Ezra hakuwa amemtania. Alimaanisha. Usiku huo hapakuwa na
simu ya mazungumzo ya kuliwazwa na kutakiwa usiku mwema kutoka kwake. Mwanzoni
akaona ni afadhali ili aweze kufikiria vizuri. Akatulia. Lakini kadiri muda
ulivyozidi kwenda, akaanza kuhangaika kitandani. Anageuka kila upande.
Kisha akagundua hapakuwa hata na ujumbe wa kutakiwa usiku
mwema! Akaanza kusumbua simu. Shika, angalia, weka pembeni akisubiria ujumbe wa
kutakiwa usiku mwema. Jelini mpenda kupendwa, kufuatilizwa na kubembelezwa.
Hayo aliyawezea Ezra. Ule usiku mrefu, wa upweke na mawazo akijifikiria mwisho
wake bila jibu akihisi ndoto zake za kuja kumiliki wake ndio amezizika,
aliokuwa akipata kwa miaka mingi, kwa muda mfupi sana, Ezra alishaziba hilo
pengo. Hana afanyalo ni kumfurahisha huyo kiumbe. Usiku kuwa naye kwa
hili na lile, akimbembeleza kwa sauti yake tulivu, kisha kumuombea usiku mwema.
Usiku huo na yeye historia ikamrudia. Akashindwa kulala
kabisa akabaki akiangalia simu yake bila kuchoka akihisi pengine Ezra atamtumia
hata ujumbe mfupi wa kumtakia usiku mwema! Akasubiri, akahisi pengine uliingia
huo ujumbe, umejificha kwenye jumbe nyingine. Akakwapua tena simu yake. Akaanza
kuperuzi. Hakukuta za usiku huo ila za siku zilizopita. Akabaki akirudia
kuanzia mwanzo wa mawasiliano yao mpaka mwisho. Akaona atulie.
Kumbukumbu za muda mtulivu aliokuwa nao juma zima
zikamrudia. Kwa asili Ezra alikuwa mtulivu sana. Rahisi mno kumpuuza. Ni
wale watu unaoweza kuwafanyia chochote kisha ukaomba msamaha na akasamehe.
Mtulivu mpaka sauti yake. Ila alimjali sana Jelini. Jelini akaanza kutokwa na
machozi kila akimkumbuka Colins.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Colins aliyekuwa naye muda mrefu, na anampenda.
Akamlinganisha na Ezra aliyekuja kwenye maisha yake kwa muda mfupi. Kadiri
alivyofikiria, hao viumbe wawili kwake na anachokitaka, mizani ikazidi kulemea
kwa Ezra. Akamtetea hivi na vile Colins wake, mwanaume aliyempenda bila
kujisingizia, lakini mizani ikazidi kulemea kwa Ezra. Jinsi anavyomjali na
kumpa kipaumbele.
Ni jumamoja tu, lakini aliweza kupanda mbegu iliyomea kwa
nguvu sana na kugusa moyo wa Jelini vilivyo. Kwa hakika Ezra alikuja kama majibu
ya maombi na ndoto zake, lakini ikawa amefika kwenye moyo uliokuwa umejaa
Colins! Akalia akitamani kama ingekuwa tofauti. Yote ya Ezra apewe Colins.
Akamfikiria Colins. Tokea waanzane mpaka waachane. Akavuta
kumbukumbu zote nzuri. “Alinibembeleza sana
nilivyomfumania yule mzee. Halafu aka..” Akakwamia hapo. Kila
akikumbuka kama walishatoka na kuwa wakila pamoja kama na Ezra, akaishia
kukumbuka sababu za kushindwa kuwa naye. “Ila
tulishatoka kwenda kula wakati ule…” Akajaribu kumtetea. Lakini
akakumbuka ndio kipindi hicho, tena mara moja akilia kusalitiwa na Kasa,
kwengine kote ni sababu. Akakumbuka ahadi ya kuwa naye hospitalini
kwenda kupimwa UKIMWI, akaishia mikononi kwa Doro, na kwenda kulewa kupitiliza.
Hapajawahi kuwa na kumbukumbu nzuri kati yake na Colins, ila
kwa muda mfupi aliokuja Ezra, akafanikiwa kuweka historia ya namna yake. Hofu
ya kurudi kuwa mpweke ikamuingia gafla mpaka kumtia hofu. Akakumbuka
hali aliyomkuta nayo Ezra siku chache zilizopita. Mpweke moyoni, akihofia
kuzeeka peke yake. Lakini Ezra akamjali akiacha warembo wengi pale kanisani!
Akimkataa yeye, sio kwamba atashindwa kupata mwingine!
Akakumbuka mabinti wanavyommezea mate pale kanisani. Ezra si mweupe kama Colins,
lakini ukweli analipa. Analipa kimuonekano na kipato pia. Hata kwa mwanamke
mjanja wa mjini anayependa maendeleo, mwenye viwango vya juu, bado Ezra
analipa. Hofu ikamuingia kadiri alivyokumbuka jinsi walivyoachana
naye usiku huo. Alimuacha si kwa kumbembeleza tena. Alimuacha kwa uhuru
japo alikuwa ameumia.
“Mungu wangu nimechezea
shilingi chooni.”
Hofu ikazidi kumuingia. Akavuta simu yake tena ili aangalie pengine Ezra
amemtafuta. Lakini wapi! “Huyu Colins si wangu, na
wala hatakaa awe wangu maishani. Hilo wazazi wake na dada yake wamelithibitisha
kwa vitendo.” Akazidi kulia kila akimfikiria Colins, na historia yao
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akalia hapo mwishoni akaenda kujisalimisha chumbani kwa mama
yake. Jeremy alisharudi chumbani kwake. Alishamtengenezea mwanae chumba chake.
Akajaza vitu vya thamani kama alivyokuwa akitamani. Kikapangiliwa hicho chumba,
ungependa kuwepo humo chumbani kwa Jeremy. Na kwa kuwa mama Jema ndiye mwenye
nyumba, basi palikuwa pasafi muda wote. Kwa hiyo hakuwa akilala na bibi yake
tena.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mama Jema akashituka sana. Jelini aliingia ndani ya shuka
alilojifunika mama yake akilia sana. “Kuna nini tena!? Mbona unalia?” “Colins amerudi.” Mama Jema alishituka, akawasha
taa kama aliyehisi anatembelewa na nyoka mwilini. “Safari hii amerudi na sababu
gani?!” Ndilo swali mama Jema aliuliza na kumfanya Jelini azidi kulia. Ila
ikabidi amsimulie kila kitu.
“Utafanyaje Jelini mwanangu!? Unarudia yale maisha ya hekaheka
ya huko kwa kina Colins? Na kweli umesahau jinsi walivyokuja hapa
kutudhalilisha kwa matusi?” Jelini akazidi kulia. “Sijakuona ukiwa na furaha
kwa muda mrefu kama siku hizi chache! Hata ulipokuwa na Colins, hukuwa na
furaha hivi. Wakati wote ni hekaheka na yule kijana, ukiachwa hapa ukilia kila
siku usiku. Hata siku ile ulipokuwa nyumbani kwake, nikadhani ungelala, pia
mlishindwana. Usiku mmoja tu, ukiwa umelewa hujitambui, ndipo mliweza kulala
nyumba moja. Lakini kesho yake mlishindwana ukarudi hapa kwa usafiri wa
kuunganisha!”
“Hujawahi kupata furaha kama uliyokuwa nayo ulipokuwa na
Ezra. Ulipata utulivu, mwenyewe ulikiri yote uliyokuwa ukiyatamani na kuomba
Mungu akujalie kwa mwanaume, Ezra anayo isipokuwa rangi tu. Sasa unataka
uwe na mwanaume mweupe lakini huna furaha!?” Mama yake akamuuliza taratibu tu
kama anayetaka afikirie.
“Mimi nafikiri sasahivi nampenda Ezra, mama.
Sijawahi pendwa kwa namna hii. Halafu Ezra ametulia mama yangu. Atabaki kuwa
wangu daima.”
“Nimesikia sifa zake zikiimbwa pale kanisani. Yeye na yule mtoto wa mchungaji.
Wamefanikiwa lakini wametulia.” “Ndicho
kilichonivutia kwake. Lakini baada ya kumsahau usiku huu, na akajua
sababu ni Colins, amejitoa kabisa. Hajanitafuta hata kwa usiku mwema,
wakati si kawaida yake!”
“Nisikilize Jelini. Ezra anajua umuhimu au historia ya
Colins kwenye maisha yako. Cha kwanza, ameshaumizwa na mwanamke mwingine kwa
kusalitiwa. Aliachwa na kuchaguliwa mwanaume mwingine. Akatulia miaka yote
mpaka kukufikia wewe. Hudhani yupo kwenye hofu ya historia kujirudia?” “Mimi siwezi kumsaliti.” “Jelini!? Tunamzungumzia
Colins! Kweli?” Jelini akazidi kulia akishindwa kujibu.
“Na cha pili, kwa jinsi ulivyonisimulia, nafikiri anataka
kukupa muda ufikirie unachotaka. Kama ukirudi kwake, iwe kweli umemchagua yeye
sio tu kama unasimamia maneno yako, ni kwa sababu unampenda yeye. Na
hutambadilikia.” Jelini akazidi kulia.
“Mimi nakushauri kama Ezra. Tulia. Pata muda wa kuingiza
taarifa za kuwa Colins amerudi. Pima kwa upana na urefu. Linganisha hao wanaume
wawili. Ukiwa umetulia, na kujifikiria wewe mwenyewe. Nini unataka maishani
bila kuweka hisia za mihemko. Kisha chukua hatua kama Jema mwenzio.” Hapo
akamkumbusha msimamo wa Jema maishani, na mama Jema alifanya makusudi.
“Ni kwambie ukweli mama?” “Juu ya nini?” “Japokuwa nampenda sana Colins, lakini huwezi kabisa
kumlinganisha na Ezra.” Na mama Jema alijua. Ila hakutaka kusema moja
kwa moja ili amsikie mwenyewe. “Japokuwa
nimemfahamu Colins kwa muda mrefu, na kuwa naye kwenye chochote tutakachoita.
Maana hata hayajawahi kuwa mahusiano. Niseme ukaribu, lakini hatuna mambo
mazuri, au niseme sina wakati mzuri ninao weza usema tunao kama mimi na Ezra.
Nafasi niliyompa Ezra ni kama tu niliyompa Colins, ila kwa Colins imekua zaidi.
Nilijiachia sana kwake kwa kuwa mimi mwenyewe ndiye niliyempenda sana. Lakini
naweza sema kwa Ezra nina msingi mzuri. Historia nzuri. Nimepata wakati mzuri
kuliko niliowahi kuwa nao kwa Colins.”
“Sasa hivi ni mgonjwa. Atapona na kurudisha
nguvu. Lakini naona tutarudi palepale tukihangaika. Na ukweli ambao siwezi kuupuuza
kwao mimi ni chaguo ambalo linawalazimu tu kuwepo. Inamaana kama Colins
asingekuwa akinitafuta alipokuwa mgonjwa, wale wazazi wasingenifungulia mimi
mlango. Na kila wakati nakumbuka jinsi Colins alivyokuwa akiniacha hapa usiku
kucha nalia, yeye yupo kwa Love. Ezra hawezi fanya hivyo. Ezra ananifikiria
mama, mpaka utamuhurumia! Halafu mtulivu sana.”
“Anakopita Ezra sasahivi, usiku huu, na mimi
amenipitisha Colins. Tena zaidi ya mara moja! Kusahauliwa
sababu ya mtu mwingine. Leo nimemsahau Ezra, sababu ya Colins. Roho inaniuma,
na natamani ungemuona leo. Mpaka ungemuhurumia! Amenikumbusha ile hali
niliyokuwa nayo, nikimsubiria Colins. Nikitegemea itakuja kufika zamu
yangu. Nikisubiri na kusubiri bila mafanikio. Naumia kumfanyia hivyo Ezra, mtu
mzuri. Mimi siwezi kulala tena.” “Mimi nashauri pengine tulale,
halafu kesho…” Jelini akazidi kulia kwa sauti.
“Sasa unataka tufanyaje Jelini, mama yangu mzazi, usiku wote
huu!?” “Tukamtafute Ezra.” Mama Jema
hakuamini. “Jelini!? Nashauri tula....” Kabla hajamaliza, akaongeza sauti ya
kilio. “Sasa tunampata wapi huyo Ezra usiku huu?” “Mimi
sijui! Ila ninachojua nimechezea bahati. Sitakuja tena pata mtu kama Ezra na
naona wewe hujali.” “Sasa si ndio nashauri tulale mpaka kesho,
tukamuulizie pale kanisani!” Jelini akazidi kulia.
Kwa Jema&James.
Ilikuwa saa sita usiku. Mama Jema akafikiria. Akajua
asipopatikana Ezra, huyo Jelini kesho ataamka akili ipo kwa Colins, na yeye hamtaki
tena Colins kwenye maisha ya mwanae. Shilingi ikapinduka. Ilikuwa wazazi wa
Colins hawamtaki Jelini, sasahivi mama Jema ndio hataki hata kumsikia Colins. Akafikiria
kwa haraka, wazo likamjia. Jema. Hapo hapo bila ya kujali muda, akampigia
simu.
Jema akashituka sana mpaka akamuamsha mumewe. “Mama anapiga
usiku huu! Si kawaida yake.” “Pokea tujue tatizo.” James akamwambia mkewe. “Kwema mama!?” “Wewe unajua anakoishi Ezra?” “Hapana mama!
Kwani vipi?” “Naona leo hakuna kulala humu ndani, mpaka tumpate Ezra.
Anatafutwa na Jelini.” “Si nimesikia Colins amerudi na Jelini alikuwa huko karibu
siku nzima!?” “Sasa hilo ndilo tatizo.” Jema akawa hajaelewa. Ila
akamsikia akilia hapo pembeni ya mama yake.
“Mpe simu Jelini. Na mwambie aache kulia, aniambie
tatizo ni nini.”
Akampa simu Jelini. “Na amesema uache kulia, umuelezee vizuri.” “Wewe unajua Ezra anakoishi?” “Kabla hujaeleza mengi, naomba kukutahadharisha na kukuomba
kitu Jelini. Maana mimi nakujua wewe na Colins. Msimuingize Ezra katikati yenu,
mkamuumiza.” “Mimi sij…” “Hapana Jelini. Tafadhali nisikilize.” Hapo Jema
akaweka ukali kabisa.
“Nipo katika kikundi cha wakina mama wazee na
wakina mama vijana pale kanisani. Hakuna mtu anamsema vibaya Ezra na Junior,
kitu ambacho ni cha ajabu sana. Huwezi kupendwa na watu wote kwenye jamii moja.
Lakini hii imekua tofauti. Hakuna mtu anawasema vibaya hawa vijana wawili, ndio
maana nikavutiwa nao. Hawana makuu, na wanampenda Mungu sana. Ezra ni
mstaarabu kama unavyomuona. Hana neno na mtu, na nasikia tabia yake ni mtu
ambaye anaweza msamehe mtu bila kumuwekea kinyongo. Nimuelewa. Hana makuu.”
“Sasa. Kwa kuwa Colins amerudi. Na nyinyi wawili
tunawafahamu. Tafadhali sana. Kabla hamjafika mbali na Ezra, mwache yule
kijana. Maana ana historia ngumu sana juu ya mapenzi. Alinisimulia Junior kuwa
aliachwa siku chache kabla ya harusi. Mwanamke ameolewa huko nje ya nchi, na
hata aliporudi na huyo mume wake wakizungu na watoto wawili nasikia akajifanya
ni kama hamkumbuki kabisa Ezra. Lakini bado Ezra amelipokea na kulinyamazia.” Jelini akazidi
kulia.
“Tafadhali sana Jelini. Junior na Ezra ni kama
wadogo zangu pale kanisani. Tunaheshimiana nao sana. Ni vijana waliotulia.
Hawastahili hekaheka zako na Colins. Usimuingize Ezra kwenye michezo yako na
Colins, isiyowahi kuisha.” Jelini alilia sana.
“Unanielewa?” Jelini akaendelea kulia. “Katika hili, ni lazima uniahidi na uniambie umeelewa
Jelini. Sikutanii.” Hapo Jema akawa mkali zaidi. “Nilimsahau kidogo tu, kwa mshituko wa kumkuta Colins na
hali ile, Jema. Lakini sio kwamba simjali Ezra. Hata Colins na wazazi wake
nimewaambia sasahivi nipo na Ezra. Na siwezi fanya kitu kingine tena, bila
makubaliano yangu na Ezra.” James akasikia akiwa amejilaza hapo
kitandani alipokuwa amelala na mkewe. Akashituka sana.
“Sio nilikusikia ukiwaambia wasitafute mtu, wewe
utakuwepo kumuuguza Colins!?” James akauliza swali kwa mshangao mkubwa sana. Mama Jema
akatingisha kichwa kwa masikitiko akisikiliza hapo kitandani na yeye alipokuwa
amelala naye akilia. “Nilibadilisha shem.
Ulipoondoka tu ndio nikakumbuka nipo kwenye mahusiano na Ezra, na…” “Jelini?!” “Kweli shem. Ni
vile nyinyi hamnifahamu. Mimi nikiwa kwenye mahusiano na mtu, nakuwa mwaminifu
kwake.” Jelini akaendelea akijaribu kutulia ili aaminike. Zaidi na Jema
akijua ameelezwa na mumewe jinsi alivyokuwa amejaa huko kwa kina Colins, halafu
sasahivi anasema Ezra! Akajua lazima aeleweke.
“Siwezi kudanganya, nilipofuatwa kwa mara ya pili
na Connie, na kuambiwa Colins ni mgonjwa sana. Halafu nikapata taarifa za
kilichokuwa kikiendelea huko alikokuwa akiishi na Love, huruma ya ajabu
ikaniingia. Ukweli kwa muda fulani ni kama dunia nzima ilisimama, nikajiona
nipo tu mimi na Colins. Nikasahau uhakilisia wa maisha. Na siwezi
kudanganya kwamba simpendi Colins jamani. Nitakuwa nikidanganya. Nampenda, na
ukweli bila kificho, nilikuwa nikimsubiria muda wote huo na ndio maana nilikuwa
nikikataa wanaume wote, nikidhania atarudi tena,…” “na sababu ingine
nzuri?” Mama Jema akamkatisha.
“Najua unanikejeli mama. Lakini ndivyo nilivyodhania, na
nilikusudia kumsamehe tuendelee.” “Nahisi wewe si mzima wa akili wewe. Na kama
uchawi kweli upo, basi wewe ndio umelogwa wala si bure.” Mama Jema akaongea kwa
hasira kidogo kama aliyeanza kuchefukwa tayari. “Mwache
aendelee, mama. Mwache tu.” Jema akadakia akitaka kumsikia mdogo wake.
Maana alijua wakimuachia mama yao hapo, pataanza kutibuka zaidi.
“Lakini si nilimkubali Ezra?” Akawa
kama anayemuuliza mama yake kwa kujitetea. “Unataka
kuniudhi Jelini? Wewe uje utukanwe hapa. Wanitukane mimi mbele yenu, bado
umsubirie ili iweje tena? Tunakuja kuwa na mahusiano ya namna gani na hiyo
familia inayotudharau na kushindwa hata kutusitiri? Ingekuwa sisi ni zile
familia kama zao, kweli wangethubutu kuja kunitusi hapa kwangu,
tena hadharani, mbele ya wanangu!? Kweli? Ushajua wameshatukana hivyo
watu wa ngapi kama si sisi tu waliotuona duni?” “Jelini
muache mama. Wewe eleza tukuelewe.” Jema akadakia, akijua moto unazidi
kuongezeka, unakaribia kulipuka.
“Ndio nilikuwa nikisema, ni juzi tu, tumekubaliana
na Ezra, tuanze mahusiano yetu. Nikaamua kuachana kabisa na mambo yakusubiri.”
“Sasa si ndio amerudi?”
Jema akadakia na yeye kwa ukali. Mama Jema
akafyonza kwa hasira na kutoka kabisa hapo kitandani kuelekea jikoni kuchukua
maji.
“Sawa amerudi, lakini amerudi na kunikuta mimi ni
wa Ezra. Siwezi kubadilika. Hata wao nimewaambia sitafanya lolote bila kuwa
na baraka za Ezra.” “Kwamba kweli Ezra akikwambia hapana kwenda kwa Colins?
Hutaenda wewe?” “Hakika siendi, Jema. Siwezi kumuumiza mtu wangu sababu ya mtu
mwingine. Ezra ndio jukumu langu la kwanza, Jema. Nahusika na furaha ya Ezra kwanza
kabla ya mtu mwingine, ndio maana mimi nilikuwa nikimshangaa Colins, eti
anakuwa radhi kumfurahisha Love na wazazi wake na sio mimi!” Hapo akaanza kuwatuliza.
Wakabaki kumsikiliza. Mama Jema akarudi.
“Ezra ni wangu. Na nimemuahidi nitakua naye.
Siwezi kuyumba sasahivi. Kwa kuwa hata mimi sitaki aje ayumbe baadaye. Tumeweka
msingi wetu. Hata kama hautavutia sasahivi, lakini tumekubaliana tujenge cha kwetu.
Pengine ndio jaribu letu la kwanza kwenye kuanza kujenga kwetu? Siwezi kukubali
tushindwe mapema hivi! Hapana Jema. Ezra ana kila kitu cha mwanaume ninayetaka
awe wangu. Na nipo tayari nibaki naye tu, mengine nijue mbele ya safari.
Na sitamsaliti hata iweje, labda anitamkie hanitaki tena. Lakini
simuachi kwa sababu ingine yeyote ile.”
“Hata Colins?” Jema akataka uhakika. “Hata Colins.” “Unauhakika Jelini?” Ni kama Jema
aliwakilisha hofu yao wote hapo. Ni Colins jamani! “Kwa
hiyo unachotaka kuniambia wewe Jema, hapo ulipo na shem. Akaja mwanaume wako wa
zamani uliyekuwa ukimpenda sana, ndio utamuacha shem kwa sababu yake huyo ex
wako?” “James ni mume wangu! Unawezaje kufananisha?” Akaweka na kaukali,
chakupaniki, James akimtizama.
“Basi uzito wa kiapo chako kwa shem, au ahadi zako
zote ulizompa baba JJ, ndivyo mwenzio na mimi nachukulia viapo vyangu
kwa kila mwanamme ninayempa. Mpaka wenyewe wanikatae. Kama walivyofanya
wanaume wote isipokuwa Ezra tu. Naweza nisiwe mcha Mungu kama
wewe Jema, lakini mwenzio huwa sitoe ahadi zangu za kimapenzi hovyo kwa
mwanaume. Hata kama inanigarimu mwenyewe baadaye, kama nilivyoishi na Colins
akiniliza wakati wote, lakini nilikuwa nikimsubiri tu. Ndivyo hivyohivyo
nafanya kwa Ezra. Nakusudia kuwa mwaminifu kwake mpaka mwenyewe aseme basi.
Hanitaki tena.”
“Lakini ndoa au viapo vya ndoa siku ile ya sherehe, ni vya baadaye nikiwa
nimeishi maneno yangu tokea mwanzo. Mimi sio muhuni. Neno langu kwa mwanaume
sisemi hovyo. Na nikisema, nalisimamia.” Mpaka hapo wote kimya.
“Nimekutumia
namba ya simu ya Junior. Alipo Ezra, masaa 24, lazima Junior ajue. Na ndio
hivyohivyo kwa Junior. Ukitaka kumpata Junior, muulize Ezra. Usiku mwema. Na
kuwa makini.” “Asante Jema. Na samahani shem kwa usumbufu.” “Daaah! Usiku mwema
Jelini. Sina chakuongeza.” James akaongea kwa masikitiko.
“Najua
unampenda Colins, shem. Najua amerudi tena. Na najua kwa mara nyingine tena
amerudi na sababu nzito yakueleweka ya kwa nini alipotea muda wote huu, akiishi
na Love. Lakini shem, inawezekana Colins hakuwa andiko langu. Tumejaribu sana
na wewe ni shahidi, kila wakati tumeshindwa, na mimi umri unakwenda. Si binti
mdogo, ni mama mwenye mtoto mkubwa tu. Nahitaji kutulia kama hivyo Jema.”
“Kumpenda
Colins imekua ni adhabu kwangu! Sioni mwisho wake. Lakini na Ezra,
nimetulia mpaka nafsini mwangu, shem. Madhaifu yote wanayonitukania nayo kwa
kina Colins, eti Ezra ananitia moyo nayo na kuniambia ndio nguvu yangu ya sasa
na baadaye! Eti kwamba ndiyo yananifanya niwe hivi nilivyo leo. Amenipokea kwa
upendo wa hali ya juu, akinijua mimi ni nani na maisha yangu yote mabaya ya
nyuma. Amefuta siku zangu zote zile za vilio na majonzi. Nilishasahau kulia
hivi, sababu ya Ezra. Nina uhakika kama leo sikuwa nimemuumiza, nipo naye,
usiku huu ningekuwa nimelala usingizi mzuri tu. Yote niliyokuwa nikiyatamani,
Ezra anayo.” Akajifuta
machozi na kuendelea.
“Ninachotaka
kukuomba, tafadhali naomba na yeye umpokee. Ukijaribu, au kumfungulia mlango,
utagundua ni mtu mzuri sana. Ni wale bahati inayomjia mtu mara moja
maishani. Inaweza isije nirudia tena. Ni mwanaume ninayeona uzee wangu naye.”
“Jelini!” “Kweli shem. Tafadhali mpe nafasi, utagundua ninachokwambia ni kweli.
Ni mtu mzuri sana. Ukikaa naye, unajisikia kutulia, hana hekaheka. Amepoa haswa,
mstaarabu wa asili. Nakuomba shem, mpe nafasi.” “Mmh!” James akaguna kwa
sauti ya kuishiwa kabisa.
Wote kimya
wakisikiliza. James akabaki akifikiria kwa muda. Mwishoe akasema. “Mimi ninachotaka ni uishie kwenye mikono salama Jelini.
Sehemu utakayokuwa na furaha. Na kama Ezra ndiye unaona atakupa furaha, mtafute
mzungumze.” Jelini alifurahi huyo kama Jema tu. “Nakushukuru
sana shem. Usiku mwema. Acha na mimi nitengeneze kwangu.” Akakata na
kumpigia simu Junior hapohapo akiwa kitandani kwa mama yake.
Kwa Junior.
Simu iliita mara
kadhaa, akapokea. “Mimi ni Jelini. Samahani kwa
kukusumbua. Namtafuta Ezra.” Kimya. “Junior?”
“Ezra amepumzika.” Jinsi alivyomjibu, Jelini akajua wazi hana furaha
naye. Lakini hakujali. “Wapi?” Jelini
akamuuliza. Kimya. “Nilazima uniambie. Siwezi kulala
bila kuzungumza na Ezra. Na usiponiambia, namfuata baba yako. Yaani mchungaji.”
“Namjua baba yangu, Jelini.” “Basi namfuata usiku huu huu anisaidie kumtafuta
Ezra.” “Wewe unajua anapoishi baba yangu mchungaji?” Jelini akafikiria
kwa muda akakwama.
“Au
unapafahamu nyumbani kwa Ezra?” Akamuuliza tena kwa kumsuta kidogo, ila kwa utulivu kama
pacha wake Ezra. Kimya. “I didn’t think so.
Usiku mwema Jelini.” Akataka kumkatia simu kama anayemwambia anampotezea
muda. “Nampenda
Ezra.” Jelini kwa mara ya nyingine tena siku hiyo, akatamka. Ila
kwa mtu asiye sahihi. “Hayo anayajua Ezra? Kwamba
ulishawahi kumwambia kama unampenda?” Jelini akazidi kulia. Akalia wee,
Junior akimsikiliza asiamini kama Jelini anamlilia Ezra!
Mwishoe na yeye
akamuuliza. “Kwani unafikiri nimechelewa? Niambie
tu ukweli.” Junior akavuta pumzi kwa nguvu, na kuzishusha taratibu,
kimya. “Eti Junior?” “Inategemea Jelini. Wewe unataka nini?” “Mimi
si mkamilifu, Junior. Nimekosea leo. Lakini simu ilikuwa mbali, na haikuwa na
sauti.” “Ndio kushindwa kuwasiliana naye kwa
muda wote huo?!” Akajua inamaana Junior anajua kila kitu.
“Ezra
anakupenda sana Jelini. Anakujali kupita nafsi yake. Anakufikiria kwa kila
dakika. Kweli umeshindwa kuwasiliana naye siku nzima, ukamuacha anahangaika!
Hajui ulipo! Hajui kilichokupata! Kumbe wewe umetulia kwa mwanaume au aliyekuwa
mpenzi wako!”
“Nilikuwa kwenye paniki, Junior. Nilikosea.
Nilipatwa na mshituko mbaya sana kukutana naye. Huyu mtu alipotea akiwa na
nguvu, na akili yake. Nimefuatwa na mama yake, nikakataa. Alipokuja dada
yake na kunisihi, ikabidi tu kwenda kumuona, nikakutana na kiumbe cha ajabu
sana. Kijana yupo kama babu kabisa! Colins amedhoofu, amebaki kama fimbo!
Amejawa madonda. Hana nywele kabisa.”
“Mimi
nimuoga sana wa hospitali. Kile chumba kilijaa vitu kama hospitali. Ile hali
ikanivuruga kabisa nisiwaze chochote mpaka alipokuja kuombewa na kutolewa
mapepo. Kumbe ni mambo ya ushirikina. Amekuja kuwekwa huru ilishakuwa usiku.
Rafiki wa shem ndiye aliyefika pale kumuombea. Hapo ndipo kila mtu akakaa sawa.
Lakini hata wao niliwaambia nipo na Ezra. Na siwezi kufanya chochote hata
kurudi pale mpaka baraka za Ezra. Mimi si msaliti Junior, ila nimekosa.”
Akajikuta machozi
yakimtoka tena.
“Nampenda
Ezra wangu. Na mimi nahusika na furaha yake yeye kwanza kuliko mtu mwingine.
Tafadhali nisaidie kujua alipo, nizungumze naye. Siwezi nikamuacha alale na
uchungu.”
Jelini aliongea kwa upendo na kuupata moyo wa Junior vilivyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini ni mzuri
bwana. Na yeye humuona tu kanisani jinsi alivyo wa viwango. Hata Ezra
alipomwambia anajitosa kwake, alimuonya na kumwambia hatamuweza. Ikawa
kinyume. Ezra akawa akimwambia juu ya Jelini, wakawa wote wakishangazwa na
uhalisia wa Jelini na ule muonekano wake. Sasa usiku huo Ezra alipomwambia juu
ya kurudi kwake Colins kwenye maisha ya Jelini, Junior alimuhurumia sana Ezra.
Akajua historia inajirudia kwa pacha mwenzie. Sasa kuja kumsikia usiku huo
Jelini akimzungumzia hivyo Ezra, akimlilia, akapoa kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Tafadhali
usimuumize Ezra. Ni mtu mzuri sana.” “Basi nikwambie, na mimi ni mtu mzuri
sana.”
Junior akaanza kucheka. “Uwe unamwambia Ezra asije
niumiza mimi. Maana mimi nipo sana tu. Junior.” “Unauhakika Jelini?”
“Sasa unataka uhakika wakati mimi mwenyewe sijasamehewa hapa? Wewe nielekeze
alipo, nisamehewe, ndio utathibitisha uwepo wangu wa mpaka kifo, kwenye maisha
ya Ezra.” Akawa kama amekumbuka kitu. “Ujue Ezra
hata hajanitumia ujumbe wa ‘usiku mwema’!” “Kwa kuwa anakupa nafasi.” “Mimi
sitaki nafasi mbali na yeye. Nataka nafasi kati yetu na ulimwengu.”
Junior akacheka akifarijika.
“Naona
kweli umeamua.” “Niambie alipo sasa!” “Alishindwa kulala kwake, akaja hapa
kwangu. Yaani tumeachana hapa muda si mrefu, ameingia chumbani kwenda
kujipumzisha. Na hapo nimemlazimisha sababu ya siku ndefu kesho.” “Nakuja.” Jelini akatoka
kitandani kwa mama yake kama akimbie.
“Usiku huu!?”
“Ni kipengele kipi ambacho hujaelewa sasa? Kwamba mimi siwezi kulala,..”
“Sababu hujatakiwa usiku mwema?” “Hilo au kwamba Ezra amelala na uchungu?”
“Naona nimeelewa, ila nashauri iwe kesho.” “Basi nikwambie kabisa, ushauri wako
sio mzuri. Huwezi kunishauri nimuache Ezra hivyo. Ukute bado hajalala.” “Na
kweli anaweza akawa hajalala, ila anahitaji kupumzika.” “Ila sio mbali na mimi.
Usiponielekeza nyumbani kwako nampigia…” “Baba yangu mchungaji?” Junior akamalizia
kwa swali, nakumfanya Jelini acheke.
“Safari hii
nampigia mama yako. Ninayo namba yake.” “Usiku huu wa saa saba!?” “Kumbe wewe
hujanijua! Hapa navaa, nimfuate Ezra wangu.” “Basi ukiwa kwenye gari unipigie
nikuelekeze kwangu.” “Usimwambie Ezra mpaka nifike mwenyewe.” Junior akacheka na
kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Je, Jelini Amekumbuka Shuka Kumekuchwa? Atabaki kwa Ezra au ni paniki tu?
Itaendelea.
0 Comments:
Post a Comment