Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 21 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 21

James aliitizama ile hali, akaumia sana. “Acha nikwambie ukweli mama Jema.” Akaanza James baada ya Jelini kutoka na yeye akikimbilia saluni. “Wazazi wanamchango mkubwa sana kwenye maisha ya watoto wao. Wanaweza kuharibu au kujenga. Nitakwenda kuzungumza na familia ya kina Colins, na Colins mwenyewe. Lakini mama Jema, hiki wazazi wa Colins wamefanya, na mimi nimetaka kumsababishia dada yangu. Nimeangalia hapa, nakuumia sana. Sina tofauti na wazazi wa Colins.”

Akamsimulia mama Jema juu yake na Bale. Hakumficha kabisa. “Lakini ona heshima aliyoweka huyu mchungaji hapa! Haijachukua hata lisaa. Lakini ameweka msingi ambao si rahisi si kwa Ezra tu, hata kwa Jelini mwenyewe, hawezi kuuvunja. Hawa wawili kuanzia sasa, watatembea wakijua jicho la wazazi lipo kwao. Hata wakikumbana na changamoto zingine, wanazisogelea kwa kuzitatua si kukimbiana.”

“Najua usingependa kulisikia hili, lakini mama Jema, kwa hakika namuhurumia sana Colins. Anampenda sana Jelini. Na anamkosa kwa sababu ya wazazi kuchangia. Acha na mimi nijitoe kwenye mahusiano ya dada yangu.” James na yeye akaaga.

    Akiwa garini anataka kuondoka akashitukia mama Jema anamfuata tena kumpa maagizo ya kina Colins. Kwamba akifika huko, asije sahau pointi za msingi za kuzungumza nao. Aliongea kwa msisitizo na kwa kituo kama aandike, ili wamuelewe na wasije sahau. James aliposema ameelewa na atafikisha ujumbe kama ulivyo, ndipo akamruhusu kuondoka.

Heshima Haiombwi.

    Njiani akaona ampigie simu Bale. “Mnaendeleaje?” “Aisee sisi niwazima kabisa, tunamshukuru Mungu, ila sipo na Vai.” Alishituka James, akajua ameshamuharibia dada yake. “Kwema!?” “Kwema kabisa. Anamitihani ya vitendo kesho, nimetoka kumshusha hosteli akajisomee na wenzie.” James akahema kwa nguvu kama aliyepata aghueni.

“Mnaendeleaje na familia?” Akauliza Bale. “Sisi ni wazima kabisa, ila nilitaka kukushukuru kwa jinsi ulivyojitoa kwa Vai. Asante sana Bale.” Bale hakuamini, akapata ububu.

    “Acha niwe mkweli kwako. Vai na Viola wamekua ni kama wakijiangalia wenyewe kwa muda mrefu. Najua nimezembea kwa sehemu fulani. Ni kweli niliwakatia tamaa. Hichi anachokifanya Vai, sikujua kama anaweza kuja kukifanya, na najua unachangia Bale. Asante sana.” Alijishusha James, usingetegemea azungumze hivyo na Bale. Dunia shule ya kila mtu. Lazima ujifunze tu.

    “Nampenda Vai, James. Namuhesabu ni kama nawajibika kwake moja kwa moja. Ni sehemu yangu. Na Vai ananipenda kwa dhati. Amenivumilia nikiwa sina kitu kabisa. Sitaki mtu mwingine aje afaidi alikopanda yeye. Anastahili kula kila matunda yangu. Nampenda Vai. Na nitakusubiria bila kuchoka, mpaka mnipe baraka zenu, nimuoe.” Akaongea Bale kama anayemsihi James.

    “Kama ni kumuoa, ulitaka iwe lini?” “Akiwa likizo. Atakuwa na likizo ndefu tu. Naweza kufanya yote, na mpaka anarudi chuo tunakuwa tumemaliza. Joshua ameniahidi kunisaidia mpaka nikamilishe maswala ya ndoa. Na nakuhidi sitamuharibia maisha. Nitahakikisha anamaliza chuo. Na kumtunza vizuri.” “Nakamini Bale. Kitendo cha kuwepo chuo mpaka leo! Najua kwa hakika unachangia.” Ukweli alimfanya Bale ajisikie vizuri.

    “Acha nizungumze na mzee, nitampa Joshua taratibu zote. Lakini kwa sasa wewe ndio umtaarifu Joshua. Ninaona unastahili heshima yangu Bale. Sio sawa kukutumia majibu kwa kupitia Joshua. Wewe ndiye unatunza dada zangu. Naona bora nikurudishie hiyo heshima.” “Nakushukuru sana James. Asante.” Akaaga bila mengi zaidi, huku akielekea nyumbani kwa kina Colins.

~~~~~~~~~~~~~~~

    Hapohapo akamtumia ujumbe Joshua. ‘Mungu wa Elia, amejibu kwa moto. James amekubali nimuoe Vai. Anakwenda kuzungumza na baba yao. Atakupa taratibu zinazofuata.’ ‘Hongera sana. Nitamsubiria wakati na sisi tukijipanga. Nina uhakika kila kitu kitakuwa sawa Bale. Lakini wakati tukisubiria, tafadhali fuatilia ile hati ya kile kiwanja chako. Naomba iwe kipaumbele. Huwezi kuendelea kuishi hapo ukiwa unafamilia.’ ‘Sawa. Lakini sina pete ya kumchumbia Vai. Nataka pete nzuri SANA.’ Joshua alivyosoma hivyo akacheka na kumjibu. ‘Nitakupigia, tujipange kuoa kwa heshima.’ Bale alifurahia sana kusikia hivyo. Ni Joshua! Kwake haliharibiki jambo.

    Akatulia akianza kujifikiria atakavyoishi na Vai kama mkewe. “Vai ni mzuri sana.” Akaishia kuwaza hivyo akicheka. Kisha akamtumia ujumbe Vai mwenyewe. ‘Nakupenda Vai.’ Hapo hapo Vai akamjibu. ‘Ushani miss?’ ‘Tokea nakushusha hapo.’ Vai akacheka. ‘Na mimi nakupenda Bale. Kesho tutakuwa wote, usijali. Nenda mazoezini kupoteza muda. Usiwe mpweke muda mrefu.’ ‘Naona nitafanya hivyo. Wazo zuri. Maana naona tokea uondoke hapa, dakika hazisogei kabisa. Nakwenda gym.’ Vai akacheka alivyosoma hivyo.

Bale akapata wazo na kumtumia ujumbe James. ‘Tafadhali usimwambie Vai kama umetoa baraka zako, kwetu. Nafikiria jinsi ya kum surprise na pete ya uchumba.’ James alisoma akiwa kwenye mataa akielekea kwa kina Colins, na kujibu tu kwa kifupi. ‘Sawa.’

Kwa kina Colins.

Alifika nyumbani kwa kina Colins akakuta kumetulia, ila wote wapo sebuleni, kasoro Colins. Akasalimia na kukaa. “Vipi Colins?” “Yupo hapo chumbani.” Akatulia kidogo asielewe ile simanzi ni ya nini wakati Colins amerudishiwa ufahamu wake, inamaana ni kama nusu ya uponyaji wake! Asijue kilichokuwa kikiendelea usiku uliopita. Akaomba kwenda kumuona Colins, akakaribishwa. “Ila nilikuwa na ujumbe wenu, kutoka kwa mama Jema. Nitaomba nafasi na nyinyi wote ili mnisikilize. “Bila shaka.”

~~~~~~~~~~~~~~~

    James akaingia chumbani kwa Colins. Akakuta hajalala, ametulia tuli kitandani, macho kwenye luninga. Akamtizama alipoingia. “Vipi?” Colins akajiweka sawa. “Sasa hivi unafanya kazi na nani? Maana kwa muda wote huo ambao sikuwepo pale, si watakuwa wamejaza nafasi yangu?” Akauliza taratibu tu kwa sauti ya chini, lakini James aliweza kumsikia na kumuelewa. “Ndiyo.” Akatulia.

    “Vipi lakini?” “Nimegundua nimepoteza miezi kama 10 ambayo sina ufahamu wa kuiishi kabisa!” “Hukumbuki chochote kabisa!?” “Ilikuwa kama ndoto. Wewe si unajua ndoto? Hapakuwa na uhalisia halisi. Kumbukumbu nzuri ziliniishia siku wazazi na Love walipokuja kwangu, wakanilazimisha maombi, na mimi nikipambana kutoka ili nimuwahi Jelini. Yule mtu aliyekuja nao aliponifunika kitambaa usoni, nahisi nilipoteza fahamu. Ndio sikumbuki tena. Yaani jana ndio nimejua imeshapita zaidi ya miezi 10 tokea siku ile.” James akakaa kama mwenye mengi kichwani. Kimya kikapita kwa muda ila akimuhurumia sana Colins.

Akawa kama amekumbuka kitu. “Aisee samahani leo nimechelewa kuja. Siku ya ibada leo. Nakwenda na familia. Kama upo tayari tukaoge.” “Nashukuru. Nipo sawa kabisa. Labda unisaidie kutoka hapa ndani, angalau nione nje.” “Una madonda kwenye nyayo mzee, utakanyagaje? Sio tutayatonesha zaidi?” “James. Ipo wheelchair. Unaweza tumia. Acha niifungue ipo hapohapo chumbani.” Akaingia mzee kwa haraka. Akaifungua na James akamuweka hapo.

    Akamtoa mpaka sebuleni. “Sasa kabla sijamtoa Colins nje, tafadhali naomba nifikishe ujumbe kutoka kwa mama Jema. Na maadamu wote mpo hapa, naomba niwakilishe.” Wazazi na Connie pamoja na Colins wakabaki wakimtizama James. Akaona akae kwa kuwa na wao walikuwa wamekaa.

Tajiri Na Mali Zake, Msikini Na Mkokoteni, lakini ni wake!

    “Labda nianzie mbali kidogo.” Akaanza James. “Jelini alipokuwa shule ya sekondari, kuna mwalimu alikuwa akimbaka na kuwa akimpiga sana akimtishia asiseme. Atamuua mama yake na Jema. Nafikiri alishajua hawana mzazi wakiume, wanalelewa na mama tu. Akatumia huo mwanya kumtumia Jelini vibaya sana. Jinsi alivyoeleza, alikuwa mpaka akimtuma kwake, kisha kwenda kumtumia huko vibaya, kikatili kisha kumpiga akimtisha asiseme.” James akaendelea.

    “Kile kitu kikamuathiri sana Jelini, na hakuweza kusema. Ikaendela hivyo mpaka akashika mimba ambayo pia anasema alipomwambia, alimpiga mpaka akapoteza fahamu. Na kumtisha asije sema. Akafukuzwa shule. Nyumbani akijulikana kama mtoto mbaya sana. Swala la shule akawa hataki tena, akijua historia itajirudia. Hicho kitu kikazidi kumuhuzunisha mama yake wasijue jinsi ya kumsaidia.”

    “Baada ya yote akajaliwa mtoto, akiwa nyumbani, hataki shule wala kazi, ndipo akakutana na rafiki aliyemtambulisha pombe. Alipogundua uwezo wa pombe kuwa unaweza kunywa halafu usikumbuke chochote kwa muda, akaanza ulevi, akishinda baa na sehemu yeyote inayopatikanika pombe au anayoweza fikia pombe, ili tu alewe. Si kunywa kama ladha, alikuwa akitafuta ile hali ya kulewa ili asikumbuke yale mambo aliyokuwa akifanyiwa na yule mwalimu. Shule hataki, na akaingiwa na hofu ya ajira pia. Hataki kuajiriwa akihofia asije angukia kwa bosi ambaye anaweza mfanyia kama yule mwalimu.”

    “Kwa hiyo, akawa mtoto ambaye yupo tu. Sehemu zinazo patikana pombe ndio ikawa sehemu yake rafiki. Ni mwaka jana tu, ndipo ameweza kusema na yule mwalimu kukamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Ikawa kama nafuu ya Jelini, wameanzisha biashara na mama yake. Kwa mara ya kwanza maishani, Jelini ameweza kutulia na kufanya kitu kinachoeleweka. Na ukweli anajuhudi sana. Japokuwa hajasoma kwa viwango vya juu, lakini anaakili ya biashara kama mama yake. Chochote unachomuona anacho sasahivi, ni juhudi yake yeye mwenyewe Jeilini, akifikiria na kujituma mchana na usiku.” James akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Hili hata Colins analijua. Mama Jema anajua watu wanadharau binti zake sababu wanalelewa na yeye ambaye watu wanamuona ni duni, hawana baba. Kitendo kama kile mlichomfanyia yeye. Kumfuata nyumbani kwake. Mbele yetu sisi. Mkimtusi na kumpa shutuma mbaya sana. Huku mkimdhalilisha kwa sauti ya juu, anajua kwa asilia 100, hamuwezi kufanya hivyo kwenye familia kama hizi zenu, jamii yenu ya wasomi, iliyowazunguka.” Hapo James akawapa sekunde kadhaa za kuingiza hilo kichwani.

    Kisha akaendelea kwa msisitizo. “Nikimaanisha hivi, mlichokifanya kwake na binti yake, ni kweli bila kupinga, kuwa hamuwezi kwenda kufanya hivyo kwenye nyumba ya kina Love.” Hapo James akaweka tena kituo akiwatizama kwa zamu.

“Ukimya huo, unaashiria ni kweli. Sidhani kama baada ya kujua alichokifanya Love kwa Colins, nisiseme sana, pengine mlishaenda kwa kina Love, mkafanya kama mlichokifanya kwa Jelini.” Kimya. “Kwa ukimya huo, inamaana, japokuwa kwa Love mnao uthibitisho wa ubaya wote, lakini hamtakwenda kufanya kama mlichokifanya kwa mama Jema, na binti yake, mbele yetu.” Akaendelea.

    “Sasa amenituma niwaambie, mlichokifanya kwake lilikuwa ni kosa kubwa sana. Kwanza kisheria, pili hata mbele ya jamii. Mlimfuata nyumbani kwake, mkamfanyia fujo mbele ya watoto wake, mkimtupia tuhuma mbaya na za uongo, kwamba yeye na binti zake, ni wachawi.” Colins kimya akisikiliza lakini machozi yakimtoka kama mvua.

    “Mama Jema anasema, amelinyamazia hilo. ILA. Hapo ameweka msisitizo. Kitendo cha kumfuata Jelini. Popote alipo. Nakumtoa kwenye kile ambacho mlimtukana mkimsema vibaya hawezi kukifanya. Sasahivi Jelini anaendesha maisha yake vizuri na kwa utulivu, nafikiri mmemuona. Yupo bora kuliko hata wasomi wengi tu, mama Jema anasema HILO ni kosa ambalo, hatalinyamazia, na hatasamehe.”

    “Ameomba rasmi. Mtu yeyote wa kutoka hapa kwenu, asipotee njia hata kwenda kununua kitu dukani kwa Jelini. Asiwahi kusikia mtu anamsogelea Jelini hata kwa salamu. Ameomba, alipo Jelini, nyinyi msiwepo. Na ikitokea mnamuona sehemu, mumuwache kabisa. Anasema mlisema wazi kabisa, ‘hamtaki mtu kama Jelini awe na kijana wenu’, anasema walitii, wakakaa pembeni. Anaomba ibakie hivyo.”

    “Amenituma ramsi, niwaambie, kukiuka haya, nikutangaza vita na yeye. Na amenituma kuwaambia, katika hiyo vita, yeye atashinda, na mtakimbia huu mji. Naomba niweke msisitizo. Kwa sasa haya maneno yanaweza kusikika ni kama vitisho tu. Lakini jamani, nawasihi, mfanye kama sisi tulivyoheshimu maneno yenu. Tulikaa mbali. Hamtaki kuingia ugomvini na mama Jema. Hamtamuweza. Atawashitaki vibaya sana. Mpaka mje mmalizane naye, haitaleta maana tena.”

    “Maadamu mmepata mlichokuwa mkikihangaikia japo si kwa njia sahihi, basi tukae kwa usalama. Jelini hatarudi tena hapa. Inamaana kile mlichotamani kukiona kwa kijana wenu, hatimaye kinakua. Sasahivi nyinyi wazazi wa pande zote mbili mmeshinda, kasoro Colins, na najua wazi hata Jelini anampenda sana Colins, lakini mmesaidia kuwatenganisha kwa nguvu nyingi sana. Kwa hakika mmefanikiwa.”

    “Niombe tuanze sasa, kuishi kuanzia hapa. Tujenge mahusiano mapya mkijua hawa watu hawapo tena kwenye maisha yenu, Colins yupo huru. Ni hilo tu. Nyinyi ndio mpo kwenye nafasi ya kutekeleza au kutotekeleza hayo ya mama Jema. Mimi ni mjumbe tu.” Pakazuka ukimya. Akasimama. “Basi acha nimtoe Colins hapo nje.” Hakuna aliyejibu. James akazunguka nyuma ya kigari na kumtoa Colins nje.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

    Alipotulia akamgeukia James. “Bado una mawasiliano na Chaz?” “Ndiyo, lakini siku hizi anafanya kazi kule Car wash. Nimempa kazi kule.” Akawa kama amekwama. “Ulitaka nini?” “Nataka mtu wakunisaidia kwa kama majuma mawili tu. Nina uhakika baada ya hapo nitaweza kujitegemea.” “Nitazungumza naye. Nahisi yeye atatufaa kwa sababu kwanza anakufahamu, halafu hanaga shida. Yeye bora pesa iingie.” “Nitashukuru sana.” Akatulia hapo kwa muda akitafakari kwa kina maisha yake kuanzia hapo. Kimya kati yao kama waliopoteza mtiririko mzima wa mazungumzo yao, wakati walikuwa marafiki waliokaribia udugu! Maisha yamewabadilikia! Kimya chakutosha kikapita. Baadaye akaomba arudishwe chumbani.

Aluta Kontinua.

    Ilikuwa lazima maisha yaendelee kwa picha yeyote ile. Sasa yanaendeleaje! Ndio hapo. Alipoingia hapo sebuleni akaomba James asubiri. “Baba!” Mzee akamwangalia, japo kwa shida. “Naomba ukitoka, nisaidie vitu vya mazoezi ili nianze kujenga misuli tena. Najihisi mwili hauna nguvu kabisa. Nahitaji kuanza taratibu kurudisha uelewa na kwenye viungo vyangu pia.” “Sawa.” Kisha akamgeukia mama yake.

     “Naomba nisaidie virutubisho vya aina yeyote ile ila vyenye uhakika kunisaidia kuupa mwili nguvu kwa haraka na kuujenga kuanzia ndani. Unaweza kuchanganya. Vikawa vya hapa nyumbani lakini zaidi naomba vile vyakunywa kama GNLD. Nirudishe virutubisho vilivyopotea.” “Sawa.” Akakubali mama mtu.

    “Halafu baba, kabla ya kulala usiku, tafadhali naomba uje chumbani, tujipange jinsi ya kuweza kulinda ile kazi kule kwenye hospitali yenu. Ili nikipona, nirudi kazini. Au unafikiri watakuwa wameshapata mtu mwingine?” Hawakuamini. Lakini mzee akajikaza. “Ningejua.” “Basi naomba tujipange vizuri. Hata kuwapelekea barua ya ugonjwa. Kuwataarifu nipo kwenye matibabu. Nikipona nitarudi kazini. Nashauri iwe mapema ili mzee Simba asije pata sababu.” “Nitafanya hivyo.” “Nitashukuru sana.”

    “Na Connie, naomba uende Kigamboni, ukanifutie laptop zangu zote. Au vitu vyangu vitakuwa hapo kwangu?” “Nyumba yako tuliikodisha Colins. Hivi nimeshazungumza na huyo mpangaji, kumuomba mwezi huu iwe mwisho, ili urudi kwako. Kwa hiyo vitu vyako vyote vipo Kigamboni.” “Hamna haja yakufanya hivyo. Acha ibaki kama mlivyopanga. Nikipata nguvu, mimi nitarudi kuishi Kigamboni.” Ukweli aliwashangaza na kuwatia hofu kidogo. Maana ni kama safari hii anafanya kila kitu wanachokitaka bila kushurutishwa! Colins! Ikawa ni jambo jema, lakini likawaacha na maswali mengi mno. Kimya.

James akamtoa hapo sebuleni baada ya kumuona amemaliza. “James, kabla hujaondoka, nisaidie chakula kabisa. Nile ndio nipate usingizi wa mchana.” Akamuomba akiwa anamuweka kitandani. James akamfanyia yote. Akasaidia na kumpeleka chooni, alipoomba aachwe alale, ndipo akaondoka sasa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Hatimaye Juhudi Za Wazazi Wa Colins Zinazaa Matunda. Ni Kama Colins Amesalimu Amri, Anatembea Kwenye Ramani Ya Wazazi Wake.

Lakini, Ni Nini Anapanga Huyo Colins?

Ni Kweli Amekubali Kuwa, Sikio Halizidi Kichwa, Au?!

Usipitwe Na Ya Harusini Alikokaribishwa Jelini.

Mazito Na Makubwa Yapo Mbeleni.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment