“Maana kama ni huyo Jelini, mimi simfahamu na wakati nilipotaka
kumfahamu, alinidharau. Nikaona nimuache tu. Maana najua Ezra ni rafiki
yako wewe na…” Hope alizungumza kwa kupaniki mpaka akamshangaza Junior.
Akatulia kimya akimsikiliza. Aliongea na kuongea bila Junior kupata sababu
yakueleweka.
“Kwa hiyo ndio hivyo.” “Umemaliza? Maana mimi ndiye
niliyekuwa nikizungumza.” Hope akagundua Junior amebadilika.
“Nakusikiliza.” Junior akatulia kidogo kisha akaendelea. “Najua unafanya vizuri
sana kanisani. Lakini mambo yanayotuhusu sisi. Nikimaanisha mimi na wewe,
nafikiri ndiyo tuyape kipaumbele. Kama bado unaona kuna nafasi
kati yetu.” Hope alishituka hakutegemea.
“Kwamba leo unaona kuna tatizo kati yetu sababu ya
Jelini!?” “Sababu ya mahusiano YETU. Wakati wote, wewe umekuwa kipaumbe
changu. Chochote kinachokuhusu wewe, nimekua nikikitilia maanani, na kukuunga
mkono bila kuzembea. Kitendo cha mimi kutaka kukutambulisha Jelini. Mtu wa
muhimu sana kwa Ezra, ukakipuuza kwa kumdharau waziwazi kwa kazi
anayofanya, mbele yao, binafsi sijapenda Hope.” “Kwa sababu
nilikuwa na haraka na pia kwa kuwa nilishakutana naye kwenye shuguli za Ester
nikajua ni kama tumeshafahamia, na tungefahamiana naye zaidi kwenye mazingira
tulivu.” Akajua anajitetea tu na akawa ameshajichanganya.
“Nisikilize Hope. Kila kitu ni ziada, ila mimi na
wewe ndio wa kwanza na muhimu. Sijui kama unanielewa? Siwezi kukupuuza
wewe sababu ya kukimbilia majukumu mengine. Sijawahi kufanya na
sitarajii kufanya hivyo. Ezra ni mtu muhimu sana kwangu.” “Naona kuliko
mimi.” Akalalamika.
“Nisikilize Hope. Ulinikuta na ramani nzima ya maisha
yangu, akiwepo Ezra.” Hope hakuamini! Kwa mara ya kwanza Junior
alimbadilikia vibaya sana. “Kama Ezra angekuwa tishio kwenye mahusiano yetu,
ningekuwa tayari kubadilisha. Ila ulinikuta na Ezra. Nikakutambulisha kwake, akakupokea
na kukuheshimu. Anakujali kwa hali ya juu sana, kama mimi tu. Leo sina
wasiwasi kwamba nikioa na nikawa na watoto, endapo nikatangulia
na kumuacha yeye, mke wangu na watoto hawatapata shida. Atalinda familia
yangu, na mimi nitamfanyia hivyohivyo. Samahani kukwambia hili, sipo tayari
kubadilisha hilo.” Mpaka Hope akaishiwa nguvu.
“Sijui kama unanielewa Hope? Maana Jelini ni mtu muhimu sana
kwa Ezra. Nilitarajia umrudishie fadhila. Kama vile alivyokupokea wewe na
kukusogeza katikati yetu, nilitegemea ungemfanyia hivyohivyo Jelini, lakini si
kumfanyia kama ulivyomfanyia leo! Kwa mara ya kwanza leo, wewe,
umeanza kutengeneza madaraja ambayo hayajawahi kuwepo nyumbani kwetu
tokea Ezra anakuja kwetu. Mama ameona na baba ameona wameomba tuzungumze.”
Hope alishituka sana, akazidi kuishiwa ujasiri.
“Pale kwetu Ezra anapendwa sana. Mama aliapa kumlea
kama vile mimi. Baba ameomba tukizungumzie hiki kitu mapema, kabla hakijaleta
matatizo. Leo Ezra kwa mara ya kwanza amejiona hastahili kuwa pamoja na
sisi! Ameshindwa kujumuika na sisi, ameenda kukaa nyuma kabisa kama mtu baki! Hapana
Hope. Tafadhali kama kuna tatizo naomba tuzungumze.”
“Maana tumejaribu mara nne, lakini umemkataa kabisa Jelini!
Tumeanza kwenye swala la picha. Ukakataa bila kufikiria ni kwa nini Jelini na
sio mtu mwingine katika picha kama ile! Tukakuacha. Tukakujaribu mara ingine
baada ya ile picha yako kukamilika, pia ukakataa!
Tena unakataa bila adabu, mbele ya watu, wazazi wakikuangalia! Halafu
ukatufuata nikataka kukutambulisha kwake nikidhani pengine hujaelewa kuwa
Jelini yupo pale kwa sababu kwanza mimi na Ezra tulimkaribisha, pili ni mtu
wa Ezra! Lakini pia ukakataa! Haya, baba ametufuata, kutaka turudi kukaa
mbele, meza uliyokuwa umekaa wewe ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili yetu
akiwepo na Ezra. Na ilikuwa wazi kabisa! Eti wanahamia pale, wewe unahama!
Kweli Hope?! Pengine unipe sababu nitakayoweza kuielewa.” Hope kimya.
“Tafadhali unijibu Hope. Ndoa si kitu cha kufikirika.
Ni uhalisia kabisa. Tunajenga kitu chetu. Sasa kama wewe hupendi
ninavyopenda mimi, hudhani kama itakusumbua? Tutakuwa na maisha
gani hayo?” “Kwa hiyo unataka kusema nini?” “Ndio nakuuliza wewe! Na katika
hili tafadhali tuzungumze. Nataka kukusikia Hope. Na ukweli leo haikuwa
nzuri. Hata Noah mwenyewe ameongelea hili. Tena yeye amesema mbele ya Ezra na
Jelini, kuwa umemkataa Jelini. Sasa nataka kujua sababu.” Alivyoona
amekabwa, akabadili gia.
Akaanza kulia. “Mimi simfahamu
Jelini, na hata nilipotaka kumfahamu wakati wa kitchen party alionekana
hayupo tayari. Kama hakutaka ukaribu na mimi kabisa. Ndio nikaamua kuachana
naye.” “Ulitegemea umfahamu vipi au urekebishaje hilo wakati ulikataa
utambulisho, na hata alipokuja kukaa na sisi ulimkimbia?” Junior
akaendelea kumkaba, na hapo Hope akajua katika hilo hatatoka. Machozi
hayakusadia kabisa. Mchumba aliweza kuendelea na hoja yake akiyapita hayo
machozi yake. Akasalimu amri.
“Nimekosa Junior. Nitajirekebisha.” Hapo Junior akapoa.
“Nashukuru Hope. Tafadhali linapofika jambo letu. Sisi wawili, kama
familia, naomba ulitilie maanani. Maana baada ya yote, sisi tunabaki
peke yetu. Sitaki tubaki peke yetu, baada ya kufanikishia kila mtu, hata
kanisani, halafu eti sisi wenyewe tunakuwa tumeparanganyika! Hakuna amani!
Hakuna heshima! Hakuna upendo! Hilo hapana kwakweli. Sisi kwanza,
mengine baadaye.” “Sawa.” Akajibu hivyo na kuaga. “Usiku mwema.” Kisha akashuka
garini.
Ila ukweli aliingiwa hofu. Hakutegemea. Ni kama usiku huo Junior
anayemfahamu yeye, mpole na anamuongoza katika kila jambo, usiku huo alichora
mstari. Ni kama alivuka mstari ambao Junior alikuwa akiulinda kwa garama
kubwa sana na hakutaka chochote kitokee, kwa garama yeyote ile. Ni kama alikuwa
tayari kabisa kumuacha! Furaha yote ya harusi ikamuisha. Akanywea
kabisa, asiamini.
Ezra&Junior.
Ezra alipofika tu nyumbani akamtumia ujumbe Junior. ‘Nampenda sana Jelini. Ameahidi kusimama na mimi mpaka kifo. Nakusudia
kumuoa. Inamaana atakuwa kwenye maisha yangu ya hapa duniani daima.’
Junior aliposoma huo ujumbe, akaelewa. Alishakuwa amepanda kitandani, tayari
kukamilisha hiyo siku kwa usingizi. Ila mawazo yalimzuia kulala. Akaamua
kumfuata nyumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Nakuomba unisamehe Ezra.” “Tafadhali naomba unielewe. Sio
katika kuombana msamaha, ila kuelewa alipo na anakotoka. Jema ametueleza
historia yake. Kwa mara ya kwanza Jelini ndio anafanya kitu na kinaeleweka.
Inawezekana kwa wengine kinaweza kisiwe cha kisomi, lakini Jelini amefanikiwa
kwenye anapowekeza juhudi zake. Ametoka kwenye kudharauliwa kwa maisha
aliyoishi. Mimi kwangu ni nguvu yangu. Udhaifu wa kule ndio natumia mimi kama silaha
ya kumvuta kwangu. Sasa kama anakutana na yale aliyoyaacha kule, ana sababu
gani ya kubaki kwangu na Colins amerudi!?” Ezra akaendelea kwa msisitizo.
“Leo umemsikia akisema wazi kabisa alidhania huku kwa watu
tunao mjua Mungu ingekuwa tofauti. Sasa ana sababu gani ya kubaki
na mimi, apitie yaleyale?” “Samahani sana Ezra. Tafadhali naomba unisamehe. Ila
nimezungumza vizuri na Hope. Naamini ameelewa. Ameomba msamaha, na ameahidi
kubadilika. Tafadhali naomba unisamehe. Nahisi ni kama sikuwa nimeandaa
mazingira mazuri kwa ajili ya Jelini! Kwa sehemu nimejisikia kuhusika
kuchangia usiku aliokuwa amejiandaa nao vizuri, kuuharibu. Lakini unajua
nampenda Jelini. Siwezi rudia kosa tena. Tutahakikisha safari ingine akija,
anajisikia nyumbani.” “Nashukuru.” Bado alikuwa na nguo za harusini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akahisi kana kwamba ndio ameingia, na bado alikuwa akichat.
Akajua ni Jelini tu. “Kwamba ndio umerudi?!” “Tulikuwa tumekaa palepale
hotelini, kwenye gari yangu. Ndio nimehakikisha Jelini amelala, na mimi nataka
nikalale.” Akamuona anacheka kwa hisia. Akajua ni mapenzi tu. “Nini?” “Ni mengi
Junior! Acha tuzungumze kesho kazini.” “Acha masihara!” Ezra akacheka
kama anayevuta kumbukumbu.
“Kwa kifupi, nataka ujue, maishani mwangu kote, sijawahi
shika mikononi mwangu, kitu kizuri na cha thamani kama Jelini.” Junior
alicheka sana. “Junior! Acha kaka! Mimi na utuuzima huu, sijawahi aisee!
Akitulia hapa kifuani! Acha!” “Pesa haioni ndani?” “Hii ya madafu? Hakuna kaka.
Mtoto kama sufu! Halafu sasa anajua kutulia mikononi! Nimeshindwa kujizuia.”
“Acha masihara Ezra!” “Aisee nimeshindwa Junior. Nimepata kiss
hiyo, haijawahi tokea!” “Ezra!” “Kabisa. Na nikahakikisha nimeitendea
haki, mpaka Jelini mwenyewe ameikubali.” Junior akacheka ila akawa kama
anayefikiria.
“Najua nimeku disappoint. Lakini, Junior!
Nimeshindwa. Kwanza alikuwa akitaka kunibusu shavuni. Wakati nageuka ikawa kama
bahati mbaya. Midomo ikagusana. Akapaniki kwa kuwa nilishamwambia
nasubiri mpaka ndoa. Akajua ameharibu. Akataka kuondoka kwa kupaniki.
Nikasema nimtulize kwa kumkiss kidogo, asiondoke akiwa amepata wakati
mgumu ukumbini na pale. Nikajua akiondoka usiku ule, vile, nitakuwa nimepoteza
pointi zote.”
“Aisee yule mtoto ni
mtamu Junior! Nimesalimu amri. Sikujua kama unaweza mkiss mtu zaidi ya
dakika 5 mfululizo, na bado usiridhike! Aisee utanisamehe kwa kuvunja maagano
yetu.” “Hapana. Umebahatika Ezra. Mimi nakuelewa. Lazima uweke msingi
unaooleweka, lasivyo utakosa thamani. Na uzuri Jelini anakupenda na mwenyewe
anakiri anakuhitaji. Halafu anaonekana anahekima. Moyo wake hauna hila.”
Aliongea kama ambaye anawaza yake. Ezra akaelewa ikabidi ajishushe.
“Nisikilize Junior. Hope unamjua jinsi alivyo. Na wewe
ulimpenda kama alivyo na ile haiba yake. Kwa hili, ameomba
msamaha, na amesema atajirekebisha, si ndivyo?” “Lakini leo amenifanya
nifikirie mara mbilimbili. Kitendo cha kunikatalia bila adabu mbele ya
watu! Hakika kimenishitua sana Ezra. Sana. Unajua mpaka baba ameniomba
nizungumze naye.” “Haiwezekani Junior!” “Kabisa. Wakati wanaondoka na mama,
wakaniomba niwasindikize kwenye gari yao. Mama amesema Jelini anaonekana ana
moyo mzuri sana. Upo wazi kuusoma moyo wake. Anaonekana ana upendo na kujali.
Hana hila na mtu. Anasema alimuona hivyo tokea anatambulishwa kwake na Jema,
kwenye swala la kitchen party. Baba ameomba nizungumze na Hope, tujue
kuna tatizo gani.” “Sasa yeye amesema kuna tatizo gani!?” Ezra naye akataka
kujua.
“Kwani anamfahamu vizuri Jelini!?” “Ni kumuona tu! Na ni kama
aligusia eti huko kwenye shuguli za Ester, eti ni kama Jelini alimpuuza. Akawa
akimuongelesha sijui Ester na mama tu na watu wengine, yeye akampuuza! Sasa
sijui ni kweli au ni kujitetea tu, lakini bado sidhani kama hiyo ni sababu
yakutosha. Aisee mama hajapenda kabisa. Na ameongea kabisa, kwamba
tuweke sawa hilo jambo. Jelini ni binti mzuri na alijiandaa kwa wakati mzuri.
Kitendo tulichomfanyia, kitamnyima uhuru wa kuja kurudi tena kwenye
shuguli zetu.” Hapo Ezra akanyamaza.
“Sijui Ezra! Sijui aisee!” “Naomba tufanye kama alivyosema
Jelini.” “Ule ni ushauri mzuri sana, lakini sipo tayari kuutekeleza Ezra.”
Mpaka Ezra akashituka. “Hapana aisee! Sina sababu ya kufanya hivyo. Kwa
nini?! Ifike sehemu achague kama atakuwa mmoja wetu au la.” Ezra akajua
amekasirika. Akamtuliza.
“Leo tumekuwa na siku ndefu. Tena tokea jana. Hatukulala
vizuri sababu ya Jelini. Leo ni Hope. Tafadhali tuchukue hatua moja nyuma, tutulie.
Ona jana kwangu mambo yalivyokaa sawa! Tafadhali tutulie.” Akazungumza naye,
mpaka akamuona ametulia kabisa. Ndipo wakaagana na kwenda kujipumzisha kwa kazi
kesho yake.
Jumatatu.
Wakati wakipanga mipango ya jinsi ya kumsuprise
Jelini na pete ya uchumba, wakiwa ofisini kwao, akapata ujumbe kutoka kwa baba
yake. Ilikuwa kama barua pepe iliyopigwa picha kisha akamtumia kijana wake.
Akaifungua. Ezra akamuona kadiri anavyosoma, ndivyo anavyobadilika. “Ni nini?!”
Akamuona anatingisha kichwa kwa masikitiko huku akiendelea kusoma. Akasimama
kutoka kwenye meza yake na kwenda kuchukua simu ya Junior.
Ilikuwa barua kutoka kwa Hope, akimuandikia mchungaji wa
kanisa, ambaye ni baba mkwe wake, kujiudhuru haraka iwezekanavyo, kwenye
nafasi yake. Hakutoa sababu. Lakini akasema kuanzia siku hiyo, anajitoa
madarakani. Ezra akatulia kwa sekunde kadhaa na kumtizama Junior. “Utafanyaje?”
Akamuona anafikiria, kisha akampigia simu baba yake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akamsikia akimsalimia na kwenda moja kwa moja kwenye pointi
ya msingi. “Kwanza niombe radhi kwa hili la
kushitukizwa, baba.” “Wewe unajua sababu!?” Mzee akauliza. “Hapana. Mimi ndio naisikia kutoka kwako hata mimi hajaniambia.
Sasa kwa sababu hajasema sababu, naweza hisi ni hasira sababu nilizungumza naye
jana. Na huku ni kuzira tu. Tumempa majukumu makubwa sana pale kanisani.
Na kwakuwa kila kitu kinakwenda sawa, anaweza bweteka, akadhania ni
juhudi zake mwenyewe kumbe hii ni kazi ya Mungu. Na Mungu ana watu wengi sana.” Ezra kimya
akisikiliza.
“Sasa kwa kumsaidia, tafadhali mjibu kuwa
maombi yake yamepokelewa. Na ungependa makabidhiano yote kabla ya
ijumaa ili kujipanga vizuri.” “Una uhakika Junior?!” Mzee mwenyewe
hakutegemea. “Kabisa baba.” “Sasa nani atashikilia hayo
majukumu? Nashauri tuzungumze naye, tumsihi aendelee.” “Hapana baba. Hutambembeleza Hope. Hiyo ni kazi ya
Mungu, na sisi wote tumekubali kutenda kazi pamoja na wewe. Atakayeweza
kusimama na kumtumikia Mungu kwa moyo wa unyenyekevu, atakaribishwa. Ambaye
hawezi, basi. Hatutambembeleza mtu. Hatuwezi kuendesha mambo kwa namna hiyo.”
Junior akaendelea ila hata kumshangaza baba yake. Kwamba mchumba asibembelezwe!
Akatulia kusikia mwisho wake.
“Nitasimamia hiyo nafasi mpaka utakapopata mtu
mwingine atakayeweza kuikaimu. Ila kwa sasa mwache tu.” Ikabidi Mzee akubali
tu. Hakuwa na jinsi kwa sababu ni Junior na ameahidi kusimamia mwenyewe. Hata
hivyo Junior ndio kama mwenyekiti anayewaongoza wote bila wao kujua, ila baba
yake alijua. Ana jinsi yake ya kuongoza kwa chinichini huku akikupa wewe sifa.
Kama huna akili ya kufikiria, unaweza kujikuta una vimba kichwa,
kwa akili ya Junior.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hope akaandikiwa barua ya kukubaliwa ombi lake. Mzee wito ni
mchungaji, aliiandaa vizuri tu hiyo barua. Kiuchungaji kwa kondoo wake.
Kwamba ombi lake limepokelewa kwa heshima. Akamshukuru kwa kujitolea kwa
hali na mali. Hapo akataja majukumu mazito ya kikanisa aliyokuwa akiyafanya na
kuyakamilisha kwa uaminifu na juhudi zake akijitolea bila kuchoka. Mchungaji
akamshukuru kwa dhati. Na kumtaarifu kuanzia siku hiyo anapokelewa majukumu
yote ya ukatibu. Itaandaliwa barua ya kupeleka benki, ya kutolewa
kwenye waweka saini kwenye hundi za kanisa. Atatolewa katika security system
zote za kanisa ambazo kabla ya ijumaa aliombwa afike ofisi za kanisa
akabidhishe funguo zote za jengo na mafaili ya kanisa.
Kiberiti Kilichojaa.
Hope alikuwa akitingisha kibiriti, akakuta safari hii
kimejaa. Alipopokea hayo majibu, alishituka mpaka tumbo likaanza kumuuma.
Hakutegemea hivyo hata kidogo. Alichotaka kukifanya mchungaji, ndicho alichodhania
kingefanyika. Kuitwa na kubembelezwa. Kwa kuwa ni kweli aliiwezea hiyo
nafasi. Pamoja na shule yake, akaweza kuongoza ibada zote mbili. Hakutegemea
kuvuliwa uongozi kwa barua pepe moja tu! Ukweli alitishika. Hofu ikamuingia
akijua ameharibu. Akatamani ile lawama ya jana yake usiku, kuliko hiyo
fedheha. Inamaana itajulikana si kiongozi tena! Akazidi kufedheheka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Nafasi Zinazowajia
Watu Maishani Na Kutufanya Tubweteke, Tukiona Tunastahili. Iwe Ndoa, Malezi Kwa Watu Mungu Ametuamini Nao Hata Wafanyakazi Wetu Wa Ndani, Mahusiano, Kazi, Biashara.
Inaweza Fika Mahali Ukokosa Sababu Ya
Kung’ang’ania Ulicho Nacho, UKADHARAU, Mpaka Mungu Anapokitoa Mkononi Mwako Na
Kumkabidhi Mwingine Ndipo Unaona UMUHIMU WAKE.
Wakati Mwingine
hubahatika Kupata Nafasi Ya Pili, Na Wakati Mwingine Tunapoteza Kabisa.
Umakini Na Tulivyo
Navyo Mkononi, Ni Muhimu Sana. Weka Heshima Kwenye Chako/VYAKO Na Kumbatia Kwa Moyo Wako
Wote Na Akili Zako Zote Kana Kwamba Hakutakuwa Na Kesho,
Au Hutaki Upokonywe.
Kila Kitu
Tulicho Nacho Ni Dhamana Tu, Na Vyote VINA Muda.
Usikubali Majuto Yakaja Kuwa Mjukuu.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment