Jelini akaendelea taratibu tu. “Ilianza kidogo sana. Kama
hivihivi tu, lakini ikaendelea mpaka wakafanikiwa. Na huwa ina mtindo wa
kufungua milango kwenye mambo mengi, kwa sababu ni amani. Amani anapotoweka
sehemu, mambo mengi yanajiinua kwenye hiyo sehemu iliyoachwa wazi bila amani.”
“Lakini nyinyi ni marafiki wa muda mrefu. Najua mnatamani
mambo fulanifulani yatokee kwetu. Lakini Junior, mahusiano huwa hayalazimishwi.
Hujengwa. Na hili nilijifunza kwa Jema. Mengine huchukua muda mrefu,
mengine ni muda mfupi tu. Mnakutana mara moja, mnazungumza, vina click,
kuanzia hapo mnaanza kutafutana. Na kuna mtu mwingine anamchukia mtu
mara tu, anapomuona. Unakuta tu moyo wake umemkataa huyo mtu. Baadaye sana,
anakuja kugundua yule mtu anafaa kwenye maisha yake, anamleta karibu au
kushindwa kabisa kuwa karibu. Inatokea kabisa.”
“Ninachotaka kukutuliza ni kuwa, kuwa na amani.
Usilazimishie. Kwa sababu unaweza ukakuta katika hili, badala ya kujenga, ndio
unabomoa kabisa. Itawasumbua nyinyi wawili ambao ni marafiki wa muda mrefu.
Kisha kuja kusumbua wazazi. Na baadaye wewe na Hope. Mwishoe jambo zuri
linageuka kuwa baya. Tafadhali tulia, tujipe muda. Naamini kila kitu kitakuwa
sawa.”
“Najua wewe huna tatizo na mimi. Umenisaidia, umenikarimu
nyumbani kwako, ukaweka mazingira mazuri mpaka nimeweza kuzungumza na kupatana
na Ezra. Katika hilo nitakushukuru daima. Na sitataka nyinyi mgombane
sababu yangu. Tuliache hili jambo kabisa, na wala usiwe unaniomba msamaha.
Inatosha Junior.” “Najisikia vibaya!” “Tafadhali kuwa na amani. Tutulie kabisa.
Unaweza ukaja ukakuta baadaye kukawa na amani. Tukajikuta wote tupo karibu, au
ndio ikashindikana kuwa na mahusiano mliyokuwa mkiyatamani nyinyi. Lakini
kwenye hiyo hali, wote tukagundua jinsi ya kuishi pamoja bila kukwaruzana.
Naomba usijali Junior. Mimi naelewa kabisa.”
“Pengine anahitaji muda wa kunifahamu vizuri. Maana ni kweli
nimeingia tu kwenye maisha yenu, hamifahamu vizuri na yeye ndiye kama
aliyekuwa katikati yenu. Unaweza kuta ni upendo wake kwenu, anawalinda hataki
mpatwe na baya lolote, ndio maana yupo makini. Tafadhali mpeni muda.” Junior na
Ezra wakaangaliana kama wasiokuwa wanaamini kusikia hivyo kutoka kwa Jelini.
“Daah! Umebahatika Ezra!” Wakaanza kucheka. “Sikutanii.
Sasahivi nakuelewa zaidi kwa nini unapenda kumtafuta ili uwe naye.” “Umeona
eeh!” Wakaanza kutaniana. Kidogo wakawasogelea watu wanao wafahamu hao kina
Ezra. Salamu haziishia! Jelini akashangaa Ezra anaaga kuwa anamsindikiza
Jelini. Akamshika mkono na kuondoka hapo akimuachia Junior hao watu.
Jelini&Ezra
“Naona pale hatutapata muda mtulivu. Kila mtu anataka
kuzungumza na sisi kisha wanafanya makao kabisa.” Jelini akacheka akiwa
ameshikwa mkono, mpaka alipoegesha gari yake Ezra. “Tukae hapa nyuma.”
Akamfungulia mlango, akaingia na kufunga. Akaenda kuwasha gari na kurudi kukaa
kiti cha nyuma pembeni ya Jelini kama walivyozea kukaa wakati wa kula.
“Nashukuru kuja kuwa nami hapa harusini. Inamaana kubwa sana
kwangu.” “Karibu Ezra. Na mimi nimefurahia kuwa na wewe.” Akamtizama na kucheka
kama mwenye kitu anashindwa kukisema akihofia atakosea. “Ni nini?” “Nakupenda
Jelini. Nakupenda sana mpaka nahofia nisije kukupoteza kwa namna yeyote
ile. Sitaki kutokee kosa.” “Na mimi nakupenda Ezra. Natamani tuishie hivi.” “Lakini
yupo Colins ambaye unataka ukamuuguze! Na mimi sijui ndio inakuaje!
Unakua kama nesi? Au unakuwa ukifanyaje? Nisadie maana hapo nimekwama kabisa.”
“Labda nikuombe radhi Ezra. Nafikiri sikufanya vizuri.
Nimefikiria, na naona mama yupo sahihi. Wakati nikikwambia hivyo, nafikiri bado
sikuwa nimefikiria vizuri. Narudi kwa Colins kama nani wake? Hilo ndilo swali
la msingi. Nyumbani kwao karibu wote ni wa uguzi. Wana wafanyakazi pia. Mimi
nikiwa mpenzi wako, kisha kwenda kule kumuuguza, nimeona haitaleta picha
nzuri. Pengine ingekuwa labda yupo peke yake, hana msaada wowote ule, hapo
sawa. Lakini kwa sasa, sioni tena nafasi yangu kwake. Mimi si mpenzi wake wala
si rafiki tena. Nakwenda kwake kama nani!” Ezra alifurahi, ila akajikaza.
“Unauhakika Jelini?” “Kwa asilimia 100. Naona nitulie,
nijenge kwetu. Niache kuyumba yumba na maisha ya watu wengine.
Nimekusudia kutulia na wewe Ezra. Labda kama wewe utaona haupo tayari na mimi.”
“Nakuhitaji Jelini, kwa moyo wangu wote. Na naomba usifananishe hali ya
leo na kwa kina Colins.” Jelini akatulia kidogo akijaribu kuelewa.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Jinsi alivyokufanyia Hope, usifananishe na kwa kina Colins.
Hata kama yeye hatakukubali, hesabu tu kama mtu mwingine baki.” “Lakini ni
mpenzi wa Junior, na Junior ni mtu muhimu sana kwako!” “Unakumbuka nilikwambia
wewe ndio wa kwanza kwenye kila kitu changu hapa duniani?” “Ezra!”
“Hakika sikutanii Jelini. Hivi nilivyo, ndivyo nimemaliza. Sina baba sina mama
wala ndugu.” Jelini akashituka sana.
“Pole Ezra.” “Asante, lakini nilikuahidi nitakujibu swala la
wazazi wangu. Una muda au unataka kuwahi nyumbani.” “Nafurahia kuwa na wewe
Ezra. Labda wewe kwa kuwa kesho unatakiwa kazini asubuhi na mapema.” “Hamna
shida. Nimefurahi umeniulizia maswala yangu binafsi. Acha unifahamu vizuri.”
Akaendelea.
“Na mimi nilikuwa mtoto wa kwanza kwetu kama Junior tu.
Wadogo zangu wawili kama hivyo Junior, lakini wadogo zangu walikuwa wakiume
watupu. Nilifaulu darasa la saba kwenda kidato cha kwanza bweni ndiko
nilikokutana na Junior. Nimetoka familia ya wafugaji. Ndio ilikuwa kitu kikubwa
nyumbani kwetu. Mimi nimeanza kuchunga ng’ombe na mifugo mingine nikiwa mdogo
kabisa. Na ndio kitu nilikuwa nikifanya nyumbani.”
“Nilipokuwa shuleni, muhula wa pili tu. Nikapata taarifa
natakiwa kurudi nyumbani, baba amefariki gafla. Nikiwa nimefika tu, mama naye
akafariki siku ileile. Kesho yake akafariki mdogo wangu anayenifuata. Ikawa ni
mshituko. Katika fununu, ikasikika kuwa baba alipitisha mifugo yake kwenye
shamba la mtu, mifugo yetu ikala na kuharibu sana mazao ya huyo mtu ndio huyo
mtu anatuua.” Jelini alishituka!
“Ezra?” “Ndivyo walivyosema. Ikabidi sasa wazee waende
kumuomba msamaha. Akasema yeye ameshafanya mambo yake, hawezi
kubadili. Familia yote ya baba itakufa. Aisee hawakutania. Siku hiyohiyo wakati
hao wazee wanarudi nyumbani kutoa hizo taarifa. Kabla hawajafika nyumbani mdogo
wangu wa mwisho naye akafa.” Jelini akabaki akitetemeka.
“Sasa pona yangu ilikuwa hivi, nilipokutana na Junior
sekondari ya Pugu, tukatengeneza urafiki mkubwa sana. Akaniambia baba yake ni
mchungaji. Na yeye anapiga vyombo kanisani. Wengine walikuwa wakimcheka, ila
mimi nikapenda. Nilitokea kwenye ukoo usio na dini, ila kuabudu mizimu. Ndipo
nikawa nikienda na Junior nyumbani kwao. Mwanzoni tu, kwa kuwa tulipendana sana
na Junior. Na nilimpenda vile alivyo, nikataka kuwa kama yeye.”
“Junior akaniambia ni kuokoka. Akanipeleka kwa baba
yake. Akanieleza habari ya Yesu. Nguvu zake na uwezo wake. Na pumziko unaloweza
pata na ulinzi, endapo ukimpokea Yeye. Nikaomba na mimi waniombee. Kwa hiyo
tukaendelea kuwa karibu zaidi, na baba yake Junior ndio akawa baba yangu wa
kiroho. Wakati huo hakuwa na kanisa kubwa kama hivi sasa wala hawakuwa na pesa
kama hivi. Alikuwa mchungaji wa kawaida sana. Lakini akanipokea na kuanza
kunitunza kama Junior.”
“Samahani nikukatishe kwa swali. Umesema ulipenda kuwa kama
Junior. Kivipi?” Ezra akacheka akimfikiria Junior. “Umeshawahi kusikia watu
wenye roho nzuri zisizo na hila hata kidogo?” Jelini akatulia akifikiria. “Basi
ni Junior. Shida yake ni kuona kila mtu anafanikiwa. Kiroho na kimwili.
Mtaratibu sana, hana makuu. Halafu alijaliwa uwezo mkubwa sana wa kufikiri,
anaakili. Lakini ni mnyenyekevu huwezi jua mafanikio aliyo nayo na alivyo.
Darasani alikuwa hapendi kuona mtu anafeli. Kama huyo mtu yupo tayari, anaweza
msaidia huyo mtu kwa garama yeyote ile, ilimradi tu na yeye afaulu.”
“Kanisa la baba yake kufika hapo lilipo ni akili ya Junior
na hayupo kwenye uongozi wowote ule pale kanisani, ila naweza kukwambia yupo
kwenye akili ya baba yake. Akiongea chochote hata kwa kunong’ona, yule mzee atasikia
na atafanya bila kupinga. Sasa kwa sababu yeye hapendi mambo ya kuongoza, ndio
Hope akapewa ukatibu wa kanisa.” “Ooooh!” “Ewaah. Yeye anauwezo wa
kufanya mambo yaende kama yalivyopangwa.”
“Na uzuri wa Hope yupo na juhudi na anapenda kuongoza mambo
na watu. Halafu amesoma vizuri tu. Kwahiyo hayo mambo yamemsadia kuweza
kushikilia kanisa katika ibada zote. Ile ya walionazo na wasomi, wa asubuhi,
ibada ya kwanza. Na hii ibada ya pili ambayo ni mchanganyiko. Hana shida ya
kujitolea kwa chochote na muda wake mwingi amewekeza kanisani. Ndio maana
unamuona yupo juu juu. Huwa hataki jambo liharibike.” “Kumbe!” Hapo Jelini
akajituliza na kupoa kabisa. Akamuona amepoa na kupotea kabisa hapo. Yaleyale
ya Love!
“Niangalie Jelini.” “Mmmh! Naona hii historia inataka
kujirudia.” Akalalamika akiwa amenyongea kabisa. Akamgeukia vizuri na kumshika
mikono yote miwili, kumgeuza kwake. “Sio na mimi.” “Ilikuwa hivihivi kule kwa
kina…” “Sio kwangu, na sio na mimi. Hope si sehemu ya maisha yetu, labda
atake yeye. Na hilo nitamuweka sawa kabisa. Hutaolewa na Junior,
ila mimi. Hutaishi na Junior ila mimi.” “Ila kanisani yupo na ndio katibu!
Nimekuta pale kuna amani, na wewe ukisifiwa sana. Sitaki mimi ndio niwe chanzo
cha matatizo!”
“Pengine kwake ndio utakuwa tatizo lakini sio
kwangu. Na sitaki yeye akunyime raha. Ulizungumza vizuri sana na Junior.
Tafadhali ukumbuke ulichomwambia. Si lazima nyinyi mkawa marafiki. Na hapo
ndipo yeye atatafuta jinsi ya kuishi na wewe, maana sisi hatuna neno naye.
Akishindwa kuwepo tulipo, basi aondoke.” “Kama pale ukumbini? Maana tulipohamia
pale mezani kwao, yeye aliondoka na hakurudi tena!” “Basi itabakia hivyohivyo.
Mwache yeye mwenye tatizo ndio atukimbie. Na nahisi mchungaji
ameshaliona hilo ndio maana alikutambulisha maalumu pale mbele na kutaka picha
nyingine za familia. Mimi na Junior tunahisi amefanya kusudi.” “Kweli Ezra?”
“Kabisa. Picha zote, tena kama ile aliyotaka pale ukumbini,
vilevile, tulishapiga nje. Na ni vile hujamfahamu yule mzee. Hana makando.
Hana tajiri wala masikini. Na hapendi kuona mtu anaonewa. Pasipokuwa na amani,
ni lazima ataitafuta, ndio maana umeona mimi na Junior tumedumu sana.”
“Nilipofiwa na familia yangu, wazee walifanya tambiko na
kunisihi niondoke na nisirudi tena pale kijijini kama kuokoa
ukoo.” “Ezra!” “Si kwa ubaya, lakini imani yao ndivyo ilivyowatuma hivyo. Kuwa,
ili ile roho ya mauti isiendelee mpaka kwa ukoo mzima, kwa kuwa kwangu
ni kama ilishindwa kuniingia, basi waliniomba mimi niondoke
nisiwasababishie wao vifo. Sasa kwa kuwa nilishakuwa nimepazoea kwa kina
Junior, ndio ikawa sehemu ya kwanza kukimbilia. Na wakovu ndio ikawa pona
yangu. Bila Yesu ungekuta ningekuwa nimeangamia kama familia yangu.”
“Sasa kuanzia hapo, nikawa nikiishi kwa kina Junior. Yule
mzee na mkewe wakanipokea kama mtoto wao kabisa. Sijawahi lia shida. Walichompa
Junior ndicho walichonipa mimi. Na unavyomuona Junior tabia zake zipo kama mama
yake. Mpole sana na ana upendo wakupitiliza. Anajali mpaka utamuonea
huruma kumpa matatizo yako. Hajawahi kunipa sababu yeyote ya kumfikiria tofauti
ya mama yangu wa kunizaa. Kwa hiyo akisema ni ‘kama amenilea’, ujue ni
amenilea tokea kijana mdogo. Ananifahamu kama anavyomfahamu Junior. Ananipenda
bila kujisingizia.”
“Kwa hiyo ndio historia yangu. Ninapokwambia nakuhitaji,
ujue nahitaji faraja yako Jelini. Nakutaka usimame na mimi tujenge chetu
kama unavyosema, kitu kinachonifariji. Kwanza sikutegemea kupata mwanamke
atakayesema eti yupo tayari tujenge kwetu! Sikutegemea. Kwa hiyo naomba
Hope asikutoe kwangu. Tafadhali Jelini. Nakuhitaji sana. Na ujue mimi,
Junior na wazee, tutasimama na wewe. Na leo umeona.” Jelini akajisikia kutulia.
“Eti Jelini?” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Unafikiria kuniacha?” “Hapana Ezra! Ila nilijua upande wa kanisani.
Nikimaanisha kuwa na mtu kama wewe umetokea kanisani, ingekuwa tofauti! Kumbe
changamoto zipo kila mahali! Nitajifunza jinsi ya kuishi naye ili kusipotee
amani.” “Hapo utanisaidia Jelini. Na asante kwa hilo.” “Wewe ni mtu mzuri sana
Ezra. Ila sikuwa najua kama una historia ya kusikitisha hivyo! Pole.” Akajinyanyua
ili ambusu shavuni, Ezra akawa anageuka, akaishia mdomoni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini alipaniki vibaya sana. “Samahani sana. Sikuwa
nimekusudia kukubusu hapa.” Akajionyeshea kwenye midomo yake. Akionekana na
hofu ya waziwazi. “Samahani sana. Acha niondoke. Naona nimeshaanza kufanya
mambo ya ajabu. Sitaki niku…” Taratibu bila ya kumjibu, Ezra akamshika kwa
kiganja chake, juu ya shingo mpaka kwenye sikio. Akampa mdomo.
Jelini hakuamini. Akambusu mara kadhaa juu ya midomo yake.
Kisha akamsogeza karibu zaidi akimbusu midomo hapo juu mpaka Jelini akasalimu
amri, akafungua midomo, wakaanza kupata romance ya haja, Jelini
asiamini. Bwana Ezra alitulia kwenye hiyo kiss, Jelini hakutegemea.
Alimshika vizuri, akaendelea kupata kiss isiyo na papara ila kumuhisi
anafurahia sana kupata midomo ya Jelini.
Alipofanikiwa kupata ulimi wake, hapo Jelini alishindwa
uzalendo. Ezra alicheza na huo ulimi, akionyonya kama pipi aliyoipenda
ladha yake. Taratibu bila kuachia mate mengi ya kumkera Jelini. Hakika
Jelini alipenda. Alitamani asimalize. Hakuwahi kupata denda ya muda
mrefu kwa kiasi hicho, tena mfululizo! Alifurahi sana.
Akafanya hivyo kwa muda wa kutosha, akamuachia taratibu
akimbusu juu ya midomo kama kujituliza kutoka kwenye hali ya juu waliyoipata
kutoka kwenye kissing. Kisha akamuachia midomo bila kumuachia vile
alivyomshikilia shingoni. Akabaki akimuangalia huku amemshikilia shingoni.
Jelini aliona aibu na kushindwa kumtizana. Akajivuta na kumsogezea kwake zaidi,
kisha akamkumbatia. Jelini akajiweka sawa na kumlalia kifuani. Wakatulia.
“Asante Ezra. Nimefurahi sana. Sikutegemea!” Ezra akacheka
na kuinama kumchungulia pale alipojilaza. Jelini aliponyanyua uso kumtizama,
wakashindwa kuachana. Wakaanza tena. Walikiss mfululizo bila kuchoka.
Jelini akajisikia hisia za kimapenzi za hali ya juu kitu alichokitamani
kukipata kwa Ezra, kama alivyojisikia kwa Colins.
Alikuwa akiogopa akihofia kwa kuwa alishajisikia hivyo kwa
Colins, pengine inaweza isijirudie tena kwa mwanaume mwingine! Lakini
ikawa tofauti kabisa kwa Ezra. Jinsi alivyomshika vizuri na kumkiss kwa
upendo vile, akaibua hisia nzito sana ndani yake mpaka machozi yakamtoka. Ezra
akamuachia taratibu na kumfuta machozi.
Wakati akitaka kumuuliza kwa nini analia, Jelini akamdaka
midomo yake, wakaanza tena. Waliendelea bila kuchoka kila mmoja akimfurahia
mwenzie. “Nakupenda Ezra. Nakupenda sana.” “Nakupenda Jelini. Tuone, tuishi
pamoja, unitoe upweke.” Mwili mzima wa Jelini ulikuwa ukisisimkwa.
Akambusu tena kidogo, na kumuachia, akarudi kujilaza kifuani wakihema kama
kujituliza, maana walitaka kupitiliza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baadaye akiwa amemlalia kifuani akamuuliza taratibu kama
aliyekumbuka kitu. “Unaishi wapi?” Akamsikia Ezra anacheka. Jelini akanyanyua
uso na kumwangalia. “Junior ameniambia hukujua kama anaishi gorofani.” Jelini
mwenyewe akaanza kucheka. “Nyumbani kwake pazuri sana bwana! Li empire
kabisa! Lipo kama lihekalu la kiarabu sijui! Mamilango yenyewe ni ya mapesa
mengi. Mavitasa ya ajabuajabu!” Ezra akazidi kukaukiwa kwa kucheka. “Ngumu
kudhania mtu kama yeye anaweza kumiliki jumba kama lile bwana!” “Hivi
wewe unadhania Junior anafanya kazi wapi?” Hapo akamfanya Jelini afikirie.
“Hilo swali la msingi. Mimi nilikuwa nikimchukulia poa sana!”
“Junior anayo pesa, Jelini. Analipwa pesa nzuri sana. Na bado marupurupu. Ila
ni mnyenyekevu mno. Ngumu kumfananisha na mafanikio yake ya kimwili. Ila
amefanikiwa kwenye anachofanya au tunachofanya.” Hapo Jelini akakaa kwa
mshituko.
“Kwamba na kazi pia mnafanya pamoja!?” Ezra akaanza kucheka
tena. “Bwana haiwezekani!” Akaendelea kucheka akitingisha kichwa kukubali.
“Ezra?” “Watu wanapotuita mapacha si kwa sababu ya muonekano, ni kwa
kuwa kila kitu chetu kinafanana.” Jelini akakunja uso akifikiria.
Kisha akauliza kama ambaye ameshapata jibu analolipinga. “Usiniambie
na nyumba zenu pia zinafanana!” Ezra akacheka kwa sauti ya juu zaidi. “Nyie
jamani!” Jelini hakuamini. “Ezra!” “Na mipaka yetu ya nyumba imepakana.” Jelini
alishituka sana.
“Kwamba na wewe unakaa mtaa uleule?” “Nyuma ya ukuta wake.
Kiwanja alitupa mzee. Tukagawana na kila mmoja kutengeneza hati yake. Ramani
moja. Mpaka vitasa vya milango yetu, vinafanana. Na tulifanya makusudi, ili
wake zetu wasije oneana wivu.” Jelini alichoka kabisa. Ezra hana mbavu.
“Kwa hiyo na kazi mnafanya wapi?” “BOT.” Akajibu Ezra
akicheka sana. Jelini akahisi pengine hajamuelewa. “Ukisema BOT unamaanisha,
BOT ya benki kuu ya Tanzania?!” Ezra hana mbavu. “Nyie jamani! Kumbee!” Mpaka
akahisi vipele vya mwilini vimesimama. Hakujua yupo na mtu mambo safi.
Alipokuwa akimwambia ametoroka kazini, muda wa chakula cha mchana, alijua kazi yenyewe ni ya
vichochoroni! Kumbe Ezra anajielewa! Anatokea BOT kumletea yeye matunda
anakouza vipodizi! Jelini akanywea kabisa na hofu kidogo ikamuingia. Kwamba
yupo na mtu wa namna hiyo! Ezra akabaki akicheka.
“Na kukupunguzia swali la baaadaye, ndiyo, tupo ofisi moja.
Yaani chumba kimoja.” “Haiwezekani jamani!” Ezra akazidi kucheka. “Tumeshindwa
kutengana na Junior. Ni mtu rahisi sana kuishi naye. Neno samahani lipo
karibu sana kwake.” Akaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Noah anashindwa kuishi kwao, huwa mara nyingi yupo kwa
Junior au kwangu. Usipomkuta kwa Junior, ujue amegombana na Hope, ataondoka ili
hasira zipungue, ila ujue atarudi tu.” Jelini akashangaa.
“Kwa nini agombane na Hope tena!?” “Noah ni mlevi. Hapendi
kujishugulisha na chochote, sasa hicho ndicho kinacho mkera Hope. Anataka
ajishugulishe. Ila mzuri sana kwa vyombo vya mziki. Pale kanisani
wanamtegemea.” “Haiwezekani!” “Ila na sisi cha moto tunakipata. Anaweza
kwenda mazoezini amelewa, anaishia kulala kwenye gari mpaka tuitwe kwenda
kumtoa kwenye gari, ndio anakwenda mazoezini. Anaimba yule, hujawahi ona. Na
ana uwezo mkubwa sana wakufundisha kuimba na kutumia vyombo. Akikosekana pale
kwenye mazoezi, kila mtu analalamika.”
“Ibada zote, yeye ndio anaongoza kwenye kusifu na kuabudu.
Hakuna eneo kwenye mziki, ukamuweka, ukajuta. Sasa anasemaga Hope ni afande
aliyekimbia jeshi.” Jelini alicheka mpaka machozi. “Nilimsikia pale ukumbini.”
“Sasa usifikiri anaishia hapo. Akimuona Hope eti anampigia saluti. Akimwambia
ndio salamu inayomfaa.” Wakazidi kucheka. Jelini hana mbavu.
“Sasa Hope hapendi amfanyie hivyo au amuite afande.
Basi ugomvi wake mpaka kwa wazazi. Lakini Noah haachi. Akilewa ndio inakua
mbaya, mpaka huwa tunamfukuza alipo Hope. Na sehemu inayowalazimu wawe pamoja
ni mpaka Junior, mimi, au mzee tuwepo. Ndipo patakalika na kuweza kumuuliza
jambo, Noah akamjibu vizuri” “Anafanya kazi wapi?” “Pale kanisani ambako Hope
ni katibu, ndiko Noah anakofanyia kazi na ndio huko wanagombana zaidi.
Maana ni kama Hope ndio bosi wake. Na analipwa mshahara kabisa. Ameishia kidato
cha pili, anasema yeye ameshamaliza shule. Ila mama yake anampenda, ndio roho
yake. Mziwanda wake. Ukimkuta anambembeleza, unaweza ondoka hapo. Unaweza
fikiri ananyonya. Mzee anasema ndio maana hakui. Ila nafikiri wewe
amekupenda.” “Kwa nini?”
“Hajuagi kuweka kitu kichwani kwake. Kinachopita kichwani
mwake, mtakijua hapohapo ndio maana baba yake hapendi awepo kwenye vikao vya
wafanyakazi pale kanisani au wazee. Anaweza kuzungumza jambo juu ya mtu, mpaka
ukashika kichwa. Jambo la siri kabisa. Anaweza lisikia mahali, akaenda
kumuuli huyo mtu kikaoni, mbele ya baba yake.” “Haiwezekani Ezra!” “Wewe
utamfahamu tu. Wala hutamtafuta. Unaweza ukawa umelala usiku, unashitukia
anakugongea. Kwamba anahali mbaya, hawezi kurudi kwao wala kwa Junior. Hapo
pengine ni saa saba usiku. Amelewa, ni wakumfungulia, na kumsaidia afike
kitandani.” Jelini akacheka akifikiria ndio yalikuwa maisha yake hayo.
“Ila na yeye ni mtu mzuri tu. Si mkorofi. Kwao wamejaliwa
upendo sana. Hata Ester yupo hivyohivyo kama mama yao. Mtulivu mno. Sikupata
shida kabisa nilipohamia kwao. Wote walinifanya nijisikie nipo nyumbani japo kipindi
hicho Noah na Ester walikuwa bado wadogo, zaidi Noah. Alikuwa mdogo sana. Huwa
hata wanasahau kama mimi si kaka yao wakuzaliwa tumbo moja.” “Basi ni
familia nzuri.” “Sana.”
“Na yule mzee pesa haijambadilisha kabisa. Yupo vilevile
tokea zamani.” “Kwamba amefanikiwa sana!?” “SANA. Wewe unafikiri kwa huduma
kama ile wanamlipa mshahara mdogo? Halafu kama unavyomuona. Washirika wake
wanampenda sana. Anaweza pewa zawadi ya mamilioni ya pesa au thamani kama hizo
mpaka ukashangaa. Ila ni mtu wakujali sana. Usiogope. Tutakuwa sawa. Na usijilinganishe
kabisa na ulivyokuwa kwenye familia ya kina Colins. Huku utapendwa na kuheshimiwa.
Nina uhakika kwa sababu na mimi walinifanyia hivyo.” Jelini akatulia.
“Unaswali jingine unalotamani kuniuliza ili unifahamu
zaidi?” “Naona leo nimekufahamu vizuri na kunishangaza.” “Nini tena?” Jelini
akaanza kucheka kisha akamuona anaongeza aibu. Akahisi anachofikiria. Akaanza
kucheka na kumuuliza tena. “Ni nini?” “Ni mengi ila mimi ulivyoniambia wewe na
Junior mnasubiri mpaka ndoa, nikajua…” Ezra alicheka sana. Akacheka kwa
sauti. Akacheka sana.
“Usiniambie umekubali kiss langu?!” Jelini akajificha
akicheka kwa aibu. “Kwamba wewe ulijua hatufanyi kwa kuwa hatujui?!”
Jelini akazidi kucheka na kuuliza. “Sasa utakuwa umejulia wapi kukiss
vizuri hivyo!?” Ezra alicheka sana. “Mimi sijawahi kukisiwa hivyo bwana!”
Ezra akazidi kucheka ila kwa furaha. “Usiniambie kama umenikubali?” “Ila
sasahivi sikumbuki tena.” Akajinung’unisha kwa aibu. Ezra akajua ndio
anaomba kiss ingine. Akajiweka sawa, akamkumbatia vizuri. Jelini mpenda
mikono, akajipanga vizuri. Yakaanza tena.
~~~~~~~~~~~~~~~
Vimenoga kwa Jelini&Ezra.
Ni nini Kitaendelea?
USIPITWE.
0 Comments:
Post a Comment