaendelea ndipo Ezra akaomba afungiwe chakula cha Jelini, akaondoka kwenda
kukutana na Jelini, akimuacha Junior nyumbani akiweka sawa mipango ya kanisa na
baba yao.
Hope.
Hope alipopata ujumbe kutoka kwa moja wa viongozi waliokuwa
wakitumika pamoja, akiulizwa mbona ametolewa kwenye makundi yote ya viongozi,
alishindwa kujibu. Akakimbilia kuthibitisha. Akakuta kweli ametolewa.
Aliumia akashindwa kujizuia ila machozi. Alilia kwa uchungu, asijue kama ni
majuto au kuona pengo lake linazibwa kirahisi kwa kiasi hicho!
Mtoto Hakui Kwa Baba.
Wakaona Junior haondoki. Kama mwenye jambo anataka
kuzungumza, ila hakuna mazingira sahihi. Mama yake aliposoma hiyo hali, akajua anataka
kuzungumza na baba yake. Akamfanya Noah aondoke na yeye akaaga kuwa ndio
anakwenda kulala. Akabaki na baba yake.
Akamuona ameinama anafikiria kama anayetafuta kwa kuanzia.
Mzee kimya. Akijua ni mambo ya Hope tu. “Labda niombe radhi kwa kuingilia mambo
ya kanisani nikiyahusisha na mambo yangu binafsi.” Akaanza, mzee kimya
akimtizama. “Nimejisahau kama mbali ya kuwa Hope ni mchumba wangu, pia ni
mtumishi wa Mungu na anatenda kazi na sisi. Jinsi unavyoongoza kondoo
wako, sikupaswa kuingilia. Lakini baba, jua mimi natafuta mke sio
katibu.” Mzee akacheka.
“Kweli baba. Nataka mke wangu mimi sio katibu wa kanisa
lako. Natambua juhudi za Hope kanisani, lakini pia nimegundua tunatatizo kwenye
mahusiano yetu. Inawezekana ni msingi mbovu tulioanza naye, lakini sipo tayari
kuingia naye kwenye ndoa akiwa hivyo alivyo. Hapana baba. Nitakuwa na maisha ya
shida, ambayo nitakuwa nimejitakia tu bila sababu! Kwa jinsi alivyo sasahivi,
pengine anaweza faa kwa mwingine, lakini sio mimi baba. Nina vitu vyangu vidogovidogo
sana, ni kama nilivisahau, lakini kwenye harusi ya Ester ndio kama nimekumbushwa.
Nini nataka na ndoa si majaribisho, ni halisi.”
“Kwa hiyo ndio maana nimechukua hatua moja nyuma, ili nione
kama tutaweza kuona nafasi zetu kwenye kila maisha ya mmoja wetu bila majukumu
au kukiwa na majukumu mengine ila bado sisi tuwe pamoja. Utakachofanya na Hope
kuanzia sasa, sitakuingilia. Ila naomba iwe kama mchungaji kwa
kondoo wake, sio baba mkwe. Hapo nitakujulisha baadaye. Ni hilo tu.”
“Sawa. Naruhusiwa kushauri?” Junior akabaki kimya.
“Junior?” “Naomba katika hili nipate nafasi ya kuweka sawa
mimi mwenyewe baba, bila shindikizo.” Akajua amekasirika. “Ni ushauri na
sitakushindikiza.” Junior akasita kama ambaye hataki. “Junior?” Baba yake
akasisitiza, mwishoe akakubali. “Sawa baba.” “Kuwa makini. Kuwa makini sana na
ujue mahusiano yeyote yale hujengwa. Chochote unachotaka kukiona kwa
Hope na hakipo, unayo nafasi ya kukijenga.” “Mbona mimi nimeishi naye kwa
vitendo, baba? Nimempenda kwa vitendo na sijawahi kumpuuza katika chochote.
Ulitaka nifanye nini?!”
“Cha kwanza najua umekasirika.” “Sijasirika ila..” “Junior. Umekasirika.”
Akatulia. “Na mabadiliko si ya siku moja. Ni afadhali wewe umegundua hivyo
mapema, na unanafasi ya kuweka sawa. Sikupingi kwa unachotaka kufanya. Fanya
kabisa ili kuweka msingi wa kile unachotaka kukiona kwenye ndoa yako. Narudia
ni msingi. Si yote utaona yanakwenda sawa kwa haraka. Itachukua muda, lakini
itakuwa safari inayoelekea kwenye ukamilifu.”
“Hili niliwaambia wewe na Ezra. Ndoa
ni kamilifu sana. Imewekwa au ni taasisi iliyoanzisha na Aliye Mkamilifu sana.
Ubaya, inaingiwa na watu wasio
wakamilifu. Wote mkishajua hilo, ndio mnaanzia kujengea kuanzia hapo, na ikiwa
msingi ni Yesu, itakuwa rahisi sana. Hutakaa ukapata aliye mkamilifu.”
“Mimi sitaki aliyemkamilifu.” Baba yake akabaki akimtizama.
“Sijasema nataka mkamilifu baba! Nataka mke wangu mimi.” “Na
mimi sijakataa. Na wala sikulazimishi umuoe Hope. Na hili niliwaambia wewe na
Ezra tokea vijana wadogo sana. Sitamtafutia mtu mke, kila mtu
atawajibika katika hili. Ila nasisitiza, umekasirika na moyo wenye
hasira hauna nafasi ya msamaha. Unanielewa Junior.” “Ndio baba.” “Kuanzia hapa
sasahivi, lazima ujiambie hutapata mtu aliye sahihi, na watu hukosea.
Unawajibika kusamehe. Lazima kusamehe. Hapo huna jinsi. Samehe kwanza
ndipo akili yako itaweza kufikiria hatua ya pili. Bila hivyo, utakaa sana hapo
na wewe na mwenzio hamtaoa kwa haraka.”
“Mimi nimemruhusu Ezra aendelee na taratibu zake. Na aoe tu.
Asinisubiri na nimemuahidi kusimama naye mpaka mwisho. Hata pete ya
Jelini nimemsindikiza kutafuta.” “Akakubali?” Kimya. “Junior?” Kimya. “Sasa
usikae hapo kwenye hasira, mkazidi kuchelewa. Cha kwanza wewe huna uzoefu
wa kukasirika Junior. Hujui kukasirika na kuweza kutenda sawasawa.
Hasira haijawahi kuwa sehemu yako tokea mtoto mdogo, ndivyo ulivyoumbwa.
Hujui kukasirika. Sasa usishikilie hapo, utaharibu vibaya sana. Usisahau
umeshikilia hatima ya ndoa mbili, sio moja tu. Utamyumbisha sana Ezra,
kama hutaweka mambo yako sawa. Umenielewa?” “Nimeelewa baba.” “Usiku mwema.”
Mzee akasimama, Junior ndio akajua anatakiwa aondoke, milango ifungwe.
Akaondoka.
Mioyo Inayoingia Kwenye Vitu Sahihi, Lakini Ikiwa Imebeba Majeraha
Na Kumbukumbu Za Maumivu.
Yeye akiwa amejawa furaha ya mipango yake kwenda vizuri,
wazazi wakiwa na baraka zote na kusimama naye kwenye kila jambo kufanikisha
kila jambo tena kifanisi, lakini akakuta na Jelini aliyekuwa akimsubiria ila
kwa wasiwasi sana. Alimtumia tu ujumbe kuwa amefika, akatoka kwa haraka bila ya
kuchelewa. Akamfuata mpaka garini. Akamsalimia kwa kunyongea, na yeye akapatwa
wasiwasi.
“Huyu ni Colins tu. Ndio kuachwa huku!” Akawaza Ezra. Hofu
ya ajabu ikamuingia, ila akajikaza. “Upo mzima?” “Nipo mzima. Pole na
majukumu.” “Asante. Nimekuletea chakula. Ingia ndani ya gari ule.” Alikuwa
amesimama dirishani kama ambaye alishasahau utaratibu wao.
Akainama hapo dirishani kama ambaye anasita. “Ni nini
Jelini?!” “Nilijua huji tena. Hivi nimebakia wa mwisho
nikijituliza pengine hata utakumbuka kunitumia ujumbe kuniambia
kulikoni, lakini kimya! Nilijua huji tena Ezra.” Ndio Ezra kugutuka na
kuangalia saa, akashituka kuona mishale yake ya saa inasoma saa 4:30 usiku. Alishituka,
hakuamini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Maana huko alikotoka aliacha kumechangamka haswa. Kama bado
ni mapema sana wakifurahia kupata kwake mchumba. Asijue ni kweli aliwahi kutoka
kazini ili asikae sana nyumbani asimchelewe Jelini, lakini alipofika kwao, hapo
ndipo alipopoteza ramani nzima. Vilijaa vicheko. Mama mchungaji hajui kupunja
meza, zaidi akisikia hao wawili wanakwenda kula nyumbani. Kukawa na kula na kuongeza
tena na tena haswa kutaka kumfurahisha mama yao. Anaondoka kwa kukimbia,
asiangalie hata simu akijua mida hiyo Jelini yupo busy na wateja, kumbe
alishapoteza muda mwingi tu. Na biashara ilishafungwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Samahani sana Jelini. Tafadhali usilie. Samahani sana.”
Ikambidi ashuke kabisa garini akirudisha mawazo pale na kuangalia mazingira.
Palishaanza kutulia kwenye hilo eneo la biashara na maduka mengi yalishafungwa
likiwepo na la Jelini ila walinzi na vijana waliokuwa wakitumia hapo kwa malazi
na makazi, walishajongea vibarazani mwa maduka hayo ya biashara. Wengine
kumalizia siku yao kwa malazi maeneo hayo, na kwa walinzi kuanza kazi.
“Kikao nyumbani kimevuta sana. Hapa nimeondoka kwa
kulazimishia tu. Hata Junior nimemuacha huko. Tafadhali nisamehe.” “Hamna shida. Nahisi sasa hivi naanza kuelewa. Sema
niliingiwa hofu! Ila sikulaumu. Ni vile kwanza hujawahi kuchelewa hata mara
moja. Na uliniahidi mimi nitakua dharula yako ya kwanza, Ezra. Sasa nikajiambia
hata kama kuna jambo na vile nakufahamu wewe ni mtu wa mawasiliano, basi
ungenijulisha, au hata kujibu jumbe zangu, usingekuwa kimya. Ndio maana nikajua
pengine umeamua ku…” Akasita alichokuwa akitaka kumalizia akijifuta
machozi.
Ezra akajua ameharibu na amekua kinyume na msimamo wake hata
maneno. Mbaya zaidi hata hizo jumbe anazozungumzia Jelini hakuwa ameona
kabisa. Ndio anasikia hapo kama kuna jumbe zilitumwa. Alipigwa na baridi kali,
taarifa nyingi kwa wakati mmoja zilikikuwa zikiendelea kichwani mwake.
“Acha nikapumzike Ezra. Usiku mwema.” “Tafadhali usiondoke
Jelini. Nimekuletea chakula. Tafadhali ingia garini ule kabla hujaondoka, na
tuzungumze.” “Sina uwezo wa kukaa. Hata hapo dukani
nilikuwa nimesimama, nikikusubiria. Nafikiri sababu ya hofu nimeanza siku zangu
gafla na sikuwa nimejiandaa kabisa, na nilikuwa nikishindwa kuondoka, nikihofia
pengine unaweza kuja na kunikosa.” Ezra akazidi kuishiwa nguvu.
“Nitakapokaa popote, nitachafua. Acha nikaoge
nipumzike.”
“Samahani sana Jelini.” “Usijali Ezra. Nafikiri si
wewe, ila mimi mwenyewe. Na naona kweli kuna mambo inabidi niyafikirie zaidi na
kujirekebisha. Inawezekana kweli nakimbiza kitu ambacho hakipo. Natafuta kitu
ambacho kwa uhalisia ni kama sitakipata.” “Jelini!” “Si wewe Ezra. Hakika si wewe. Wananiambia nina waza
kitoto. Nataka vitu visivyokuwepo. Naanza kuamini. Hata niliokuwa nikiwalaumu,
nakuona hawafai, inawezekana hawakuwa na kosa kama nilivyodhania ila maisha
ndivyo yalivyo.” Akajua siku hiyo na Colins amekumbukwa kwamba hakuwa na
kosa ni kama hivyo tu.
“Hata huko nilikokuwa nimechelewa, ilikuwa ni kwa ajili yako,
Jelini. Naandaa kitu cha kukufurahisha wewe mpenzi wangu.” Alibanwa, mpaka
akaanza kutoa mipango ya surprise. “Furaha
yangu haijawahi kukamilishwa na vitu, Ezra. Ila mtu. Mawasiliano kati
yetu ndio furaha yangu wala tatizo hapa si kuwepo hapa usiku huu tena kwa
wakati. Na hili nilikuomba ramsi Ezra. Mwanzoni kabisa. Ukishindwa kitu, si tatizo.
Ila nitaarifu, usiniache nikikusubiria, tena na kushindwa hata kujibu jumbe zangu!
Sina kitu nahitaji cha muhimu na maana kama mtu mwenyewe. Usiku mwema Ezra.
Acha nikaoge, nilale.” Akajua akisema hakuona jumbe, ndio ataharibu
zaidi.
“Nakupenda Jelini. Nakupenda sana.” Jelini akabaki kimya
akiendela kujifuta machozi, na hapo amesimama mbali kidogo na alipo Ezra. Ni
kama alimkwepa wakati anashuka garini kama hata asimguse. “Nimekosa Jelini.
Tafadhali naomba unisamehe. Sijui nimetingwa vipi, nikashindwa kuangalia simu.
Hapa nilikuwa nikiendesha akili zote zipo kwako. Kukufikia na kukuona wewe
mpenzi wangu. Sikukusudia kukuumiza ila kukufurahisha.” “Nashukuru Ezra. Usiku mwema.” Akaondoka na kuelekea kwenye
gari yake.
Akamuona anatandika vitu kadhaa kwenye kiti cha dereva kabla
hajakaa. Akamkimbilia. “Nikusaidie?” “Nafikiri kwa sasa nipo sawa. Asante.” “Na
ile zawadi yangu?” Akamuwahi kabla hajaondoka ili kujaribu kubadili ile hali
pale. Kimya kama hajasikia. “Jelini?” “Haina maana tena, Ezra.” “Kwangu
inamaana. Maana nilikuwa nikiisubiria kwa hamu.” “Imeharibika. Haitafaa tena.
Usiku mwema.” Akapanda garini na kumuacha Ezra amesimama nje ya gari ameduaa.
Mipango ya kuchumbia imekamilika, ila hana uhakika na mchumba. Alibaki
amesimama hapo miguu ikishindwa hata kunyanyuka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa hakika
usiku huo sivyo alivyodhania ungeishia kwa staili hiyo.
Alikuwa na
ahadi ya kupokea zawadi nzuri, ila sana.
Alijua na
usiku huo atamuweka mikononi, apate na kiss. Lakini ndio ikaishia hivyo, bila
ya kutarajia!
Ni Nini
Kitaendelea?
USIPITWE.
0 Comments:
Post a Comment