“Usinitanie Jema
wewe!” Jema akajua kibao kitamgeukia muda si mrefu. “Au unataka na yeye yampate
kama aliyokufanyia Temu?” Akajua tayari. Ameshaletwa mchumba aliyemtapeli
yeye zamani, akajua tayari kibao kimemgeukia. Anatakiwa kurudisha akili hapo
kwa haraka sana kabla hapajaharibika kwake zaidi. “Mmelogwa nyinyi wawili?!”
“Kama ni siku ile walipokuja wazazi wa Colins, tulikuwepo. Na hata James
alikuwepo. James njoo hapa chumbani.” Akatoka mbio kumuita mumewe, maana akajua
huo moto utaendelea na kwake, bora alete mume kumkumbusha alishaolewa.
James akasogea na
mtoto wake aliacha sebuleni akamwambia Jeremy amwangalie. Akamkuta Jelini
akilia, amejikunja kitandani, mama Jema anawaka. “Wakati wakisema Jelini hafai
kuwa na kijana wao, nyinyi mlikuwepo hapa?” “Tulikuwepo.” James akajibu kwa
haraka akikumbuka uchelewaji wa kujibu kwa Jema.
“Kwa hiyo
kilichobadilika leo nini mpaka kumfuata mwanangu, kama si kunitafuta
mimi?” Akaendelea mama Jema. Kabla hajajibu, akaendelea. “Walikuja kumtusi
huyu, na kunivua nguo mbele yenu hapa! Nilinyamaza kimya, kama mjinga
vile, mpaka wakamaliza yao. Wakasema Jelini hafai. Leo anajenga kwake,
eti ndio wanakwenda kumvuruga!” Kimya.
“Walisema hajasoma. Nikanyamaza tu. Amejianzishia vitu
vyake. Vinaenda vizuri, wanaanza kurudi kinyumenyume kutaka yeye ndio akwame.
Aharibikiwe. Kisha mambo ya kijana wao yakienda sawa, waanze kumtusi tena mwanangu,
huku wanamuunganisha kijana wao na mtu mwingine!”
“Sasa nakutuma kwao, James.” Jema akajivuta pembeni kabisa.
Alishaingiwa hofu. “Wakati ukizungumza na James, mimi naona nikanyonyeshe.”
“Unataka kuniudhi Jema wewe?” “Mimi naona nikae tu hapahapa kitandani, ulipo
wewe mama yangu. Mtoto atanyonya hata baadaye.” Haraka akaenda kukaa palepale
kitandani.
“Wakumbushe jinsi walivyonikosea. Kuja nyumbani kwangu na
kunitusi mbele ya familia yangu. Waambie hilo nililinyamazia. Ila.” Hapo
akaweka kituo akimtizama James kwa ukali. “Nikija kusikia wamemfuata
Jelini popote pale, hakika wanaanzisha vita na mimi. Na waambie huwa
sikubali kushindwa. Wao si wanajiona wasomi sana wamefanikiwa, watu wao
ni wa viwango vya juu?” James kimya, mpaka rangi ya sura imembadilika.
“Sasa waambie wamemuanza mama Jema, sina shida ya
kuwamaliza. Wakithubutu kumsogelea Jelini tena, au kurudi hapa nyumbani kwangu
tena, hakika wataniona mbaya. Na waambie vita yangu hawaitaiweza.
Waliona wanangu dhaifu kwa kuwa hawana baba. Hawana mwanaume wa
kuwatetea kama wao walivyokuja kumtetea kijana wao hapa kwangu, sasa waambie wasimamie
hapohapo na wakumbushane hapa si pakurudi. Hakika watakimbia huu mji.”
Akaendelea.
“Mwambie Colins, hapa kwangu amenyea kambi, sitaki
kumuona tena. Nilimpenda, nikamuheshimu, lakini hakuishiwa sababu. Kutwa
akitoa sababu zisizoisha, asifanye lolote kwa Jelini ila kumliza kila
wakati, na kumrudisha baa ambako alitoka. Nalo pia nikalivumilia nikiamini
maneno yake. Ila kamwambie wazazi wake, bibi na babu yake, walirudi kugongelea
msumari wa mwisho. Hapa kwangu apaone chumba cha maiti. Sio pakuja
kutembea.”
“Kama walivyomkataa Jelini, kamwambie na mimi nimemkataa.
Jelini hataolewa na mwanaume kama yeye. Akatafute kwingine. Sasa na wewe
Jelini unisikilize na unijibu.” Kama James aondoke vile, lakini miguu ikawa
mizito.
“Maana wewe nahisi kichwa chako si kizuri. Kuna
aliyekudondosha ulipokuwa mchanga. Na kwa sababu sio mimi, basi ni Jema.” Jema
akabaki kimya. “Maana humu ndani nilikuwa mimi na Jema tu. Sasa atakayekuwa
amekugonga kichwa, ukawa mpuuzi wa kiasi hicho, huwezi kufikiria
hata kidogo, unakimbilia kulekule ulikofukuzwa na matusi, ni nani kama sio
Jema?” Wote kimya.
“Wewe unaacha biashara jana, unakimbilia kwa mpuuzi yule!”
Mama Jema akaendelea akiwaka kwelikweli. “Akiwa mzima, wanakutusi na
kukufukuza. Wanampa ujana wake mwanamke wanayeona anafaa. Akiwa mgonjwa ndio
wanakutafuta wewe mjinga, wanayejua unaweza acha shuguli zako, zisizo
muhimu kwao, ukamuuguze. Ulimkuta huyo mwanamke wake hapo kwao?” Jelini kimya
akilia.
“Usinitanie Jelini wewe?” “Sijamkuta
mama.” “Sasa hujioni kwamba wewe ni mjinga wa kupindukia!? Kwa nini
wewe uwepo huyo mwanamke wanayeona anafaa yeye asiwepo hapo?” Kimya. “Au unaona
sawa vile walivyokuja kunitukana mimi hapa?” Jelini akapandisha mabega kukataa.
“Sasa unijibu na usinipotezee muda. Unataka undugu na
kina Colins au unabaki hapa na mimi pamoja na Jeremy?” “Kwamba
utanifukuza!?” Jelini akauliza akilia, asiamini. “Tena sasa hivi na
mizigo yako. Na nisiwahi kukuona tena hapa. Maana wao si ndio unawataka? Ukiwafuata
tu, kule yakishindikana, nisikuone ukirudi hapa. Maana na Colins lazima
yatashindikana tu. Sasa hapa usirudi.” “Mama umekasirika, pengine…” “Jema!?”
“Basi mama yangu, mzazi. Basi mama.” Akajirudi kwa haraka.
“Wewe unaona hivi anavyoyumba yumba huyu ni sawa? Nakuuliza
Jema? Unataka aendelee kuyumba hivi mpaka amyumbushe na Jeremy! Mungu amempa
mtoto mtulivu. Aliyeamua kutulia humu ndani. Ameona havinogi, akaenda
kuniletea mwanaume mpaka humu ndani alikotulia mtoto! Tena mwanaume asiye na
maana! Amemvuruga Jeremy mpaka leo amebaki na maswali juu ya huyo Colins, na
hakuna mwenye majibu ya maaana yakumpa.”
“Mimi nishakuapia sitaleta mwanaume mwingine tena
humu ndani, ukaamini. Mbona sasa unani…” “Kwa hiyo unataka niwe na kazi ya
kukuapisha kwa kila jambo? Sasa hivi tena nikuapishe kuwa na biashara hutaacha
sababu ya wanaume? Unaniona mimi mjinga sana?” Jelini akapandisha mabega
kukataa.
“Mbona ulipokuwa na Ezra, biashara zilikuwa zikienda, tena
anakufuata mpaka kazini. Anakusubiria. Mnakula naye pale na kuhakikisha unarudi
tena kazini. Huaribikiwi. Anakutengenezea mazingira mazuri ya kazi. Mpaka cooler
si umepewa wewe ili ukiwa na shuguli zako njiani, usihangaike kwa vinywaji? Sasa
umeona vimetulia, roho yako inakutanga, unakwenda kutafuta
hekaheka. Si wazimu huo ni nini?”
“Wewe badala ufikirie swala la mtoto wako la baadaye,
unakimbizana na wanaume wenye maisha yao. Ushajua Jeremy akimaliza hapo
anakwenda shule gani? Maana ada ya hapa ilishalipwa. Huko kwengine?” Kimya. “Na
nakuonya Jelini huyu mtoto asirudi chini!” “Mimi
simrudishi Jeremy chini.” “Mpaka sasa ushakusanya ada yake kiasi gani
yakumfanya aendelee kusoma shule inayoendana na shule anayosoma sasahivi?”
Kimya.
“We Jelini?” Akamuita kwa ukali. “Badala umfikirie mwanao na
maisha yake ya baadaye, unakimbizana na wanaume wasio na maana. Na biashara
unafunga! Unafikiri mimi nahangaika mchana kutwa kwa ajili ya nani?” Kimya.
“Sasa wakati wewe ukihangaika na wanaume, mimi nishajua
akimaliza hapo anakwenda wapi, na ada yake ndio nahangaika mchana na usiku, kuikamilisha.
Kama huyu baba alivyomlipia ada mpaka amalize, asikwame, basi na mimi amenitia
shauku, nafanya kama yeye. Ndio maana mwenzio nikipata faida, naigawa mara
tatu. Kuendeleza biashara, ada yake huyu, na kulipa mishahara. Wewe akili hiyo
huna. Upo radhi uache kila kitu, mpaka familia yako, ukimbilie huko
wasikokutaka. Sasa leo niambie, nijue moja, utoke hapa, usinichanganye.
Unanielewa Jelini?” Jelini akazidi kulia.
“Eti unamwambia Ezra, unataka ukamuuguze Colins! Unaakili
wewe au umechanganyikiwa? Halafu yeye awe na kazi ya kukusubiria tu ukimuuguza
mwanaume wako! Kwanza wewe kama nani? Kama sio kukazania kubaki kwenye fungu
la kukosa tu! Apone huko, aanze sababu nyingine, na Ezra alishaoa.
Hivi unaakili wewe? Kwanza jibu swali langu. Maana ushakua mkubwa, upo huru
kufanya ujinga wako, lakini si hapa ndani, tena mbele ya Jeremy.
Hutamchanganya Jeremy. Sasa unaenda kwa kina Colins au unabaki hapa na sisi?” “Mimi siendi tena.” Jelini akajibu na kilio.
“Umesema nini Jelini wewe?” “Nimesema
mimi siendi tena huko kwa kina Colins. Natulia na Ezra. Na nimesema
sitamleta mwanaume hapa. Mbona sasa huniamini?” “Nipe sababu ya
kukuamini, uone kama sitakuamini. Kichwa chako kipo kama kimegongwa msumari,
hutulii! Ni jana tu umetoka kusamehewa na huyo Ezra, eti leo unamwambia urudi
kwa kina Colins, ukamuuguze! Unawazimu wewe mtoto!?”
“Mimi natulia mama.” “Hakika tulia
Jelini. Tulia kama mwenzio Jema, upate kitu kizuri.” “Mimi
mtoto mbaya. Hunipendi tena. Unaniona sifai. Unanifukuza kwako.” Akazidi
kulia Jelini, ila Jema alitegemea ndio njia yake yakumtuliza mama yao. “Hunitaki. Unanifukuza nikapotelee huko nje!” “Si
kwa kuwa hutulii?” “Mimi najua kunipendi tu mama.
Unataka niondoke humu ndani. Nikaharibikiwe moja kwa moja.” “Sitaki
uharibikiwe ndio maana nakukumbusha.” “Sasa badala
unisaidie nikiwa karibu yako, unanifukuza! Utafikiri mimi sio mtoto wako.
Wakati ulikuwa ukiniambia majuzi tu hapa nimebadilika, nimekua mtoto mzuri,
nina juhudi kama Jema! Sasa hivi mimi tena sifai.” Akazidi kulia.
James akazidi kuchanganyikiwa, lakini akashangaa mama Jema
amepoa kabisa. Jema alivyoona tu hivyo akamfanyia ishara mume wake aondoke.
James akawa hajaelewa halafu anaogopa. “Nenda kamwangalie mtoto James.” Kama
akimbie maana alijua panapoelekea ni kufukuzwa na yeye humo ndani. Maana na
yeye ni timu Colins.
“Mimi humu ndani ndio peke yangu mimi sipendwi!
Nakua mtu baki tu, wengine wote unawataka.” “Na kweli ulitulia, ukawa unafanya
vizuri. Kwa nini sasa ulikubali kudanganywa na kina Colins? Unaacha mambo yako
kwa ajili ya watu kama wale? Wanakudharau wenzio kama hujui.” Hapo mama Jema
anaongea ametulia kabisa kama sio yeye.
“Mimi kichwa kimeanza kuuma.” Akaendelea kulia.
“Nyamaza mama yangu mzazi kichwa kisizidi kuuma tena. Maana kilikuwa kimepoa
kabisa, mpaka Colins amerudi nacho. Mshenzi kabisa! Jema kalete maji ya kunywa.
Mama mzazi anywe dawa.” Kama akimbie vile na yeye. Break ya kwanza kwa
mumewe.
“Vipi, ndio kumeshapoa?” James akauliza akinong’ona. “Bado.
Hapo Jelini atamlilia. Ili abakie akimbembeleza yeye.” “Haiwezekani Jema!”
“Kumbe hujawajua hawa! Muulize Jeremy. Ndio kazi yao. Sasa na yeye Jelini
anamfanyiaga kusudi. Atalia hapo, mpaka mama apoe kabisa, abakie yeye ndio
mbaya. Sasa sio leo. Ujue ndio na ibada tumechelewa.” “Au tusiende?” James
akachomekea. “Usinitanie James!” “Ni wazo tu Jema! Leo mbona kama mmeniamulia
jamani!” “We Jema? Kinachokushinda kuleta maji kwa haraka ni nini? Au unaona
raha hivi mwenzio anavyolia?” “Naleta mama.” Akakimbilia jikoni.
Baada ya nusu saa ndio nyumba ikapoa, Jelini akapewa dawa ya
maumivu ya kichwa, akarudi kulala. Akaachwa hapo yeye ndio amelala, wengine
ndio wakaenda kanisani.
Mtaka Cha Uvunguni.
Ikawa kama Ezra alikuwa akiwasubiria wao. Wakati wakiingia
akagundua Jelini hayupo nao. Akili ikapaa. Akajua ameenda kwa mgonjwa, Colins.
Akaanza kuhangaika, hawezi hata kupumua. Junior akamuona. “Vipi?” “Jelini
hayupo nao.” Akaongea hivyo tu, Junior akaelewa. Akaangaza macho, akagundua
kila mtu kwenye familia yao yupo kasoro Jelini. Akachukua simu ya Ezra, akaandika
ujumbe. ‘Shalom dada Jema. Samahani kwa usumbufu.
Sijamuona Jelini. Yupo mzima?’ Akamuonyesha,
Ezra akamuangalia na kuutuma. Baada ya muda mfupi akapata majibu. Asifungue
asome, akamvuta Junior. “Amejibu!” Akampokonya tena simu. ‘Shalom! Jelini tumemuacha amelala. Anaumwa kichwa.’ Wakaangaliana.
Wakatoka nje kabisa ya kanisa. “Lazima nimuone. Lasivyo
sitatulia.” “Sawa.” “Lakini aliniambia kwao haparuhusiwi mwanaume, isipokuwa
huyo mwanaume ameenda na wazazi.” Junior akafikiria kwa haraka. “Tumuwahi mzee
kabla hajasimama kuhubiri.” Ezra akafikiria, wakacheka kwa pamoja. “Atalalamika
maana leo siku ya harusi. Lakini tumwambie ni 911.” “Mtumie ujumbe mwambie
arudi ofisini, nimuhimu sana.” Junior akaandika kwenye kikaratasi. “Sasa hivi
hashiki tena simu mpaka baada ya mahubiri. Ujumbe wa simu tutachemsha.” Wawili hao
wakakubaliana.
Wakamkabidhi shemasi hicho kikaratasi walichoandika, kwamba amfikishie
mzee pale mbele alipokuwa amekaa, kwa haraka kabla hajaenda madhabahuni. Mzee
aliposoma, ‘911, ofisini kwako.’ Akageuka nyuma
kumtafuta mtumaji ambaye alijua lazima ni Junior au Ezra. Ndio lugha yao hiyo.
Alipomkosa akaelekea ofisini.
Akawakuta wakimsubiria. “Kuna nini!? Mbona 911.” “Jelini ni
mgonjwa, na kwao hapafikiki bila kijana, kusindikizwa na mzazi wake.” Akaongea
hivyo Ezra, na kumuacha mchungaji ameduaa. “Kukusaidia tu, Jelini ni mdogo wake
Jema, mke mtarajiwa wa Ezra. Tupo kwenye hatua za awali. Karibuni
sana utajulishwa.” Mzee akabaki akimtizama Junior.
Ezra akapokea. “Nampenda. Na bila kumuona leo, siwezi
kufikiria.” “Tutarudi Milimani.” Junior akaongeza. Mzee akashangaa sana. “Ndio
ipo serious hivyo!?” “Kabisa. Jelini ni mke wangu.” “Mbona…” Akataka kuwauliza
tena, lakini akaona hana huo muda kwa wakati huo. “Labda maswali mengine iwe
kesho. Lakini hivi mnakumbuka kama leo ni harusi ya dada yenu?” “Esta
ameshapata wake. Tumebaki sisi. Au unataka leo ndio iwe harusi ya mwisho?”
Junior akaongeza. Walishawazoea hao wawili. Uhitaji wa Junior ujue ndio wa Ezra.
“Naomba utusindikize, tafadhali. Hatutakaa sana. Nakuahidi
hautachelewa.” “Hivi mnajua kama Ester hatakubali kuolewa leo bila mimi?”
“Nakuahidi hutachelewa. Na tutakueleza kesho kwa kituo, ila ujue ni muhimu.” “It’s
either now, or never.” Akaongeza Ezra. “Na ili usichelewe, ibada ikiisha
tu, usianze kusalimia watu. Wewe sema una udhuru.” Mzee akakabwa, akichangiwa
na maneno kutoka kwa kila mmoja wao hapo, akashindwa cha kujibu, akaondoka
kurudi kanisani. Wakabaki wakiangaliana.
“Tuma ujumbe kwa Jema, mwambie baada ya ibada tunaomba
kwenda kumuona Jelini. Na tutafuata mashariti ya mama.” Na yeye Ezra akaandika
ujumbe hivyohivyo kama alivyozungumza mwenzie. “Ongeza hatutakaa sana, kwa hiyo
wasisumbuke kwa chochote.” Ezra akaongeza na kutuma. Hapo wapo ofisini kwa mzee
wao. Ibada ikiendelea. Wakabaki wakisubiria majibu kama watoto wadogo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jema aliposoma ujumbe akashangaa na kumuonyesha mama yake.
“Soma kuanzia hapa.” Akamnong’oneza mama yake. Mama Jema akasoma kuanzia mazungumzo
yao asubuhi hiyo wakimuulizia Jelini mpaka mwisho. “Mashariti gani?” Akamuuliza
mama yake baada ya kumuona amemaliza. “Kwa hiyo unataka nikuambie sasahivi
katikati ya ibada?” Alivyoulizwa hivyo akarudisha akili kwa haraka.
“Mimi naona kweli nisubiri tu. Maana leo!” Mama yake
akamtizama na kumrudishia simu yake. “Sasa nimjibuje? Maana ndio ujue anakuomba
ruhusa.” “Sawa.” Jema akacheka akitingisha kichwa. Akajua Ezra amepokelewa.
Akamjibu Ezra bila ya kuchelewa. ‘Mama amewakaribisha
nyumbani. Karibuni sana.’
~~~~~~~~~~~~~~~
Walipopata hayo majibu hapo ofisini walipokuwa wakisubiria,
acha wafurahie huko ofisini, kama watoto wadogo.
Baada ya kumaliza mahubiri, wakamsikia mzee
anamalizia kwa kusema, “Japokuwa leo nina ozesha binti yangu, lakini nina dharula
ingine itanipasa niwahi kutoka mara tu baada ya ibada. Nikikamilisha hilo,
ndipo tutakutana harusini na tutasalimiana tukiwa na vinywaji mkononi. Mungu
awabariki.” Ndipo akashuka, Junior na Ezra wakasimama kama mshale kurudi
ofisini kwa mzee wao. Wakamkuta na yeye ndio anaingia.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Tafadhalini tuwahi.” “Tunakushukuru mzee wangu.” Junior
akaongeza kwa furaha sana kama yeye ndiye Ezra. “Ila hamtanipeleka ukweni
mikono mitupu.” “Hilo usijali mzee wangu. Wakati wewe unatumika pale mimbarini,
tulishatuma mtu kununua vitu. Hivi hapa anarudi na kila kitu tulichoagiza.”
“Hivi nyinyi mkoje!? Ningekataa!” “Ni imani tu. Sisi tuna imani na wewe
mzee.” Hakutaka kujibu. Akazunguka kwenye meza yake, akaweka vitu vyake ili
atoke nao.
“Mshitue Jema, mwambie mzee ana haraka, ndio tunatoka kwenda
kwao.” “Nyinyi mpaka kutongoza, mnatongoza pamoja!?” Wakacheka, Ezra akaandika
ujumbe kwa haraka. Akatuma.
Jema alipopata huo ujumbe, akamuonyesha mama yake. “Jema!” Akashituka
hakutegemea. “Ndio nashangaa kumbe dharula aliyotangaza mchungaji pale
ni Jelini!” “Mimi sikutegemea! Nilijua ni…’ Akakwama. “Acha niwahi nyumbani.
Sasa na nyinyi msichelewe.” “Tulete nini?” “Nina vinywaji. Pitia sambusa na
vitu vidogovidogo. Sasa sio uje kesho.” “Sikawii mama Jema! Mbona leo hivi?” Mama
Jema akaondoka kwa haraka akiwa na Jeremy.
Full Swing.
Akafika kwake akaanza kuandaa vitu akasahau kumuamsha
muhusika. Jema na mumewe wakiwa wanaingia getini, wakaona na gari ya mchungaji
pamoja na gari ya Ezra. “Kazi ipo!” Ikabidi James ashuke awakaribishe ndani.
“Ingizeni tu magari ndani.” Wakaongozana. Wakawakaribisha ndani. Mama Jema
akatoka kuwasalimia.
“Imekua gafla, hatujajiandaa vizuri. Karibuni sana.” Heshima
ikaongezeka maana na huyo mchungaji alikuwepo. “Usijali mama. Sisi tunashukuru
kwa kutufungulia tu mlango. Maana naona na harusini kusingeendeka bila
kumuona Jelini!” Akaongea mchungaji akimtizama Ezra na Junior, wakacheka.
“Hatutakaa, na wala usihangaike kwa chochote hata maji.”
“Kweli mchungaji! Hutaki kutuachia
baraka?” “Hapana mama. Huku tu kunifungulia mlango, tena kwa gafla hivi,
mmegusa moyo wangu. Tukimuona Jelini, tukafanya maombi mafupi, siku nyingine
tutarudi tukae na tule kabisa.” Mchungaji ndiye akawa mzungumzaji, Junior na
Ezra kimya.
Ndipo akaenda kuamshwa Jelini, mpenda usingizi. Hapo alikuwa
ndio kama saa sita usiku. Kalala hana habari. Alikuwa kwenye usingizi mzito.
“Vipi mama?” Mama yake akamuamsha kwa upendo. “Sasahivi kichwa kimepoa.” “Una
wageni.” Jelini akashangaa sana. “Wageni gani?!” “Ezra na…” Alivyosikia tu Ezra
akatoka kitandani mbio. “Ungeosha hata uso bwana Jelini! Vipi wewe?” “Ezra
amekuja kuniona!” Wakasikia sebuleni na kuanza kucheka.
“Osha hata uso bwana! Jiweke sawa ndio utoke. Yupo na
mchungaji.” “Mama! Yule mchungaji mkuu, baba Junior!” Akashituka
nakufanya wacheke zaidi. “Mimi nimeingiwa hofu.” “Sasa ufanye haraka utoke,
wanaharaka.” Jelini akakimbilia bafuni na kutoka akiwa na nguo ileile ya jana
yake aliyoenda kuombea msamaha. Alilala nayo na kuamka nayo. Kabla ya kwenda
kuoga ndio akamtibua mama yake. Likatokea la kutokea, akabembelezwa na kurudi
kulala na nguo zake vilevile.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akatoka na cheko la aibu. “Kwetu hapajawahi tembelewa na
mchungaji.” Akaanza Jelini akiwasogelea pale sebuleni. Wote wakasimama
wakicheka. Akamsalimia mchungaji kwa kumpa mkono. Mtoto wakichaga
akaweka na goti la kinyakyusa. Akitoa heshima. “Pole sana mama.”
“Asante. Lakini msingehangaika. Naendelea vizuri. Hapa nilijitegeshea alam, ili
niamke na kujiandaa, niungane na Ezra kwenye harusi.” “Sio usumbufu hata
kidogo. Pole.” Wakajikuta wakiongea wote kwa pamoja.
Jelini akacheka akimtizama Ezra na kumsogelea pale alipokuwa
amesimama. Akamshika mkono kwa upendo mbele ya wote. “Nimefurahi umekuja
kuniona.” Wote wakacheka. “Na mimi nimekuja Jelini!” “Wewe bado sijakuona
kabisa Junior.” “Kweli Jelini?” “Nakutania bwana. Junior wewe mtu wangu sana
tu. Nimefurahi mmekuja. Wote. Na mchungaji ndio zaidi. Nimefurahi nahisi
nishapona kabisa.” Hapo anaongea mkono kamshika Ezra.
Akamtizama na cheko la deko. “Nimefurahi. Nimefurahi sana.”
Akarudia kwa kunong’ona. Lakini akasikaka na kufanya wacheke. Ezra akaubusu ule
mkono aliokuwa ameushika, kwa upendo mkubwa sana, kiasi cha kumshangaza
mchungaji. Mchungaji alikuwa haamini kama kuna mahusiano mazito hivyo, yalikuwa
yakiendelea, yeye mpeleka mlimani, bado haja taarifiwa! Ameachwa bado akiombea
mke kwa huyo Ezra!
“Pole. Ila ungeniambia.” “Sikutaka kukutia wasiwasi.” Jelini
cha deko akajibu kwa upendo akimtizama. “Wala haijasaidia.” Akadakia Junior,
mzee wao akiwatizama kama aliyejawa na maswali lakini hawezi uliza pale, zaidi
siku hiyo ambayo muda si rafiki kabisa. Ukweli ilikuwa ni 911 kwake. Kama
emegency ya
America. Maana hapo alikuwa kama ametekwa nyara, si sehemu alidhania angekuwepo
siku hiyo, zaidi muda huo ambao anasubiriwa na binti yake wa pekee aende
akamtoe kanisani kwa atakaye kuwa mumewe.
“Sasa si uwakaribishe wakae?” Mama Jema akaingilia. Maana
wote walibaki wamesimama wakiwaangalia Jelini na Ezra. “Mimi naomba tufanye
maombi tukiwa hivihivi tumesimama, na uturuhusu tuondoke mama. Estar hataolewa
leo, asiponiona pale na kumsindikiza mpaka mbele madhabahuni akafunge ndoa.
Nitarudi rasmi, nikae tuzungumze vizuri kukiwa kumetulia. Tule na kunywa mpaka
mtufukuze.” “Bila shaka. Tunaelewa.” Mchungaji akashuka sala fupi ila nzuri.
Akatamka baraka pale, akamuombea Jelini na kuwakabidhi wote kwenye ulinzi wa
kimungu. Bila kurudi kukaa, akaaga.
Wakawasindikiza mpaka nje, mchungaji akaomba apokelewe
mizigo iliyokuwa nyuma ya gari yake. Wote hawakutegemea. Walikuwa wamejifungasha
kama ambao si dharula. James na kina Junior wakasaidia kushusha na kuingiza
ndani. “Msingehangaika jamani. Vitu vyote hivi!” “Si usumbufu hata kidogo,
mama. Ubarikiwe wewe na watoto wako wote. Siku zenu zikawe za baraka na amani.”
Akaongeza mchungaji. Baada ya kumaliza kutoa vitu vyote, akaingia kwenye gari
yake na kuondoka kwa haraka akiwaacha Ezra na Junior hapo nje.
~~~~~~~~~~~~~~~
Walipomaliza tu,
Jelini akamdaka tena Ezra. Akamshika tena mkono vizuri. “Asanteni sana. Junior,
asante kwa upendo wenu.” “Karibu Jelini. Siku nyingine usiache kutuambia bwana!
Ili na sisi tujue. Usimuachie mama mzigo peke yake. Jua na sisi tupo. Tunahusika
moja kwa moja.” Akaongeza Junior kwa kujali, Jelini akasikia kupendwa huyo! Akamtizama
Ezra na kucheka. “Nitafanya hivyo. Sasa acha
na mimi nijiandae, nitakuja japo kwa kuchelewa. Naweza nikakosa ibada ya ndoa,
lakini sitachelewa.” “Usijali. Nitakuwa nikikusubiri.” Ezra akaongea
akimtizama. Bado Jelini alikuwa amemshika mkono.
“Kwani harusi yenyewe inafanyikia wapi?” Jema akauliza akiwa
anamsogelea Junior. “Wametaka kufungia harusi baharini.” Wakaona Ezra na Junior
wanacheka wakitingisha vichwa baada ya Junior mwenyewe kusema hivyo. “Ester!” Ezra
akaongeza na kufanya wacheke. “Lakini si sehemu mbaya.” Jema akaongeza na yeye
akicheka.
“Siyo sehemu mbaya kabisa, ila garama sana. Maana
wamekodi huo upande wa bahari na wamekodi
ukumbi hapohapo.” “Lakini wanaonekana wamepaandaa vizuri kwakweli. Upande wa
bahari wanapofungia, kulikuwa kunatengenezwa tokea jana. Wamefanya vizuri
kwakweli. Ila pesa yake ni ndefu sana.” “Hongereni sana.” Akadakia mama Jema.
“Asante mama yangu. Natamani tungejua mapema, wote tungejumuika kwa pamoja.”
“Hamna shida. Jelini atatuwakilisha.” Ungemuona anavyozungumza mama Jema,
ungejua tu amefurahi. Nao hao wawili wakaaga na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ezra Ameingia,
Full Swing. Mzima Mzima, Bila Kubakiza. Yeye Amekuja
Na Gia Kubwa, Mpaka Mzazi, Tena Mchungaji, Aliyetamka BARAKA kwa mama Jema na wanae. Ametimiza Yote Anayoyataka Mama Jema.
Ni Nini
Kitaendelea?
Kwa Kina
Colins? Ndio amekosa kabisa? Maisha Yake Yatakuaje Baada
Ya Kurudi Na Kukutana Na Yote Yanayoendelea?
James ametumwa kwao.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment