Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 22 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 22

Huyo Jelini alishatafuta nguo maalumu ya kuvaa siku hiyo. Akatoka hapo bila ya kula akakimbilia saluni. Aliwaambia ana haraka. Maneno mengi kwa anti yake basi akaacha kila mtu akaanza kumtengeneza yeye. Ule upendo na kutotaka kumtoza pesa, akajua tu yake na Mzee Kasa yanamuendea vizuri. Maana alishahama eneo. Akakodi sehemu kubwa sana. Vile alivyopatengeza tu, alijua ni pesa ya Kasa. Hakutaka hata kumuulizia. Akatengenezwa vizuri. Akaingia sehemu ya kuvaa, akavaa kabisa na kutoka kwa haraka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Njiani akampigia simu Ezra, kuwa ndio anaelekea huko ukumbini. Mapigo ya moyo ya Ezra yakaanza kwenda kasi. Ni Jelini. Akatoka kabisa nje ya hoteli kumsubiria. Hata yeye alikuwa amependeza. Mavazi ramsi ya harusi. Aliliona gari la Jelini likiingia. Akasogea kule alikopata nafasi ya kuegesha gari yake.

Akaenda mpaka mlango wa dereva. Akafumfungulia. Ukweli Ezra alibabaika kwa wazi kabisa alipomuona Jelini. Alipendeza kupita kawaida. “Jelini!” Akacheka akijua anachomaanisha. “Umependeza mno! Na hiyo rangi ya gauni imekukaa vizuri sana mwilini mwako!” “Nimefurahi kama umependa. Nilitaka ufurahi. Sitaki kukuabisha.” “Wewe ni mzuri Jelini. Hakuna utakachovaa kikaniabisha. Umependeza sana.” “Asante. Ila na wewe suti yako imekukaa vizuri sana. Imekupendeza na inaonekana ni ya pesa nzuri sana.” Ezra akacheka akiwa kama haamini.

    “Samahani nimechelewa.” “Hamna shida. Nimefurahi umekuja kuungana na sisi.” “Nipo hapa kwa ajili yako wewe Ezra. Mimi hao wengine siwafahamu.” Ezra akacheka kwa furaha. “Basi nimefurahi umeungana na mimi. Asante.” “Karibu. Sasa sasahivi wanafanya nini?” “Ni picha tu. Kuna sehemu nzuri sana humo ndani ya kupigia picha.” “Sasa si utapitwa? Twende ili usikose picha za familia, za ukumbusho.” “Hamna shida. Kuna ambazo nishapiga. Ila nina ombi moja.” Jelini akacheka akikubali.

    “Naomba leo tupate picha moja, nipate za kuweka na mimi kama kumbukumbu.” “Ninavyopenda picha, utachoka wewe.” “Kweli hutaona usumbufu?” “Wewe nisumbue utakavyo.” Akacheka akimtizama. “Aisee siamini! Jelini umependeza kupita hivi ninavyokwambia.” “Asante. Nimefurahi kama nimekuwakilisha vizuri.” “Naona umepitiliza.” Wakapiga baadhi ya picha zao hapo nje. Mpaka Ezra mwenyewe akaridhika ndipo wakaongozana mpaka ndani walipokuta wateja wengine wakila, wakaendelea kwenda upande wa harusini, wanakopiga picha.

    Junior alipowaona wanawasogelea, akaacha umati na kuwafuata. “Jelini umependeza sana!” “Asante Junior. Hata na wewe umependeza sana.” “Asante. Vipi kichwa?” “Kimepoa.” “Pole.” Wakawa wanaitwa hao wawili wapige picha na maharusi bila wasimamizi.

    Ilikuwa wapige hiyo picha na maharusi, wao kina Ezra, na wachumba zao pia. Sasa Junior yeye ndiye anamchumba rasmi, Ezra angekuwa hana mtu. Yaani mchumba. Lakini Jelini si ndio amekuja sasa! Inamaana wangekuwa tayari 6. Picha ingekuwa imekamilika. Wakageuka ili kuwasogelea maharusi watu wakimshangaa zaidi Jelini jinsi anavyovutia.

    “Nafikiri tunaweza piga na Jelini.” Junior akatoa wazo lililomfurahisha sana Ezra. Lakini mchumba wa Junior akadakia kwa haraka na kwa sauti ya juu. “Ni sisi tu na maharusi.” Ikawa kama anamkataa Jelini. Jelini akawa muungwana, maana alishamuelewa kuwa hamtaki kwenye hiyo picha. Akajiwahi ili kuleta amani. “Nyinyi endeleeni tu, mpate picha ya ukumbusho.” “Na wewe unatakiwa kwenye kumbukumbu hii ya harusi. Twende.” “Sasa hiyo itakuwa picha yenu. Hii ni yetu, na watu wanasubiria. Acheni kuvutana. Njooni.” Akasisitiza huyo mchumba mtu, na kufanya kila mtu kubaki wakiwatizama wao.

    Ni kama kile kitu Ezra na Junior hawakukipenda! Jelini hakuwa amemuona mchungaji. Akasikia sauti yake kwa pembeni. “Jelini, mama, umepona kichwa?” Akageuka na kumuona. Akacheka na kumgeukia tena Ezra kabla hajaenda kwa mchungaji aliyekuwa kama anaokoa jahazi katika sakata la picha. “Nenda kapate picha ya ukumbusho, mimi naongea na mchungaji.” Ikambidi Ezra akaungane na maharusi, Junior na huyo mchumba mtu bila wasimamizi.

    “Shikamoo tena.” Jelini akamsalimia mchungaji akimsogelea. Akacheka na kuitika. “Marahaba tena.” Jelini mwenyewe akacheka. “Vile tu kuja nyinyi pale, mimi nimepona kabisaaa. Ujue wewe ni mchungaji mkubwa sana, halafu mchungaji mashuhuri, halafu tena ni mtu mzuri sana?” Mchungaji akacheka asijue kama ni swali au comment! “Kuja nyumbani kwetu ni kama muujiza! Nimefurahi sana mmefika kwetu. Sisi hatupatagi wageni wa maana kama yako. Kwahiyo ukumbuke ahadi yako. Urudi tena. Nitakupikia vitu vizuri vitupu. Halafu vingiii.” “Jelini hujambo?” Alikuwa mama Junior, mke wa mchungaji.

    Akamsalimia na goti la kinyaki. “Umependeza sana binti yangu. Sana.” “Asante mama. Na wewe umependeza, kama mchungaji. Na hongereni kwa kuozesha. Shuguli zenu zote zimekua nzuri sana!” Hao wanafahamiana kwa karibu, tokea Jelini awakodishe vitu vya shuhuli ya huyo binti yao. Ndio ukaribu ukaongezeka na mama mchungaji huyo anayezungukwa na wakina mama wa  maana.

    “Ujue wenzio leo tumetembelewa na mchungaji nyumbani kwetu?” Mama Junior akaanza kucheka. “Tumekuwa wamaana wenzio! Na ameahidi atarudi tena.” “Na mimi nimepewa taarifa. Kichwa kimepona?” “Mimi naona hakitakaa kiume tena.” “Sababu ya mchungaji?” “Kabisa!” Wote wakacheka.

    Akaguswa bega, akageuka. “Ezra!” Hivyo alivyomuita na cheko limemjaa usoni kama ameona alumasi. “Naomba nikatishe mazungumzo kidogo, twende tukapige picha.” “Sawa.” Jelini akakubali bila shida. Wakati Ezra na Jelini wakiwasogelea maharusi, huyo mchumba wa Junior akaondoka hapo kwa maharusi walipokuwa wakipiga picha, kama ambaye hataki kupiga picha nao. “Mbona sasa unaondoka?!” Akauliza Junior kwa mshangao. “Mimi nishamaliza, naendelea na mengine.” Akaondoka.

    Jelini akaendelea kuwasogelea maharusi. “Nyinyi couple yenu nzuri sana. Mmependezana. Na mnaonekana mnapendana sana. Mmependeza mno.” Sasa Ester alishamuona Jelini siku ya kitchen party yake na akajua ndiye mwenye vile viti walivyokalia, wakapata na muda wa kusalimiana na kama kawaida yake, Jelini maneno mengi, akamsifia sana Ester akimpamba kwa maneno mengi. Hao maharusi wakacheka kwa pamoja. “Wewe Jelini kila kitu chako kizuri, mpaka viti!” “Sasa kwani mimi siku ile nilikwambiaje?” “Unapenda vitu vizuri.” Akajibu Ester nakufanya wacheke kidogo.

    “Ila Ester umependeza sana! Na hiyo furaha usoni, inaonekana inatoka ndani yako inakufanya hata ulivyopambwa uvutie! Umependeza sana.” “Asante Jelini. Na nashukuru kwa kuja.” “Mimi mwenyewe nimefurahi kuwa hapa. Acha tupige picha tuwapishe wengine. Tutazungumza wakati mwingine. Nisikuchoshe na maneno mengi, leo siku yako.” Wakapiga picha, na kusogea pembeni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

    Akamshika Ezra mkono kama anayetaka kumnong’oneza kitu, Ezra akampa sikio. “Sasa mbona siwaoni wazazi wako? Au hawajaja?” Ezra akatoa tabasamu fulani hivi, lakini Jelini akajua sio la furaha. “Nitakwambia baadaye.” Jelini akakubali kwa kutingisha kichwa akimwangalia kama ameanza kumuhurumia kutoka na sura iliyobadilika gafla baada ya swali.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Wakaona waondoke hapo, wakatafute sehemu ambayo itakuwa na sehemu ya kukaa. Wakaenda sehemu ya wateja wengine ambao hawaja hudhuria harusi hiyo, nje tu, karibu na baharini. Wakakaa hapo wakisubiria kuingia ukumbini. “Samahani kwa kile kilichojitokeza pale kwenye kupiga picha.” “Wala usijali. Najua kila mahali kuna mipango yake. Ila ujue nimefurahi umekuja kuniona. Nimefurahi sana Ezra. Sikutegemea!” “Nakupenda Jelini. Naona tatizo lako ni langu. Sitaki upate shida peke yako.” Jelini akacheka kidogo na kupotelea mawazoni. Akajua amerudi kwa Colins kimawazo.

    “Samahani sijakupa jibu juu ya Colins mpaka sasa.” Akamshitua Jelini na kumrudisha hapo kimawazo. “Hap…” Kabla Jelini hajamalizia anachotaka kusema, wakasikia Junior akimuita Ezra. Wakageuka kwa pamoja “Mbona mmejificha huku!?” “Nimeona kuna upepo mzuri. Vipi?” Akasogea Junior kama mwenye kitu chakutaka kusema, akasita. Ezra na Jelini wakabaki wakimwangalia. Alikuwa bado amesimama.

    “Labda niombe radhi kwa kile kilichotokea pale kwenye picha. Tafadhali usijisikie vibaya. Hope ni mtu wa mipango. Na ikiwekwa anapenda kuisimamia.” “Usijali kabisa. Mimi mbona naelewa tu. Mambo hayawezi kwenda vizuri bila utaratibu. Ona kulivyopendeza! Hongereni sana.” “Asante.” Jelini akawaona bado hawapo sawa.

    Akaona abadili hiyo hali. Akaanza kucheka. “Sasa unacheka nini?” Junior akamuuliza na yeye akianza kucheka. “Kwa hiyo nyinyi mpo kama mapacha? Maana na suti zenu nzuri, halafu pia zimefanana!” Wakacheka. “Mmependeza sana.” Angalau Junior akaweza kukaa hapo.

    “Kwani nyinyi mmefahamiana kwa muda gani?” Wakaangaliana na kucheka. “Tokea kidato cha kwanza. Shule ya sekondari Pugu. Tulipangiwa bweni na cubic moja. Kuanzia hapo ndio tukawa pamoja.” “Mpaka chuo!?” “Alichosomea Ezra, na mimi ndio nimesomea. Alama alizopata yeye darasani na mimi hivyohivyo.” “Basi mlikuwa mkiigiliziana.” Wakaanza kucheka.

    “Jelini! Sasa kwa nini usiseme tulikuwa tukisoma pamoja?” “Ndio mpate kila kitu sawa!? Mimi nina wasiwasi na nyinyi bwana.” Utani ukaanza hapo. Wakajisahau.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Akawafuata kijana mmoja hivi, akaanza kuongea kabla hajawafikia. “Mnaitwa na dingi.” “Acha kumuita hivyo bwana!” Akakoroma Junior akisimama, yeye akikaa. “Sasa mbona wewe unakaa?!” “Anawaita nyinyi. Sio mimi. Maana anataka kunichanganya tu. Bora nikae hapa.” “Huwezi kukaa hapa wakati muda wa kuingia ukumbini umefika. Acha kumkorofisha mzee, wakati unajua leo ni siku ya Ester. Twende.” Junior akazidi kumsisitiza. “Kwani nyinyi mnajisikije bila kuniona mbele ya macho yenu kila wakati? Si nimesema nakuja!?” “Acha ubishi Noah. Twende.” Ezra akaweka msisitizo. “Au unataka na sisi tutumwe kuja kukuita?” Ezra akaongeza swali.

    Mara huyo Hope akaja na yeye. “Mbona mnatafutwa, halafu nyinyi mmejificha huku?” “Hatukuwa tumejificha, tumekaa tu huku kwenye upepo mzuri. Vipi?” Akajibu Junior akimsogelea. Jelini na Ezra walishakuwa wamesimama tangia aanze kulalamika. Jelini alishamuona ni kama hajampenda, na yeye akajituliza. Huyo Noah akawa amebaki amekaa tu akiwatizama.

    “Huyu ni Jelini.” Junior akawa anatoa utambulisho kama kutaka wafahamiane zaidi. “Namfahamu. Si anafanya biashara ya kukodisha vitu vya harusi huyu? Namfahamu vizuri sana.” Akajijibu mwenyewe ila kama kwa dharau kidogo akimpuuza huyo Jelini. Akafupisha kabisa utambulisho na kuongeza. “Mnatafutwa. Tusiendelee kupoteza muda hapa, tukitengeneza mapumziko yetu, au kikundi kingine wakati leo ni shuguli ya Ester. Sio sawa. Twendeni.” Akajibu hivyo na kuongoza njia. Junior alipoa, mpaka ungemuhurumia. Ezra akamgeukia Jelini, akamshika mkono akamuongoza njia. Jelini akawa anamfuata kwa nyuma, kimya.

Ukumbini.

    Walipofika ukumbini, Ezra akafanya makusudi kujivuta mpaka wote wakaingia na kukaa, akaenda kutafuta sehemu ya kukaa kama waalikwa tu wengine, Jelini asijue kuwa walishakuwa na sehemu maalumu ya kukaa hao ndugu wa bibi harusi. Tena akatafuta sehemu mwisho kabisa ya ukumbi kama anayeepusha shari. Shuguli ikaanza, ndugu wa bibi harusi wamekaa sehemu maalumu upande wa mbele kabisa. Ukweli ilikuwa shuguli ya kifahari. Kwamba huyo Ester alikuwa akiolewa pazuri. Jelini na Ezra wakajituliza hapo nyuma.

    Alipomuona Ezra amepotelea mawazoni, akavuta kiti karibu yake kabisa, akamchukua mkono wake na kuupakata vizuri. Ezra akatoa tabasamu. “Hii harusi inaonekana imeandaliwa kwa kiwango cha juu sana!” “Jamaa mwenyewe anayo pesa.” Akajibu Ezra. “Nimefurahi upo hapa na mimi.” “Mimi mwenyewe nimefurahi tupo wote.” Hapo wanaongeleshana wapo karibu, wanaangaliana kana kwamba ukumbi mzima wapo peke yao, mambo yakiendelea.

    Katikati ya harusi ikawa kama Junior ndio amempata Ezra. “Mbona mmekaa huku!?” Jelini akamtizama Ezra. “Nimeona hapa patatufaa. Hamna shida. Vipi?” “Nilikuwa nikiwatafuta, muda wa utambulisho. Twendeni.” “Nakuja.” Akajibu Ezra. “Na Jelini?” “Naomba yeye tumuache tu. Ila mimi nitakuja.” Junior akafikiria kidogo, akaona akubaliane naye. Akaondoka.

    “Unisubiri, nitarudi baada ya utambulisho.” “Hamna shida.” Wakaangaliana kwa muda, Jelini akacheka taratibu na kuinama. Akambusu shavuni na kusimama kisha akarudi kumnong’oneza. “Nakupenda Jelini. Usije sahau.” Kisha akaondoka bila yakusubiri jibu, ila ni kama alibadilika. Hakuwa na ile furaha aliyomkuta nayo alipoenda kumpokea garini. Akajua mambo ya Hope hakuyafurahia. Jelini akatulia na kupotelea mawazoni.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Mchungaji akapewa nafasi ya kutambulisha alioongozana nao. Jelini akajiweka sawa. Akaanza kusema kuwa Ester anao kaka watatu. Junior, Ezra na Noah. Ndipo akaelewa Noah ni kijana wa mchungaji. Swali likabaki ni mdogo wa Ezra au Junior wa kuzaliwa tumbo moja? Lakini mchungaji akaongeza kuwa akitoka huyo Ester ndio Junior kijana wao wa mwisho. “Sasa huyu Ezra yeye wazazi wake na ndugu zake wa kuzaliwa pamoja mbona siwaoni?!” Akajiuliza macho mbele.

    Hapo mama mzazi wa Ester alikuwa pembeni ya mumewe. Kisha akasikia akitambulishwa Hope ambaye ni rafiki kipenzi wa Ester na mchumba wa Junior. “Kumbe hawa wapo serious!” Akajiwazia Jelini akisikiliza utambulisho na vigelegele. Mchungaji akatambulisha wote mpaka kina bibi na babu za bibi harusi, lakini akamalizia na utambulisho uliomshitua sana Jelini.

    “Yupo mgeni wetu mwingine. Na leo nilikuwa naye baada ya ibada. Hapa nimemtizama simuoni tena. Lakini naye ni binti yangu, rafiki wa Junior na Ezra. Jelini upo wapi, mama?” Jelini alishituka, akatamani kuingia chini ya meza ila ikabidi asimame kupunga mkono lakini akaitwa pale mbele walipo ndugu wote. Ikabidi aende kwa haraka ila akasogea alipo Ezra, maana alimnyoshea mkono kama anayempokea. Akamvutia karibu yake. Akatulia pembeni ya Ezra.

    “Jamani kazi mliyonipa, nimekamilisha kwa ufupi. Hawa ni wachache wanao wakilisha familia yangu. Nina watu wengi sana. Nikiendelea hapa, nitaharibu ratiba nzima. Kwa hiyo kama kuna picha ya ukoo wa Ester, naomba hawa wawakilishe.” Ezra na Junior wakajua mzee amefanya makusudi kutaka picha ya familia na Jelini akiwepo ili kutuliza lile tukio zima la picha kule nje.

    “Tafadhali tunamuomba na Ester apate picha na sisi. Ikawe ukumbusho wake. Awe anakumbuka na wanyumbani.” Mchungaji akaongeza na kuamsha vigelegele. Vikashamiri wakati bibi harusi akiwa anashuka jukwaani walipokuwa wamekaa maharusi, ili kuungana na hiyo familia yake. Baba yake akaenda kumpokea akicheza. Watu wakazidi kushangilia maana Ester naye akaanza kucheza na baba yake, wakirudi pale walipoacha familia. Ukweli ilipendeza sana. Walijawa cheko muda wote. Zikapigwa picha za kutosha, Jelini na Ezra wakarudi kule walipokuwa wamekaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

    Mc akatangaza ni wakati wa keki. Hilo zoezi likaendelea likawa linafuatiwa na chakula. Ndugu wa maharusi waliokuwa wamekaa viti vya mbele, walitakiwa waongozane na maharusi. Inamaana Ezra alitakiwa kuwa mbele kwenye hivyo viti maalumu, lakini akawa nyuma na Jelini. “Nenda mimi nitakusubiri.” “Unataka nikuletee nini?” “Chochote utakachopenda wewe, mimi nitakula.” Ezra akasimama na kuondoka.

    Baada ya muda akashangaa Ezra na Junior wanakuja pamoja, halafu Noah amewabebea vinywaji na chakula chake amebeba Junior. Ikabidi wale waliokuwa wamekaa nao kwenye ile meza, wawapishe, wahamie meza ingine ya pembeni. Ilikuwa na nafasi. Wakawashukuru. Jelini akacheka akiwatengenezea mazingira ya kuweka chakula, Ezra akamuwekea sahani yake yenye chakula na kinywaji. Halafu wote wakakaa hapohapo mezani, wakaanza kula huku mziki wa taratibu ukiendelea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

    “Unakunywa nini Noah?” “Hivi unajua nimeondoka kule mbele sababu ya maswali kama hayohayo, bro! Tafadhali niacheni leo nifurahie.” “Mbona swali dogo tu lakini unapaniki? Unakunywa nini?” “Si unaona ni kopo la Coca hili!” “Lakini ni kinywaji gani kipo ndani? Na ukumbuke ahadi uliyomuahidi mama na baba.” “Siwezi kulewa hapa. Wewe usijali. Hapa nashitua tu, nikitoka hapa ndio naenda sasa kunywa.” Junior akamtizama na kuendelea na kula.

    “Kule nje utambulisho wako ulikatishwa. Wewe ni nani tena?” “Wewe hukusikia baba akimtambulisha pale mbele?” Junior akamuuliza, akaanza kucheka. “Usipoangalia bro, familia yako itakua ya kijeshi aisee! Maana demu wako ni afande aliyekimbia kwata. Naona na wewe ameanza kukuambukiza. Hukuwa hivyo! Maana kuna ubaya gani kufanya mazungumzo na mtu ambaye mimi nataka kumfahamu? Maana demu wako wazi kaonyesha hataki undugu naye. Sasa mimi ninayeonyesha…” “Umeshalewa Noah, na wakati leo umeahidi watu wote hutalewa. Siku ya leo umesema unampa Esta.” Ezra akaingilia lakini Noah akaanza kucheka tena, kama asiyejali.

    Akamgeukia Jelini. “Mimi naitwa Noah. Wewe ni nani mwenzangu?” “Naitwa Jelini.” “Safi sana Jelini. Kwanza bwana wewe umzuri sana. Halafu umependeza sana.” “Asante Noah. Na wewe umependeza.” “Ila sasa wewe kupendeza kwako si kwa mavazi! Yaani wewe ni mzuri haswa. Jelini wewe mkali bwana! Halaf…” “Inatosha Noah.” Akazidi kucheka. “Hutaki nimpe sifa zake, bro? Nani atamsifia kama sisi wakaribu yake tuna….” Wakamuona anaangalia mbele kisha anaficha kopo lake hilo la Coca. “Mzee huyo!” Akainamia sahani yake. Kimya.

    “Kwa nini nyinyi mmekaa huku nyuma, wakati nawategemea kule mbele?” “Mimi nakuja baba.” Noah akawahi kwa makusudi tu. “Namaanisha Ezra na Junior. Wewe umeshalewa. Na nakuomba utulie.” “Unapata dhambi za bure baba yangu! Sasa mimi nimelewa saa ngapi, wakati unaniona nakunywa Coca?”  Hapo anajitetea na cheko. “Tafadhali naomba muhamie mbele ili tutoe zawadi ya familia pamoja. Na Noah, tafadhali usiku wa leo naomba uishe vizuri. Mama yako aondoke hapa na furaha.” “Sawa baba.” Akakubali akicheka.

    “Na ameuliza.” Akawa kama anasita kusema alichotumwa na mkewe. “Amesisitiza ule.” Akaona amalizie tu hivyo. “Lakini hivyo sivyo ulivyotumwa baba! Kwani wewe umetumwa nini?” Noah akamuhoji na tabasamu kubwa akijua hataki kusema, anaona si muhimu.

    “Achana naye baba. Wewe mwambie mama tupo naye na atakula.” Junior akamsaidia baba yao, akaondoka. “Familia hii bwana! Sasa mtu anatumwa, lakini hataki kufikisha ujumbe wote. Kama sijapata kitu chakula ninachokipenda? Maana pale nahisi nyama nimepunjwa na mama anataka kujua hilo.” “Tafadhali muache mama, Noah. Mwache apumzike na afurahie. Wewe unataka kufuatwa nyuma kila siku kama mtoto mdogo!” Ezra akawa kama anamgombesha. “Na nyama ya nyongeza hii hapa. Usiende kumsumbua mama.” Junior akamuongeza nyama kutoka kwenye sahani yake. Noah akashukuru akicheka, akaendelea kula nyama tu bila kitu kingine.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

    “Tafadhali naomba utangulie Junior ili nibaki na Jelini. Nitakuja wakati wa zawadi. Asikae hapa muda mrefu peke yake.” “Mimi nitabaki naye.” Akajitolea Noah. “Tunashukuru kwa msaada wako, lakini hapana.” “Watu hawana imani na mimi!” “Naomba uhamie mbele  Noah. Namaanisha uondoke sasahivi.” Noah akasimama akicheka. Akamimina kinywaji chote kilichokuwa kwenye kopo mdomoni, kisha akachukua Coca ya kaka yake, akajiwekea kwenye hilohilo kopo na kuondoka akicheka.

    “Nakwenda kuangalia viti kule mbele. Nikipata vya kututosha, nitakutumia ujumbe mje.” “Wazo zuri.” Junior akaondoka. “Naomba kukushauri Ezra. Hii shuguli ni leo tu. Mimi na wewe ni mpaka kifo.” Ezra akacheka na kumbusu shavuni. Jelini akafurahi huyo, akashukuru akicheka. “Nafurahi kusikia hivyo! Hujui tu.” “Nashauri nenda ukawe nao. Mimi nakusubiri hapa. Ikiisha, tutapata muda wetu.” “Nashukuru kwa ushauri wako, lakini siwezi kukuacha hapa Jelini. Akili yangu itashindwa kufanya kazi kabisa. Hujui ni kiasi gani nathamini kila sekunde ninayokuwa karibu na wewe. Nataka kuwa na wewe kila wakati.” Jelini akacheka na kumbusu na yeye shavuni, wasijue watu wanawatizama, wao hawana habari.

    Junior akatuma ujumbe kuwa amepata nafasi yao, wahamie mbele. “Tafadhali naomba nivumilie Jelini. Siwezi kumuacha Junior peke yake. Hatatulia kule mbele, na ndio tutasababisha kufuatwa huku nyuma na kila mtu. Naomba tuongozane, tukakae mbele. Nahisi wanakaribia kumaliza.” “Wewe wala usihangaike kuniomba. Ulipo ndipo nitakuwepo. Niongoze vile utakavyo.” Wakaongozana mpaka alipokuwa Junior.

    Meza moja na Hope pamoja na Noah. Wakamuweka Jelini katikati yao. Wakatulia hapo. Lakini baada ya muda mfupi sana, Hope akasimama na kuondoka. Hakurudi kukaa hapo tena mpaka harusi ilipoisha. Jelini hakujua alihamia wapi, na hakutaka kugeukageuka asije zua jingine. Akajituliza na kunyamaza.

    Iliisha muda mzuri tu. Saa tatu wakawa wamemaliza. Ezra akamuaga Junior kuwa atakuwa na Jelini, mpaka muda wa kwenda kulala. “Tunaweza kuzungumza hapo nje kabla hamjaondoka?” “Bila shaka.” “Acha niwaage mchungaji na mama mchungaji. Nisiondoke kimya kimya.” Jelini akajipenyeza katikati ya umati uliokuwa umewazunguka, maana na wao walikuwa wakipokea pongezi ya kuozesha binti yao wa pekee. Akaaga na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ndio Mwanzoni Tu, Na Huku Nako, Anakutana Na Kipingamizi Kingine.

Kule Ilikuwa Love, Huku Hope.

Mambo Yanaendelea.

Je, Itakuwa Ni Kuruka Majivu NA Kuishia Kukanyaga Moto?

Kule Colins Alipambana, Wazazi Wakamshinda Nguvu. Je, Huku Ezra Atafanyaje?

Je, Ni Bora Jelini Kurudi Alikotoka (Colins) Au Aendelee Tu Na Safari(Ezra)?

Kwani  Ni Nini Shida Ya Hope Kwa Jelini?

INAENDELEA.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment