“Bado amelala?”
Akanong’ona wakiwa hapo nje alipokwenda kumpokea. “Alitoka kuchukua maji, najua
hawezi kulala kwa urahisi. Alishapita hapa alipo, kwa uchungu na maumivu makali
sana. Ni kama historia inajirudia.” “Sio na mimi. Mimi sio tapeli. Na ndio maana
mwanzo nilishindwa kabisa kumkubalia. Sikuwa tayari. Sasahivi nipo tayari naye.
Hawezi kulala akiwa na hali hiyo. Naomba nikaribishe tu nikamuone.” Akaongoza
njia.
Akamuona anacheka.
“Jelini! Sasa unacheka nini?” “Ujue mtu akikuona pale kanisani, anaweza
kukuchukulia poa! Kumbe mwenyewe mambo yako safi.” Mpaka Junior
akacheka. “Kweli. Kwako kuzuri. Na si kuzuri tu, kwa viwango. Nitakusifia zaidi
baadaye. Maana nilijua ni zile nyumba hazina hata geti, nitaanza kuibiwa vioo
vya gari yangu kisha radio. Lakini nikasema bora wachukue tu, mimi nipatane na
Ezra.” “Jelini!” “Haki tena. Nilijua ni uswahilini, nje kuna kuna…” Akaanza
kuangaza macho akicheka. “Mwaya kwako pazuri sana. Maua yako pia mazuri
sana. Kumepangiliwa kwa kisasa. Maua yamewekwa kwa mpangilio mzuri. Halafu mwenyewe
unaishi gorofani!” Junior akacheka akimwangalia.
Akamfungulia mlango
wa kuingia ndani. “Asante kunikaribisha kwako.” “Karibu sana.” “Nikimfuata
alipolala ni vibaya?” Akanong’ona. “Hapana. Na huna haja ya kunong’ona. Vyumba
vya kulala vipo juu kabisa.” “Junior naye! Si useme juu gorofani!” Junior
alicheka mpaka akainama. “Jelini wewe ni mtundu!” “Sijawahi ishi gorofani
mwenzio.” “Basi karibu. Chumba chake kipo…” “Wewe naona ungenisindikiza tu,
nisijeingia ambapo sipo.” Junior akaongoza njia akicheka huku akimtafakari
Jelini. Hakujua kama yupo hivyo ndio akamuelewa Ezra. Akamfikisha juu na kumuonyeshea
chumba kwa kidole.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona anasogea kwa
taratibu mpaka kwenye hicho chumba. Akamuona ana vuta pumzi mara kadhaa nje ya
mlango kwa hofu, mpaka akashagaa. Akabaki akimtizama. Kwamba Jelini ana hofu na
Ezra! Akabaki akijiuliza akimtizama. Akamuona akihema mara kadhaa na kufuta
mikono kwenye gauni kama iliyoanza kutoa jasho. Kisha akashika kitasa, akaachia
na kurudi kwa Junior aliyekuwa bado akimtizama.
“Au labda nikanywe
kwanza maji? Mimi nahisi nina kiu sana.” Ujanja wote akaona umemuishia.
“Huna kiu, Jelini. Ingia tu.” Akataka kumkabidhi pochi yake. “Nishikie pochi
yangu.” Junior hakuamini. “Unanipa pochi!?” “Sasa hivi nishaingiwa hofu, siwezi
kufikiria tena. Halafu hii pochi ishakua nzito. Bora ningeacha tu kwenye gari.
Sasa wewe jiulize, usiku huu pochi ya nini?” Akaanza kulalamika. “Au labda
nirudi nikaiweke tu kwenye gari?” Akajua amepaniki. “Nipe nikushikie.”
Akamkabidhi na kurudi kwenye chumba.
Pegu zisizooza.
Jinsi alivyopanda
upendo na kujali kwa huyo Jelini, Jelini mwenyewe akajikuta anayavulia maji
nguo, ili kufika ng’ambo ya pili alipo Ezra. Safari hii akamuona akifungua
mlango taratibu na kuingia akinyata. Ezra alipoona mlango unafunguliwa bila
hodi usiku huo, akajua moja kwa moja ni Junior. “Junior?” Akaita akiwa
anajiweka sawa kitandani. “Ni mimi Jelini.” Ezra alishituka, hakutegemea.
Akawasha taa ndogo, ya meza ndogo, pembeni ya kitanda kwa haraka. “Jelini!?” “Umenizimia simu, sikupati Ezra.” Akaanza kulia.
“Njoo hapa.” Akabaki amesimama karibu ya mlango akijiliza. Ezra akatoka kitandani
na kwenda kumshika mkono na kumvutia kitandani. Akamkalisha.
“Nataka uamini
sijakuzimia simu. Ila nilitaka kukupa nafasi.” “Mimi
sitaki nafasi mbali na wewe. Nataka tusimame pamoja. Ndio tumejenga tu msingi
wetu! Jaribu la kwanza tu kutujia, tayari nyumba imeanguka! Umenikimbia!
Hujanitakia usiku mwema! Hujazungumza na mimi na kuniombea usingizi mzuri!
Umenizimia simu! Hivyo mimi sijapenda Ezra.” “Nisamehe Jelini. Ila
nilitaka kukupa nafasi. Na sikujua kama..” Akasita.
Jelini akaendelea
kulia taratibu. “Usilie nikwambie ukweli.” Akamsaidia kumfuta machozi kama
mtoto mdogo. “Acha niwe muwazi Jelini. Unahistoria kubwa sana na Colins. Mimi
ndio nimekuja tu kwako. Sikujua kama kwa sasa natakiwa kufanya nini isipokuwa
kukupa nafasi.” “Yote niliyokwambia, ujue
namaanisha Ezra. Mimi sijakudanganya.” “Hata kwa Colins?!” Akataka
uhakika, bado haamini, kama ilivyokuwa kwa Jema tu.
“Sasa hivi wewe ndio jukumu
langu la kwanza Ezra. Hata Colins ananijua. Mimi si msaliti.” “Hayo ndio
nisiyoyataka Jelini! Sitaki uwe na mimi sababu ya kutunza ahadi. Nataka
kuwa na mtu anayenipenda mimi kwa dhati, na kunichagua mimi kama Ezra. Lakini
kwako imekua ngumu hata kuniambia unanipenda, Jelini!” Jelini akapoa.
“Uliniambia ni kwa
kiasi gani unampenda Colins, lakini hajawahi hata kuropoka kwangu!
Nikajiambia pengine unahitaji muda, utakuja kujisikia ninachojisikia kwako, na
kukwambia kila wakati, tena nakurudiarudia. Lakini kabla hata hujafikia hapo,
ndio taarifa za uliyesema unampenda SANA,
na ulikuwa ukimsubiri muda wote na msamaha wake mkononi, amerudi. Kisha
kunisahau kabisa! Ulitegemea nifanye nini?” Ezra akamuuliza taratibu tu.
“Nimekosea
Ezra. Sio kwamba najitetea. Lakini pengine ungemuona Colins, ungeelewa
kuchanganyikiwa kwangu. Yule mtu huwezi kumtambua kama hutaambiwa ni yeye.” Akamueleza mazingira
yote jinsi ilivyokuwa mpaka kuombewa na kurudishiwa ufahamu wake.
“Lakini
Ezra, sipo na wewe kwa kukuhurumia. Mimi najijua. Maisha yangu bila mtu
kama wewe, yatabaki kuwa hovyo tu. Na inawezekana wewe mwenyewe sijakwambia,
lakini nakuhitaji, na ndio maana unaniona usiku huu nipo hapa. Ile hisia
ya kufikiri tu eti maisha yangu yanarudi tena kuwa kama zamani bila wewe,
nahisi sitaweza. Nakupenda Ezra na nakuhitaji kwenye maisha yangu. Na
ninaomba tubakie sisi wawili. Nisamehe kwa nilichofanya. Nimekosa.
Nakuahidi nitajitahidi niwe kama wewe unavyonijali.” Ezra akavuta pumzi
kwa nguvu akifikiria.
“Nakupenda Ezra.”
Ezra akacheka na kumtizama. “Nilivyokuwa nikisubiri nikusikie!” “Watu
wanalitumia hilo neno sana. Tena hovyohovyo tu, mpaka linakua linapoteza ladha
ya maana yake. Mtu anakuona mara moja tu, hakujui, anakwambia hilo neno. Kwangu
nilitaka nikikwambia, ulisikie na kuleta maana, sio kulirusha tu. Lakini
kuanzia sasa nitakuwa nikikwambia. Na ujue namaanisha.”
“Na Colins? Maana
hatuwezi kuepuka swala la kurudi kwake.” “Ndio tuamue mimi na wewe. Na wenyewe
nimewaambia. Na namaanisha Ezra. Sitafanya chochote juu ya Colins, bila baraka
zako.” “Kweli Jelini?!” Ezra hakuamini.
“Najua unaweza
usiamini Ezra. Lakini mimi ninasimama na wewe. Wewe ni wangu mimi.
Nisipokulinda nje na kukutetea, hakuna atakayekulinda. Nahusika na furaha yako
kwanza. Na kila mtu nimemwambia. Siwezi nikaenda kutengeneza kwa watu,
wakati kwangu kuna teketea. Najua ndio tumeanza. Kamsingi ketu kanaweza
kasilete maana hata kwetu. Lakini mwenzio nathamini chetu. Changu mimi
na wewe. Tumeanza kidogo, lakini tukiwa pamoja, na sisi tutajenga kitu
kitakacholeta maana baadaye. Naomba usinikatie tamaa.” Ezra hakuamini.
“Sikujua kama
mwenzangu ndio unachukulia kwa uzito huo! Nilijua msingi wetu hata nchi moja
haujafika, hauna maana!” “Mungu aliumba dunia yote kwa kutamka tu. Na
sisi tumetamka. Tumekubaliana. Naomba uamini itakua. Mimi
nimeamini. Na kama baba yake Junior alivyofundisha, alisema nyumba yeyote
lazima ipate majaribu. Nina uhakika hili ni jaribu letu la kwanza Ezra. Usiniache nipambane peke yangu, nitashindwa. Mimi
najijua. Nisaidie katika hili nifanye vizuri, lakini tubaki sisi ndio
tumesimama.” “Daah! Hujui ni kiasi gani nilikuwa nikimlilia Mungu nipate
mtu kama wewe Jelini! Kumbe ndio unaimani ya kiutu uzima hivyo!” Jelini
akacheka akijifuta machozi.
“Sikujua kama una
msimamo wa kiasi hicho!” “Nakupenda Ezra. Na nimeamua kuwa na wewe. Nitatulia
na wewe tu, ili na sisi tuwe na kitu chetu kizuri chenye amani na utulivu kama
jinsi wewe ulivyo. Nakutaka wewe Ezra.” Ezra akataka kumkumbatia. Jelini
mpenda mikono, akajiweka vizuri kwa kupandisha kabisa miguu kitandani,
akajipanga vizuri, Ezra akamkumbatia kwa furaha zote ila kwa heshima kidogo
asije pitiliza. Mikono juu kabisa ya mwili wake.
“Nimefurahi!
Nimefurahi sana Jelini. Hujui tu. Sikutegemea! Maana tulifanya michezo mingi
sana juzi kwenye makubaliano yetu. Sikujua kama imeleta maana.”
“Linapofika swala la mahusiano ya kimapenzi, huwa sina mchezo. Nisingekwambia
ili tu kukufurahisha. Kama ningekua sikutaki, au sijakupenda, wala usingekaa na
mimi kwenye gari lako tukala. Mimi sipo hivyo. Kwenye mahusiano ya kimapenzi,
sijui kwa nini Ezra! Nimeipa heshima kubwa sana. Ndio maana nafikiri
nimeshindwa kuendana na wengi.”
“Siwezi kukuahidi
wewe, na mwingine. Siwezi nikakubali mtu yeyote yule anishike hivi halafu na
mwingine tena akanishika hivi! Siwezi. Na huwa sifanyi hivyo kwenye
mwili wangu. Nimekukubalia wewe, tafadhali amini nitatulia na wewe tu.”
“Nashukuru Jelini. Nimefurahi sana. Asante kwa kunifuata usiku huu.
Kwangu inamaana kubwa sana. Nilikuwa na wakati mgumu kupita nitakavyokueleza.”
“Najua. Pole mpenzi wangu. Tutakua sawa.” Wakatulia huku wamekumbatiana.
“Nimefurahi Jelini!
Nimefurahi sana. Natamani ungejua moyo wangu.” “Unaupendo wa dhati Ezra. Siwezi
pata mwanaume kama wewe. Umebeba majibu yote ya kilio changu. Nilikuwa
nikitamani mwanaume kama wewe. Siwezi kuzembea. Nilikosa.” “Hayo
yameisha na nimesamehe. Nafikiri na wivu pia ulikuwa ukinisumbua.” Jelini
akambusu kwa muda mrefu shingoni. Lilikuwa busu moja tu, aliloweza kuligandisha
sehemu moja ya shingo kwa muda mrefu, bila mengi, lakini Ezra alilipata mpaka
rohoni. Kisha akajirudisha kumuegemea kifuani akiwa amemkumbatia vizuri.
Baada ya muda
akajitoa. “Sasa hivi nasikia usingizi. Acha nirudi nyumbani, nikuache na wewe
upumzike.” “Ni sawa nikipata muda wa kufikiria juu ya swala la Colins?”
“Kabisa. Ukiwa tayari nijulishe. Ila natamani tusimtupe sasahivi akiwa
mgonjwa sana. Sitaki waje waone sisi ni wakatili, hatujali. Nimeshamuweka sawa
juu yetu. Na Colins anajua msimamo wangu. Na anajua siyumbishwi.
Naomba, katika swala la ugonjwa nisijiweke pembeni kabisa. Nifanye kwa vile
mimi na wewe tunaona ni sawa. Ila ukiona tu kuna mazingira yanakusumbua,
tafadhali usinyamazie. Tuzungumze.” “Sawa. Basi tutajipanga vizuri kesho. Si
bado wazo la harusini lipo?” “Kabisa. Ulipo ndipo nitakuwepo Ezra. Sisi
kwanza, ndio ratiba nyingine.” Ezra akacheka asiamini.
“Najisikia kukupenda
zaidi Jelini! Kumbe wewe ni wa kuaminika hivyo!?” “Kwa sababu nakuhitaji Ezra.
Mwenzio sitaki kukupoteza.” “Hutanipoteza.” “Bado mimi ni dharula yako
ya kwanza?” Ezra akacheka sana. “Naona kama umebakia peke yako vile!” Jelini
akacheka taratibu. “Usingizi umekulemea?” “Sana. Halafu imekua gafla. Nafikiri
nilipatwa na hofu ya gafla, nikapaniki, nikijua hunitaki tena, nimekuumiza.
Usingizi ukapotea kabisa! Lakini sasahivi nakuona unafuraha, akili imetulia
ndio na usingizi umekolea.” “Basi acha nikurudishe nyumbani. Junior atatufuata
kwa nyuma, ili nirudi naye.” Jelini akacheka akiwa na usingizi.
“Usijali. Nitafika
tu. Wewe pumzika.” “Naomba kukurudisha Jelini. Ndio nitakuwa na amani.” “Sawa.”
Wakatoka hapo chumbani, wakamkuta Junior yupo chini sebuleni kwenye kompyuta
yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipowasikia
wakishuka ngazi akanyanyua uso kuwatizama. “Naona nyuso za furaha.” “Na usingizi.”
Akadakia Ezra na kuongeza. “Naomba tumrudishe nyumbani.” “Bila shaka.” Safari
ya kumrudisha kwao ikaanza, kimya garini. Ezra anaendesha gari ya Jelini,
Junior anafuata nyuma mpaka nje ya geti. Ezra akashuka na kwenda alikokuwa
amekaa Jelini. Akamfungulia mlango. Jelini akashuka. Wakajikuta wamekumbatiana
tena. Akamnong’oneza sikioni akiwa amemkumbatia. Jelini mpenda mikono,
alijituliza hapo kana kwamba mwenzie ndio haondoki tena.
“Ukalale unono,
ukijua Ezra yupo na anakupenda sana.” Akajisikia vizuri, akamsikia akicheka
taratibu hapo kifuani kwake. Akambusu pale kifuani alipokuwa amemlalia,
akajitoa. “Na wewe urudi kulala kwa amani, ukijua Jelini ni wako, na hakuna
wakukupokonya. Hata Colins.” Ezra akacheka. Akambusu kwenye kipanda uso.
Mlinzi akafungua geti, Jelini akarudi kwenye kiti cha dereva ili kuingiza gari.
Ezra akarudi kwenye gari ya Junior, wakaondoka wakati walipojiridhisha geti
limefungwa baada ya Jelini kuingia.
Ezra & Junior.
Akamuona akicheka
kama asiyeamini. “Aisee amenibusu shingoni, mwili kama umepigwa shoti ya
umeme!” Junior alicheka sana. “Mimi sikujua kama anamsimamo hivi!” “Ila na wewe
ulionyesha kumpenda aisee! Asingeweza kukuachia kirahisi hivyo.” “Ila
sikutegemea kama ni mpaka kwa Colins!” “Sasa mmekubalianaje?” “Aisee sijui
Junior. Nishauri.”
“Kwa nini?” “Kwa jinsi alivyoniambia, amewaambia hata
nyumbani kwa kina Colins, hataweza kuendelea kufanya chochote mpaka sisi
tukubaliane. Lakini Colins ameshanitisha sana aisee! Sijui nafanyaje! Sitaki
apone halafu aje anipindue. Nimempenda Jelini. Siwezi pata mwanamke
mzuri vile, halafu mwenye msimamo kama wake. Anayejali hisia zangu! Sijawahi aisee!”
“Halafu kumbe ndio mtundu vile!” “Nilikwambia.” Wakaanza kuzungumza juu ya
Jelini, wakicheka.
“Sasa utafanyaje?” “Sijui Junior! Ila ninachojua kwa hakika,
sitaki kumpoteza Jelini kwenye maisha yangu. Na sitaki kumfungulia au kumpa
mwanya Colins. Kwa hakika ananitisha. Hawa watu wanahistoria Junior!”
“Nakuelewa kabisa. Inamaana haitachukua muda au nguvu kubwa kurudi
walipoishia.” “Daah! Na sitaki kumpa wakati mgumu Jelini! Ameomba kwa kipindi
hiki kama tunaweza tusimtupe. Amsaidie. Lakini aisee sijui ndio inakuaje! Naona
hofu ya kumpoteza inazidi kufunika maamuzi yangu! Nisije nikakosea
Junior!”
“Kabla ya kulala, nashauri na hili tuliombee. Ila nashauri
hii furaha ya sasahivi, ikusaidie ulale, usikaribishe hofu, ikakupokonya furaha
yote. Tulia kwanza. Wakati mwingine kuna mambo yanajijibu. Tufanye kama kawaida
yetu. Tusiharakishe.” “Hata katika hili!?” “Zaidi katika hili.” Junior
akaweka msisitizo akiendelea kukanyaga mafuta, kurudi kwake.
Shilingi Imepinduka.
Jelini akarudi na
kuingia chumbani kwake kwa kunyata ili asimsumbue mama yake. Akajitupa
kitandani na kupotelea usingizini mpaka mida ya saa tatu asubuhi mama yake
akaingia hapo chumbani kwake. “Hatuendi kanisani?” “Lazima. Nimepitiwa tu
usingizi.” “Vipi mambo yako na Ezra?” Akauliza akikaa kitandani kwa Jelini.
Jelini naye akajiweka sawa.
“Naona tumewekana
sawa. Nimemuomba msamaha, na kumuelezea hali ilivyokuwa. Na ameelewa. Ezra
ananipenda sana mama. Mpole na najua wazi tutakuwa na maisha mazuri. Hana hekaheka.
Halafu nitakuwa peke yangu. Nishapata mwenzio mtu wangu wa peke yangu, niliyekuwa
nikimtafuta.” Mama Jema akacheka akitingisha kichwa. Alimjua Jelini.
“Kila mtu niliyekuwa
nikimwambia alikuwa anaona haiwezekani. Wakawa wanaona mimi natafuta
vitu visivyowezekana. Mbona imewezekana? Shem ametulia. Na huyo Ezra
pia. Unakumbuka ulivyoniambia nisikate tamaa? Ona sasahivi na mimi nimepata.”
Mama Jema akawa anamwangalia vile alivyojawa furaha.
“Na kwa Ezra kweli
utatulia.”Akaongeza mama Jema kwa furaha kama anayemsifia. “Ila nimemuomba kama
tunaweza msaidia Colins kipindi hiki mgonjwa.” Hapo ndipo alipo haribu.
“Unasema umemuomba
Ezra nini?!” “Kwamba kwa kipindi hiki Colins ni mgonjwa, nisaidie.”
“Unasaidiaje?” Akaanza mama Jema. Jinsi alivyouliza, Jelini akajua anatakiwa
kuongeza umakini. “Kwa ugonjwa.” “Ndio nakuuliza, wewe mwenzangu na mimi,
ambaye huna shule ya unesi. Pale kwao amezungukwa na madaktari na mama
yake ni nesi. Halafu wana wafanyakazi chungu mzima! Wewe ulitaka kwenda
kusaidia nini, na kama nani?” Kimya, maana aliona ameshaanza
kubadili gia.
“Walikuja hapa,
wakakuita wewe mjinga. Hujasoma. Huna mbele wala nyuma. Mchawi. Wakakutusi hayo
yote. Wakasema ‘mtu kama wewe’ hufai kwa kijana wao. Kwamba gafla leo
umesahau?!” “Sijasahau mama. Ila…” “Ila nini kama sio ukichaa huo? Wao waje wanitukane
hapa. Wakatae na kijana wao. Leo unataka kuharibu biashara nzima. Ambayo umehangaikia
tokea akuache hapa huyo Colins. Yaani kama vile jana ulivyotelekeza biashara, ukaacha
pale dukani bila mtu! Na hukufanya chochote jana, wakati kawaida yako siku ya
jumamosi ndio siku unatengeneza pesa zaidi! Ukaacha kila kitu, ukakimbilia huko
kwa kina Colins, tena kwa kuitwa tu. Unawazimu wewe mtoto!?” Mama Jema akazidi
kulipuka.
Sauti ikaongezeka,
Jeremey akagonga taratibu na kuingia. Alimjua bibi yake huwa anamuweza vizuri
sana mama yake, lakini si kwa ukali wa siku hiyo, tena asubuhi
waliyokuwa wakijiandaa kwenda kanisani! Yeye alishakuwa tayari. “Kaniletee simu
yangu haraka sana. Ipo kitandani.” Jeremy akatoka kwa haraka, akimuacha mama
yake akilia, wote wamekaa hapo kitandani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Simu ikaletwa akiwa
anawaka kwelikweli kama moto. Akapigiwa simu Jema. “Namalizia kujiandaa tutoke. James ameshatoka na JJ. Tukutane
kanisani.” “Hapana. Njooni hapa. Tena sasahivi. Maana wanataka kunichezea
mimi?” “Ni nini tena mama Jema!? Huu ni muda wa kani…” “Kwamba unaona kanisani ni
muhimu kuliko kuitikia wito wangu?” “Nakuja mama yangu mzazi. Sasahivi nakuja.
Yaani hapa natoka mlangoni, safari ni ya kwako hii wala si kanisani.”
Simu ikakatwa kama itupwe. Mama Jema anawaka kwelikweli. Anagomba, Jelini
analia kitandani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Shilingi Imepinduka Pabaya.
Ilikuwa Familia Ya Kisomi, Ya Kina Colins, Hawamtaki Jelini KWA Kijana Wao. Sasa Safari Hii ni Mama Jema Ndio Hamtaki Msomi, Na Mwenye
Hela, Colins Kwa Binti Yake.
Je, Jelini Atafanyaje? Kweli Atabakiwa Na Msimamo Aliotangaza Usiku Uliopita,
Hata Kwa Colins!?
ITAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment