Sasa kuona na mkwe amekubali ajitoe kanisani, hofu
ikamuingia. Kama na wakwe nao wanamtema, kweli kuna ndoa hapo! Tayari
siku yake ikaharibika. Ikawa bora lawama, kuliko fedheha. Inamaana
kanisa zima sasa litajua hana tena cheo kwenye kanisa la baba mkwe! Akazidi
kuvurugukiwa maana hicho nacho pia kilimpa kiburi hata hapo kanisani, akaweza kuenea
kote na kwa wote akijulikana ameshika nafasi kubwa ya kanisa kubwa kama hilo na
ni mtoto wa nyumbani.
Kulikobaki Mpini Wa Mapenzi.
Ezra akamuacha kidogo kama atulie, kisha akamuuliza. “Tafadhali
naomba kujua unachokifikiria juu ya Hope. Maana mimi nakujua Junior. Zoezi la
kuchumbia ulishafunga na hukuwa ukitaka kuanza tena. Ni nini
kinaendelea?” “Jana wakati mume wa Ester akila kile kiapo alichomtengenezea
Ester, pale mbele ya umati, ilinifanya nifikirie sana Ezra na aliyoyafanya Hope
jana kama kuchorea mstari majibu yanayo niogopesha. Ulitilia maanani kile kiapo
cha Devin?” Akataka kujua.
“Nilisikiliza. Ila kumbuka hawa watu wawili, Ester na Devin wametoka mbali sana
Junior! Halafu ni Ester. Ni mwanaume mjinga tu na mpumbavu ndiye atakayeshindwa
kujua kama amebahatika kupata mwanamke kama Ester!”
“Sawa. Lakini katika yote, mimi imenibidi nifikirie Ezra. Baada
ya sisi kula na kunywa pale kifahari, hawa watu wawili wanakwenda kujifungia
mahali kwa siku 7! Hizo siku 7 ni msingi wa siku nyingi sana za peke yao mpaka
kifo.”
“Unakumbuka kitu aliwaambia Jelini?” Ezra akatulia. “Kwamba
wanaonekana wanapendana. Ester anafuraha mpaka inaonyesha usoni.”
“Huwezi mfananisha Hope na Ester, Junior! Au nyinyi na wao! Na wewe unajua.
Hope amekukuta na kila kitu, Ester na Devin wameanzana zamani sana. Na Ester alikataa
kila mwanaume, akimsubiria Devin bila kuchoka!” “Sasa hayo ndiyo yamenifanya
nifikirie tulicho nacho na Hope! Tukiwa peke yetu. Mimi na yeye. Hakuna kanisa
la mzee na hakuna mipango anayopenda yeye kuisimamia. Tumebaki sisi wawili tu,
tunafanyaje?” Kimya Ezra akijaribu na yeye kufikiria.
“Ndio nikagundua HATUNA. Ni kama tunaunganishwa na majukumu
tu! Muda mwingi tunazungumzia kufanikisha mambo ya watu na
si yetu! Sasa inawezekana ni kwa sababu yetu yamekaa vizuri! Sijui! Au pengine
tuna msingi mbovu.” Akaendelea bila jazba.
“Na kama unaona kujifananisha sisi na kina
Ester ni mbali sana, basi acha nijifananishe na wewe na Jelini. Mbona
anakufuata mpaka usiku, eti hataki ulale na uchungu moyoni. Anang’ang’ania
mjenge ‘chenu’, huku hakufahamu kabisa pesa uliyo nayo!” Ezra kimya. “Sema
Ezra? Niambie kama wewe hujashangazwa na kitendo cha Jelini eti anakukimbilia
na kukung’ang’ania hivyo, kumbe mpaka jana hakuwa akijua kama una mali
hivi! Yaani ni kukupenda tu wewe! Yupo tayari kudhalilishwa na Hope, bado
anabaki na wewe, bila kinyongo! Anasema atatafuta jinsi ya kuishi naye.
Ili kwanza mimi na wewe tusigombane, na nyinyi mbaki pamoja!
Kweli Ezra? Si wote hawa wanawake wametukuta watu wazima tu? Jelini hakujui
wewe ni nani, Hope alinijua mimi hata kabla sijamchumbia! Sasa unataka kusema
nini?” Ezra kimya.
“Hakika imenifanya nifikirie mara mbilimbili. Au si kweli
kama kwa muda wote, Jelini hakuwa akijua kama una nyumba kama ile!” “Mungu ni
shahidi, alishituka sana, tena mpaka ikabidi nimtulize kwa kucheka kwa jinsi
alivyokuwa ameishiwa nguvu.”
“Hope haniheshimu Ezra.” “Sidhani kama ni hatokukuheshimu.”
“Basi hatuna kitu chetu. Hata upendo wetu sisi wenyewe wawili
sidhani kama upo wa dhati. Sidhani kama tumeunganishwa na mapenzi ya dhati.
Ndio maana nimefikiria na kutaka achukue hatua chache nyuma. Bila hayo majukumu
yote au pesa yangu. Abakiwe na sisi tu, nione kama anaweza kujenga chetu.
Lakini mpaka sasa hana, na nasikitika ni kama amekosa sababu.”
“Sasa, sitaki ajione ana vitu vingi sana. Nikimaanisha mali,
akasahau watu na utu. Ni kweli sitaki kuanza upya kwenye swala la uchumba. Ningependa
kuendelea na Hope, lakini sipo tayari kumuoa alivyo. Hapana Ezra! Sina
sababu ya kufanya hivyo. Nampa nafasi ya mwisho. Aitafute nafasi yake
kwenye maisha yangu, kwa kuwa mimi naijua nafasi yangu kwake na nimeisimamia
kwa uaminifu sana, na sijazembea. Akishindwa kuipata nafasi yake.
Akang’ang’ania kuwa juu hivihivi, BASI.” “Junior!”
“Hakika Ezra, sikutanii. Na mimi nataka mwanamke
atakayenipenda na kuniheshimu! Kwa nini nijiingize sehemu itakayoninyima raha
kwenye maisha yangu yote ya hapa duniani! HAPANA! Kama atashindwa kujishusha.
Akang’ang’ania kuwa juu, hakika basi.”
“Kama hichi alichokifanya leo, sijakifurahia hata
kidogo. Mimi ninapofanya mambo yangu huwa namshirikisha tena anapata nafasi ya
kushauri. Tena kama unavyomjua Hope, anakua king’ang’anizi akitaka yeye ndio ashinde
hata kwenye mambo yangu! Leo anaacha nafasi kubwa hivi, inayo heshimiwa, na
anajua anategemewa, kweli anamtaarifu baba yangu kwa barua pepe! Kana kwamba
hatambui umuhimu wa hiyo nafasi, eti anamwambia ni kuanzia leo! Heshima
ya wapi hiyo, Ezra?!”
“Anategemewa majukumu mazito aliyoaminiwa nayo, nani
ayafanye kama si kutaka kuadhibu wazazi wangu na mimi, kwa sababu ya kumuhoji
jana? Anatukomoa, akidhani tutashindwa! Anasahau ile ni kazi ni ya Mungu
wala si ya mzee! Hata mzee akifa leo, ile kazi itaendelea tu. Acha tuone kama
baada ya yote, sisi tutabaki tumesimama. Mwache tu.” Ezra akapoa kabisa,
akabaki akitafakari.
“Na naomba usimtafute kuzungumza naye.” Akawa kama amesoma
mawazo yake. “Umepatwa na nini Junior?!” “Wewe hudhani sistaili kama ulichopata
wewe? Mtu wa kukuhitaji wewe kama wewe?” “Unastahili Junior. Lakini si kwamba
mimi na Jelini tutakuwa bila matatizo. Itatupasa tuzungumze na kurekebishana
ili tuwe ukurasa mmoja.” “Ewaah! Iwe anataka yeye na si wewe kumuwekea kwenye
akili yake. Mimi nataka kuhitajiwa wala sihitaji mtu mkamilifu.
Maana na mimi si mkamilifu. Ila nataka mtu atakayenitaka mimi kama mimi
na akubali tutembee pamoja na kufanya hicho unachozungumza. Sitaki kuuziwa
mbuzi kwenye gunia. Tafadhali Ezra.” “Nakuahidi sitaingilia. Nitafanya kama
ulivyofanya kwangu na Jelini. Atakaponitafuta, ndio nitazungumza naye.” “Na
tafadhali ibakie hivyo. Akikutafuta. Akaonyesha anahitaji mahusiano na
mimi, hapo sawa.” “Sawa.” Ikabidi Ezra awe mpole.
Aluta.
Wakiwa katikati ya kazi, mida ya saa nne asubuhi hiyohiyo
ujumbe ukaingia. ‘Baada ya kazi naomba mpitie nyumbani,
tujipange swala la Jelini. Nataka tumalize taratibu za awali kabla sijasimama
jumapili kuhubiri pale madhabahuni. Ili maswali yote ya jana, yajijibu yenyewe.
Nisibakiwe kuhubiri habari za uchumba wenu.’ Ezra
aliposoma akacheka na kutingisha kichwa.
“Ni nini?” “Mimi naona usome mwenyewe.” Akamrushia simu
yake. Junior akasoma na kucheka. “Mzee anataka uchumbie.” “Nimemuelewa. Sasa
pete!” “Unajua size yake? Maana kwa kuzipata sio tatizo.” “Itakuwa kazi
ya leo. Nitajitahidi kumchunguza mpaka nijue.” Akamuona anahamasika.
“Nini?” “Hebu fikiria maisha yangu Junior. Yaani ndio
nabahatika kila siku kuamka pembeni ya Jelini!” “Itakua Ezra. Jelini anakupenda
na anakiri kukuhitaji. Na inaonekana hata kwao wamekukubali. Sioni sababu
yakutokuwa. Na najua mama anaandaa mazingira ya kuja kumkaribisha tena kwenye
familia, ili kutengeneza palipoharibika jana na kutambulisha familia yetu rasmi
kwake na kwao.” Ezra akabaki akifikiria na kurudisha majibu kwa mchungaji. ‘Tutakuwa hapo mzee wangu na asante sana.’ Kisha akapiga
simu kuomba atengenezewe matunda. Kwamba saa 5 atayapitia akiwa anakwenda kwa
Jelini.
Penzi Kikohozi.
Mara akaona simu ya Jelini inaingia ila kwa video.
Alifurahi, karibia asimame, Junior akimwangalia tu. Akapokea. “Upo busy? Sitaki kukusumbua mida ya kazi.” “Nimefurahi
kukuona Jelini! Umependeza sana. Unakwenda wapi!?” “Asante. Nasaka pesa
mwenzio. Naenda kumbembeleza mwenye saluni moja maeneo ya Posta, anipe kazi
yakumpelekea bidhaa zaidi. Alinipa kazi ndogo, lakini nimemfikiria, nimeona
naweza kufanya naye biashara kubwa zaidi.” “Unaakili ya biashara wewe?” Akamuona
anacheka na kushukuru.
“Nimekumiss mpenzi wangu. Nikasema nikusalimie kwa
kukuona. Japo tumeshasalimiana kwa jumbe za asubuhi.” “Nimefurahi kukuona
Jelini. Na asante. Na ujue hunisumbui hata kidogo. Muda na wakati wowote ule,
ukiwa na nafasi uwe ukinipigia.” “Nitafanya hivyo. Na nina zawadi yako nzuriii.
Usiku si tutaonana?” “Lazima. Au unaratiba ingine?” “Sisi kwanza. Na
wewe ndio ratiba yangu ya kwanza.” Ezra akacheka na kuona atoke tu hapo
asimkere Junior.
“Nakupenda Jelini.” “Mimi mwenyewe nakupenda. Ila
sema mimi nakupenda sanaaa.” Ezra mfanyakazi wa mshahara kama anavyojiita mwenyewe,
akaenda kutulia nje ya ofisi, BOT mjengoni, akifanya ya kimapenzi na si kazi.
Wakapanga kukutana kabla hajarudi dukani kwake, hapohapo mjini, kisha akarudi
ofisini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya saa sita Jelini akampigia Ezra kuwa amemaliza,
anakwenda kumsubiria maeneo ya Ocean Road, upande wa baharini karibu na
hospitali ya Agakhani. Nusu Ezra aruke. Maana ilikuwa sehemu sahihi. Akapitia
matunda kwenye hiyo restaurant wanayo mtengenezeaga, akakimbilia
kumfuata Jelini.
Akamkuta akimsubiria garini kwake ila ameshusha vioo na gari
kazima. Jelini alifurahi huyo kama ambaye ameona nini sijui! Ezra akamdaka
midomo akiwa amesimama dirishani. Wakabadilishana ndimi kwa muda tu, kisha
akamuachia. “Nilikuwa sina uhakika kama utanikiss tena!” Ezra alicheka
sana. “Mimi nilijua ni jana tu!” “Na leo.” Jelini akacheka, akashuka garini.
Ezra akamdaka mkono, akaungalia kwa makini, akaubusu na
kubaki ameushikilia kwa kupitanisha vidole vyao. Jelini akidhania ni mapenzi
kumbe mwenzie yupo na agenda yake. “Nimefurahi umenipigia simu kwa video. Na
mimi nilishakuwa na hamu na wewe.” “Kweli Ezra? Maana najua upo busy.”
“Sio sana kushindwa kukupa wewe muda. Nikitingwa nitakwambia. Ila usiache
kunitafuta ukihofia ubusy.” “Sawa. Ila usiku usihangaike chakula. Mimi
nitaagiza.” “Hapana Jelini. Tulia kazini, mimi nitatafuta chakula. Mida hiyo
wewe unakua busy wakati mimi nakuwa nilishatoka kazini, sina chakufanya.”
“Kwanza nahisi nitakuletea chakula kutoka nyumbani. Maana
leo tukitoka kazini tunapitia nyumbani kwa mzee. Najua mama lazima ataanda meza
nzuri na kubwa. Huwa anapenda sana tukienda nyumbani. Kwa hiyo nitakubebea na
wewe. Au unataka kitu maalumu?” “Mwenzio huwa si mchaguzi wa vyakula. Nitakula
utakachokula wewe.” Ezra akacheka akimwangalia.
“Nikuulize kitu, Jelini?” Jelini akaingiwa na wasiwasi maana
alishaongeza heshima kwa huyo Ezra. “Juu ya nini!?” “Sio kitu kibaya bwana!
Acha woga.” Akamtuliza. “Umeshafikiria maisha yetu? Angalau tu kupita akilini
mwako.” “Nakufikiria Ezra. Nakufikiria sana. Ndio maana nimeamka tu na
kuangalia simu kama umenitafuta na ndio nikakutumia ujumbe na wewe.” Ikawa kama
anajitetea tena.
“Hapana Jelini. Namaanisha maisha yetu. Tukiwa tunaishi
pamoja.” Jelini akacheka na kuinama akifikiria. “Eti Jelini? Ushawahi hata
kufikiria?” “Ni kwambie ukweli?” “Ndio ningefurahi.” “Kidogo umenitisha Ezra.
Mimi sikukujua kwa wadhifa huu. Kwa hiyo Ezra niliyekuwa naye kwenye picha ni
Ezra wa kawaida ambaye hata mambo yake ni kawaida sana. Nikajipatia picha hivyo
unavyonipenda, eti ndio nitakuwa nikiishi na wewe kwa maisha yetu ya kawaida
yasiyo na mambo mengi.” Ezra akawa kama hujampata vizuri.
"Ukiwa unamaanisha nini!?” “Mimi sijasoma sana Ezra. Na huo
ni ukweli. Nimeishia kidato cha pili, nikiwa na elimu ya mpaka kidato cha
kwanza. Sikujua kama wewe ni mtu uliyesoma kwa kiwango hicho na kufanya kazi
kubwa hivyo!” Ezra akacheka ila akiwa na swali. “Kabla hujamalizia wasiwasi
wako, naomba uongeze kwenye maelezo yako, aina ya kazi uliyodhania
nafanya.” Jelini akazidi kubabaika.
“Niambie tu usiwe nawasiwasi.” “Unakumbuka jinsi
tunavyokutana mida ya mchana? Unakuwa smart sana. Huvai koti la suti,
lakini nadhifu sana na unakua wakati mwingine na tai kabisa au unakua
unaonekana wazi umetoa tai muda si mrefu. Nikajua wewe ni misheni town.”
Ezra alicheka. Akacheka mpaka machozi.
“Bwana acha kucheka!” “Subiri kwanza Jelini. Ndio nakuwa
nafanya nini?” “Unafanya kwenye ofisi za watu, unatumwa hiki na kile. Karatasi
hii peleka benki hii, bandarini, TRA ilimradi kukamilisha mipango ya ofisi ya
mtu.” Ezra akacheka kwa kutulia akifikiria. “Ezra wewe ni mtulivu sana,
rahisi kukufikiria hivyo. Maana wengi niliokutana nao mimi ambao pengine
wanakaribia tu nafasi zako, hata hawajakufikia hapo ulipo, mwanzoni sana,
utawajua kama wamesoma na wananafasi kubwa kimaisha.”
“Sasa kukutana na wewe. Huzungumzii unachofanya. Huonekani
kama una shule yakueleweka kwa kiwango hicho, hakika wewe na Junior
nikawachukulia poa.” “Sasa mbona kama hiki ni kitu kizuri?” Bado Ezra hakuona
tatizo.
“Si kwa upande niliosimama mimi, huku. Nishakutana na
wanaume wasomi na wenye pesa. Wao wenyewe, na wanao wazunguka walinionyesha
kwa vitendo na maneno, siwastahili sababu mimi sijasoma. Kwa kina
Colins ndio ilikuwa waziwazi kabisa. Walinifuata mpaka nyumbani kwetu. Mbele ya mama yangu na mwanangu, wakaniambia kijana wao
hawezi kuoa msichana kama wa aina yangu. Wakitaja shule na maendeleo ni
moja ya vigezo ambavyo mimi sikuwa navyo.” “Acha kulia Jelini. Tafadhali
usilie. Pole.”
“Iliniumiza Ezra. Iliniumiza sana. Mbele ya
mwanangu! Sasa kwako nikaona hicho kipengele sitakuwa nacho. Kuja kusikia tena
na wewe ni walewale na una mjengo kama wa Junior! Na vile Hope uliyeniambia
amesoma vizuri, kuja kunitambua kwa kudharau ninachokifanya!” Ezra akashituka
akajikaza. “Mimi nishaanza kujishuku. Naona
historia inajirudia. Narudi kulekule kwa walewale!” “Hivi
ujue Jelini kwako sijakurupuka?” Akamuuliza akimfuta machozi.
“Nilikufuata nikiwa nakufahamu kwa asilimia kubwa sana
zilizoniridhisha kuwa utanifaa mimi. Na kabla hujauliza nilikufahamia wapi, jua
huko vyuoni nilikopita, nilisoma na wasichana warembo tu. Hapo kazini kwetu,
wapo wasichana ambao bado hawajaolewa. Inamaana na wenyewe wamesoma, au wana uwezo
wa kunikaribia mimi. Nikimaanisha kwa sababu sisi pale kazini tumeshakaa muda
mrefu, hata vyeo vimeongezeka. Kwa kuwa hata shahada ya pili tumesoma tukiwa
kazini. Kwa hiyo tupo kwenye nafasi za juu kwa sababu tupo pale muda mrefu.
Nikimaanisha wapo na wanaajiriwa binti wadogo tu mpaka sasa. Lakini mbona
nilikusubiria wewe?” Jelini akakunja uso.
“Unakumbuka ulianza kunikimbia kila unaponiona?” Jelini
akacheka akiendelea kujifuta machozi. “Umeshajiuliza ni kwa nini nilirudi tena
kwako?” Akapandisha mabega kukataa kama anayesema hajui. “Kwa sababu
nilikupenda Jelini. Na nimekuchagua wewe hivyo ulivyo. Sijakurupuka. Nakuletea
chakula pale kazini kwako na ukakikataa, ukisema hutaki kilete picha ya
hongo, hilo nalo likanivutia zaidi japo nilitamani ukipokee kile chakula.
Ikaniongezea moyo wa kukusubiri. Kwa hiyo jua upo na mtu anayekufahamu. Amekuchagua
wewe. Na Ezra anakutaka wewe akiwa anakujua na sina mpango wa
kubadilisha chochote kwenye maisha yako.”
“Hivyo ulivyo nakutaka wewe. Na jumla yako yote.
Umenielewa?” “Kwa hiyo kumbe tena una shahada zaidi ya moja!?” Ezra alicheka
sana. “Kumbe nazidi kuharibu si kutengeneza?” “Bwana
wewe umesoma sana bwana Ezra!” “Basi acha kuangali nilivyo navyo ila
mwanaume uliyempenda tokea mwanzo. Jua hayo mengine yatatusaidia
maishani. Ni ziada tu. Kwamba familia yetu itakuwa imebarikiwa zaidi. Kuna
mfanyakazi na mfanyabiashara. Tutakuwa na maisha mazuri. Hapo vipi?”
“Sasa mbona husemi kama utakuwa ukinikumbatia!?” Ezra
alicheka sana. “Bwana Jelini wewe mahitaji yako madogo sana! Wenzio wakijua
mchumba anapesa, wanaanza kuomba magari! Wewe unataka mikono tu?” “Na
kulala nikiwa nimekumbatiwa usiku mpaka asubuhi.” Ezra alicheka hana mbavu.
“Na nini tena?” “Usiache kunijali Ezra. Wewe unanijali sana
Ezra, mpaka nabaki nikikuwaza wewe kila wakati! Usije badilika. Hata
tukizaa watoto wengi namna gani, usinisahau mimi.” “Kumbe unaona mpaka
watoto wetu? Wangapi?” Jelini akaanza kucheka. “Ni wengi sana Ezra. Inabidi
kutafuta uzazi wa mpango.” Ezra hana mbavu. “Tuishie watatu tu?” Ezra
akamuuliza akicheka. “Mimi naona watatu watoshe bwana! Wengine tuwaachie
wengine.” “Nimelikubali wazo lako. Kwa hiyo jumla tutakuwa na watoto wanne,
pamoja na Jeremy?” Akamuona anapoa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mama hataki naye. Amesema mimi nitaondoka mle ndani lakini
si Jeremy. Ujue nilimzaa Jeremy nikiwa mdogo sana.” “Uliniambia.” “Halafu
nilimzaa nikiwa na uchungu. Nilikuwa sijui kitu chakufanya, mama akamchukua
tokea siku namzaa. Yaani mimi nimemzaa, nalia
siku ile pale leba, si kwa maumivu ya kujifungua bali sijui kitu
chakufanya naye huyo mtoto. Nimetolewa, naambiwa nirudi wodini, nalia
kwa hofu. Lakini nilipotoka nikakuta bado mama ananisubiria nje, amemtuma Jema
akaniletee uji na supu. Sitasahau ile siku. Nilikuwa nalia, nina hofu na mtoto
mkononi.” Akamfuta machozi.
“Niliporudi tu wodini, mama akamchukua Jeremy
kutoka kwenye mikono yangu. Akamfunika vizuri maana nilikuwa nalia, wala sijui
chakufanya. Basi, akatusaidia mimi na mwanangu, ndio nikaanza kutulia. Ila ule
uchungu haukuwa umeisha Ezra. Nilikuwa naumia naona nimepokonya utoto
wangu nikiwa sipo tayari kukua. Kufupisha habari ili urudi kazini, tokea siku
hiyo mama akaanza kumlea Jeremy, mimi nikatafuta kitu cha kunituliza. Pombe.”
“Nilipojua uwezo wa pombe. Kwamba ukinywa nyingi, kwa muda
huo uchungu unapotea, nikaanza kuinywa kila wakati. Ikiisha tu kichwani,
natafuta ingine bila kujali muda. Hivyo unavyomuona Noah, ndio ilikuwa maisha
yangu. Tena naona bora Noah yeye analewa na kurudi kanisani. Mimi nilikuwa nikishinda
baa. Sijui kula wala vaa ya Jeremy. Sijui uzima wake wala kuugua kwake. Sijui
hata lini alipewa chango, mbali ya zile za mwanzoni kabla sijajua pombe.
Nilimuachia mama moja kwa moja.”
“Sasa alivyokuja Colins, ikawa ni mwanaume wa kwanza na yeye
kuweka mipango mpaka ya Jeremy. Akitaka tukioana mpaka Jeremy atumie
jina lake. Ikanifanya nimlete karibu ya Jeremy. Akampenda sana, maana
alipenda anachokifanya Colins. Maswala ya puzzle, na Lego’s
wakawa ndio kitu chao kinawaunganisha, wakijenga pamoja. Ndio yakatokea
yakutokea, halafu Colins hakurudi tena, ikamuumiza sana Jeremy. Akabaki akipiga
picha kila puzzle au legos anazotengeneza, anataka mama mtunzie
hizo picha ili Colins akirudi amuonyeshe.”
“Ndio mama ameniapisha, mbele ya Jema, kuwa pale
nyumbani kwake ni kwa Jeremy. Hata akifa yeye leo, pale patabakia kwa
Jeremy na mimi nisiwahi kumyumbisha kwa wanaume. Anayemtaka Jeremy,
atakuwa akienda pale kumsalimia, basi. Yaani hata mimi nikihama pale,
amesema niondoke na mizigo yangu tu, ili yakinishinda huko, nirudi pale,
nitawakuta wao bila kumchanganya Jeremy. Amesema hakuna mwanaume wakumtoa
Jeremy pale. Hata akifa, asitolewe pale ili tusimyumbishe kwenye majumba
ya watu.” Ezra akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Tutakuwa sawa Jelini. Na ahadi ya kulala umekumbatiwa, ipo,
nakupa.” Jelini akacheka sana. “Usiku kucha utakuwa hapa.” Akimuonyeshea
kifuani. Jelini furaha kama yote! Cheko la deko njenje. “Ukichoka?”
“Tutabadilisha style za ulalaji mpaka papambazuke. Ila ukiwa mikononi mwangu.”
Akamuona ameridhika.
“Swali la mwisho kabla sijaondoka. Nani amekupa habari
zangu?” “Jibu jioni. Ila ujue huna haja ya kubadilika. Nilikupenda na
nakupenda hivyo ulivyo. Hope si sehemu ya maisha yetu. Habadilishi
mtazamo wangu kwako. Katika watu wangu muhimu, hakuna atakayekubugudhi na
kukutaka ubadilike. Ila ujue familia ya mchungaji ni waombaji sana. Hilo
watakulazimisha. Huwa wana mkesha wa maombi mara moja kwa mwezi unao ambatana
na mfungo, hiyo najua utakaribishwa.” “Hilo si tatizo.” Jelini akakubali
bila shida. “Basi kama ndio hivyo, mpaka hapo tupo sawa. Si ndio?” Akatingisha
kichwa kukubali.
“Sisi kwanza. Ezra kama Ezra, na Jelini kama Jelini, mengine
yote ni ziada na baraka zetu kutoka kwa Mungu. Mali na elimu havita tu define
sisi, ila sisi kama sisi. Sisi kwanza, mengine baadaye.” “Hapo sawa.” “Na mimi
si misheni town.” Jelini alicheka sana.
“Ila nyinyi wawili mmezidi bwana!” “Mwenzio imeniongezea
furaha, kuona umenikubali ukidhani nipo chini, hujanipendea mali. Maana
sasahivi ni ngumu kuoa Jelini, ngumu sana. Huwezi jua anayekupenda kwa
dhati au anayetaka kukutumia tu.” “Nakupenda Ezra.” “Najua. Tutazungumza vizuri
usiku. Acha nirudi kazini, na nimekuletea matunda.” Jelini akafurahia kana
kwamba amepewa alumasi. “Asante kujali Ezra. Asante sana. Na wewe nimekuletea
matunda.” Ezra hakutegemea.
Akafungua kwenye gari yake, kiti cha nyuma. Yalikuwa matunda
mengi tu. Ila yamepambwa maalumu kama zawadi. Kadi nzuri sana ya love,
na maua mekundu ya roses. Mazuri, fresh, yamefungwa pamoja. Yananukia!
“Kama Valentine!” Ezra mwenyewe akashangaa na
kushindwa kuamini. “Basi nikwambie, kwetu sisi, na mpenzi wangu Valentine
ni kila siku.” Hilo likamfurahisha sana Ezra, asiamini. Akaanza kupokea. “Mbona
mimi sikupi vikiwa vimefungwa vizuri hivi!” “Sio mashindano Ezra. Mwenyewe
ulisema. Halafu wewe unafanya zaidi yangu. Unaacha kazi, unapambana na foleni
kurudi mpaka kule Tegeta kutokea huku Posta, kuniletea mimi matunda! Hata
ungeyaleta kwenye mfuko hayajaoshwa pia ningekushukuru sana.” “Umejawa
shukurani Jelini!” Kisha akampa kiss ya kama dakika mbili hivi,
akamuachia.
“Asante sana, Jelini mpenzi wangu. Nimefurahi sana.”
“Na usifikiri hii ndio zawadi yako ya leo! Hapana. Mimi nimekuandalia zawadi
nzuriii. Ila sana.” “Mimi nilijua zawadi ndio hii!” “Hata kidogo. Jiandae
kufurahi sana usiku. Wewe sasahivi rudi kazini. Mkale hayo matunda na Junior.
Nimechukua matunda mengi na kuna uma mbili nikijua mtakula naye.” “Yalivyo
hivi, tutavuta nyuki ofisini kwetu.” Wakaagana, na kutawanyika.
Ofisini.
Junior mwenyewe alibaki ametoa macho wakati Ezra anaingia.
“Ni Valentine, kwamba nimesahau?” “Basi nikwambie, kwetu sisi, na mpenzi
wangu Valentine ni kila siku.” Junior akacheka sana jinsi
alivyozungumza. “Jelini huyo?” “Nani mwengine? ‘Na usifikiri hii ndio zawadi
yako ya leo! Hapana. Mimi nimekuandalia zawadi nzuriii. Ila sana’.” Junior hana
mbavu vile anavyomuigilizia. “Namuuliza unataka nini, maana aliingiwa hofu na
nafasi aliyojua ninayo kwenye maisha.” Ezra akamsimulia mazungumzo yao.
“Sasa alivyotulia nikamuuliza kama ameelewa. Yaani yeye
akaanza kushangazwa kwamba katika hayo maelezo yangu hakuna mpango wa kumkumbatia!”
Junior hana mbavu. “Jelini! Wenzake wakiona mchumba ana pesa wanaanza
mahitaji!” “Kama ulikuwepo! Nikamwambia hivyohivyo. Yeye anataka akumbatiwe na
ajaliwe yeye kwanza. Hata tukiwa na watoto wengi, yeye abakie wa kwanza.
Namuuliza kwani unaona tutakuwa na watoto wangapi? Anasema yeye ameona tuna
watoto wengi sana, inabidi tutumie uzazi wa mpango, tuachie wengine.” Junior
hana mbavu.
“Jelini! Amenipa hayo matunda na amesema kuna uma mbili
akitaka na wewe ule.” “Huyu ni wakukimbiza kanisani Ezra.” “Sasa naona
tunarudi nyuma Junior!” “Katika hili usinisubiri. Endelea tu. Ukicheza
tu, watakupora.” “Na alivyo mzuri! Leo yenyewe amenibabaisha. Jelini ni mzuri
bwana! Inabidi tununue pete nzuri. Si unakumbuka alimwambia hata Ester anapenda
vitu vizuri?” “Lazima. Anastahili. Umepata size sasa?” Junior akasimama ili
kufikia matunda yaliyokuwa bado yametunzwa vizuri kwa kuvutia.
“Nimepata aisee. Ana vidole vizuri huyo! Nina uhakika anavaa
size 6.” Watu wakaanza kujaa hapo ofisini kwao, wakaanza kugawana hayo
matunda na utani kibao. Ila ukweli Jelini alijua kuweka furaha kwa Ezra.
Aliifanya siku yake ikawa ya furaha sana. Maua aliyaweka mezani kwake akabaki
akiyaangalia huku akifanya kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kila penye
jema kuna changamoto zake. Zipi tena kwa Jelini na Ezra?
Yapi yanawajia
Wakati harakati
za kuchumbia zikiendelea? Maana andiko husema,
(1 Wathe
5:3) 'Wakati wasemapo, Kuna
amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu
umjiavyo mwenye mimba... '
Huku nako marafiki
hao
wafanyao kila kitu pamoja, uhalisia wa maisha unaanza kuwatenga. Wakati kwa
Ezra ndio kuna noga, kwa Junior kumeingia dosari.
Ni nini
kitaendelea?
USIPITWE.
0 Comments:
Post a Comment